RSS

JE, UNAPENDA KUWA MTAJIRI?

JE, UNAPENDA KUWA MTAJIRI? HAYA, SOME YAFUATAYO, KWANI YATAKUAMBIA YATAKAYOTOKEA KWAKO.

“Lakini hao WATAKAO kuwa na mali (KUWA TAJIRI) HUANGUKA katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ZIWATOSAZO WANADAMU KATIKA UPOTEVU NA UHARIBIFU. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni KUPENDA FEDHA; ambayo WENGINE HALI WAKIITAMANI HIYO WAMEFARAKANA NA IMANI, na kujichoma kwa MAUMIVU MENGI.” 1 Timotheo 6:9,10.

Yaandikwayo hapo juu ni sehemu yako na sehemu ya maisha ya baadaye yako, kwa mujibu wa neno la Mungu. Tambue, mistari hii inahusu UNALOTAKA kweli kweli moyoni mwako. Lengo la mawazo yako yote moyoni mwako ni nini? Kimsingi, unatafuta nini, unataka nini? Je, unaweza kujibu kwa dhati kwamba unatafuta KWANZA ufalme wa Mungu na haki Yake kuliko mambo mengine yote? Je, unaweza kusema pamoja na Paulo, unayahesabu mambo yote kuwa kama ‘mavi’ kulinganisha na ‘UZURI USIO NA KIASI WA KUMJUA KRISTO YESU’?

WATU WOTE kwenye facebook (waumini?) wanaochapa ‘AMEN’ chini ya PICHA YA PESA nyingi, au chini ya AHADI YA PESA nyingi inayotolewa na ‘nabii’ fulani, hao wote (pamoja na yule ‘nabii’) wamefarakana na imani na hawamfuati  Yesu Kristo.

WATU WOTE ambao wanasikiliza na kuamini WAHUBIRI WANAOWAAHIDI watapata nyumba, gari, milioni, bilioni, na mafanikio katika biashara, wote pamoja – wale wahubiri na wasikilizaji – wamefarakana na imani na hawamfuati  Yesu Kristo.

HAO WATU WOTE wamejidanganywa kwa upesi (na hata ‘kwa furaha’) kwa sababu ya kupenda fedha kwao, na idadi yao ni kubwa sana.

Shauri la Paulo ni nini? Tusome. “Bali wewe, mtu wa Mungu, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa, imani, upendo, saburi, upole.” 1 Timotheo 6:11.

Na Yesu anatufundisha nini juu ya utajiri? Tusome. “Msijiwekee hazina duniani…bali jiwekeeni hazina mbinguni…kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako.” Mathayo 6:19-21.

“Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo.” Luka 12:15.

“Lakini Mungu akamwambia, ‘Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?’ Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.” Luka 12:20,21

Hata kanisa linaweza kujidanganya na kujiinua kwa sababu ya utajiri na mafanikio yake! “Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi…BASI UWE NA BIDII, UKATUBU.” Ufunuo 3:16,17,19.

AIDHA, JE, IFUATAYO NDIYO NIA YAKO YA DHATI? JE, HUO NI MTAZAMO WAKO WA DHATI…..

“WALAKINI UTAUWA PAMOJA NA KURIDHIKA NI FAIDA KUBWA. Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila tukiwa na chakula na nguo TUTARIDHIKA NA VITU HIVYO.” (1 Tim.6:6-8)

Kama ni sivyo, je, sio wakati ubadilishe mtazamo wako?

Ukijishughulisha na mambo ya ‘mafanikio’ TU, moyo wako upo wapi?

Je, unaamini “utauwa ni njia ya kupata faida.”? Kama ni hivyo, soma 1 Timotheo 6:3-5 kwani mistari hii imeandikwa juu yako!

Labda utasema, “Lakini je! Nifanyaje juu ya biashara yangu?” Hamna tatizo. Lifuate neno la Mungu la hapo juu tu na fanye biashara yako! Biashara yako sio tatizo. Mambo hayo yanahusu hali ya kiroho ya moyo wako na lengo la fikra zako.

Baada ya kusoma hayo, ukisema kama yafuatyo, “Lakini kuwa tajiri siyo dhambi! Umaskini hauleti utukufu kwa Mungu! Biblia haishabiki umaskini. Umasikini si sifa ya Wokovu. Utajiri ni mapenzi ya Mungu!” Ukisema mambo kama hayo baada ya kusoma somo hili, inamaanisha, hujaelewa mzigo na muktadha wa somo hili, hata kidogo; hujaelewa uliyoyasoma, na inawezekana kimsingi huelewi mafundisho ya Biblia. Kama umesema mambo kama hayo moyoni mwako, shida ni katika moyo wako na siyo kwenye somo la hapo juu.

Mpendwa msomaji, bado muda upo ubadili mtazamo wako kama umekosea. Nimeandika mambo hayo kwani wengi wanatafuta pesa na ‘baraka’ za vitu kuliko kumfuata Yesu Kristo.

Na Mungu aiguse mioyo yetu siku hizi kwa neno lake na neema yake!

© David Stamen  2016                   http://www.somabiblia.com

 

Comments are closed.

 
%d bloggers like this: