SOMO: MAISHA YA MAOMBI KWA MKRISTO (Part 3)
KUWAACHA WATU NA KWENDA KUOMBA!
Hili ni tendo la ajabu sana ambalo Yesu alilifanya! Lilikuwa ni fundisho kwetu! Hebu jaribu kufikiri; Kwa jinsi Yesu ambavyo ana kila kitu, LAKINI PAMOJA NA YESU NA KUWA NA KILA KITU, lakini alijua pasipo maombi yote aliyokuwa nayo HAIWEZEKANI! Yesu mwenyewe alikuwa anajua hapa bila maombi hamna kitu! Alifikia mahali anawaacha makutano halafu anakwenda kuomba. Luka 5:12-16. Hebu tusome mstari wa 16.
“Lakini yeye alikuwa akijiepua,akaenda mahali pasipokuwa na watu,akaomba.”
Hapo Yesu anawakimbia makutano na kuelekea zake kwenye maombi, japokuwa ni ngumu sana kwa baadhi ya watu kuwaacha watu na kwenda kwa kuomba katika mazingira kama haya ya Yesu, kwao ni utukufu. Ikiwa Yesu alifanya hivyo, sisi tunapaswa kufanya hivyo na kuzidi kulingana na maisha yetu na dunia ya leo, lakini leo mtu anasema hana muda wa kuomba, eti kazi zinambana, na kwa sababu nyingine zinazofanana na hizo, lakini bado mtu huyohuyo ambaye anasema hana muda wa kuomba huyo huyo unaweza kumuona katika makundi ya watu au marafiki akiongea muda mrefu, lakini hao hao wanaosema hawana muda wa kuomba ni watu hodari sana kwa kuchat, hana muda wa kuomba lakini ana muda wa kuchat na watu kwa njia ya whatsapp, muda wote anafanya kazi huku yuko whats app! Hana muda wa kuomba lakini ana muda wa kuongea na watu kwenye simu masaa na masaa, hana mua wa kuomba lakini anaangalia movie masaa na masaa; hana muda wa kuomba lakini ana muda wa kuangalia mpira …ninaweza kusema huyu hana muda wa kuongea na Mungu lakini ana muda wa kuongea na watu! Kwa sababu maombi ndiyo kuongea na Mungu.
Kuongea na watu si vibaya; si vibaya kuchat na watu kwa njia mbalimbali za mitandao, lakini ni mbaya kama tuna muda wa kufanya hivyo lakini hatuna muda wa kuomba! Ni mbaya sana! Sana ! Inatakiwa ifikie mahali tunaongea na watu lakini ukifika muda fulani tunajiepua na kwenda mahali kusikokuwa na watu au mahali ambapo tutaweza kuomba bila buguza! Hapa Yesu hakwenda kanisani! Maombi tunaomba popote pale kama mazingira hayaturuhusu kwenda kanisani, tukipata nafasi tu kidogo tu; tunaomba hata kimoyomoyo! Kuomba sio lazima iwe kanisani.
Bila maombi tutajikuta tunaishi maisha ya unafiki! Maisha ya uhitaji wa kupitiliza na kujikuta kwenye madeni wakati wote, ukiondoa maombi hata unahubiri kila siku lazima iko siku utaanguka tu! LAZIMA! Tuache mambo ya kukaa kaa na watu na kuongeaongea muda mwingi tunaumalizia kwa watu. Tena wakati mwingine mambo mengine hayana hata maana, tunaopoteza kuongea na watu ambao hata tukienda kulala hata hawajui yanayotusibu katika usingizi wetu. Hawana sifa ya kuongea na sisi kabla ya kuongea na Mungu wetu! Kama Yesu aliomba mwenye huduma kubwa kuliko huduma yako wewe ambaye unalewa na sifa za watu lakini kuomba hutaki! Sisi tutapona? Shetani alikuwa hana kitu kwa Yesu lakini bado Yesu alikuwa anaomba. Tusidanganywe na sifa zinazotoka vinywani mwa watu.
Tuweke ratiba kwamba! Kuanzia muda fulani ni muda wa maombi. Hapo hata simu ipigwe hakuna kupokea, tunakwenda mahali pasipokuwa na watu kifikra! Yesu alikwenda sehemu halisi! Lakini kama mazingira yetu hayaturuhusu kufanya hivyo, tunapaswa kwenda mbali na watu kifikra! Wakati wa kuomba ikiwezekana zima simu yako au weka silent kama simu yako ndio kila kitu! Nikiwa na maana kuna bible n.k.
Yesu naye tungesema hana muda, kwa sababu pale alikuwa kazini! Lakini alijua umuhimu wa maombi! Kama wewe huna muda usile chakula basi! Kinachokufanya ule nini wakati huna muda?