RSS

JE, MUNGU ANANIADHIBU KUPITIA MATESO?

“Wanafunzi Wake wakamwuliza, “Rabi, ni nani aliyetenda dhambi, ni huyu mtu au wazazi wake hata azaliwe kipofu?’’ Yesu akawajibu, “HUYU MTU WALA WAZAZI WAKE HAWAKUTENDA DHAMBI. Alizaliwa kipofu ili kazi za Mungu zidhihirishwe katika maisha yake.” (Yoh.9:1-3).

Ni kweli kwamba Shetani anataka kuwashambulia wakristo. Ni kweili kwamba dhambi ya mtu zinaweza kuleta au kuvuta shida na mateso. LAKINI KWA NINI Wakristo wengi sana wanapomwona mtu ambaye alipatwa na shida au mateso au eti ni maskini, MARA MOJA wanafikiri alifanya dhambi, au haishi karibu na Mungu, au anakosa baraka ya Mungu! Wakristo wengi pia mara wanapopatwa na shida kubwa au mateso wanafikiri Mungu anawaadhibu au ni mashambulio ya Shetani. Kwa nini? Bila kumwamini Bwana Yesu, bila kungojea Mungu awaongoze na kuwaonyesha analofanya katika maisha yao, mara moja wanafikiri kwamba hawampendezi Mungu, au eti Shetani anatawala katika mazingira au maisha yao! Kwa nini? Sababu ya shida na mateso zinaweza kuwa nyingi! Kwa nini wengi mara moja – ‘automatically’ – wanafikiri lazima sababu iwe mbaya! KWA KIASI, inawezekana nia hiyo inatokana na utamaduni au mila ya uchawi, yaani, kama ukipatwa na mateso na shida lazima ina maana nguvu ya giza fulani imetumwa kukutesa! Na hata mafundisho wa wahubiri wengi yanaimarisha mawazo na nia hiyo mioyoni mwa watu wa Mungu. Lakini bila shaka mawazo haya ni jambo la ushirikina na yanatokana na kutokuamini na kutokujua Mungu. Lazima tusome na tutafakari neno la Mungu sana ili “tugeuze kwa kufanya upya nia zetu” (War.12:2), au tena “tufanywe upya roho ya nia zetu” (Waefeso 4:23). Kwa wengi bado nia zao zinaambukizwa na maisha ya nyuma, lakini Mungu ametupa Roho Yake ili tujue mambo yale Mungu aliyowaandalia wale wampendao (1 Wakor.2:9,10) na tena tujue kwamba “katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema.” (War.8:28).

Paulo alikutana na matatizo pamoja na majaribu mengi lakini ushuhuda wake na mafundisho yake ni kuwa tunajua kuwa mambo yote hufanya kazi pamoja kwa wema kwa wao wampendao Mungu! Paulo alivunjikiwa na jahazi mara tatu. Je, hii inamanisha kuwa Mungu alikuwa kinyume naye? Je Mungu alikuwa anamwadhibu? Bibilia iko wazi kwamba jibu lake ni ‘Hapana’.

Mwana wa Mungu aliongozwa nyikani. Aliongozwa na nani nyikani? Yesu aliongozwa na Roho Mtakatifu nyikani. Kwa kusudi gani aliongozwa nyikani? Ili ajaribiwe! Alijaribiwa na nani? Alijaribiwa na Ibilisi! Yesu Kristo aliongozwa na Roho Mtakatifu nyikani ILI ajaribiwe na Shetani. (Mathayo 4:1; Luka 4:1,2). Unaona? Yesu alipatwa na njaa nyikani. Je, inamaanisha kuwa Mungu alimwacha au alimadhibu Mwanawe? Hapana! Maandiko yanasema kwamba Yesu aliingia nyikani “hali AMEJAA Roho Mtakatifu”, naye akarudi “kwa NGUVU za Roho.” (Luka 4:1,14). Shida na majaribu hayatokei bure, bila kusudi! Yana kusudi la KUTUIMARISHA sisi katika imani yetu kwa Kristo!

Sasa inakuwaje basi baadhi ya waamini wanafikiri mara moja kuwa Mungu hapendezwi nao kwa sababu tu eti mambo yao wakati mwingine hayaendi sawa au kwa sababu wanakutana na shida? Hiyo siyo imani. Hizo ni imani za kishirikina. Bila sababu yoyote tunafikiri kuwa majeshi ya giza fulani yapo kinyume nasi na kwamba yanataka kutuadhibu.Tunapokuwa tunafanya aina hii ya hofu, tunakuwa hatumheshimu Mungu. Kama tukifikiri hivyo, ndipo lazima tutubu na kujalia neno la Mungu na Roho ya Mungu kutusafisha na kufanya nia zetu upya! Kwa mujibu wa neno la Mungu, lengo la dhiki na majaribu ni nini? Sikiliza neno la Mungu:

“Wala si hivyo tu, ila na MFURAHI KATIKA DHIKI pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini; na tumaini halitahayarishi; KWA MAANA PENDO LA MUNGU LIMEKWISHA KUMIMINWA KATIKA MIOYO YETU NA ROHO MTAKATIFU tuliyepewa sisi.” (Warumi 5:3-5.)

Na Yakobo anasema vile vile, “Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno.” (Yakobo 1:2-4).

Na Petro anasema vile vile, “Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali; ILI KWAMBA KUJARIBIWA KWA IMANI YENU, ambayo INA THAMANI KUU KULIKO DHAHABU IPOTEAYO, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo. (1 Petro 1:6,7).

Kwa hiyo Paulo anaendelea kusema:

“Tuseme nini basi kuhusu haya? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, ni nani awezaye kuwa kinyume chetu? Ikiwa Mungu hakumhurumia Mwanawe, bali alimtoa kwa ajili yetu sote, atakosaje basi kutupatia vitu vyote kwa ukarimu pamoja Naye? Ni nani atakayewashtaki wale ambao Mungu amewachagua? Ni Mungu mwenyewe ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani basi atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa, naam, zaidi ya hayo, ndiye aliyefufuka kutoka kwa wafu, yuko mkono wa kuume wa Mungu, naye ndiye anayetuombea.” (Warumi 8:31-34).

Mambo mengi yanatokea siyo kutuadhibu au kutuangamiza, ila kutupeleka TUKUE katika imani na katika Kristo Yesu. Huo ndio mpango wa Mungu kwa ajili yako na kwa ajili yangu!

Labda ni muda tubadili mtazamo na fikra zetu, na tujaze mioyo yetu na ukweli wa Mungu ili furaha yake iwe ndani yetu nasi tumheshimu Bwana na nia zetu. Wengi wanapenda ‘kuota moto’. Basi, ni vizuri sana ‘kuota’ neno la Mungu kila siku! Mungu awabariki!

© David Stamen 2016                somabiblia.com

 

Comments are closed.

 
%d bloggers like this: