RSS

Dalili za Mtumishi wa Mungu kwelikweli

– Mtumishi wa Mungu hawatawali washirika wa kanisa.

“Yesu akawaita, akawaambia, ‘Wafalme wa Mataifa huwatawala,…na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini kwenu ninyi sivyo; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote.” (Luka 22:25; Marko 10:42-44).

Mtumishi wa kweli hajifanyi kama ‘Bwana’ juu ya watu wa Mungu – hajiinui juu ya washirika kama ‘rais’ wa watu. Kumbuka, Bwana Yesu, Mwana wa Mungu, alisema ‘KWENU NINYI SIVYO’. Mchungaji huharibu sura ya Yesu machoni pa watu kama akitawala kama ‘mkuu wa kijiji’ juu ya washirika; ameacha tabia ya Yesu kama anajifanya ‘mkubwa’ kanisani. Hayo yote ni kosa kubwa sana. Kama mchungaji akiwatawala watu kwa nguvu, ndipo yeye hafuati Yesu. Paulo aliandika juu ya huduma yake, “Si kwamba tunatawala imani yenu; bali tu WASAIDIZI wa furaha yenu… Kwa maana hatujihubiri wenyewe, bali Kristo Yesu ya kuwa ni Bwana; na sisi wenyewe kuwa tu WATUMISHI WENU kwa ajili ya Yesu.” (2 Wakor.1:24; 4:5).

Mtume Petro aliwaandikia wazee/wachungaji ifuatyo: “lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. WALA SI KAMA WAJIFANYAO MABWANA JUU YA MITAA YAO, bali kwa kujifanya VIELELEZO kwa lile kundi.” (Waebr.13:2,3). Inapaswa mtumishi wa Mungu awe kielelezo kwa washirika na siyo kujifanya ‘Bwana’. Bwana Yesu ametufundisha inapaswa awe ‘mtumishi’ au ‘mtumwa’ wa washirika!

– Kwa sababu ya upendo wake kwa kunid la Bwana, mtumishi wa Mungu yupo tayari kutoa maisha yake kwa ajili ya kundi la Bwana hata kama Yesu Kristo alivyofanya, “nasi tukiwatumaini KWA UPENDO MWINGI, tuliona furaha kuwapa, si Injili ya Mungu tu, BALI NA ROHO ZETU pia, kwa sababu mmekuwa wapendwa wetu.” (1 Wathes.2:8). Kwa hiyo…

– Mtumishi wa Mungu kwelikweli anawatumikia washirika kwa upole and unyenyekevu:

“bali tulikuwa wapole katikati yenu, kama vile mlezi awatunzavyo watoto wake mwenyewe… mimi Paulo mwenyewe nawasihi kwa upole na utaratibu wa Kristo; mimi niliye mnyenyekevu nikiwapo pamoja nanyi” (1 Wathes.2:7; 2 Wakor.10:1).

– Kwa maneno na matendo yake mtumishi wa kweli hachukizi dhamiri za washirika – dhamiri zao zinamshuhudia kwamba mwendo wake ni safi kabisa katika sehemu yote!

“tumekataa mambo ya aibu yaliyositirika, wala hatuenendi kwa hila, wala kulichanganya neno la Mungu na uongo; bali kwa kuidhihirisha iliyo kweli twajionyesha kuwa na haki, DHAMIRI ZA WATU ZIKITUSHUHUDIA MBELE ZA MUNGU…Ninyi ni mashahidi, na MUNGU PIA, jinsi tulivyokaa kwenu ninyi mnaoamini, kwa utakatifu, na kwa haki, bila kulaumiwa;  (2 Wakor.4:2; 1 Wathes.2:10). 

Hakuna sababu kumlaumu! “Tusiwe kwazo la namna yo yote katika jambo lo lote, ili utumishi wetu usilaumiwe.” (2 Wakor.6:3). Na hata Mungu ni shahidi mwendo wake! (1 Wathes.2:5).

– Mtumishi wa kweli wa Mungu HATAFUTI fedha zako. HATAMANI pesa zako wala hatakulazimisha umpe pesa kwa ajili ya huduma au maombi yake.

“Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu.” (Matendo 20:33). Huyu ni mtumishi wa Mungu kwelikweli.

– Mtumishi wa Mungu HATAFUTI kujifanya mtajiri kupitia huduma yake kwako.

“Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho.” (Mat.3:6). Mtume Petro pamoja na mitume wengine walipokea pesa nyingi sana kwa ajili ya waumini maskini lakini, kumbe, hawakuchukua pesa kwa ajili ya faida yao kujifanya matajiri! Hawakuishi kwenye nyumba ya fahari wala hawakuwa na walinzi wa binafsi. (Au unafakiri Petro au Paulo wangeweza kuwa na magari mengi ya gharama kubwa sana au kuishi katika nyumba ya fahari au kuwa na ndege ya binafsi kama ‘wahubiri’ wengine siku hizi? Je, unafikiri kuishi kwa fahari kama hiyo inawakilisha tabia ya Yesu Kristo?) Mitume wa Bwana walikuwa na moyo safi na walifanya huduma yao bila unyonyaji, “Maana hatukuwa na … maneno ya juujuu ya kuficha choyo; Mungu ni shahidi.” (1 Wathes.2:5). “Basi thawabu yangu ni nini? Ni hii, ya kuwa nihubiripo, nitaitoa Injili bila gharama, bila kutumia kwa utimilifu uwezo wangu nilio nao katika Injili.” (1 Wakor.9:18).

Neno la Mungu ni dhidi wachungaji ambao wanawahudumia watu Wake kwa ajili ya faida zao, kujitajirisha wenyewe. “Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wachungaji wa Israeli, wanaojilisha wenyewe; je! Haiwapasi wachungaji kuwalisha kondoo? …Mnawala walionona, mnajivika manyoya, …lakini hamwalishi kondoo.” Ezekieli 34:2,3.

– Mtumishi wa Mungu HATAFUTI vyake mwenyewe.

“Maana wote wanatafuta vyao wenyewe, sivyo vya Kristo Yesu.” Tutambue, Paulo anasema ‘wote’! Basi, kwa uhakika maana yake ni idadi isiyopungua ‘wengi’! Ina maana, watumishi wengi/wote (ila Timotheo) walitafuta vyao wenyewe! Walitumia huduma yao kwa ajili ya faida yao yenyewe. Jambo la kuhuzunishwa sana! Je, ni tofauti sana siku hizi?

– Mtumishi wa Mungu HATAFUTI kuwapendeza watu, hasemi mambo kwa kusudi la kuvuta watu kanisani kwake ili ajenge kanisa kubwa kwa ajili ya sifa yake.

“Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza wanadamu, singekuwa mtumwa wa Kristo.” (Wagal.1:10). “Kama vile tulivyopata kibali kwa Mungu tuwekewe amana Injili, ndivyo tunenavyo; si kama wapendezao wanadamu, bali wampendezao Mungu. Maana hatukuwa na maneno ya kujipendekeza wakati wo wote, kama mjuavyo.” (1 Wathes.2:4,5).

– Mtumishi wa Mungu HATAFUTI sifa ya watu. “Hatukutafuta utukufu kwa wanadamu, wala kwenu, wala kwa wengine.” (1 Wathes.2:6). 

– Mtumishi wa Mungu HAVITAFUTI vitu vyako … wala faida yake! Anatafuta faida ya kiroho ya waumini.

“Maana sivitafuti vitu vyenu, bali nawatafuta ninyi…” 2 Wakor.12:14. Maneno ya ajabu! Mtume wa kweli anajitoa kwa ajili ya faida ya kiroho ya washirika!  Paulo alipenda waumini, siyo ‘vitu vyao’! Hatafuti vitu vyao, pesa zao, sifa zao au utukufu kwa watu! Mtumishi wa Mungu anajitoa kwa ajili ya faida ya wale awahudumiao. Anayo nia moja tu, “Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi.” (2 Wakor.11:2). Naye yupo tayari kujimwaga kwa ajili ya watu wa Mungu ili wapate faida ya kiroho, “Nami kwa furaha nyingi nitatapanya, tena nitatapanywa kwa ajili ya roho zenu. Hata kama kadiri nizidivyo kuwapenda sana, ninapungukiwa kupendwa.” (2 Wakor.12:15).

Maneno ya kuchanga moto! Mtumishi ya Mungu huzidi kuwapenda waumini awahudumiao hata hivyo anapungukiwa kupendwa!

– Mtumishi anamtegemea Mungu kwa ajili ya mahitaji yake.

“Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; MAANA NIMEJIFUNZA KUWA RADHI NA HALI YO YOTE NILIYO NAYO. Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; KATIKA HALI YO YOTE, na katika mambo yo yote, nimefundishwa KUSHIBA NA KUONA NJAA, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.” (Wafilipi 4:11-13).

– Mtumishi wa Mungu hufurahi kwa ajili ya waumini wanapotambua ni jambo la haki na la pendo kumsaidia mtumishi ambaye anafanya kazi mbele ya Mungu kwa ajili yao.

“Nalifurahi sana katika Bwana, kwa kuwa sasa mwisho mmehuisha tena fikira zenu kwa ajili yangu, kama vile mlivyokuwa mkinifikiri hali yangu lakini hamkupata nafasi….Lakini mlifanya vema, mliposhiriki nami katika dhiki yangu…. hakuna kanisa lingine lililoshirikiana nami katika habari hii ya kutoa na kupokea, ila ninyi peke yenu. Kwa kuwa hata huko Thesalonike mliniletea msaada kwa mahitaji yangu, wala si mara moja. SI KWAMBA NAKITAMANI KILE KIPAWA, bali nayatamani mazao yanayozidi kuwa mengi, KATIKA HESABU YENU. Lakini ninavyo vitu vyote na kuzidi, tena nimejaa tele; nimepokea kwa mkono wa Epafrodito vitu vile vilivyotoka kwenu, HARUFU YA MANUKATO, sadaka yenye kibali, IMPENDEZAYO MUNGU.”

Ndiyo. Paulo alikuwa na mahitaji na alipokea kile kipawa kwa ajili ya MAHITAJI yake (SIYO KWA AJILI KUMFANYA MTAJIRI) kwa furaha – lakini siyo kutokana na uchoyo au tamani yake apate fedha, lakini alifurahi KWA AJILI YA WAUMINI TU. Katika utoaji wao Paulo alitambua matunda ya pendo katika maisha yao ambayo ni kama harufu ya manukato impendezayo Mungu! Alifurahi kwa ajili ya hayo tu! Tena ni wazi hapo kwamba mtumishi wa Mungu hawalazimishi waumini wamtoe pesa. Anafurahi waumini watoe kipawa kwa hiari kutokana na pendo la Mungu mioyoni mwao!

Ni kweli kabisa, na neno la Mungu linatufundisha kwamba ni jambo la haki na la pendo kuwasaidia watumishi wa Mungu SAWASAWA NA MAHITAJI YAO kama wanajitoa kwa ajili yetu. Lakini ndani ya moyo wa mtumishi wa Mungu kwelikweli hamna uchoyo au tamani kwa pesa, kwa sifa, kwa kujiinua, kwa kujifanya mtajiri au kuishi kwa fahari, wala hawalizimishi watu wa Mungu kumpa pesa.

© 2016  David Stamen    somabiblia.com

KUPAKUA SOMO HILI BONYEZA LINK IFUATAYO:  DALILI KADHAA YA MTUMISHI WA MUNGU

Unaweza kusoma na kusikiliza zaidi kupitia links hapo chini:

https://somabiblia.wordpress.com/huduma-na-pesa/

https://somabiblia.wordpress.com/mambo-ya-zaka-utoaji-sadaka-fungu-la-kumi-na-pesa/

https://somabiblia.wordpress.com/uongozi-na-wachungaji-wa-kweli-semina-ya-viongozi/

 https://somabiblia.wordpress.com/utoaji-na-kikiumi-jambo-la-unyonyaji/

 

Comments are closed.

 
%d bloggers like this: