RSS

NDIYO DHAMBI

‘Waumini’ wengi wanadai umaskini wa ndugu zao katika Kristo unatokana na 1) DHAMBI zao (au hawaishi karibu na Mungu); au 2) unatokana na mambo fulanifulani katika ULIMWENGU WA KIROHO (na kwamba inawapasa watu hao kugundua hali zao hizo za kiroho na “kuzifunga” kabla hata hujaleta “kufunguliwa” kwao kutoka kwenye ufukara wao); au 3) unatokana na upungufu wa maarifa na MTAZAMO MBOVU (na ni lazima wabadili mtazamo wao tu ili kuacha hali ya umaskini).

Sasa, wapi Yesu au mitume katika Agano jipya wanasema au wanafundisha mawazo kama hayo? Hamna! Yote ni uongo na udanganyifu tu. Ni wapi ambapo Yesu au mitume WANAWAKEMEA watu wake maskini kwa ajili ya umaskini wao? Hamna! Hamna hata mstari mmoja! Wapi Agano Jipya linafundisha kwamba waumini maskini ni maskini kwa sababu ya dhambi zao? Hamna. Wapi Agano Jipya linafundisha kwamba waumini maskini ni maskini kwa sababu ya ulimwengu wa kiroho? Hamna hata mstari mmoja! Wapi Agano Jipya linafundisha kwamba waumini maskini ni maskini kwa sababu ya na upungufu wa maarifa na mtazamo mbovu? Hamna hata mstari mmoja! Wapi Agano Jipya linafundisha kwamba waumini maskini ni maskini kwa sababu ya kosa fulani lao? Hamna hata mstari mmoja! Vipi watu wenye akili wanavyoweza kusema na kufundisha makosa hayo? Ni kwa sababu ya kupenda fedha tu. Kupenda fedha mioyoni mwao kunawafanya wawe vipofu juu ya mambo yaliyo wazi katika Biblia, wapo vipofu juu ya  mafundisho ya Biblia. Wanajaribu kutetea madai matupu yao kwa mantiki ya kibinadamu kwa kunukuu mistari fulani ovyo ovyo tu bila kujali muktadha lakini KWA SEHEMU KUBWA SANA HAWAJALI mambo yale Biblia inayoyafundisha kwa wazi!

Kaitka Agano Jipya, badala ya kuwakemea waumini maskini, jambo la kukusanya pesa kwa ajili ya kuwapa waumini waliokuwa wakiishi maisha ya dhiki au wale walio kuwa ni masikini lilikuwa ni JAMBO LA KAWAIDA. Makanisa katika Agano Jipya, sio tu wao waliwatunza na kuwasaidia washirika masikini bali waliwafundisha jinsi gani wakristo WATATAKIWA KUFANYA HIVYO. (Wagal. 2:10; Matendo 2:45; 4:34; 11:29; Warumi 12:13; 15:26; 1 Wakor.16:1,2; 2 Wakor. 8:7; 9:1; Wahebr.6:10; Yakobo 1:27; 1 Yoh 3:17). Ukisoma Agano Jipya, utaona kwa ujumla pesa zilikusanywa kwa ajili ya washirika maskini! Sasa, wapi Paulo au Petro au Yesu aliwaambia waumini maskini kwamba umaskini wao ni matokeo ya dhambi zao, au shida katika ‘ulimwengu wa kiroho’, au mtazamo mbovu? Hamna! Usipokubali, naomba utoe mstari mmoja kutoka Agano Jipya. Petro alimwambia Paulo ‘awakumbuke maskini’ (Wagal.2:10). Kwa nini? Kuwakemea au kuwashauri juu ya umaskini wao? HAPANA! Ila kusanya pesa makanisani kwa ajili ya washirika maskini!

Jambo moja ni wazi, Biblia INAONYA dhidi ya uvivu – 2 Wathesalonike 3:10 na Mithali 6:10,11. Biblia inafundisha uvivu zinaweza kuleta umaskini, lakini hiyo inatokea katika Biblia kama MAONYO KWA UJUMLA, kama tunavyoona katika mistari niliyoinukuu. Pia, Mungu aliwaonya na kuwakemea TAIFA LA ISRAEL juu ya KUABUDU SANAMU KWAO na aliwaambia hali ya unyonge yao ilitokana na dhambi zao za KUMWACHA MUNGU (Kumbukumbu 28).

LAKINI MUNGU HAKUWAKEMEA WATU WAKE MASKINI KWA SABABU YA UMASKINI WAO, WALA KATIKA AGANO LA KALE, WALA KATIKA AGANO JIPYA. Tafute tu! Tuambie ni wapi!

BADALA YAKE, KWA SEHEMU KUBWA SANA BIBLIA NZIMA inathibitisha uhalisi wa maisha (the realities of life), yaani, wapo ndugu maskini na watakuwepo ndugu maskini na tunatakiwa kuwahurumia na kuwasadia – siyo kuwakemea na kuwadharau!

“Na ikiwa ndugu yako AMEKUWA MASKINI, na mkono wake umelegea kwako, ndipo UTAMSAIDIA. (Walawi 25:35). Kwa maana MASKINI HAWATAKOMA KATIKA NCHI MILELE; ndipo NINAKUAMURU na kukuambia, MFUMBULIE kwa kweli mkono wako nduguyo, MHITAJI WAKO, MASKINI WAKO, katika nchi yako.” (Kumbu.15:11). “Kwa maana MASKINI MNAO SIKUZOTE PAMOJA NANYI; bali mimi hamnami sikuzote.” (Yoh.12:8.) Hata Yesu na mitume walichukua mfuko kwa ajili ya maskini! (Yoh.13:29).

Biblia inathibitisha ukweli huo, yaani, watakuwepo waumini maskini miongoni mwetu. KWA HIYO, MUNGU MWENYEWE anasema, “Amdharauye mwenzake AFANYA DHAMBI; Bali AMHURUMIAYE MASKINI ana heri… Amwoneaye maskini HUMSUTA MUUMBA WAKE; Bali yeye AWAHURUMIAYE WAHITAJI HUMHESHIMU… Azibaye masikio yake asisikie kilio cha maskini, Yeye naye atalia, lakini hatasikiwa… Mwenye jicho la ukarimu atabarikiwa; MAANA HUWAPA MASKINI CHAKULA CHAKE… MWENYE HAKI huyaangalia madai ya maskini; BALI MTU MBAYA hana ufahamu hata ayajue….” (Mithali 14:21,31; 21:13; 22:9; 29:7 ).

Na Mungu aliwapa watu wake maagizo juu ya jinsi ya kuwasaidia ndugu zao maskini, “lakini mwaka wa saba utaiacha nchi ipumzike na kutulia; hao maskini miongoni mwa watu wako WAPATE KULA… Kama akiwapo mtu maskini pamoja nawe, nduguzo mmojawapo, ndani ya malango yako mojawapo, katika nchi yako akupayo Bwana, Mungu wako, USIFANYE MOYO WAKO KUWA MGUMU, wala usimfumbie mkono wako nduguyo maskini;” (Kutoka 23:11 na Walawi 25:35; Kumbu 15:7).

Na Agano Jipya linakubaliana na hayo kabisa, “ila neno moja tu walitutakia, tuwakumbuke maskini; nami neno lilo hilo NALIKUWA NA BIDII KULIFANYA. …Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona NDUGU YAKE ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! UPENDO WA MUNGU WAKAAJE NDANI YAKE HUYO?” (Wagal.2:10; 1 Yoh.3:17).

Sasa je, wewe una BIDII kulifanya lile lile, yaani, kuwakumbuka maskini, kama Petro na Paulo walivyofanya? Kama wewe usipowasaidia ndugu zako maskini, upendo wa Mungu wakaaje ndani yako?

Ulimwengu wote wanatambua ukweli huo, yaani, umaskini wa watu wengi unaweza kutokana na mazingira yao, na ukame, na sababu mbalimbali, na siyo kosa lao. Inatokeaje ni baadhi ya wakristo tu ambao hawatambui mambo hayo yaliyo wazi? Inatokeaje wengi wa wakristo hao hao wasemao mambo hayo ni wenye elimu ya juu!? Tutawezaje kueleza ishara hii? Wengi, kwa sababu ya kupenda pesa kwao WANAFANYA MIOYO YAO IWE NGUMU, na wanadai umaskini wa ndugu zao ni matokeo ya makosa fulani yao! Kupenda fedha mioyoni mwao kunawafanya wawe vipofu juu ya mambo yaliyo wazi katika Biblia, na katika maisha. KWA MADAI MATUPU wanajipatia sababu kutokuwasaidia ndugu zao maskini na zaidi ya hayo wanazuia wengine kufanya hivyo! Hiyo ni dhambi kubwa mbele ya Mungu na wao wanawatenda dhambi ndugu zao maskini.

Usiulize, “Je, ina maana lazima watu wa Mungu wabaki maskini? Je, ni dhambi kuwa tajiri? Je, ni mapenzi ya Mungu watu wake wawe maskini?” Je, moyo wako unataka nini???  Je, hujaelewa yaliyoandikwa hapo juu? Jiulize mwenyewe kwa makini mbele ya Mungu KWA NINI unauliza maswali hayo kwa upesi! Ya kwanza, katika somo hili sijishughulishi na maswali hayo! Ya pili, je, unataka sheria au kanuni juu ya umaskini na utajiri pale ambapo neno la Mungu lenyewe halijishughulishi na maswali hayo moja kwa moja! Nini inafanya kazi ndani ya moyo wako? Je, neno la Mungu halitoshi kwako? Soma neno la Mungu. Pokea neno la Mungu. Ishi kwa neno la Mungu. Tafuta ufalme wa Mungu na haki yake kwanza, na mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.  

Wengine wanadharau ndugu zao maskini na huruma ya Mungu wakisema mambo ya ujinga na udanganyifu kama yafuatyo, “Umaskini hauleti utukufu kwa Mungu! Biblia haishabiki umaskini. Umaskini si sifa ya Wokovu. Utajiri ni mapenzi ya Mungu!” Wanaongea kama hawajasoma Biblia au kama wanafuata dini nyingine! Je, kwa mfano, hawajasoma mstari ufuatao?

“Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao?” (Yakobo 2:5).

Inawezekana mstari ambao tumeshasoma unahusu watu kama hao, yaani, “MWENYE HAKI huyaangalia madai ya maskini; BALI MTU MBAYA hana ufahamu hata ayajue.”

Inaonekana ni muda watu wengi wabadili mtazamo wao, na hata watubu sana.

Hiyo si neno kwa wote. Imenihuzunisha sana kusoma mambo yale watu kadhaa waliyoyaandika kwenye mtandao na nilipenda kuweka wazi mambo yale Biblia inayofundisha juu ya hayo. Sijui nimeshinda kwa kiasi gani lakini natumaini niliyoyaandika yatawasaidia baadhi ya watu!

© David Stamen  2016                   somabiblia.com

 

Comments are closed.

 
%d bloggers like this: