RSS

SIYO SAWA! MAMBO YA NDOA

“Ndipo Sarai akamtesa Hagari (Hajiri) hivyo akamtoroka.” (Mwanzo 16:6).

Ndipo malaika wa BWANA akamwambia Hagari, ‘‘Rudi kwa bibi yako ukajishushe chini yake.’’ (Mwanzo 16:9).

Mungu hutazamia tulitii neno lake. Alimwagiza Hagari arudi kwa Sarai haijalishi tabia ya Sarai jinsi ilivyo! Je, pengine ungeweza kusema hapo, ‘Si mapenzi yangu, bali Yako yatendeke’? Sarai alikuwa amemtesa Hagari sana (kwa sababu Hagari alipata mimba kupitia Abramu) lakini Bwana alimwambia Hagari ajishushe chini yake! Tafakari hilo! Labda ungefikiri agizo hili la Mungu siyo sawa! Kwa nini napaswa kujishusha chini yake anayenitesa?! Lakini kusudi la Mungu ni kuwa mapenzi yake yatimizwe duniani (na uzima wa Kristo uumbike ndani yetu – Wagal.4:19) kutokana na shida na majaribu yale tunayoyapita. Kwa hiyo pengine Mungu hajali kabisa hali ya shida yetu ili aweze kudhihirisha utukufu Wake ndani yetu na kutimiza mapenzi yake duniani. Tafakari maisha ya Yusufu! Shida na mateso yake yalileta baraka kubwa sana na wokovu kwa ajili ya familia yake, na watu wa Mungu, na kwa mataifa!

Mungu alimwonyesha Yusufu kupitia ndoto kwamba atamkweza na atatawala juu wengine. Lakini neno la Mungu linatufundisha kitu cha muhimu juu ya njia Mungu anayoitumia ili kutumiza lengo lake kwenye maisha ya Yusufu – na hata maishani mwetu! Linasema, “Hata wakati wa kuwadia neno lake, Ahadi ya Bwana ilimjaribu.” (Zaburi 105:19). Ilimjaribu Yusufu kwa njia gani? Kwa njia ya shida na mateso, “Yusufu aliuzwa utumwani. Walimwumiza miguu yake kwa pingu, Akatiwa katika minyororo ya chuma.” (Zaburi 105:17,18). Kumbe. Mungu alimuahidi Yusufu baraka, na akapata mateso! Unafikiri hiyo siyo sawa? Lakini Yusufu alimpenda Mungu sana kuliko baraka! Alimwamini Mungu wakati akipita shida na mateso. Na imani hiyo ilikuwa imani ya kweli. Kwa nini ninasema hiyo? Kwa sababu imani yake ilimpelekea ‘kunyenyekea chini ya mkono wa Mungu ulio hodari na kujidhili mbele za Bwana’ (Yakobo 4:10; 1 Petro 5:6) – akiamini Mungu atamkweze na kumkuza wakati Wake! Yusufu alivumilia mambo yote na mateso yote kwa ajili ya neno la Mungu na kwa sababu ya imani yake Kwake Mungu! Na wewe, na mimi?

Inaonekana kuwa waumini wengi hawatambui mambo yale yatakayowaletea baraka ya dhati ya Mungu!

Malaika aliahidi Hagari, “Hakika nitauzidisha uzao wako, wala hautahesabika kwa jinsi utakavyokuwa mwingi.” (Mwanzo 16:10). Lakini kwanza lazima ‘ajishushe chini ya Sarai.’ Ki-Msingi Mungu hajali ‘raha’ yetu. Lengo lake ni kutimiza mapenzi Yake na kulitukuza jina Lake – kwa njia Yake – katika maisha yetu. Tukimruhusu kufanya hivyo, tukimtii, tukinyenyekea chini mkono Wake, tutabarikiwa kupita kiasi kwa baraka za dhati, za milele!

Wakati waumini wengine wanapopitia shida wanaweza kufikiri watu wametumwa na shetani kuwasumbua. Wanasema, ‘Huyo ni shetani.’ Labda ni kweli, labda sivyo! Yusufu aliweza kufikiri ndugu zake walikuwa wanalitimiza kusudi la shetani, lakini haikuwa hivyo! Mungu alikuwepo katika mambo yote yaliyotokea juu ya Yusufu! Kimsingi, kusudi la Mungu lilikuwa linatimizwa na siyo mapenzi ya shetani! Sasa, badala ya kupokea neema zaidi ili waweze kuvumilia matatizo, waumini wanaomba sana Mungu aondoe ‘kazi ya shetani’! Lakini katika matukio hapo juu, Mungu alisema, ‘‘Rudi kwa bibi yako ukajishushe chini yake.’’ Labda angejibu, ‘Lakini Sarai ni mtu mkali! Ananichukia!’ Haidhuru. ‘‘Rudi tu kwa bibi yako ukajishushe chini yake.’’ Labda angeendelea kwa kulalamika, ‘Siyo sawa! Atanitesa tena!’ Haidhuru! ‘‘Rudi kwa bibi yako ukajishushe chini yake.’’

Petro ana mambo ya muhimu sana kutufundisha juu ya mateso. Sikiliza kwa makini na yaingie mioyoni mwetu sana – kiasi cha kubadilisha nia yetu, na maisha yetu,

“Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya. …Lakini mjapoteswa kwa sababu ya haki mna heri. Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike; bali mtakaseni Kristo Bwana mioyoni mwenu.” (1 Petro 3:17,14).

“Basi wao wateswao kwa mapenzi ya Mungu na wamwekee amana roho zao, katika kutenda mema, kama kwa Muumba mwaminifu.” (1 Petro 4:19).

“Lakini kustahimili, mtendapo mema na kupata mateso, huu ndio wema hasa mbele za Mungu.” (1 Petro 4:19).

Je, tunafikiri mioyoni mwetu, ‘Siyo sawa.’ Ujue, Mungu wetu, Baba yetu hutaka kuondoa lalamiko hili – ‘Siyo sawa!’ – kutoka katika mioyo yetu!

Tunaweza kufikiri mazingira yetu au hali ya shida ni ‘adui’ yetu, au huyu au yule ni ‘adui’ yetu, na tunaanza ‘kupigana’ na mazingira yetu, na tunakataa kujishusha chini ya mapango na mapenzi ya Mungu – kwa sababu hatuchukui muda mbele ya Mungu ili tutambue mapenzi yake! Yokobo alisema, “Ninyi mmenipokonya watoto wangu. Yusufu hayupo na Simeoni hayupo, tena na sasa mnataka kumchukua Benyamini. Kila kitu ni kinyume yangu!” (Mw.42:36). Unaona? Yakobo alifikiri mazingira yake yalikuwa kinyume yake naye alipigana na mazingo na hali ya mazingira yake, yaani, alikataa kabisa kumwacha Benyamini aende Misri na alipinga ushauri wa watoto wake! Alifikiri hali ya ukame, matukio haya yote na watoto wake ni ‘maadui’ yake! ‘Kila kitu ni kinyume yangu!” Kwa sababu ya kujipendeza (wakati ule) alikataa kujishusha chini ya matukio hayo (ambayo yaliwakilisha mapenzi ya Mungu kwake!); kwa sababu ya kujipendeza hakuweza kutambua mpango wa Mungu katika mambo hayo yote! Matokeo ya tabia hiyo ni taabu, mahangaiko, huzuni, uchungu na malalamiko moyoni mwetu! ‘Siyo sawa! Kila kitu ni kinyume yangu!’ Lakini ilikiwa kinyume chake! Mungu alikuwa anayatumia mambo yale yote ili kumwongoza Yakobo na watoto wake waingie katika baraka kupita kiasi! Mwishoni Yakobo alijishusha chini ya matukio yale.

Ndugu, tusiwe vipofu kwa sababu ya kujipendezesha wenyewe, kwa sababu sisi wenyewe tunataka ‘kutawala’ juu ya mazingira yetu kama Yakobo alivyofanya. Nimewaona watu (waumini) wengi ambao wanajisumbua sana, wanalalamika, wanajihangaika wenyewe sana tena sana bila sababu ya dhati kwa sababu hawapendi, hawataki kujishusha chini ya mkono wa Mungu. Wanashindana na mazingari yao. Hawapendi kabisa kuistahamili hali inayoonekana kuwapinga, kuvumilia kuteswa! Wanaacha kumtegemea Mungu na kujitoa Kwake, na wanajitahidi na wanajishughulisha sana kuitengeneza tengeneza au kuibadilisha hali ya mazingira yao kwa kutumia mbinu hiyo au mbinu ile! Hawana ‘raha’ mpaka wanajisikia ‘wanatawala’ juu ya mambo! Ni kana kwamba wanataka kuwa Mungu katika mambo yanayotokea!

Wengi wanataka Mungu aiondoe shida yao. Naelewa. Lakini ni lazima sana pia tujue maana ya kweli ya maneno ya Paulo na uzoefu wa Paulo anaposema, “Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia.” (Warumi 5:3). (Nilipofundisha mistari hii katika kanisa fulani lilipo Dar Es Salaam, mtafsiri wangu ghafla alinikatiza akiniambia kwa Kiingereza, ‘Washirika hawapendi kusikia mambo haya juu ya ‘dhiki’!)

Wakati mwingine mapenzi ya Mungu siyo kubadilisha mazingira yako au watu karibu nawe, mapenzi ya Mungu ni kukubadilisha wewe, ili ‘ufananishwe na mfano wa Mwana wake’ na uwe ‘manukato na harufu ya Kristo mbele ya Mungu.’ Hiyo ni mapenzi ya Mungu kwa ajili yako na yangu! Je, kufurahi katika dhiki kwa sababu tunapenda dhiki? Hapana. Ni kwa sababu, “MKIJUA ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini; na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi.” (Warumi 5:3-5). Unaona, lengo la Mungu kupitia mambo yote ni upendo! Kwa hiyo Paulo anatangaza, “TWAJUA ya kuwa katika MAMBO YOTE Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia MEMA, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.” (Warumi 8:28). Je, tunaamini mstari huo? Je, tunayajua mambo hayo kama Paulo alivyojua? Au unajaribu kupigana na mambo yale yanayoonekana kuwa kinyume yako au kupinga unalotaka?

‘Mume wangu ni mtu mgumu.’ Haidhuru. (Hapa naongea juu ya Wakristo na juu ya mambo ya kila siku, ya kawaida tu.) Mungu hakuambii kumpenda mume wako kwa sababu yeye ni mkamilifu! Neno la Mungu linakuambia kumpenda mume wako na kumtii ili udhihirishe tabia na Roho Yake duniani,  “uyapambe mafundisho ya Mwokozi wetu Yesu” (Tito 2:10) katika mambo yote na kuitimiza mapenzi Yake!  ‘Mke wangu ni mtu mgumu!’ Haidhuru. Mungu hakuambii kumpenda mke wako kwa sababu yeye ni mzuri na mwenye upole kila wakati au mkamilifu! Mungu anatuagiza wewe na mimi tuwapende wake wetu na tusiwe na uchungu nao! Lakini waweza kusema ‘mke wangu hanitii kila wakati!’ Kwa kweli? Utafanyaje? Je, umpige mke wako kwa fimbo ili akutii? Au je, utapiga kelele ukimwamuru lazima kukutii kwa sababu ya Wakolosai 3:18? Mungu anatuambia, ‘Mpende na usiwe na uchungu naye!’ Sasa wewe Unasema, ‘Sio sawa! Siyo haki!’ Labda. Lakini ukitafuta lile lililo ‘sawa’ na ‘haki’ kwa ajili yako mwenyewe, kwa nini unataka kumfuata Yule aliyeziacha ‘haki’ zake kwa ajili ya wenye dhambi kama wewe na mimi? Unafikiri ni sawa kama Bwana Yesu akikuacha kabisa sasa hivi ubaki bila Mwokozi kwa sababu wewe siyo mkamilifu nawe inawezekana wakati wengine humtii? Unasemaje?

Mungu amekuita kumpenda mke wako, “kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake.” Utafanyaje?

““Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake. Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake. Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki.” (1 Petro 2:21-23).

Mume na mke, wote wawili wanaweza kulalamika juu ya mwingine, na kubishana na kupiga kelele na kuacha neema, upendo na amani  – kwa sababu wanafikiri ‘haki’ ipo upande wao! Tunapaswa, kwa ajili ya upendo mkuu ya Mungu kwetu, tuwe na nia ya Yesu Kristo ‘aliyejikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki.’ Usiitafute ‘haki’ kwa ajili yako, mtafute Yesu; utafute uzima wake uwe ndani yako; itafute nia Yake…

“Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu;ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu,… bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.” (Wafil.2:5-8).

Kwa nini watu wanayo shida kubwa katika ndoa zao? (Siongei juu ya dhambi mbaya hapo; naongea juu ya upungufu wa neema, rehema, msamaha na upendo). Kwa sababu hatutaki kujinyenyekeza chini ya mkono wa Mungu! Mume na mke wanaweza kulaumiana na kugombana, kila mmoja akidai yeye anayo haki, badala ya kila mmoja peke yake “…akaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili apewe rehema, na kupata neema ya kumsaidia wakati wa mahitaji…” (Waebr.4:16). Kwa sababu ya kiburi changu, ninakasirika; kwa sababu ya kijipendezesha kwangu, ninachukizwa; kwa sababu ya kujipenda, ninao uchungu na ninajihurumia mwenyewe! ‘Sitaki kufa (pamoja na Kristo) na kujitoa maisha yangu yawe ‘manukato na harufu ya Kristo mbele ya Mungu’ (Wakor. 2:14,15)! Hiyo siyo nia ya Yesu. Mapenzi ya Mungu ni kuwa maisha yangu na yako nyumbani na kazini yanayo harufu na manukato ya Yesu kwa Baba? Kumbe, kama Mungu katika Agano la Kale alimwambia Hagari ‘‘Rudi kwa bibi yako ukajishushe chini yake,’’ na alitazamia afanye hivyo, kwa uhakika Mungu anaweza kutazamia nimpende mke wangu, umpende mume wako – hata kama tabia yake siyo kamilifu, hata kama pengine analofanya halinipendeza! Tunaimba ‘Yote yanawezekana.’ Ni kweli ndugu yangu, ni kweli dada yangu! Yote yanawezekana maishani mwangu na maishani mwako kwa neema Yake aliyesema, “Neema yangu yakutosha.” !

Unaamini hiyo? Labda unajibu, ‘Ndiyo, naamini Mungu anaweza kubadilisha mume wangu, mke wangu!’ Ngoja. Sikumaanisha hiyo. Namaanisha kuwa unaamini Mungu anaweza kubadilisha wewe? Mungu anatazamia sisi tubadilike. Mungu alitoa Mwanawe msalabani ili kubadilisha maisha yetu kabisa, kwa hiyo Yeye anasema kwa maandiko,

Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya; tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.” (Waefeso 4:31,32)

Mungu hutazamia kuwa tumtii, tuchague lililo jema,

Mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli. (Waefeso 4:22-24). Na tena,

“Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana…Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu. (Wakol.3:12-14).

Tunayo machaguo, siyo ndiyo? Maisha yanatusababisha tuchukue uchaguzi. Utachaguaje? Kujipendeza mwenyewe, au kumpendeza Bwana Yesu? Kufuata upendo, au kutafuta ‘haki’ yako? Kujihurumia, au kumsamehe mwingine? Kutafuta amani na upendo, au kutafuta ushinde katika majadiliano? Kujipendeza mwenyewe, au kujikana mwenyewe ili Kristo Yesu adhihirishe maishani mwako?

Labda unafikiri moyoni mwako juu ya mke au mume wako, ‘Siyo sawa! Siyo haki alilosema, alilotenda!’ Sasa, ukijaribiwa kukasirika au kuchukizwa au kujihurumia nenda mara moja kwa Bwana. Usiseme cho chote wakati unapokasirika au kuchukizwa “kwa maana hasira ya mwanadamu haiitendi haki ya Mungu.” (Yakobo 1:20). Lile litakalotoka vinyani mwako litaumiza mke/mume wako tu au litachochea ugomvi tu. Kusema kutokana na hasira na kuchukizwa ni jambo la kulipiza kisasi, la kujipendeza mwenyewe tu – umeumia na sasa unataka kumwumiza mke/mume wako. Hilo ni jambo la kiburi, kujipenda na kujihurumia. Hiyo siyo Roho ya Kristo. Aidha, bila shaka shetani anapenda sana kusababisha na kutumia hali ya kutoelewana kati ya mume na mke – shetani anataka kusababisha na kutumia jambo dogo sana liwe jambo kubwa sana lisababisholo fitina, ugomvi, hasira na hata kama inawezekana chuki. Hiyo ni mbuni na hila yake. Lakini anajenga mambo hayo juu ya msingi wa kiburi, kujipendeza na kujihurumia kwetu tu – kama tukimruhusu!

Jihadhari! Hasa wakati unapochoka, shetani atataka kutumia fursa hiyo – udhaifu huu wako – asababishe ujibu ovyo au kutokujali, kujibu bila uvumilivu wo wote na hata kwa hasira!

Ndio maana neno la Mungu linasema kwetu ‘msimpe Ibilisi nafasi’ na ‘mvue’, ‘mkavae’, ‘jivikeni’. Tunatakiwa kufanya kitu! Lazima tuchague! Hiyo ni sehemu yetu; hiyo ni wajibu wetu – kujikana, kuvua uchungu wote na hasira, yaondoke kwetu kabisa; kuvaa utu mpya, kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana… na upendo! Chagua Kristo! Katika maisha yetu ya kikristo uchaguzi wetu ni kati ya Kristo… au Mimi mwenyewe. Tumchague Kristo. Katika ndoa yangu, nimpendeze Kristo, siyo mimi mwenyewe; nimfuate Kristo, siyo ‘haki’ yangu; nidhihirishe Kristo, siyo nafsi – ili maisha yangu yawe ‘manukato ya Kristo, mbele za Mungu’ (2 Wakor.2:15) kwanza, na baraka kwa familia yangu pia!

Kwenye mstari ufuatao imeandikwa, “harufu ya mauti iletayo mauti.” Yaani, kama nimekufa juu ya ‘utu wa zamani’, kama nikimchagua Kristo na siyo mimi, itakuwa kama harufu ya Kristo nyumbani kwangu – na mke wangu, mume wako, ataguswa na ‘harufu’ hiyo afuate njia ile ile ya ‘mauti’, yaani, kuchagua njia ya Kristo badala ya kujipendeza. Hiyo ni njia bora kabisa kuliko kumkosoa na kumlaumu mke wako, mume wako, ili ‘abadilike’ au ili nishinde magomvi!

Kama nilivyosema, kama ukijaribiwa kukasirika, kuchukizwa au kujihurumia, usiitikie! Hilo ni shauri langu. Tambue, wewe mwenyewe unatakiwa kwenda mbele ya Bwana kwanza afanye kitu ndani yako! Hisia ya hasira, kuchukizwa na hasa ya kujihurumia ni adui wako mkubwa sana. Kujihurumia ni adui mkubwa sana kwako siyo katika ndoa yako tu bali katika maisha yako ya kiroho – itaharibu maisha yako ya kiroho kama ukijifariji mwenyewe na hisia ya kujihurumia! Unafikiri Yesu alijihurumia? Nenda kwa Bwana. Ifuate njia ya Bwana Yesu. Utoe uhai wako Kwake Yesu – usitoe uhai wako kwa uchungu na hasira. Utoe mwili wako uwe dhabihu ulio hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu – siyo kujipendeza. Kama Yesu alivyofanya, na sasa wewe ujikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki. Usisite kujinyenyekeza uwe mtii hata mauti – usiruhusu mambo ya maovu yakae moyoni mwako bali ‘mtakase Kristo Bwana moyoni mwako.’

Tukichukizwa, tukiumizwa, tukikasirika ndipo tunapojaribu kushinda kwa maneno makali ya ugomvi, lakini usifikiri utaweza kubadilisha mke/mume wako au kumshawishi kupitia ugomvi wa namna hiyo, kwa tabia ya namna hiyo! Ukijaribu kumlaumu mke/mume wako na kumrekebisha, utamsukumu ajitetee tu.

Ukisema, ‘Nataka raha!’, sikiliza Mungu asemalo, “Leo, kama mtaisikia sauti yake, msifanye migumu mioyo yenu”, lakini “tufanye bidii kuingia katika raha ile” yaani, raha ya Mungu! (Waebr.4:7,11). Raha yangu ya dunia hii siyo muhimu sana; kuingia katika raha ya Mungu ili nijue amani na upendo Wake – haijalishi mazinginra yangu ni namna gani – na ili maisha ya Kristo yadhihirishe maishani mwangu, hiyo ni muhimu, hiyo ni muhimu kuliko mambo yote nyingine.

Kama tukijitoa kwake Bwana na tumruhusu “tufanywe wapya katika roho ya nia zetu” na “kuvaa utu mpya”, ndipo tutakapoangalia mazingira na mambo yote tofauti, kwa macho mapya. Macho ya neema na upendo. Lile ambalo lilionekana kama jambo kubwa sasa siyo lile lile. Pale ambapo sikuelewa vizuri mke/mume wangu, sasa naweza kuelewa afadhali. Mazingira yangu hayajabadilika, lakini sasa mimi nimebadilika kwa neema ya Mungu! Sasa kama nataka kusema kitu, naweza kusema kwa neema na kwa faida. “Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia.” (Waefeso 4:29)

Tunaimba, “Siyo mimi ninayeishi, bali Kristo ndani yangu…” Je, tunaishi katika yale tuimbayo? Sasa inatakiwa maneno haya yawe halisi katika maisha yangu, katika ndoa yangu!

Umetambua yaliyoandikwa hapo juu, yaani, neno la Mungu linasema, “Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo.” Je, ulijua unaweza kuchagua upendo? Ndiyo, ni kweli kabisa. “Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi.” (Yoh.15:12). “Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake… msiwe na uchungu nao.” (Waefeso 5:25;  Wakol.3:19). “Wanawake… wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao.” (Tito 2:4). Na tunajua kwamba, “Pendo halimfanyii jirani (wala mke wala mume wako) neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria.” (Warumi 13:10).

Upendo siyo hisia tu. Mungu ni Upendo. Tabia ya Mungu ni upendo. Upendo unahusu tabia ya Mungu – uvumulivu wake, upole wake, wema wake, fadhili yake, neema yake. Upendo ‘hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; huvumilia yote; hutumaini yote; hustahimili yote.’ (1 Wakor.13).

Unasema juu ya Mwokozi wetu, “naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo.” (Yoh.13:1). Neno hili ‘upeo’ ina maana ‘mpaka mwisho’ pia!

Chagua upendo huo huo. Chagua kupenda. Ipo neema.

Kwa nini waumini wengine wanahangaika sana na kulalamika? Matamanio yao wawe na kile wanachokipenda inawapelekea wasimtegemee Mungu, wasijitoe kwa Mungu ili wapate neema yake. Neema ni kitu kile ambacho kinatuwezesha kuvumilia mambo yale yanaonekana yapo kinyume yetu! Ipo neema ya kutosha. Neema ya kushinda. Neno la Mungu linasema, “Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu.” (Yak.4:6). Kwa nini wengine hawana neema? Kwa mujibu wa neno la Mungu, ni kwa sababu wanakataa kujinyenyekeza mbele Yake – Yeye huwapa neema wanyenyekevu.

Imeandikwa, “Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema.” (Yoh.1:16). Tena, imeandikwa, “Neema yangu yakutosha…”. Unamini hiyo? Au utamwambia Bwana, “Neema yako hainitoshi!” Na tujifunze, “Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake.”

Najua shetani anaweza kutumia watu kwa ajili ya kazi yake, lakini mara nyingi waumini wanalaumu shetani kwa sababu wanataka hali ya mazingira yao yabadalike mara moja! Hawataki hata kidogo kuvumilia mambo yale ambayo yanaonekana kuwa kinyume chao. Kwa hiyo wanaomba Mungu aiondoe shida hiyo! Lakini labda Mungu yupo katika shida yetu, na jukumu letu ni tutambue mapenzi yake na tujishushe chini ya kusudi lake ili tukue katika upendo na neema ya Mungu na kudhihirisha uzima wa Kristo tunapopatwa na shida na majiribu! Mungu alijibu Paulo katika shida yake akisema, “Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu.” (2 Wakor.12:9). Paulo alipokea neno la Mungu na alitangaza, “Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.” (2 Wakor.12:9,10). Kumbe, Paulo hakujaribu ‘kutoroka’ shida yake, badala yake aligundua na akapokea neema ya Mungu na uzima wa Kristo katika shida yake! Kwa kumtegemea Mungu na kwa kujishusha chini ya neno lake, Paulo aliibadilisha shida yake iwe baraka kubwa sana!

“…siku zote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu. Kwa maana sisi tulio hai, siku zote twatolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu ipatikanayo na mauti.” (2 Wakor.4:9,10).

Wengine hawataki kuifuata njia hiyo, yaani, kutolewa wafe kwa ajili ya Yesu ili uzima wake udhihirishwe ndani yetu. Ni nini inayotuzuia tusijtoe? Kiburi, kujipendezesha wenyewe, kujihurumia, kutokumtegemea Mungu, matamanio yetu ni tutawale au tushinde juu ya wengine, kusisitiza na kushika ‘haki’ zetu. Ndio maana waumini wengine hawapendi watolewe wafe. Matokeo ya haya ni usumbufu, hangaiko, uchungu na malalamiko. Kwa waumini kama hao njia ya Mungu inawezekana kuonekana ‘ngumu’; kwa waumini wale wanaonyenyekea chini ya mkono wa Mungu wanatambua  ‘amri za Mungu si nzito’ na ‘nira ya Yesu Kristo ni laini, na mzigo wake ni mwepesi.’ Kwa nini wengine wanapungukiwa na neema? Wanakataa kunyenyekea na kujishusha chini ya mkono wa Bwana. Neno la Mungu linadhihirisha ya kuwa ‘njia ya asiye mwaminifu ni ngumu.’ (Mithali 13:15); Biblia haisemi po pote ‘njia ya Mungu ni ngumu’. Siyo kitu kigumu sana kutolewa tufe kama tunao moyo wa kumpenda Mungu. Tukiifuata njia hiyo,uzima wa Kristo Yesu utazidi kukua katika maisha yetu kuliko kabla ya hapo na inaleta amani na furaha.

“Wanaopenda sheria yako wana amani tele, wala hakuna kitu kinachoweza kuwakwaza.” (Zaburi 119:165).

Je, mambo yanaweza kukukwaza kwa urahisi? Unachukizwa kwa urahisi? Watu wanajishughulisha mno siku hizi na ‘haki’. Mungu anajishughulisha na tabia yetu, yaani, tukue katika Kristo Yesu, tudhihirishe uzima wa Kristo hapo duniani na tuwe manukato ya Kristo ‘mbele za Mungu, katika wao wanaookolewa, na katika wao wanaopotea’ – nyumbani, kanisani, kazini na sokoni.

Tumeshaona Mungu hakujali hali ya shida ya Hagari ili kulitimiza lengo lake duniani, na mtume Petro anafundisha jambo la maana sana katika waraka wake,

“Enyi watumishi, watiini bwana zenu kwa hofu nyingi, sio wao walio wema na wenye upole tu, bali nao walio wakali. Maana huu ndio wema hasa, mtu akivumilia huzuni kwa kumkumbuka Mungu, pale ateswapo isivyo haki…… kustahimili, mtendapo mema na kupata mateso, huu ndio wema hasa mbele za Mungu.” (1 Petro 2:18-20).

Unafikirije juu ya neno la Mungu hilo? Linakukwaza? Unaifuata njia ipi? Utakwenda njia ipi? Binadamu wanapiga kelele kwa sauti kuu, ‘Siyo haki! Siyo haki! Siyo sawa!’ Lile lisilo ‘sawa’ na lile lisilo la haki katika mizani ya dunia hii nikuona kuwa Mwana wa Mungu Mtakatifu alikufa kwa ajili yako na yangu tulipokuwa wenye dhambi. Hii ni kutokana na pendo lake mwenyewe kwetu. Na alifanya hivyo ili tusiifuate njia yetu bali kumfuata Yeye ambaye ni Njia, Kweli na Uzima.

Je, unapenda ‘kuwezeshwa kwa uwezo wote kwa kadiri ya nguvu ya utukufu wa Mungu’?

Ndiyo? Kwa kusudi gani? Tafakari vizuri! Sikiliza mtume Paulo analosema,

hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu ili mjazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni; mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu; mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na saburi ya kila namna na uvumilivu pamoja na furaha; mkimshukuru Baba…” (Wakol.1:9-12).

Nguvu ya utukufu wa Mungu inatupewa ili tuwezeshe tupate na saburi ya kila namna na uvumilivu…pamoja na furaha na shukrani!

Upo tayari kuipokea?

Unaweza kusoma makala juu ya ndoa; unaweza kwenda semina ya ndoa bila mwisho na kujifunza mambo mengi mazuri. Lakini yote yanategemea na hali yako ya kiroho, na hali ya moyo wako. Yote yanategemea na uhusiano wako na Bwana Yesu! Huwezi kukimbia ukweli huo! Mungu kwa upande wake, hatakujalia ubaki mtu yule yule, kama ulivyo. Kama wewe mwenyewe binafsi haupo tayari kuendelea na Bwana na kubadilishwa, mafundisho yote na semina yote juu ya ndoa hayatakusaidia!

Najua inaweza kuna matatizo mbalimbali katika ndoa na mimi sijajishughulisha na mambo yote ya ndoa, lakini naamini niliyoyaandika yanahusu jambo la msingi, siyo juu ya ndoa bali juu ya maisha yetu ya kiroho kwa ujumla.

Neema ya Mungu iwe nawe.

© David Stamen 2016              http://www.somabiblia.com

UNAWEZA KUPAKUA SOMO HILI KWA BONYEZA LINK HIYO:   siyo-sawa-mambo-ya-ndoa

RUDI KWA HOMEPAGE

 

 

 

 

 

 

2 responses to “SIYO SAWA! MAMBO YA NDOA

  1. Flora

    October 23, 2017 at 4:43 pm

    Amina nimebarikiwa sana tens sana Mungu akubariki utufunze zaidi

     
  2. SAMWEL

    November 29, 2017 at 2:12 pm

    Ameeen

     

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

 
%d bloggers like this: