JUU YA MFUMO WA KUIWEKA WAKFU ARDHI AU NYUMBA YAKO.
UNATAKA KUIWEKA WAKFU KWA BWANA ARDHI AU NYUMBA YAKO?
Katika somo hili, tutakwenda kuyaangalia kwa makini mawazo yafuatayo ili kuyaainisha iwapo yamekaa kiroho au hapana.
Jambo la kwanza, ni vema tujue: je, neno la Mungu linakuhitaji wewe utakase au uweke wakfu kwa Mungu lile shamba lako, nyumba yako au hata mali zako zozote?
Jambo la pili: je, neno la Mungu linatufundisha kuwa ikiwa hatutaweka wakfu au kutakasa mashamba yetu au mali zetu kwa Bwana, basi laana itabakia kudumu na kukandamiza mashamba yetu, na kwamba shetani sasa atapata fursa ya kutuumiza kupitia mali zetu hizo?
Sioni ugumu wowote, na wala si vigumu kuonyesha kuwa mawazo kama hayo siyo ya kiBiblia.
Hebu kwanza tufikirie fundisho la Agano Jipya. Je, ni wapi basi ambapo Yesu mwenyewe, au hata mitume wake aliokuwa akiambatana nao wakitenda huduma walipofundisha kwamba tunapaswa kuziweka wakfu au kutakasa mashamba, nyumba zetu au hata mali zetu kwa Bwana? Ikiwa unaijua Biblia vizuri, basi hakika utalijua jibu la maswali haya mara moja. Wazo hili halijawahi, na wala fundisho lake haliyafundishwa kwenye Agano Jipya hata kidogo. Wala Yesu mwenyewe hata mitume wake hawakufundisha fundisho kama hilo, na wala hawakupata kutamka hata neno moja kuhusu jambo kama hili. Au je, unaweza kuuonyesha mfano wowote ule ambapo mwamini anaweka wakfu kwa Mungu, mashamba yao, nyumba zao ambazo wamezinunua? Hapana! Haupo mfano wowote ule wa aina hii kwenye Agano Jipya lote. Hii itoshe kwetu kutambua kuwa Wakristo hawalazimiki/hawawajibiki hata kidogo kufanya mambo kama hayo. Lakini tutaendelea kuliangalia jambo hili kwa ukamilifu zaidi.
Kwenye tafsiri ya Kiswahili (Union Version), neno “wakfu” amelitumia Yesu pale alipokuwa akiwakosoa Mafarisayo aliokuwa wakifundisha mafundisho ya uwongo (Matayo15:5). Lakini muktadha wake hapo hauhusiki na lolote lihusulo kuiweka wakfu nyumba, mashamba kwa Bwana, kama tunavyosikia walimu wa leo wakifundisha watu.
Hebu basi sasa tuangalie katika Agano la Kale nalo. Hebu tujiulize ni sehemu gani inayotuonyesha kuwa Mungu waamuru watu wake waweke wakfu mashamba, nyumba zao kwake? Jibu lake ni jepesi sana! Hakuna amri ya aina hiyo hata moja ambayo Mungu aliitoa kwa watu wake. Au je upo mfano wowote ambao tunamwona Myahudi anaweka wakfu mashamba yake, nyumba yake aliyoyanunua, kwa Mungu? Hapana, hakuna jambo kama hili, wala hakuna hata mfano wowote unaoelekeza jambo kama hili lifanyike na watu wa Mungu katika Agano la Kale.
Hayo tunayoyasikia yakifundishwa na walimu hawa wa kipindi hiki, ni mambo mageni na ni yakushangaza. Wawezaje basi kufundisha, au kuwataka waumini waende katika mapitio mbaya hata hayaja fundishwa kwenye Biblia na wala hakuna mfano hata mmoja katika Biblia unaoelezea mambo kama hayo? Jambo kama hili linaweza tu kuwapeleka watu katika makosa na vifungo.
Ipo sura moja katika vitabu vya Agano la Kale ambayo inaongelea kuhusu mtu ambaye anaweka wakfu au kutoa mali zake kwa Bwana, sura hiyo ni katika Kitabu cha Walawi 27:14-28. Lakini somo linaloelezwa katika sura ile ni tofauti kabisa na somo tunaloliangalia hapa. Sura ile inahusika na watu ambao kwa hiari yao wameamua kujitolea kutoa mashamba yao na nyumba zao kwa Mungu. Hivyo basi hapa tunaona kuwa kwanza, ni uchaguzi wa mtu mwenyewe kufanya hivyo, wala hafungwi na sheria yoyote kufanya hayo, na wala haikuwepo sheria wala masharti yoyote yaliyowekwa kuwafunga watu lazima wafanye hivyo. Jambo la pili na hili ni la muhimu zaidi, ni kwamba mistari ile ya neno la Mungu inazungumzia juu ya watu wale tu waliochagua wao mwenyewe kwa hiari zao kuyatoa mashamba yako na nyumba zao kwa Bwana. Kwa maneno mengine, mali zile hazibakii tena mikononi kwa waliozitoa kwa Bwana. Zinakuwa si mali zao tena, maana wamezitoa kwa Mungu. Na hiyo ndiyo sababu unasoma katika sura ile kuwa makuhani lazima wathaminishe thamani ya mali zile zilizotolewa wakfu kwa Mungu.
Mali iliyotolewa wakfu kwa Mungu ilikuwa aidha iuzwe (na pesa zinazopatikana zitumike kurekebishia au kutengenezea maeneo ya hekalu) au walikuwa wanawapatia makuhani (soma mstari ule wa 21). Lakini iwapo ilitokea mtu yule mwenye kuweka wakfu mali zake anapenda kubaki nazo mali zake ambazo tayari amaziweka wakfu kwa Bwana, basi mtu wa namna hiyo ilimpasa kulipia thamani yote ya mali ile (kulingana na tathimini iliyofanywa na kuhani) pamoja na asilimia 20℅ ya thamani yote ya mali ile; malipo hayo yote kwa pamoja alipwe kuhani. Na kulikuwepo na kanuni nyinginezo kulingana na mwendelezo huo.
Lakini sasa kama unavyoona, maelezo hayo yaliyomo kwenye maandiko inaelezea wazi kabisa juu ya kuzitoa kabisa mali zako kwa ajili ya kazi ya Bwana kama tulivyoliona wenyewe jambo hili kwenye maandiko hayo ya neno la Mungu. Ni jambo la tukio la kujitolea kwa hiari kwa upande wake yule anayetoa mali zake. Hivyo basi eneo lile halihusiani na somo letu hata kidogo.
Basi kama hatulioni fundisho lolote na wala halipo fundisho la aina hiyo kwenye Biblia lisemalo kuwa yatupasa kuweka wakfu nyumba pamoja na ardhi zetu, ndipo kwa hakika wazo la pili ni la uongo pia, yaani, fundisho lile wanalofundisha kwamba eti kama hatutaweka wakfu mali zetu basi zitaingia kwenye laana, au maroho ya uovu yatamiliki mali hizo. Habari za fundisho kama hilo ni uongo mtupu, ni kuchezea akili za waumini na kuyumbisha uelewa wa watoto wa Mungu. Kwa sababu hakuna mahala popote kwenye Biblia panapofundisha jambo kama hilo. Wala kwenye Agano la Kale au hata kwenye Agano Jipya, habari kama hizo hazipo. Hakuna mahala popote pasema kwamba mali zako zitalaaniwa au zitateseka kwa mapepo ya giza au uovu iwapo hutaziweka wakfu mali hizo! Tafute tu uone mwenyewe.
Hivyo basi hiyo imefanyika rahisi sasa kwako na mimi. Hatuhitajiki kwenda Chuo cha Biblia; hatuhitajiki kukijua kiyunani au kihebrania ili kuyajua mambo hayo. Tunaweza kumshukuru Mungu kwa Neno lake na namna ambavyo linatuelekeza mioyo yetu kwenye kweli yake pasipo tatizo lolote. Tumepewa Roho wa Mungu, ili kwamba tupate kuyajua mambo ambayo Mungu yametolewa bure kwetu. Jina lake lisifiwe. Haupo kwenye ulazima tena wa kuwekea mali zako wakfu au kuzitakasa, yaani kiweka wakfu mashamba, nyumba, wanyama au biashara zako, nk. kwa Mungu. Ikiwa wewe ni mwana wa Mungu, hivyo wewe tayari ni wa Mungu. Unahusika naye, ni mali yake Mungu – kila kitu ulicho nacho ni mali yake Mungu ni vyake. Ikiwa atatokea mtu na akakuaambia yakupasa rasmi au kidini weka wakfu ardhi yako kwa Mungu, hao basi watakuwa wanakutumbukiza kwenye vifungo! Au kama watasema kuwa shetani, au laana inayo nguvu au haki juu ya ardhi yako iwapo hutaiweka wakfu, basi huo ni ushirikina tu, fundisho la aina hili linapatikana kutoka katika desturi ya uchawi tu. Haitoki kwenye fundisho halisi la Biblia au Agano Jipya. Mambo kama hayo yanafundishwa wapi na Yesu mwenyewe au mitume? Aina hii ya mafundisho yanasaidia tu kukuza hofu miongoni kwa watu, na sio imani! Aina hii ya mafundisho yanawafanya watu wafikiri kimwili na sio kiroho, na yanawatumbukiza kwenye vifungo, na sio kuwaweka huru.
Kwa vyovyote ni sawa kwamba katika Biblia tunakutana na maneno kama kutakaswa, ‘kutakasa’, ‘kuweka wakfu’ na ‘kulaani’, lakini sasa huwezi kuyatumia maneno hayo kwa njia yoyote ile uitakayo wewe (ovyoovyo tu) na kuingiza au kujengea fundisho lako mwenyewe, kisha ukadai kuwa fundisho hilo ni fundisho la kiBiblia!
Mambo kama hayo yote ni mambo ya hatari sana. Hebu angalia jinsi mtume Paulo anavyoyandikia makanisa ya huko Galatia, “Nawachelea, isiwe labda nimejitaabisha bure kwa ajili yenu… Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema…Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa?” (Wagalatia 4:11; 5:4; 3:1). Awezaje mtume Paulo kuwaandikia mambo kama hayo Wakristo waliopo kule Wagalatia? Alikuwa amewahubiria na baadhi yao walikuwa wameamini au kuokolewa kupitia huduma yake (Galatia 3:14,15)! Wakristo hawa wa huko Galatia walikuwa wameiamini Injili, walikuwa wameamini kuwa Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu, na kwamba alikuwa ni Mwokozi wao, na kwamba walipata msamaha wa dhambi kupitia damu yake; waliamini juu ya nguvu au uweza uliomo katika Roho na miujiza! Inakuwaje sasa basi mtume Paulo awaandikie watu hawa kuwa kazi yake yote aliyoifanya katikati yao itakuwa ni kazi bure imeharibika; na baadhi yao watakuwa wameanguka kutoka katika neema ya Mungu; na kwamba Yesu hajaleta badiliko lolote kwenye maisha yao? Anasema watakuwa WAMELOGWA!
Ni nani basi amewaloga Wakristo hao kiasi kwamba ionekane kuwa imani yao katika Kristo sasa haina maana tena? Paulo analitoa jawabu la swali hilo kwa uwazi kabisa! Mambo ambayo yalikuwa yanawadanganya na kuwapotosha Wakristo wale na kuifanya hata imani yao waliyoipata ionekane haina maana, ni kwamba Wakristo wale walikuwa wanarudi nyuma kuelekea kwenye Agano la Kale, na kuzitii sheria ambazo zilitolewa kwa mambo ya nje. Walianza kuziheshimu na kuzitunza siku takatifu na masikukuu ya sheria za Musa (Wagal 4:10). Walikuwa wanafundishwa kuwa yawapasa kutahiriwa ili wapate kuokolewa (Wagal.5:2,6). Paulo aliwaandia barua hii akiwa na huzuni nyingi moyoni mwake. Walikuwa wanakaribia kupoteza imani yao kabisa! Hivyo katika barua ile Paulo anaweka wazi kuwa wasiende kwa kuzifuata sheria za Musa, hizo zilikuwa zinaelezea mambo ya kiinje tu – kama vile kutahiriwa, au kutunza aina fulani za siku za sikukuu au sherehe – kana kwamba kwa kutunza hayo ndiyo itakufanya uwe mtakatifu au utampendeza Mungu. Uweza na neema ya Yesu inayotufanya tuwe kwenye haki na tumpendeze vizuri Mungu sasa iko kwa Yesu Kristo kupitia imani. Hiyo ndiyo hoja ya Paulo katika nyaraka hizo zote. Ikiwa tutaanza kufikiri kuwa kwa kutunza mambo ya kidini ya nje – kama vile kutunza sabato, au kutahiriwa, (au hata ni lazima kuweka wafu mali zetu) – kwamba hayo ndiyo mambo ya haki kuyafanya, ndipo Paulo anasema tumeupoteza msingi wetu wetu wa imani na haki mbele za Mungu.
Unaona jinsi ilivyo hatari mambo hayo na jinsi madhara yake yalivyo mabaya? Ijapokuwa Wakristo wa huko Galatia waliamini mambo mengi yenye kweli muhimu na kimsingi, lakini tendo lao la kuanza kuzifuata sheria za kiinje za sheria za Musa, ilimaanisha kuwa watu hawa tayari wamekwisha geuzia migongo yao kwenye imani, na Yesu Kristo pia. Hilo ndilo fundisho la neno la Mungu kupitia mtume nyaraka za Paulo. Nyingi ya sheria hizo ambazo ni vielelezo vya kiinje tu vilikuwa vinatuelekeza kwa Yesu Kristo na lile atakalolikamilisha kwenye msalaba! Na kwa sababu ya hata mambo ya kiinje mambo yanayotokana na Agano la Kale hayakuwa yakituhusu sisi kwa vyovyote vile, kwa sababu hakuna jambo lolote kutoka katika sheria hizo ambazo zingetuweka sisi tuonekane wenye haki. Na hiyo ndiyo sababu inayomfanya mtume Paulo aseme, “enyi Wagalatia wajinga, ni nani aliyewaloga hata mshindwe kuitii kweli, ambayo imewekwa wazi mbele ya macho yenu kuwa Yesu Kristo amesulubiwa kwenu?
Hii ni hatari kubwa sana na udanganyifu wa hao wanaotufundisha na kutuambia ni lazima kutunza shughuli za kidini za kiinje, hata inatupa upofu tusijue nguvu za Kiroho ambazo zimemwagwa kwetu sisi tu kupitia imani inayopatikana kwa kile alicho kifanya Yesu Kristo pale Msalabani kupitia ufufuo wake. Unaweza ukajiuliza, ‘Je, haitupasi kutekeleza kwa kuyafanya yote mawili? Yaani, tunaiamini Injili na hayo ni mambo machache tu ya kanuni za nje?” Basi, sasa ile barua ya Paulo anayowandikia Wagalatia yenyewe inakueleza ni vigumu kama nini kuyabeba hayo mambo mawili kwa pamoja, yaani mambo ya kiroho na mambo ya kiinje. Inasema wazi kuwa haiwezekani. Huwezii kuuweka mguu wako mmoja kwenye sheria za Musa kisha na mguu wako wa pili unauweka kwa Yesu Kristo. Jambo kama hilo halipo. (Warumi 6:14; 7:4).
Unaweza pengine ukadanganyika ukasema, “Aha! Lakini mbona anayefundisha fundisho hili ni mtu maarufu anayefahamika sana!” Msikilize Paulo anachoandika kwenye like sura ya kwanza ya Wagalatia,
“Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine wala si nyingine, lakini wapo watu wawatabishao na kutaka kuigeuza Injili ya Kristo. Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yoyote isipokuwa hii tuliyowahubiri, na alaaniwe, kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yoyote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe!” (Waalatia 1:6-8).
Hii ni lugha nzito sana! Anawaambia kwamba wale wafundishao mambo haya wanawasumbua tu, na kuizuia Injili ya Kristo! Kuanza kutii na kuyafuata mambo ya kiinje ya sheria za Musa ilikuwa ni kuwaondoa watu mbali na neema ya Kristo na kuwaingiza kwenye dini zao wao wenyewe – ambazo Paulo anaziita “injili nyingine”. Na kama utasoma vizuri ule mstari wa 8, utaweza kukubaliana nami kuwa hakuna hata mmoja ambaye angependa kuishi chini ya hukumu ya mstari ule! Kosa la fundisho hili ni hatari kiasi kwamba haliwezi kuwa hatari zaidi!
Injili aliyoihubiri Paulo ilimwinua Kristo na kazi ya msalaba, siyo mambo ya mfumo wa nje!
Mtu mmoja aliuliza kama ninalikataa Agano la Kale! Ni swali la mshangao mkubwa sana hilo! Je, Paulo mtume naye alilikataa Agano la Kale kwa sababu tu yeye aliyaandika mambo haya? Lakini ebu ngoja nikuulize, je, unaamini kwamba unahitajika kutahiriwa ili uwe Mkristo wa kweli? Kama huamini hivyo, KWA NINI basi huamini? Je, unaleta ng’ombe au mbuzi au kondoo kanisani siku za jumapili, au mara moja kila mwaka ili kuwachinja kwa ajli ya msamaha wa dhambi zako? Kama hufanyi hivyo, KWA NINI basi hufanyi? Je, unaishika siku ya sabato kama vile wayahudi wanavyofanya? Kama hufanyi hivyo, KWA NINI basi huyafanyi hayo? Na kama huyafanyi mambo kama hayo, huyafanyi kwa sababu wewe unalikataa Agano Jipya? Kwa vyovyote hulikatai Agano la Kale, lakini kinyume chake, sisi hatufanyi hayo kwa sababu tunaiamini Biblia. Biblia nzima, kwamba ni neno la Mungu. Hatuyafanyi mambo hayo kwa sababu Yesu Kristo alikufa pale Kalvari kutuokoa kutokana na dhambi zetu na kutukomboa kutoka kwenye laana ya sheria!
Hatuhutaji kutahiriwa katika mwili, kwa sababu hiyo ilikuwa ni kiwakilishi au dalili tu ya nje ya kile ambacho Mungu anakwenda kukifanya ndani ya mioyo yetu kwa Roho Yake kupitia kifo chake Kristo Yesu na ufufuo wake (Warumi 2:26-29; Wakolosai 2:11,12). Leo hii hatuitunzi tena siku ya sabato ya kiinje, kwa sababu kupitia kifo cha Kristo Yesu na ufufuo wake tumeingizwa kwenye pumziko la Sabato ya Kiroho ya Mungu (Hebrania 4:1-11). Hatuleti tena wanyama ili wachinjwe kule kanisani kama sadaka ya msamaha wa dhambi zetu kwa sababu mkombozi wetu, Mwana wa Mungu, alikufa pale msalabani ili kukuweka wewe na mimi huru kutokana na dhambi na nguvu yake, kutufanya tuwe safi, tuwe watakatifu! Jina la Bwana libarikiwe!
Hii ndiyo sababu Paulo anawaandikia Wagalatia, anawaambia,
“…kwa hiyo simameni wala MSINASWE tena chini ya kongwa la utumwa.” (Wagalatia 5:1).
Hapo anaongelea kuhusu wale wanaotaka kuturudisha nyuma kwenye matendo ya kiinje ya sheria ya Musa, naye akasema, simameni imara kinyume nao (muwapinge) hao, wala msiporwe Uhuru wenu ambao Kristo ameuingiza kwenu. Anaendelea kusema kuwa wale wote wanaotafuta kutuweka chini ya Agano la Kale tena ambayo ni sheria na matendo ya nje tu, watu hao wanatuweka kwenye vifungo tu – na hicho ndicho mafundisho hayo yanachokifanya, wanawaleta watu kwenye vifungo.
Hivyo ndivyo mtume Paulo alivyowaambia Wakolosai,
“Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.” (Wakol.2:16,17).
Hapo anawaambia Wakristo wa huko Kolosai ya kwamba wasimwachie mtu yeyote yule KUWAHUKUMU, eti kwa kuwa tu hawazifuati sheria za nje za Agano la Kale, wala usimruhusu mtu yeyote yule akulazimishe kuzishika desturi zozote zile za Agano la Kale kwa kukuwekea vitisho vyake, na kukuhofisha kwamba eti usipofanya mambo hayo basi utakuwa humpendezi Mungu, au kwamba utaingia katika hukumu yake. Vitisho hivyo vya hukumu ni uwongo – hivyo ndivyo Paulo anavyo waagiza Wakolosai.
Mambo hayo aliyowaonya Paulo yanafanana kabisa na hali inavyoendeshwa leo huko makanisani. Ni ajabu na kweli kuona makanisa mengi yanaishi ndani ya Agano Jipya lakini makanisa hayo yanakula chakula cha Agano la Kale! Iko vilevile hata leo watu wanapoambiwa wawajibike kuweka dhabihu au utakaso wa nyumba zao au ardhi. Ulazima wa aina hii yanatambulisha au yanawakilisha tu mifumo ya kidini iliyobobea katika mila na desturi za kisheria. Na wahubiri ndio watakao kuelekeza ni hatua gani utachukua ili kutimiza wajibu huu wa kidini. Hayo yote ni mambo yanayowakilisha sheria tu ambayo inapaswa kuifuata – na kama itatokea hatuifuati sheria hii, mwisho wake italeta matokeo ya matatizo kwetu kiroho na hali kadhalika kimwili! Hiyo ndiyo hali halisia iliyomfanya mtume Paulo ahubiri kuyapinga mafundisho hayo!
Tofauti mojawapo kubwa kati ya sheria ambayo Paulo alikuwa akiihubiri kinyume, na wajibu huu wa kidini, au sheria iliyowekwa inayoelezea mambo gani mtu aweke wakfu mali zake, ni kwamba mambo ambayo Paulo alikuwa akiyasemea kinyume chake ilikuwa ni sheria iliyotolewa katika Agano la Kale! Wajibu huu wa kidini wa kuweka wakfu mali zako haupatikani popote pale kwenye Biblia, wala katika maisha yote ya kanisa. Sasa ikiwa mtume Paulo alikuwa mkali katika kutufundisha kwamba tusiishike sheria iliyotolewa na Mungu mwenyewe katika Agano la Kale, je, hili sio tendo baya zaidi kwa wahubiri hawa kutuambia tutunze au kushika wajibu wa kidini, au mifumo ya uwekaji wakfu ambayo haikuagizwa na Mungu kufanya hivyo? Haikuagizwa na Mungu kwenye Agano la Kale wala hata Agano jipya nalo hakuagiza.
Tunaipata wapi basi mifumo hii ya kidini ambapo unahitajika kuweka wakfu nyumba yako na ardhi yako pale unapo inunua na kuanza kuijenga pale? Unaona jambo hili katika dini nyinginezo au katika jumuia za kichawi tu, wanafanya mifumo ya ainia hii, lakini hutayaona hayo katika mifumo ya Biblia. Lakini wanaamini kuwa wasipofanya makafara yao na dhabihu zao, basi miungu yao itakasirika na italeta balaa kwenye familia, kwenye mali zao nk. Nasikitika sana kuona mafundisho na desturi ya dini nyingine sasa inahamishiwa makanisani, na ndani ya maisha ya Wakristo. Mambo hayo yanawaingizia hofu, woga, machanganyiko na kuanza kuuzoelea ushirikina.
Msomaji wangu mpendwa, je, huoni jambo hili? Kama Mungu angehitaji uchukue hatua maalum ili kuweka wakfu mashamba yako au nyumba yako, basi angekuambia tu! Angetuambia hivyo kwenye Neno Lake! Ikiwa jambo la kuweka wakfu mali, nyumba na mashamba ni muhimu na ya lazima kiasi hicho wanachotutisha wahubiri hao, kwa nini basi Biblia ikae kimya juu ya jambo hili? Kwa nini Mungu atuache gizani kwa jambo muhimu analotutarajia tumletee matokeo mazuri? Kwa sababu zipi hasa eti akuachilie wewe umwendee mhubiri fulani mkubwa, au mwalimu fulani kana kwamba kumfuata mganga wa kienyeji ili kupata siri fulani fulani za maarifa ambayo haya kwenye Biblia yenyewe hazipatikani? Wapendwa hapo mnaongozwa kuelekea gizani, kwenye jumuia na anga za kishirikina tu! Kwa nini watu wanamfuata mwanadamu badala kufuata Mungu na neno lake? Neno la Bwana linasema, “Neno lako ni taa ya miguu Yangu na mwanga wa hatua zangu.” (Zab.119:105). Tunapaswa kuishi kwa kulifuata Neno la Mungu. Tunapaswa kuishi kwa kufuata kile ambacho Neno la Mungu LIMETUFUNULIA. Ndipo tutakuwa tukitembea nuruni! Kila kitu unachohitaji kukijua kipo ndani ya Biblia. Mungu aliweka mambo yote tunayohitaji kuyajua ndani ya Biblia ili tusiangamie.
————————–
Wahubiri wengi hufundisha mambo mengi wanayatoa kutoka katika Agano la Kale. Wanawafanya watu waonekane kuwa ni Wayahudi na sio Wakristo kwa kufanya hivyo wafanyavyo wanatengeneza dini ya matendo ya nje tu badala ya kuhubiri juu ya nguvu ya Roho Mtakatifu ambaye amekuja kubadilisha maisha yetu ya ndani kwanza, na kisha kutuweka huru mbali na dhambi (soma Warumi 8:1-4). Wanafundisha tu mambo ya nje, mambo ya kimwili, wala kwa hakika sio mambo ya kiroho hata kidogo. Wanafundisha kana kwamba Yesu hajafa, hajamwaga damu yake na kumwaga Roho wake Mtakatifu ili tupate kuyajua mambo ambayo tayari yametolewa bure kwetu na Mungu, “….lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao. Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu. Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu. Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu. Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni. ” (1 Wakor. 2:9-13).
Je, unaona hapo? Ni ile huduma ya Roho Mtakatifu itufundishayo juu ya mambo ya ajabu ambayo Mungu mwenyewe ametuandalia – na katika sura ileile ya Wakoritho ambapo mtume Paulo anatueleza juu ya kiini na lengo la mafundisho yetu yote yaelekezwe, na hiyo ni “Yesu Kristo mwenyewe, yeye aliyesulubiwa.” Tunapoongelea juu ya utofauti wa huduma kati ya Agano la Kale na Jipya, mtume Paulo anasena mambo yafuatayo, “Naye ndiye aliyetutoshelezakuwa wahudumu wa Agano Jipya, si wa andiko bali wa Roho, kwa maana andiko huua, bali Roho huhuisha…” (2 Wakorintho 3:6). Je, umegundua anachokisema kwenye sura ya waraka huu? Ikiwa huduma yako inalenga au inarudi kutupeleka nyuma kwenye mambo ya nje ya kanuni za utendaji wa kidini uliojaa sheria za Musa, basi wewe huduma yako ni moja kwa moja ya vifo – kwa sababu itawatia watu upofu wasiujue ukweli na nguvu ya Injili iliyomo kwenye Agano Jipya.(2 Wakorinthi 3:14,15).
Badala ya kumhubiri Kristo na kile alichokifanya kwa ajili yetu kwa kutukomboa mbali na laana ya sheria, na nguvu ya dhambi, wahubiri wengine sasa wanapenda kufundisha mambo yahusuyo laana, eti wanafundisha kuhusu kuziondoa laana kutoka katika ardhi yako, nyumba yako na duka au biashara yako. Wanaongelea na kufundisha namna ya kuweka wakfu ardhi yako, nyumba, mtoto au duka; wanaongelea namna ya kuitumia damu ya Yesu kufunika mali zako, au gari, kana kwamba hiyo ni hirizi ya kiuchawi. Wanafundisha mambo ambayo yanazalisha hofu na ushirikina badala ya kuzalisha imani na uhuru upatikanao kupitia Agano Jjipya ambalo Kristo Yesu alimwaga damu yake ili kutuingiza sisi ndani yake. Kwa mafundisho yao hayo huwachukua wasikilizaji wao au wasomaji wao nyuma tena, kwenye Agano la Kale na kuwafanya wafikiri kuwa wapo chini ya Agano la Kale tena,na kuwafanya watu waishi kana kwamba wanaishi nyakati za Agano la Kale tena! Tatizo hapa si kwamba wanafundisha kutoka Agano la Kale tu, lakini hata Agano la Kale lenyewe hawalielewi. Kwanza yawapasa kujua kuwa mambo mengi ya muhimu yaliyoandikwa katika Agano la Kale kwa leo hii ni kivuli cha mambo halisia ambayo Kristo amekuja kuyatimiliza. (Waebr. sura zile ya 8-10). Jambo la pili, mistari yote wanayoinukuu wanapofundisha, wanaitumia kwa makosa. Mambo yale yote yalihusu mambo ya nje, ya kimwili. Lakini Mungu Baba, kupitia Kristo ametaka kutubadilisha kutoka ndani yetu ili tupate kujua Uhuru ambao ametufanya tuwe huru, Lakini sasa mafundisho hayo yao yanatufanya tubaki katika vifungo kwa mambo ya nje na katika njia ya kufikiri ambayo kwa hakika sio ya kiroho.
Tatizo kama hili mtume Paulo alikutana nalo pia kwenye huduma yake yote! Alikutana na wahubiri ambao walikuwa wanatumia desturi za Agano la Kale kwa waumini wa kikristo ambao tayari walikuwa wamesha kuzaliwa upya kutoka juu. Wakawa wanafundisha kuwa yakupasa kutahiriwa! Yakupasa kuishika siku takatifu. Hupaswi kula kile na kile! Haya ni baadhi ya aina ya mambo ambayo walikuwa wakifundisha watu walioamini Yesu. Hebu niseme hivi, uwe makini, kwa sababu ni vyepesi sana mtu kuishi kimwili kuliko kuishi kiroho! Na hivyo ndivyo mafunfisho haya ya kileo yanavyo wafanyia watu.yanawaongoza watu kuishi katika mfumo wa kufikiri kimwili, na kuishi na kuwanyima maarifa ya kweli ya Mungu na ya nguvu za Roho Mtakatifu katika maisha yao.
Tafadhali kumbuka jambo hili, kuwa mambo muhimu yaliyoandikwa katika Agano la Kale ni mambo ya lazima na kimsingi yanayoonyesha picha au sura ya Yesu Kristo na kile ambacho atakifanya kwa ajili yetu kwa kifo chake pale Kalvari na kufufuka tena! Kwa hiyo kila kweli muhimu ipatikanayo katika Agano la Kale itapatikana pia katika Agano Jipya – lakini wakati huu inaelezea katika hali ya kweli ya kiroho kwamba mifano yote ya kimwili iliyotajwa katika Agano la Kale ilikuwa ni picha/sura yake.
Kama nilivyokwisha kusema aina hii ya mafundisho kwa ujumla wake inachanganya watu wanashindwa kulielewa hata Agano la Kale lenyewe. Kwa kifupi, karibu vitu vyote vilivyokuwa vikiwekwa wakfu kwa Mungu katika Agano la Kale ilijuwa ni picha/sura au yanatangulia kuelezea kile atakachokifanya Mungu kupitia Yesu Kristo, atakavyo tutakasa Yesu mwenyewe, atakavyo watakasa watu wake na kanisa lake. Hii ndiyo sababu mistari mingi ya neno la Mungu inayoelezea kuweka wakfu inafananishwa na kuweka wakfu kwa hema/hekalu ambalo lilitabiria au kuekezea mapema juu ya kanisa, au mwili wa Kristo (Waefeso 2:20-22), na kuwekwa wakfu kwa makuhani – na kama vile kwa sasa tunavyofahamu, tumefanyika hivyo kupitia damu yake Yesu na kwa Roho wake Mungu, ukoo mtakatifu wa kikuhani mbele za Mungu. Sadaka na wakfu za wanyana ambayo ndiyo inayowakilisha toleo la Yesu Kristo kwa ajili ya dhambi zetu!
Katika kitabu cha Kutoka ile sura ya 13, Mungu alisema kuwa kila uzao wa kwanza lazima uwekwe wakfu kwake. Kama tujuavyo nyakati zile za pasaka wazaliwa wote wa kwanza katika nchi ya Misri iliwapasa kuuawa kwa hukumu ya Mungu iliyopita juu ya nchi nzima kule Misri. Mistari hii ya neno la Mungu haikutolewa kwa ajili yetu, ili kutuweka tena katika aina fulani ya sheria kwamba inatupasa kuweka wakfu mashamba yetu, na nyumba zetu! Mistari hiyo na matukio yake yote yakiyotokea kule Misri inatuonyesha sisi tuone kuwa ulimwengu mzima uko chini ya hukumu ya Mungu na sisi tulioiamini Injili tumekombolewa kwa damu ya Yesu na tumeokolewa kutoka kwenye hukumu hiyo. Hiyo ndiyo maana halisi ya kiroho ya mistari ile ya Biblia. Hivi ndivyo inavyotumika kwetu leo. Hii ndio sababu tunaitwa kanisa la uzao wa kwanza (Waebrania 12:23; Warumi 8:29). Kuitumia ile sura ya 13 ya Kitabu cha Kutoka au sura ya 3 (ambapo Mungu alimwambia Musa ili kuwafundisha watu namna ya kuweka wakfu ardhi zao na nyumba zao ni sasa na kuitumia vibaya mistari hiyo ya neno la Mungu. Fundisho kama hilo linawafanya watu wakazie kufikiria mambo ya kimwili juu ya shughuli za kidini na inachochea hofu ya mioyo ya watu tu iwapo watashindwa kuyafanya mambo sawasawa. Jambo la pili, inawapora watu ule ufahamu wao wa kweli ya kiroho na kuwanyima nguvu za kiroho na baraka ambazo kweli hii inatuwakilishia. Jambo la tatu. Soma Agano la Kale! Ni mahali gani utaona panaelezea kuwa jambo hili la kuweka wakfu kwa Mungu ardhi, mashamba au biashara zao ambayo waliyanunua. Sasa eti, ilikuwa ni desturi/mila za kiyahudi kufanya hivyo? Hiyo haikuwa ni mila na desturi yao kamwe! Tuambie ni wapi unasoma kuwa eti hiyo sasa ilikuwa ndiyo tabia yao na desturi ambayo iliwataka wafanye hivyo katika Agano la Kale! Je, unaona jinsi makosa na hasa pasipo msingi wowote mafundisho ya aina hii yanapoharibu na yanavyoweza kukutumbukiza kwenye giza na vifungo tena!
Matukio yote muhimu katika Agano la Kale, na mambo ambayo Mungu aliwaamuru watu wake wayafanye, yote yanamwakilisha Kristo na Kile ambacho Mungu angekwenda kukifanya kupitia Kristo. Hivyo, Agano la Kale hunena juu ya Kristo!
Kama imeandikwa, “Basi torati, kwa kuwa ni KIVULI cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo…” (Waebr.10:1).
Mambo ya nje/kimwili ya Agano la Kale yalikuwa ni kivuli halisia cha kimwili inayoonyesha kweli ya kiroho na NGUVU ambayo Kristo angetupatia kutokana na kifo chake na ufufuo wake! Unaweza kuandaa meza nje ya nyumba yako na ukaandaa juu yake vyakula vizuri kama nini! Jua linawaka na huleta kivuli cha meza ile pamoja na chakula, kinaonekana ardhini. Sasa unaweza kujaribu kukila kile kivuli cha meza na vyakula vyake ambavyo vinaonekana pale ardhini chini ya ile meza halisia yenye vyakula! Kitatokea nini!? Ukijaribu kumega tonge lako kwenye kile kivuli, mkono wako hautaambulia kitu, au utaishia kumega tonge la mchanga tu kwenye mkono wako! Je, unaweza kuishi kwa jinsi ya namna hii? Utawaita rafiki zako pamoja na majirani na kuwaambia, “Karibuni tule kivuli cha chakula hiki kizuri sana!” Kwa vyovyote hutafanya hivyo kwa maana utakufa! Ikiwa utajaribu kuishi kutokana na kivuli cha chakula, UTAKUFA. Tendo la kula vivuli vya vitu halisia, haitakuweka hai! Lakini sasa hivyo ndivyo vilevile wanavyofanya wahubiri hawa wanapotutaka tufuate mifumo ya majukumu ya nje ya kidini tu. Wanayaua maisha ya kiroho ya wale wanaowahubiria.
Je, unaona hapo? Mambo mengi ambayo Mungu aliwaagiza Waisrael wayafanye yalikuwa ni kiwasilisho cha Kristo na kile ambacho anakuja kutufanyia – ilikuwa ni KIVULI na kiini cha kweli cha nguvu ya maisha halisia ya kiroho ambayo Kristo yalikuwa anaenda kutuletea kupitia wokovu wake. Kristo yeye mwenyewe ni chakula chetu – ile mana ambayo Waisrael waliila, na yale maji waliyokunywa yaliyotoka kwenye mwamba kule jangwani – na hiyo nayo yote ilimwakilisha Yesu. (1Wakor.10:1-4). Kwa nini sasa unataka urudi nyuma kula vivuli, au mavumbi ya ardhini? Kwa nini basi mtu ahubiri kivuli wakati kile kitu halisia kinapopatikana?
Kutahiriwa kwa sasa haifanyiki kimwili bali ni kiroho (Warumi 2:29). Kutahiriwa kwa nje (yaani kimwili) inawakilisha wokovu wetu kutoka dhambini ambao Kristo ameuleta kupitia kifo na kufufuka kwake (Wakolosai 2:11). Kule kuvuka kwa wana wa Israel kupitia bahari ya shamu inawakilisha ubatizo wetu katika Kristo (1 Wakor.10:1,2). Damu ya kondoo iliyopakwa kwenye miimo na kizingiti za milango ya nyumba za Waisrael kule Misri, hiyo inanena juu ya Kristo kwa ajili ya UKOMBOZI WA ROHO ZETU kupitia damu yake – kamwe haiwakilishi aina yoyote ya hirizi ambayo unaitumia leo kufunika nyumba yako kwa damu ya Yesu kana kwamba damu yake hirizi ya kiuchawi! Kuharibika kwa Wamisri kwenye bahari ya Shamu inawakilisha ushindi wa Yesu dhidi ya nguvu ya shetani pale Kalvari; kutolewa kwa sheria za Musa pale mlima wa Sinai inawakilisha utoaji wa Roho Mtakatifu siku ile ya Pentekoste. Kuhani Mkuu inamwakilisha Kristo. Dhabihu za hema/hekalu zinamwakilisha Kristo; madhabahu inawakilisha msalaba wa Yesu; mikate ya wonyesho pamoja na vinara kwenye hekalu inamwakilisha Kristo (Yoh.6:35; 8:12). Hekalu linawakilisha Kanisa au mwili Wa Kristo (Waefeso 2:22). Kiti cha Rehema hewani/hekaluni kinawakilisha Krsto Yesu! (Warumi 3:25; 1 Yoh.2:2). Nakadhalika, nakadhalika, nakadhalika.
Msoamji mpendwa, ikiwa unapenda kujua kuhusu ‘uwekaji wakfu’ kwa dhati, basi soma kitabu cha Warumi.12:1,2; inasema,
“Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”
Tafakari pia 2 Wakorintho 5:14,15, inayosema, “Maana upendo wa Kristo watubidisha, maana tumehukumu hivi ya kwamba mmoja alikufa kwa ajili ya wote, ili waliohai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao mwenyewe, bali kwa ajili yake yeye aljyekufa akafufuka kwa ajili yao.”
Hayo ni mafundisho ya Agano Jipya yahusuyo ‘uwekaji wakfu’ na dhabihu. Hii hapa ndiyo kweli halisi ya Injili ihusuyo uwekaji wakfu wako. “Au hamjui yakuwa miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu mwenyewe, maana mlinunuliwa kwa thamani, sasa basi mtukuzeni Mungu katika miili yenu.” (1 Wakor.6:19-20).
Tumenunuliwa kwa bei, yenye thamani kubwa, kwa damu ya thamani ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu! Sisi si mali yetu wenyewe tena bali tu mali yake Kristo, na chochote unachokimiliki ni mali yake Kristo. Tunapaswa kujikabidhi wenyewe kwa Mungu na kumuishia yeye siku kwa siku, na maisha yetu yanatakiwa yawe ni sadaka kwa Mungu, tunapo kuwa majumbani, tunapokuwa makazini mwetu, popote pale, na kila mahali. ( 2 Wakor.2:14-16).
Kama unapenda kuongelea jambo lihusulo ‘kuweka wakfu’, basi hiyo sasa ndiyo wakfu ya kweli, ni wakfu pekee ambayo unapaswa kuijua na kumuishia Mungu katika maisha yako yote. Mungu ametununua ili tuingie katika mahusiano binafsi pamoja naye ambayo yanaingia ndani zaidi kuliko wajibu wowote ule wa nje wa kidini ambayo twaweza kuingizwa ndani yake!
Unaona sasa jinsi mafundisho ya kidini yanayokazia na kulenga mambo ya nje yanavyokupeleka mbali na mahusiano yako na Yesu Kristo. Yanakupeleka mbali zaidi ya nguvu ya Injili, na namna Injili ilivyokusudiwa kukubadilisha maisha yako. Aidha, inakuondoa mbali na imani yako katika Kristo na nguvu zake katika maisha yako na inakuongoza ili uweke matumaini yako kwenye mambo ya nje / ya kimwili, kana kwamba mambo hayo ndiyo yatampendeza Mungu au uweze kukubaliwa naye! Kwa hiyo Paulo anasema, “kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya.” (Wagalatia 6:15). Kuwekeza matumaini yako katika mifumo ya nje ya kidini tu, haitakusaidia chochote, kabisa. Tunatakiwa tufanyike kuwa viumbe vipya katika Kristo Yesu, na tuishi kwa imani na kwa uzima wake ndani yetu kama Paulo alivyosema, “Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.” (Wagalatia.2:20).
MAWAZO YA MWISHO
Sasa kama unayo mashamba yako, na kunatokea hali ya hewa kuwa mbaya, kwa ujumla nafahamu wazi kuwa kama utaomba kwa Bwana alinde au atunze mazao yako. Hili ni jambo la tofauti na tunachoongelea hapa. Hata hivyo, kama wewe unafikiri inakupasa kuomba kila siku ili kwamba Bwana apate kulinda mashamba yako na penginepo hata kuyafunika kwa damu ya Yesu, basi kwa hakika haupo kwenye imani, wewe upo kwenye woga, unaendeshwa na hofu, wala huishi katika nyakati hizi za Agano Jipya la neema na upendo wa Mungu, unaishi katika mifumo ya kiushirikina.
Hali kadhalika, ikiwa utanunua nyumba au shamba, kumshukuru Mungu kwa kuwezesha kupata mali hizo, je, hiyo siyo kielelezo cha mahusiano yako na Mungu? Je, hatuvipati vitu hivyo kutoka kwenye mikono yake? Tukijua kwamba ni yeye ndiye atulindaye na kutubariki? Huhitaji ‘sheria’ yoyote wala ‘amri’ yoyote ili kukuambia ufanye hivyo! Kufanya tendo kama hilo inapasa iwe ni hali ya kawaida tu kwetu kufanya kama wana wa Baba yetu, kumshukuru yeye kwa maongozi yake kutupatia vitu katika maisha yetu.
Je, mtume Paulo hasemi jambo linalofanana na hili katika nyaraka zake kwenye 1 Timotheo 4? Anataja pale kuwa watajitokeza watu ambao watawafundisha kuwa usioe, na kwamba usile aina fulani fulani ya vyakula, “wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli. Kwa maana kila kiumbe cha Mungu ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokewa kwa shukrani; kwa kuwa kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba.” (1Timoth4:3-5). Je, hatumshukuru Mungu kwa vyakula tunavyo kula? Ndiyo, kwa sababu ni yeye Mungu ndiye aliyeviumba na alitupatia vyakula na ametangaza kuwa jambo kama hili ni Jema (soma Mwanzo 1:29; 9:3). Naye ndiye anayetujibu maombi yetu, “utupatie leo mkate wetu wa kila siku.” Na katika Agano Jipya ile tofauti ya vyakula visafi na visivyovisafi imeondolewa, na watu wanaweza kula vyakula vya aina zote kwa kuwa Mungu mwenyewe amevifanya safi (amevitakasa ) kwa neno lake – Mathayo 15:11; Matendo 10:15; 15:28,29; Warumi 14:6. Hivyo maombi yetu ya shukurani ni ukiri wetu wa mambo haya na yanatakasa vyakula vyetu tunavyovitumia – kama vile Yesu mwenyewe alivyoshukuru kwa vyakula alivyokula na akawashirikisha na wengine (Mathayo 14:19; Marko 8:6).
Kama vile nilivyokwisha kusema kwamba mambo kama haya yanapaswa yawe ni kielelezo cha kawaida kinachoonyesha mahusiano yetu na Mungu ambayo hayawajibiki kwa lolote lile katika kuzifuata baadhi ya hatua za majukumu ya kidini
– ni kielelezo cha mahusiano yetu na Mungu aliyesema, “Maana kama lile la kwanza lingalikuwa halina upungufu, nafasi isingalitafutwa kwa lile la pili. Maana, awalaumupo, asema Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, Nami nitawatimizia nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda Agano Jipya; HALITAKUWA KAMA AGANO LILE nililoagana na baba zao, katika siku ile nilipowashika mikono yao niwatoe katika nchi ya Misri. Kwa sababu hawakudumu katika agano langu, Mimi nami sikuwajali asema Bwana. Maana hili ndilo agano nitakaloagana na nyumba ya Israeli Baada ya siku zile, asema Bwana; Nitawapa sheria zangu katika nia zao, na katika mioyo yao nitaziandika; Nami nitakuwa Mungu kwao, nao watakuwa watu wangu. Nao hawatafundishana kila mtu na jirani yake, Na kila mtu na ndugu yake, akisema, Mjue Bwana; Kwa maana wote watanijua, tangu mdogo wao hata mkubwa wao.”
Unaona sasa! Kupitia Agano Jipya, na kupitia toleo lake kwetu la Roho Mtakatifu, Mungu ametufanya tuwe ni watoto wake ili kwamba tupate KUMJUA, toka wadogo hadi wakubwa katikati yetu! Mpaka hapo, haumhitaji MTU yeyote yule kukuelezea kuhusu mambo maalum, au hatua za kisiri anazozijua yeye tu, na kwenye Biblia hazipo, ambazo inakupasa uzichukue kutakasa au kuweka wakfu mali zako, au juu ya kitu kingine chochote kile. Ikiwa jambo kama hilo hulioni likiandikwa kwenye Agano Jipya, kwa nini basi unataka kuingiza kanuni mpya, na kwa nini basi unataka kurudi nyuma kuzifuata njia za Agano la Kale, njia ambalo kwa mujibu wa Mungu mwenyewe, imeshindwa?
Uzima Wa milele ni nini? Yesu mwenyewe anatueleza hapa, “Na uzima wa milele ndio huu, WAKUJUE wewe, Mungu wa pekee wa kweli na Yesu Kristo uliye mtuma.” (Yoh.17:3). Mungu hajakubatiza wewe katika mtiririko/mfuatano wa majukumu ya kidini ya mifumo ya nje, bali yeye amekubatiza ( iwapo tayari umebatizwa) katika Mwanae kupitia Roho Mtakatifu ili kwamba upate KUMJUA YEYE, na NGUVU za uzima wake ndani yako! Mfumo wa kukazia na kulenga mambo ya nje itakunyang’anya kweli hii muhimu na nguvu zake katika maisha yako.
Kwa hiyo, mpendwa msomaji, “Katika ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa.” (Wagal.5:1).
© David Stamen 2017 somabiblia.com
Unaweza kudownload somo hili kwa kubofya link ifuatayo: JUU YA MFUMO WA KUIWEKA WAKFU ARDHI NA NYUMBA YAKO