RSS

UUNGU WA YESU KRISTO

NA NENO ALIKUWA MUNGU

Je, wewe unamwabudu yeye ambaye si Mungu? Au haumwabudu Mungu?

MUNGU NA MWANAWE KATIKA KITI CHA ENZI.

Kwenye siku ile huko mbinguni, je utamwabudu Yesu Kristo kama Mungu?

Katika kitabu cha Ufunuo ile sura ya 4 na ule mstari wake wa 2, tunasoma kuhusu habari ya ‘kiti cha enzi kule mbinguni’, na ‘mmoja aketiye katika kile kiti cha enzi’. Na kukizunguka hicho kiti chake cha enzi cha ajabu wamezunguka wazee 24 wameketi katika viti vyao vya enzi. Na katikati ya kile kiti cha enzi na kukizunguka kiti hicho wapo pia viumbe wenye uhai wanne, na hao hawakupumzika wakitoa utukufu na heshima na shukrani kwake yeye aketiye katika kile kiti cha enzi na ambaye huishi milele na milele, wakisema, “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu Bwana Mungu mwenye uweza yeye aliyekuwepo na aliyepo na yeye ajaye.” (Mstari 8). Na hao viumbe wanne wanapofanya hayo, ndipo hao wazee 24 wote huanguka chini na kumwabudu yeye aketiye katika kile kiti cha enzi, wakisema, “Umestahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, kuupokea utukufu na heshima na uweza; kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumb wa.” (Mistari 10,11).

Yeye aketiye katika kile kiti cha enzi ni ‘Bwana Mungu Mwenyezi’. Kadhalika anaitwa “Yeye aliyekuwako, na aliyeko na atakayekuja.” Na wote humwabudu yeye na kumpa utukufu! Amina! Ni mandhari ya ajabu jinsi gani hiyo?

Sura inayofuatia ni ile sura ya 5. Hiyo nayo inatupatia mandhari nyingineyo ya ajabu nayo yamtambulisha Mwingine ambaye naye hupewa utukufu na heshima na wale wote waliopo mbinguni.

Yeye aketiye katika kile kiti cha enzi ameshika kitabu katika mkono wake wa kuume, naye ndiye pekee kule mbinguni na duniani ambaye ndiye astahiliye kukichukua kile kitabu na kukifungua ni “Mwanakondoo kana kwamba amechinjwa”. Huyo Mwanakondoo alijitokeza katikati ya kile kiti cha enzi na akakichukua kile kitabu kutoka kwenye mkono wa kuume wa Yeye aketiye katika kiti kile cha enzi. Ndipo sasa wale viumbe waliohai wanne pamoja na wale wazee 24 wakaanguka chini mbele ya Mwanakondoo – ni vilevile kama walivyofanya katika sura iliyotangulia ya 4 walipokuwa wakimwabudu Bwana Mungu Mwenye nguvu – nao wakiimba mwimbo mpya wakikiri kuwa Mwanakondoo anastahili kukichukua kitabu kile na kwamba yeye ndiye aliyewakomboa mbele zake Mungu kwa damu yake. Hapa sasa wanatoa heshima na utukufu kwa Mwanakondoo ambaye ndiye Bwana Yesu Kristo. Yeye ndiye aliyewakomboa kwa Mungu kwa damu yake ya thamani!

Sasa hebu sikiliza hii! Kisha mtume Yohana akasikia sauti ya malaika wengi na ya wale wazee na ya wale wenye uhai wanne waliozunguka kile kiti cha enzi – kwa ujumla wao walikuwa zaidi ya milioni mia moja – na wote wakikiri kwa sauti kubwa wakisema, “Astahili Mwanakondoo yeye ambaye alichinjwa, kupokea uweza, na utajiri, na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka.” (Mstari 12). Je, huo ni ufunuo wa jinsi gani wapendwa? Mbingu yote inampatia utukufu, na heshima Yesu Kristo Mwana wa Mungu – ni vilvile kama walivyokuwa akifanya katika kumwabudu Mungu Baba katika ile sura ya nne. Ni eneo lenye kushangaza, “Mungu anamwinua mwanae na kumpatia jina ambalo ni juu ya kila jina, ili kwamba kwa jina la Yesu, kila goti lipigwe, juu ya mambo yaliyopo mbinguni na yale yaliyomo duniani na yale yote yaliyopo chini ya nchi. (Wafilipi 2:9,10)

Katika ile sura ya 4 mbingu zinakiri kwamba Mungu yeye aketiye katika kile kiti cha enzi anastahili kupokea “utukufu na heshima na uweza”. Katika ile sura ya 5 nayo, inasema mbingu yote inakiri kwamba Mwanakondoo aliyechinjwa anastahili kupokea “uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka.” Kama vile wanavyotoa utukufu kwa Mungu (Baba) ndivyo na namna ileile mbingu yote hutoa utukufu na heshima kwa Yesu Kristo (Mwanawe), Mwanakondoo wa Mungu! Mbingu yote hutoa utukufu na heshima na wakimwabudu Mungu Baba na Mwanawe!

Kweli hii imeonyeshwa kwa uwazi kabisa kwenye ile sura ya 5 mwishoni (mistari 13,14), eneo ambalo kuabudu na kusifu kwa viumbe vyote vimeungana wakiwapatia utukufu Mungu Baba na Mwanakondoo, Yesu Kristo. Kama vile kulivyokuabudu kwa Mungu, ndivyo ilivyo kwa Mwana wa Mungu. Kama vile wanavyotoa utukufu na heshima kwake Mungu basi ni kwa namna hiyo hiyo wanatoa utukufu na heshima kwa Mwana! Hakuna tofauti yeyote hapa katika mistari hiyo! Baba na Mwana, wao ni wamoja katika sifa na kuabudu ambazo huzipokea.

“Na kila kiumbe kilichoko mbinguni na juu ya nchi na chini ya nchi ya juu ya bahari, na vitu vyote vilivyomo ndani yake, nalivisikia, vikisema, Baraka na heshima na utukufu na uweza una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na yeye Mwana-Kondoo, hata milele na milele. Na wale wenye uhai wanne wakasema, Amina. Na wale wazee wakaanguka, wakasujudu.” (Ufunuo 5:13,14).

Na sasa wewe! Unasita kumwabudu Yesu Kristo mwanakondoo wa Mungu aketiye katika kiti chake cha enzi pamoja na Baba yake? Je, unajiuliza wewe mwenyewe iwapo ni sahihi kumwabudu Yesu Kristo? Au wewe unamwabudu mwingine ambaye yeye si Mungu? Kufanya hivyo itakuwa ni kuabudu sanamu! Je, unasita kumheshimu Mwana kwa namna ile ile ambayo unasema kuwa unamheshimu Baba? Je, unajitenga mwenyewe nje ya kuabudu kunakofanyika mbinguni pamoja na viumbe vyake vyote? Je, hujapata kusikia kwamba,

“…watu wote wamheshimu mwana kama vile wanavyomheshimu baba? Asiyemheshimu mwana hamheshimu baba aliyempeleka.” (Yohana 5:23).

Wale wote ambao hawaheshimu Mwana kama vile wanavyopaswa kumheshimu Baba, basi hawamheshimu Baba wala Mwana. Hili ndilo fundisho la neno la Mungu. Na kwa wale ambao wanatumia muda wao mwingi hapa duniani au wanaifanya kuwa ndio kusudi la maisha yao kujaribu kuthibitisha kuwa eti Yesu sio Mungu, watafanya nini watu hawa siku ile mbele ya kungamano kuu la mbinguni? Je, wataanza kusimama na kulia kuwa, “Usimwabudu yeye kwa sababu yeye sio Mungu”? Je, wataendelea kutukuza mitazamo na mantiki yao ya kibinadamu tu mbele ya Mwanakondoo na kutangaza kuwa yeye sio Mungu?

WOTE WANAMWABUDU YESU KRISTO.

Wakati Yesu Kristo alipokuja katika ulimwengu huu malaika wote walimwabudu yeye,

“Hata tena amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, anasema ‘na wamsujudu malaika wote wa Mungu’”. (Waebrania 1:6).

Wale watu wenye busara toka mashariki walikuja na wakamsujudia,

“Wakaingia nyumbani wakamwona mtoto pamoja na Mariam mamaye, wakanguka wakamsujudu.” (Mathayo 2:11).

Na watu walimwabudu yeye na yeye hakuwakataza!

“Na tazama alikuja mtu mwenye ukoma akamwabudu akisema, ‘Bwana ikiwa unapenda waweza kunitakasa…alipo kuwa akisema maneno hayo kwao…tazama akamjia mtawala mmoja, naye akamsujudia…na yule mtu aliyeponywa akamjia akisema, Bwana naamimi, Na akamwabudu…” (Mathayo 8:2; 9:18; Yoh. 9:38).

Na wanafunzi wake nao wakamwabudu na wala hakuwasahihisha wala kuwakataa!

“Na wakaenda kuwaambia wanafunzi wake, na tazama Yesu akakutana nao, akasema Salam! Wakakaribia wakamshika miguu wakamwabudu…Na wakamwabudu na wakarejea Yerusalem wakiwa na furaha kubwa…”. (Mathayo 28:9; Luka 24:52).

Mbingu na dunia wanamwabudu Yesu, Mwana wa Mungu! Je, unaweza kumwabudu yeyote ambaye si Mungu? Shetani alijaribu kumpatia Yesu ufalme za ulimwengu huu kama Yesu angeanguka chini na kumsujudia. Hivi ndivyo sasa Yesu alivyomjibu shetani,

“Na Yesu akajibu akamwambia shetani, ‘Rudi nyuma yangu, ewe shetani, maana imeandikwa, Utamwabudu Bwana Mungu wako naye pekee ndiye utakayemtumikia’”. (Mat. 4:8-10).

Hii ni kweli, ni Mungu pekee ndiye anayepaswa kuabudiwa. Unainama chini mbele ya Mungu tu katika kuabudu. Ile amri kuu ya kwanza ambayo Mungu aliwapatia wana wa Israel ilikuwa ni kweli ile ile kabisa,

“Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni…Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako…” (Kutoka 20:2-5).

Tumekwisha kuona hapa kuwa wale wenye uhai wanne na wale wazee 24 wakianguka na kumwabudu mwanakondoo, na wale watu katika dunia pia walianguka chini na kumsujudia na kumwabudu Kristo! Na hakuna wakati wowote watu hao wakirekebishwa au hata kukemewa kwa kufanya hivyo! Wala mtumeThomaso hakusahihishwa alipomwona Bwana Yesu aliyefufuliwa, na akamwita Bwana wake na Mungu wake!

“Na Thomaso akajibu akasema, ‘Bwana wangu na Mungu wangu’,….na Yesu akamwambia, ‘Thomaso kwa sababu umeniona mimi ndiyo umeamini. Wanaheri wale ambao huamini pasipo kuona.’” (Yoh. 20:28-29).

Thomaso alishangaa kwa kumwona Yesu, na kile alichokisema ulikuwa ni udhihirisho wa wazi wa kushangaa kwake, lakini ilikuwa pia ni wazi zaidi kuliko hivyo. Ilikuwa ni ufunuo wa moyo – na hapo napo si tu kwamba Yesu mwenyewe hakumsahihisha Thomaso kwa kile alichokisema, badala yake yeye aliwapongeza wale ambao huamini pasipo kuona – kuamini nini? Kuamini kwamba Yesu Kristo ni Bwana na ni Mungu!.

Nilikuwa najadili Uungu wa Kristo na mtu aliyesema kuwa ni Mkristo, ila alikataa kuwa Yesu ni Mungu. Hivyo basi, nilimuuliza iwapo anamwabudu Yesu Kristo. Mwanzoni alikataa kujibu! Kwa nini mtu aliyeokolewa na Yesu Kristo kutokana na dhambi, kifo, nguvu za Shetani na hukumu ya milele na aliyepewa maisha mapya, na yeye asite na kukataa kujibu swali hili – kwa nini asite kujibu moja kwa moja tena kwa furaha na shukrani? Lakini haya ndiyo yaliyofanyika – hakunijibu swali langu. Je, mtu kama huyo ana uhusiano wa aina gani na Yesu Kristo? Zaidi ya huo, ni wokovu wa aina gani alio nao mtu kama huyo ambaye hangeweza kukiri mara moja kwamba anamwabudu Kristo? Baadaye nikamuuliza tena swali hilo hilo ila wakati huo akanipa jibu fupi, “Ndio, ninamwabudu.” Lakini kwa kweli aliyasema maneno hayo kwa kusita, bila furaha wala shukrani. Labda, kwa upande moja, alikuwa anajua maandiko ambayo tumeyaangalia hapo juu na alihisi kuwa hangeweza kujitenga na wanaomwabudu Yesu Kristo. Lakini kwa upande mwingine, alisita kukiri hili kwa sababu alikuwa anajua kuwa Mungu ndiye tu anayestahili kuabudiwa – na hakutaka kuonekana anakiri kuwa Yesu ndiye Mungu!

Tumeona pia kuwa viumbe vyote humpa utukufu Mwana kwa namna ileile wampavyo Mungu (Baba). Kutokana na tabia hii ya umoja huo haitatushangaza sisi kuona kuwa Mwana anachukua majina na vyeo ambavyo vimeainishwa kwa Mungu katika neno la Mungu. (Yohana14:9; 2 Wakor. 4:4,6; 5:19; Waebr.1:3).

ALFA NA OMEGA, MWANZO NA MWISHO

Tukirejea katika kile kitabu cha Ufunuo pale mwanzoni kabisa mwa kitabu hicho tunajulishwa kuwa huo ni ufunuo wa Mungu mwenyewe ambao alimpatia Yesu Kristo ili apate kuuonyesha kwa watumishi wake. Kwa maneno mengine, katika kitabu hiki Kristo hapa anawasilisha kwa watumishi wake ule ufunuo ambao Mungu alimpatia. Baada ya utangulizi katika ule mstari wa 5 hadi 7, pale inazungumzwa kuhusu Yesu na kile alichokifanya kwa ajili ya watakatifu, halikadhalika na juu ya kurudi kwake mara ya pili. Ule mstari wa 8 mara moja unafuatia na maneno hayo,

“Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.”

Kulingana na mistari iliyopo hapo juu kabla ya hii, inaonekana wazi kuwa maneno hayo anazungumza Yesu. Hali kadhalika kulingana na muktadha baada ya mstari huu inaonekana sana huyo ni Kristo – kutokana na ukweli kwamba Yohana anapogeuka “kuiona” ile sauti ambayo ilikuwa inasema naye, alimwona YESU KRISTO (mstari wa 12-18). Katika ule mstari wa 8, yeye anatangaza kuwa ni Bwana (Mungu) ALIYEKO, NA ALIYEKUWAKO NA ATAKAYEKUJA, MWENYEZI. Nimeliweka neno ‘Mungu’ katika mibani hapo juu kwa sababu yapo maandiko ya kizamani yanaonyesha neno ‘Mungu’ na hii ndiyo tafsiri inayopendelewa zaidi nyakati hizi kama vile ilivyo katika tafsiri ya Swahili SUV. Ikiwa hivyo ndivyo ilivyo, basi huo utakuwa ni mstari wa ajabu, ambao ndani yake Yesu Kristo anajitangaza mwenyewe kuwa yeye ni Bwana Mungu. Haungekuwepo ushuhuda mwingine mkuu wa Uungu wa Kristo usemao kuwa yeye ni Mungu kama maelezo ya aina hii!

Hata hivyo, watu wengine wangeweza kudai kuwa neno hili (yaani, ‘Mungu’) lisijumuishwe kwa sababu maandiko mengi mengine hayana neno hilo. Lakini bado maneno hayo “Bwana, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi” yanabaki katika tangazo hili.

Sasa, wacha tukumbuke kuwa katika ile sura ya 4, Mungu aketiye katika kiti chake cha enzi ameelezwa kuwa yeye ni “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja.” Majina yale yale yanatolewa kwa wote wawili – kwa Mungu aketiye katika enzi (katika ile sura ya nne), na kwa Yesu Kristo (kama ilivyo katika ile sura ya kwanza), yaani, ‘aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi’. Je, kunaweza kuwepo jambo jingine lolote lililo kuu zaidi ya hili? Usemi huo unaelekeza juu ya uwepo wa Mungu nyakati zote, ule umilele wake – katika nyakati zote zilizopita, na katika nyakati hizi za sasa, na kwamba yeye atadumu milele na milele, kama Biblia inavyoeleza kumhusu yeye katika Zaburi, “tangu milele hata milele ndiwe Mungu.” (Zaburi 90:2). Katika sura hizo maneno hayo hayo yanatumika kwa wote wawili Baba na Mwana. Aidha, katika mistari hiyo miwili, Bwana katika Ufunuo 1:8, na Mungu katika ule mstari wa 4:8, wote wanaitwa ‘Mwenyezi’, ambazo ni jina la kipekee ambalo linaelekeza juu ya utawala na nguvu za Mungu. Vifungu hivyo vyote ambavyo vinabeba lugha yenye kufanana kwa wote wawili Baba na Mwana vina umuhimu au uzito mkubwa na huongelea juu ya Uungu wake Kristo katika istilahi ya hali ya juu. Ikiweka msingi wa ukweli ambao Kristo mwenyewe ametufunulia pale asemapo kuwa, “Mimi na Baba tu umoja”, na kwamba “watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka.” (Yoh. 10:30; 5:23).

Wengine wangeweza kuwa na maoni kuwa ule mstari wa 8 haukusemwa na Yesu Kristo, lakini huyo ni Mungu asemaye hapo, lakini nimeonyesha hayo kutokana na muktadha wake wa kile ambacho kinaonekana kinaweza kulingana na jambo hili. Hata hivyo hebu tutazame mistari ifuatayo,

“Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja name…Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho…Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzao wa Daudi, ile nyota yenye kung’aa ya asubuhi.” (Ufunuo 22:12 -16).

Katika ile sura ya mwisho ya kitabu cha Ufunuo kwenye ile mistari niliyoinukulu hapo juu, inaonyesha wazi kabisa kuwa azungumzaye hapo juu ni Yesu Kristo mwenyewe. Lile neno lisemwalo “Naja upesi” ni maneno ambayo yamesemwa na Yesu Kristo pia kwenye Ufunuo 3:1. Na tena hata pale mwishoni mwa sura hii anaposema, “Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, ‘Naam; naja upesi.’ Amina; na uje, Bwana Yesu.” ( Ufunuo 22:20). Hapo mwandishi anayajibu maneno ya Yesu kwa kusema “njoo, Bwana Yesu”, hivyo anamtambulisha mnenaji wa kauli hiyo kuwa ni Yesu. Haitushangazi hapa hata kidogo, kwa sababu hata mistari yenyewe ya neno la Mungu tu nayo hujirudiarudia kuwa huyo atakuwa ni Bwana Yesu mwenyewe ambaye atarudi tena hapa duniani katika utukufu wa Baba yake. (Mt.16:27, 25:31;Luka 9:26; 2 Watheslonike1:7-10, nkd).

Katika sura hiyo Bwana Yesu anatangaza, “Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho…” (Ufunuo 22:13), ambayo hiyo ni maneno yaleyale yanayopatikana kwenye ule mstari wa 8 ile sura ya kwanza ambayo na yenyewe tumekwisha kuitazama hapo juu. Hivyo basi Huyo atakuwa ni Yesu ambaye anayanena maneno hayo katika ile sura ya kwanza – au ikiwa Huyo anenaye atakuwa ni Mungu ndipo basi tunaona ya kuwa Kristo kule kwenye ile sura ya 22 yeye kabeba majina yaleyale yenye utukufu wa Baba aliyekuwa pamoja na Mwana tokea mwanzo kwamba wakiwa ni wamoja pamoja naye. Hebu pia tutambue ya kuwa katika ile sura ya 22 kwa mujibu wa mistari iliyonukuliwa hapo juu, Yesu Kristo amejitangaza yeye mwenyewe kuwa yeye ni “wa Kwanza na wa Mwisho”, na usemi huo huo Yesu anautumia kwa uwazi kabisa kumhusu yeye mwenyewe katika Ufunuo 1:17 na 2:8.

Zaidi ya hayo yote, mlinganisho huu wa maandiko na kule kufanana kwake kunatia fora zaidi tunapofikiria maneno yaliyomo katika sura ile ya 21. Kwenye sura ile twasoma kuwa “Na yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema, ‘Tazama, nayafanya yote kuwa mapya.’ Akaniambia, ‘Andika ya kwamba maneno hayo ni amini na kweli.’ Akaniambia, ‘Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure. Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.” (Ufunuo 21:5-7).

Katika sura hii ni wazi kabisa kuwa Huyo anenaye hapo ni Mungu (‘…nami nitakuwa Mungu wake’), anayanena maneno hayo kutoka katika kiti chake cha enzi. Lakini liangalie tangazo alilolifanya, “Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho” – hayo yote ni maneno yaleyale yaliyotumiwa na Mwana wa Mungu kwenye ile sura ya 22 tuliyoiangalîa hapo juu. Baba na Mwana wao ndio mwanzo na mwisho wa mambo yote – Mwanzo na Mwisho, Alfa na Omega. Kama tulivyoona, hayo ni maneno yaleyale yaliyotumiwa na Yesu katika sura ya kwanza na mstari wa nane.

Tunaweza kusimama kwenye kicho tu juu ya ukuu huo!  Maana hii iko juu ya uchambuzi wetu wa kibinadamu. Hayo yote ndiyo yanayotupelekea kuanguka chini na kuabudu mbele za Baba na Mwana. Mwana anashiriki tabia na majina ya Baba (Yoh. 14:9; 2 Wakor. 4:6; 5:19; Heb 1:3) na pia Mwana anashiriki katika nguvu za Baba (Mat. 28:18; Yoh5:21;.Ufunuo11:15). Kweli hii ya hapa mwishoni inakaziwa na ile sura ya mwishoni mwa Biblia mahala ambapo tunakuta maandiko yakisema juu ya kiti cha enzi kimoja – ambacho ni kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwanakondoo.

“Kisha akanionyesha mto wa maji ya uzima, wenye kung’aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwana-Kondoo…Wala hapatakuwa na laana yo yote tena. Na kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo ndani yake. Na watumwa wake watamtumikia.” (Ufunuo 22:1,3).

Kinaitwa kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwanakondoo. Lugha ya Kiyunani inaweka wazi zaidi hapo kuwa hicho ni kiti cha enzi kimoja, na hii ndiyo inavyomaanisha hapo juu. Tunafahamu ya kuwa Yesu Kristo alisema kwamba, “Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.” ( Ufunuo 3:21). Je, ni utukufu wa jinsi gani huo kupata fursa hii na ahadi ya jinsi hii. Ile sura ya 22 inazungumzia tu kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwanakondoo kwamba hicho ndicho chanzo cha uzima, wokovu, uweza na uponyaji wote. Kwa sababu neema yoyote tutakayoipokea wala wito wetu mkuu wowote utakaotupelekea sisi kwenye neema hii ya Mungu, bado sisi sio chanzo cha Uzima na Wema – bali ni Mungu na Mwanakondoo wake anayetawala katika mamlaka na ufalme juu ya wote. Huyo ndiye chanzo cha uzima wote! Ni kutokana na wao ndiko ambapo mto wa maji ya uzima unatokana!

Nimekwishaelezea ukweli kuwa Yesu alijiita mwenyewe kuwa yeye ni “wa Kwanza na wa Mwisho”, na kwa vyovyote hii inadhihirisha ukweli uleule wa maana halisia ya ile “Alfa na Omega”, na ile ya Mwanzo na Mwisho”. Hebu tuliangalie jambo hili sasa kwa ukaribu zaidi na utagundua kuwa jambo hili linakubaliana na kila kitu ambacho tumekwisha kukielezea hapa.

WA KWANZA NA WA MWISHO                                        

Hebu sasa tuendelee kuyatazama maandiko yanayotuonyesha kwamba majina ambayo Mungu hujifunua mwenyewe ni kweli ni majina ya Yesu Kristo. Kwa mfano tunasoma kuwa Yesu Kristo hujifunua mwenyewe kuwa ‘ni mwanzo na mwisho’.

“Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, ‘Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele… Na kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna andika; Haya ndiyo aneneyo yeye aliye wa kwanza na wa mwisho, aliyekuwa amekufa, kisha akawa hai.’” (Ufunuo 1:17,18; 2:8).

Hakuna shaka yoyote kuwa maneno hayo yalisemwa na Yesu Kristo Mwana wa Mungu. Yesu anasema mwenyewe kuwa “Mimi ni wa kwanza na wa mwisho”. Na je, Mungu hujifunua mwenyewe kwa majina gani ndani ya maandiko? Twasoma hivi,

“Ni nani aliyetenda na kufanya jambo hilo, aviitaye vizazi tangu mwanzo? Mimi, Bwana, wa kwanza na wa mwisho, mimi ndiye… Bwana, Mfalme wa Israeli, Mkombozi wako, Bwana wa majeshi, asema hivi; Mimi ni wa kwanza, na mimi ni wa mwisho; zaidi yangu mimi hapana Mungu. (Isaya 41:4; 44:6).

Hakuna Mungu yeyote isipokuwa yeye aliye ‘wa kwanza na wa mwisho’! Na Yesu Kristo anayatumia majina hayohayo juu yake mwenyewe kama tulivyoona hapo juu! Hili ni jambo la kushangaza sana!  Kwenye maandiko Mungu anajifunua mwenyewe kuwa ndiye “wa kwanza na wa mwisho”, na “mwanzo na mwisho”. Kristo naye anajiita mwenyewe kwa majina hayohayo yanayomhusu Mungu, yaani, yeye ni “wa kwanza na wa mwisho”. Hii inafunua kuwa yeye ni wamoja pamoja na Baba, kama mwanzo na mwisho, kutoka umilele hadi umilele. Kutoka kwenye tabia ileile huja majina yaleyale. Lakini majina hata ambayo sasa tunayafikiria yanahusu Mungu tu. Iwe Baba, au iwe Mwana, majina hayo yanahusu Mungu tu. Kutokana na umoja wa Baba na Mwana wao wanashirikisha majina yaleyale. Katika umoja wa Baba na Mwana inatoa au huleta kielelezo kinacholingana, mafunuo ya majina yanayofanana na tabia inayolingana.

Chochote kile cha baraka zozote ambazo Mungu hutupatia nasi, yoyote ile aitendayo ndani yetu ya kutubadilisha na kutufanya watoto wake milele, hatutaweza kulitumia jina lake kujionyesha mwenyewe au kujiita mwenyewe “wa kwanza na wa mwisho”! Ni Mungu pekee ndiye ajiitaye kuwa ni “wa kwanza na wa mwisho.”

Hayo ni majina yake Mungu pekee, yakielezea umilele wake Mungu na uweza wake! Sasa, tunawezaje sisi kwa lugha zetu za kibinadamu kuitendea haki maana hii. Tumeachwa tukisimama na kicho tukiuangilia ukuu wake Mungu pamoja na nguvu za enzi yake. Kama Daudi asemavyo, “Bwana ndiye mkuu mwenye kusifiwa sana, wala ukuu wake hautambulikani.”  (Zab.145:3).

MIMI NIKO AMBAYE NIKO

Kama ilivyo nyakati hizi, vivyo hivyo ndivyo ilivyokuwa nyakati zake Yesu alipokuwa hapa duniani – wapo wale ambao wanapinga kuwa Yesu ni Mungu. Wayahudi walielewa vizuri sana juu ya kile ambacho Yesu alikuwa akiwaambia, na kwa ajili hiyo walimchukia na wakatafuta kumwua kwa vile Yesu alidai kuwa yeye ni wamoja na Baba Mungu. Na pia alitumia maelezo ambayo ni ya ki-Mungu pekee. Hebu sasa tusome mafungu ya maandiko yanayofanana kwa vile mafungo hayo yanakubaliana na yanathibitisha ile tulichokiandika hadi hapa tulipofikia katika somo hili.

“ ‘Mimi na Baba tu umoja.’ Basi Wayahudi wakaokota mawe tena ili wampige. Yesu akawajibu, ‘Kazi njema nyingi nimewaonyesha, zitokazo kwa Baba; kwa ajili ya kazi ipi katika hizo mnanipiga kwa mawe?’ Wayahudi wakamjibu, ‘Kwa ajili ya kazi njema hatukupigi kwa mawe; bali kwa kukufuru, na kwa sababu wewe uliye mwanadamu wajifanya mwenyewe u Mungu.’” (Yoh. 10:30 – 33). Yesu aliposema yeye ni wamoja pamoja na Baba na ndiye Mwana wa Mungu, hapo Wayahudi walielewa vema sana kuwa ni sawa na kusema kuwa yeye alikuwa ni Mungu, na kwa hilo walitafuta kumwua.

Na kwenye ile sura ya 8 tunakutana na hali hiyohiyo. Twasoma, “ Yesu akawaambia, ‘Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko.’ Basi wakaokota mawe ili wamtupie.” (Yoh. 8.58-59).

Wayahudi walielewa vizuri sana maana ya maneno yale ya Yesu alipotumia kuelezea “Mimi niko”, kuwa inamwelezea yeye mwenyewe. Hiki ni kielelezo cha uthibitisho wa moja kwa moja wa jina ambalo Mungu amejifunua kwalo kwa Musa na kwa watu wa Israel kwenye kitabu cha Kutoka 3:14,

“Mungu akamwambia Musa, ‘MIMI NIKO AMBAYE NIKO’; akasema, ‘Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli; MIMI NIKO amenituma kwenu..’”

Hili ndilo jina la Mungu. Kupitia jina hilo Mungu alijifunua kwa Musa. “Mimi Niko, ambaye Niko”. Yeye ndiye aliyekuweko na yupo na atakayekuwepo; yeye ni yule milele! Na Bwana Yesu naye anatumia jina hilo hilo akijitambulisha mwenyewe! Wala haishangazi kuona kuwa Wayahudi walitaka kumwua Yesu kwa sababu walitambua kuwa kwa kutumia jina hili alikuwa akijifananisha mwenyewe kuwa ni Mungu.

Hapo Yesu alithibitisha mambo yale ambayo tumeshayasoma katika somo hili, yaani, yeye alikuwepo pamoja na Baba toka mwanzo, kabla ya kuwekwa misingi wa ulimwengu! Mimi niko!

[Katika tafsiri ya Kiyunani ya Agano la Kale (liitwalo Septuagint) kwenye mstari ambao mpaka sasa tumekwishauangalia (Isaya 41:4), maelezo yaleyale yanatumika na Mungu: “Ni nani aliyetenda na kufanya jambo hilo, aviitaye vizazi tangu mwanzo? Mimi, Bwana, wa kwanza na wa mwisho, mimi ndiye.” Kwa Kiyunani neno hili “Mimi ndiye” mwishoni mwa mstari huo ni ‘εγω ειμι’ (kwa kutamka: ‘ego emi’), na maneno hayo hayo (ego emi) yalitumiwa na Yesu alipowaambia Wayahudi, “Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko.” Hayo maneno ‘mimi niko’ (au tunaweza kuyatafsiri ‘Mimi ndiye’) kwa Kiyunani (lugha ya asili ya Agano Jipya) ni yale yale yaliyoyatumiwa na Mungu kwenye Isaya, yaani, ‘εγω ειμι’ (ego emi).]

Yesu alipowaambia Wayahudi, ‘mimi niko’, hapo hamna hoja wala machanganyiko wala kutokuelewa – walijua alitumia usemi wa Mungu juu yake mwenyewe.

Siku za leo watu hawatumii mawe bali wao hutumia mantiki za kibinadamu tu kuiangamiza kweli hii. Yesu anaposema, “Mimi niko”, hii inamaanisha kuwa Yeye ndiye yeye yule milele na milele, inamaanisha kuwa hazikupata kutokea nyakati ambazo Yeye hakuwepo. Maana Yesu in yeye yule jana, leo, na milele (Waebr. 13:8). Alikuwepo, na yupo na adumu milele.

Katika kile kitabu cha Waebrania sura ya saba, mwandishi pale analinganisha ukuhani wake Yesu Kristo na ule wa Melkizedeki ambaye “hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wa siku zake wala mwisho wa uhai wake, bali amefananishwa na Mwana wa Mungu; huyo adumu kuhani milele”. (Waebr. 6:20; 7:3). Mambo mengi yangeweza kusemwa kuhusiana na mistari hiyo, lakini katika huu mstari wa mwisho hebu tugundue kuwa Melkizedeki alifanyika kuwa mfano wa Mwana wa Mungu – hii inamaanisha  kuwa yeye naye hakuwa na mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake. Hicho ni kielelezo cha Mwana wa Mungu. Yesu yuko hivyo, yeye hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake, lakini alikuwa pamoja na Baba ‘hapo mwanzo’.

Kwa sababu Yesu Kristo ni Mwana wa Baba yake na wote wawili ni wamoja, inawezekanaje Kristo kama Mwana asiwe Mungu?

KITI CHAKO CHA ENZI, MUNGU, NI CHA MILELE NA MILELE.

Akiuongelea utukufu wa Mwana kwenye kile kitabu cha Waebrania, mwandishi anaonyesha jinsi Mungu alivyomwinua Mwanawe zaidi kuliko malaika, akisema,

“Na kwa habari za malaika asema, ‘Afanyaye malaika zake kuwa pepo, Na watumishi wake kuwa miali ya moto.’ Lakini kwa habari za Mwana asema, ‘Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele; Na fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili.’” (Waebr.1:7-8).

Na hapa sasa mwandishi ananukuu kutoka katika kitabu cha Zaburi 45:6, napo hapo panatuonyesha sisi kwamba mstari huu wa kuunabii unamhusu Mwana, Yesu Kristo; “Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele, Fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili.”

Kwa kweli hakuna tangazo kuu kuliko hilo linalomhusu Yesu Kristo! Je, kweli haitupasi sisi kuhofu kuacha kukimbilia kufanya matafsiri ya mstari huu ambayo utaleta michanganyiko ya  maana yake ya wazi? Katika somo hili ni matumaini yangu kuwa utatambua kuwa tunaongozwa na neno la Mungu katika kuuelewa ukweli wake. Tunaachilia maana halisia na ya wazi ya mistari mingi ichonge kufikiri kwetu na kuelewa kwetu. Wale wenye maoni kwamba Yesu sio Mungu wanalazimika kutafuta sababu kwa nini mistari hii inabeba maana tofauti kabisa, au kwa ujumla ni tofauti kabisa na maana halisia na ya wazi iliyotolewa na neno lolilotumika katika mistari hiyo. [Kiyunani cha mstari huu kiko wazi, ““προς δε τον υιον (λεγει) ο θρονος σου ο θεος εις τον αιωνα του αιωνος”, ambayo kinatafsiri, “kwa Mwana anasema, kiti chako cha enzi Mungu ni cha milele na  milele.” Na kiebrania cha Zaburi 45:6 inaweza tu kutafsiriwa kwa namna hii!] Watu ambao hawataki kukubaliana na ukweli huu huvunja kanuni zote za lugha na sarufi zake ili kutaka kuifanya mistari iseme kitu kingine tofauti na kile ambacho tayari kimeshasemwa!

Kwenye Ufunuo sura ya 22 tayari tumeshaona kwamba kile kiti cha enzi ni kiti cha Mungu na cha Mwana-kondoo. Kwenye Waebrania sura ya kwanza, kweli hiyo inakazwa tu.

 

IMANUELI

Neno la Mungu hufanya ukweli huu wazi tena na tena. Katika Isaya 7:14 tunasoma unabii huu: “Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.” Na Mariamu alipokuwa ana ujauzito wa Yesu, Mathayo ananukuu kifungu hiki kutoka Isaya 7 na anaonyesha kwamba ujauzito wa Mariamu ulikuwa utimilifu wa unabii wa Isaya, akituelezea kwamba Imanueli anamaanisha “Mungu yuko nasi”. (Mathayo 1:23).

Yesu Kristo ni “Mungu pamoja nasi!”

Mungu, kupitia malaika, alimwambia Yosefu kwamba jina ambalo Yesu angepewa ni “Mungu pamoja nasi”, na kama Yesu alivyosema katika Yohana 10:35, ‘maandiko hayawezi kuvunjika’ – na pia andiko hili katika Mathayo 1 haliwezi kuvunjika ambavyo linasema kwamba Yesu Kristo ni “Mungu pamoja nasi”! Kwa maneno mengine, hii ni ukweli haijalishi mtu ye yote anasemaje! Yesu ni Mungu…pamoja nasi!

Mathayo anamnukuu tena Isaya kuonyesha jinsi unabii umetimia juu ya Yesu Kristo. Yesu anaenda kukaa Kapernaumu, na Mathayo anatuambia hiyo ni utimilifu wa unabii wa Isaya ambapo inasema, “Watu wale waliokaa katika giza wameona mwanga mkuu, nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti Mwanga umewazukia,” (Mathayo 4:16), ambayo ni maneno yale yale tunayopata katika Isaya 9:2. Lakini tunapoangalia chini katika sura ya 9, tunasoma hii: “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani.” (Isaya 9:6).

Hii inamzungumzia Bwana Yesu Kristo, mwokozi wetu – yeye ni Mungu mwenye nguvu. Ni mtoto aliyezaliwa, na mwana aliyetolewa kwa ajili ya wokovu wetu. Amepewa nguvu zote mbinguni na duniani. Amani imehubiriwa kwetu na Yesu Kristo ambaye ni Bwana wa wote (Matendo 10:36), kwa maana yeye ndiye amani yetu (Waefeso 2:14). Ni Mkuu wa uzima (Matendo 3:15), na Mungu amemtukuza awe Mkuu na Mwokozi (Matendo 5:31). Kristo ni hekima ya Mungu kwetu (1Wakorintho 1:24,30) ambaye ndani yake yeye hazina zote za hekima na maarifa zimesitirika (Wakolosaia 2:3). Kristo ambaye ni mng’ao wa utukufu wa Mungu na chapa ya nafsi yake ni ya ajabu kwetu katika utukufu wake! Ni Mungu mwenye nguvu  kwetu.

Kuhusu maelezo ya ‘Baba wa milele’, ambayo yanaweza yasiwe rahisi kueleweka kwa kuyalinganisha na Yesu Kristo, ngoja niseme haya. Kama tutakavyoona, Baba na Mwana wote wamehusika katika wokovu wa mwanadamu. Wote, Baba na Mwana huitwa,  ‘Mwokozi’; tunapokea neema na amani kutoka kwao, Baba na Mwana, na bila shaka tumezaliwa mara ya pili katika msingi wa kufa na kufufuka kwa Kristo, kama asemavyo Petro, “Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi ALITUZAA MARA YA PILI ili tupate tumaini lenye uzima KWA KUFUFUKA KWAKE YESU KRISTO KATIKA WAFU.” (1Petro 1:3). Akiwaandikia Wakorintho Paulo alisema, “Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu. Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na KATIKA KRISTO WOTE WATAHUISHWA…Mtu wa kwanza Adamu, akawa nafsi iliyo hai; Adamu wa mwisho ni roho yenye kuhuisha” (1Wakorintho 15: 21-22,45). Kristo, ambaye ndiye Adamu wa pili, ndiye Roho mtoa uzima ambaye kwake tunapata uzima. Ni Mkuu wa uzao mpya wa wanaume na wanawake wenye haki kwa njia yake na ambao wataishi milele na yeye. “Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki…..Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika yeye.” (Warumi 5:19; 2 Wakorintho 5:21). Kama Baba anavyohusika na wokovu wetu na kuongezeka kwake, vivyo hivyo kwa kufa na kufufuka kwa Kristo tunaokolewa na kuzaliwa mara ya pili. Na neno la Mungu linatufundisha kwamba tumezaliwa mara ya pili “kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu.” (1 Petro 1:3).

BWANA WA MABWANA, NA MFALME WA WAFALME

Katika waraka wa kwanza wa Timotheo, Mtume Paulo anampa Mungu utukufu kwa maneno haya,

“Sasa kwa Mfalme wa milele, asiyeweza kuona uharibifu, asiyeonekana, Mungu peke yake, na iwe heshima na utukufu milele na milele.” (1 Tim. 1:17).

Kwenye sura ya sita, Paulo anamhimiza Timotheo kwa maneno haya;

“kwamba uilinde amri hii pasipo mawaa, pasipo lawama, hata kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo; ambako yeye kwa majira yake atakudhihirisha, yeye aliyehimidiwa, Mwenye uweza peke yake, Mfalme wa wafalme, Bwana wa mabwana; ambaye yeye peke yake hapatikani na mauti…”. (1 Tim. 6:14-16). 

Katika maandiko haya tunaona kuwa Mungu anatajwa kuwa Mfalme wa Milele, Mfalme wa Wafalme, Bwana wa Mabwana, yeye pekee ndiye aliye na hali ya kutokufa. Ni nani sifa hizi ila Mungu pekee? Tuangalie kitabu cha Ufunuo mahali kinaposema kuwa,

“Hawa watafanya vita na Mwana-Kondoo, na Mwana Kondoo atawashinda, kwa maana Yeye ni Bwana wa Mabwana, na Mfalme wa Wafalme, na hao walio pamoja naye ndio walioitwa, na wateule, na waaminifu.” (Ufuno 17:14).

Bila shaka, Mwana kondoo ni Bwana Yesu Kristo naye ndiye anayeitwa Bwana wa Mabwana na Mfalme wa Wafalme! Tena kwenye kitabu cha Ufunuo twasoma haya:

“Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita. Na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi…Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu. Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi. Na upanga mkali hutoka kinywani mwake ili awapige mataifa kwa huo. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, naye anakanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu Mwenyezi. Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, mfalme wa wafalme, na bwana wa mabwana.” (Ufunuo 19:11-16).

Bila shaka haya yanaongea kumhusu Yesu Kristo. Katika kifungu hiki, yule aliyempanda farasi anaitwa ‘Mwaminifu na Wa-kweli’, na katika Ufunuo 3:14 Yesu asema, “Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli.” Kwenye kifungu hiki tunaambiwa “macho yake yalikuwa kama mwali wa moto” na “upanga mkali hutoka kinywani mwake”, na ndiyo tunayosoma kwenye Ufunuo 1:14,16 na 2:18 kuhusu Yesu Kristo. Yesu ndiye ‘Neno la Mungu’ na hili linatukumbusha Yohana 1:1. Na Je, ni nani huyo ambaye vazi lake limechovywa kwenye damu ila Mwokozi wetu Yesu Kristo. Na Yesu Kristo huyu huyu anaitwa ‘mfalme wa wafalme, na bwana wa mabwana’ katika kifungu hiki! Yeye ndiye Mkuu wa Wafalme wa dunia! (Ufunuo 1:5).

Iwapo kauli inayosema “Mfalme wa Wafalme na Bwana wa Mabwana ambaye pekee ni wa milele” inaongea kumhusu Mungu, basi ujue kuwa Yesu Kristo pia ni Mfalme wa Wafalme na Bwana wa Mabwana  naye ni Mungu! Wote wawili wana majina sawa – isipokuwa unamini kuwa 1 Timotheo 6: 14-16 pia inamhusu Yesu Kristo na aya hizi zote zinarejelea Kristo.

KILA GOTI LITAPIGWA MBELE ZANGU

Sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo. Hii ndio Paulo anasema katika Warumi 14:10 -12: “Lakini wewe je! Mbona wamhukumu ndugu yako? Au wewe je! Mbona wamdharau ndugu yako? Kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo. Kwa kuwa imeandikwa, ‘Kama niishivyo, anena Bwana, kila goti litapigwa mbele zangu; Na kila ulimi utamkiri Mungu.’ Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu.” Hapa, Paulo ananukuu kutoka Isaya 45: 22,23, ambapo anasema,

“Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana mimi ni Mungu; hapana mwingine. Kwa nafsi yangu nimeapa, neno hili limetoka kinywani mwangu katika haki, wala halitarudi, ya kwamba mbele zangu kila goti litapigwa, kila ulimi utaapa.”

Lakini hii inasemwa kuhusu Mungu kwamba kila goti litapiga magoti na kila ulimi wataapa kwa MUNGU, na bado Paulo ananukuu aya hii kutoka kwa Isaya na kufanya ireje kwa Yesu Kristo.

Lazima ifahamike kuwa katika Warumi 14:10 miswada mingi sana ina maneno haya, “kiti cha hukumu cha Kristo”, kama ilivyo nukuliwa hapo juu. Hata hivyo miswada michache sana ya kale ina maneno haya: “kiti cha hukumu cha Mungu”, na wasomi wengi wa kisasa hupendelea kufuata nakala za hii miswada ya kale. Lakini  hapana shaka kwa kile kilichoandikwa katika 2 Wakorintho 5:10, isemayo kuwa, “Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.” Hivyo maandiko yanafundisha wazi kwamba sote tutadhihirika mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo.

Na tunasoma nini katika Wafilipi sura ya pili? Tunasoma yafuatayo:

“Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.” (Wafilipi 2:9-11).

Maneno haya yanatukumbusha aya za Isaya 45 zilizonukuliwa hapo juu, zikisema kuwa kila goti litapigwa mbele za Mungu na kila ulimi utamkiri yeye.

Katika muktadha huu tutanukuu kutoka Ufunuo 20 inayozungumzia kuhusu hukumu ijayo:

“Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana. Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.” (Ufunuo 20:11-12).

Katika kifungu hiki tunaambiwa kuwa kila mmoja atasimama mbele ya Mungu na kuhukumiwa kwa kadri ya matendo yake, hii ni sawa na tulivyosoma hapo juu katika 2 Wakorintho, yaani sote tutadhihirika mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, na kuhukumiwa kwa kadri ya yale tuliyotenda. Kifungu hiki katika Ufunuo kinazungumzia, ‘kiti cha enzi kikubwa cheupe’ ambapo ndipo hukumu itakapotolewa, na anapozungumza habari ya kurudi kwake duniani kuhukumu ulimwengu, Kristo anasema hivi,

“Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake; na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi.” (Mathayo.25:31-32).

Siku hiyo ya hukumu, Kristo atakaa katika kiti cha enzi cha utukufu wake kuhukumu mataifa. Huku kulingana na kufanana kwa aya hizi ni maajabu – kinachosemwa juu ya Mungu, ndicho kinachosemwa juu ya Bwana Yesu!

Ukweli kwamba Kristo atauhukumu ulimwengu unathibitishwa katika aya mbili zifuatazo.

“Akatuagiza tuwahubiri watu na kushuhudia ya kuwa huyu (Kristo Yesu) ndiye aliyeamriwa na Mungu awe Mhukumu wa walio hai na wafu.” (Matendo10:42).

“Tena Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana hukumu yote.” (Yohana 5:22).

Katika kifungu cha Ufunuo aya ya 20 iliyonukuliwa hapo juu, pia tunasoma kuhusu ‘kitabu cha uzima’, ambamo watu waume na wake watahukumiwa. Kitabu hiki pia huitwa, ‘kitabu cha uzima cha mwanakondoo aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia’ na  ‘kitabu cha uzima cha mwana kondoo’. (Ufunuo.13:8; 21:27). Ni wazi kwamba hii inarejelea kwa Yesu Kristo, na ni wale pekee ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima cha mwanakondoo ambao watarithi uzima wa milele! (Ufunuo.13:8; 17:8; 20:15). Kama tutakavyoendelea kuona katika somo hili, tunapata uzima wa milele kupitia kwa Yesu Kristo na ndani yake tu! (1Yoh 5 :11,12).

Na wataonekana wapi, wale waliokana Uungu wa Yesu, waliodai kwamba Yesu si Mungu?

Yesu alisema, mimi na baba tu umoja (Yohana 10:30), na ukweli wa ‘umoja’ huu baina ya Baba na Mwana unafunuliwa katika jina ambalo wote huitwa na katika Uungu wanaoshiriki!

Yesu Kristo sio aina fulani ya kiumbe maalum cha kiungu! Yeye ni Mwana wa milele wa Baba wa milele, na yeye ni mmoja pamoja naye, ili kila mtu amheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba (Yohana 5:23).

Uungu wa Yesu Kristo na umoja wake na Baba umeonyeshwa zaidi na vifungu vingi vya maandiko.

MUNGU MWOKOZI WETU, KRISTO MWOKOZI WETU

Mwanzoni mwa kila barua ambayo Paulo anaandika anasema hivi, “Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.” (Warumi 1:7). Petro anaandika vivyo hivyo, na Yohana anasema hivi, “Neema iwe nanyi, rehema na amani, kutoka kwa Mungu Baba na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo, Mwana wa Baba, kwa ukweli na upendo.” (2 Yohana 3). Tumeona jinsi Baba na Mwana wanavyoabudiwa pamoja mbinguni na jinsi Mwana anakaa na Baba yake kwenye kiti cha enzi (Ufunuo 3:21), na sasa tunaona jambo lingine la kushangaza. Neema, rehema na amani ambayo imetajwa katika aya hizi inaweza tu kutolewa kutoka kwa Mungu. Hakuna malaika, hakuna kiumbe aliyeumbwa, hakuna mwanadamu anayeweza kutupatia neema, rehema na amani inayotupatia neema ya kuokoa na nguvu ya Mungu ya kututunza – hii inatoka kwa Mungu pekee. Na katika aya hizi tunaona kuwa Baba na Mwana ni mmoja katika kuwapa neema ya kimungu wanaume na wanawake rehema na amani. Hakuna mtu isipokuwa Yeye ambaye ni Mungu awezaye kufanya hivi.

Mungu ametajwa kama “Mungu Mwokozi wetu” katika Agano Jipya (Kwa mfano, 1 Tim. 2:3). Lakini tunajua kuwa hii pia ni jina alilopewa Yesu Kristo – Yesu Kristo ni “Mwokozi wetu”, kama anavyosema Petro kwenye barua yake ya kwanza, “Lakini kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo.” (2 Petro 3:18). Mungu hutuokoa, na Kristo Yesu hutuokoa. Ni nani anayeweza kuokoa kutoka kwa dhambi, kifo na nguvu za Shetani isipokuwa Mungu pekee? Baba na Mwana ni moja katika kazi ya wokovu (pamoja na Roho Mtakatifu), na wokovu ni kazi ya Mungu – sio kazi ya malaika aliyeumbwa au mwanadamu. Kwa sisi kuokolewa na kusafishwa kutoka kwa dhambi, ilibidi Mungu aliyejitoa msalabani kwa ajili yetu – dhabihu ya malaika aliye juu zaidi, au sadaka ya kiumbe kingine cha aina ye yote, hakuna hata kimoja katika hivi vyote vinavyoweza kutuokoa kutoka kwa dhambi na kifo.

Petro anasema hivi katika barua yake ya pili: “Simoni Petro, mtumwa na mtume wa Yesu Kristo, kwa wale waliopata imani moja na sisi, yenye thamani, katika haki ya Mungu wetu, na Mwokozi Yesu Kristo…” (2 Petro 1:1). Aya hii inasema kwamba tunapokea imani kupitia HAKI ya Mungu na ya Bwana Yesu Kristo. Ni haki moja ambayo hutoka kwa Baba na Mwana! Labda hii haijulikani wazi katika tafsiri ya Kiswahili lakini maandishi ya Kiyunani yuko wazi – ni haki inayotokana na Mungu na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Haki ya nani inaweza kukuokoa isipokuwa haki ya Mungu?

Lakini katika ufafanuzi kuhusu aya hii ni lazima ieleweke kwamba tafsiri kwa Kiswahili na kwa Kiingereza haifuati miswada karibu yote ya Kiyunani ambayo yalisomeka hivi, “…kupitia haki ya Mungu na Mwokozi wetu Yesu Kristo”, sio, “…kupitia haki ya Mungu wetu na ya Mwokozi Yesu Kristo.” Yaani, sawasawa na miswada karibu yote (hata ya kale sana) ya Kiyunani ya Agano Jipya Petro aliandika kwamba Yesu Kristo ni “Mungu na Mwokozi wetu.” Jambo la ajabu! Tunakutana na kweli hii tena na tena katika maandiko.

KUJAZWA NA UTIMILIFU WA MUNGU NA KRISTO.

Katika sura ya tatu ya waraka wa Paulo kwa Waefeso, Paulo aliomba kwamba waumini wapate kufahamu kiwango kamili cha “upendo wa Kristo, ili kwamba wajazwe na utimilifu wa Mungu.” Kujua utimilifu wa upendo wa Kristo hapa inalinganishwa na kujazwa utimilifu wote wa Mungu! Pasipo kujua kina cha upendo wa Kristo, hatuwezi kujua “utimilifu wa Mungu” maishani mwetu! Unaweza kuona ni kwa jinsi gani wawili wanakuwa mmoja katika Uungu wao? Huu siyo upendo wa malaika au kiumbe mzuri! Bali yeye ambaye ni Muumba na Mwokozi wetu anaweza kutupenda kama alivyotupenda, na kutoa uhai wake kama alivyofanya kwa ajili yetu. Huyu atakuwa ni Mungu pekee. Ni upendo wa Mungu kuelekea kwetu; ni upendo wa Kristo kwa ajili yetu. Mungu ni pendo, na upendo wa Kristo unawakilisha utimilifu wa upendo wa Mungu, kwa sababu ni Mungu. Katika sura inayofuata Paulo anaeleza na kufundisha jinsi kila huduma ya kanisani inapaswa kutuleta “kwenye kipimo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.” Katika hizi aya mbili (Waefeso 3:19; 4:13) Paulo haonyeshi kutofautisha utimilifu wa Mungu na utimilifu wa Kristo. Utimilifu wa Kristo ndio utimilifu wa Mungu, hata Wakolosai 2:9 anatangaza: “Maana katika yeye (Kristo) unakaa utimilifu wote wa Mungu kwa jinsi ya kimwili.” Ni ajabu gani maandiko yote yanakubaliana na kutegemeza ukweli huo!

INJILI YA MUNGU NA YA KRISTO

Katika Warumi Paulo anatueleza kwamba “alitengwa kwa ajili ya Injili ya Mungu,” (Warumi 1:1), na baadaye katika sura 15 anasema juu ya huduma yake, “…mpaka Iliriko nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa utimilifu.” (Warumi 15:19). Habari njema ya Mungu ni habari njema ya Yesu Kristo. Maandiko hayatofautishi; yanatuonyesha kuwa Baba na Mwana ni wamoja kwa asili na kwa huduma. Habari njema ya wokovu inatoka kwa Baba na kwa Mwana.

MUNGU MKOMBOZI WETU

Bwana Mungu anatangaza mwenyewe kuwa Mkombozi wa Israeli (Zaburi 78:35; Isaya 48:17), na katika Agano Jipya lote, Yesu ametangazwa kama ndiye atupaye ukombozi, na ambaye anatukomboa toka kwenye dhambi na uovu (Luka 2:38; Waefeso 1:7; Warumi 3:24; Tito 2:14). Baba na Mwana ni kama mmoja katika ukombozi wetu na kubeba jina la Mkombozi.

MUNGU MUME WETU, KRISTO YESU MUME WETU

Katika Isaya 54:5, “Mungu wa dunia nzima” anaitwa ‘mume’ wa Israeli: “Kwa sababu Muumba wako ni mume wako; Bwana wa majeshi ndilo jina lake; na Mtakatifu wa Israeli ndiye Mkombozi wako; Yeye ataitwa Mungu wa dunia yote.” Katika Agano Jipya uhusiano kama huu unaonekana kati ya Kanisa na Yesu Kristo, ambapo Kanisa linaitwa Bibi harusi wa Kristo; Kristo ni Mume wetu mtarajiwa: “Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi.” (Wakor. 11:2 pamoja na Warumi 7:4; 2 Ufunuo 21:2).

BWANA MCHUNGAJI WETU

Katika Agano la Kale, Bwana Mungu ndiye aliyewaita watu wake kundi na Kondoo wa malisho yake, na katika Isaya alipotangaza habari njema itakayotangazwa Yerusalrmu, Mungu alisema atalisha kundi lake kama mchungaji. Haya ni maneno ya ajabu tusomayo: “Jueni kwamba BWANA ndiye Mungu; ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake; na kondoo wa malisho yake” (Zaburi 100:3); na katika Isaya, “wewe uhubiriye Sayuni habari njema, panda juu ya mlima mrefu; wewe uuhubiriye Yerusalemu habari njema, paza sauti kwa nguvu; paza sauti yako usiogope; iambie miji ya Yuda, tazameni, Mungu wenu…..atalilisha kundi lake kama mchungaji: atawakusanya wana kondoo mikononi mwake na kuwaweka kifuani mwake, nao wanyonyeshao atawaongoza polepole.” (Isaya 40:9-11).

Ni Yesu Kristo aliyejitambulisha mwenyewe kama mchungaji wetu mwema; sisi ni kondoo wake na kundi lake na ni kupitia yeye tunapata malisho. (Yohana 10:9,14,16). “Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu”. (Zaburi 23:1). Ni nani huyu Bwana, mchungaji wangu? Ni Yesu Kristo. Ni Mungu.

Unawezaje kutenganisha wawili hao? Ni nani atakayetenga Kristo na Mungu? Nani atakayemtenga Kristo na Uungu? Ni nani atakayetenga Kristo asiwe Mungu? Haiwezekani. Haifikiriki.

Kama mbinguni ambapo wote Baba na Mwana huabudiwa, kwa hivyo katika aya zilizo hapo juu ambazo tumeangalia tu neno la Mungu hazifanyi tofauti kati ya Baba na Mwana kuhusu umungu wao, na kwa kuzingatia nguvu yao ya kuokoa na kutunza.

USHIRIKA PAMOJA NA BABA NA MWANA

Tunapata mstari mwingine wa kushangaza katika 1 Yohana 1:3 ambapo inasema, “Hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo.” Kupitia wokovu huu tunaletwa katika ushirika na Baba na Mwana! Hatushiriki na aina mbili tofauti za maisha! Hapana. Tunashikiri uzima huo mmoja wa milele ulio ndani ya Baba na Mwana, kama Yesu alivyosema, ‘yeye ambaye ameniona amemwona Baba’.

Kukubaliana na hii ndivyo Yesu anasema katika maombi yake kwa Baba katika Yohana 17; 3: “Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.” Je! Uzima wa milele ni nini? Uzima wa milele ni KUMJUA BABA NA KUMJUA MWANA. Hakuna aina mbili tofauti za maisha! Uzima wa milele ni kumjua Baba na Mwana – ni maisha mamoja kwa wote wawili. Hakuna tofauti. Yeye aliye na Mwana anao uzima! (Yohana 3:36; 1 Yohana 5:12).

Yesu aliposema, “wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli”,  hii inasemwa kwa kulinganisha na miungu wanayoiabudu watu. Siyo kuukana Uungu wa Kristo. Kama tulivyoona, uzima wa milele ni kumjua Baba na Mwana. Zaidi ya hayo, tutaona katika 1 Yohana 5:20 mtume Yohana anamwita Yesu “Mungu wa kweli na uzima wa milele”.

Kuna aya nzuri na ahadi ya ajabu ambapo Yesu anasema maneno haya: “Ikiwa mtu ananipenda, atashika maneno yangu, na Baba yangu atampenda, na TUTAKUJA kwake, na KUFANYA MAKAO KWAKE.” (Yohana 14:23). Mungu anakuja kuishi ndani yetu – Baba na Mwana, kwa Roho Mtakatifu! (Yohana 14:16-23). Pale Yesu alipo, Mungu yupo.  Pale Mungu alipo, Yesu yupo, kama ilivyoandikwa, “Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na yeye, bila kuwahesabia makosa yao,”  (2 Wakorintho 5:19), na tena, “Mimi na Baba tu umoja.”

Zaidi ya hii, katika 1 Wakorintho 6:19 tumefundishwa kuwa sisi ni hekalu la Roho Mtakatifu.  Je! Unaona?  Baba, Mwana na Roho Mtakatifu hukaa ndani ya mwamini.

Kristo ndiye kila kitu kwetu.  Kristo ni Mungu kwetu! (1 Wakor. 1:30).

—————————————–

Hebu hadi hapa tuweke wazi juu ya maeneo muhimu mawili hivi juu ya hatua hii tuliyofikia.

  1. Yesu Kristo alisema “Mimi na Baba tu wamoja”. (Yoh.10:30). Lakini hapo ujue kuwa Yesu hakusema kuwa “Mimi ni Baba” wala hakuna lolote kwenye Biblia linaoelezea kuwa eti Yesu ni Baba. Kuna mistari mingi ya neno la Mungu yenye kuelezea uwazi wa kutosha kabisa kwamba kuna Baba na Mwana. Mfano mmojawapo mzuri unapatikatina katika Injili ya Yohana 5:30 na mistari mingine mingi mingi.
  2. Kama ukiyajua maandiko, basi utagundua kuwa Biblia haizungumzii juu ya Miungu wawili au watatu. Biblia yenyewe haitumii aina hii ya lugha. Kile kinachofanywa wazi na neno la Mungu ni kwamba kuna Mungu mmoja.( Kumbukumbu 6:4; Waefeso 4:6). Nitagusia ili kuelezea juu ya kipengele hiki na mambo yanayohusiana nacho mwishoni mwa somo hili.

NENO ALIKUWA MUNGU

YOHANA 1

Sasa tutaendelea na somo letu kwa kuangalia kifungu cha ajabu katika sura ya kwanza ya Injili ya Yohana.

Baadhi ya watu hupenda kubishana kuhusu maana ya maneno ya lugha ya Kiyunani katika Injili ya Yohana 1:1, mfano ni Mashahidi wa Yehova, lakini ukweli ni ule tuliousoma kwenye maandiko hapo juu. Natumaini unatambua ya kwamba hatuchukui neno moja nje ya muktadha na kujaribu kuunda mafundisho yetu, bali tunaunganisha aya zinazozungumzia jambo moja, pasipo kutoa maelezo marefu au kutengeneza mafafanuzi yetu wenyewe.

Hebu sasa tuutazame Injili ya Yohana:

“Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.” (Yoh. 1:1)

Hebu tuanze na maneno, “Hapo mwanzo…”

Basi tutambue na kukubali ukweli kwamba neno la Mungu linalotupeleka kwenye ‘mwanzo’. Fikra za binadamu haziwezi kutufanyia hayo. Hakika hata mantiki ya binadamu na akili yake haziwezi kutufanyia hayo. Mungu tu ndiye anaweza kutueleza mambo hayo katika aya hizo hapo juu. Injili ya Yohana sura ya kwanza aya ya kwanza inatambulisha na kuainisha ule ‘mwanzo’ kwa ajili ya uelewa wetu. “Hapo mwanzo…MUNGU” – Baba na Mwana! Huu ni ufunuo. Hakuna popote katika Biblia inapotaja au kutaka kutueleza ilivyokuwa ‘kabla’ ya ‘mwanzo’! Mungu ni mwanzo – Alfa na Omega, wa kwanza na mwisho, tangu milele hata milele. Hakuna ‘mwanzo’ kabla Yake!

Kila kitu huanza na Baba na Mwana. “Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako.” (Yohana 17:5). Huu ndio ‘mwanzo’ uliofunuliwa kwetu katika maandiko matakatifu. Kabla ya kuumbwa kitu chochote, alikuwepo Baba na Mwana – (na Roho wa milele, Waebrania 9:14, lakini hili siyo la kuzingatia katika somo hili.) Maandiko hayazungumzii lolote kuhusu ‘kabla’ ya huo mwanzo, kwa sababu hakuna cha kujifunza, zaidi ya kwamba Baba alikuwepo pamoja na Mwana.

Tatizo huja pale watu wanapotumia hoja za kibinadamu na kunukuu vifungu vichache vya maandiko vyenye kuashiria uwepo wa matukio ‘kabla ya huo mwanzo’. Hii inaleta machanganyiko na matatizo tu. Kwa nini? Kwa sababu neno la Mungu halitupeleki huko wala halitufunulii ilivyokuwa kabla ya ‘huo mwanzo’. Kutumia hoja za kibinadamu kwa kudhania mambo na kubahatisha (to speculate) hakuleti mwanga wa ufahamu. Kama utajaribu kufanya hivi, utasema mambo ambayo hayasemwi na Biblia, kwa kudai mambo yasiyofundishwa na Biblia. Kama neno la Mungu halitupi ufahamu ama ufunuo kuhusu jambo fulani ni dhahiri kwamba utazusha wazo lisilopatana na Biblia kwa kutumia lugha isiyokuwepo katika neno la Mungu. Katika historia haya ndiyo matokeo pale watu walipojaribu kwenda nje ya upeo wa kile kinachosemwa na Biblia.

Hivi kuna jina kubwa au jina lenye nguvu kuliko hili — Mungu akamwambia Musa, “MIMI NIKO AMBAYE NIKO”? Na akaendelea na maneno Haya, “Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli; MIMI NIKO amenituma kwenu” (Kutoka 3:14). Yesu alisema namna hiyo alipoongea na Wayahudi, “kabla Ibrahimu hajakuwako, Mimi niko”. Maneno hayo yana maana sana ni marejeo ya umilele wa Baba na Mwana — alikuwepo, yupo na atakuwepo milele na milele! Libarikiwe jina lake!

Unatafuta maarifa gani tena? Hakuna. Ni maajabu gani ungegundua? Hakuna hata moja. Kulikuwa na ‘tukio’ gani kabla ya huo mwanzo? Biblia haisemi kuhusu ‘tukio’ lolote, bali yatueleza kuwa hapo mwanzo, kabla ya kuumbwa kitu chochote, Baba na Mwana walishiriki utukufu pamoja. Wapo milele na milele.

“Kabla haijazaliwa milima, wala hujaumba dunia, na tangu milele hata milele ndiwe Mungu” (Zaburi 90:2).

Yesu uhai wake hauna mwanzo wala mwisho (Waebrania 7:3), ni Baba milele na milele (Isaya 9:6)

Neno la Mungu haliwafungulii milango wale wabahatishao ama wenye hoja za kibinadamu kwa suala hili. Tunapaswa kupokea neno la Mungu kwa unyenyekevu na kumwabudu Baba aliyemtoa mwanawe kwetu, na kumwabudu Mwana aliyetoa uhai wake kwako na kwangu.

Baadhi ya watu husema kuwa hatupaswi kutumia jina la ‘Yesu Kristo’ tunapoeleza kuhusu ‘neno aliyekuwepo hapo mwanzo’. Lakini tunapaswa kukumbuka kuwa Baba na Mwana wametupatia wokovu kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu! (Waefeso 1:4; 1Petro 1:20; Ufunuo13:8). Yesu aliwekwa kuwa mwokozi na masihi kabla ya kuumbwa dunia, tena ndiye Yesu Kristo aliyeomba maneno yafuatayo: “Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako.”

Kwa kweli, mwanzo wa Injili ya Yohana unatukumbusha aya ya kwanza kwenye Biblia:

“Hapo mwanzo Mungu aliumba…”

Kwa wale wanaoielewa lugha ya Kiebrania ambayo ilitumika kuandika Agano la Kale, wanatusimulia kuwa neno ‘Mungu’ kwa kiebrania ni ‘Elohim’ katika mstari huo wa kwanza kwenye Biblia, na neno hilo ni neno la uwingi pale – linawakilisha wengi, siyo mmoja. Hadi kufikia hapa, sifanyi jambo jingine lolote isipokuwa ni kutufanya tuelewe hayo, ila pamoja na haya, katika sura hii ya kwanza ya Biblia tunasoma haya:

“Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale…Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.” (Mwanzo 1:26-27).

Hapa tena twaona uwingi unatumika anaposema “na tumfanye …”. Je, hapo Mungu anaongea na Malaika? Jambo hilo haliwezi kuwa hivyo! Mungu alimwuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe – wala sio kwa mfano wa malaika. Twajua kuwa Yesu Kristo anashiriki utukufu wa Mungu Baba kabla ya ulimwenhu hauja kuwepo (Yoh.17:3.) Zaidi ya hayo, kama tutakavyoona, neno la Mungu linatufundisha kuwa Mungu aliumba vitu vyote kupitia Yesu Kristo (Efeso 3:9; Wakolosai 1:16; Yohana 1:3; Ebr. 1:2). Kwa mawazo haya na aya hizi, ninataka kukufanya ufahamu uhusiano unaowezekana kati ya maandiko haya na ukweli unaofunuliwa., kwa hivyo tunapolinganisha haya na lugha ya Mwanzo sura ya kwanza, tunaweza kuona uhusiano uliopo kwa urahisi, inaposema, “Na tufanye…”. Hapo mwanzo, Baba na Mwana waliumba mbingu na nchi na mwanadamu juu ya dunia kupitia utendaji wa Roho Mtakatifu.

Tunaendelea na nukuu zetu toka Yohana sura ya kwanza.

“Hapo mwanzo kulikuwako Neno …”. (Yohana 1:1).

Katika Ufunuo19 inazungumza juu ya mtu anayeketi juu ya farasi mweupe (kutoka mstari wa 11 hadi mstari wa 16), na kutoka kwa maelezo tunaelewa kuwa humwelezea Yesu Mwana wa Mungu, kwa sababu hutumia lugha hiyo hiyo kumwelezea Yesu katika sura ya kwanza – “Macho yake yalikuwa kama moto wa moto…Na katika kinywa chake hutoka upanga mkali.” Anaitwa pia Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana, na katika aya ya 13 Yesu Kristo anaitwa ‘neno la Mungu’. Tusiwe na shaka – Yesu ndiye ‘neno la Mungu’, na yeye ndiye ‘neno’ lile katika Yohana 1:1. Kabla ya kitu kingine chochote kuumbwa, Neno lilikuwepo, Yesu Mwana wa Mungu alikuwepo. ‘Hapo mwanzo kulikuwa na Neno…’. Wakolosai 1:16,17 inathibitisha ukweli huu mzuri kwa kutuambia Kristo Yesu “yuko kabla ya vitu vyote”; alikuwepo kabla ya kitu chochote kuumbwa.

Kama tulivyoona, huu ni ufunuo wa maandiko. Injili ya Yohana inaturudisha nyuma kabisa katika mwanzo na kutueleza kuwa Yesu Kristo alikuwepo hapo mwanzo. Hakuna uthibitisho wa mwanzo zaidi ya huu unaotajwa au kufunuliwa na Biblia. Ni nani sasa anadhani anaweza kutengeneza mafundisho ya kile anachodhani kilitokea kabla ya ‘hapo mwanzo’? Ni njia ya kuleta machafuko na makosa kuanzisha mafundisho yasiyotokana na ufunuo wa maandiko. “Hapo mwanzo kulikuwako neno…” Huu ni uwazi na udhahiri wa neno la Mungu.

“na Neno alikuwa kwa Mungu.”

Kama tumeshaona, ukweli huu unathibitishwa wazi kwa maneno ya Yesu wakati wa kuomba kwa Baba katika sura ya 17,

“Na sasa, Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako.” (Yohana :17:5).

Huu ndio ukweli huo huo ambao tumetazingatia hapo juu. Hapo mwanzo, kabla ya ulimwengu kuwako, Mwana alikuwa na Baba na alishiriki utukufu wake. Ukweli huu, na ukaribu wa uhusiano huu unafunuliwa zaidi katika Yohana 17:24, ambapo Yesu anasema katika sala yake kwa Baba, “kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa kwa msingi ya ulimwengu.” Baba alimpenda Mwana, Yesu Kristo, kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu, na anampenda sasa! (Mstari wa 26). Mtu yeyote anawezaje kudai kwamba Yesu, Mwana wa Mungu, hakuwapo hapo mwanzo na Mungu Baba? Mungu alimpenda Mwana wake Yesu Kristo hata kabla ya ulimwengu kuwako ! Huu ni ufunuo wa neno la Mungu kwetu.

Yesu Kristo, Mwana wa pekee wa Mungu, ambaye alikuwa kifuani mwa Baba, na ambaye alishiriki utukufu na Baba kabla ya ulimwengu, alikuja na kutuonyesha utukufu wake (Yohana 1:18; 17:5). Na kwa hivyo katika aya ya 14 ya Yohana 1 tunaambiwa kwamba ‘neno’, Yesu Kristo, alifanywa mwili na akaishi kati yetu. Maandishi haya yote yanafaaje kwa kushangaza, kutangaza ukweli sawa!

Wale ambao wanadai kuwa Yesu Kristo hakuwapo na Baba huyo tangu mwanzo wanajiweka kati ya wale wanaokataa na kumdhalilisha Baba na Mwana;

“Ili kwamba watu wote wamheshimu Mwana, kama vile wanavyomheshimu Baba. Yeye asiyemheshimu Mwana hawezi mtukuza Baba aliyemtuma … Yeyote anayemkataa Mwana, kadhalika amemkataa Baba; lakini yeye anayekiri Mwana anamkiri Baba pia. “ (Yohana 5:23; 1 Yohana 2: 23).

Kulingana na maneno haya, wale wanaomkataa Mwana, hawana Baba, wala Mwana. Kukataa kwamba Mwana alikuwa na Baba tangu mwanzo ni kupinga ukweli uliofunuliwa kwa neno la Mungu mwenyewe.

Tunaendelea na nukuu zetu toka Yohana sura ya kwanza.

“…na Neno alikuwa Mungu.”

Tumekwisha kuona aya nyingi zinazothibitisha ukweli huu kuhusu Yesu Kristo, basi haishangazi sasa kwamba tunakutana na ukweli huu katika aya hii, ikieleza wazi kwa ajili yetu.

Hapo haisemwi kuwa, ‘Neno alifanywa kuwa Mungu’; haisemwi kuwa ‘neno lilifanyika Mungu’; wala haisemwi kuwa ‘neno alikuwa usemi wa Mungu.’ Bali inasema kuwa, “Neno alikuwa Mungu.” Kama tulivyoona kuwa Neno ni Yesu Kristo kama vile ilivyoelezewa kwa uwazi katika ule mstari wa 14,

“Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”

Katika waraka wa kwanza wake, Yohana anafafanua mambo yanayofanana na kweli hii,

“Lile lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu ikalipapasa, kwa habari ya Neno la uzima; (na uzima huo ulidhihirika, nasi tumeona, tena twashuhudia, na kuwahubiri ninyi ule uzima wa milele, uliokuwa kwa Baba, ukadhihirika kwetu); hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo.” (1 Yoh. 1:1-3).

Katika mistari hiyo hapo juu Yohana anazungumzia kumhusu Yesu Kristo ambaye wanafunzi wake wamemwona, wamemsikia, na kumgusa. Yohana anamwita Yesu “Neno la uzima”, akisema kuwa uzima ambao ulidhihirishwa kwao ulikuwa ni huo uzima wa milele ambao ulikuwepo pamoja na Baba pale mwanzo. Kwa maneno mengine ni kwamba ule uzima wa milele ambao ulikuwa kwa Baba na Mwana pale mwanzo, sasa umedhihirishwa kwetu kwa kuja wake Yesu Kristo hapa duniani. Yesu Kristo ni udhihirisho na ufunuo wa uzima wa milele. Uzima wa milele ni nini, isipokuwa tabia na asili ya Mungu Mwenyewe. Kimsingi, Uzima wa milele hauhusu ‘muda’ bila mwisho, bali unahusu ile tabia na uzima wa Mungu Mwenyewe, na ndiyo uzima huo ambao ni uzima wa milele.

Yesu Kristo alikuja duniani na alituonyesha kikamilifu sifa zote na vipengele vyote vya tabia ya Mungu kwa sababu ule uzima wa milele ulikuwa ndani Yake.

Na ambaye ni nani tunaye shirikiana naye? Ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana! Sio pamoja na Baba tu, ila pamoja na Baba na Mwana. Na katika ile sura ya mwisho ya 1 Yohana tunaelezwa kuwa uzima wa milele umo ndani ya Yesu Kristo. Ni nani mwenye uzima wa milele isipokuwa Mungu? Na ni wale tu waliye naye Mwana wanao huo uzima (wa milele ).

“Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima.” (1 Yoh. 5:11,12).

Kutokana na mistari hiyo katika waraka wa Yohana, tunafunzwa kwamba Yesu Kristo ndiye uzima wa milele! Na kwa uhakika, katika Yohana 17:3, uzima wa milele umeelezewa kwa ufafanuzi huu:

“Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.”

Uzima wa milele ni kumjua Baba na Mwana. Hakuna malaika wala kiumbe cha juu anaweza kukupatia wewe uzima wa milele. Unaweza tu kupata uzima wa milele kwa kuupata uzima uliomo katika Baba na katika Mwana.

Lile ‘neno’ siyo neno fulani fulani lililonenwa na Mungu. Lile neno ni Mwana wa Mungu Yesu Kristo amabaye alikuwepo pamoja na Baba hapo mwanzo na akafanyika kuwa mwanadamu, kama tulivyona kwa uwazi!

Katika yote neno la Mungu linafunua kuwa Mungu ametupa uzima wa milele, na kwamba huo uzima wa milele unakuja kwetu kupitia Kristo Yesu, na huo uzima wa milele uko ndani ya Kristo Yesu! Ni nani aliye na uzima milele kama siyo Mungu?

Tunaendelea na nukuu zetu toka Yohana sura ya kwanza.

“Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.”

Je, tafsiri ya mstari huu kutoka Kigiriki ni mzuri? Ndiyo, ni tafsiri nzuri. Watu wengine wamejaribu kuugeuza ili uonyeshe maana nyingine kabisa, wakidai wanajua sarufi ya Kiyunani, lakini tafsiri hii ni tafsiri sahihi na tafsiri ya kawaida tu ya Kiyunani. Kwa sababu ya sarufi ya Kigiriki, mpangilio wa maneno yake umetofautiana, inasema, “na Mungu alikuwa neno” (και θεος ην ο λογος). Lakini kwa sababu ya muktadha na maumbo ya sentesi yake yote, basi tafsiri tuliyonayo inaelezea maana yake vizuri sana. (Sasa, kama unayo Digrii ya chuo kikuu, hiyo haimaanishi unachosema ni kweli kila mara, lakini ili ujue sisemi mambo hayo kutokana na ujinga wa lugha ya Kiyunani, naweza kukujulisha nilijifunza lugha ya Kiyunani ya Agano Jipya kwenye chuo kikuu kwa miaka minne.)

“Neno alikuwa Mungu…..na Neno akafanyika kuwa mwili.” Kweli hii inakaa vizuri sana na kwa usahihi kutokana na yale ambayo mtume Paulo ameyasema,

“Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu. Mungu alidhihirishwa katika mwili, Akajulika kuwa na haki katika roho, Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa juu katika utukufu.” (1 Timotheo 3:16).

“Mungu alidhihirishwa katika mwili…” Hii Paulo anaiita “siri ya utauwa” na anatangaza kuwa ni ‘siri kuu’. Aya yote inaonyesha kuwa anazungumza kuhusu Yesu Kristo.

Maandiko mengi sana ya Kiyunani ya Agano Jipya yanayo maneno hayo, na zinaukubaliana na misitari yote ya Biblia tuliyoiangalia katika somo hili.

Zipo miswada michache sana ambazo kwa sehemu kidogo zinatofautiana andiko hilo, na miswada ambazo watu huvutana nazo zinaitwa Codex Alexandrinus. Muswada huo husema kwamba, “Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu, ambaye alidhihirishwa katika mwili….”. Basi, hivyo neno “Mungu” limebadilishwa lisomeke “ambaye”. Katika kisarufi neno ‘Mungu’ ni jina (noun), na neno ‘ambaye’ ni ‘kiwakilishi cha kihusiano’ (‘relative pronoun’), na neno hilo ‘ambaye’ linahusu mtu ambaye alitajwa kabla ya hapo (yaani, kabla ya neno ‘ambaye’). Lakini wataalamu wengi hawakubalani juu ya usahihi wa andiko hilo (yaani, Codex Alexandrinus).Tatizo moja la mfumo wa maneno haya ni kwamba neno “ambaye” halina jina (noun) la wazi ambayo unaweza kuliunganisha nalo. Pasipo kutoa somo kwa Kigiriki, hebu kwanza nielezee tatizo la kutumia lugha ya Kiswahili. Ikiwa tutaweka neno ‘ambaye’ badala ya kuandika ‘Mungu’ katika sehemu hiyo, basi ndipo tutapata lugha ifuaatayo, “…siri ya utauwa ni mkuu ambaye alidhihirishwa katika mwili…”

Je, sasa unaliona tatizo hapa? Ni lazima iwepo jina fulani (noun au subject) kwa neno ‘ambaye’ – lakini hii haiwezi kuwa neno ‘siri’ kwa sababu ikiwa ‘siri’ ni neno (subject) linalohusu neno ‘ambaye’ ndipo sasa Kiswahili chake kinapaswa kiwe kama ifuatavyo – “siri ya utawa ni kuu, ambayo ilidhihirishwa katika mwili”. Ni kosa la ki-lugha kama ukisema au kuandika yafuatayo, “Siri ya utauwa ni mkuu ambaye alidhihirisha…”. Kutokana na sheria ya lugha tunapaswa kusema, “Siri ya utauwa ni mkuu ambayo ilidhihirisha…”.  Hii sasa ni tatizo sawasawa kama ilivyo katika Kigiriki ikiwa tutabadilisha neno “Mungu” na kuweka “ambaye”. Hakuna neno (noun) ya wazi kwa ajili ya neno “ambaye”. Lakini kama tunafuata andiko la maandishi wengi sana (karibu yote) tunaona tatizo la lugha hamna  – “…siri ya utauwa ni kuu. Mungu alidhihirishwa katika mwili…”.

Hivyo tunachoweza kusema ni hiki, maandishi (manuscripts) mengi sana yana neno ‘Mungu’ na siyo ‘ambaye’, hivyo kuleta maana ya ile sentesi ieleweke kwa uwazi kabisa – katika mstari huo hakuna tatizo la kisarufi wala michanganyiko ya maana zake. Hatimaye andiko hilo linakubaliana na kweli inayopatikana katika mistari mingine ambayo tunaiangalia katika somo hili (Yohana 10:30; 14:9; 2Wakor. 5:19).

‘Mzaliwa pekee Mungu aliye katika kifua cha Baba.’

Labda sasa ni nafasi nzuri kutaja jambo moja linalohusu mada hiyo juu ya Uungu wa Yesu Kristo. Wapo watu wanaopendelea miswada ya Kigiriki (Greek manuscripts) ya Agano Jipya ya zamani sana, miswada ambayo iliandikwa mapema kuliko miswada mingine iliyofuata baadaye. Watu hawa wanapenda kutegemea na kunukuu hasa miswada ya Kigiriki itwayo ‘Codex Vaticanus’ na ‘Codex Sinaiticus’ kwa sababu hayo ni zamani kuliko miswada mingine. Wanakosa kufikiri au kudai kwamba lazima maandiko ya miswada hiyo ni sahihi kila mara kuliko miswada mingine. Hii miswada miwili iliingia katika uwanja wa umma katika karne ya 19, na imeleta ushawishi mkubwa wa tafsiri ya Agano Jipya. Kwa vyovyote iwavyo, tunapoangalia maandishi ya miswada hiyo kuhusu Yohana 1:18 tunakuta walichosema ni hiki:

“Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mzaliwa pekee Mungu aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua.” Kwa Kiingereza inatafsiriwa ‘the only begotten God who is in the bosom of the father’.

Kumbe, maandishi hayo mawili ya zamani sana yanasema kwamba ‘mzaliwa pekee Mungu’ (au ‘Mungu mzaliwa pekee’) yupo katika kifua cha Baba! Yaani, sawasawa na andiko la maandishi hayo, Yesu ni mzaliwa pekee Mungu ambaye ni katika kifua cha Baba.

Biblia ya Kiingereza ambayo inafuata Kigiriki (Kiyunani) ya maandishi karibu yote inasema, “…Mzaliwa pekee Mwana…” (the only begotten Son).

Ni jambo la kigeni kwamba tafsiri ya Kiswahili SUV haifuati andiko la maandishi la Kigiriki yoyote –  wafasiri walichagua kuzingatia na kuchanganya maneno hayo kwa kuandika, “Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba…”. Hata hivyo, andiko hilo la SUV inatoa maana lilelile ya kwamba ‘Mwana ni Mungu mzaliwa pekee’. Sasa wao wapendeleao maandishi ya Kigiriki hayo mawili watambue na kupokea yanachodai – Yesu ni Mungu!

WAKOLOSAI 1

Hebu tuangalie tena Wakolosai 1 ambapo tunasoma aya hizi za kushangaza, ambazo zinafunua kweli zifuatazo za utukufu juu ya Yesu Kristo:

“…naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye. Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote.” (Wakolosai 1:15-18).

Katika kifungu hiki tunaambiwa tena kwamba Yesu, ambaye ni mfano (au taswira) wa Mungu asiyeonekana, alikuwa kabla ya vitu vyote. Zaidi ya hii, tunasoma kwamba vitu vyote, vinavyoonekana au visivyoonekana, viliumbwa na yeye. Sio hivyo tu, lakini kwa kuwa viliumbwa kupitia yeye, vitu vyote hushikana katika yeye pia, ambayo ni Kristo Yesu!

Ikiwa kila kitu kiliumbwa na yeye, basi hakika alikuwepo kabla ya vitu vyote. Ukweli huu ambao Mungu aliumba vitu vyote kupitia Mwana wake Yesu Kristo unashuhudiwa katika maandiko mengine – 1 Wakor. 8: 6; Waefeso 3:9; Waebrania 1: 2. Huu ndio ukweli tunaupata katika sura ya kwanza ya Yohana, ambapo inasema juu ya ‘Neno’ ambayo ni Yesu, “Huyo hapo mwanzo alikuwa na Mungu. Vitu vyote viliumbwa na yeye; bila yeye hakukuwa na kitu chochote kilichotengenezwa… Alikuwa katika ulimwengu na ulimwengu ulitengenezwa na yeye, na ulimwengu haukumjua.” (Yohana 1:10; 1:3). Tunaweza kuona wazi jinsi mafungu haya yote yanavyokubaliana na kuongea, na thibitisha ukweli huo, kwamba Mwana wa Mungu alikuwa na Baba hapo mwanzo, na kwamba kupitia yeye vitu vyote viliumbwa. Na aya chache baadaye (v.14) tunaambiwa kwamba, “Naye neno alifanyika mwili, akaketi kati yetu, (na tukaona utukufu wake, utukufu kama wa mzaliwa wa pekee wa Baba)”. Mstari huu wa mwisho unaongelea ukweli kwamba Yesu, Mwana wa Mungu, ambaye alikuwa na Baba tangu mwanzo, alizaliwa kuwa Mwana wa Adamu.

Hebu ieleweke vizuri kutoka kwa aya hizi zote – kwa kuwa si ngumu kuelewa – kwamba Yesu Kristo ‘hakuumbwa’ na Mungu. Yeye hakuwa malaika ‘mkuu’ fulani ambaye alipewa nguvu maalum na mahali maalum; Yesu hakutokana na kisichokuwepo wala hakutamkwa awepo kutoka hewani kupitia neno ‘fulani’ la Mungu.

Yesu Kristo hakuwa mwana wa mungu ‘fulani wa hali ya juu’ kama dini za uongo zinavyodai; wala hakuwa mwana wa mungu maalum kati ya wana wa Mungu wengine (kwa mfano, kama wale wana wa Mungu tunaosoma katika Mwanzo 6:2). Maandiko ni ya ajabu na yana makusudi ya wazi katika jambo hili – Yesu Kristo ni Mwana pekee wa Baba. Hakuna mwingine kama yeye, hakuna mwingine aabudiwaye pamoja na Baba mbinguni na duniani isipokuwa Kristo!

Tafsiri ya Kigiriki ya Yohana 1:1 iko wazi na ni sahihi ambayo inasema ‘na neno lilikuwa Mungu’, sio ‘na neno alikuwa mungu (ya aina fulani miongoni wa miungu mingine kama vile dini zingine za uwongo zinavyodai). Neno, ‘aliumba’ halitumiwi na maandiko yanayohusiana na Mwana. Mungu aliumba vitu vyote kupitia Mwanawe. Mwana mwenyewe alihusika katika kuunda vitu vyote – hakuwa kiumbe aliyeumbwa. Wazo hili halipatikani katika Bibilia.

KRISTO NA BIBI HARUSI WAKE.

Tunataka tuiangalie tena hiyo sura ya hapo juu kwenye Wakolosai kwa sababu inaelezea kwa undani zaidi. Pale kwenye ule mstari wa 16 tunasoma kuwa, “vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake.” Mambo yote ambayo yaliumbwa, mambo yote tunayoyaona, yanayotuzunguka, na hata yale tusiyoyaona, hayo yote yaliumbwa kwa ajili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu! (Hapo tunaangalia kweli zinamhusu Mwana wa Mungu, lakini ni vivyo hivyo juu ya Mungu Baba: Warumi 11:36; 1 Wakor. 8:6; Waebr. 2:10; Ufunuo 4:11.)

Hebu basi tuyaangalie tena maandiko ili kujua ni kwa namna gani ya kuwa vitu vyote viliumbwa kwa ajili yake Yesu Kristo – na kwa kufanya hivyo tutagundua kweli nyingine ya ajabu. Mtume Paulo anawaambia Wakorintho, “Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi.” (2 Wakor 11:2). Hapo Kristo anaelezwa kuwa kama mume ambaye kwa Yeye Kanisa litawakilishwa kuwa ni bibi harusi safi, kama jinsi ilivyofunuliwa katika kweli hii imetangazwa kwenye maandiko mengineyo mengi kama vile kwenye Mathayo 9:15; 22:2; 25:5; Yoh. 3:29 na kwenye Warumi 7:4. Kanisa limeelezwa kwa njia nyingi tofauti ili kuonyesha kweli mbalimbali. Kwa mfano kanisa linawakilisha mwili wa Kristo, pia kanisa ni makazi ya kudumu ya Mungu Baba, na ni Bibi harusi wa Kristo Yesu.

Tunaupata ukweli huu katika kufungua sura za Biblia. Kile ambacho Mungu alikusudia kufanya kupitia kifo na kufufuka kwa Mwanae pale Kalvari, alitangulia kukionyesha katika uumbaji wa Adamu na Hawa.

Kama vile ilivyokuwa kwa Hawa aliumbwa wakati Adam akiwa katika usingizi mzito, ndivyo ilivyokuwa kwa kanisa pia, ambalo limeundwa kutokana na kifo na ufufuo wa Bwana wetu Yesu Kristo. Zile ambazo zinaeleza Mungu atakachofanya kupitia kifo wa mwanae pale Kalvari, aliutambulisha kwanza kwa uumbaji wa Adamu na Eva.

Kati ya vyote ambavyo Mungu aliviumba, hakuona wa kuendana na Adamu awe msaidizi. Kwa hiyo Mungu akamweka Adamu katika usingizi mzito, na wakati Adamu akiwa katika usingizi mzito Mungu aliutwaa ubavu wake na katika ubavu huu akamwumba Eva ambaye angekuwa mkewe. Adamu alipomwona Eva akasema, “huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume.” Maneno haya yanatuonyesha kwamba mwanamke aliumbwa akitoka katika mwanaume. Kupitia uumbaji wa Mungu wa Adamu na Eva tunauakisi timilifu kabisa wa mpango wa Mungu kutoa Bibi harusi kwa ajili ya Mwanawe, Yesu Kristo. Biblia inastaajabisha sana! Biblia ni neno la Mungu, ni uvuvio wa Roho Mtakatifu.  

Askari walipokuja kuutoa mwili wa Kristo pale msalabani, walikuta ameshakwisha kufa tayari lakini ili kuhakikisha wakamchoma mkuki ubavuni kwake na tazama, maji na damu vikamtoka. Damu na maji ndio viashirio vya ukombozi  na utakaso wa kanisa la Kristo, kama maandiko yanavyotufundisha,

‘Huyu ndiye aliyekuja kwa maji na damu, Yesu Kristo; si katika maji tu, bali katika maji na katika damu. (1Yohana 5:6).

‘Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno.’ (Waefeso 5:25,26).

‘…mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.’ (Matendo 20:28).

“Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.” (Yoh.3:5).

Kama Hawa alivyoumbwa kutoka kwa Adamu akiwa usingizini, ndiyo kanisa lingeundwa toka kwa Kristo kwa kufa msalabani.

Tumekwisha kujifunza kwamba haukuwepo msaada wowote wenye kufaa uliopatikana kwa ajili ya Adamu toka kwa wanyama. Na hii haishangazi! Unaweza tu kupata ushirika wa ukaribu na wenye maana na mtu fulani ambaye analingana na aina yako wewe mwenyewesawasawa na asili yako! Hivyo Mungu alimuumba Hawa kutokana na ubavu wa Adamu kwa matokeo kuwa wote waliumbwa kwa mfano wake Mungu. Na hivyo Adam akawa na uwezo wa kusema, sasa ‘huu ni mfupa wa mifupa yangu, na nyama ya nyama yangu’. Kwa sababu ya kile ambacho Kristo alikitimiza pale msalabani watu wote, wanaume kwa wanawake, wanaomwamini Yesu Kristo wanapewa uwezo wakufanyika kuwa wana wa Mungu – wamezaliwa na Mungu, kutokana na tabia yake ili waweze kuwa na ushirika wa ukaribu sana na Baba na Mwana. (Yohana 1:12,13; 1 Yohana 3:9; 4:4; 2 Petro 1:3,4).

Ni kutokana na jambo hilo basi waliomwamini Yesu wote huitwa ni ndugu zake Kristo Yesu, kwa sababu watu hao sasa wamezaliwa upya kutokana na Mungu. Katika mahusiano yao pamoja na Yesu Kristo, waumini pia wanaitwa ‘mwili’ wake, na ‘kanisa’ lake na ‘bibi harusi’ wake, kama vile tulivyokwishakuona kwenye makala hii. Undani wa mahusiano hayo umeletwa kwetu kupitia mistari ifuatayo.(Yoh.14:20,23; 17:21-23; Warumi 8:29).

Tungenukuu mistari mingine lakini nadhani ukweli uko wazi. Kama Eva aliumbwa kutoka katika ubavu wa Adamu, vile vile Bibi harusi wa Kristo ataumbwa kutoka katika vile vilivyotoka ubavuni mwake. Neno la Mungu linaunganisha habari hizi za Adamu na Kristo vizuri sana kwa sababu kutoka katika hiyo hiyo sura 5 ya Waefeso Paulo ananukuu maneno ya  Adamu kuhusu Eva anayotumia kwa Kristo na kanisa lake: “Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake, vya nyama yake na vya mifupa yake.” (Mstari wa 30. Miswada ya zamani ya Agano Jipya karibu yote zinazingatia maneno hayo, “vya nyama yake na vya mifupa yake.”). Zaidi Paulo anaendelea kunukuu kauli nyingine kwenye kitabu cha Mwanzo iliyofuatia baada ya kuumbwa kwa Eva – na tena anailinganisha na Kristo na kanisa katika njia yenye kushangaza mno – ananukuu, “Kwa sababu hii mwanaume atamwacha babaye na mamaye na ataambatana na mkewe, nao si wawili tena bali ni mwili mmoja.” Lakini tena Paulo anaongezea siri kuu, “lakini nazungumza kwa habari ya Kristo na kanisa.” Kumbe!

Mpango thabiti na wa milele wa Mungu wa kumtengeneze Mwanae Bibi harusi umewekwa wazi kwenye maandiko hayo. Tunaupata ukweli huu kwenye Agano Jipya. Paulo anasema hivi, “Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi. Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo.” (2 Wakorintho 11:2-3). Hapa pia tunapata picha nyingine ya Bibi harusi kuandaliwa kwa ajili ya Bibi harusi wake – mumewe. Hapo mwanzo Neno la Mungu lilikuwa pamoja na Mungu, na Mungu mwenyewe alipanga kumpatia Mwana wake bibi harusi tangu hata kabla ya misingi ya ulimwengu!

Biblia inamalizia na harusi ya Mwanakondoo kama tukio kubwa la mwisho litakalofanyika. Ni tukio lililotengenezwa na Mungu tangu mwanzo kabla hata ya misingi ya ulimwengu huu. Kwa maneno mengine, uumbaji wa ulimwengu uliweka jambo hili kuwa ni kusudi mojawapo kubwa kumpatia bibi harusi kwa ajili ya Mwanakondoo wa Mungu. Bibi harusi huyo ambaye ni Jerusalem mpya itakuwa pia ni makao ya Baba na Mwana.

Tunasoma juu ya utimilifu wa mpango wa Mungu kwa ajili ya mwanawe kwenye mistari ifuatayo:

“Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari. Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing’arayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni matendo ya haki ya watakatifu. Naye akaniambia, Andika, Heri walioalikwa karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo. Akaniambia, Maneno haya ni maneno ya kweli ya Mungu.” (Ufunuo 19:7–9).

Tunafahamu kwamba kanisa ni mahali pa Mungu kukaa na kutulia katika Roho, na Kristo amewapa watu wake utukufu wake (Waefeso 2:21,22; 2 Wakor.3:18). Na katika Ufunuo 21 tunaona kanisa limeelezewa kama ni Bibi harusi aliyepambwa kwa ajili ya mumewe na vile vile kama mji mpya wa Yerusalemu ambapo Bwana Mungu mkuu na mwanakondoo wanaishi. Hapo mwanzo Baba na Mwana walishiriki utukufu kwa pamoja. Sasa, tunaona ‘mwishoni’ kwamba Bibi harusi anashiriki utukufu huo.

“Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe…akanionyesha ule mji mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu; wenye utukufu wa Mungu… Nami sikuona hekalu ndani yake; kwa maana Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo, ndio hekalu lake. Na mji ule hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni Mwana-Kondoo.” (Ufunuo 21:2,10,11, 22, 23).

Biblia inahitimisha na ndoa ya Mwana-Kondoo kama tukio kubwa la mwisho – tukio alilolipanga Mungu kabla ya kuweka misingi ya dunia. Kwa maneno mengine, moja katika madhumuni makuu ya kuumbwa kwa ulimwengu yalikuwa  kupata Bibi harusi wa Mwanakondoo wa Mungu, Yesu Kristo. Bibi harusi huyu, Yerusalemu Mpya, alikuwa kwenye makao ya Baba na Mwana. Haishangazi yanavyosema maandiko kuwa ‘hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao’! (Waebr.13:14).

MWANA-KONDOO, ALIYECHINJWA TANGU KUWEKWA MISINGI YA DUNIA.

Lakini ili kumtengeneze Mwanawe Bibi harusi, Mungu angefanya nini? Kwa sababu ya dhambi, kama tulivyoona, huna budi kutoa Mwana wake kama dhabihu kwa dhambi (Isaya 53:10).

Yapo maelezo ndani ya Biblia ambayo yanatufunulia kwa ajabu sana kwamba Baba na Mwana tangu mwanzo walitengenza njia ili watu waweze kufanyika kuwa ni wana wa Mungu, na kuwa watu wa aina hii watakuwa kanisa lake nalo lifanyike kuwa ni makazi yake Mungu. Mtume Petro anasema hivi kuhusu Yesu, Mwanakondoo, “Naye amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa mwisho wa zamani kwa ajili yenu.” (1 Petro 1:20). Na mtume Yohana naye anaenda hatua moja mbele za zaidi kwenye kitabu kile cha Ufunuo 13:8, “Na watu wote wakaao juu ya nchi watamsujudu, kila ambaye jina lake halikuandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo, aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia.”

Kwenye mistari hii, neno la Mungu linatufunulia kuwa Baba na Mwana tangu mwanzo walifanya toleo katika nia yao kwa ajili yetu ili tupate kufanyika kuwa wana wa Mungu – na tukiwa tumefanyika kuwa wana wa Mungu, Bwana wetu Yesu haoni aibu kutuita sisi ndugu zake! (Waebr. 2:11). Kabla hata misingi ya ulimwengu haijafanyika, Baba yetu tayari alikwisha kujiandaa kumtoa Mwanae kwa ajili ya ukombozi na wokovu wetu; naye Mwana alikuwa tayari amekwisha kujiandaa kujitoa yeye mwenyewe kwa ajili ya kusudio hili. Nia hii ya kujiweka kafara mwenyewe ilikuwepo pale tayari katika mapenzi na tabia ya ki-Ungu tangu mwanzoni. Ibrahimu alitabiri kusudi la Mungu alipomwambia mwanawe, “Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, mwanangu.” (Mwanzo 22:8). Hii haikuwa ni kielekezo tu cha Mungu wetu cha kumtoa mbadala wa Isaka, bali zaidi sana ni umuhimu na msingi wa lazima hiyo ndiyo ilikuwa ni kielelezo cha Yesu Kristo mwenyewe ambaye aliteuliwa na Mungu kama Mwanakondoo aliyechinjwa tokea misingi ya ulimwengu huu ili kuleta uzima wa milele kwa watu wote! Ni kwake huyo mwanakondoo aliyechinjwa na kwake Mungu mbingu zote na dunia inatoa ufukufu na heshima kwenye ile sura ya 5 ya Ufunuo. Neno la Mungu linatudhihirisha kwamba ‘alituchagua katika yeye (Kristo Yesu) kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu.’ (Waefeso1:4).

Kwa nini alichinjwa? Ni kwa sababu kulikuwa hakuna njia nyingine ya kuwaleta wana wengi waufikilie utukufu – “Kwa kuwa ilimpasa yeye, ambaye kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana wengi waufikilie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso.” (Waebr. 2:10). Neno likafanyika mwili. Agano Jipya lote linashuhudia vizuri jambo hili, ya kwamba ilimpasa Yesu Kristo awe mwanadamu ili kwamba apate kutuokoa kutokana na madoa pamoja na na nguvu za dhambi, na nguvu ya shetani na ya giza. (Wafilipi 2:5 -11; Waebr 2:5 -18; 1Yoh. 3:5 – 9). Aliweza tu kufanya haya yote kupitia kifo chake pale msalabani. Kulikuwa hakuna njia nyingine ya mbadala ili kutimiza hayo (Luka 22:42). Tafakari juu ya jambo kubwa kama hili – hakuna mwingine yeyote ambaye angezibeba dhambi zetu na kuzishinda nguvu zake na kuziangamiza nguvu zake za shetani, isipokuwa ni Mungu. Hayupo hata malaika aliyeumbwa, hakuna hata malaika wa juu, wala hakuna mwingine yeyote katika jambo hili isipokuwa ni Mungu tu. Damu pekee ipasayo kutakasa na kukuokoa wewe kutokana na dhambi ni ile damu ya Mwanakondoo pekee, aketiye katika kiti cha enzi pamoja na Baba yake, akiabudiwa na wote walioko mbinguni na nchi!

Mungu alikuwa anataka kuwaleta wana kwenye utukufu wake, kuwaleta kwake mwenyewe, ili wawe pamoja naye milele yote. Na hilo ndilo kusudio lake la umilele kupitia Injili ili tuzaliwe na Mungu!

Kweli hiyo yote ambayo tumekuwa tukiifikiria kuhusiana na wokovu wetu tayari ulikwisha kupangwa au kutimizwa katika mapenzi na kusudi la Baba na la Mwana tangu pale mwanzo. Kipo kifungu kizuri sana katika kitabu cha Mithali ambapo inaongelea kuhusu ‘hekima’, lakini hiyo ni wazi kuwa hapo inamwelezea Yesu Kristo, Mwana wa Mungu,

“Bwana alikuwa nami katika mwanzo wa njia yake, Kabla ya matendo yake ya kale. Nalitukuka tokea milele, tangu awali, Kabla haijawako dunia. Wakati visipokuwako vilindi nalizaliwa, Wakati zisipokuwako chemchemi zilizojaa maji. Kabla milima haijawekwa imara, Kabla ya vilima nalizaliwa. Alipokuwa hajaiumba dunia, wala makonde Wala chanzo cha mavumbi ya dunia; Alipozithibitisha mbingu nalikuwako… Alipoiagiza misingi ya nchi; Ndipo nilipokuwa pamoja naye, kama stadi wa kazi; Nikawa furaha yake kila siku; Nikifurahi daima mbele zake.” (Mith.8:22 – 30).

Habari hiyo hapo juu inafupisha maandiko yote tuliyokuwa tukiyatazama. Haijalishi maandiko mengineyo ambayo watu wangelipenda kuyanukuu, tutambue hapa kuwa Yesu Kristo yeye alitukuka tangu umilele – na hii ndiyo matumizi mazuri ya lugha ambayo Mungu anaitumia katika kitabu cha Zaburi.

“Kabla haijazaliwa milima, wala hujaiumba dunia, Na tangu milele hata milele ndiwe Mungu.” (Zaburi 90:2).

Hivyo usijaribu kuamua jambo katika nyakati ambazo neno la Mungu halitupatii sisi hivyo. Usijaribu na wala usiwe mwerevu mwenyewe kuliko neno la Mungu kwa kutumia mantiki za kibinadamu tu! Tafakari hayo! Tangu milele Mwana alikuwa furaha ya Baba yake! Tangu milele Baba alikuwa furaha ya Mwana!

WARUMI 9:5

Tunaupaata ukweli uleule katika kitabu cha Warumi 9:5 ambapo panaongelea juu ya faida ya taifa la kiyahudi na ule ujio wa Kristo duniani katika mwili. Kwa tafsiri ya miswada yote ya Kiyunani tunapata ifuatayo,

“…ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya mwili akiwa aliye juu ya mambo yote, Mungu, mwenye kuhimidiwa milele. Amina.”

Na kwa tafsiri ya Kiingereza ya NKJV tunasoma: “Whose are the fathers, and of whom as concerning the flesh Christ came, who is over all, God blessed for ever. Amen.”)

Na tutambue baada ya neno ‘mwili’ haipo nukta bali neno ‘akiwa’, na neno hilo la ‘akiwa’ inahusu Kristo, kama tunavyoweza kuona kwa uwazi. Maandishi yote ya Kiyunani yanayo andiko hilo, maneno hayo, na inampatia Yesu Kristo heshima za hali ya juu, yaani, yeye ndiye Mungu mwenye kuhudimiwa milele!

Kuna watu wengine ambao nao wamebadilisha uwekaji wa mpangilio wa sentensi na vituo vyake kwenye mistari hiyo kwa kujiwekea tu nukta mahala popote pale hata kuifanya sentensi ionekane kuwa zipo mbili kutokana na sentensi moja, na kutenganisha sehemu ya kwanza ya mstari huu kutoka mwisho waandiko, au kucheza na kisarufi ili kwamba sehemu ya pili inawakilisha sifa kwa Mungu na wala haija unganishwa na Yesu Kristo. Hata hivyo kunakuwa hakuna machangnyiko yoyote ya maana kwenye andiko hilo.Tafsiri iliyopo hapo juu ni tafsiri ya kawaida na maana ya Kiyunani. Hata kama watu wanataka kuvutana kwamba itaweza kumaanisha kitu kingine tofauti, hata hivyo hawataweza kubisha kuwa Kiyunani cha andiko hilo kinataka tafsiri ya tofauti.Tafsiri ile ya kiasili inawakilisha kile ambacho andiko la Kiyunani la mstari huo kwa kawaida inasema.

Maelezeo ya Swahili SUV ya andiko hilo ambayo yenyewe inafuata tafsiri ya kisasa ya mistari hiyo, hutenganisha andiko ndani ya sentesi mbili,

“…ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya mwili. Ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu, mwenye kuhimidiwa milele. Amina.”

Hata hivyo kuivunja sentensi hiyo katika mapande mawili ya sentensi, siyo hali ya kawaida ya kutafsiri kwa Kiyunani.

Hebu tuiangalie tena mistari mingineyo miwili inayopatikana katika Biblia ya Swahili Union Version,

“Nikodemo akamwambia ‘awezaje mtu kuzaliwa akiwa mzee?’” (Yoh. 3:4).

“Na Yesu mwenyewe, alipoanza kufundisha, alikuwa amepata umri wake kama miaka thelathini, akiwa amedhaniwa kuwa ni mwana wa Yusufu, wa Eli.” (Luka 3:23).

Katika mistari hiyo yote miwili, neno la Kiyunani la “akiwa” ni “ων” (on). Katika ule mfano wa kwanza maneno “akiwa mzee” yanaelekeza kuwa ni “mtu”, au yanamhusu neno “mtu” lililotajwa kabla. Katika mfano wa pili, “akiwa amedhaniwa kuwa mwana wa Yusufu”, inamwelezea Yesu mapema katika sentenso hiyo. Waweza kuona kuwa isingekuwa haki kuweka nukta mara tu baada ya neno “kuzaliwa” kwenye ile sentensi ya kwanza na wala isingekuwa haki au kawaida kuweka nukta baada ya neno “thelathini” kwenye ule mfano wa pili kwa sababu kwa kufanya hivyo ingetengeneza sentensi mbili ambazo hazija unganishwa vizuri. Kwaa mfano kama tungefany hivyo, tungepata sentensi zifuatazo, “Nikodemo akamwambia, ‘Awezaje mtu kuzaliwa. Akiwa mzee?” Na tena, “…alikuwa amepata umri wake kama miaka thelathini. Akiwa amedhaniwa kuwa ni mwana wa Yusufu.” Je, unaweza kuona hapo jinsi ambavyo haipo kikawaida na inasababisha machangnyiko tu.

Aidha, je, unatambua ya kuwa katika mifano hiyo mwilii neno ‘akiwa’ linahusu mtu aliyetajwa kabla ya hapo, yaani, ‘akiwa mzee’ yanahusu neno ‘mtu’ aliyetajwa kabla ya hapo (katika mfano wa kwanza), na maneno ‘akiwa amedhaniwa kuwa ni mwana wa Yusufu’ yanamhusu Yesu aliyetajwa kwenye mwanzo wa mstari (kwenye mfano wa pili).

Vivyo hivyo maneno “akiwa yu aliye juu ya mambo yote, Mungu, mwenye kuhimidiwa milele” yanamhusu Kristo aliyetajwa kabla ya maneno hayo!

Mifano yote miwil hapo juu inawakilisha sentesi moja, na ile sehemu ya mwisho baada ya “akiwa” inaelezea neno fulani kabla yake, basi hiyo ipo sawasawa na mistari yetu – haiwi ni kawaida kuweka nukta baada ya neno “mwili” na hivyo kuigawanya sentensi katika mapande mawili, ili ile sentensi ya kwanza imwelezee Yesu Kristo, na ile sentensi ya pili kumwelezea Mungu na sio kwa Yesu. Maneno “aliye juu ya mambo yote, Mungu, mwenye kuhimidiwa milele” yanamhusu Yesu Kristo. Tafsiri hiyo inafuata kanuni za lugha. Wale wanaotaka kupinga Uungu wa Yesu wanavunja kanuni hizo.

Tafsiri nyingi za Kiingereza zinazofuata andiko la Kiyunani katika njia hii ni: King James, New King James, King James 2000, New Int. Version, English Standard Version, American Standard Version, New ASV, NASB, International Standard Version, New English Translation, English Revised Version, Jubilee Bible 2000, Webster Bible Translation, Darby Bible Translation and World English Bible.

Tangu karne ya kumi na tisa, fundisho la Biblia limepitia katika mashambulizi makubwa kutoka kwa ‘wataalamu’, hii ni pamoja na fundisho la Uungu wa Yesu Kristo, kwa hiyo kuna ‘wataalamu’ na ‘wasomi’ ambao hawaongozwi sana na maandiko ya Kiyunani bali huongozwa na imani zao kuwa eti Yesu si Mugu na kwa hiyo watatumia elimu zao kujaribu kila namna linayowezekana kutafutiza mbadala wa maana au tafsiri kwenye maadiko ambayo tumekuwa tukiyaangalia. Na sehemu ya lengo iliyopelekea kuandika masomo haya ni kuwasaidia watu wasitiwe upofu na wale ambao wanadai kuwa wanayo ufahamu wa juu ya ujuzi wa maandiko ya Kigiriki.

Hebu niseme kuhusuu mistari yote ambayo tunaipitia kwamba ni wazi kabisa inamzungumzia Yesu ya kwamba yeye ni Mungu. Kwa kuwa kuna uwezekano kuwa kati ya mistari hiyo mmoja au hata miwili yaweza kutafsiriwa tofauti, na kwa namna ambayo haielezei vizuri ya kwamba Yesu ni Mungu. Hii ni kweli. Lakini katika mistari hiyo tunaweza kusema kuwa maandiko ya Kiyunani hayataki au kuhitaji tafsiri tofauti kutoka kwenye tafsiri ya kawaida au ya kiasili. Tafsiri ya asili ya mistari hii inakubalika, na hata ni tafsiri ya kawaida zaidi ya maandiko ya Kiyunani kuliko tafsiri nyingine. Zaidi ya hayo yote, mistari hiyo yote katika somo hili hukubaliana pamoja na inazungumzia jambo moja ambalo ni kuwa Yesu Kristo ni Mungu. Watu wanapojaribu kusema kwamba mistari yote iliyonukuliwa katika somo hili inapaswa itafsiriwe kitofauti na kwamba eti hakuna mstari wowote unaosema kuwa Yesu Kristo ni Mungu, hapo ndipo ni wazi kuwa watu hao wamekosea kabisa.  Wanaendeshwa na matamanio yao wenyewe kushindwa kuthibitisha kuwa Yesu ni Mungu. Hawaongozwi na maandiko ya Kiyunani au ujuzi wa kielimu, wanatumia ujuzi wao na mitazamo ya kibinadamu kujaribu kuthibitisha kuwa Yesu Kristo si Mungu.

Tuendelee kuangalia aya nyingine zinazokubali na kuthibitisha Uungu wa Kristo.

1 YOHANA 5:20

“Nasi twajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli, nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele.” (1 Yoh. 5:20).

Sentensi ya mwisho hapo inaanza na neno lisemalo, “Huyu ndiye Mungu wa kweli”. Labda sasa nikuulize ndugu msomaji, je, maneno hayo yanamhusu Yesu au Mungu? Uwaweza kubisha tu kwa tafsiri zote mbili – maandiko ya Kiyunani inaruhusu kwa ajili ya yote. Kwa maneno mengine, hakuna chochote katika maana ya maandiko ya Kiyunani inayoweza kuzuia maneno hayo yasimzungumzie Yesu Kristo! Sababu ni ipi hata tukusudie kupendelea kuitafsiri kwamba inamhusu Yesu? Hii ni kwa sababu, kwanza, itakuwa ni yenye maana ya kawaida sana. Sentensi ya kwanza inaishia na maneno yasemayo, “…ndani ya Mwana wake Yesu Kristo”. Na mstari ufuatao unaanzia na maneno, “Huyu ndiye….”. Katika kila lugha maneno “huyu ni” ingehusu mtu wa mwisho aliye tajwa katika sentensi iliyopo nyuma yake, na katika hali hiyo mtu huyo ni Yesu Kristo. Hakuna shida, isipokuwa tayari unaamini Yesu sio Mungu na unakataa kupokea kweli hiyo.

Hali kadhalika inakubaliana na muktadha na maana iliyosalia ya waraka wa Yohana. Tayari tumekwisha kuona kuwa katika ile sura ya kwanza kuwa Yohana anamtangaza Yesu kuwa ndiye “ule uzima wa milele ambaye alikuwa pamoja na Baba naye akadhihirishwa kwetu sisi”. Na tena katika hiyo sura ya tano tunasoma kuwa , “Mungu ametupa uzima wa milele na uzima huo u ndani ya Mwanawe”. Katika Ufunuo 3:7 Yesu anasema, “Haya ndiyo anenaye yeye aliye mtakatifu aliye wa kweli…”. Kwa hiyo hii tafsiri ya 1 Yohana 5:20 inakubaliana au inakaa vizuri na maandiko ya Kiyunani na muktadha wa waraka mzima.

BWANA, MUNGU WETU, BWANA NDIYE MMOJA.

Katika somo hili nimekazia katika mistari inayotangaza au inayoonyesha ya kwamba Yesu ni Mungu. Nimefanya hivyo kwa sababu wapo wale ambao wanakana jambo hili. Hata hivyo kama wewe unaifahamu vizuri Biblia, utaelewa kuwa huu ndio ukweli ambao haujafundishwa kwa utaratibu, kama, kwa mfano, “kuhesabiwa haki kwa imani”. Ukweli huo wa Uungu wa Yesu Kristo unatokeza tena na tena kwenye maandiko kama ukweli ambayo hauwezi kujizuia kutangazwa – ukweli huo unarudia kuang’aa kupita maandiko ya neno la Mungu tena na tena!

Ukweli huu hauelezewi kwa kina, ila umetangazwa tu.

Lakini yatupasa sasa kuiangalia hii kwa muktadha mpana wa maandiko, kwa sababu maandiko hutangaza kwa uwazi tu kuwa kuna Mungu mmoja tu – kwa mfano, Kumbu. 6:4, 1 Wakor.8:6, Efeso 4:6 na 1 Timotheo 2:5

Hebu tukumbuke tunapoangalia katika neno la Mungu kwamba kile tunachokifikiria ni ule ufunuo wa Mungu ndani ya mioyo yetu. Sio Mungu, wala Mwana na wala Roho Mtakatifu, hao si vitu katika maabara za kisayansi ambayo itawekwa chini ya darubini kwa ajili ya kuainisha au kuchunguza na kuchambua kwa akili zetu za kibinadamu. Hiyo sio shughuli yetu ya kuchambua kweli ya Mungu kana kwamba ni kitu kenye bomba la kuchunguzia kwenye maabara! Maandiko yasifanywe kuwa ni kitu ambazo mantiki za kibinadamu zinaweza kucheza nayo! Ninashangazwa kuona kuwa watu wengine wanadiriki kuvutana juu ya mambo kama haya kana kwamba ni mambo yenye mantiki za kibinadamu, na huonyesha kujisahau kuwa tunaongelea kuhusu Mungu wetu na Mwokozi wetu Yesu Kristo, aliyemwaga damu yake ili sisi tupate kumjua Baba yetu na Mwanae. Kama tutapoteza heshima zetu tunapojadiliana juu ya jambo muhimu kama hili, basi tutakuwa sio tu kwamba tumepoteza majadilano hayo bali tutakuwa tunajinyima wenyewe ule uelewa wa kweli ya Mungu.

Neno la Mungu limedhamiria kutulisha sisi na kutupatia uelewa wa kiroho wa ile kweli ya Mungu. Haitupasi kulitumia neno lake kama kifaa cha akili zetu za kibinadamu na mantiki. (1 Wakor. 2:10 -14). Kama tunaweza kuongelea mambo kama haya “kiubaridi” huku tukifikiria kuwa mantiki zetu za kibinadamu zitaishinda siku hiyo, ndipo penginepo tutakuwa hatujafaulu kamwe na hatujaelewa chochote kile kama itupasavyo kuelewa.

Kamwe sijasoma kitabu chochote kuhusu Uungu wa Yesu, kwa sababu somo hili halijawahi kuwa tatizo kwangu. Nitatoa mawazo yangu na uelewa wangu yakiongozwa na maandiko husika. Lakini tafadhali tambua kwamba maelezo yangu yana mipaka kwa sababu hata hayo maandiko hayatupatii maelezo ya moja kwa moja kuhusu somo hili na ninajiepusha kwenda nje ya maandiko yasemavyo!

Na tuanze kwa kusoma katika Kitabu cha Kumbukumbu la Torati 6:4-5:

“Sikia, Ee Israeli; BWANA Mungu wetu, BWANA ndiye mmoja. Nawe mpende BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote”. Na Paulo ameandika haya katika waraka wake kwa Waefeso, “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja, Mungu mmoja naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.” (Waefeso 4:4-6). Maandiko yanasema wazi kwamba kuna Mungu mmoja. Hivyo Yesu Kristo anakuwaje Mungu?

“…nafanya sikuzote yale yampendezayo.”

Kwangu mimi kiini cha ufahamu wa somo hili ni maelezo yaliyotolewa na Yesu mwenyewe yanayopatikana katika Injili ya Yohana– Yohana 4:34, 5:19,30; 6:38; 7:28; 8:28,29; 12:49;14:28.

Aya hizi zinatuambia nini? Zinatuambia kwamba Yesu hakuja ulimwenguni kwa nia yake mwenyewe bali ni Baba ndiye aliyemtuma. Hakuja duniani kufanya mapenzi yake, bali kufanya mapenzi ya Baba yake. Katika mambo yote, Yesu alitenda mambo yaliyompendeza Baba. Kwa hakika hutuambia kwamba chakula chake ni kutenda mapenzi ya Baba yake. Hata maneno aliyosema Yesu na kazi alizofanya ni yale aliyoonyeshwa na Baba aseme na kufanya. Yesu aliyaweka mambo hayo wazi kabisa. Lakini ni muhimu kufahamu kwamba kamwe Yesu hakusita kuyatenda mapenzi ya Baba. Kinyume chake, alifurahi kuyafanya mapenzi ya Baba yake (Zaburi 40:6-8; Waebrania10:5-7).

Mistari hii katika Yohana hapo juu inaleta utayari wa Mwana kukubali na kunyenyekea kwa furaha kwa Baba. Kama Yesu alivyo Mwana kwa Baba, si ajabu kwamba anataka kufanya mambo yale yanayompendeza Baba yake. Hii inasisitiza tu ukweli wa uhusiano wa Baba na Mwana — haifanyi chochote kukanusha Uungu wa Kristo. Labda inafaa kujua kwamba aya zote za Injili ya Yohana hapo juu zinahusu huduma ya Yesu duniani. Lakini pia ni muhimu sana kufahamu kwamba Yesu hakufanya tu mapenzi ya Baba, bali alikuwa mmoja wa mapenzi ya Mungu, alikuwa kielelezo hai cha mapenzi ya Mungu (2 Wakor.5:19). Kama tumeshaona, nia ya Mwana ni moja na nia ya Baba.

“…kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi.”

Tunajua ni Baba aliyemtuma Yesu kuwa mwokozi wa ulimwengu. (1 Yohana 4:14). Na Yesu alitufunulia ukweli ufuatao, “Amin, Amin, nawaambia ninyi, mtumwa si mkuu kuliko bwana wake; wala mtume si mkuu kuliko yeye aliyempeleka.”(Yohana 13:16). Hizi aya mbili zinatupatia muktadha wa kile alichosema Yesu katika Yohana 14:28: “Mlisikia kwamba mimi naliwaambia, naenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi, kwa sababu naenda kwa Baba; kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi”. Ni katika muktadha huu wa kutumwa ulimwenguni na baadaye kurudi kwa Baba, ndipo Yesu anaposema, “Baba yangu ni mkuu kuliko mimi” – ingawa mistari kadhaa ambayo tutaangalia hivi karibuni inaweza kutoa muktadha mpana kuhusu hili.

Nafikiri ugumu moja wa kuzungumzia somo hili unapatikana hapa kwa sababu maandiko hayatupatii maelezo ya kina ya kauli hii na ukweli wake – kama tulivyoona kwamba, “bila shaka siri ya utauwa ni kuu. Mungu alidhihirishwa katika mwili.” Kwa hiyo tunaweza kushawishika na kufanya hitimisho kwa hoja zetu wenyewe kuhusu asili ya Kristo. Kwa kufanya hivi watu wengi wameishia kutoa hitimisho lisilokubaliana na maandiko, kwa kutumia lugha na misamiati ya kigeni katika Biblia. Nataka kuzuia jambo hili.

“…na kichwa cha Kristo ni Mungu…”

Lakini tunaweza kuendelea. Ukweli wa Yesu kujinyenyekeza kwa Baba unaonekana ukiangaza katika maandiko mengine pia. Kwa mfano, tunasoma kwamba,

“…kichwa cha Kristo ni Mungu.” (1 Wakorintho. 11:3).

“na vitu vyote vikiisha kutiishwa chini yake, ndipo mwana mwenyewe naye atatiishwa chini yake yeye aliyemtiishia vitu vyote, ili kwamba Mungu awe yote katika wote.” (1Wakorintho 15:28).

Wakati akiwaandikia Waefeso Paulo anasema, “Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo…”. (Waefeso1:3).

Hizi ni aya za ajabu zinajitokeza katika kifungu bila maelezo ya kina. Hata hivyo zote hulenga Mwana kujinyenyekeza kwa Baba.

Ni kwa kiwango gani aya hizi tunazoziangalia sasa yatupasa tuzielewe katika muktadha wa Yesu kutumwa ulimwenguni kama mwanadamu, mwokozi na mpatanishi wa wanadamu, ama wakiwa na utambuzi mpana na wa kina kuliko huu, ni jambo ambalo sisi sote tunaweza kutafakari, na watambuzi na wasomi wanaweza kupinga.

Inaonekana kuwa maelezo ya Mwana kunyenyekea na kumheshimu Baba yanatokana na asili ya uhusiano wao – ambao ni  wa baba na mwana. Yesu ni Mwana pekee wa Baba, na utayari wa Mwana kunyenyekea kwa furaha mapenzi ya Baba ingekuwa kwa upande mmoja kuwa asili tu kwa uhusiano kama huo hata ndani ya Uungu. Na kwa upande mwingine, inawezekana kabisa kunyenyekea huko kunafunua kipengele cha asili ya Uungu ambacho hakingaliweza kudhihirishwa kwa njia nyingine kwa uwazi wa aina hiyo. Asili ya uhusiano kati ya Baba na Mwana unatuonyesha kuwa kujitetea na kujiinua ni jambo geni kwa asili ya Mungu. (Nazungumzia juu ya mada hii katika kifungu kifuatacho, napenda kumtia moyo msomaji kuangalia kwa makini.)

Ni kwa jinsi gani lingeonekana bora kuliko utayari wa kujitoa kwa Mwana, akiwa katika namna ya Mungu, hakuona kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho! Ufunuo wa kushangaza wa asili ya Uungu! Haya yote yanaonyesha kina cha kafara na kiwango cha hupenda walichoonyesha Baba na Mwana kwa njia ya neno (Yesu Kristo) kufanyika mwili, na kifo cha Mwana wa Mungu, kama mwanadamu, msalabani. Nafikiri kwamba neema tele na hekima ya kina ya Mungu katika mambo haya ni ya kushangaza kabisa na ya ajabu. Ni udhihirisho wa utukufu wake. Mwana kujinyenyekeza kwa Baba ni ufunuo wa utukufu wa asili ya Mungu, ulioelezwa kwa namna ambaye haungeweza kuelezwa kwa kina na uwazi kwa njia nyingine!

Tumeona katika maandiko mbalimbali kuwa Yesu Kristo anatangazwa kuwa ni Mungu, na hapana shaka juu ya ukweli huu, ama ukweli huu wafaa kwa sifa yoyote.

Hata hivyo, labda ni katika muktadha wa uhusiano wa Baba na Mwana, na utayari wa Mwana kujitoa kwa Baba ambapo maandiko hutangaza kuwa kuna “Mungu mmoja ambaye ni Baba wa wote…” na kuwa “BWANA Mungu wetu ni BWANA mmoja.”

Naomba uelewe kuwa si kwamba najaribu kutoa maelezo kamili ya kile ambacho wengine wanaita ‘fumbo’ katika uhusiano wa Uungu wa Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Imeitwa ‘fumbo’ kwa sababu kama nilivyoeleza, maandiko yenyewe hayajihusishi na ufafanuzi wa mambo hayo. Nilichoandika hapo juu hakina maelezo ya ‘mwisho’ kana kwamba naanzisha mafundisho. Ni jaribio tu la kuonyesha muktadha wa ‘fumbo’ la ukweli kwamba kuna Mungu mmoja, na kwamba Yesu Kristo kama Mwana wa Mungu, ni Mungu.

Nafahamu kuwa baadhi wanaweza kuwa na tafsiri au msisitizo tofauti juu ya aya hizi, na kudhani kuwa Uungu wa Yesu umeshushwa chini na kudhoofishwa na tafsiri kama hizi. Jambo moja ambalo kwa kweli linaweza kutuletea shida kwenye ufahamu wa tafsiri haswa wa aya hizi, ni kama tunaingiza mawazo ya kibinadamu kuhusu ‘usawa’, ‘kuwa mkubwa’ au ‘kuwa mdogo’ katika Uungu. Kama tunajaribu kutafsiri maana ya ‘Mungu’ kutokana na maelezo ya metafizika au mawazo ya falsafa, inawezekana kabisa tungeweza kushindwa kuelewa mambo yale ambayo aya hizo zinataka kutufundisha. Nitashughulikia kipengele hiki muda si mrefu.

Tumekuwa tukiangalia kunyenyekea kwa mwana na Baba kutoa muktadha wa uelewa wetu wa tamko la kimaandiko kwamba kuna Mungu mmoja. Lakini hii ndiyo upande mmoja tu wa picha. Kuna upande mwingine unaangaza nuru yake juu ya Kristo Yesu kwa njia ambayo inathihirisha na kuonyesha Uungu wake wa pekee. Na lazima sasa tuangalie hii ili kutupa picha kamili, na tusaidie ufahamu wetu katika vitu hivi.

YESU ALIPATA KWA MUNGU BABA HESHIMA NA UTUKUFU.

Kama Bwana Yesu alivyofanya siku zote kumpendeza Baba, vivyo hivyo ilimpendeza Baba kumheshimu na kumwadhimisha mwanawe – Mathayo 28:18; Yohana 5:22; Wafilipi 2: 9-11. Yesu alipewa mamlaka yote mbinguni na duniani, na Bwana Yesu ndiye atakayehukumu kila mtu siku ile; na kwa Yesu Kristo kila goti litapigwa mbinguni na duniani! Mungu amekabidhi hukumu zote kwa Mwana. Kwa nini? Neno la Mungu linatuambia kwa nini ni hivyo: “ili watu wote wamheshimu mwana kama vile wanavyomheshimu Baba.” (Yohana 5:23). Mungu amekabidhi hukumu zote kwa Mwana ili wewe na mimi tumheshimu Mwana kama vile tunavyomheshimu Baba (Yohana 5:27). Hakuna tofauti. Huwezi kumheshimu mtu ambaye si Mungu kwa kiwango kile unachomheshimu Mungu. Huwezi kumheshimu kiumbe kwa vyovyote alivyo kwa kiwango kile kile unachomheshimu Mungu.

Kwa kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, na “mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake”, maandiko hayawezi kuficha ukweli kwamba Yeye ni Mungu kwa asili yake anayoshiriki na Baba. Uana wa Yesu unafafanuliwa kwa neno la Mungu lenyewe katika Waebrania sura ya kwanza kiasi kile ambacho ule ufunuo hauwezi kuwa kizuizi, na neno la Mungu linatangaza kwamba si kwa habari za malaika wala kiumbe yeyote,

“lakini kwa habari za Mwana asema, Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele.” (Waebrania 1:8).

Kama Baba akimwinua mwanawe Yesu Kristo kwa jinsi maandiko yanavyoonyesha hapo juu, kila mtu lazima awe makini kutokuheshimu au kupotosha habari za Mwana kwa kile anachofundisha.

UUNGU WA MWANA

Tunaweza kusema kwamba maelezo ya kujinyenyekeza huku na kumheshimu Baba yanatokana na asili ya uhusiano wao na ni jinsi gani unavyoakisi haya majina, Baba na Mwana – kama nilivyokwisha kusema. Kama Baba ni Mungu, kwa nini tushangae kwamba Mwana ni Mungu? Isaka kama Mwana alijishusha chini ya Ibrahimu baba yake wakati Ibrahimu alipokwenda kumtoa kafara. Je, utu wa Isaka ulikuwa pungufu kuliko wa Ibrahimu kwa sababu alitakiwa kutolewa kafara? Mungu alisema na Ibrahimu kwamba alipaswa kumtoa mwanawe wa pekee (Mwanzo 22:2), lakini ni Mungu ndiye aliyemtoa mwanawe wa pekee kufa pale Kalvari kwa ajili yako na mimi. Katika Yohana 1:14 Yesu anaitwa “mzaliwa pekee wa Baba”, na katika aya ya 18 anaitwa “mzaliwa pekee Mwana” (ila kwenye Kiswahili SUV imeandikwa “Mungu Mwana pekee”). Hakuna aliye kama Yesu! Si malaika wala binadamu au kiumbe yeyote wa kulinganishwa na Yesu Mwana wa Mungu! Ni Mwana wa Baba, na Mungu Baba anayathibitisha haya kwa wanadamu wote anaposema, “Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.” (Mathayo 3:17). Mungu hazungumzii mtu au malaika maalum aliyeumbwa – anazungumza habari za Mwana!

Ibrahimu hakusita kumtoa mwanawe! Wakati Mungu aliponena naye amtoe mwanawe wa pekee, aliamka mapema kwenda kulifanya hilo. Tayari alikuwa amemtoa mwanawe moyoni mwake – alihitajika tu kufika mahali ambapo Mungu alikuwa amepachagua kwake yeye kumtoa mwanawe! Vivyo hivyo, Baba alikuwa amechagua kumtoa mwanawe wa pekee kabla ya kuwekwa msingi wa ulimwengu, na hili lilitimizwa Kalvari, mahali ambapo Ibrahimu karibu amuue mwanawe! Kile Mungu alikuwa amemwambia Ibrahimu afanye, ndivyo Mungu angefanya kwa ajili yetu. Je! Unafikiria ilimgharimu Ibrahimu kitu kumtoa mwanawe kama dhabihu? Kwa kweli ilimgharimu! Kuna gharama gani kubwa kuliko hii kwa baba? Ni dhabihu gani kubwa kuliko hii ambayo baba anaweza kutoa? Lakini Ibrahimu alimpenda Mungu kuliko mtoto wake mwenyewe.

Je! Ilimgharimu Mungu kumtoa mwanawe wa pekee? Ni kweli ilimgharimu! Ilimgharimu mwanawe mpendwa! Mungu hakumnusuru mwanawe wa pekee (Warumi 8:32) kwa sababu ya upendo aliokuwa nao kwako wewe na mimi, kusudi akuokoe wewe na mimi, kutufanya tuwe wanawe! Hatupaswi kudunisha kile ambacho kilimgharimu Mungu kupata wokovu wetu na kutufanya tuwe wana wake! Mungu hakutoa malaika maalum au kiumbe maalum aliyeumbwa au mnyama fulani kwa wokovu wetu! Hapana. Alimtoa Mwana wake wa pekee.

Na huo ndio ukweli ambao tunapaswa kutambua na kuelewa kwamba yeye tu ambaye ni Mungu anaweza kubeba dhambi za ulimwengu wote kwenye mwili wake msalabani na kuishinda na kuiondoa! Ikiwa Yesu hakuwa Mungu, hatuna wokovu. Msalabani, Mungu alizibeba dhambi zetu (Waebr. 9:28); Mungu aliziondoa dhambi zetu (Yohana 1: 29); Mungu alihukumu dhambi (Warumi 8: 3); Mungu alisulubisha ‘utu wetu wa kale’ (Warumi 6: 6); Mungu aliharibu nguvu ya dhambi na kifo (Warumi 8: 2); Mungu aliharibu nguvu ya Shetani (Waebrania 2: 14; 1 Yohana 3:8), Mungu aliharibu mamlaka na nguvu (Wakolosai 2: 15)! Ni yeye tu ambaye ni Mungu ndiye anayeweza kufanya hivi! Sifu jina lake la ajabu! Haishangazi kuwa Mungu alimwambia mwanawe, “Kiti chako cha enzi, Ee Mungu, ni cha milele na milele: fimbo ya haki ni fimbo ya ufalme wako.” Hapa Mungu hazungumzi juu ya kiumbe aliyeumbwa, au malaika maalum – anaongea juu ya mwanawe, mwanawe wa pekee!

Kibanda kwa ajili ya Yesu?

Petro alitaka kujenga vibanda vitatu wakati Musa na Eliya walipotokea mlimani na Yesu! Hakuwa na wazo la kile alichosema! Leo hii watu wanapojaribu kutathmini hadhi ya Yesu — kwa kumlinganisha na viumbe maalumu– wanachosema hakina maana. Mwana wa Mungu huwezi kumlinganisha na yeyote au chochote. Petro alikosea sana katika ufahamu wake kwamba Mungu alituma wingu lililosababisha Musa na Eliya kutoweka, asibaki hata mmoja isipokuwa Yesu, Mwana wa Mungu. Na Mungu akasema na Petro na wale wanafunzi wengine wawili,

     “Huyu ni mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye.” (Luka 9:35). Jina la Bwana litukuzwe!

Tafadhali fahamu kuwa Yesu Kristo hakuwa aina ya kiumbe maalumu ambaye Mungu alitia roho yake ndani yake – Biblia haitambui wazo hili wala haifundishi kitu cha namna hiyo. Neno la Mungu liko wazi kuhusu jambo hili — inajirudia kumtaja Yesu mara nyingi katika maandiko kwamba ni  “Mzaliwa pekee wa Baba” au “mzaliwa pekee Mwana.” Wale tuliookolewa kwa damu ya Yesu tunaposoma neno la Mungu, Roho wa Mungu hutushawishi kwamba hakuna aliye kama Yesu. Na ukweli kwamba yeye ni Mungu unaangaza kutoka katika maandiko!

Kuna watu wanaotaka kujenga aina ya ‘kibanda cha teoljia’ kwa ajili ya Yesu ili waweze kumweka ndani chake na kumzingatia na mipaka ya mafundisho yao kwa madai kwamba, Yeye kiumbe maalumu mkuu aliyeumbwa na Mungu, na kwa jinsi hiyo ana uwezo wa kimungu japokuwa siyo Mungu! Mungu hakubali wala kutambua jambo kama hilo. Yesu ni Mwana wa Mungu. Na kwa sababu ni Mwana wa Mungu, Yesu ni Mungu – kama ilivyokuwa kwa Isaka mwana wa Ibrahimu, hakuwa simba au tai au nyoka – hapana, alikuwa mwanadamu kama Ibrahimu alivyokuwa mwanadamu!

“YEYE ATANITUKUZA MIMI.”

Tunaambiwa katika sura ya 14 ya Injili ya Yohana kwamba Baba atatuma Roho Mtakatifu baada ya kufufuka kwa Yesu Kristo (aya 26), na katika sura ya 16 Yesu alisema yeye atatuma Roho kutoka kwa Baba. Baba na Mwana hutuma Roho Mtakatifu kwa waumini. Wanafanya kazi katika umoja kwa sababu ni wamoja. Na Roho wa Mungu atafanya nini endapo atatumwa kwako au kwangu? Huduma yake ni nini? Sehemu kubwa ya huduma ya Roho Mtakatifu ni kumtukuza Yesu kwa waumini! Yesu alisema,

“Atanitukuza mimi.” (Aya 14).

Je, hii ndiyo huduma ya Roho wa Mungu inayofanyika katika maisha yako? Roho wa Mungu humtukuza Kristo. Kwa jinsi hii ni nani wa kutukuzwa kama siyo Mungu? Maajabu yoyote na neema ambazo Mungu ametutendea katika maisha yetu kukutukuza wewe au mimi (Warumi 8:30;Yohana17:22) ni kwa sababu ya Kristo, katika msingi ya kufa na kufufuka kwake ili kwamba tufanywe washirika wa uzima wake na kwa hiyo washirika wa utukufu wake na utukufu wa Baba (2 Wakorintho 3:18). Roho amekuja kumtukuza Kristo Yesu katika mioyo na akili za wanaume na wanawake. Hakuja kukutukuza wewe na mimi au malaika au kiumbe cho chote. Jina la Bwana lisifiwe!

 Sifa za kipekee za Yesu kama Mwana wa Mungu pia zimeonyeshwa kwetu katika aya ifuatayo:

“Kama baba awafufuavyo wafu na kuwahuisha, vivyo hivyo na mwana awahuisha wale awatakao.” (Yohana 5:21). Kama Baba awafufuavyo wafu na kuwahuisha, hivyo hivyo Mwana awahuisha wale awatakao. Huu ni ukweli wa ajabu.Ni nani awezaye kutoa uzima kama siyo Mungu? Kwa mara nyingine tena tunaona Baba na Mwana hufanya kazi katika umoja.

Uhusiano wa Baba na Mwana ni wa kina kiasi gani, na ukamilifu wa umoja wao ni wa namna gani inaonyeshwa katika Yohana16:15, Yesu anaposema, “Vyote alivyonavyo baba ni vyangu…”. Maelezo gani hayo! Ukweli gani huu! Vyote alivyo navyo Baba, anavyo Mwana. Watu wanawezaje kusema Yesu siyo Mungu? Kila andiko ambalo watu hunukuu kuhusu Yesu Kristo lazima linachukua ukweli tuliouona katika hizo aya hapo juu. Hupaswi kunukuu aya chache tu na kuacha ukweli uliomo katika aya nyingine.

Ndiyo, kama Mwana, Yesu alijishusha kwa Baba yake, na katika muktadha huu naamini kwamba Biblia inathibitisha kuwa kuna Mungu mmoja: “Kuna…Mungu mmoja na baba wa wote, aliye juu ya yote, na katika yote na ndani ya yote” (Waefeso 4:6) Hili ni tamko la Maandiko. Yesu siyo Baba. Yeye ni Mwana.

Kutokana na mambo yale tuliyoyaona sasa, tunapaswa kuukumbatia ukweli huu, yaani, kama ilivyompendeza Yesu kumheshimu Baba yake na kufanya mapenzi yake, vivyo hivyo ilimpendeza Mungu kumheshimu mwanawe na kumuinuaHii ni ajabu ya uhusiano kati ya Baba na Mwana. Siyo jambo geni wala jambo la kushangaza. Baba ampenda Mwana na Mwana ampenda Baba.

Kama tulivyoona, Mwana huheshimiwa kama Baba anavyoheshimiwa, na kwa sababu yeye ni Mwana wa Baba yake, anashiriki Uungu sawa na Baba, na ni kwa sababu hii ndipo ukweli huu wa Uungu wa kipekee – kwamba Yeye ni Mungu – hauwezi kujificha na unaendelea kujitokeza katika maandiko. Ni Mungu mwenyewe anayemwita Mwanawe ‘Mungu’ kwenye Waebrania 1:8.

USAWA

Uelewa wetu kumhusu Mungu na mwanawe lazima utoke kwenye maandiko. Ni Mungu ambaye kupitia kwa Roho wake aliyavuvia maandiko ili yaandikwe kwa ajili yetu, na ni Mungu ndiye aliyechagua cha kutufunulia kupitia maandiko haya. Hivyo basi, ufafanuzi au fasili yoyote ya Mungu lazima ipate msingi wake katika Biblia na wala siyo katika mabahatisho ya falsafa au makisio ya metafizikia. Ninachomaanisha ni hiki: mtu anaweza kuuliza, “Ikiwa Yesu anafuata mapenzi ya baba yake na kama maandiko yasemavyo, ‘Mungu ni kichwa cha Kristo’, na pia alivyosema Yesu kuwa ,’Baba ni mkuu kuliko mimi’, basi Yesu anawezaje kuwa Mungu? Swali hili linatokea kwa sababu tunazo dhana zetu wenyewe kuhusu fasiri ya Mungu – swali hili halizingatii aya zote tulizoziangalia katika Agano la Kale na Agano Jipya, ambazo zinaonyesha wazi kuwa Yesu ni Mungu. Kuna kanuni ya msingi inayosema kwamba tunapaswa kufasiri maandiko kwa kutumia maandiko, sio kuunda fasiri za maandiko kadhaa yanayopingana na maandiko mengine mengi. Tumeona kwamba Yesu Kristo kama Mwana wa Mungu alijitiisha kwa mapenzi ya Baba yake, lakini hilo halimaanishi kwamba yeye sio Mungu.

Kama tulivyoona, Wayahudi walielewa hili vizuri wakati Yesu alipowaambia kwamba Mungu ndiye Baba yake (Yohana 5: 17,18). Wayahudi walitaka kumuua mara moja kwa sababu alisema hivyo, na maandiko yanaelezea kwa nini walitaka kumuua – ni kwa sababu ‘alimwita Mungu Baba yake, akijifanya sawa na Mungu’. Je! Huu ndio ufahamu wako kuhusu Uungu pia? Ikiwa Yesu ni Mwana wa Mungu, basi yeye ni sawa na Mungu, yeye ni Mungu! Wayahudi walielewa mambo hayo vizuri sana.

Shida kubwa leo katika kuelewa mambo haya ni fikra zetu kuhusu usawa . Roho ya Shetani huwa kinyume cha Roho wa Mwana-Kondoo wa Mungu. Kuhusu Lusifa iliandikwa, “Umesema moyoni mwako, nitapanda mbinguni, nitainua kiti changu cha enzi juu ya nyota za Mungu … nitakuwa kama yeye Aliye juu zaidi.” (Isaya 14: 13,14). Tabia ya Shetani ni kupigania cheo na mamlaka, kujiinua kwa sababu anajiona ni mzuri tu kama wengine, mzuri kama Mungu. Na ikiwa anafikiria kuwa yeye ni mzuri tu kama Mungu, kwamba yeye ni sawa na Mungu, kwa nini amsikilize Mungu? Kwa nini ajitiishe kwa Mungu? Ni roho hiyo ambayo husema,

“Mimi ni mzuri kama wewe! Je! Kwa nini  nijitiishe kwako? Je! Kwa nini nikuheshimu? Nina mtazamo wangu ambao ni sawa na wako! Wewe ni nani uniambie cha kufanya? Unapaswa pia kuniheshimu na kusikiliza ninachosema kwa sababu mimi na wewe tunalingana!”

Hii siyo nia ya Kristo. Hii ni nia na roho ya Shetani na iko katika ulimwengu wa sasa. Watu wanataka kuwa sawa na watu wengine, lakini usawa wanaouzungumzia leo sio usawa unaofundishwa katika Biblia. Watu wanadai kwamba kwa sababu wao ni sawa na wengine, hivyo basi wanaweza kufanya mambo sawa na wanayoyafanya wengine, na wana majukumu sawa na mamlaka kama hao wengine. Wao husema, “Ikiwa siwezi kufanya mambo kama unavyofanya wewe, basi ina maana unadai kuwa wewe ni bora kuliko mimi – lakini mimi ni sawa na wewe! Na kwa nini nikupe heshima iwapo ninalingana na wewe? Wewe ni nani uniambie cha kufanya?”

Huu ndio mtazamo unaoharibu familia na jamii kwa sasa – wanayasema haya yote kwa jina la ‘usawa’ na ‘haki za kibinadamu’! Kwa hivyo watoto hawawaheshimu wazazi wao au walimu wao tena. Wazazi hupata shida kuwadhibiti na kuwaadhibu watoto wao. Wake nao humcheka na kumdharau mtu anayewaambia kuwa mume ndiye kichwa cha familia. Hili ndilo tunda la wazo hili la kisasa la “usawa”. Kila mtu amekuwa ‘mungu’ mdogo ambaye lazima aheshimiwe na wengine – na hawaruhusu yeyote awaambie cha kufanya!

Lakini neno la Mungu linasema, “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu …ambaye alijinyenyekesha na kujifanya hana utukufu.” Ingawa alikuwa na usawa na Mungu, Bwana Yesu hakupigania ‘haki’ zake, kwa hiari yake alijitiisha kwa Baba yake! Alijinyenyekesha akawa mtumwa! Kuna tofauti kubwa kati ya Roho wake na asili yake na roho iliyoko ulimwenguni leo! Mtazamo wake ni tofauti sana na kile kiitwacho na watu ‘usawa’! Je, hili  halikuwa jaribu la Shetani hapo mwanzoni? Alimwambia Hawa, “Kula hili nawe utakuwa kama Mungu.” Kwa maneno mengine, utakuwa kwenye usukani; hakuna mtu anayeweza kukuambia cha kufanya; kila mtu lazima akuheshimu; utakuwa na cheo, mamlaka na utukufu.” Hii ndio sumu ambayo ipo ulimwenguni leo na inaenea duniani kote.

Katika aya zilizonukuliwa hapo juu ambapo Yesu alisema kuwa Mungu alikuwa Baba yake na Wayahudi walitaka kumuua kwa sababu alikuwa akijiweka sawa na Mungu, wakati huo huo Yesu aliyakosoa mawazo yao ya kibinadamu na ya kidunia kuhusu usawa aliposema, “Amin, amin nawaambia, Mwana hawezi kufanya jambo lolote peke yake, yeye aweza tu kufanya lile analomwona Baba yake akifanya, kwa maana lolote afanyalo Baba, Mwana pia hufanya vivyo hivyo.” (Yohana 5:19). Roho ya Shetani ni kujikuza na kujiinua na sio kujitiisha kwa mtu yeyote au kitu chochote, lakini Roho wa Mwana wa Mungu anamwongoza kujinyenyekesha kwa mapenzi ya Baba yake. Katika aya hii Yesu anasisitiza umoja wake na mapenzi ya Baba yake. Yeye haukatai Uungu wake, ila anarekebisha mtazamo wetu kuhusu “usawa” na Uungu! Huu ndio ufunuo ambao Yesu alikuwa anatupatia. Yesu hakusisitiza usawa wake na Mungu, kwa sababu hakuwa na haja ya kufanya hivyo (Wafilipi 2: 6), na kwa sababu sio kwa asili yake kujikuza mwenyewe. Ufunuo ambao Yesu anatupa tunaupata katika Yohana 10:30:

Mimi na baba yangu tu umoja.”

Mbingu haitambui chochote kuhusu wazo la ‘usawa’ linalokuzwa na ulimwengu huu, ambapo marais wa nchi tofauti hukaa kwenye meza moja. Kama marais, wao hujiona kuwa sawa na kwa hivyo wanajitegemea wenyewe. Kila mmoja anatoa maoni yake mwenyewe, wanajadiliana, wanabishana na kila mmoja anajaribu kusisitiza mtazamo wake, mamlaka yake na cheo chake!

Mbinguni hakupo hivi. Lusifa, ambaye ndiye Shetani, alijaribu kujiinua mbinguni na kuleta migawanyiko na mitazamo tofauti, lakini mara moja alitupwa nje! Hamna nafasi kwa nia na fikra za aina hiyo mbinguni!

Mbinguni kuna lengo moja ya milele, kusudi moja – kutoka kwa Baba, kwa Mwana na kupitia Roho Mtakatifu. Baba humtukuza Mwana; Mwana humtukuza Baba (Yohana 17: 1), na Roho Mtakatifu humtukuza Mwana (Yohana 16:14). Hakuna mashindano hapa. Hakuna majadiliano ambapo wawili wanaweza kupiga kura kumpinga mwingine, ambapo chama kimoja hutafuta kuwashawishi wengine. Hakuna kusisitiza juu ya haki za kibinafsi au kujiinua na kujikuza. Hapana! Kuna kusudi na nia moja – inayoonyeshwa na Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Mbinguni kuna umoja wa nia na asili kati yao.

Utukufu wa Mungu unadhihirishwa kupitia umoja huu.

Hakuna mashindano hapa, hakuna kupigania hadhi au haki sawa! Hakuna haja! Je! Kuna tamko kubwa kuliko hili kuhusu Uungu wa Yesu Kristo? “Mimi na baba yangu tu umoja.” Wayahudi walielewa haya kikamilifu, ndio maana alipomaliza kusema hayo walichukua mawe ili wamuue. Naye Yesu alipowauliza kwa nini wanataka kumuua, jibu lao lilikuwa hili, “kwa sababu Wewe ingawa ni mwanadamu unajifanya kuwa Mungu.” (aya ya 33). Je! Ni kwa nini watu leo hawaelewi haya – watu wanaosema kuwa ni Wakristo lakini wanakana kwamba Yesu ni Mungu?

Mtu anayesema kwamba Yesu hawezi kuwa Mungu kwa sababu yeye hufuata mapenzi ya Baba, au kwa sababu Baba ni mkuu kuliko Mwana, mtu huyu haelewi asili ya Mungu. “Mimi na baba yangu tu umoja!” Utafanya nini? Wataka kuwagawanya ili useme mmoja ndiye Mungu na mwingine sio Mungu? Na katika kifungu hiki katika Yohana sura ya 10, ambapo Wayahudi wanamshutumu Yesu kwa kujifanya kuwa Mungu, Yesu hasemi chochote kukataa kwamba yeye ni Mungu. Badala yake, yeye anatumia maandiko kutoka kwenye Agano la Kale kudhibitisha kuwa yeye ni Mungu (aya ya 34-36). Alikuwa amekwisha kuwaambia katika aya ya 28 kwamba yeye huwapa kondoo wake uzima wa milele. Ni nani awezaye kuwapa uzima wa milele isipokuwa yeye ambaye ni Mungu?

Nadhani kuna kipengele kingine katika haya ambacho kina umuhimu sana.

WAFILIPI 2

Yesu anasema hivi katika Injili ya Mathayo, “Njooni kwangu … kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo.” (Mathayo 11: 28-29). Kwa kuwa Yesu ni ufunuo wa asili ya Baba kwetu (Yohana 14: 9), ni wazi kuwa upole ni sifa ya asili ya Mungu, kama inavyosema katika Isaya, “Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliyevunjika moyo na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo iliyovunjika.” (Isaya 57:15). Hili ni jambo la ajabu sana! Mungu hukaa na wanyenyekevu. Katika kuwaonya Wakorintho, Paulo anawasihi kwa upole wa Kristo (1 Kor. 10:1). Hapa duniani watu hujitafutia makubwa na wanapenda kujihusisha na watu wakubwa wenye umuhimu. BALI MUNGU hujihusisha na wanyenyekevu! Njia gani bora ambayo Mungu angeonyesha upole wake kwetu sisi zaidi ya kumtuma mwanawe! Ni kwa kumtuma mwanawe tu Mungu anaweza kutuonyesha kiwango cha upole na unyenyekevu wake.

Hili linatupeleka kwenye kifungu cha maandiko cha kushangaza. Katika sura ya pili ya Wafilipi aya ya sita inasema hivi kumhusu Yesu,

“…ambaye Yeye mwanzo alikuwa yuna namna (au ‘umbo’, au ‘kielelezo’) ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu kushikamana nacho.” (Tafsiri ya SUV).

Au kwa tafsiri ya Neno (Biblia Takatifu 2014) tunasoma yafuatayo:

 “Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa, hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa kitu cha kushikilia.”

Hapa neno linatuambia wazi kuwa Yesu alikuwa na namna (au ‘umbo’ au ‘kielelezo) ya Mungu. Je! Hili linamaanisha nini? Je, linamaanisha kwamba Yesu hakuwa Mungu wa kweli, na kuwa yeye “alionekana tu” kuwa Mungu? Kwa kweli haimaanishi hivyo hata kidogo. Linatumia neno ‘namna’ kwa sababu neno linasema katika mwanzo wa Injili ya Yohana kuwa, “Neno alifanywa mwili.” Hivi ni kumaanisha kuwa yeye aliyekuwa Mungu akafanyika mwili. Tunajua kuwa kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu Yesu alishiriki utukufu na baba (Yohana 17: 5), lakini hakukaa hukoalibadilisha ‘namna’ yake ili aje ulimwenguni kutuokoa mimi na wewe – Neno lilifanywa mwili. Hakuacha kuwa mwana wa Mungu, ila aliacha ushirika huo na hali ya utukufu aliyokuwa nayo na baba, naye akavaa mwili.

Ili kusisitiza uhalisia wa badiliko hili la ajabu maandiko matakatifu yanamzungumzia Yesu kuwa katika namna ya Mungu kwa sababu katika aya inayofuata inatuambia kwamba alijichukulia “namna ya mtumwa” – “bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu.” Badiliko ya kimiujiza lilifanyika kwa sababu ya wokovu wetu. Yeye ambaye alikuwa Mungu wa kweli alifanyika mwanadamu wa kweli (Waebrania 2: 14-18). Mwana wa Mungu akawa mwanadamu. Yesu alikuwa na mwili na damu, alikuwa anahisi uchovu, njaa na kiu, na alijaribiwa katika kila hali kama tunavyojaribiwa (Waebr. 4:15), lakini hakutenda dhambi. Je! Ni jina gani ambalo kwa kawaida Yesu alilitumia kujiita yeye mwenyewe? Alijiita ‘mwana wa Adamu’. Haikuwa mchezo. Hakuwa roho anayejifanya kuonekana kuwa binadamu na kujifanya mtumishi. Alikuwa mwanadamu wa kweli, na alikuwa mtumishi kwa kweli – kukutumikia wewe na mimi kwa neema ya Mungu na wokovu wa milele. Alikuwa katika ‘namna’ ya Mungu na alichukua ‘namna’ ya mtumwa na kuwa mwanadamu. Mungu akawa mwanadamu.

Huku kulikuwa ni kujitoa kiasi gani kwa upande wa mwana wa Mungu! Ingawa alikuwa katika namna na asili ya Mungu na alifurahia ushirika wa utukufu na baba, hakushikilia hadhi yake ya Uungu na utukufu, lakini alijifanya kuwa hana ukuu wala utukufu. Hii inaonyesha kujitolea kwa hiari na unyenyekevu wa kushangaza wa Kristo Yesu. Alikuwa na “usawa” na Mungu na bado hakupambana kuushikilia usawa huu. Kama inavyotafsiriwa katika New Living Translation: “Ingawa alikuwa Mungu, hakufikiria usawa na Mungu kama kitu cha kushikilia.” (“Though he was God, he did not think of equality with God as something to cling to.”) Neno likawa mwili!

Yesu hakuja katika utukufu mkubwa unaoonekana ili kutuvutia! Hakutumia nguvu zake kuu kututiisha. Hakutafuta utukufu kutoka kwa wanadamu. Alichukua namna ya mtumwa na akajinyenyekeza hadi kufa, kifo cha msalabani (aya ya 8). Huu ni ufunuo wa asili ya Mungu. Na aya ya tano ya Wafilipi mbili inatuambia nini? Inasema hivi, “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu…”. Nia moja hii na Roho huyo huyo ambaye alikuwa ndani ya Yesu Kristo anapaswa kuwa ndani yako na yangu. Ni nia na Roho ambayo inatuongoza kujinyenyekesha na kujifanya wasio na sifa. Inatuongoza kutopigania vyeo au usawa! Hii ndio asili ya Roho wa Mungu! Jina la Bwana litukuuzwe!

Ni katika kumtuma mwanawe ambapo Mungu angeweza kutuonyesha kiwango cha upendo wake kwetu (Warumi 5: 8; 8:32), na utukufu wa asili yake katika unyenyekevu wote! Tazama, mwana wa binadamu, mwana wa Mungu, ambaye vitu vyote viliumbwa na yeye, akija hapa duniani, kutoa maisha yake kwa ajili yako na mimi! Lakini alisingiziwa, akakataliwa, akachukiwa na kuuawa. Angeweza kutumia nguvu yake kuwashinda wale waliompinga. Alikuwa na uwezo wa kuita vikosi kumi na viwili vya malaika ili kumwokoa asikamatwe na Warumi. Angeweza kuwaangamiza wapinzani wake kwa tamko tu. Lakini yeye hakufanya mojawapo ya mambo haya. Mwana wa Mungu aliruhusu watu kumtemea mate na kumdhihaki, “aliongozwa kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni,kama vile kondoo anyamazavyo mbele ya wao wamkataye manyoya, hivyo hakufungua kinywa chake.’ (Isaya 53:7). Wanadamu hutaka kujidhihirisha kwa ukuu na nguvu, lakini Mungu anajidhihirisha katika udhaifu na unyenyekevu!

Je! Ni njia gani nyingine ambayo Mungu angetuonyesha asili yake ya kujitoa na unyenyekuvu waziwazi isipokuwa kwa kumtuma mwanawe ili awe mwanadamu. Yesu hakupigania mamlaka, cheo au kutambulika, ila alijinyenyekesha ili kuuawa na wanadamu – huu ni ufunuo wa asili ya Mungu kwa mioyo yetu. Ni nani aliye kama yeye? Mungu hangeweza kumtuma malaika au kiumbe kitukufu ili kutuonyesha yeye mwenyewe alivyo. Hapana. Ilibidi awe mwanawe ambaye alikuwa katika namna na asili ya Mungu na ambaye alionyesha tabia yake kikamilifu. (Waebrania 1: 3).

Mambo ambayo tumezingatia hivi sasa kumhusu Kristo na tabia yake hayamaanishi kuwa amepungukiwa na Uungu, lakini badala yake hutupa Ufunuo kuhusu tabia ya Uungu wenyewe.

Wacha turudi kwenye aya yetu katika kitabu cha Waefeso: “Kuna… Mungu mmoja na Baba wa wote, aliye juu ya yote, na kwa wote, na ndani yenu nyote.” (Waefeso 4: 6). Huu ndio ukweli na ufunuo – kuna Mungu mmoja aliye Baba wa wote. Hakuna miungu watatu wa kujitegemea ambao wameamua kufanya kazi pamoja na ambao wanaweza kutengana baada ya kufarakana kwa kuwa wanalingana na wana “usawa”. Hakuna kitu kama hiki mbinguni. Kuna Mungu mmoja ambaye ndiye Baba wa wote. Naye Baba ndiye ‘kichwa cha Kristo’, na Kristo kama Mwana huyafuatilia mapenzi ya Baba. Yeye ndiye Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Katika muktadha huu kuna Mungu mmoja na Baba wa wote.

Lakini tukumbuke kwamba Baba na Mwana wanadhihirisha tabia ile ile, tabia moja ile; wanafanya kazi kama mmoja wakifunua mapenzi moja, mapenzi yale yale – ‘Mimi na Baba yang tu umoja.’ Kama tulivyoona, katika Biblia yote Uungu unahesabiwa stahiki ya Bwana Yesu Kristo, sio Uungu kama malaika aliyeumbwa au kama Uungu unaokutokana na uasili (by adoption), bali yeye ni Mungu, ‘Mungu pamoja nasi’. Kuna Mungu mmoja na Baba wa wote, lakini kwa sababu Kristo Yesu ndiye Mwana wa pekee wa Baba, ufunuo huu wa Uungu wake unathibitishwa tena na tena na neno la Mungu. Yesu ni Mungu kwa sababu ya asili yake yeye anayoshiriki na Baba.

Kwa hivyo tunapoangazia suala la Uungu wa Yesu Kristo, ufahamu wetu unahitajika kuwa kwenye msingi wa ufunuo wa maandiko. Kwa maneno mengine, sio jambo la kushangaza wala kukinzana kwamba ingawa Yesu anamnyenyekea Baba yake, na Baba yake ndiye ‘kichwa cha Kristo’, wa ama Yesu ni Mungu kwa kuwa yeye ndiye Mwana. Uelewa wetu, fasili yetu ya Mungu na ya Uungu, haitoki kwenye mantiki ya kibinadamu, bali hutoka kwa neno la Mungu ambalo tunapaswa kulifuatilia.

Kusema kweli, ninachokiandika hapa labda hakiwezi kutosheleza akili au mantiki ya bindamu. Lakini kama nilivyosema hapo awali, lengo langu limekuwa kuwapa ufahamu wa mambo haya kulingana na maandiko. Kama unavyojua, na kama nilivyokwisha sema, maandiko yenyewe hayatufafanulii kikamilifu mambo haya, kwa hivyo limekuwa kusudi langu kutokupita maandiko yenyewe. Nimekwenda umbali kama niwezavyo, na kwa maana maandiko yenyewe hayafafanui mambo haya kikamilifu, haishangazi ikiwa msomaji hataridhika na kile nilichoandika hapa. Ila wacha nimkumbushe msomaji kwamba nilichokiandika katika sehemu hii ya mwisho ni jaribio langu mwenyewe kuelezea mambo ambayo hatuwezi kuyaelezea kikamilifu.

Wale wanaoamua kupita yale yaliyoandikwa katika maandiko mara nyingi hutoa mitazamo ambayo haipatikani wala kuungwa mkono na neno la Mungu. Makosa hutokea pale tunapotumia mantiki yetu wenyewe kwenye mistari fulani ya maandiko na matokeo yake ni kupata maana tofauti na yale yaliyosemwa au kufundishwa hapo. Tatizo jingine ni kwamba iwapo tutatumia mantiki ya kibinadamu au lugha ambayo haipatikani katika Biblia, basi tunaweza kushutumiana kwa urahisi mmoja kwa mwingine kwa kuleta maana ambayo haikukusudiwa na mzungumzaji au mwandishi!

BABA, MWANA NA ROHO MTAKATIFU

Hapo mwanzo Mungu alisema, “Iwe nuru; ikawa nuru”. Tunajua pia kutoka kwenye maandiko tuliyoyaangalia kwamba vitu vyote viliumbwa kupitia Yesu Kristo. Kwa hivyo tunaelewa kuwa hapo mwanzo Mungu aliumba vitu vyote kupitia kwa mwanawe Yesu Kristo. Tunaambiwa pia katika aya ya pili ya sura ya kwanza ya Mwanzo kuwa, “Roho wa Mungu alikuwa ametulia juu ya uso wa maji.” Kilicho dhahiri hapa ni kwamba Baba, Mwana na Roho Mtakatifu walikuwa wakifanya kazi kama mmoja, kwa kusudi na nia moja na wakiwa na wazo moja wakati wa kuumba ulimwengu. Kama nilivyosema, haishangazi kwamba tunasoma wingi wa kitenzi katika Mwanzo 1:26, wakati Mungu anapozungumza kuhusu kumuumba mwanadamu anasema: “Tumfanye mtu kwa mfano wetu …”. Uungu wa Mwana na wa Roho Mtakatifu pia umeorodheshwa katika Mathayo 28:19, ambapo tunasoma yafuatayo: “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.” Uungu wa Roho Mtakatifu sio mada ya somo hili lakini kutajwa kwake hakuwezi kuepukika.

HOJA MBALI MBALI

Wacha tujikumbushe kuwa kila kitu kiliumbwa kupitia Kristo Yesu. Alikuwapo na Baba hapo mwanzo. Zaidi ya haya, kama tulivyoona, kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu, Yesu, Mwana wa Mungu, alifurahia ushirika na Baba katika utukufu. Neno la Mungu halituambii chochote kabla ya haya. Biblia haituambii wakati ambapo Mwana ‘hakuwapo’! Ikiwa huo ndio ukweli wa maandiko, na ikiwa huo ndio ufunuo ambao Mungu ametupa – ambao ndio – basi kwa nini watu wanataka kutumia mantiki ya kibinadamu kutupeleka mahali ambapo neno la Mungu halitupeleki na kutufunulia kitu ambacho Biblia haitufundishi?

Wapinzani wa Uungu wake huuliza kwamba ikiwa Yesu ni Mungu, angewezaje kuzaliwa – na alizaliwa lini? Kuhusu swali la pili kati ya haya mawili, jibu linapatikana katika maandiko ambayo tumeyaangalia ambayo yanaelezea kuwa Mwana wa Mungu ni wa milele hadi milele. Yeye ni mmoja na ‘Mimi Niko’, yeye ndiye ‘Mimi Niko’. Je! Utampiga mawe kwa sababu anasema yeye ndiye Mungu? Unaangalia bure kwenye maandiko kutafuta wakati ambapo Mwana hakuwapo! Kuhusiana na swali la kwanza, usemi kuhusu Yesu kuwa yeye ndiye Mwana wa pekee wa Baba, unasisitiza kuhusu upekee mkubwa alio nao Yesu Kristo kama Mwana wa pekee wa Baba.

Wakolosai 1

Vivyo hivyo, watu hunukuu Wakolosai 1:15 na Ufunuo 3:14, ambapo yanazungumza kumhusu Yesu kama “mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote” na “mwanzo wa uumbaji wa Mungu”. Kwanza, ni wazi kutoka kwenye aya zingine na kutokana na jina lake kama Mzaliwa wa pekee wa Baba, kwamba Yesu hakuumbwa – ndiye aliyeumba vitu vyote. Aya hizi mbili lazima zifasiriwe na maandiko mengine mengi yanayogusia mada hii. Bila kuingia kwa undani zaidi, aya hiyo katika Wakolosai inasisitiza tu kwamba Yesu – kama Mwana wa pekee wa Mungu – yupo kabla ya vitu vyote na anawakilisha kichwa na ni mwenye kuanzisha uumbaji wote, na ndicho kile ambacho aya ya 16 na 17 inaendelea kuelezea na kuweka wazi!

Na katika mstari wa 18 inasema kwamba Yesu ndiye “mwanzo na mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu”, hapa haimaanishi kuwa Yesu alikuwa na mwanzo wake wakati alipofufuliwa kutoka kwa wafu! Inamaanisha kuwa hakuna mtu aliyefufuliwa kutoka kwa wafu – na kutorudi tena kwa wafu – kabla ya Yesu Kristo. Kauli anayoitoa Mungu kumhusu Yesu –  “Wewe ni Mwanangu, leo nimekuzaa” – haimaanishi mwanzo wa maisha ya Yesu Kristo, bali kufufuka kwake kutoka kwa wafu baada ya kusulubiwa kwake, kama inavyofafanuliwa katika Matendo 13:33 (…Mungu amewatimizia watoto wetu ahadi hiyo, kwa kumfufua Yesu; kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili, Wewe ndiwe Mwanangu, mimi leo nimekuzaa.).

Ukweli huo huo unaweza kutumika kwenye tafsiri ya Ufunuo 3:14. (Ni muhimu kuzingatia kuwa neno la Kiyunani ‘mwanzo’ (αρχη – arche) katika aya hii linaweza pia kumaanisha ‘mamlaka’ au ‘enzi’.)

Maombi ya Yesu bustanini.

Nilikuwa nimesema hapo awali kuwa Yesu hajawahi kupinga mapenzi ya Baba yake na hilo ni kweli kabisa. Ikiwa tutafikiria kumhusu Yesu alipoomba katika bustani ya Gethsemane na kumsihi Baba yake amuondolee kikombe hicho, huko sio kupinga mapenzi ya Mungu – bali ni kauli ya Uungu wake. Alilazimika kubeba dhambi zako na zangu Kalvari; yeye ambaye alijua tu usafi na utakatifu tu, jasho lilimtoka lililokuwa kama matone makubwa ya damu katika sala yenye kuumiza. Huo haukuwa uasi. Hii ilikuwa kafara. Tokea hili ni ufunuo wa utakatifu wa Yesu Kristo. Alikuwa bustanini katika maombi kwa uchungu kwa sababu  angefanyika dhambi kwa ajili yetu. Kuteswa kwa Yesu bustanini kulitokana na utakatifu yake, kama ilivyoandikwa, “Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye.” (2 Wakor. 5:19).

Yohana 5:26

Kwa kweli kuna aya kadhaa ambazo zinaweza kuwa si rahisi kuzifasiri, lakini fasiri yoyote ya aya lazima izingatie muktadha wa aya hiyo na muktadha wake ndani ya mafundisho ya Biblia. Katika Yohana 5:26 tunasoma yafuatayo: “Kama vile Baba alivyo na uzima ndani yake, vivyo hivyo amempa Mwana kuwa na uzima ndani yake.” Wengine wanadai kwamba hili “linathibitisha” kwamba Yesu hawezi kuwa na Uungu, hawezi kuwa Mungu. Ikiwa ni kweli, basi linapingana na aya nyingi tulizozisoma ambazo zinatangaza kwamba yeye ni Mungu! Walakini, Biblia haijipingi yenyewe. Mwana wa Mungu alifanyika Mwana wa Adamu. Yeye ambaye alikuwa katika namna ya Mungu alijinyenyekesha, akajifanya hana sifa na akawa mwanadamu. Inawezekana kwamba aya hiyo hapo juu inazungumzia uwezeshaji ambao Baba alimpa Yesu kama Mwana wa Adamu, kama Mwokozi wetu na Mpatanishi ambaye alikuwa amechukua mwili. Hili limeonyeshwa kwetu katika aya inafuatia, ambayo inasema, “Naye amempa Mwanawe mamlaka ya kuhukumu kwa kuwa yeye ni Mwana wa Adamu.”

Aya hii inatuambia kuwa Mungu amempa Yesu mamlaka ya kuwahukumu wanaume na wanawake kwa sababu yeye ni Mwana wa Adamu. Kuna mambo ambayo Baba amempa Mwana kwa sababu alifanyika Mwana wa Adamu, kwa sababu alijinyenyekesha kwa kushiriki mwili na damu (Waebrania 2:14) kwa ajili ya wokovu wetu. Mstari wa 26 (wa Yohana 5) pia ni maelezo ya mstari wa 25, ambao unasema, “Amin, amin, nawaambia, Saa inakuja, na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai.” Kwa maneno mengine, Mwana wa Mungu ana nguvu ya kuwafufua wafu kwa sauti yake na kuwapa uzima – na anaonyesha kwamba hili lingefanyika muda si mrefu. Na katika aya ya 21 tunasoma haya: “Maana kama Baba awafufuavyo wafu na kuwahuisha, vivyo hivyo na Mwana awahuisha wale awatakao.” Mwana ana nguvu ya kumpa uhai yeyote apendaye. Lakini kifungu hicho chote kinaonyesha kuwa Baba na Mwana hushiriki katika nguvu hii ya kufufua wafu, na wao hufanya kama mmoja, kwa nia moja na kwa kusudi moja. Na tena tunasoma katika aya ya 22 kuwa, “Baba hamhukumu mtu yeyote, bali amempa Mwana hukumu yote.” Kwa sababu Yesu Mwana wa Mungu alifanyika kuwa Mwana wa Adamu, Baba alimpa Mwana mambo fulani – kwa mfano, ni Mwana ndiye atakayewahukumu wanaume na wanawake (Matendo 10:42). Na kwa nini? Aya inayofuata, aya ya 23, inatuambia!

“Ili watu wote wamheshimu Mwana, kama vile wanavyomheshimu Baba. Yeye asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyemtuma. “

Ukweli ambao umefunuliwa katika kifungu hiki unafaa kutufikisha mahali ambapo tunamheshimu Mwana hata kama tunavyomheshimu Baba! Kwa nini mtu yeyote atumie aya katika kifungu hiki kumdhalilisha Mwana? Je! Kuna chochote kilichoandikwa katika kifungu hiki kwa kusudi la kutushawishi kwamba Yesu si Mungu? Ningesema kinyume chake.

Marko 13:32

Vivyo hivyo, katika kifungu ambacho Yesu anaongea kuhusu nyakati za mwisho anasema, “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba…” (Marko 13:32). Huku sio kukana Uungu wa Kristo kwa ghafla. Kama nilivyosema, mitazamo yetu kuhusu usawa hutuongoza kwa haraka kutoa fasili ya Mungu, na kisichokuwa Mungu. Katika sura hii ya Injili ya Marko, Yesu anatufunulia kwa undani mkubwa na kwa usahihi mkubwa kabisa kitakachotokea katika siku zijazo. Tunajua kuwa katika Kristo “zimefichwa hazina zote za hekima na maarifa” na kwamba ndani yake “unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili.” (Wakolosai 2: 4,9). Hatupaswi kujikwaa kwa aya kama hii katika Marko ambayo inasisitiza tu jinsi siku hiyo ilivyo ya siri. Inaweza kumaanisha tu kuwa siku hiyo haitafunuliwa na yeyote kwa sababu yoyote ile, hata na Yesu kama Mwana wa Adamu.

Luka 18:18-19

Juu ya maandiko yote tuliyoona, baadhi ya watu hupenda kunukuu aya hiyo hapo juu kwa sababu wanaamini Yesu anasema kuwa yeye siyo Mungu. Awali ya yote, tunaweza kusema watu wa namna hiyo wanasahau Yesu aliwaambia Wayahudi, “kabla ya Ibrahimu kuwepo, mimi niko” (ambalo ni jina la Mungu), na Wayahudi walipomshutumu kuwa ajifanya Mungu kwa kusema eti Mungu ni Baba yake, Yesu hakupinga madai yao.

Katika kifungu hiki tajiri anamwita Yesu, “Mwalimu mwema”. Kwa maneno mengine, mtu huyu hakumwona Yesu kama Masihi wa Mungu bali kama mtu anayefundisha vema. Ni hakika kuwa Yesu alitia changamoto ufahamu wa huyu mtu kujua yeye ni nani. Kwa maneno mengine, “Unadhani mimi ni mtu tu, mwalimu mwema na si kingine? Kama unadhani hivyo, basi hupaswi kuniita ‘mwema’, kwa sababu mwema ni Mungu tu.” Ni hakika kuwa Yesu alimfanya mtu yule afikiri zaidi kuhusu Yesu ni nani hasa! Unakumbuka Tomaso alipomwambia Yesu, “Bwana wangu na Mungu wangu”, Yesu hakumrekebisha!

Mathayo 3:14-15

Kwa upande mwingine, tumeona jinsi Yesu alivyojishusha kwa njia mbali mbali na kuwa Mwana wa Adamu – “kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo” – ili aweze kutuhurumia mimi na wewe na kutuokoa.

Tunasoma hayo wakati Yesu alipofika mto Yordani kubatizwa:

“Lakini Yohana alimzuia, akisema, ‘mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?’ Yesu akajibu akamwambia, kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kutimiza haki yote. Basi akamkubali”. (Mathayo 3:14-15). Yohana alitambua kuwa Yesu hakuhitaji ubatizo kwa sababu kama tulivyokwisha kuona, hakuwa na dhambi na hakuhitaji toba yoyote. Yesu hakuping wazo hilo la Yohana lakini alimpa maelezo haya, “ndivyo itupasavyo kutimiza haki yote.” Siyo rahisi kuelewa maelezo hayo, lakini na tutambue kuwa Yesu alisema, “inatupasa”; yaani, inafaa kwamba wote wawili watimize haki yote. Yohana alitumwa kama nabii kubatiza wote ambao wangemjia, na Yesu akajitolea mwenyewe na kumwambia Yohana amruhusu kujumuika. Yesu alikubali kubatizwa kujifananisha na sisi wenye dhambi, na tendo hili pia likatabiri tokea mbali utambulisho mkuu uliotokea msalabani Kalvari.

Tunasoma haya kuhusu Yesu, “Maana ni hakika, hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Ibrahimu. Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake. … Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili.” (Warumi 8:3; Waebr. 2:16-18). Yesu alijitoa mwenyewe msalabani kwa ajili ya dhambi zetu – lakini hakuwa na dhambi (Waebrania 4:15). Bwana alikuja kufananishwa na sisi kama wenye dhambi, na hapa katika Injili ya Mathayo alijitoa mwenyewe ili abatizwe kama alama ya atakachofanya baadaye msalabani. Hii siyo kuukana Uungu wake bali ni ufunuo wa jinsi alivyojinyenyekeza kutuhurumia ili apate kututakasa na kutuokoa toka dhambini.

HOJA LINGINE

Mtu mmoja aliniambia kwamba hakatai Uungu wa Kristo lakini anakataa tu kwamba yeye ndiye Mungu. Je! Hii inamaanisha nini? Kimsingi ni kukataa maandiko yote ambayo tumeangalia katika somo hilo. Mtu anaposema hivi, kimsingi inamaanisha kuwa Yesu ni aliyeumbwa kama kiumbe maalum ambaye Mungu amempa Roho wake, lakini yeye sio Mungu. Lakini neno la Mungu linaonyesha wazi kuwa Uungu wake unatokana na ukweli kwamba yeye ni mmoja na Baba, kwamba yuko kifuani mwa Baba na kwamba yeye ni mwana wa Baba, na kwa hivyo maandiko yanasema, ‘neno alikuwa Mungu ‘.

Neno la Mungu linatangaza kwamba, “Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwana wake wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” (Yohana 3:16). Mungu HAKUUMBA kitu cha kipekee – nje ya yeye – na kisha kumtoa kuwa mwokozi wa ulimwengu! Na ikiwa Yesu alikuwa aina fulani ya ‘kiumbe maalum aliyeumbwa’, kwa nini mbingu zote zinapaswa kumwabudu mtu aliyeumbwa na ambaye hakuwa Mungu? Ukuu wa kina na wa kiwango cha upendo wa Mungu kwako na kwangu ni kwamba alitoa Mwana wake kwa ajili yetu! Iligharimu Baba. Mungu asingeweza kutupatia kitu chochote cha thamani zaidi kuliko MWANA WAKE mwenyewe! Jina lake litukuzwe! “Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote…” (Warumi 8:32).

Ijapokuwa Yesu Kristo alikuwa Mwana wa Mungu, lakini Mungu hakumwachilia ili kutuokoa! Ingawa alikuwa mtoto wa Mungu, alikuwa tayari kubeba dhambi yako na dhambi yangu msalabani. Ni nani anayeweza kubeba dhambi za ulimwengu na kushinda, isipokuwa yeye ndiye Mungu! Mungu hakuumba kitu au kiumbe maalum kutuokoa, alimtoa yeye ambaye alikuwa kifuani mwake.

Ukweli huu umeonyeshwa kwa kushangaza katika mfano wa Ibrahimu na Isaka. Mungu hakumwambia Ibrahimu kutoa ng’ombe, au mbuzi, au kondoo elfu moja. Hapana. Mungu alimwambia Ibrahimu amtoe MTOTO WAKE WA PEKEE! Na Mungu alimwambia afanye hivi kutuonyesha ni nini Mungu mwenyewe angefanya! Hii yote ilikuwa ya kinabii. Mungu hakufanya chini ya vile alivyokuwa amemwagiza Ibrahimu kufanya – Mungu alimtoa mtoto wake wa pekee Kalvari kwa ajili ya mimi na wewe. Isaka alijisalimisha mwenyewe kwa mapenzi ya Baba yake, hata akajitolea kuwa dhabihu, lakini hii haikumfanya Isaka asiwe binadamu duni kuliko Baba yake! Baba yake Ibrahimu alikuwa binadamu kamili, na Isaka alikuwa binadamu kamili pia!

Yesu hakuwa ‘kiumbe au malaika maalum aliyeumbwa’ na Mungu, wala Yesu hakutamkwa awepo kutoka hewani (kupitia neno fulani la Mungu) –  yeye ndiye “mwana wa pekee aliye kwenye kifua cha Baba.” Andiko lote linashuhudia ukweli kwamba tangu mwanzo Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu, anayeishi katika umoja na Baba. Dhabihu ya Baba ilikuwa kubwa mno kwa kutupatia mtoto wake. Sadaka ya Mwana ilikuwa kubwa mno kubeba dhambi yetu ili itufikishe kwa Mungu!

Mungu alitaka kutuonyesha jinsi alivyo, kwa hivyo alimtuma Mwana wake wa pekee atutangazie jinsi Mungu alivyo na kuonyesha utukufu wake (Yohana 1:18), kwani, kama alivyosema, “Yeye ambaye ameniona mimi amemuona Baba.” Hakuna tofauti kati ya hawa wawili.

Tunao uzima wa milele kwa sababu tu tunashiriki uzima wa milele ulio ndani ya Kristo!

Sisi ambao tulizaliwa wenye dhambi, tumefanywa wana wa Mungu kwa sababu tu yeye ambaye ni Mwana kulingana na asili yake ya milele, alitoa maisha yake kwa ajili yetu na alibeba dhambi zetu Kalvari.

Licha ya aya nyingi ambazo tumeangalia, mafundisho mabaya kila wakati hutumia mbinu na hila hiyo hiyo – wanafikiria wamepata maandishi machache ambayo yanasaidia kile wanachotaka kuamini na kupuuza yale mengine ambayo Biblia inafundisha kwa wazi. Kwa hivyo, mtu mmoja alinukuu Yohana 17:21: “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu…”. Mtu huyu anasema kwamba katika utimilifu wa maombi ya Yesu, tutakuwa wamoja na Baba kama yeye alivyo mmoja na Baba. Anaamini hii inaonyesha kuwa Yesu si Mungu wa kweli kwa sababu kweli yake itakuwa ya kweli kwa mwamini – Yesu anaweza kuwa kiumbe maalum, anaweza kuwa mungu fulani (miongoni mwa wengine), lakini yeye sio Mungu, hili ni wazo lao. Walakini unaweza kuamini hii tu ikiwa hautaelewa asili yakow ala asili ya wokovu wetu wala asili ya Kristo.

Yesu alishiriki utukufu na Baba kabla ya ulimwengu kuwako (Yohana 17: 5), na jambo muhimu umilele la utukufu huu ni utakatifu wa Mungu (Yohana 17:11). Yesu Kristo alijua utukufu wa utakatifu huu, ambao alishiriki na Baba. Hata wakati alizaliwa duniani, Kristo alizaliwa mtakatifu (Luka 1: 35), na maandiko yako wazi kabisa juu ya asili ya Kristo: “Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye… Nanyi mnajua ya kuwa yeye alidhihirishwa, ili aziondoe dhambi; na dhambi haimo ndani yake… Maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lo lote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu.” (2 Wakorintho 5:21; 1 Yohana 3: 5; Waebrania 7:26).

Kwa hivyo watu wanafanya nini wanataka kutulinganisha na Yesu Kristo? Je! Wanataka kutuambia kuwa hakuna tofauti kubwa kati ya Kristo na sisi – sisi, ambao tulizaliwa katika dhambi, sisi ambao ni wenye dhambi kwa asili – kwa mzaliwa wa kwanza; sisi, ambao tulisababisha ghadhabu ya Mungu juu yetu na tungepotea milele bila Kristo kutufia? Je! Hawaoni? Je! Hawajui maandiko ambayo yanatuonyesha kuwa Kristo alihitaji kutufia ili tuokolewe na tuwe na uzima wa milele – mtakatifu akifia wale wasiomcha Mungu. Yesu hakuhitaji mtu yeyote kufa kwa ajili yake ili amtakase – alishiriki utukufu huu na Baba tangu mwanzo. Hii ndio sababu alitokwa na jasho kana kwamba ni matone ya damu kwenye bustani ya Gethsemane – kwa sababu angebeba dhambi yako na dhambi yangu msalabani! Yeye alikuwa mtakatifu na mwenye haki atafanywa kuwa mwenye dhambi kwa ajili yako na mimi, ili tuweze kufanywa wenye haki ya Mungu ndani yake (Warumi 5:19; 2 Wakor.5:21). Ni kupitia Kristo na ndani ya Kristo tunapata neema hii na fursa hii. Yeye ni Mwana kutoka milele, yeye ni Mwana sawasawa na tabia yake kutoka milele. Lakini sisi kwa asili yetu, kwa kuzaliwa kwa kwanza kwetu, sisi ni wenye dhambi, hatukuzaliwa kama wana wake, lakini tulipitishwa kama watoto wake kupitia kifo na ufufuko wa Yesu Kristo,

“Ili kuwakomboa wale waliokuwa chini ya sheria, ILI TUPATE KUFANYWA WANA WA MUNGU…Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe KWA NJIA YA YESU KRISTO, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake… Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu.” (Wagalatia 4:5; Waefeso 1:5; 1 Petro 1:3)

Je! Watu wanafikiria wanaweza kudharau au kukataa Uungu wa Kristo kwa kusema sisi pia tutakuwa wamoja na Baba kwa sababu ya Kristo, au kwa sababu Yesu anaitwa ndugu yetu sasa? Je! Wanafikiria kuwa wataabudiwa mbinguni kama Kristo anavyomwabudiwa sasa?

Tunayo wokovu tu kupitia Mwana wa Mungu; tuna uzima wa milele ndani ya Mwana wa Mungu tu.

“Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu ametupa uzima wa milele, na uzima huu uko kwa Mwana wake … Yeye aliye na Mwana anao uzima; na yeye ambaye hana Mwana wa Mungu hana uzima (1 Yohana 5: 11,12).

Je! Tumaini letu la utukufu ni nini? Ni ‘Kristo ndani yetu’! (Col.1: 27). Mungu amechagua sisi katika Kristo kabla ya kuwekwa msingi wa ulimwengu na kutubariki na baraka zote za kiroho katika Kristo. Wokovu wetu ni uzima wa Kristo ndani yetu (Wafilipi 1:21; Gal.2:20; 2 Wakorintho 13: 5). Aya ya mwisho haswa inatuonyesha kuwa bila Kristo ndani yetu tumepotea!

Kwa sababu ya kifo cha Yesu na ufufuko wake, Mungu “ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu,” (2 Petro 1: 4), na katika Waebrania tunasoma kwamba Mungu anashughulika na sisi kama na Mwana, ili tuweze kushiriki utakatifu wake. (Waebrania 12:10). Je! Umesoma hii? Je! Unaamini hii, ya kuwa sisi ambao tulikuwa wenye dhambi kwa asili, sasa kupitia ukombozi ulio katika Kristo, tunaweza kuwa washirika wa tabia ya Uungu na utakatifu wake? Hii ndio sababu inaitwa ‘wokovu mkubwa sana’. Kwa hivyo ikiwa tunaweza kufanywa washirika wa tabia ya Uungu na utakatifu wake, kwa nini watu wengine hukosa ukweli kwamba Yesu Kristo tangu kabla ya kuwekwa kwa ulimwengu anagawana asili ya Baba yake, anagawana asili ya Mungu na utakatifu wake kama Mwana wa Mungu wa pekee?

Kama Yesu angekuwa sio Mungu, haingekuwa na wokovu.

HITIMISHO

Sisi sote tunaweza kuwa na dhana zetu za kifalsafa au za kimetafizikia kuhusu maana ya kuwa ‘Mungu’. Na tunaweza kushikilia fikra hizi bila kuizingatia mafundisho ya Biblia. Katika somo hili naamini maandiko yanaonyesha kuwa Yesu ni Mungu kwa sababu yeye ni Mwana wa Baba. Umoja wake wa kipekee na Baba unamaanisha kuwa yeye ni mmoja na Baba katika asili yake . Tumeangalia maandiko kadhaa ambayo yanaonyesha wazi umoja huu, na pia ambayo yanafunua na kutangaza Uungu wa Kristo – kwamba Yesu Kristo ni Mungu.

Tumeona kuwa kama vile Mwana anavyomheshimu na kumtukuza Baba, ndivyo pia Baba humheshimu na kumtukuza Mwana (2 Petro 1:17). Na ukweli huu utadumu,

“Ili watu wote wamheshimu Mwana, kama vile wanavyomheshimu Baba. Yeye asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyemtuma. “

Na hivi ndivyo nilivyoanza somo hili, kwa kuonesha kutoka kwenye maandiko jinsi mbingu yote na dunia zinavyomwabudu Baba na Mwana kwenye kiti kimoja cha enzi.

Hata hivyo, kwa maana baadhi ya aya tulizoziangalia hazina maelezo ya wazi kuhusu maana kamili, mambo fulani hayana budi kubakia yakiwa yamefichwa kwetu – suala la fumbo linabakia!

MWANA WA ADAMU

“yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote…”

Mada ya somo hili imekuwa kuhusu Uungu wa Bwana Yesu Kristo, lakini wokovu wetu unategemea ukweli kwamba Mwana wa Mungu alifanyika Mwana wa Adamu, na jina hili la mwisho aghalabu lilitumiwa na Yesu kusisitiza ubinadamu wake. Haikuwa mchezo. Sala yake yenye kuumiza na jasho lake ambalo lilikuwa kama damu kwenye bustani ya Gethsemane vinaonyesha waziwazi hili. Ili kutuokoa na kutukomboa kabisa kutoka kwa nguvu ya dhambi na ya kifo na ya Shetani, na kufanywa mpatanishi na Kuhani Mkuu kwa niaba yetu, ilibidi afanywe awe kama sisi. (Waebrania 2: 9-18; Warumi 8: 1-4; 2 Kor. 5:21 – nimetaja aya chache tu zinazohusiana na haya!). Aliacha utukufu wa Baba yake na akawa mwanadamu na akakubali udhaifu na majaribu yatokanayo na hali hiyo (Waebrania 5: 2), na labda hili linaweza kusaidia kufafanua aya kadhaa ngumu zaidi tulizoziangalia. Alijaribiwa kama sisi, lakini hakutenda dhambi. (Waebrania 4:15,16).

Yesu Kristo alikuja katika mwili kushinda dhambi, kifo na ibilisi ili aweze kuja ndani ya maisha yetu kupitia Roho Mtakatifu, kutuweka huru kutokana na dhambi na kuishi ndani yetu! (Warumi 8: 1-4; 6: 1-6; Wagalatia 2:20; 2 Wakorintho 4: 8-11). Wokovu huu ni zaidi ya msamaha wa dhambi. Kristo ametupa uhai wake, uzima wa milele, maisha ambayo yameshinda na yanayoishinda dhambi na kutufananisha na mfano wa Mwana wa Mungu na kutufanya tushiriki katika Uungu na utakatifu wake. (Warumi 8:29; 2 Wakorintho 3:18; 1 Yohana 2:6; 4:17; 2 Petro 1:2-4; Waebrania 12:10). Wokovu wetu ni mkuu kiasi gani? Ndio maana mwandishi wa waraka kwa Waebrania anauliza, “Tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii?” (Waebrania 2:3). Je! Hili linawezekanaje?

Katika somo hili tumeona jinsi watu wengine wanataka kufumbua ya sirini, lakini Mungu ametutangazia waziwazi utajiri wa utukufu wa ile siri ambayo ilifichwa kwa vizazi na vizazi. Siri hii ni nini? Paulo analitangaza hivi: “Kristo ndani yako, tumaini la utukufu.” (Wakolosai 1: 25-27).

Ukweli huu ni mkuu sana na wa kina sana kiasi kwamba unazidi ufahamu wa asili. Ukweli huu hufanywa kuwa hai kwetu kupitia ya huduma ya Roho Mtakatifu (1 Kor 2:9-16). Hii ndio sababu Paulo anaomba kwamba Mungu awape watakatifu (wa huko Efeso), “Roho wa hekima na ufunuo katika kumjua yeye…ili tujue ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu.” (Efe.1:17-21). Kwa maneno mengine, nguvu ambayo kwayo Mungu Baba alimfufua Yesu Kristo kutoka kwa wafu, ndiyo nguvu inayofanya kazi ndani yetu, ikituweka huru kutoka kwa dhambi na kutufanya tufanane na mfano wa Mwanawe.

Hili ni jambo la ajabu sana! Wokovu mkuu sana. Baba na Mwana kwa Roho Mtakatifu wanatuwezesha kuishi kama Kristo. Kisichowezekana kwa mwanadamu, kinawezekana na Mungu, kinawezekana na ‘Kristo ndani yetu’. Jina lake lipewe utukufu!

Haya yote yanawezekana kwa sababu ya ‘Mwanakondoo wa Mungu aliyechinjwa tangu kuwekwa kwa msingi wa ulimwengu’ kwa ajili yako na yangu! Haishangazi kuwa mbinguni kote wanamwabudu na kumpa utukufu kama wanavyomwabudu Baba na kumpa utukufu.

NYINYI JE, MWASEMA MIMI NI NANI?

Baada ya kuwauliza wanafunzi kile ambacho watu wengine husema kumhusu yeye, Yesu aliwauliza wanafunzi wenyewe, “Nyinyi je, mwasema mimi ni nani?” Swali hilo ndilo Roho wa Mungu anatukabili nalo – unafikiria Yesu Kristo ni nani? Petro akajibu na kutangaza kwamba Yesu alikuwa “Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai”. Naye Yesu akamwambia Petro, “Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.” (Mathayo 16:17). Kwa hivyo kwa mujibu wa Yesu Kristo, tunajua yeye ni nani tu kwa kupitia ufunuo tuliopewa na Baba. Hili linathibitishwa na kile anachosema Yesu katika Mathayo sura ya 11: “hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia.” (Mathayo 11:27). Kumjua Kristo ni nani huja kwa ufunuo wa Mungu. Baada ya kukiri kwa Petro katika aya ya 17 ya Mathayo 16 ambayo tumesoma, Yesu anasema hivi: “Nami nakuambia, wewe ndiwe Petro (Kiyunani; Petros – jina la Petro linamaanisha ‘jiwe’), na juu ya mwamba (Kiyunani; Petra – ambalo linamaanisha mwamba kubwa) huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.” (Mathayo 16:18). Yesu atalijenga kanisa lake juu ya mwamba. Je, Mwamba ni nini? Ni ufunuo kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai, na ndivyo Petro alikuwa amekiri. Ukweli kwamba Yesu ndiye mwamba (kiyunani; Petra’, siyo ‘Petros’) unathibitishwa katika 1 Wakorintho 10:4: “Wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo.” Na tena tunasoma, “Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo.” (1 Wakor. 3:11).

Kanisa limejengwa juu ya ufunuo wa Mungu kwa mioyo ya wanaume na wanawake kwamba Yesu ndiye Kristo wa Mungu. Je! Baba amekufunulia Yesu Mwana wa Adamu ni nani? Au umefanya kujua Yesu ni nani kupitia mantiki yako mwenyewe? Kumbuka kwamba kulingana na Bwana Yesu, huwezi kumfahamu yeye kupitia mwili na damu. Sio matokeo ya mantiki ya kibinadamu; sio kupitia ushawishi au hoja za wanadamu. Je! Unamjua Yesu ni nani kwa sababu umetumia nguvu zako za akili kwenye maandiko (kama Mafarisayo walivyojaribu kufanya), au unamjua kwa ufunuo kutoka kwa Baba – ufunuo wa kina kuliko mantiki?

Je! Unasema Yesu Mwana wa Adamu ni nani? Hili ni swali muhimu sana! Ni kwa msingi wa jibu la swali hili ambapo Yesu atalijenga kanisa lake! Kanisa limejengwa juu ya ufunuo wa Baba kwa mioyo yetu kuhusu asili ya mwanawe! Je! Wewe ni sehemu ya kanisa lake, au unalijenga kanisa jingine na Yesu tofauti?

© David Stamen 2020

 

Comments are closed.