RSS

KANISA NI NINI?

BIBI HARUSI WA KRISTO.

Kwanza kabisa, kama tukifuata mpangilio wa mafundisho ndani ya neno la Mungu, kanisa ni Bibi harusi wa Kristo. Tunaupata ukweli huu katika kufungua sura za Biblia. Zile ambazo zinaeleza Mungu angeenda kufanya nini juu ya kifo na ufufuo wa mwanae pale Kalvari, aliutazama kwanza uumbaji wa Adamu na Eva. Kati ya vyote ambavyo alivifanya hakuona wa kuendana na Adamu awe msaidizi. Kwa hiyo Mungu akamweka Adamu katika usingizi mzito, na wakati Adamu akiwa katika usingizi mzito Mungu aliutwaa ubavu wake na katika ubavu huu akamwumba Eva ambaye angekuwa mkewe. Adamu alipomwona Eva akasema, “Huyu sasa ni mfupa katika mfupa wangu na nyama katika mwili wangu. Jina lake ataitwa ‘mwanamke’ kwa sababu ametoka katika mwanaume.” (Kwa lugha ya kiyahudi ‘mwanamke’ ni ‘isha’, na ‘mwanaume’ ni ‘ish’. Neno ‘isha’ lina maana ‘yeye aliyetoka katika mwanaume’, yaani, ‘ish’. ). Sasa pamoja na kwamba maneno haya mawili pekee yanatuonyesha kwamba mwanamke aliumbwa akitoka katika mwanaume. Kupitia uumbaji wa Mungu  wa Adamu na Eva tuna uakisi timilifu kabisa wa mpango wa Mungu kutoa Bibi harusi kwa ajili ya Mwanae, Yesu Kristo. Biblia inastaajabisha sana! Biblia ni neno la Mungu, ni uvuvio wa Roho Mtakatifu.

Askari walipokuja kuutoa mwili wa Kristo pale msalabani, walikuta ameshakwisha kufa tayari lakini ili kuhakikisha wakamchoma mkuki ubavuni kwake na tazama, maji na damu vikamtoka. Damu na maji ndio viashirio vya ukombozi  na utakaso wa kanisa la Kristo.

‘Huyu ndiye aliyekuja kwa maji na damu, Yesu Kristo; si katika maji tu, bali katika maji na katika damu. (1Yohana 5:6).

‘Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno.’ (Waefeso 5:25-26).

‘…mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.’ (Matendo 20:28b)

Tungenukuu mistari mingine lakini nadhani ukweli uko wazi. Kama Eva aliumbwa kutoka katika ubavu wa Adamu vile vile Bibi harusi wa Kristo ataumbwa kutoka katika vile vilivyotoka ubavuni mwake. Neno la Mungu linaunganisha habari hizi za Adamu na Kristo vizuri sana kwa sababu kutoka katika hiyo hiyo sura ya Waefeso Paulo ananukuu maneno ya  Adamu kuhusu Eva anayotumia kwa Kristo na kanisa lake, ‘Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake, mfupa katika mifupa yake, na nyama katika nyama yake.’ (Mstari wa 30). Zaidi Paulo anaendelea kunukuu kauli nyingine kwenye kitabu cha Mwanzo iliyofuatia baada ya kuumbwa kwa Eva – na tena anailinganisha na Kristo na kanisa katika njia yenye kushangaza mno, ananukuu, ‘Kwa sababu hii mwanaume atamwacha babaye na mamaye na ataambatana na mkewe, nao si wawili tena bali ni mwili mmoja.’ Lakini tena Paulo anaongezea ajabu / siri kuu, “lakini nazungumza kwa habari ya Kristo na kanisa.”

Mpango thabiti na wa milele wa Mungu wa kumtengeneze Mwanae Bibi harusi umewekwa wazi kwenye maandiko hayo. Tunaupata ukweli huu kwenye Agano Jipya. Paulo anasema hivi, “Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi. Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo.” (2 Wakorintho 11:2-3). Hapa pia tunapata picha nyingine ya Bibi harusi kuandaliwa kwa ajili ya Bibi harusi wake – mumewe.

Katika Mathayo 25 Yesu anatuambia kwa habari ya wanawali kumi waliotoka kukutana na bwana harusi. Ni wazi katika mfano huu Yesu anajitambulisha kama bwana harusi na kwamba wale wanawali wenye hekima wanawakilisha kanisa lake lililo tayari kumpokea ajapo katika siku ile kuu. Vivyo hivyo kwenye mfano mwingine kwenye ile Mathayo 22, Yesu anazungumza kwa habari ya wale walioalikwa kwenye sherehe ya harusi na anaweka kwa uwazi kabisa kwamba ni wale waliokubali kweli kweli kuisikia Injili ndio watakaokubaliwa kuingia ijapo siku ya sherehe hiyo. Na tunasoma kutimilizwa kwa hili katika kitabu cha Ufunuo.

“Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari. Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ingarayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni matendo ya haki ya watakatifu. Naye akaniambia, Andika, Heri walioalikwa karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo. Akaniambia, Maneno haya ni maneno ya kweli ya Mungu.” (Ufunuo 19:7-9).

Katika Ufunuo 21, Yohana anaandika hivi, “Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe. . . Akaja mmoja wa wale malaika saba,…naye akanena nami,  akisema, Njoo huku,  nami nitakuonyesha yule Bibi-arusi, mke wa Mwana-Kondoo. Akanichukua katika Roho mpaka mlima mkubwa,  mrefu,  akanionyesha ule mji mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu; wenye utukufu wa Mungu, na mwangaza wake ulikuwa mfano wa kito chenye thamani nyingi kama kito cha yaspi,  safi kama bilauri.” (Ufunuo 21:2, 9-11). Tunafahamu kwamba kanisa ni mahali pa Mungu kukaa na kutulia katika Roho, na Kristo amewapa watu wake utukufu wake (Waefeso 2:21,22; 2 Wakor.3:18). Na sasa katika Ufunuo 21 tunaona kanisa limeelezewa kama ni harusi aliyepambwa kwa ajili ya mumewe na vile vile kama mji mpya wa Yerusalemu ambapo Bwana Mungu mkuu na mwanakondoo wanaishi, na ni utukufu wake Mungu ung’aao na kuleta nuru.

Ukweli huu haujafungwa kwa habari ya muda ujao tu. Rohoni, tayari sisi ni sehemu ya haya na pia tuna nafasi katika kanisa hili la Kristo Yesu. Akiandika kuhusiana na wote waliozaliwa na Roho wa Mungu katika Wagalatia, ‘Bali Yerusalemu wa juu ni mwungwana, naye ndiye mama yetu sisi.’ (Wagalatia 4:26). Katika Yohan 3:3 Yesu anasema, “Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu”. Neno ‘mara ya pili’ (tena) pia linamaanisha (kwa lugha ya Kigiriki) kutoka juu. Tumezaliwa kutoka juu, kwa Roho ya Mungu iliyotumwa toka mbinguni na tunaweza kuziingia nyua za utukufu wake mbinguni, yaani, kuingia katika uwepo wa Mungu mbinguni (Waefeso 2:3, 2:6, Waebrania 10:19). Ngoja tusome andiko hili muhimu, “Bali ninyi mmeufikilia mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na majeshi ya malaika elfu nyingi,  mkutano mkuu na kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye haki waliokamilika, na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.” (Waebrania 12:22-24). Hii ni mistari ya kustaajabisha; ni ufunuo kwetu wa kweli juu ya mambo makuu ambayo Mungu ameyatenda kwetu na kwa ajili yetu.

Unaweza kuona sasa ni kwa namna gani ufahamu wetu kuhusu kanisa la Kristo unahitaji kutegemea na kujazwa na Neno lake Mungu mwenyewe ili kuelewa kwetu kukue kupita tuonavyo kawaida, kidunia na katika mwili. Kuikubali kwetu kweli hii na kuelewa kwetu kunabidi kuchimbwe mno na Roho wa Mungu.

Kanisa ni Bibi harusi wa Yesu, mahali pale pa kukaa katika ukuu na umilele wake. Katika tamati hii Adamu na Eva waliumbwa! Ni kusudi tukufu la Mungu kutuokoa sisi (mimi na wewe) na kutufanya kuwa Bibi harusi wa Kristo. Bibi harusi ni nani? Kanisa ni nani? Ni wale waliokombolewa kwa damu ya Yesu na waliookolewa kwa Neema ya Mungu kupitia wokovu uliomo ndani ya Kristo pekee. Ni wale waliozaliwa, si kwa damu wala kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa matakwa ya mwanadamu bali kwa Mungu. Kama Yohana anasema ‘tunatokana na Mungu’ (1 Yoh.4:4). Maneno ya ajabu sana!

Tumeokolewa kwa neema kwa njia ya imani. Hata hivyo kuna baadhi ya maandiko yanayotuhimiza kuwa na bidii katika kufanywa imara kwa habari ya kuitwa kwetu na uteule wetu (2 Petro: 1:10). Kwa hiyo tunaona pale mwisho kwenye ule mfano wa wanawali kumi, Yesu anatuhimiza kwa maneno haya, ‘Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa ajayo Mwana wa Adamu.’ (Mathayo 25:13). Yesu anatoa tahadhari hii kwa sababu kwenye huu mfano, nusu ya wanawali hawakuwa tayari kwa ajili ya kumpokea Bwana harusi na wakakataliwa kuingia katika uwepo wake. Alipokuwa akiongekea kuhusu makanisa saba katika ule ufunuo, Yesu analiambia kila kanisa kwamba ahadi ya kushiriki naye katika ufalme wake wa milele inawahusu wale washindi tu. Ahadi hii inawagusa waliovumilia hata mwisho na waliojiweka tayari katika mahusiano yao na Bwana kwa ajili ya kurudi kwake. Yesu alijitoa kwa ajili ya kanisa ili…

‘apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa.’ (Waefeso 5:27).

MWILI WA KRISTO.

Kwa hiyo, ukweli huu ya kwamba kanisa ni Bibi harusi wa Kristo tunaupata katika maandiko kutoka Mwanzo hadi ufunuo. Tungeweza kusema kwamba kuwa Bibi harusi wa Kristo kunasisitiza mahusiano yetu naye.

Hata hivyo, kuna ukweli mwingine maandiko yanazungumza kuhusu kanisa kuwa mwili wa Kristo.Tunaweza sema maelezo haya yanasisitiza maisha na kazi au shughuli (function) ya kanisa,

‘…akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.’ (Waefeso 1:22-23).

‘Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake.’(1Wakorintho 12:27).

‘…kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe.’ (Waefeso 4:12).

Ipo kweli nyingine kuu. Kama tumezaliwa kwa mara ya pili na Roho wa Mungu, tukishiriki uzima katika Kristo Yesu; tu ndani ya Kristo, na Kristo ndani yetu. Sisi tu roho moja naye! (Yohana 14:20; 1 Wakorintho 1:30; 6:17; 13:5). Kristo pekee ndiye uzima wetu! (Wafilipi 1:21; Wagalatia 2:20).

‘Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili. Na ninyi mmetimilika katika yeye aliye kichwa cha enzi yote na mamlaka. (Wakolosai 2:9,10).

Kupitia umoja wetu na Kristo katika Roho tunamiliki utele uliko ndani yake! Huu ndio ukweli – tu mwili wake!

Neno la Mungu linatufundisha ya kwamba mwili unatenda kazi na unakua kutegemea mchango wa kila kiungo, na Mungu hutoa karama kwa kila kiungo kwa hekima yake na kama apendavyo. Hili ni fundisho la sura ya 12 ya waraka wa kwanza kwa Wakorintho:

‘Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.’ (Mstari wa 7). Kwa kiwango gani ukweli huu utatambulika na kufanyiwa kazi inategemea na kanisa la mahali pamoja au dhehebu uliloko! Inaonekana makanisa mengi huwa wanakosa kusudi hasa la Mungu kwenye jambo hili. Kimsingi, kwenye kitabu cha Waefeso sura ya 4, Paulo anafunua kweli hii ya kwamba kanisa litaongezeka na kukua katika kujiimarisha lenyewe katika upendo iwapo kila mmoja ndani ya kanisa atatumia vema alichojaliwa sawasawa na kipimo cha Neema ya Mungu juu yake (Waefeso 4:15,16). Afya na ukuaji wa mwili kufikia hadhi ya utele wa Kristo ni muhimu kiasi kwamba Paulo anasema huduma zote ambazo Mungu amezitoa kwa kanisa ni kwa kusudi ambalo ni kuongezeka na kukua kwa mwili utele wa Kristo, ambaye ndiye kichwa cha mwili huu. Jambo hili ni muhimu mno na imenipasa kunukuu aya ifuatayo,

‘Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo. Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo. (Waefeso 4:11-16).

[Kwa bahati mbaya, makanisa yameunda mfumo ambao mchungaji anaendesha au kuelekeza akiwa mbele, na kwa mapana haya, tofauti na kuimba, washirika hukaa na kusikiliza wakichangia kiasi kidogo sana. Huku ni kujitoa kwenye kile tunachosoma kwenye Agano Jipya ambapo Paulo anasema, ‘Basi, ndugu, imekuwaje? Mkutanapo pamoja, kila mmoja ana zaburi, ana fundisho, ana ufunuo, ana lugha, ana tafsiri. Mambo yote na yatendeke kwa kusudi la kujenga…. Na manabii wanene wawili, au watatu, na wengine wapambanue. Lakini mwingine aliyeketi akifunuliwa neno, yule wa kwanza na anyamaze.’ (1Wakorintho 14:26-30). Katika kanisa hili la kwanza, wengi waliashiki kwenye mikutano ya kanisa (na wakati mwingine) kulingana na vipawa/karama za Roho Mtakatifu alivyowajaalia. Soma 1 Wakorintho 12:4-12 kwa makini. Ingawaje hatuwezi kulifuatilia somo hili hapa.]

Tunapozungumzia mwili Wake, hatuzungumzii mwili wa kawaida bali kusanyiko la watu ambao Biblia inawaita ‘mawe hai, nyumba ya kiroho, uzao wa kikuhani kwa ajili ya kutoa sadaka za rohoni mbele za Mungu’ (1Petro 2:5), ambapo kila kiungo ni muhimu kwa ajili ya utendaji yakinifu wa mwili mzima, na ambapo washirika (viungo) wanashirikiana na kujaliana kwa usawa (1Wakorintho 12:25)! Tayari tunaweza kujionea katika jambo hili kwamba kanisa la Yesu Kristo sio taasisi, wala sio shirika! Ni mwili, ni mwili wa Kristo, ambapo neema ya Mungu na Roho hufanya kazi kupitia kila mshirika kwa kuufaidia mwili mzima (washirika wote).

Kristo hakumwaga damu yake kwa ajili ya taasisi, dhehebu ama shirika. Yesu alikufa kwa ajili ya wanawake na wanaume ili kwamba awabatize katika mwili mmoja na Roho moja (1 Wakor. 12:13). Na yeye ndiye Kichwa mkuu wa mwili wake.

KRISTO KAMA KICHWA CHA KANISA.

“Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote.” (Wakolosai 1:18).

“Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili.” (Waefeso 5:23.)

Hapa tena tunao ukweli wa wazi kabisa, sio kanisa la mtu. Ni kanisa la Mungu, ni kanisa la Kristo naye ndiye kichwa. Ukweli huu unahitajika kutambuliwa kwa undani kwa kila mshirika na kila mchungaji. Kanisa la Kristo sio mahali ambapo watu hujenga ufalme wao wenyewe, mahali ambapo watu hutawala na kuwaongoza wengine kama ifanyikavyo na watu wa ulimwengu.

Kanisa la Kristo sio biashara na haliendeshwi kama biashara.

“Yesu akawaita, akawaambia, ‘Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini HAITAKUWA HIVYO KWENU; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote. Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.Kuponywa kwa Kipofu Bartimayo’. ” (Marko 10:42-45).

 

Hii iko tofauti sana na ulimwengu, ama sivyo? Kanisa la Mungu halijengwi kwa mikakati na akili nyingi za kibinadamu! Halijengwi na uwezo wa watu kitaaluma na kiutawala. Yesu alisema hivi,

nitalijenga kanisa langu” (Mathayo 16:18).

Kama tukiangalia matendo ya baadhi ya watu leo, inaonekana kabisa kwamba walishasahau kabisa kwamba Yesu alishasema hivi! Ukweli mwingine tunapaswa kukumbuka ni ufuatao,

“Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure.” (Zaburi 127:1).

Mungu huwatumia wale wanyenyekevu, wale aliowaita, aliowapa vipawa na wale watembea katika roho ile ile ya upole na huduma kama Kristo mwenyewe.

Ni hatari sana kujaribu kujenga ‘ufalme wako’ au ‘kujifanya mabwana juu ya kundi la Mungu’, kama Paulo alivyosema,

“Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo. Lakini kama mtu akijenga juu ya msingi huo, dhahabu au fedha au mawe ya thamani, au miti au majani au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa dhahiri. Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. Kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa, atapata thawabu. Kazi ya mtu ikiteketea, atapata hasara…” (1 Wakor.3:11-15).

Mtume Paulo hakuwa na maono binafsi au mkakati uliopangwa ili kuanzisha makanisa! Tunamwona kama nabii na mwalimu akiwa katika kanisa la Antiokia, alipokuwa akiomba na kufanya ibada mbele za Bwana na wengine. Alikuwa ni mtu aliyejitoa kwa Mungu, akimtumika Mungu, na kisha Roho Mtakatifu akasema, “Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia.” (Matendo 13:2). Kuna watu wachache wataishi kwa nidhamu hii ya kiroho mbele za Mungu. Wengi hukosa uvumilivu au hata kuchanganyikiwa na njia ya Mungu na mwishowe huishia kuunda njia zao za namna ya kuendeleza ufame wa Mungu.

Wengine hutaka tu nguvu na mamlaka yaletayo kule kuitwa tu kiongozi ndani ya kanisa. Lakini ufalme wa Mungu kiukweli haundelezwi na watu hao, bali na wale watu ambao wamejitoa kwa Mungu, wale wamtumikiao na kumgonja Yeye na wale wenye moyo wa hakika ndani yao kulihudumia kanisa. Ni kwa kupitia watu hao Kristo hulijenga kanisa. Watu wengi hutafuta faida zao, kama pesa, madaraka na nafasi kiutawala. Na hii ndio sababu Paulo alisema, “Walakini natumaini katika Bwana Yesu kumtuma Timotheo afike kwenu karibu, nifarijiwe na mimi, nikiijua hali yenu. Maana sina mtu mwingine mwenye nia moja nami, atakayeiangalia hali yenu kweli kweli. Maana wote wanatafuta vyao wenyewe, sivyo vya Kristo Yesu. (Wafilipi 2:19,21) – kauli ya kustaajabisha kabisa! Wahudumu wengi au wahubiri ambao Paulo aliwajua hawakuwa wakiwahudumia watu wa Mungu kweli kweli – walikuwa wakitafuta faida yao wenyewe! Ni vivyo hivyo siku hizi.

Yesu alisema kuwa mchungaji mwema hutoa maisha yake kwa ajili ya kondoo, huuondoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Ni wachungaji wangapi wana moyo huu na wanaonyesha haya maishani mwao? Japokuwa wengi katika Korintho hawakumkubali Paulo kama mtume na waliidhihaki huduma yake (2 Wakor.10:10), haikujalisha yeye, hakutafuta kuwatawala wala kuwaendesha lakini alikuwa tayari kuwapenda zaidi na kuutoa uhai wake kwa ajili yao (2 Wakor.12:15). Hakuja kama mkuu wa kijiji, au bosi (au mchawi) kwamba aamrishe watu nini cha kufanya akitarajia wamtii kama watumwa wake! Alisema, “Basi, mimi Paulo mwenyewe nawasihi kwa upole na utaratibu wa Kristo; mimi niliye mnyenyekevu nikiwapo pamoja nanyi, bali nisipokuwapo ni mwenye ujasiri kwenu.” (2 Wakor. 10:1).

Huyu ndiye mtu awatumikiaye watu wa Mungu, aliyewapenda watu wa Mungu kabisa, yaani, aliyeyalaza maisha yake kwa ajili yao. Aliwakaribia nduguze katika Kristo nao wakamkaribia. Anasema, “Hatukutafuta utukufu kwa wanadamu, wala kwenu, wala kwa wengine tulipokuwa tukiweza kuwalemea kama mitume wa Kristo, bali tulikuwa wapole katikati yenu, kama vile mlezi awatunzavyo watoto wake mwenyewe. Vivyo hivyo nasi tukiwatumaini kwa upendo mwingi, tuliona furaha kuwapa, si Injili ya Mungu tu, bali na roho zetu pia, kwa sababu mmekuwa wapendwa wetu.” (1 Wathess.2:6-8).

Kanisa linahitaji watumishi kama hawa leo. Kwa nini wachungaji wengi huweka viti vikubwa vya kifahari vya kuketi mbele ya washirika kanisani?  Wanaharibu ‘sura ya Mungu’, wanapotosha ‘tabia ya Kristo’ mbele ya washirika kwa kujiinua huku! Hawawakilishi Kristo Yesu. Yesu hakufanya hivyo alipokuwepo duniani. Je, kufanya hivyo kunawakilisha mtumishi, mtumwa wa Mungu? Je, hawajui wanatengeneza taswira – lakini si taswira inayoakisi asili ya Kristo! Wanaunda ya kujifanya wao muhimu zaidi na wako juu zaidi ya wengine; taswira ya kukandamiza na kutawala kimabavu. Wanatengeneza ile taswira ya aliye madarakani hawezi kuulizwa – kama mkuu wa kijiji au raisi – na wanatarajia kutiiwa kwa haraka katika kila amri yao – la sivyo huyo mtu anaweza afukuzwe kanisani! Wanataraji waamini wawe kama watumishi wao. Huo sio mfano wa kanisa la Bwana.

Wachungaji wengi na viongozi wanatengeneza taswira ya uongo ya Kristo na kanisa lake, na waamini wengi wanaikubali taswira hii mbaya mioyoni mwao na akilini, na hujinyenyekeza katika taswira hii ya uongozi wenye taswira danganyifu kama ni jambo fulani la kawaida mno katika kanisa la Kristo! Sio kawaida! Ni kinyume cha asili ya Kristo! Ndio, ni haki kwamba tunatakiwa kuonyeshana heshima. Hata hivyo, lakini ni huzuni na kinyume cha kanisa la Kristo kwamba watoto wa Mungu wanatakiwa kuishi katika hofu dhidi ya mchungaji kana kwamba yeye ni mchawi au mtemi wa kijiji. Kuna jambo haliko sawa hapa.

Kristo ni Kichwa cha kanisa na tunatakiwa wote kunyenyekea kwake na kuhudumu huku tukuhudumiana sisi kwa sisi.

Je? Mitume walianzisha dhehebu lolote? Waliunda mfumo wowote wa kidhehebu? Hapana, hawakufanya hivyo .Hakukuwa na mfumo huo. Mitume na wengine walihubiri habari za Yesu na wengi waliokoka katika huduma zao. Makanisa yaliyoanzishwa kupitia huduma ya kitume kiuhalisia yalitaka sana kuendelea kuwepo chini ya uangalizi na mafundisho ya mitume. Hii inaonekana kuwa kweli kabisa maana ilikuwa ni mara ya kwanza kwamba wokovu kwa njia ya Kristo ulikuwa umehubiriwa ulimwenguni na mitume waliwakilisha chanzo cha mafundisho haya. Ilikuwa wazi kwamba mitume na wote waliotenda kazi nao walitaka kuendelea kuyapa huduma makanisa yale na kuyapa mafundisho na uangalizi wa hali ya juu. Hata hivyo, hakuna mfumo wowote wa kufuatwa ulioanzishwa. Mitume walifuata maelekezo waliyopewa na Kristo. Ngoja tutazame kwenye maandiko tena maana ni ya msingi na muhimu mno,

“Yesu akawaita, akawaambia, Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini HAITAKUWA HIVYO KWENU; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote. Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.” (Marko 10:42-45).

Pamoja na kwamba ni mitume haikujalisha, huduma yao ilikuwa ni kulitazama makanisa na kuyahudumia, sio kuyatiisha na kuyatawala. Tunayaona haya tunaposoma katika kitabu cha Matendo ya Mitume. Ni kupitia mtume Paulo kanisa la Wakorintho lilianzishwa – iliwapasa kuja kwa Yesu kupitia mahubiri yake. Anasema kwamba amewazaa kupitia Injili (1Kor 4:15). Pamoja na hayo, anapokuwa akijishughulisha na matatizo yao, anatangaza kwamba hatawali imani zao,

Si kwamba tunatawala imani yenu; bali tu wasaidizi wa furaha yenu; maana kwa imani yenu mnasimama.” (2 Wakor. 1:24).

Hii ni kauli muhimu mno. Tunaona mtazamo huu kwenye nyaraka za mtume Paulo. Kwenye kanisa la Wakorintho kuna wengi ambao hawakuitambua huduma ya kitume ya Paulo, pamoja na kwamba alilijenga kanisa hakujilazimisha kukubalika kwako kisa huduma yake ya kitume, hakutafuta kuwa na utawala ndani ya kanisa eti, awafukuze ambao hawakumtambua; hakutaka kuiweka kama kiongozi au mtawala wao. Hakufanya lolote kati ya hayo. Ndio, aliwafundisha, akawasahihisha na hata kuwakaripia ilipobidi, ila tu aliyatenda haya kwa moyo wa kitumishi na alikuwa tayari kuwahudumia na kuwapenda hata mwisho.

Hiki pekee ni somo kubwa sana. Ni nadra sana kupata uwiano wenye afya njema kati ya ‘huduma ya kichungaji’ na ‘madaraka au utawala wa kichungaji’. Kwa bahati mbaya utaratibu huu huelekezwa katika kutawala na kuwa na madaraka. Ngoja tuone neno la mwisho la Mtume Petro aliloliweka vema kabisa,

“Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi.” (1Petro 5:1-3).

MWENYE MWILI AWAYE YEYOTE ASIJISIFU MBELE ZA MUNGU. UTUKUFU WA KANISA

Imeandikwa kuwa Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia vilivyodharauliwa “ili aviaibishe venye nguvu; mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu.” (1 Wakor.1:28, 29). Na hii ndivyo inavyopasa kuwa ndani ya kanisa. Kanisani si eneo la mtu kujiinua yeye mwenyewe, kujitukuza au kujionyesha uwezo wake. Kwa kuwa Mungu amesema kuwa, “Mimi ni Mungu na hilo ndilo jina langu na utukufu wangu sitampa mwingine.”(Isaya 42:8).

Katika Ufunuo sura ya kwanza, Yohana anamwona Mwana wa Mungu akiwa amesimama katikati vinara saba vya taa vya dhahabu. Vinara vile vinaliwakilisha makanisa, na Kristo ndiye mtazamo mkuu wa utukufu wa kanisa lake.

Tumegundua hapa kuwa kumbe kanisa linawakilishwa na vile vinara, na sasa kusudi hasa la hivyo vinara ni nini? Ni kubeba taa kwa ajili ya wengine ili wapate kuona. Makusudio ya vile vinara sio kuweka kama mapambo, wala vinara vile havipo pale ili kujionyesha tu, kujionyesha jinsi vilivyo pendeza. Viko pale ili kushika na kuleta nuru, na nuru ile ndiyo Yesu Kristo.

Yeye ndiye utukufu wa kanisa lake. Kwa hiyo haijalishi kama unahubiri au unaimba au kitu chochote kinachofanyika ndani ya kanisa, tunapaswa kufanya kila kitu kwa utukufu wa Mungu. Hii  inamaanisha kuwa tunapaswa kufanya kila kitu kwa namna ambayo inaonyesha tabia ya Mungu mwenyewe.

Kama nilivyosema hapo juu, wachungaji ambao wanakalia viti vikubwa vya thamani kubwa kule mbele ya washirika kanisani, hao hawamwakilishi Kristo. Watu wengine wanapojitokeza kuja mbele ya waumini na wanapoanza kuhubiri, nasikitika sana jamani eti, wanabadili sauti zao jamani! Na inatengeneza sauti rasmi zaidi. Kwa nini wanafanya hivyo? Kufanya hivyo si lazima. Inaweza kuonekana kama unatengeneza ubandia fulani, kwa kuwa watu wanaokusikiliza wanakufahamu, unakutana nao nyumbani, unakutana nao kwenye migahawa, unakutana nao kwenye maofisi mengine na sauti yako wanaifahamu, sasa watakushangaa unaigiza sauti ambayo siyo yako! Kwa nini?

Wengine wamefikia kiasi cha kufikiri kuwa kupiga kelele wakati wa kuhubiri au kurukaruka mbele ya watu inamaanisha kuwa eti, umevuviwa upako wa roho mtakatifu! Kwa nini mambo kama hayo jamani! Haipo hivyo hata siku moja. Ingawa tunapandisha sauti zetu tunapohubiri nyakati fulani fulani, wazo ya kwamba unapaswa kuhubiri kwa sauti kubwa au kurukaruka mbele ya watu ili kuwa uwaonyeshe wasikilizaji wako kuwa wewe umevuviwa na Roho Mtakatifu hilo ni wazo lisilofaa na ni uwongo mtupu. Badala yake, watu wengi au wahubiri wengi wanapiga makelele mengi kwa sauti kubwa, hii ni dalili ya mwanzo kabisa kuwa mhubiri huyo amepungukiwa na uwepo wa Roho Mtakatifu katika mahubiri yake. Tunapaswa kuhubiri kulingana na nguvu ambazo Mungu ametujalia kuwa nazo. Kuna mstari mzuri mno katika Matendo ya Mitume unaosema kuwa,

“Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu. (Matendo 4:13).

Kimsingi, kinachohitajika na kanisa sio watu wenye madigree, au hata Ph.D, au hata wale ambao wamewahi kupitia masomo kwenye vyo vya Bibilia. Kanisa linahitaji watu wanaotumia muda wao pamoja na Kristo, wakimngojea yeye, wakijifunza kutoka kwake, wakisoma neno lake na wakiomba kwake. Kanisa halimhitaji mhubiri ambaye yuko na pirikapirika akijitukuza kama vile yeye ni meneja wa shirika fulani, au anatumia muda wake mwingi akiandika andika na akitayarisha jumbe kwa ajili ya kuhuburi siku ya jumapili. Kanisa linahitaji wachungaji na wahubiri amabao watu wanaweza kuwatambuakuwa mtu huyu ametumia muda wake pamoja na Kristo, ametumia muda mbele ya Mungu, ambaye atawahubiria watu hao neno la Mungu ambalo amelipata kutokana na matokeo ya kukaa pamoja na Kristo, akimsubiria yeye na akiwa anafundishwa naye kwa kupitia neno lake! Tunahitaji mhubiri anayetafuta chakula cha kiroho toka kwa Mungu kwa nidhamu ya kiroho na kimwili pia (1Wakor.9:27) ili aweze kuwalisha watu wa Mungu chakula kinachofaa, awe na nidhamu ya kuomba, kufunga pamoja na kumngojea Mungu.

Petro na Yohana walikuwa ni watu wasio na elimu na ni watu wa kawaida kabisa! Ni jambo la ajabu gani hili! Tunahitaji watu ambao wana hiari kupitia nidhamu ya kiroho katika maisha yao, ili kwamba wanakuwa ni watu wanaomjua Mungu. Elimu ni sehemu ndogo sana, au haina thamani kwa kulinganisha na jambo kama hili. Petro hakuridhia juu ya kujishughulisha na mambo ya kiutawala / uwakili (administration). Alisema, “Sisi tutajitoa wenyewe ili kuendelea katika kuomba na kuhudumia neno.” (Matendo 6:4). Ni jambo la kusikitisha na kwa ujumla ni makosa kwetu kufikiri kuwa mtu anakuwa katika nafasi nzuri ya kuhubiri neno la Mungu anayo elimu nzuri. Kuwa na elimu si makosa, lakini elimu haipaswi kuwa ndio mbadala wa kutembea katika nidhamu ya kiroho ya maisha ambayo ndiyo inamwongoza mtu kumjua Mungu. Pia tukumbuke neno la Mungu lisemalo, “Ujuzi huleta majivuno, bali upendo hujenga.” (1 Wakor.8:1).

Mtume Petro analiweka jambo hili kwa uwazi zaidi pale anaposema,

“Mtu akisema, na aseme kama mausia ya Mungu; mtu akihudumu, na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na Mungu; ili Mungu atukuzwe katika mambo yote kwa Yesu Kristo.” (1 Petro 4:11).

Unaona? Tunapaswa kuhudumu kwa uwezo anaojaliwa na Mungu! Yote yanapaswa kutokana na neema ya Mungu, siyo kutokana na uwezo wetu wa kibinadamu, ili katika mambo yote Kristo atukuzwe!

Lipo eneo lingine ambalo watu hutukuza mwilini katika nyakati hizi za siku hizi. Ni sehemu ya uimbaji. Utawaona watu wanakuja mbele ya washirika ili kuimba, na wanasema wanafanya hivyo kwa utukufu wa Mungu! Mara nyingi sio kweli. Wanafanya hivyo kwa sababu wanajiridhisha wao wenyewe katika nafsi zao kule kuimba mbele za watu. Ukiwatazama na kusikiliza nyimbo zao utaona kuwa wanaimba vile vile kama dunia waimbavyo, hakuna tofauti – uimbaji wao, unenguaji viuno vyao, maringo ya macho yao. Wanatamashisha mbele ya watu kanisani kama vile dunia inavyofanya matamasha yao. Wanataka kujionyesha wenyewe ule uwezo wao wa kuimba, na kunengua viono vyao hadharani na kuwafurahisha watu. Utawaona wengine wanabeba CD zao ili ziimbwe kanisani, na kisha wimbo uleule unaoimba na CD na wao wanaigiliza kwa kuuimba tena wakati CD zao zinapoimba! Baada ya semina moja, mwimbaji mmoja aliniuliza kama napenda kununua CD yake! Jamani, kwa nini hivyo! Tunawezaje kuyaamini mambo kama hayo! Kwa nini tunajifanyia hila wenyewe katika kujifikia kuwa mambo haya yanafanyika ili kumpa Mungu utukufu!

Usinielewe vibaya! Ndiyo, nimewahi kuwasikia watu wakiwa wamesimama mbele ya kanisa na wanaimba kwa sababu wanampenda Mungu, na ni tendo la kuabudu na waumini wanaokuwemo katika ibada hiyo wanabarikiwa. Lakini jambo ambalo ni la kawaida siku hizi za leo (na linazidi sana), wachungaji wakiruhusu vijana kulitumia kanisa ili kujitangaza wao wenyewe pamoja na uimbaji wao. Ni nani sasa anayepaswa kuwajibika katika mambo kama haya? Wachungaji na viongozi wengi wanashindwa kutoa mafunzo ya kweli ya uongozi katika nyakti kama hizi. Kwa nini? Hawataki waonekane kuwa ni watu wasiojulikana na jamii?

Tulikuwa na semina fulani ya siku mbili na wanachuo, semina iliyoandaliwa na Huduma ya Shirika la kikrisho la wanachuo. Kiongozi wao aliniambia, ‘Kama tusingewaruhusu wanachuo kuja mbele kuimba, basi wasingekuja kuhudhuria semina.’ Hayo ni maneno yake yeye mwenyewe! Uimbaji ulikuwa mzuri nami niliufurahia lakini kuna jambo pale ambalo sio sahihi iwapo tutaiachilia bali hiyo kuwa ndiyo tabia yetu.

Mambo ni mabaya zaidi kwa nyakati hizi tulizo nazo, kwa sababu wachungaji wananyenyekea kwa vijana, kuimba na kucheza (kusiko) na kiasi katika mikutano ya hadhara. Ni mfano mmojawapo mbaya wa kujitukuza katika mwili ambao tunauona nyakati hizi. Waimbaji wanajitokeza mbele ya washirika wakiwa katika kundi kubwa na wanacheza kwa unenguaji mbele ya waumini. Watu hawa wanautumia muda wao mwingi wakifanyia mazoezi ya aina hiyo ya unenguaji. Je, wanautumia muda wa aina hiyohiyo ya mazoezi kwa kuomba ili kwamba Mungu aweze kuleta neno lake na kuwabariki watu wake katika mikutano hiyo? Bila shaka unajua jibu la jambo hili! Eti, wao wenyewe wanasema kuwa wanayafanya hayo yote kwa utukufu wa Mungu. Ni wazi kabisa kuwa hii sio kweli kwa mambo yote niliyoyashuhudia mwenyewe kwa kuyaona.

Huo ni mfano mwingine wa wazi unaoonyesha maana nyingine ya kujitukuza katika mwili. Wanacheza kwa sababu wanafurahia kuigiza kutoka ulimwenguni na kuyaingiza kama tamasha ndani ya kanisa. Basi, kwa ujumla ni makosa kufikiri kuwa watu hao wanafanya hivyo kwa kulifaidisha kanisa! Wananengua minenguo yao kwa muda hata wa dakika 10 na zaidi huku wakitokwa na majasho kwenye miili yao na kisha wanapomaliza kucheza hivyo wanaenda kukaa wamejichosha. Je, hilo ndilo kanisa mpendwa! Je, mifumo kama hii ndiyo inamwakilisha Kristo kwa waumini wake? Je, na wale watu wanaokuwa ameketi kanisani wakiwaangalia hao wanenguaji, huwa wanafikiri nini hasa wakati huo? Je, hayo yanawafanya  wanafikiri juu ya utakatifu wa Bwana? Je, hiyo inawaongoza kumpenda Kristo zaidi? Je, hii inaliinua kanisa? Kwa vyovyote matukio hayo hayawezi kulijenga kanisa. Matokeo ya vituko hivyo vyote vinavyoonyeshwa humo kanisani vinasaidia tu kuchochea matamanio ya kimwili.

Lakini pamoja na hayo yote bado wachungaji na viongozi wa kanisa hawana ujasiri wa kuwaelekeza vijana wao kulingana na neno la Mungu kwa namna ambayo itawasababishia wao kukua katika Kristo wakiwa ni wakristo walioimarika. Badala yake wao wanayaruhusu mambo kama hayo yatokee, yaendelee kufanyika kanisani mara zote – kisha hatimaye wanakuja kushangaa kwa nini tendo la dhambi ya uzinzi inakuwa ni tatizo kubwa la kanisa kati ya vijana katika makanisa!

Tulikuwa na mkutano wa siku tatu huko kwenye milima ya Udzungwa mkoa wa Iringa. Kila mara mwishoni mwa mkutano watu huimba na kusalimiana pale nje ya mlango wa kanisa kama ilivyo desturi ya mila za kanisa huko. Walikuwa wamekoka moto nje ya kanisa kwa sababu ni inchi ya baridi. Watu huota moto huo, basi watu waliendelea kucheza na kuimba kwa nguvu wakiuzunguka moto ule, na shughuli hii iliendelea kwa muda wa dakika kama 15 hivi. Kisha nikamweleza mzee wa kanisa kuwa angefunga uchezaji ule sasa vinginevyo vijana wale wangejiingiza kwenye matatizo. Alinielewa nilivyosema na mara moja akasema, “Tulishawahi kupata matatizo!” Mwenendo kama huu hauwaongozi vijana wa kiume na wa kike kwenda misituni kuomba maombi! Mwenendo huo unasababisha dhambi tu!

Je, hatuwapendi vijana wetu! Kwa nini kunaonekana kuna upungufu au kukosekana kabisa kwa mafundisho ya Kimungu na miongozo katika makanisa!

Nafahamu kuwa mfalme Daudi alicheza walipolirudisha sanduku la Bwana Jerusalem, lakini ebu tusijidanganye wenyewe kwamba eti, kinachotokea leo makanisani kinaweza kulinganishwa kwa namna yoyote ile na alichokifanya Daudi. Daudi alikuwa haleti matamasha ya kidunia kwa watu wa Mungu kila wiki!

Jambo hili linafanana pia na mambo ya muziki na vikuza sauti vya muziki makanisani. Vijana wanaruhusiwa kutawala uimbaji na kuabudu na wanafanya hivyo kwa sauti kubwa ya juu kwa kutumia vyombo vya muziki vilivyokuzwa sauti kubwa hata inawafanya washirika wenyewe wasisikie hata sauti yao wenyewe. Ndiyo vijana wanapenda kutumia fursa kama hizo kuigiza ulimwengu na kutamashisha hivyo hivyo makanisani. Sikiliza hii nayo! Nilikuwa katika kanisa fulani huko Dar Es Salaam, ambapo mchungaji alimwambia yule anayesimamia muziki wa kwaya ili ajaribu kupunguza sauti ya vyombo maana ilikuwa juu mmno. Japo kuwa mchungaji huyu alimwomba kijana yule mara mbili zote kupunguza sauti ile lakini kijana yule hakupunguza sauti, aliendelea kuburudisha kwa sauti ya juu ya vyombo vile. Hivyo mchungaji yule alilazimika kwenda kwenye eneo la vyombo vya muziki na kupunguza sauti ya vyombo vile yeye mwenyewe!

Ndiyo, hata mimi nawapenda sana vijana na kwa ujumla ni kutokana na kule kuwapenda vijana kiasi kwamba inaniumiza mimi sana kuona wachungaji wengi wanawaharibu vijana kiroho.

Unijalie niseme kitu zaidi. Unafikiri ingetokea nini kama mwislamu kijana angependa kuanzisha mambo ya kukuza sauti kwa ajili ya kuimbia msikitini mwao kama vile kijana huyo angetamani kuleta bendi kwa ajili ya kuabudu msikitini humu kwa kutumia vyombo vya muziki vya umeme?! Jibu liko wazi, liko wazi kabisa! Kulingana na uaminifu walionao kwa lile wanaloliamini, basi vijana wao wa kiislamu hata hawawezi kupata muda wakufikiria kufanya jambo kama hili. Ikiwa ingetokea wakapeleka ombi lao kama hili kwa viongozi wao wa msikitini, je, wasingeweza kukemewa kwa ukali!

Kama leo utaenda kuingia msikitini, hutakipata kitu chochote kinavyo kuburudisha wewe kama tamasha humo, au kuvutia mwili wako. Wao wanakaza na kuonyesha unyenyekevu wao kwa kile wanachokiamini. Niacheni niseme hili kwa masikitiko makubwa kuona waislamu wanaonyesha heshima yao kwa kile wanachokiamini kuliko wachungaji wengi wafanyavyo kwa Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ili tupate kuwavutia watu makanisani mwetu tunamuuza Mungu wetu kwa urahisi. Je, hatuna hata chembe ya aibu kweli pale tunapoacha kumheshimu Mungu kwa kuyaruhusu mambo kama haya yatokee makanisani?

Labda unashtushwa na maneno hayo, lakini hili si wazo langu tu – Ilikuwa ni Mungu mwenyewe alisema kuhusu watu wake kupitia nabii Jeremia, “Je! Taifa wamebadili miungu yao, ingawa siyo miungu? Lakini watu wangu wameubadili utukufu wao kwa ajili ya kitu kisichofaidia. Enyi mbingu, staajabuni kwa ajili ya jambo hili, mkaogope sana, na kuwa ukiwa sana, asema Bwana. Kwa maana watu wangu hawa wametenda maovu mawili; wameniacha mimi, niliye chemchemi ya maji ya uzima, wamejichimbia mabirika, mabirika yavujayo, yasiyoweza kuweka maji.” (Jeremia 2:11-13).

Hapa Mungu anashangaa kuona kuwa mataifa mengine yanaheshimu miungu yao – ni watu hawa Wake pekee ndio wanaomwacha na kufuata mifumo mingine ya kuabudu!

Niliwahi kusema kuwa kanisa sio biashara! Dhambi nyingine ambayo imeenea sana ambayo inalazimisha na kuwasukuma watu kutoa vikumi na matoleo kanisani huku wakitishwa kwa laana au kufukuzwa kanisani iwapo hawafanyi vile kama mchungaji wao alivyowaamuru kufanya. Jambo kama hili kwa hakika halitukuzi jina la Bwana na wala haliwakilishi kabisa kanisa lake! Kusema kwa ujumla wake, haimhusu mtu yoyote yule kujua ni kiasi gani unatoa katika matoleo yako kwa wiki nzima au mwezi nzima, kwa sababu matoleo ni kati yako na Mungu. Basi! Kanisa halina haki yoyote kukuuliza wewe kiasi gani cha mshahara unapata, kadhalika haina haki ya kutaka kujua ni kiasi gani cha fedha unatoa. Mambo kama haya yote yanaiingiza Injili ya Bwana wetu Yesu katika jina baya. Tunaugeuza utukufu wa Mungu kuwa ni fedheha tupu!

Yesu Kristo ndiye anayesimama katikati ya kanisa ambaye macho yake yanawaka kama mwali wa moto akiangalia moja kwa moja kwenye hamasa ya kweli na hali ya mioyo huku akiona kila jambo lililofichika. Na ndiye anayepima thamani halisi ya kile anachokiona kwetu. Na mara zote hayapimi mambo kama tufanyavyo wanadamu! Analiambia kanisa mojawapo, wasipotubu atakiondoa kinara, ambayo inamaanisha kuwa kanisa hilo halitakuwa tena kanisa lake (Ufunuo 2:5). Kanisa lingine ambalo lenyewe lilijiona kuwa ni tajiri, yeye analiita kanisa hilo kuwa ni nyonge, na ni fukara, na yuko tayari kulitema kanisa hilo kutoka katika kinywa chake (Ufunuo 3:15-17). Na hivyo ndivyo ilivyo hata leo. Washirika wanakutana mahala pamoja kwenye jengo kisha wanajiita wenyewe kuwa ni kanisa la Kikristo, lakini Kristo halitambui kuwa ni kanisa lake! Hawang’ali kwa utukufu wake! Wamebadilisha utukufu wa Mungu (ambao ndiyo tabia yake Mungu) na jambo jingine linalotokana na mwanadamu, jambo ambalo sasa linamtukuza mwanadamu na kazi zake tu!

Je unaweza kuiona sura halisi ya jambo hili hapa? Tukutanikapo pamoja basi mkazo wetu uwe ni Kristo. Anapaswa kukuzwa na kutukuzwa katikati ya kusanyiko letu. Haipaswi kuwepo na wivu au mashindano wala kusiwepo na kujiridhisha binafsi. Hatuji kukusanyika ili kukidhi furaha yetu wenyewe, yaani kujifurahisha wenyewe au kujipendeza wenyewe. Tunakuja ili kumpatia sifa na kumtukuza kisha kumwacha Mungu aongee ndani ya mioyo yetu! Tunakuja kumheshimu na kumwonyesha heshima yetu. Kila tukifanyacho kinapaswa kifanyike kwa utukufu wake peke yake, na wala isiwe kwa ajili ya utukufu wetu sisi. Kila jambo linalosemwa na kufanyika liwe ni la kumfurahisha yeye na wala sio sisi!

Ni Kristo ndiyo anayepaswa kudhihirishwa na kuonekana katikati yetu. Neema yake inayofanya kazi kwa kila mshirika ndiyo kwa hakika inayolibariki kanisa zima. Kanisani sio mahala pa kujisifu au kujionyesha uwezo wetu wa kupiga vyombo, kuimba, kucheza na hata kuhubiri! Tunapaswa kuwa na mioyo inayoabudu ambayo inainama mbele zake. Wala tusitafute kumnyang’anya Mungu utukufu wake kwa kuwafanya watu waanze kutupongeza  kwa kile tunachokifanya. Heshima yetu kwa Mungu mwokozi wetu ijaze mioyoni mwetu, na ndiye anayepaswa kusujudiwa nasi kiasi kwamba hakuna mwili unaomtukuza mbele ya uwepo wake. Anasimama katikati ya kanisa lake! Je, kwa kweli tunautaka utukufu wake pamoja na uwepo wake? Kama jibu ni ndiyo, hii inamaanisha ni kifo cha aina zote za matangazo hayo na kujinadi huko.

Tunasoma haya katika kitabu cha matendo ya mitume, “Na kwa mikono ya mitume zikafanyika ishara na maajabu mengi katika watu; nao wote walikuwako kwa nia moja katika ukumbi wa Sulemani; na katika wote wengine hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao; ila watu waliwaadhimisha; walioamini wakazidi kuongezeka kwa Bwana, wengi, wanaume na wanawake.” (Matendo 5:12-14).

Je, unakiona kile tulichonacho hapa? Washirika wanapokusanyika pamoja, hapakuwepo hata mtu mmoja aliyethubutu kujiunga nao! Kwa nini? Je, ni kwa sababu Wakristo walijifanya kuwa ni watu muhimu na wenye kuwalaani wale wasioamini? Hapana! Je, ni kwa sababu Wakristo walikuwa ni wanafiki ambapo walijifanya kuwa ni watakatifu kuliko wengineo? Hapana! Watu wengine waliwatukuza! Sasa, kwa nini basi hata mmoja hakuthubutu kujiunga pamoja nao walipokuwa wakikutanika? Hii ni kwa sababubu watu hao walipokuwa wakikusanyika mkazo wao wote na upendo wao wote, na ibada yao ilielekezwa kwa Mungu tu ambaye amewaokoa kutoka katika dhambi zao! Hivyo upendo wao, ibada yao kuabudu kwao na heshima yao kwa Mungu ilijaza mioyo yao na ilidhihirishwa kwa uwazi pale walipokutanika pamoja.  Walikuwa wamekazia katika ibada yao kwa Bwana Mungu wao, kiasi kwamba kama wewe bado hujabadilishwa kwa wokovu huo huo, ungefahamu kuwa upo nje ya kile kilichokuwa kinajaza mioyo ya waumini. Mara moja ungetambua kuwa humjui Mungu wao, na kuwa nawe usingekuwa na njia nyingine ya kuabudu Mungu kama wanavyofanya wao! Ungetambua kuwa kile kilichokuwa kikiwasukuma wao kuomba, kuabudu kwa namna ya mtindo huo, haina nafasi kabisa katika maisha yako!

Ungethubutu tu kwenda pale iwapo tu kama ungekuwa na jambo maalum linalo kuvutia ili kubadilishwa na wokovu huu ambao umewabadilisha wengine wengi! Ibada yao kwa Mungu ilikuwa ni kamilifu kiasi kwamba ni kwa Mungu mwenyewe ndiko nyimbo zao, maombi yao na kuhubiri kwao walimwelekezea. Na kutokana na sababu hii ndiyo maana watu wengine walitambua ni waumini wa dhati, na hiyo waliwaadhimisha. Je, kutokana na hayo kanisa liliendelea kusinyaa? Hapana! Inasemwa kuwa waumini wengi waliongezeka kwa Bwana na makundi makubwa ya wanaume na wanawake!

Watu wengi wameacha hali hiyo ya kanisa la kwanza siku hizi za leo.

Nilinukuu kutoka katika kitabu cha Yeremia ambapo Mungu analalamika kuwa ni watu wake tu ambao wamemwacha ili kuabudu mambo mengine. Katika sura ileile ya neno la Mungu, Mungu anasema kuwa, “Makuhani hawakusema, Yuko wapi Bwana? Wala wana-sheria hawakunijua; wachungaji nao waliniasi, nao manabii walitoa unabii kwa Baali, wakafuata mambo yasiyofaidia kitu.” (Yeremia 2:8).

Unaona? Sasa, badala ya kuhubiri ‘Yesu Kristo, naye amesulibiwa’ na ‘neno la msalaba’, badala ya kutambua kutokuwepo kwa uwepo halisi na nguvu ya Bwana katika makanisa yetu, badala ya kutambua hitaji letu la kumhitaji yeye kwa kuliita jina lake, kuomba kwake yeye, na kumngojea yeye ili kwamba yeye apate kufanya kazi katika maisha yetu na katikati ya kanisa, sasa viongozi wanageukia kwenye namna nyingine nyepesi za mtindo wa kuwavutia watu kanisani. Na matokeo ya hayo yote ni kwamba wachungaji, viongozi, manabii, maaskofu na mitume wa aina hiyo wanaohubiri kutoka kwenye Biblia hawamjui Mungu kweli kweli.

Wachungaji wanafurahia kuwaruhusu vijana kusherehesha watu kanisani, kwa nyimbo zao nakucheza kwao. Wachungaji wengi wanapenda kuhubiri juu ya uamsho, upako, na nguvu au wanahubiri kuhusu mafanikio na mapesa, lakini mengi ya mafundisho ya aina hii hayana maana yoyote – ‘Hawa ni visima visivyo na maji, na mawingu yachukuliwayo na tufani”. Kwenye mahubiri yao wanawaahidi watu mambo mengi lakini ukiuangalia mwisho wake unagundua kuwa hakuna lolote wanalopokea watu – ni maneno matupu ambayo yanawahamasisha watu kwa muda mfupi tu, lakini wamenyimwa neno la Mungu katika maisha yao. Hapa tena Mungu analalamika zaidi dhidi ya watu wake kwenye Yeremia,

Jambo la ajabu, la kuchukiza, limetokea katika nchi hii! Manabii wanatabiri uongo, na makuhani wanatawala kwa msaada wa hao; na watu wangu wanapenda mambo yawe hivyo. Nanyi mtafanya nini mwisho wake? (Yeremia 5:30-31).

Siku hizi viongozi wengi hawahubiri tena neno la Mungu. Wanahubiri mambo yanayo wafurahisha watu. Tena tunayo maeelezo yenye kuhuzunisha sana ambapo Mungu anasema kuwa, “na watu wangu wanapenda mambo yawe hivyo!’ Na ndivyo ilivyo leo katika makanisa mengi. Watu wanapenda na kuridhia kushereheshwa makanisani; wanapenda kusikia ahadi kubwa kubwa zinazohusu maisha yao zinazotolewa na wahubiri. Na sasa mwishowe watafanya nini? Na matokeo ya mambo kama hayo itakuwa nini?

Mtume Yohana alimwona mwanakondoo alionekana kana kwamba amechinjwa, katikati ya kiti cha enzi cha Mungu. (Ufunuo 5:6).

Je, tunapenda Yesu Kristo asimame katikati yetu? Je, tunampatia nafasi ndani ya mioyo yetu na katika maisha yetu, katika kanisa letu? Yeye anasimama kama mwanakondoo aliychinjwa; yeye ambaye hajitafutii mambo yake mwenyewe lakini badala yake yeye huyaweka chini maisha yake kwa ajili ya kanisa. Nasi tunapaswa kufanya vilevile! Yeye apendaye maisha yake atayapoteza, lakini yeye apotezaye maisha yake atayapata tena! Kama wewe unatafuta madaraka na vyeo kanisani na kuonekana na watu wengine katika yale unayoyafanya, basi hapo utapoteza maisha yako. Hapo utakuwa humtumikii Bwana Mungu bali unajitumikisha mwenyewe tu, unajipendeza mwenyewe tu. Ikiwa makanisa leo yanataka yahesabiwe kuwa ni kanisa lakeYesu, basi hapo makanisa mengi yatapaswa yafanye mageuzi kwa kiasi kikubwa – ambapo pasipo mashaka yoyote mageuzi hayo yatahusisha na kutubu!

Mungu ageuzie mioyo yetu kwake, nyakati hizi ili kwamba apate utukufu ambao ni stahiki ya jina lake! Kama Daudi alivyoomba, “Ee Mungu, uturudishe, Uangazishe uso wako nasi tutaokoka.”  (Zaburi 80:3).

HEKALU LA MUNGU.  ‘NYUMBA’ YA MUNGU NA ‘MADHABAHU’ NI NINI?

Hebu niseme neno linalowasumbua baadhi ya watu. Sasa sisi tupo katika Agano Jipya.  Mambo yote ya nje yahusuyo sheria ya Musa yalitolewa kwetu ili kutufundisha sisi kuhusu Yesu, kuhusu kifo chake, dhabihu na ufufuo wake kuwa umekamilishwa. Sasa ni kwamba Kristo amekufa na amefufuka tena, hakuna haja tena ya vielelezo vya nje vya uhalisia wa kiroho kuendelea. Kwa kweli vielelezo vya kiinje vimeondolewa kwa sababu ya kile kilichokuwa kikielezea kimekwisha timilika kwa kuja kwake Kristo Yesu. Hivyo ndivyo kitabu cha Waebrania kinavyotufundisha kwa uwazi kabisa (Waebr.

7:11,12,19,22; 8:3-8; 9:11, 24;10:1). Halipo tena hema! Sisi sasa, ambao ni watakatifu, ndio makazi, jengo na hema ambamo Mungu anaishi kwa Roho. (Kwa hiyo Agano la Kale ni mwalimu wa kutuleta kwa Yesu.)

“…bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu…Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho. (Waefeso 2:19-22).

“Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.” (1 Wakor.3:17).

Kwa hiyo kama kuna mtu yeyote atasema kuwa jengo au chumba ambacho Wakristo hukutanika siku za jumapili kuwa hiyo ni ‘nyumba ya Mungu’ au akisema “Karibuni kwenye nyumba ya Mungu,” basi watu hao watakuwa wanaupotosha ukweli mkuu wa Agano Jipya. Ni makosa na watakuwa wanawafundisha watu wa Mungu kimakosa – wanawafanya wafikiri kuwa ukweli huu wenye nguvu za kiroho unahusu tu mambo ya nje – kama vile matofali na chokaa. Sisi tu kanisa. Sisi ni hekalu la Mungu kiroho. Mahali pale wanapokutanika watu wa Mungu hapo ndipo kanisa la Mungu lilipo – hata kama mahali hapo ni chini ya mti! Katika Agano Jipya makanisa mengi walikutanika kwenye nyumba za waumini (Warumi 16:5; 1 Wakor.16:9; Wakolosai 4:15; Filemon 2). Lakini nyumba ya Mungu ni kanisa, na kanisa ni watu wa Mungu

“Lakini nikikawia, upate kujua jinsi iwapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya Mungu, iliyo kanisa la Mungu aliye hai, nguzo na msingi wa kweli.” (1 Timotheo 3:15).

Maana halisia ya neno ‘Kanisa’ imekuwa haieleweki kutokana na tafsiri katika lugha ya asilia ya kigiriki, ambayo hata mtume Paulo ameitumia katika kuandika nyaraka zake. Neno hilo (yaani ‘kanisa’) ni ‘ekklesia’ – hii inamaanisha ni watu ‘walioitwa’. Inatumika kwa kikundi cha watu waliokusanyika mahali pamoja kwa kusudi maalum, kwa kawaida ni kwa kusudi la kidini. Jambo muhimu kwetu kutambua hapa ni kwamba neno ‘kanisa’ kinahusu watu, na wala kamwe si majengo yanayotumiwa na watu kukutania.

Hakuna tena mwendelezo wa kuhani wala ukuhani kati yetu sisi na Mungu – kwa sababu tumefanywa kuwa ukuhani mtakatifu, ukuhani wa kifalme (1 Petro 2:5-9), na Yesu ndiye kuhani wetu mkuu (Waebr4:14). Na yeye pekee ndiye mpatanishi kati ya mwanadamu na Mungu. (1 Timotheo 2:5). Kwa hapa duniani sisi ambao ni watu wa Mungu, tu hekalu la Mungu. Kupitia Yesu Kristo tunayo nafasi ya kuingia katika uwepo wa Mungu, katika patakatifu pa patakatifu mbinguni kila wakati (Waebr.4:16,10:19).

(Katika Agano la kale makuhani walivaa nguo maalum kwa ajili ya kazi yao ya ukuhani. Nguo hizo pia zilikuwa kama alama kwao ya kuwekwa wakfu kwa Mungu na katika kazi yao kama makuhani – walivaa mavazi “matakatifu”. Katika Agano Jipya tumetakaswa si kwa damu ya mafahali na mbuzi, ila tumetakaswa kwa damu ya Yesu na kufanywa kuwa ukuhani mtakatifu. Kwa hiyo katika Agano Jipya hatusomi mchungaji au mtume kuvaa mavazi yanayomtofautisha yeye na waumini wengine – na  wala hii haipaswi kuwa desturi yetu! Kuvaa mavazi hayo huharibu au kuleta mchanganyiko wa kazi ya Yesu aliyoifanya pale Kalvari, ambapo kwa damu yake ametutakasa sisi sote na kutuleta katika uwepo wa Mungu; na wala hatuhitaji Kuhani kusimama kwa ajili yetu. Ili kujali au kuheshimu kile ambacho Yesu amekifanya na ili kuishikilia kweli ya msalaba, hakuna hata mmoja anayepaswa kuvaa joho au utepe kana kwamba ni mapenzi ya Mungu au chaguo la Mungu kwa ajili ya kanisa!)

Kwa mtu yeyote yule kudai kuwa jengo ndio nyumba ya Mungu, hilo ni kosa kabisa. Kwa mtu yeyote yule kudai kuwa bado ipo madhabahu hapa duniani ambayo inawapasa Wakristo kuiendea, huo ni udanganyifu kwa ujumla wake. Kusema au kudai kuwa kuna aina fulani ya madhabahu inayoonekana ambapo Wakristo wanakutana pamoja huko ni kulikataa Agano Jipya na kazi ya Yesu msalabani.

Katika Mathayo 5:23-24 Yesu anazungumza juu ya kuleta sadaka /zawadi zao madhabahuni. Lakini hapo yeye alikuwa anawaambia Wayahudi ambao bado walikuwa wakiishi katika sheria. Ni sawasawa vilevile kama Yesu alivyomweleza mtu yule aliyeponywa ugonjwa wa ukoma kwamba aende akajionyeshe kwa kuhani wake na akatoe sadaka ya njiwa wawili. Hivyo Yesu anazungumza kwa wayahudi katika Matayo 5. Anazungumza katika mantiki ya mfumo wao waliouelewa na ambao ndio walikuwa wakiishi wakati ule. Na kama ilivyo leo kwa mtu ambaye ameponywa kwa ukoma haimhitaji yeye leo aende Yerusalem kumtafuta kuhani wa kiyahudi ili akatoe sadaka yake ya njiwa wawili kwa alili ya uponyaji wake, basi twaona kuwa siku za leo hatuna madhabahu zinazoonekana, ambazo tunaziendea.

Kuwafundisha watu leo jambo kama hilo ni kuwadanganya na kuwanyang’anya maarifa ya Mungu. Ndiyo, kulikuwepo na Wayahudi ambao waliendelea kutoa matoleo kwenye madhabahu kwa mujibu wa sheria za Musa. Mwandishi anasema kwamba wao waliokuwa wakitumika katika madhabahu za aina hizo, hawakuwa na haki ya kuvila vitu vitokanavyo na madhabahu hizo ambazo waamini wameshiriki katika hilo.

“Tuna madhabahu ambayo wale waihudumiao ile hema hawana ruhusa kula vitu vyake. Maana wanyama wale ambao damu yao huletwa ndani ya patakatifu na kuhani mkuu kwa ajili ya dhambi, viwiliwili vyao huteketezwa nje ya kambi. Kwa ajili hii Yesu naye, ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa nje ya lango. Basi na tutoke tumwendee nje ya kambi, tukichukua shutumu lake. Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao. Basi, kwa njia yake yeye, na tumpe Mungu dhabihu ya sifa daima, yaani, tunda la midomo iliungamayo jina lake.  (waebr 13:10-15).

Kimsingi, anachokisema mwandishi hapa ni kuwa waumini hawahusiki na lolote lihusulo vitu vya kiinje, wala taratibu za ibada za sheria za Musa. Paulo anasema kwamba tunapaswa kwenda nje ya kambi, ambayo inamaanisha hatuna lolote la kufanya kwa madhabahu na mahekalu ya sheria za kiyahudi ambapo dhabihu zilikuwa zikifanyika. Yesu tayari alishatuondoa mbali na mambo kama hayo kwa kifo chake pale msalabani. Nasi tunapaswa sasa kumfuata Yeye nje ya kambi. Hii nje ya kambi inamaanisha nini basi? Katika mstari ufuatao unaelezwa, “hapa hatuna mji udumuo, bali tunautafuta ule utakao kuja.” Mahali pale tulipoletwa si pale kwenye madhabahu ya dunia hii, bali ni pale kwenye uhalisia wa kiroho wa mbinguni, ndiyo maana Paulo anasema kuwa uwenyeji wetu upo mbinguni (Wafilipi 3:20). Tumezaliwa kutoka juu. Ndiyo sababu Paulo anatangaza kuwa Yerusalem ambao uko juu ni mama wa sisi sote! (Wagal.4:26). Mungu ametuinua sisi juu pamoja na mwanae Yesu Kristo ili kwamba tupate kuketi pamoja naye mahala mbinguni. Hapo ndipo mahala ambapo Mungu ametubarikia sote kwa baraka za kimbinguni (Waefeso 1:3; 2:6).

Kwa kule kutubatiza kwake kwa Roho Mtakatifu, Mungu ametufanya sisi tuwe ni watu wa kiroho (Yohana 4:24; 1 Wakor. 2:15; Wagalatia 6:1). Mungu hutufanya sisi kuwa ni nyumba yake ya kiroho tupate kutoa dhabihu za kiroho (1 Petro 2:5). Sisi tu hekalu la Mungu, ni maskani ya kuishi Mungu (Waefeso 2:22). Nasi tunao uweza wa kupaingia kwenye uwepo wake wakati wowote (Waebrania 10:19). Hatuhitaji kutumia masanamu au picha za kidini ili kutusaidia kuomba au kutusaidia kufikiria mambo ya kiroho. Kufanya hivyo ni kuabudu sanamu. Hakuna jengo la hekalu lililojengwa kwa matofali ambalo litaitwa ni ‘nyumba’ ya Mungu. Huo ni uongo na ni fikra za kiushirikina. Halikadhalika hakuna madhabu inayoonekana kwa nje wala hakuna meza ya mkate wa wonyesho au madhabahu ya uvumba au kitu kingine chochote cha aina hiyo. Basi sasa, kuunda mambo ya aina hiyo ni kutokuielewa Injili na Agano Jipya – ni kuunda dini ya uongo inayoturudisha nyuma kwenye Agano la Kale ambalo mtume Paulo anatuonya kwa nguvu sana tusifanye katika nyaraka zake kwa Wagalatia.

Lakini, ebu turudi kwenye mstari uliopo kwenye Waebrania 13, ambapo mwandishi anasema kuwa, “Tuna madhabahu ambayo wale waihudumiayo ile hema hawana ruhusa ya kula vitu vyake.” Hapa mwandishi anasema kuwa tunayo madhabahu ambayo hao waifuatayo sheria ya Musa (madhabahu ya nje) hawana ruhusa ya kula vitu vyake. Mwandishi anaiongelea madhabahu kama ni mahali tunapotumia kula, na hii ni kweli halisi, ni kweli kabisa. Sikiliza  ukweli mkuu ambao Paulo anatukumbusha,

“Hamjui ya kuwa wale wazifanyao kazi za hekaluni hula katika vitu vya hekalu, na wale waihudumiao madhabahu huwa na fungu lao katika vitu vya madhabahu?” (1 Wakor. 9:13).

Unaona, wanyama walitolewa dhabihu juu ya madhabahu zile na makuhani walikula sehemu ya dhabihu ile. Walikuwa ni washirika wa madhabahu ile. Hicho ndicho mwandishi anacho kiongelea hapo. Katika kitabu cha Kutoka, Mungu aliwaagiza makuhani yafuatyo,

“Nao watakula vile vitu ambavyo upatanisho ulifanywa kwa hivyo, ili kuwaweka kwa kazi takatifu na kuwatakasa; lakini mgeni asivile, maana, ni vitu vitakatifu.” (Kutoka 29:33).

Tunajua Waisraeli walitakiwa kula mwanakondoo wa Pasaka walipotoka Misri. Lakini sasa Paulo anatangaza,

“Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo.” (1 Wakor.5:7).

Basi ebu niambie, ni madhabahu gani wewe unaitumia kuila dhabihu yake, na kitu gani unachokula! Jibu la swali hili lipo wazi. Yesu Kristo ndiye aliyetolewa awe dhabihu ya dhambi zetu, nasi tuwashirika naye, tunamla yeye, kama Yesu mwenyewe alivyosema katika Injili ya Yohana sura ya 6,

“Basi Yesu akawaambia, Amini amini nawaambieni, msipoula mwili wake mwana wa adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu, anao uzima wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho, maana mwili wangu ni chakula cha kweli na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Yeye aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu, hukaa ndani yangu nami hukaa ndani yake” (Yoh. 6:53-56). Sasa wengi wa wanafunzi wake hawakuelewa na maneno haya ya Yesu, waliliona jambo hilo ni gumu sana kulielewa hata wakarudi nyuma katika kumfuata Yesu.

Tunajua kuwa Yesu hapo alikuwa haongelei juu ya mwili na damu hii ya nyama kwa sababu damu na nyama haviwezi kuurithi ufalme wa Mungu. Ninaamini maneno haya ya Yesu yanaelezea ushirika wetu wa kiroho pamoja na yeye. Alikufa ili tushiriki maisha yake. Jambo hili limeelezwa kwa wazi kabisa na baadhi ya waandishi wengineo katika Agano Jipya: “tumefanywa kuwa washirika wake Yesu. . . Kristo ambaye ndiye uzima wetu. . .yeye aliyeunganishwa na Bwana ni Roho moja. . . ili kwamba upate kufanyika kuwa mshirika wa tabia ya kiUngu.” (Waebrania 3:4; Wakolosai 3:4; 1 Wakor 6:17; 2 Petro 1:4). Maisha haya ya kiroho ya kuwa na Yesu Krist ndani yetu (Wakolosai 1:27) yanaimarishwa na ushirika wetu pamoja na Bwana. Akizungumzia juu ya mkate na kikombe tukinywecho, mtume Paulo anasema, “Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate ni mmoja na sisi tulio wengi tu mwili mmoja, kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja (1Wakor. 10:16,17). Damu na mwili wake Yesu vyanena juu ya uhai wake. Inawakilisha uhai wake. Usifananishe na kunywa damu ya kimwili. Jambo hili halipo hapa. Kinachomaanishwa hapa ni kufanywa mshirika wa uhai wake, wa jinsi alivyo.

Ushirika huu pamoja na Yesu ni lazima liwe ni jambo linalofanyika kila siku katika maisha yetu. Ni kama vile yunavyohitaji chakula na maji ili kusalimika kimwili, vivyo hivyo tunahitaji kuwa na muda kushirikiana pamoja Kristo, katika maombi, katika kumwabudu, katika upendo, katika mahusiano pamoja naye, ili kwamba tupate kusalimika kiroho, ili kwamba maisha yetu yapate kuimarishwa kiroho. Sikiliza Yohana asemavyo, “Tukisema ya kwamba twashirikiana naye tena tukienenda gizani twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli; bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu mwana wake yatusafisha dhambi zote. (1 Yoh. 1:6,7). Unaona, ni pale tu tunaposhirikiana na Yesu Kristo ndipo tunapoweza kutembea katika nuru -katika ushirika huo damu yake Yesu inatenda kazi katika kututunza sisi tuwe safi kutokana na dhambi. Kushiriki kwa mkate na kikombe chake kunawakilisha ushirika wake kiroho ambao inatupasa kushiriki mara zote katika maisha yetu. Yohana anasema katika sura ile ile, “Kweli ushirika wetu ni pamoja na Baba na Mwana”, na Paulo anatangaza kweli hiyohiyo katika 1Wakor 1:9, “Mungu ni mwaminifu ambaye muliitwa na yeye muingie katika ushirika wa mwawe, Yesu Kristo Bwana wetu.”

Ni katika ushirika huu tunabadilishwa na kufanywa upya katika roho ya nia zetu, kama Paulo asemavyo, “Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho.” (2 Wakor 3:18). Tunabadilishwa tufanane naye, kadiri tunavyo shirikiana naye, na ‘tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo’ – hii ina maana kwamba tunapaswa kumtafakari Yesu, kumwangalia Yesu, kumpenda Yesu, kuchukua muda tuwe pamoja na Yesu, na kupitia hayo kugeuzwa, kadiri tunavyojitoa wenyewe kwake kwa imani, utii na upendo. Na kwa mfano upi ambao tunabadilishwa? Tunabadilishwa kwa mfano wake Bwana!

Je unafahamu lolote kuhusu ushirika huo katika maisha yako?

Kwa hiyo madhabahu anayoizungumzia katika Waebrania 13 ni mahala tunapojikabidhi wenyewe kwa Yesu. Ni sehemu tunaposhiriki pamoja naye, tunapofanyika kuwa washirika wa Yesu. Hapo ndipo mahala ambapo anashirikiana pamoja nasi, ndipo anapotubadilisha kiroho. Hapo ndipo mahala tunapomtolea dhabihu yetu ya sifa. Maisha yetu hutolewa kwa Mungu kwa shukurani, ibada na kujitoa.

Mungu anatupatia maelezo ya ajabu pamoja na vielelezo kuhusiana na jambo hili kwenye kitabu cha Kutoka 29, ambapo Mungu aliamuru kwamba kila siku asubuhi na jioni, mwanakondoo apate kutolewa kama sadaka ya kuteketezwa kwenye madhabahu ya dhabihu.

 “Basi sadaka utakazozitoa juu ya madhabahu ni hizi; wana-kondoo wa mwaka mmoja wawili siku baada ya siku daima. Mwana-kondoo mmoja utamchinja asubuhi; na mwana-kondoo wa pili utamchinja jioniiwe harufu nzuri, ni dhabihu ya kusongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto. Itakuwa ni sadaka ya kuteketezwa milele katika vizazi vyenu vyote mlangoni pa ile hema ya kukutania mbele ya Bwana; hapo nitakapokutana nanyi, ili ninene na wewe hapo. Nami nitakutana na wana wa Israeli hapo, na hiyo Hema itafanywa takatifu na utukufu wangu.” (Kutoka 29:38-43)

Hii hapa sio matoleo ya sadaka ya dhambi, bali ni matoleo yote ya sadaka ya kuteketezwa. Matoleo ya sadaka ya kuteketezwa yalikuwa ni matoleo yatolewayo kwa uchaguzi wa hiari ya aabuduye (Mambo ya Walawi 1:3), ilipaswa kuwa ni yenye harufu tamu/nzuri kwa Bwana. Ilikuwa inawakilisha kujitoa kukamilifu kwa waabuduo kwa Bwana. Angalia pale anachokisema Mungu mahali pale – hapa ndipo Mungu atakapokutana nasi. Anakutana na watu wake mahala pale ambapo watu wake wanakutana kwa hiari zao kutoa maisha yao pasipo masharti ya aina yoyote ile na pasipo kubakiza lolote. Lakini ebu nasi tukumbuke kuwa mwana kondoo inamwakilisha Yesu Kristo. Kwa maneno mengine, Mungu anatarajia kupata harufu ya manukato ya maisha ya mwanae kutoka katika maisha yetu ya kujitoa. Kama tulivyoona hapo ndipo mahali pa matoleo, na ni mahala pa ushirika na Bwana. Mahala ambapo maisha yetu yanafanyika kuwa ndiyo maisha Yake hapa duniani – na hiyo humpendeza sana Mungu.

Paulo anaelekeza kwetu juu ya ukweli huu wa ajabu katika nyaraka zake akisema, “Ila Mungu ashukuriwe, anayetushangiliza daima katika Kristo, na kuidhihirisha harufu ya kumjua yeye kila mahali kwa kazi yetu. Kwa maana sisi tu manukato ya Kristo, mbele za Mungu, katika wao wanaookolewa, na katika wao wanaopotea katika hao wa pili harufu ya mauti iletayo mauti; katika hao wa kwanza harufu ya uzima iletayo uzima. Naye ni nani atoshaye kwa mambo hayo?” (2 Wakor. 2:14-16).

Je, sasa unaona jinsi ya ajabu kabisa ambavyo neno la Mungu linavyokaa vizuri kwa pamoja? Bila shaka Paulo alifikiria Kutoka 29 alipoandika mistari hiyo. Na je, unaona jinsi Warumi 12 inavyokaa kwa makubaliano mazuri na eneo hili?

“Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”  (Warumi 12:1-2).

Sasa hapo ndipo tunapokutana na ukweli wa jambo hili. Haipo madhabahu inayoonekana wala hakuna haja. Hakuna mahali popote panapoonekana ambapo tunapaswa kupaendea ili kusogelea penye madhabahu. Wala hakuna kuhani wa kibinadamu hata mmoja ambaye tunapaswa kumwendea. Katika jengo (‘kanisa’) ambapo washirika wanakusanyika hakuna madhabahu  ya nje yoyote! Kwa hiyo ni kosa kubwa sana kupaita mahala mbele ya washirika katika jengo la kanisa ‘madhabahu’ kwani kanisani hakuna madhabuhu! Je, Yesu Kristo hakufa msalabani, au unataka kumsulibisha kila wiki kanisani?

Tunapasa kuendelea kumtolea Mungu maisha yetu iwe dhabihu iliyo hai ili kwamba tupate kumjua Yeye, na kuyajua mapenzi yake na tuweze kubadilishwa ili tufanane na Kristo ili kwamba tupate kuwa harufu ya manukato ya Kristo hapa ulimwenguni. Hiyo ndiyo madhabahu yako, ni mahala ambapo unajitoa mwenyewe kwa Mungu. Mahala ambapo wewe unashirikiana na Mungu, na Mungu naye anashirikiana na wewe. Mahali ambapo nyakati za tabu yako na magumu, huchagui kuamini uongo wa shetani wala kuufuata mwili wako, wala kuchagua kufuata njia zako au mambo yako unayoyapendelea, bali kuchagua kwa hiari yako kujitoa mwenyewe kwa ukamilifu kwa Mungu, ili akuelekeze na kukuongoza na akujaze ndani yako kwake mwenyewe.

Paulo alisema maneno haya ya ajabu,

“Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.” (Wagalatia 2:20).

Neno la mwisho. Ye yote asemaye lazima ulete pesa yako YOTE (ya zaka au kadhalika) mahali ambapo washirika wanakusanyika jumapili kwa sababu madhabahu yapo pale pale tu, asema uongo. Anajaribu kufanya kanisa liwe kama biashara! Hamna mafundisho hayo katika kanisa la Bwana katika Agano Jipya. Kinyume chake, wazo hili linajaribu kuuharibu ukweli wa Mungu tuliousoma katika somo hili. Usinelewe vibaya, kwa ujumla ni jambo la kawaida kuleta pesa ya sadaka yetu ‘kanisani’, hata hivyo hamna fundisho kuwa lazima utoe pesa yako yote kwa kanisa. Wazo hili inakaribia ushirikina. Upendo wa Mungu mioyoni mwenu utatuongoza kutoa pesa yetu kwa ajili ya mahitaji aina ya mbalimbali.

Kama mtu ananukuu Kumbukumbu la Torati 12:4-8 au Malaki 3:10, na anadai kwamba haya maandiko yanamaanisha kwamba inakupasa ulete sadaka zako zote hizi kwenye mahali ambapo Mungu amepachagua au kwenye madhabahuni yake, kulingana na mistari hiyo, mwambie apeleke sadaka zake Yerusalemu (kwani Yerusalemu ni mahali ambapo Mungu alikuwa amepachagua, 2 Wafalme 21:7) – lakini hawezi kuipata madhabahu hapa! Wala hawezi kuipata madhabahu iliyochaguliwa na Mungu kijiji chochote au mji katika nchi yoyote hapa duniani!

KANISA LA KIROHO: Juu ya mafundisho lipo kanisa ‘lionekanalo’ na ‘lisiloonekana’ (the ‘visible’ church and the ‘invisible’ church).

Kipo, naam, kiwango cha kiroho katika kanisa. Tumeshanukuu Waefeso ambapo panasema kwamba kanisa ni makao ya Mungu katika Roho (Waefeso 2:22). Ni sheria ya uzima ya Roho katika Kristo Yesu iliyotuweka huru mbali na sheria ya dhambi na mauti (Warumi 8:2). Kulingana na Waefeso  sura ya pili, tumefufuka na Kristo na kuketishwa pamoja naye mahali pa juu mbinguni. Na sababu ya mambo haya tunatakiwa kuwa watu wa rohoni katika maisha yetu ya kila siku (Wagal.5:25). Mtume Petro anatangaza, “Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo.” (1Petro 2:5). Pia nimenukuu mistari mingine ambayo pia inagusa swala la asili ya roho ya kanisa na washirika mwanzo kabisa wa mada hii. Yapo mengi tu, lakini haya yanatosha kwa kutimiza kusudi la somo hili.

Hata hivyo, haimaanishi kwamba kanisa halionekani kwa sababu tu ya kuwa na kiwango cha rohoni. Hakuna mahali kwenye Agano Jipya kanisa (la duniani) limeelezwa kuwa ‘lisiloonekana’. Maelezo ya kanisa lisiloonekana hayapatikani kabisa kwenye Biblia. Wala hata maelezo ya kanisa ‘lionekanalo’ hayamo kwenye Biblia. Neno la Mungu haliweki hizi tofauti popote. Kwa hiyo tofauti hizi zatoka wapi? Mafundisho haya yalitengenezwa zaidi baadaye, baada ya nyakati za Agano Jipya, ambapo makanisa yalianza kuwekewa mifumo na kuendelezwa kwenye madhehebu tofauti tofauti. Watu walianzia haya mafundisho kwa sababu ni wazi tunaona katika madhehebu mengi kulikuwa na wakristo jina tu, au walikuwa wakristo wa uongo watafutao faida yao tu kwa kusudi moja au lingine. Na tena, madhehebu haya na viongozi wao hawakuenenda katika zile tabia za Kristo! Kwa hiyo wanatheolojia hawa ilikuwa ni tatizo kuzungumza badala ya ‘Kanisa’ kama wawakilishi wa wale wajiitao Wakristo, kwa sababu walifahamu fika kwenye makanisa mengi kulikuwamo wale ambao hawakuwa wameokoka na hivyo hawakuwa sehemu kabisa ya mwili wa Kristo; na zaidi ya hayo, Wakristo wengi hawakuishi wakivyotakiwa kuwa. Kwa hiyo tunapozungumzia kanisa hawakutaka watu wafikiri kwamba kila aliyeenda kanisani alikuwa ni mkristo kwelikweli, au kwamba vitendo vibaya au viovu vya baadhi ya walioitwa Wakristo vilimwakilisha Kristo. Na matokeo yake waligeuza maneno ‘Kanisa lionekanalo’ na ‘kanisa lisiloonekana’. Kwa tafisiri hii, kanisa ‘linaloonekana’ likimaanisha makanisa na madhehebu tunayoona yametapakaa; na kanisa ‘lisiloonekana’ linamaanisha tu wale waliookoka kiukweli wakauacha ulimwengu katika makanisa mengi tofauti. Na kwa sababu huwezi huona kwa macho waamini hawa kama kundi moja pamoja, neno “Kanisa lisiloonekana” likaundwa! Kwahiyo lugha hii inaweza kutetea lengo katika kueleza jambo fulani, lakini ni lazima tukumbuke kwamba neno la Mungu haliyatengi makanisa kwa mtindo wa kanisa ‘linaloonekana’ na ‘lisiloonekana’.

Sasa, nafikiri wengi wetu kwa urahisi tutatambua kwamba kuna wengi waendao kanisani lakini si kweli kwamba wameokoka kikamilifu na kwamba ni wakristo kwa majina tu, na kwamba wakristo wengi hawaishi walivyotakiwa waishi. Hata hivyo, kama wewe u mwanimi wa kweli na kuna wakristo wa uongo kanisani kwenu, hii haimaanishi huonekani, rafiki! Kwa sababu kuna wale wasiokuwa Wakristo wa kweli katika makanisa, hii haimaanishi Wakristo wa kweli katika makanisa kutokuonekana! Biblia haina mafundisho haya. Sababu moja kwa haya ni kwamba Mungu hatambui madhehebu. Anatambua watu wake vivyo hivyo kama walivyo na po pote wanapokuwepo.

Kuna kanisa moja, bibi harusi mmoja, mwili mmoja (Efeso 4:4). Haya ndiyo mafundisho ya Biblia.

Ingawa kuna viwango vya kiroho, hata hivyo kanisa la kweli la Kristo linaonekana bayana duniani – lilitazamiwa kuwepo.

” Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima.” (Mathayo 5:14)

“Mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu.” (Wafilipi 2:15)

“Mwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa. (1Peter 2:12).

Maandiko haya yanatosha kutengeneza mwongozo, ingawa mengine yanaweza pia kunukuliwa. Je, kulikuwa na manabii wa uongo kwenye Agano Jipya? Ndio walikuwepo! “Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wa kwetu, wangalikaa pamoja nasi. Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote walio wa kwetu.” (1 Yohana 2:19; pia 2 Petro 2:1). Kwenye nyakati za Agano Jjipya kulikuwa na wakristo waliokuwa na sifa mbaya na watendao dhambi? Ndio, walikuwepo. Hebu soma waraka wa kwanza kwa Wakorintho!

Kwa hiyo tunaona katika Agano Jjipya kulikuwa na tatizo lile lile, lakini katika mafundisho yao mitume hawajengi hoja ya kuwa na makanisa mawili – moja linaloonekana na lingine lisiloonekana – kuelezea hili, hivyo na sisi hatupaswi kulielezea. Hatupaswi kwa sababu neno la Mungu halijaeleza kuhusu hili pia. Pili, hatuhitaji lugha hii kuulezea kile ambacho wengi wetu tunakijua kama sio wote.

Wazo lingine la kutumia lugha hii ya kanisa linaloonekana na lisiloonekana ni kuwa wanasema ni vigumu kujua yupi ni Mkristo wa kweli na yupi si wa kweli. Kama hili ni kweli, hii si sababu ya kuwaita Wakristo wa kweli ‘wasioonekana’! Pia, Yesu Kristo alijua tatizo gani litatokea na akatuambia kuwa makini na kutambua na kutofautisha mambo – Mathayo 7:15-19. Pia Yohana katika waraka wake wa kwanza , alitoa angalizo kwa Wakristo juu ya walimu wa uongo na waumini wa uongo, anawaambia wazijaribu roho ili kujua zimetokana na Mungu au la! Yohana pia anawapa fundisho lingine la kutofautisha anayeamini kweli na asiye amini kweli. Kwa hiyo tunaona japo ni tatizo kama hili lilikuwepo pia katika kanisa la mwanzo, mitume hawakutumia lugha ya kanisa ‘linaloonekana’ na ‘lisiloonekana’ kuelezea tatizo hili, bali waliwafundisha waaminio mafundisho na mashauri mazuri kuwasaidia kutofautisha wale wanaomwamini Yesu  Kristo na wale wasiomwamini, ili waweze kujua namna iwapasavyo kuenenda katika nyumba ya Mungu ambayo ni kanisa la Mungu aliye hai! (1 Timotheo 3:15).

Mungu hana makanisa mawili hapa duniani – kanisa linaloonekana na lisiloonekana. Hasemi ana kanisa moja lenye mchanganyiko wa waaminio na wasioamini na kanisa lingine lenye Wakristo waaminio  pekee! Kristo atakaporudi atarudi kwa ajili ya kanisa lake moja tu. Hakufa na kufufuka kwa ajili ya dhehebu, kikundi au taasisi! Atakaporudi atachukua wale aliowakomboa  na wala si taasisi au dhehebu.

Kama nimezaliwa upya na Roho wa Mungu na kuwa na ushirika na Baba na Mwana, naweza kuwa na ushirika na waaminio wowote wale duniani bila kujali wala kutazama dhehebu lao. Na hili ni kweli.

Kwa hiyo tunaona japo hii lugha inatumika kuweka wazi mambo yaliyoko wazi, lakini ni lugha isiyo ya lazimakwa sababu mambo haya yalikuwa wazi katika kanisa la kwanza ambao hawakutumia lugha hii. Na kwa kuwa Neno la Mungu halitumii lugha hii na sisi hatupaswi kuitumia hata kidogo kuelezea mambo ambayo neno la Mungu halikufundisha, kwani tukitumia lugha hiyo, tunaweza kusababisha machanganyiko juu ya mafundisho ya neno la Mungu. Namaanisha kuna mengi katika dhehebu ambayo Mungu hakuyapanga wala si mapenzi yake kwa kanisa, na tunaweza weka udhihirisho wa uongo juu ya hili kwa chini ya kichwa cha ‘kanisa  linaoonekana’. Ni afadhali tutambue tulichokosea katika muundo huu, kile ambacho si sawa na Neno la Mungu, tukajinyenyekeza  na kufuata njia ya Mungu ambayo tunayo katika Agano Jipya.

© David Stamen 2016        somabiblia.com

KUPAKUA SOMO HILI, BONYEZA LINK IFUATAYO:  KANISA NI NINI?

 

6 responses to “KANISA NI NINI?

 1. Benester Owigo

  June 11, 2017 at 11:54 am

  Mafundisho Matamu na yenye kujenga M/Mungu awabariki sana

   
 2. Mussa Mubuga

  August 13, 2017 at 3:05 pm

  Upo sawa mtumishi ila wabishi hawatakuelewa

   
 3. Anonymous

  November 13, 2018 at 10:22 am

  HAKIKA MUNGU AMEKUTUMIA ALIVYOKUSUDIA IMENICHUKUA MAA 4 KUSOMA YOOTE HAPA LAKINI NIPATA MAJIBU SAHIHI MUNGU AKUBARIKI. NATAMANI KUJUA IKIWA UNA KITABU N. K

   
 4. Anonymous

  June 20, 2019 at 4:18 pm

  Ubarikiwe sana.

   
 5. MESHACK TIMOTH

  October 23, 2021 at 5:59 pm

  Mungu amekutumia vyema na umetenda kazi njema Mungu akubariki sana

   
  • dsta12

   November 14, 2021 at 9:00 am

   Asante kwa comment, Meshack.

    

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

 
%d bloggers like this: