Huduma na Pesa.
HUDUMA NA PESA
Katika kitabu cha Matendo ya Mitume sura ile ya tatu na mstari wa sita, tunasoma kitu chenye nguvu sana. Petro na Yohana walikuwa wanakwenda hekaluni kuomba na wakakutana na mtu mmoja ambaye alikuwa ni kiwete. Alikuwa akiomba omba na kutegemea kupata pesa toka kwao, lakini mtume Petro alisema maneno haya ya kushangaza sana, “Mimi sina dhahabu wala fedha…” Je, ni watu wangapi leo ambao wanajiita mitume, manabii au hata wachungaji katika miji mikubwa, wanao uwezo wa kuyasema maneno haya yakiwa na chembe yoyote ya ukweli? Kwa Petro na Yohana maneno haya yalikuwa ni kauli ya ukweli kuhusiana na hali yao. Kwa upande mwingine, ni jambo la kushangaza kabisa pale tunapowaza kuhusu baadhi ya watu leo, ambao wanasema wanatumika kama mitume, manabii au hata wachungaji, wanajikusanyia kiwango kikubwa cha utajiri kwa ajili yao wenyewe kupitia huduma. Lakini haikuwa hivi kwa mitume wa Agano Jipya. Hawakujikusanyia kiango kikubwa cha mali kwa ajili yao wenyewe wala kujitajirisha kwa kupitia huduma ambayo Mungu amewapa. Tunasoma katika kitabu kile cha Matendo ya Mitume sura ya pili na nne kwamba waamini wapya waliuza nyumba na mali walizokuwa wakimiliki na kuleta pesa na kuziweka miguuni kwa mitume. Mitume lazima walikuwa wakipokea kiwango kikubwa sana cha fedha! Walizifanyia nini hizi pesa? Walichukua kiasi gani kwa ajili yao wenyewe? Katika matendo 2:44,45 na 4:34,35 inasema kwamba pesa ziligawanywa kwa masikini, kutokana na uhitaji wao. Sikia kile mtume Paulo alisema baada ya miaka mingi ya huduma, kwenye Matendo 20:33, alisema kwa wale aliokuwa akiwahudumia, ”sikumuomba (au ‘sikutamani’) mtu yoyote anipe fedha, dhahabu wala nguo….” Ni neno zuri kiasi gani hili! Haya ni madhihirisho ya vitendo kabisa, kwenye kanisa na katika ulimwengu, ya asili ya Yesu Kristo kupitia maisha ya mtu.
Sio kwamba tu mitume katika Agano Jipya hawakujitajirisha kwa pesa, majumba makubwa na mavazi mazuri, hawakudiriki hata kutamani fedha za watu waliokuwa wakiwatumikia! Hii ni ya kustaajabisha sana! Hawa ni watumishi hasa wa Mungu. Hawajitafutii wenyewe kwa faida yao bali kwa ajili ya Yesu Kristo na kanisa lake! Mtume Paulo alisema kitu cha kushangaza kwenye kitabu cha Wafilipi katika sura ile ya pili. Anasema, “… Wote wanajitafutia kwa ajili yao na wala si kwa ajili ya Yesu Kristo”. Haya ndiyo aliyoyaona katika wakati wake na hakuna shaka ilimuumiza sana moyo wake, hivyo basi hatpaswi kustaajabu pale mambo yale yale yanapotukia kati yetu, hiyo ni kwamba, wapo wale wanaoitumia huduma kwa faida zao binafsi, kujikusanyia pesa, majumba, nguo nzuri za kifahari, na magari. Paulo anasema katika sura hiyo hiyo kuwa hayupo mtu mwingine kama Timotheo ambaye ataangalia hali yenu kwa halisi na kwa kweli. Na je, hili sio hitaji kubwa leo, kwamba tunahitaji watu ambao hawataangalia na kujijali wenyewe tu kwa faida zao, ambao hawatafuti kuzijenga huduma zao kwa sababu ya kujikusanyia utajiri wao wenyewe, bali watu watakaojitoa nafsi zao kwa ajili ya kazi ya Bwana, kwa watu wa Bwana na faida yao tu?
Wapo watu leo wanaotumia huduma kujenga majengo makubwa ya makanisa kwa ajili yao. Wanavaa mavazi mazuri yenye thamani kubwa sana kwa sababu wanadhani kimakosakwamba hiyo inaonyesha Baraka za Mungu na hiyo ndiyo alama ya maisha ya kiroho yenye mafanikio! Na wanajaribu kushawishi na wengine kufikiri hivyo. Mtu mmoja wa namna hiyo toka Marekani aliwaomba wafuasi wake na waamini wengine kuchangia mamilioni ya dola za kimarekani ili yeye aweze kununua ndege itakayomuwezesha kusafiri sehemu mbalimbali duniani kwa urahisi zaidi kwenda kuhudumu. Mtu mwingine akitokea katika nchi ya Kenya, anasafiri na msafara wa magari ya kifahari sana na kikundi kikubwa cha ngoma kikiwa mbele yake kikipiga muziki; maelfu ya watu wakijipanga mitaani na kumshangilia akielekea kwenye uwanja mkubwa ambapo maelfu pia wanamsubiri; akatoka kwenye gari lake la gharama na watu wake wanaomlinda wakiwa wamemzunguka na unaweza kudhania yeye ni Rais wan nchi! Amejiweka kuwa mtu wa muhimu sana, amejiinua! Anajiita nabii lakini hatusomi hivyo kwenye Agano Jipya! Unaweza tu kutafakari kama Petro na Paulo wangejiweka hivyo? Mtu mwingine toka nchi ya Nigeria, anasema yeye anayo maji maalum ya miujiza ambayo yanao uwezo wa kuponya watu na kufukuza roho wabaya. Mtu huyu anajaribu kutetea vitendo vyake kwa kurejea kwa mtume Paulo amabe vitambaa vilivyotoka kwake vilichukuliwa na kusambazwa kwa watu waliokuwa wagonjwa. Lakini mtume Paulo hakupata faida yoyote kutokana na vitambaa hivyo, hakutaka kupewa pesa kwa ajili ya vitambaa hivyo; vitambaa vilipelekwa kwa yeyote aliyekuwa na mahitaji, haikuwa ni lazima kwa muhitaji kuhudhuria mikutano ya Paulo ili avipate hivyo vitambaa! Lakini kwa mtu huyu, yote haya yamekuwa kweli! Haya maji yanatumika kunadi huduma yake. Kwa nyakati pesa imekuwa ikitakiwa; nyakati nyingine unaweza tu kuyapata maji kwa kuudhuria mikutno yake au kwa kununua moja ya bidhaa zake! Hii ni biashara. Hii sio huduma. Hii ni kujitengenezea faida tu, si kuwatumikia watu wa Mungu. Katika kitabu cha Matendo ya Mitume sura ile ya nane, mtu aitwaye Simoni alidhania ya kuwa vipawa vya Mungu vyaweza kununuliwa kwa pesa. Hivi ndivyo Petro alimwambia, “pesa yako ipotelee mbali na wewe mwenyewe, kwa sababu umedhania ya kuwa vipawa vya Mungu vyaweza kununuliwa kwa pesa…moyo wako hauko sawa mbele za Mungu” (Matendo 8: 20-21). Mioyo yetu pia haikuwa sawa mbele za Mungu kama tutafikiri ya kuwa Baraka za Mungu tunaweza kuzinunua kwa pesa! Mtu mwingine mwenye huduma ya kimataifa alikuja katika jiji la Dar Es Salaam na mwishonni mwa mafundisho ya jioni na maombezi kwa wagonjwa, akawataka watu watoe pesa kwa ajili ya kuitegemeza huduma yake. Akawaambia maelfu ya watu waliokuwa wamekusanyika pale kwamba Mungu hana haja na sarafu zao bali anataka noti! Hii ndiyo sababu Paulo alisema kuwa wote hawa wanatafuta kwa ajili yao na wala sio kwa ajili ya Kristo! Rafiki yangu mmoja ambaye ni Mtanzania akaniambia kwamba alikimbia toka kwenye huo mkutano kwa sababu hakuwa na noti ya kutoa na alidhani kuwa mtu huyu alikuwa mtu wa Mungu na anaongea maneno ya Mungu, hivyo akaogopa kwa kuwa hakuwa na noti ya kutoa kwenye huduma ya mtu huyo! Mtu yeyote asemaye au hata kukupigia kelele pale kunapokuwa na makusanyo kwamba Mungu havutiwi na utoaji wa sarafu bali noti, hamuwakilishi Yesu Kristo na hamtumikii Yesu Kristo, anajitumikia yeye mwenyewe. Inakuwaje mtu ambaye ametokea Marekani anaweka shinikizo kwa watu masikini wa Tanzania, wengi wao wana pesa kidogo au hawana kabisa, kutegemeza huduma yake na noti toka kwenye mifuko yao? Hii ni biashara na ni udanganyifu na sio huduma ya Yesu Kristo.
Bila shaka tunaweza kuzitegemeza huduma na kuwapa pesa wale wanaoifanya kazi ya Mungu. Ni jambo la haki kutoa bila shinikizo kwa wale wasio na kazi kwa sababu wanajihusisha na huduma ya Bwana na kuwajali na kuwatumikia watu wa Mungu kwa moyo. Tunasoma katika Agano Jipya kwamba Paulo alipokea matoleo ya aina hiyo toka kwa waamini wengine. Lakini utoaji huu ulikuwa ni kwa ajili ya mahitaji ya lazima kama chakula na malazi, haikuwa kwa ajili ya kumtajirisha ili awe na uwezo wa kununua nguo za gharama na kuishi kwenye jumba la kifahari au kitu chochote kinachofanana na hayo. Wala Paulo hakumuwekea shinikizo mtu yeyote kutegemeza huduma yake. Kumbuka Petro alisema, “sina pesa wala dhahabu…”, na Paulo akasema,” sikuchukua pesa wala dhahabu wala nguo toka kwa mtu yeyote.” Mbeleni Paulo anatuambia katika Matendo na 1 Wakorontho ya kwamba alifanya kazi ya mikono yake kujitegemeza mwenyewe ili aweze kuifanya Injili iwe bure kwa watu wote! Ni tofauti kiasi gani na watu wengi leo ambao wanataka kujitengenezea nafasi, heshima za kitaifa na kimataifa, ambao wanajijengea ufalme kupitia huduma zao, kupitia majengo makubwa sana ya makanisa huku wakiishi katika majumba makubwa ya gharama sana na kuendesha magari ya kifahari na kuvaa mavazi mazuri. Hatusomi vitu kama hivyo kwenye Agano Jipya, isipokuwa kuhusu wale ambao waligeuka kinyume na Mungu na kukimbilia umaarufu na pesa (2 Tim 4:10). Lakini kama ilivyokuwa kwenye siku za Paulo ndivyo ilivyo hata leo. Sio tu watumishi na manabii wa uongo ambao wanapotosha wengine, lakini wapo wanaopenda kudanganywa kwa sababu wanapenda vitu visivyo sahihi!
Sikia kile Paulo alisema katika kitabu cha 2 Wakor. 11:20, “…maana mwachukuliana na mtu akiwatia utumwani, akiwameza, akiwateka nyara, akijikuza, akiwapiga usoni”. Mtume Paulo anawaambia waamini Wakorintho kwamba wana mtazamo usio sahihi kabisa. Kufikiri kwao kulikuwa ni kwa kidunia na kimwili! Walidhani kwamba kama mtu akijiita mtume au nabii, inamaanisha ni ‘mtu muhimu wa Mungu’ na kwa hiyo ana nguvu juu yao na anastahili kusifiwa na anastahili pesa na kuwatawala vyovyote vile apendavyo, kwa sababu ni ‘mtu wa Mungu’! Tatizo ni kwamba mtazamo wao wa mtu wa Mungu ulikuwa sio sahihi kabisa! Yesu alifundisha kwamba yeyote atakaye kuwa wa kwanza ni lazima awatumikie wengine na sio kutawala wengine! Wakorintho wengine hawakumtambua Paulo kama mtume kwa sababu tu hakutaka pesa toka kwao! Akawauliza swali hili kwenye 2 Wakor. 11:7, “Je! Nalifanya dhambi kwa kunyenyekea ili ninyi mtukuzwe, kwa sababu naliwahubiri Injili ya Mungu bila ujira?” Unaweza kufikiri? Watu wanakuwa na shaka kama mtu ni mtume kwa sababu tu hakuwaomba pesa! Lakini ilikuwa tu kama kwenye kanisa la Korintho ndivyo ilivyo kwa baadhi ya watu leo! Mtazamo na motisha wa wakorintho ulikuwa si sahihi kabisa. Walipenda ‘nafasi’, walipenda ‘nguvu’, walipenda swala la ‘mafanikio’. Hivyo waliwapenda kuwapokea na kuwasikiliza watu waliojiinua na kuinua nafasi zao na walioonyesha kufanikiwa na kudai pesa toka kwa watu waliowahudumu.
Ni sawa sawa kabisa na yanayotokea duniani kote siku za leo! Paulo anawaambia baadhi ya Wakorintho kwamba wanadanganyika na yeye anaogopa kwa ajili yao. Anawatahadharisha kuwa kwa sababu wanapenda mambo yasiyo sahihi, na kwa hilyo shetani anapata nafasi ya fursa ya kuwahadaa! Anawaeleza pale katika kitabu cha 2 WaKor 11 kwamba wako tayari, kwa sababu ya nia zao mbaya, kumpokea Yesu mwingine, roho mwingine na Injili nyingine! Hili ni onyo kali sana analowapa. Kupenda kwao kwa mafanikio na kile wanachodhani kuwa ni huduma yenye nguvu kumepita kiasi na inawahadaa. Na Paulo alisema nini katika sura hiyo hiyo kuhusiana na watu wanaojiinua kwa namna hii? Anasema, ”…hao ni mitume wa uongo, watendakazi wadanganyao, wanaojifanya ya kuwa ni mitume wa Kristo. Na si ajabu; kwa kuwa shetani mwenyewe hujifanya malaika wa nuru, hivyo basi, sio jambo gumu kwa watumishi wake kujifanya kuwa ni watumishi wa haki; mwisho wao utakuwa sawa sawa na kazi yao.” (2 Wakor. 11:13-15). Hili sio jambo la mchezo! linaweza kuwa ni swala la umakini zaidi. Shetani kuwadanganya Wakristo – kuwadanganya wote kuanzia kwa wahubiri mpaka wale wanaowasikiliza – kwa sababu ya misukumo yao mibaya na kufikiri kwao kusiko sahihi. Jinsi ya kufikiri kwa watu hutegemea sana shauku zao mbaya na mitazamo yao mibaya, na sio kwa neno la Mungu wala maandiko! Niliona video ya mtu mmoja mwenye kanisa kubwa pale katika nchi ya Afrika ya Kusini. Anavaa mavazi ya gharama kubwa sana na kuendesha magari ya kifahari sana huku akiwa amezungukwa na walinzi pande zote. Anauza bidhaa zake kwenye kanisa lake na watu wanadhani watabarikiwa tu kwa kununua bidhaa hizo, vitu hivyo ni kama nguo na vifaa vya nyumbani. Kama utanunua bidhaa yoyote kwa kudhani tu itakubariki, basi umekwisha kudanganyika na unafanya dhambi pia. Ni jambo moja kupata au kununua kitabu cha kikristo au CD yenye ujumbe wakikristo, ambayo inaweza kukubariki sana kwa kusoma ama kusikiliza, lakini ni jambo tofauti kabisa kununua nguo ama kifaa cha nyumbani eti kwa sababu tu kinauzwa na mtu ambae unadhani kuwa ni mtu wa Mungu na hivyo unadhani kwa kutumia kifaa hicho utapata Baraka kwenye maisha yako! Mtu huyo anafanya biashara na kupata faida toka kwako na wewe umedanganyika na unafanya dhambi kwa sababu unadhani ya kwamba Baraka za Mungu zaweza kununuliwa kwa fedha. Katika video hiyo, mshirika mmoja wa kanisa hilo alisema kwamba yeye anataka kumfuata muhubiri aliyefanikiwa, ambaye ana fedha nyingi, avaae nguo za gharama na kutembelea magari ya kifahari. Anasema anataka kumfuata mtu ambaye amefanikiwa kupata kitu maishani mwake kwa sababu na yeye pia anataka apate kitu na awe mtu mwenye mafanikio! Hana haja ya kumfuata mtu aishiye maisha ya kawaida tu. Anataka mafanikio, ni kwa jinsi gani mtu mwenye maisha ya kawaida atamsaidia maisha yake yaweze kwenda mbele! Alikuwa akiongea kana kwamba hajawahi kusoma Biblia kabisa! Alikuwa akiongea na kuonesha ya kwamba hafahamu kabisa mafundisho ya Agano Jipa. Lakini kutokuelewa huku na kujidanganya hakuletwi na ukosefu wa elimu. Huletwa na shauku mbaya zitokazo mioyoni mwetu! Sikiliza Paulo anayoyasema, ‘…watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, huku wakidhani ya kuwa utauwa ni njia ya kupata faida. Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa….tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi. Bali wewe, mtu wa Mungu, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa, imani, upendo, saburi, upole.’ (1 Tim.6:5-11).
Kama ilivyokuwa kwenye kanisa la Korinto siku zile za Paulo, ndivyo ilivyo hata leo. Wakristo walio wengi wataamini karibu kila asemacho muhubiri kama tu ataonyesha anaweza kufanya miujiza. Japokuwa, fumo wa maisha ya muhubiri ni muhimu zaidi kuliko hata miujiza ambayo anaonekana akifanya. Hili linadhihirishwa na Mwana wa Mungu pale aliposema, ”Wengi watasema siku hiyo, Bwana Bwana, je hatukutabiri kwa jina lako? Na kwa jina lako hatukutoa pepo? Na kwa jina lako hatukufanya kazi nyingi za kustaajabisha? Na mimi nitawajibu, siwajie nyie, ondokeni kwangu, enyi watenda kazi wa uovu”. (Mathayo 7:22-23). Ile tu kwamba mtu anaonekana anafanya miujiza haitoshi kumfanya kuwa mtu wa Mungu na kukufanya umfuate. Kama mtu huyu anajikusanyia utajiri binafsi kwa ajili yake yeye mwenyewe na anatafuta kujikweza mbele ya watu wengine na kujijengea ‘ufalme’ wake mwenyewe, huyu hamuwakilishi Yesu Kristo. Baadhi ya Wakorintho walipenda kuona maajabu, vitu visivyo vya kawaida na miujiza, lakini shauku yao iliyopita kiasi ya vitu hivyo iliifanya mioyo yao kwenda njia isiyo sahihi na kumpa shetani mwanya wa kuwadanganya!
Usifuate wahubiri wa namna hiyo kama unathamini nafsi yako mbele za Mungu. Kumbuka kwamba Yesu alisema, ”Mungu awajua mioyo yenu: kwa kuwa kilichotukuka kwa wanadamu huwa chukizo mbele za Mungu.” (Luka 16:15). Soma neno la Mungu, lifuate, lipende, sikiliza watu wanaolihubiri hilo tu; sikiliza wale wanaomuhubiri Kristo na kusulubiwa kwake tu! Sikiliza toka kwa watu kama Timotheo, ambaye kwa dhati ya moyo wake alikuwa akijali nafsi za watu na sio kutafuta faida yake mwenyewe toka kwa watu – hata kama mtu kama huyo atapatikana kwenye dimbwi la matope, fuatana na mtu huyo ahubiriye Kristu na kuishi Kristu!
Bila shaka tunamshukuru Mungu kwa uponyaji na miujiza, lakini kamwe usiruhusu kupenda kwako vitu hivyo kukufanye usahau ama kupuuzia vitu vile ambavyo Biblia inafundisha kwa uwazi mkubwa, kinyume cha hapo utadanganywa na kupotezwa.
Hasa katika nchi maskini mabapo maisha ni magumu, hawa walimu na wahubiri wa uongo huamsha watu kuamini katika matumaini yasiyo ya kweli na kuweka ahadi za uongo kwa kutumia maandiko vibaya ili wapate wafuasi na kujitengenezea faida toka kwa hao wafuasi. Wanahubiri maswala ya kufikiri kwa usahihi, na wanawafanya makutano kurudia rudia kauli zao kuhusiana na hali zao za sasa na za baadaye; wanatumia maandiko vibaya kuwafundisha watu jinsi ya kuwa na mafanikio katika maisha yao, wakiwatia moyo kwamba watakuwa na biashara zilizofanikiwa na kwamba watakutana na watu sahihi wa kuwasaidia kusonga mbele kwenye maisha. Wakati wa mahubiri hayo, muhubiri huinua hisia na matumaini ya watu, hivyo mara nyingi wasikilizaji hunyanyuka juu kwa ghafla na kupiga kelele na kupunga mikono yao juu kwa sababu wanaamini, au wanajaribu kuamini ya kwamba Mungu atawainua toka kwenye hali zao au kuwafanikisha katika maisha yao
Huwahitaji waalimu wa uongo. Yesu alisema kwamba kama utautafuta kwanza ufalme wa Mungu, chochote kile unachokiitaji utazidishiwa. Lakini inaonyesha ya kuwa wengi wanataka zaidi ya yale ambayo Yesu alifundisha.
Kitabu cha Wafilipi 4:13 Mtume Paulo anasema ya kwamba, ‘anayaweza yote katika Kristo amtiaye nguvu!’ Hii ni kauli ya kustaajabisha! Je! Unaamini hayo Paulo aliyoyasema? Sikiliza kile alisema katika mstari uliyotangulia, ”najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yoyote, na katika mambo yoyote nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa”! Ni mambo haya ambayo Paulo anaweza kuyafanya kupitia Kristo! Je hali ikoje kwetu mimi na wewe? Au unataka wahubiri wakuambie ni kwa kiasi gani utakwenda kufanikiwa; wakwambie ni kwa namna gani biashara yako inakwenda kufanikiwa; wakwambie kwamba unakwenda maeneo maishani mwako na kwamba mambo yatakwenda kukuendea vizuri? Kama ni hivyo, basi huyaelewi maneno ya mtume Paulo wala asili ya Yesu Kristo. Je! Unadhani ya kuwa mtume Paulo alifuata ‘mafanikio’? Kama tutafata mafanikio, tutakuwa hatumfuati Yesu. Ni jambo moja kuwa na ushabiki na Yesu kwa kuwa unaamini atakubariki katika hili ama lile. Na pia ni jambo jingine kabisa kujikana nafsi yako na kumfuata Yesu na kuachia maisha yako yajayo katika mikono yake kabisa! Neon la Mungu linatufundisha, ”mtegemee BWANA kwa moyo wako wote na wala usizitegemee akili zako. Katika njia zako zote mkiri yeye, naye atakuongoza njia zako.” Mithali 3:5-6
Ukifuatisha ndoto zako, unajipendezesha wewe mwenyewe tu. Kama utamfuata Yesu, utampendeza yeye. Ukifuatisha ndoto zako basi unajitumikia mwenyewe. Ukimfuata Yesy utamtumikia yeye na kanisa lake. Ukifuatisha ndoto zako unajitengenezea nia kwa ajili yako mwenyewe. Ukimfuata Yesu, ataandaa njia kwa ajili yako.
Kama vile nilivyosema hapo juu, bila shaka tunaweza kutoa pesa kwa wale wanaomtumikia Bwana na watu wake. Utoaji huo unatakiwa kuwa wa hiari ya mtu kabisa, toka moyoni, na bila shinikizo lolote la kutoka nje! Katika Agano Jipya tunaona kwamba mtume Paulo alisaidiwa kwa mfumo huo na wakristo wengine katika baadhi ya nyakati. Lakini hakuwahi kuyaomba matoleo hayo wala kuwawekea shinikizo watoaji waweze kumtegemeza kifedha. Aliliweka hili wazi kwenye 1 Wakor 9.
Kwenye Agano Jipya tunasoma kwamba karibu makusanyo yote yaliyokuwa yakikusanywa toka kwa waamini kwenye makanisa yalikuwa yakisambazwa kwa waamini maskini. Kwenye 1 Wakor. 16, Paulo anaainisha kwamba waamini wanapaswa kutoa fedha katika siku ya kwanza ya juma (hiyo ilikuwa Jumapili), kulingana na kiwango ambacho Mungu amewafanikisha na alisema kwa uwazi kuwa hizo pesa ilikuwa ni kwa ajili ya waamini maskini. Haikuwa ni kwa ajili ya mchungaji, japokuwa kanisa linaweza kuamua kumtegemeza mchungaji wao kupata mahitaji ya msingi kama hana kazi, lakini utoaji huo haupaswi kutumika kumtajirisha mchungaji ama kumfanya awe tajiri zaidi ya makutano. Na pia utoaji huo unatakiwa kuwa wa hiari kutoka moyoni. Hakuna mtu yeyote mwenye haki ya kuchukua makusanyo ya Jumapili na kuyafanya yake binafsi! Mtu huyo anafanya biashara kanisani na kuwanyonya watu wa Mungu.
Kama vile nimesema awali, kwenye Agano Jipya, kwa njia ya kufundisha na kwa mifano, wakristo katika kanisa la kwanza walikusanya fedha ili kuwasaidia waamini maskini. Matendo 2:44,45; 4:34,35; 11:29,30; 20:33-35; Warumi 12:13; 15:35,26; 1 Wakor. 16:1,2; 2 Wakor. 8:1-7; 9:1,2; 1 Yohana 3:17.
Ndio, tunaweza kuwategemeza wale wafanyao kazi kwa ajili ya Bwana, na hatutakiwi kumuacha mchungaji ambae anatuhudumia vizuri katika Bwana ateseke kwa kukosa mahitaji ya msingi ya maisha, lakini tunatakiwa kutambua na kutosahau ya kuwa mzigo mkubwa wa kanisa la kwanza ulikuwa ni kuwasaidia wale waamini maskini zaidi ambao walikuwa wanapata shida hata kupata yale mahitaji ya msingi kabisa ya maisha. Kutokana na Agano Jipya, hili ndilo hasa eneo ambalo makusanyo yetu ya kawaida yanatakiwa kuelekezewa huko. Mungu aiongoze mioyo yetu katika mambo haya ili tuweze kutoa kwa hiari na kwa moyo wenye furaha na kuwasaidia wale waamini ambao wanahitaji hasa msaada wetu.
© David Stamen 2014 somabiblia.com
Kupakua somo hili bonyeza link: HUDUMA NA PESA
Pascal Nyangi
June 22, 2015 at 11:22 am
somo hili ni zuri limelipenda na lafaa kwa mafundisho hasa kwa ajili ya watumishi hapa tz