RSS

HABARI

ZAMBIA YAPIGA MARUFUKU MAKANISA KUUZA MAFUTA YA UPAKO

Serikali ya Zambia imeyataka makanisa nchini humo kuacha kuuza mafuta na maji ya upako, matendo ambayo yameenea katika baadhi ya makanisa. Waziri wa Mwongozo wa Kitaifa na Mambo ya Dini nchini humo, Godfridah Sumaili ameelezea uuzaji wa mafuta na maji ya upako kuwa ni sawa na kuchezea akili za watu na ni kuwadhulumu.

“Kuuza mafuta ya upako na maji matakatifu ni wizi, ni jinai, acheni kuwauzia watu wasio na uelewa. Uweza unatoka kwa Mungu; Mungu anawatumia nyie [wachungaji] kama chombo, mmepokea bure kutoka kwa Mungu ni lazima mtoe bure,” alisema Sumaili, ambaye naye ni mchungaji.

Akizungumza na wachungaji wanachama wa ushirika wa Livingstone Pastors Fellowship, hivi karibuni, Mchungaji Sumaili alisema manabii wanaouza mafuta na maji ya upako wanajinufaisha kupitia baadhi ya watu waliokata tamaa.

Alisema ni bahati mbaya Wazambia wamekuwa wakichezewa akili na kulipa kiasi kikubwa cha fedha kwa manabii kwa kubadilishana na miujiza, mafuta ya upako na maji matakatifu. Miezi michache iliyopita Serikali ya Zambia ilitangaza kuwa haitaruhusu manabii na wamisionari kuingia nchini humo kwa lengo la kujipatia fedha kupitia huduma za kiroho, kutoka kwa Wazambia maskini waliokata tamaa.

Mchungaji Sumaili alisema nchi hiyo ni taifa la Kikristo lenye sheria zinazoliongoza na Serikali inatarajia kuona manabii wote na watumishi wa Mungu wengine wakizingatia sheria.

“Ni watu wa Mungu pekee, iwe wachungaji, wamisionari na manabii wanaohubiri injili ya kweli ya Bwana Yesu Kristo ndio watakaoruhusiwa hapa nchini. Wizara yangu inapenda kuona hekima katika mwili wa Kristo”, alisema Mchungaji Sumaili.

Alisema watumishi wa Mungu wanaotaka kutoza fedha kwenye mikutano yao hawataruhusiwa nchini humo. Alikuwa akizungumzia hatua ya Serikali ya kumzuia kuingia nchini humo Nabii wa Zimbabwe, Uebert Angel ambaye alikuwa ahubiri kwenye kongamano la ‘kiroho’ jijini Lusaka, ambalo watu walitakiwa kuingia kwa kulipa Kwacha 20,000 (sawa na Shilingi za Tanzania zaidi ya milioni 10). Kongamano hilo lilidaiwa kuwa lililenga kuwapa washiriki mbinu za ‘kiroho’ za kuwa mamilionea na lilijulikana kama Milionare Academy.

“Ni kuwafanya watu waone kuwa jambo hili ni kweli, hasa wale ambao wamekata tamaa na wameweka matumaini yao kiroho kupitia mikutano kama hiyo. Je, injili ni kwa watu matajiri peke yao? Vipi kuhusu Wazambia maskini? Manabii wengine wanataka waje wajipatie fedha na waondoke zao, jambo ambalo wizara yangu haitaliruhusu”, alisema.

Wakati huo Idara ya Uhamiaji katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kenneth Kaunda ilimzuia kuingia nchini Zambia Nabii Uebert Angel Nabii Uebert, ambaye ni mwanzilishi wa huduma ya Kipentekoste ya Spirit Embassy nchini Zimbabwe alikuwa akitokea nchini Uingereza akiwa na mkewe pamoja na watu wengine wawili, walipanda ndege ya shirika la Emirates.

Aliwasili katika uwanja huo majira ya saa tisa alasiri ambapo Uebert na kundi lake walikataliwa kuingia Zambia na hivyo kulazimika kurejea Uingereza kwa kutumia ndege hiyo hiyo.

Vyanzo: Zambia Daily Mail/Lusakatimes.com/

www.mwanzonews.com

MANABII ZIMBABWE WAWEKWA KAPU MOJA NA WAGANGA WA KIENYEJI.

Na Sunday Mail, Harare, Zimbabwe

Manabii, wachungaji, waganga wa kienyeji na waombeaji nchini Zimbabwe wamepigwa marufuku kufanya shughuli zao bila kuwa na kibali kutoka Baraza la Waganga wa Kienyeji, Naibu Waziri wa Afya na Uangalizi wa Mtoto nchini humo, Dk Aldrin Musiiwa amesema.

Amesema Wizara ya Afya imewaandikia barua viongozi wa kanisa ambao wanajulikana kuwa hufanya “miujiza” kuwataarifu juu ya kujisajili kwenye Baraza la Waganga wa Kienyeji.

Dk Musiiwa amesema utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na wizara yake umeonyesha kuwa asilimia 85 ya Wazimbabwe hufuata huduma kwa manabii na waganga wa kienyeji.

“Yeyote anayetoa huduma ya uponyaji wa kiimani, awe mchungaji au mganga wa kienyeji asipofuata maelekezo haya, Waziri wa Afya Dk David Parirenyatwa hatakuwa na namna nyingine isipokuwa kupiga marufuku huduma zinazofanywa na mhusika,” alisema.

“Hatusemi kuwa makanisa yanatakiwa kujisajili kwetu bali ni wale wanaofanya shughuli za uponyaji wa kiimani ndio wanatakiwa na sheria kujisajili.”

Dk Musiiwa ameeleza kuwa ingawa uhuru wa kuabudu umeainishwa katika Katiba ya nchi, lakini uponyaji ni jambo ambalo linapaswa kuratibiwa na Wizara ya Afya.

“Mlezi wa masuala yote ya afya ni Wizara ya Afya na Malezi ya Mtoto. Uponyaji wa kimiujiza ni majibu ya kitabibu na matokeo yanayokusudiwa ni kumponya mtu maradhi. Kwa hiyo hoja hapa ni namna ya tiba ilivyofanyika kupitia kwa daktari au mganga wa kienyeji au Mtumishi wa Mungu.

“Kwa kutumia dawa, kunakuwa na ushahidi wa vipimo ambao huelekeza namna ya matibabu na ukweli huu unakubalika duniani kote na uko kisheria nchini Zimbabwe.

“Tunapokuja kwenye uponyaji wa kiroho, ni jambo ambalo linategemeana na kanuni za kiimani kuliko ushahidi wa vipimo au wakati mwingine ulaghai wa kisaikolojia. Wale ambao hawataki kujisajili wanajijua kuwa ni feki. Ni kazi ya Wizara ya Afya kuwalinda wananchi dhidi ya dhuluma wanayoweza kufanyiwa kupitia udanganyifu wa kisaikolojia.”

Dk Musiiwa alisema ni makosa watu kuwafananisha wanaofanya uponyaji wa kiimani na “wachawi”.

“Pale watu wanaposema chakula cha asili au mavazi ya asili wanamaanisha kwamba hivyo vitu ni vya (n’ángas) wachawi? Hapana! Baraza la Waganga wa Kienyeji ni chombo tu cha Serikali ambacho kinaruhusu waponyaji kwa njia ya imani (manabii, mitume, maaskofu, wachungaji na [n’ángas] waganga wa kienyeji kuponya watu),” alisema.

“Baadhi ya makanisa yenye vitengo vya wakunga hasa kanisa la mitume lazima yajisajili kwenye Baraza la Waganga wa Kienyeji,” alisema.

Mwenyekiti wa bodi ya baraza hilo, Sekuru Friday Chisanyu alisema kuwa usajili wa watu wote wanaoendesha shughuli za uponyaji utawaondoa wale ambao ni waponyaji bandia.

“Wanapotoa maelekezo juu ya matumizi maji ya upako, bangili, na mapambo mengine bila kusajiliwa ni kinyume cha sheria,” alisema na kuongeza kuwa wale ambao watakataa kusajiliwa watashtakiwa.

Mchungaji Wyson Dutch, rais wa Grace International Churches and Ministries, ambao ni mwavuli wa makanisa ya kievanjeliko na kipentekoste, alisema baadhi ya waombeaji wanawahadaa watu ili wajipatie mali.

“Hawa wanaoitwa manabii wanafanya kazi za waganga wa kienyeji na madaktari ambao wamesajiliwa. Ni lazima wasajiliwe,” alisema Mchungaji Dutch.

Hata hivyo, kiongozi wa huduma ya Body of Christ Ministries International Nabii Gamuchirai Sande alisema ni vigumu kutenganisha uponyaji na ibada.

“Yesu alipokuwa hapa duniani aliponya watu kama sehemu ya kazi yake maalum, hivyo kama Wakristo ambao tumeitwa kwa jina lake tunatakiwa kufanya yale aliyofanya. Hakuna haja ya kusajili uponyaji,” alisema.

Chanzo: gazeti la Sunday Mail la Zimbabwe

—————————————————————————————————————————————————————————————————

KUSOMA MAKALA ZAIDI, BONYEZA LINK IFUATAYO:   GAZETI LA MWANZO 2

Aidha, unaweza kupokea Gazeti hili moja kwa moja. Group Executive Editor wa mwanzonews.com Jackson Malugu anaandika:

Gazeti hili hutolewa kila Jumapili na huwafikia wasomaji wake kwa njia ya emails, whatsapp na facebook. Pia linakuwa katika tovuti yetu. Ni mkusanyiko wa habari kutoka katika makanisa mbalimbali nchini pamoja na makala kutoka kwa watumishi wa Mungu. Kuwa tayari kupokea toleo la jarida letu la kila mwezi la PASTOR’S LIFE MAGAZINE kwa ajili ya Septemba ambalo litakufikia wakati wowote ndani ya muda wa saa 48. Jarida hili linakuwa na habari za kina, mahojiano na watumishi mbalimbali pamoja na makala za uchambuzi wa kina wa neno la Mungu. Unaweza pia kutembelea tovuti yetu ya mwanzonews.com ambayo inakuwa na habari mbalimbali za Kikristo, ikiwemo habari mpasuko

Tunahitaji sana maoni yako juu ya huduma hii.

Mungu akubariki sana.

Jackson Malugu

 

Comments are closed.