RSS

MASOMO MAFUPI YA KUTIA MOYO

VITA UNAVYOPITIA MAISHANI VINAKUIMARISHA. USIOGOPE.
KWA MAANA KUJIZOEZA KUPATA NGUVU…
LAANA AU BARAKA
HAPANA UCHAWI JUU YA YAKOBO
MIMI ni THAWABU YAKO KUBWA SANA
TUSEME NINI BASI?
UNAIFUATA MIUJIZA?
MWANA HATAUCHUKUA UOVU WA BABA YAKE
USIPIME UPENDO WA MUNGU KWA MUJIBU WA MAZINGIRA YAKO
YESU MWENYEWE NDIYE NJIA
VIPI TUNAYAHESABU MATESO YA MAISHA YETU?
UPENDO HAUPUNGUI NENO
SIO TAMU. NI SUMU!
BWANA HUUJARIBU MOYO
ABIGAILI NA MAMBO YA NDOA

1

VITA UNAVYOPITIA MAISHANI VINAKUIMARISHA. USIOGOPE.

Mtu wa Mungu naomba nikutie moyo katika vita unavyopitia maishani. Mungu ameruhusu hivyo vita maana anajua njia ya pekee ya wewe kuendelea kuimarika katika maisha yako ya imani na mahusiano yako na Yeye ni kwa njia ya hivyo vita na hizo changamoto unazopitia maishani.

Kumbuka siku zote uwapo vitani, haijalishi hiyo vita ni kubwa kiasi gani, si kubwa ukilinganisha na vita vilivyo mbele yako katika siku za usoni. Vita vya jana vinakuandaa kwa ajili ya vita vya leo na kadhalika vita vya leo vinakuandaa kwa ajili ya vita vya kesho.

Wakati Daudi akiwa peke yake kule nyikani na kondoo za baba yake, alitokewa na dubu na simba. Daudi angeweza kukimbia maana kw a kweli ukilinganisha dubu na simba na Daudi, Daudi asingekuwa kabisa na uwezo kwa namna ya kawaida kukabiliana nao. Lakini Daudi katika ushuhuda wake kwa Sauli alisema kuwa Mungu alimwokoa na kinywa na makucha ya Dubu na Simba.Ushuhuda wa vita vyake vya jana vilikuwa kianzio vya vita vyake vya leo. Daudi aliandaliwa na vita vyake dhidi ya dubu na simba kukabiliana na Goliati maana Mungu aliyemwona alipokabiliana na dubu na simba alikuwa na uhakika kabisa kuwa ni Mungu atakayemwona atakapokabiliana na Goliati.

Usidharau vita vyako vya leo maana vinakuandaa kwa ajili ya vita kubwa zaidi kesho. Mungu anaikuza imani yako kupitia vita vyako vya leo ili iwe imara vya kutosha kwa ajili ya vita vyako vya kesho.

Usikubali kunyong’onyeshwa na pito lolote la leo.

Chukulia kama ni maandalizi kwa ajili ya mapito makubwa zaidi kesho.

Endelea kumwamini Mungu katika lile ulipitialo leo.

Katikati ya vita unavyopitia ukihakikisha haya unayafanya kwa uaminifu na nidhamu ya hali ya juu utu wako wa ndani utazidi kuimarishwa katika hali hiyo unayopitia.

Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana; tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele. (2 KOR. 4:16-18 SUV).

Na Carlos R. W. Kirimbai

RUDI KWA MWANZO

2

KWA MAANA KUJIZOEZA KUPATA NGUVU…

Nataka niseme na sisi kidogo kuhusu mazoezi.

Sio kila mara unapomwona mchezaji anaingia uwanjani anaingia uwanjani kwa ajili ya mechi au mashindano. Mchezaji anaingia uwanjani mara nyingi zaidi kwa ajili ya maandalizi na mazoezi kuliko anavyoingia kwa ajili ya mechi au mashindano. Kiwango cha ufanisi cha mchezaji katika mechi au mashindano kinategemea sana alijiandaaje na mazoezi aliyoyafanya. Kuna mazoezi anayoyafanya mchezaji ambayo yanamwongezea nguvu. Yapo ambayo yanamwongezea pumzi. Yapo yanayomwongezea ujuzi, uwepesi na umahiri.

Ninachojaribu kusema ni ubora wa mchezaji hautokani na uwezo wake wa kucheza au kushindana bali maandalizi yake na mazoezi yake. Kadhalika katika mambo ya rohoni. Maandalizi ni muhimu mno mno mno.

Usisubiri upate shida ndo uombe.

Yapo maombi kwa kusudi la kupata majibu ya mambo mbali mbali maishani alafu yapo yale ambayo ni maandalizi na mazoezi hasa yale ambayo unalazimika kila siku kuamka kuomba. Unapotegea maombi yako binafsi au yale ya kanisani kwenu au kikundi ulichopo unajitegea mwenyewe kwenye maandalizi na mazoezi yako ya kiroho.

Kadhalika usomaji wa neno na kufunga. Vyote hivi ni mazoezi ya kiroho yanayomwimarisha na kumtia nguvu mtu wa ndani ili siku ya mechi (changamoto, taabu, shida, uhitaji) uwe upo vizuri kukabiliana.

Wengi tunafeli siku ya dhiki maana nguvu zetu ni kidogo. Hatujajijengea nidhamu ya kuomba, kusoma neno, kuhudhuria ibada, kufunga nk ambayo itamwimarisha na kumwandaa mtu wetu wa ndani kwa ajili ya siku ya uovu na vita. Kama mazoezi yalivyo ya muhimu kwa ajili ya kumwandaa mwanamichezo hodari, mahiri, mwenye ujuzi, pumzi na nguvu, kadhalika mazoezi ya kiroho ni muhimu mno kwa ajili ya kumwandaa wewe mwenye nguvu za kiroho, pumzi ya kiroho, umahiri na uweledi wa kiroho.

Acha kuendelea kupuuzia mazoezi ya kiroho.

Itakugharimu siku ya vita.

Kumbuka: Jasho jingi mazoezini, damu chache vitani. Jasho kidogo mazoezini, damu nyingi vitani.

“Kwa maana kujizoeza kupata nguvu za mwili kwafaa kidogo, lakini utauwa hufaa kwa mambo yote; yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye.” (1 Ti.4:8).

Na Carlos R. W. Kirimbai

RUDI KWA MWANZO

3

LAANA AU BARAKA (Kum.30:19)

Mtu wa Mungu tunapoyasoma maandiko ya Agano la Kale lazima tusaidiwe na Roho Mtakatifu kuyatafsiri katika muktadha wa Agano Jipya la Neema. Mungu anazishuhudiza mbingu na nchi juu yetu na kusema ameweka mbele yetu uzima na mauti, baraka na laana na anatuambia tuchague uzima ili tuwe hai sisi na uzao wetu. Hili andiko linasema nasi katika Agano Jipya la Neema kuwa unapomchagua Yesu umechagua uzima na baraka na unapomkataa unakuwa umechagua mauti na laana. Kwa wale waaminio hamna kitu kama uzima na mauti bali kuna uzima tu.

Kwa wale waliyoamua kumfanya Yesu Bwana na Mwokozi wa maisha yao hakuna laana na baraka bali kuna baraka tu. Kwa hiyo mtu wa Mungu uwe unayaangalia maandiko ya Agano la Kale na kuyasoma na kuyaelewa katika muktadha sahihi wa Agano Jipya la Neema. Tunapokosea hatujiletei laana bali tunajiletea kurudiwa na Bwana maana Mungu kwetu ni Baba na sio Baba Aliye mwepesi wa hasira yaani tukikosea tu anatulaani. Atatukemea na kuturudi ndiyo lakini kutulaani hapana maana ameshatubariki kwa baraka zote za rohoni katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo Yesu sio kwa sababu ya chochote tulichofanya bali kwa sababu ya kile Yesu alifanya kwa ajili yetu pale msalabani.

Yeye asiyejua dhambi alifanywa dhambi kwa ajili yetu ili sisi tuwe haki ya Mungu katika Kristo Yesu. Kristo alitukomboa toka katika laana ya Torati maana alifanyika laana kwa ajili yetu au kwa maneno mengine badala yetu, maana imeandikwa amelaaniwa kila mmoja aangikwaye juu ya mti ili baraka ya Ibrahimu itufikilie sisi mataifa kupitia Kristo Yesu. Laana zimeshachukuliwa na Yesu kwa hiyo haiwezekani wewe uliye katika Yesu ulaaniwe.

Acha kuwaza mauti na laana anza kuwaza uzima na baraka vilivyo fungu lako katika Kristo Yesu. Roho hushuhudia pamoja na roho zetu kuwa sisi ni wana wa Mungu na kama ni wana basi tu warithi turithio pamoja na Kristo. Kama tu warithi turithio pamoja na Kristo, kama Yesu hawezi rithi laana mimi siwezi kurithi laana. Kama Yesu ni mrithi wa Baraka za Baba Yake mimi pia ni mrithi wa Baraka.

Badilisha unavyofikiri.

Carlos Ricky Wilson Kirimbai

RUDI KWA MWANZO

“HAPANA UCHAWI JUU YA YAKOBO”

Katika Agano la Kale Balaamu hakuweza kuwalaani watu wa Mungu. Balaki alitaka Balaamu awalaani Israel ili kuzuia maendeleo yao, lakini Mungu Mwenyewe alimzuia Balaamu!

Mungu ni Mwamuzi wa watu Wake, siyo mwingine!

Balaamu alilazimishwa kutangaza, “Tazama, nimepewa amri kubariki, Yeye amebariki, NAMI SIWEZI KULITANGUA. Hakika HAPANA UCHAWI JUU YA YAKOBO, wala hapana uganga juu ya Israeli. Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa, Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu!” (Hesabu 23:20,23).

Unaona? Hata kabla ya kufa kwa Yesu msalabani, haukuwa uchawi juu ya watu wa Mungu, haukuwa uganga dhidi yao! Kwa nini wahubiri wengi wa siku hizi wanawatisha Wakriso kwa mafundisho ya uongo wakidai kama mkristo akiwa na tatizo, shida, ugonjwa, mateso au kutokufanikiwa, inawezekana au hata lazima kutokana na laana – laana kutokana na babu zao, au na nchi yao au hata na shetani nkd! Sio kweli! Ni udanganyifu kabisa. Wahubiri hao wamechanganya kabisa hukumu wa Mungu juu ya watu wake katika Agano la Kale, na laana inayotoakana na uchawi! Hata katika Agano la Kale wachawi hawakuweza kuwagusa watu wa Mungu kwa uchawi na uganga wao! Mungu mwenyewe angewahukumu watu Wake! 

Baada ya kufa kwa Yesu msalabani baraka na ulinzi wa Mungu zimezidishwa kwa wingi katika Kristo Yesu! Kama tunavyofundishwa na Neno la Mungu, “Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ALIYETUBARIKI KWA BARAKA ZOTE za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo.” Kama tumeokoka na “uhai wetu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu” (Wakol.3:3) ndipo hamna laana kutokana na shetani, na wazazi, na mababu, na wachawi au na maneno ya watu ambayo yanaweza kuyajeruhi au kuyaathiri maisha yetu katika Kristo Yesu! Amen!  Haiwezekani! Mungu apewe sifa kwa neema kuu hiyo na kwa wokovu wa ajabu! Usimruhusu mwingine akudanganye au akuchanganyike! “Katika ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa.” (Wagal.5:1).

Juu ya shetani neno la Mungu linasema, “Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.” (1 Yoh.3:8); kuhusu nguvu za giza, “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake.” (Wakol.1:13).

Mafundisho hayo kuhusu laana ni kinyume cha Biblia, yanapinga moja kwa moja neno la Mungu ambalo linasema, “Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu… ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.” (Wagal.3:13,14). Unaona, Yesu Kristo alitukomboa katika laana ya torati ya Agano la Kale! Wapi mitume kwenye waraka zao wanafundisha au hata kutaja neno mmoja kuwa laana (haijalishi inatoaka wapi!) inaweza kuwatesa, kuwaumiza au kuwadhuru waumini – au kuzuia maendeleo ya maisha ya kiroho ya wakristo? Hamna mafundisho hayo! Wapi Bwana Yesu aliwaonya wanafunzi wake juu ya nguvu za ‘laana’? Hamna! Petro anasema, “Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema?”

“Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. 

Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea.” (Warumi 8:31-34).  

Neema ya Bwana Yesu iwe kwako siku ya leo!

RUDI KWA MWANZO

5

‘‘Usiogope, Abramu. MIMI ni ngao yako na THAWABU YAKO…. KUBWA SANA.’’

Abramu alitaka kupewa mtoto wa kiume. Je, Mungu hakusema, “Mimi nitakufanya taifa kubwa na nitakubariki”? Basi, Abramu alikuwa anawaza sana juu ya hivyo; alikuwa anatumaini, anatarijia apate mtoto. Lakini Mungu alikatisha mawazo yake, tumaini lake na matarajio yake…

“…neno la BWANA likamjia Abramu katika maono: Usiogope, Abramu. MIMI ni ngao yako na thawabu yako kubwa sana.” (Mwanzo 15:1).

Kabla ya kupokea mambo yale tunayoyahesabu muhimu na ya thamani saaaana kwa maisha yetu, hata baraka za dhati, lazima tumeitengenza mioyo yetu kumdhamini na kumpenda Mungu na Mwokozi wetu kuliko yote nyingine – lazima tumhesabu Mungu thamani kiasi cha kuhesabu mambo yote nyingine si kitu kulinganisha na kumjua na kumpenda Yeye! Lazima kumhesabu siyo ‘thawabu yetu’ tu, bali ‘thawabu yetu KUBWA SANA’. Ndipo tu tutakapokuwa tayari kuipokea ‘baraka’ zingine za dhati. Je, tupo tayari kumruhusu Mungu kukatisha matarajio yetu na neno lake? Je, tupo tayari Mungu atuongoze kwa njia Yake na kutubariki kwa wakati auchaguaye Yeye? Na kufanya hiyo bila kuingojea ngojea kwa kutoksubiri ‘baraka’ ifike, bali kumpokea Bwana, na kufurahi katika Bwana kama thawabu yetu kubwa sana? Tunajua Abrahamu alikuwa na tabia ya namna hiyo, kwa sababu baadaye alikuwa tayari kutoa mwana wake wa pekee aliyempenda kama dhabihu kwa ajili ya Mungu wake!

Je, unamtafuta mchumba, unataka kuoa au kuolewa, kuwa mwimbaji, au unatafuta huduma au kufanikiwa katika kazi au biashara yako…..

‘‘Usiogope. MIMI ni ngao yako na THAWABU YAKO…. KUBWA SANA.’’

Sisemi tutapata tutakalo, lakini tutapata lile bora kabisa, duniani na kwa milele!

Haifai kama maneno haya yakizigusu hisia zetu kwa saa moja, au siku moja, au hata wiki moja. Lazima ukweli huo uingie mioyo yetu na uwe tabia yetu daima. Mungu atusaidie kwa neema Yake kuu siku ya leo tumchague awe thawabu yetu kubwa sana! Amen.

RUDI KWA MWANZO

6

TUSEME NINI BASI?

LAZIMA KILA MTU AJIBU SWALI HILI:

‘Tuseme nini basi? Je, tuendelee kutenda dhambi…’ (Warumi 6:1)

Paulo anajibu, ‘Hasha!’

Au, ‘Je, tuendelee kutenda dhambi ili neema ipate kuongezeka?

Paulo anajibu, ‘Hasha!’

Yeye anatuuliza tena, ‘Sisi tulioifia dhambi TUTAISHIJE TENA katika dhambi?’ 

Tuseme nini? Tujibu nini?

Paulo anaeleza. ‘mkijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, TUSITUMIKIE DHAMBI TENA.’

Wengine wanajaribu kuleta kisingizio, udhuru au kisababu kwa kutenda dhambi kwa njia ya kunukulu 1 Yoh.1:10. Lakini Yohana anaendelea kusema katika mstari ufuatao, ‘nawaandikia haya ili kwamba MSITENDE dhambi.’. Zaidi ya hayo, anatufundisha kwamba, ‘Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, …wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa KUTOKANA NA MUNGU.’ (1 Yoh.3:9). 

Wakristo kweli kweli wamezaliwa kutokana na Mungu. ‘Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili AZIVUNJE kazi za Ibilisi.’ Na kazi ya Ibilisi ni nini? ‘Ibilisi HUTENDA DHAMBI tangu mwanzo.’ Kwa hiyo Yohana anafundisha, ‘atendaye dhambi ni wa Ibilisi.’ Yesu alisema kwamba, ‘Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli ITAWAWEKA HURU.’  (Yoh.8:32).

Watu wa dini hawakuelewa maneno ya Yesu, walifikiri DINI YAO iliwaweka huru! Lakini Yesu alieleza kwa wazi!  ‘Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni MTUMWA WA DHAMBI…Basi Mwana akiwaweka huru, MTAKUWA HURU KWELI KWELI.’ Basi Yesu aliweka wazi kwamba uhuru ule ambao Yesu huwapa watu ni kuwaweka huru mbali na dhambi! Yohana na Paulo wanakubiliana na yale Yesu aliyoyasema. Paulo anasema, ‘Mungu na ashukuriwe, kwa maana MLIKUWA watumwa wa dhambi… na mlipokwisha KUWEKWA HURU MBALI NA DHAMBI, mkawa WATUMWA WA HAKI.’ (Warumi 6:17,18).

Sasa nini, au nani atakuokoa na dhambi zako; nini au nani utakuweka huru mbali na dhambi? Kifo cha mwili wako utakapokufa? Au Yesu Kristo siku hiyo hiyo? Unasemaje?

‘…utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.’ (Mat.1:21).

Kwa kweli ni wokovu mkuu! 

RUDI KWA MWANZO

7

UKIIFUATA MIUJIZA TU, YESU HATAKUWA MFALME WAKO.

Yesu alifanya muujiza. Aliwalisha waume elfu tano kutokana na mikate mitano na samaki wawili. Ndipo tunasoma, “Kisha Yesu, hali akitambua ya kuwa walitaka kuja kumshika ili wamfanye mfalme, AKAJITENGA, akaenda tena mlimani yeye PEKE YAKE.” (Yoh.6:15). Kwa nini Bwana Yesu alijitenga? Ilionekana kuwa nafasi ya ajabu awe mfalme juu ya watu!

Hapana! Watu wale walitaka kumfanya Yesu mfalme KWA AJILI YA FAIDA YAO TU ili wapate baraka za kimwili au za nje tu! Inawezekana walijiambia kama yafuatavyo: “Kumbe! Anafanya miujiza! Hatutahitaji cho chote tena! Yeye atatubariki kupita kiasi na sisi tutafanikiwa! Atabadilisha mazingira yetu! Ataondoa maadui zetu Warumi! Atatuletea mafanikio! Ataboresha maisha yetu! Biashara yetu itafanikiwa, na yote tulilolitaka, yametimizwa! Twende tumfanye mfalme!” Vivyo hivyo hayo yanatokea siku hizi. Watu wanaifuata miujiza na baraka za kimwili kuliko kumfuata Yesu na njia Yake.

Miujiza siyo tatizo. Tatizo linaweza kuwa lengo letu la kiini la kumfuata Yesu.

Bwana Yesu, Yeye aliye na macho yake kama mwali wa moto, huangalia na kuchunguza makasudi (motives) yetu kweli kweli yaliyoweza kufichwa ndani sana ya mioyo yetu! (Waebr.4:12). Watu wanaweza kusema hivi na hivi, wanaweza kuwa na hamu kwa ajili hivi na hivi, hata kumfuata Yeye, lakini Yesu anachunguza makusudi kweli kweli ya mioyo yetu! Maneno ya Yesu yanaingia mioyo yetu moja kwa moja kuuliza, “Unataka nini?” Yesu hatafuti kuwakusanya watu kujenga ‘umaarufu’ wake kupitia ‘miujiza’ au ‘upako’ wake! Kwa maneno yake na kazi yake katika maisha yetu, Yesu Kristo anachunguza chunguza mioyo yetu mpaka makasudi yetu ya kiini kabisa yamefunuliwa; mpaka tutakapotoa maisha yetu Kwake kabisa, bila masharti yoyote kwa upande wetu, bila manung’uniko yoyote; tuwe tayari tupate hasara ili tupate Kristo na uzuri usio na kiasi wa kumjua Yeye! (Wafilipi 3:8).

Je, na wewe na mimi, tunataka mfalme wa namna ileile Wayahudi kwenye Yohana 6 walivyomtaka? Kama ni hivyo, huwezi kumfuata Mwokozi Yesu Kristo! Huwezi kuwa mwanafunzi Wake – humjui, huitambui tabia Yake. Atajitenga nawe. Yesu alikataa KABISA kuwa mfalme juu ya msingi wa kujipendeza kwa watu! Alijitenga na akaenda mlimani peke Yake. Je, utamfuata pale, pale jangwani, mlimani, pale ambapo hakuna cho chote ILA YESU TU na MSALABA wake?

Je, Yesu Mwenyewe tu anatosha kwako na kwangu? Tunaimba, “Wewe tu ndiwe utoshaye.” Je, ni kweli kwako na kwangu kila siku?

Tunataka nini? Tunatafuta nini?

Yesu alisema, “Akawaambia WOTE, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate… Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. (Luka 9:23; 14:33).

Hayo ni msingi wa kumfuata Yesu Kristo. Je, ninampenda Yesu kuliko baraka za kimwili, kuliko miujiza, kuliko ‘mafanikio’, kuliko huduma yangu, kuliko sifa yangu mbele ya watu, kuliko baba au mama au mume au mke au watoto wangu? Yesu alitoa maisha yake kwa ajili yetu ili atupate kabisa, kwa ndani, kwa milele. Ni Mwokozi wa ajabu anayestahili tutoe maisha yetu yawe dhabihu yalio hai mbele Yake daima.

Mungu alibariki neno lake kwa mioyo yetu!

RUDI KWA MWANZO

8

“Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa; MWANA HATAUCHUKUA UOVU WA BABA YAKE, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe.” (Ezekiel 18:20).

Mungu aliwakemea sana wana wa Israel kwa sababu waliamini watoto hudhurika na kuadhiriwa na dhambi za wazazi wao! Na wahubiri wengi siku hizi wanastahili kukemewa pia kwa kufundisha yaleyale, kana kwamba muumini kweli anaweza kubeba laana kutokana na dhambi za wazazi wake! Huo ni uongo kubwa ya namna gani? Mungu anaendelea kuwakemea Waisraeli, “Je! Maana yake ni nini hata mkatumia mithali hii katika Israeli, mkisema, Baba wamekula zabibu mbichi, nao watoto wakatiwa ganzi la meno? KAMA MIMI NIISHIVYO, asema Bwana MUNGU, HAMTAKUWA NA SABABU ya kuitumia tena mithali hii katika Israeli….Lakini ninyi mwasema, Kwani yule mwana asiuchukue uovu wa baba yake? Yule mwana atakapofanya yaliyo halali na haki, na kuzishika amri zangu na kuzitenda, hakika ataishi.” (Ezekiel 18:2,3,19). Kumbuka, hayo yote yalikuwa kweli kabla ya Yesu hajakufa na kufufuka! Aidha, hata katika Agano la Kale uchawi haukuweza kuathiri wala kudhuru watu wa Mungu walioongozwa naye! Sikiliza!

“Mungu SI MTU, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza? Tazama, NIMEPEWA AMRI KUBARIKI, Yeye amebariki, nami SIWEZI KULITANGUA. …Bwana, Mungu wake, yu pamoja naye, Na sauti kuu ya mfalme i katikati yao. Hakika HAPANA UCHAWI JUU YA YAKOBO, Wala HAPANA UGANGA JUU YA ISRAELI. Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa, NI MAMBO GANI ALIYOYATENDA MUNGU!” (Hesabu 23:19-23).

Kumbuka, hayo yalikuwa kweli wakati wa Agano la Kale! Je, ni mambo gani aliyoyatenda Mungu kwa ajili yetu SASA kupitia Mwanawe Yesu Kristo? Sikiliza, “Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo.” (Waefeso 1:3).

Pamoja na hayo, neno la Mungu linatudhihirsha ukweli ufuatao: “Kristo alitukomboa katika laana ya torati…” (Wagal.3:13).

Kutokana na hayo tunaona wote wanaofundisha kuwa maisha ya Mkristo (ya kimwili na kiroho) anaweza kushambuliwa na kudhurika na laana yanatokana na uchawi au na dhambi ya wazazi, wanapinga neno la Mungu na wanakaribia kujiweka chini ya hatari ya Wagalatia 1:6-8. Kwa hiyo,

“Katika ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa.”

RUDI KWA MWANZO

9

USIPIME UPENDO WA MUNGU KWA MUJIBU WA MAZINGIRA YAKO! UTAPIMA KWA UJINGA TU. Ukitaka kupima upendo wa Mungu kwako, TAZAMA KALVARI TU! Hapo hapo utatambua kiwango cha upendo wa Mungu kwa ajili yako!

“Basi imani…ni bayana ya mambo yasiyoonekana.” (Waebr.11:1).

Wengi wanaweza kumwamini na kumsifu Mungu wakati anapofanya mambo kwa ajili yao. Lakini kwa wengi ni shida kumwamini Mungu wakati INAONEKANA asipofanya cho chote kwa ajili yao. Kwa hiyo Mungu anasema, “Kama mkiisikia sauti yake leo, msiifanye migumu mioyo yenu kama mlivyofanya kule Meriba kama mlivyofanya siku ile kule Masab jangwani, ambapo baba zenu walinijaribu na kunipima, ingawa walikuwa wameyaona niliyoyafanya.” (Zaburi 95:7-9). Baada ya kutoka Misri, watu wa Mungu waliimba kwa furaha kubwa mbele ya Mungu, lakini baada ya hapo hawakupata maji ya kunywa na mara moja walimnung’unikia Musa, yaani, kwa msingi walimnung’unikia Mungu!

Kwa urahisi waliacha kumwamini Mungu. Kwa kutokuamini huku tunaifanya migumu mioyo yetu na hatutajua raha ya Mungu. Biblia inatufundisha, “kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina THAMANI KUU kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo.” (1 Petro 1:7). Kumwamini Mungu wakati wa shida na matatizo, hasa wakati INAONEKANA Mungu hafanyi cho chote kwa ajli yetu, NI THAMANI KUU KULIKO DHAHABU.

Shadraki, Meshaki na Abednego walijibu mfalme Nebukadneza kwa na maneno ya ajabu:

“Ee Nebukadneza, hatuhitaji kujitetea wenyewe mbele zako kuhusu jambo hili, ikiwa tutatupwa ndani ya tanuru iwakayo moto, Mungu tunayemtumikia ANAWEZA KUTUOKOA na moto, naye atatuokoa kutoka mkononi mwako, Ee mfalme. Lakini HATA IKIWA HATATUOKOA, Ee mfalme, tunataka ufahamu kwamba, HATUTAITUMIKIA miungu yako wala kuiabudu sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.’’ (Danieli 3:16-18).

Watu watatu hawa walimamini Mungu HAIJALISHI Mungu afanyalo au asilofanya kwa ajili yao! (Na wewe?). HIYO NI IMANI.

Shida kwa wengi ni ifuatayo: wanajua Mungu anaweza kufanya lo lote (tunaimba ‘Yote yawezekana’). Lakini kama ‘inaonekana’ kuwa Mungu hafanyi cho chote kwa ajili yao wakati wakipitia kipindi cha shida na majaribu, wanachukizwa na wanaamini Mungu amewaacha! Wanakosa kwa kufikiri dalili ya pekee ya uwepo wa Mungu nao ni ‘baraka’ (za kimwili). Wanaishi kwa ‘kuviangilia vinavyoonekana tu na siyo kwa visivyoonekana’. Kama ‘baraka’ zipo katika maisha yao, wanaamini ina maana Mungu ‘yupo’ na wanaimba kwa furaha ‘Mungu yu mwema’. Kama ‘INAONEKANA’ Mungu anawanyima watu hao baraka yake, mara moja wananungunika, kuchukizwa na kufikiri Mungu wamewaacha na hata wanawachukia, vile vile Waisraeli walivyofanya, “…mkanung’unika hemani mwenu, mkasema, Ni kwa sababu Bwana AMETUCHUKIA, ndipo akatutoa katika nchi ya Misri, apate kututia katika mikono ya Waamori, ili KUTUANGAMIZA.” (Kumbu.1:27). Mapenzi ya Mungu yalikuwa kuwabariki Waisraeli KUPITIA KIASI kwa kuwaongoza katika nchi ya Ahadi, kwa sababu ALIWAPENDA SANA! Lakini kumbe, kwa sababu HAWAKUELEWA njia ya Bwana – kwa sababu ya KUTOKUAMINI kwao! – walifikiri Mungu aliwachukia na hata alitaka kuwaangamiza!

Na sisi? Imani yetu iko wapi? Una imani kwa Bwana au kwa ‘baraka’? Tafakari swali hili kwa makini moyoni mwako kabla ya kujibu. Shadraki, Meshaki na Abednego walimwamini Mungu TU, bila kujali mazingira yao, bila kutazamia lazima Mungu abadilishe mazingira yao!

Imani yao haikutegemei na mambo Mungu aliyofanya au asiyofanya kwa ajili yao!

Na sisi? Je, tunaishi kwa ‘kuviangilia vinavyoonekana au visivyoonekana’?

Tatizo kubwa sana kwa Ayubu lilikwa hakujua SABABU ya mambo yale yaliyotokea ambayo yalimletea maumivu makali yale katika maisha yake! Hii ni changamoto kubwa kwetu pia, yaani, kupita pagumu bila kujua sababu! Kwa kweli, hii ni kujaribiwa kwa imani yetu! Kwa hiyo, tukipita pagumu tusimlaumu Mungu bali tukumbuke na tuamini kuwa anatuwazia mema tu. Mungu wetu ni mwaminifu na hawezi kutuacha, hutupa majaribu kwa sababu ametuandalia ushindi katika majaribu hayo tupitiayo. Hivyo basi tukatae kushawishiwa na shetani ili tumchukie au kumlaumu Mungu kwa sababu ya shida tunazopitia. Kumbuka Shadraki, Meshaki na Abednego! Imani yao ilijaribiwa kwa moto wa dhati! Lakini mwishoni imani yao ilimtukuza Mungu mbele ya watu wote! Itakuwa vivyo hivyo kwako kama ukiishi kwa imani, hata kama ilijaribiwa ‘kwa moto’. Siku ile imani yetu itaonekana kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo. Kumbuka pia, ni wapi Shadraki, Meshaki na Abednego walipokuta naye Yesu? Katika moto!

Usipime upendo wa Mungu kwa mujibu wa mazingira yako! Utapima kwa ujinga tu. Ukitaka kupima upendo wa Mungu kwako, TAZAMA KALVARI TU! Hapo hapo utatambua kiwango cha upendo wa Mungu kwa ajili yako!

“Basi IMANI ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo YASIYOONEKANA.”

“Kama mkiisikia sauti yake leo, MSIIFANYE MIGUMU mioyo yenu.”

RUDI KWA MWANZO

10

YESU mwenyewe ndiye njia. Biblia haisemi ujuzi au maarifa kuhusu Yesu ni njia. Yesu Mwenyewe ndiye Njia. “MIMI ndimi njia.” (Yoh.14:6). Yaani, tabia Yake ni njia! YESU ndiye uzima. Siyo kujifunza au kujua mambo juu ya Yesu ni uzima. YESU MWENYEWE ndiye uzima.

“Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; NA UZIMA HUU UMO KATIKA MWANAWE (1 Yoh.5:11).

Haitoshi kuyajua mambo mengi KUHUSU Yesu Kristo. Lazima tuwe ndani Yake na Yeye awe ndani yetu. Kwa hiyo pia Paulo anasema,

“Twajua ya kuwa sisi sote tuna ujuzi. Ujuzi huleta majivuno, bali upendo hujenga.” (1Wakor.8:1);

na Yohana anasema, “Ye yote anayesema anakaa ndani Yake hana budi kuenenda kama Yesu alivyoenenda.” (1 Yoh.2:6).

Ni changamoto. Lakini imeandikwa, “Mungu ashukuriwe, anayetushangiliza daima katika Kristo, na kuidhihirisha HARUFU YA KUMJUA YEYE kila mahali kupitia sisi. Kwa maana sisi tuwe MANUKATO YA KRISTO, mbele za Mungu, katika wao wanaookolewa, na katika wao wanaopotea.” (2 Wakor.2:14,15).

Unaona? Kusudi la Mungu ndilo tuwe manukato ya Kristo mbele ya watu na mbele ya Mungu; tuidhihirishe harafu ya KUMJUA Yeye. Ni jambo la tabia, siyo la ujuzi. Inagusa halisia ya maisha yetu – kama ninamjua Yesu au ninajua juu Yake tu. Kama ninao ujuzi tu JUU YA Yesu, nitakuwa na harufu ya utupu au kiburi mbele ya watu na nitatembea kama mtu kipofu.

Uzima wa milele ni nini? Kujua mengi juu ya Yesu? Hapana. Bwana Yesu ameshaufunuliwa kwetu,

“uzima wa milele ndio huu, WAKUJUE WEWE, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.” (Yoh.17:3).

Je, naweza kuyajua mengi juu ya Yesu bila kumjua? Ndiyo. “Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake.” (1 Yoh.2:4). Hatuwezi kumjua Yesu na Baba Yake isipokuwa sisi tubadilishwe siku hadi siku tufanane na mfano wa Bwana toka utukufu hata utukufu. (2 Wakor.3:18). Njia moja ya ulazima sana ambayo tunapata kumjua Yeye nidyo kupitia USHIRIKA wetu naye – tunabadilishwa na mambo yale tunayoshirikana nayo katika mioyo, akili na roho zetu! Tabia yetu na mwenendo wetu ni matokeo ya ushirika wetu – ushirika wetu iwe na mambo mabaya au mazuri. Bila shaka tunashirikiana na jambo fulani muda wote mioyoni na akilini zetu. Je, tunatumia na kushika muda ili tupate nafasi tuwe na ushirika na Baba na Mwana – siyo kuomba kwa ajili ya mahitaji tu, bali kushirikiana na Baba na Mwana katika upendo na kubadilishwa na ushirika huo! (1 Yoh.1:3). Na tutambue, Yesu Kristo alimwagika damu yake ili tuingize katika ushirika huo. Je, kipo kitu kikuu kuliko kuujua ushirika na Baba na Mwana?

Mistari hiyo ndio neno la Mungu kwangu, na neno la Mungu kwako. Nategemea mambo hayo siyo jambo geni kwetu! Kama ni jambo geni kwako, ujitoe maisha yako Mwokozi Yesu Kristo kabisa, siyo ovyoovyo, bali kwa moyo wako wote; omba unalohitaji kuomba. Na mwombe Mungu akuongoze kuingia katika ushirika Naye na akujaze na Roho Wake ili umjue kwelikweli. Paulo aliomba akisema, “siachi kutoa shukrani kwa ajili yenu; nikiwakumbuka katika sala zangu, Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo KATIKA KUMJUA YEYE; (Waefeso 1:16,17). Amen.

Na Yesu awe maisha na njia yetu – nyumbani, shuleni, kazini, barabarani na kanisani.

RUDI KWA MWANZO

11

Je, vipi tunayahesabu mateso ya maisha yetu? Je, tunafikiri pengine dhiki na mateso ya maisha yetu yanazidi kupita kiasi – kiasi ambacho hatuwezi kukivumilia? Ni mzigo ambao hatuwezi kuubeba, na tunakata tamaa? Je, tunazama katika mambo ya magumu ya maisha? Paulo hakusita kutangaza ukweli huu,

“Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu.” (Warumi 8:18).

Je, mtume Paulo hakuyakuta na mateso katika maisha yake? Kinyume chake! Yeye alipata mateso zaidi ya karibu watu wote! (2 Wakor.6:48; 11:2328). Lakini aliyahesabu ‘si kitu’! Utukufu ule utakaofunuliwa kwetu ni mkuu mno kuliko mateso ya maisha yetu kiasi cha kutokuweza kulinganisha utukufu ule na mateso ya maisha yetu! Je, hiyo ni nia yetu? Utukufu ule ni wa milele! Lakini juu ya matatizo yetu, neno la Mungu linatufundisha kwamba,

“Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana.” (2 Wakor.4:17).

Kumbe, Paulo ni muumini wa namna gani! Anasema ‘dhiki yetu nyepesi’ na tena ‘ya muda wa kitambo tu’! Lakini hiyo siyo maneno na mtu tu – ni ukweli wa Mungu kwa mioyo yetu. Je, tunaishi kwa nia hiyo na kadiri ya ukweli huo? Haitoshi kufikiria ukweli huo kwa dakikia kadhaa, au kwa siku moja tu. Lazima ukweli huo uingie moyoni mwako kwa kina sana na kubadilisha nia yako ili uyahesabu mateso ya maisha yako kwa macho mapya! Vipi? Njia moja ni kama ifautavyo,

“tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele.” (2 Wakor.4:18).

Lakini tunahitaji saburi na ustahimili,

“Basi msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kuu. Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate ile ahadi.” (Waebr.10:35,36).

Na Paulo anatufafanulia kwamba, “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.” (1 Wakor.10:13)

Na mwandishi wa Waraka kwa Waebrania anatutia moyo kwa maneno haya pia,

“Sasa bado hatujaona vitu vyote kutiwa chini yake, ILA TWAMWONA YEYE,’ yaani, Yesu! (Waebr.2: 8,9).

Mungu atubariki siku ya leo ili “tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu, TUKIMTAZAMA YESU.”  Amina!

RUDI KWA MWANZO

12

UPENDO HAUPUNGUI NENO

Yesu alikuwa amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda UPEO, MPAKA MWISHO. Waume, wapendeni wake zenu, vivyo hivyo. Wake, wapendeni waume zenu, vivyo hivyo, kwani…

…upendo HUVUMILIA yote. Upendo hustahimili YOTE. Upendo hautafuti mambo YAKE. Upendo haupungui neno WAKATI WO WOTE. Kwani Mungu ni upendo.

Haiwezekani? Lakini kumbuka, tunaimba ‘Yote yawezekana.’ Na neno Lake linatuambia kwamba HAKUNA neno lisilowezekana kwa Mungu.

Je, tunatembea na Mungu?

“Neema yangu yakutosha.” Je, unadai haitoshi?

Unapaswa kujibu maswali hayo mbili kwa dhati.

Kama umejibu neema yake haitoshi, maisha ya kiroho yako wapi?

Tatizo ni nini?

Tunaimba, ‘Siyo mimi ninayeishi, bali Kristo ndani yangu!’ Lakini mke au mume wako anajua kama hiyo ni kweli nyumbani au sivyo! Tatizo ni hili: SISI tunataka KUISHI badala ya kujinyenyekeza mbele ya Mungu ili Kristo aishi ndani yetu. Tunasisitiza kushika HAKI YETU yenyewe na kutangaza ‘siyo sawa!’ Tunakataa tusife (kusulibiwa pamoja na Kristo)!

Tunaanguka katika kujihurumia. Hiyo ni jambo la kujipenda na kutokujali neno la Mungu.Tunachukizwa, kukasirika na tunapatwa na uchungu. Hiyo ni jambo la kiburi.

Hayo ndiyo matatizo ya watu. Tufanyaje?

‘Mungu HUWAPINGA wajikuzao, bali HUWAPA NEEMA wanyenyekevu.’ (Yakobo 4:6). Waumini wengi wanapungukiwa na neema kwa sababu ya hiyo, yaani, wanakataa ‘kunyenyekea chini ya mkono wa Mungu.’ (1 Petro 5:6).

Lakini maandiko yanasema, ‘..hutujalia sisi neema iliyozidi.’ (Yakobo 4:6). Au unadai siyo hivyo?

Njia yetu ni kujinyenyekea ‘chini ya mkono wa Mungu.’

Lakini tusifikiri hilo ni jambo gumu kana kwamba lazima sasa nibebe mzigo nzito kila siku! Hapana! Neno la Mungu linatangaza kwamba, “Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito.” (Yoh.5:3); na Yesu amewaita watu kwa maneno hayo, “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni NIRA YANGU, mjifunze KWANGU; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi MTAPATA RAHA nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni LAINI, na mzigo wangu ni MWEPESI.”

Ungweza kwenda kwa ‘Semina ya Ndoa’ (tena?) au kununua kitabu kingine juu ya mada hiyo, na labda ‘ungejifunza’ mambo yaliyofaa. Lakini kama usipo tayari kujinyenyekea chini ya mkono wa Mungu na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani (Yakobo 1:21) katika MAMBO YALE yanayotokea nyumbani mwako kila siku, hutapata faida yo yote kupitia ‘Semina ya Ndoa’ au kitabu chochote.

Jambo hili ni muhimu sana, na hamna ‘Siri ya Ndoa yenye Furaha’, siyo jambo la kujifunza ‘mbinu wa kufanikiwa’, hata siyo jambo la saikolojia. Jambo hili linahusu uhusiano wako na Mungu na hali ya moyo wako mbele Yake! Linahusu uhusiano wako na neno la Mungu na kama utaishi sawasawa na neno Lake au la. Hiyo tu.

Twende katika njia ile ambaye Bwana Yesu ameshatutayarishia.

Upendo haupungui neno wakati wo wote kwani Upendo hautafuti mambo yake.

Mungu alibariki neno lake kwetu.

RUDI KWA MWANZO

13

SIO TAMU. NI SUMU! Picha za machafu kwenye mtandao.

“Tafuteni kwa bidii…huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao.” (Waebr.12:14).

Swali ni hili. Je, mimi ni mtu wa dini tu anayeishi dhambini, au nimezaliwa kwa Roho ya Mungu, nimewekwa huru mbali na dhambi, na ninashinda dhambi kwa neema ya Mungu? Lengo la agizo la Mungu ni ‘upendo utokao katika moyo safi.’ (1 Tim.1:5). Basi, kama tukipenda kuziona picha za machafu kwenye mtandao au mahali po pote mengine, jinsi tunavyoweza kumwona Bwana siku ile? Kama tunajifurahisha na mambo machafu kwenye mtandao, ujuzi wetu wote juu ya Injili hautaweza kutuokoa au kutusaidia siku ile. Kama tunapenda kuziona picha za machafu, hatutaurithi ufalme wa Mungu. Picha za ngono kwenye mtandao ni sumu ya kiroho! Ni dhambi kubwa sana kuziona. Itaangamiza maisha yako ya kiroho. Zinajaza akili yako na mawazo machafu, na mawazo haya yanapelekea kufanya matendo machafu – zitayaangamiza maisha yako kabisa! Kama tukicheza na dhambi hiyo, hatuwezi kuwahudumia wengine! Tunajidanganya tu. Kwa nini ‘waumini’ sio wachache wamejiunga na facebook groups zinazoonyesha picha za machafu? Siyo tamu! Ni sumu! Kila mara dhambi hutaka kuwavuta watu ikidai ni kitu kitamu! Shetani husema, “Hutakufa! Ni tamu! Utajifurahisha!” Lakini inaleta kifo! Wengine wanajidai ni wakristo lakini hatuwezi kumtumikia Bwana na kuitumikia dhambi. Inanihuzunisha sana kwamba wao wanaodai kuwa waumini wanafurahia kuangalia picha za namna hizo. [Kama mtu mwingine alilibandikisha jina lako na group kama hiyo bila wewe kuja (hiyo ni kosa la facebook), mara unapotambua, zifute tu! – vinginevyo watu wengine wanapoona facebook yako watafikiri ulijiunga kwa kusudi! ]

Bwana Yesu ameitayarisha njia ya kukusamehe, kukusafisha na kukweka huru mbali na dhambi. 

RUDI KWA MWANZO

14

“KALIBU NI KWA FEDHA NA TANURU KWA DHAHABU, BALI BWANA HUUJARIBU MOYO.” (Mithali 17:3).

Kazi ya kupata dhahabu safi kabisa ni ngumu sana na inahitaji moto mkali sana ili kuitenga na mambo mengine tusiyoyataka na yasiyofaa!  Vile vile neno la Bwana linafanya kazi ndani ya mioyo na maisha yetu kama kalibu na tanuru ili kutofautishiana kati ya maneno na hamu yetu (na yale tunayoyadai), na makusudi yetu kweli kweli ndani ya mioyo yetu! Mungu ni mwaminifu na mwenye neema, rehema na uvumilivu katika kazi hii ili tufananishwe na Mwana Wake Yesu Kristo hapa duniani. Kwa hiyo, tuziache ngao zetu za nje tulizozitengeneza na kuijenga kwa ajili ya watu ili tujionyeshe vizuri au hata tuonekane kuwa na adabu. Macho ya Bwana ni kama mwali wa moto yanayochunguza kwa kiini sana mioyo yetu. Na tumruhusu Yesu Kristo kutubadilisha kwa ndani sana, pale ambapo watu hawaoni jinsi tulivyo kweli kweli. Anaweza kufanya hivyo kama tukijinyenyekesha mbele Yake na tusipotafuta mapenzi yetu! Wengi wanadai wanamtumikia Mungu bali ukweli ni wanajitumikia wenyewe. Kama tunadai tunafanya kazi sana kwa ajili ya ufalme wa Mungu lakini ukweli ni kwamba tunaifuata njia ya kujipendeza, cheo, fahari au matekelezo ya makusidi yetu, ndipo na tuwe wazi juu ya hali ya mioyo yetu na kukiri makosa yetu makubwa na kutubu na toba ambayo itabadilisha mwelekeo wa maisha yetu na nia ya mioyo yetu. Wengi wanadhamini malengo na ndoto zao kuliko yote, wanazishika sana kana kwamba hawaiwezi kuziacha. Ingekuwa ‘kifo’ kwao kuziacha na kuyakumbatia mapenzi ya Mungu na msalaba wa Kristo Yesu. Lakini italeta uzima wa milele. Hakuna wengi walio tayari kupokea kifo cha tamani yao wawe kitu au kuwa na kitu kwa ajili ya kumfuata Yesu. Lakini kama tusipomruhusu Bwana kuutengeneza mioyo yetu wakati tulipo duniani, siku inakuja sawasawa na neno la Mungu,

“…kama mtu akijenga juu ya msingi huo (Yesu Krsito), dhahabu au fedha au mawe ya thamani, au miti au majani au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa dhahiri. Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. Kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa, atapata thawabu. Kazi ya mtu ikiteketea, atapata hasara.” (1 Wakor.3:12-15).

Kwa hiyo na tujitoe kwa Bwana kwa sababu,

“BWANA hatazami katika vile vitu mwanadamu avitazamavyo. Mwanadamu hutazama katika sura ya nje, lakini BWANA hutazama moyoni.” (1 Samweli 16:7).

RUDI KWA MWANZO

15

ABIGAILI NA MAMBO YA NDOA.

Je, unafikiri mume au mke wako ni mgumu kuishi naye? Je, unamcha mungu kuliko kujipendeza mwenyewe? Abigaili hakuwa na kanisa. Abigaili hakuwa na Biblia. Abigaili hakuwa amebatizwa na Roho Mtakatifu. Lakini basi kinyume chake, Abigaili alikuwa na mume tu aliyekuwa hana adabu, tena mwovu, tena mkorofi, aliyeitwa Nabali.

Lakini Abigaili ALIMCHA Mungu. Na huyo mwanamke alikuwa mwenye akili njema, mzuri wa uso.

Katika 1 Samweli 25 tunasoma juu ya Nabali. Kondoo na mbuzi wa Nabali walikuwa na usalama wakati wote walipokaa chini ya ulinzi wa watumishi wa Daudi. Baadaye Daudi alipoomba Nabali awape watumishi wake msaada wa vyakula, Nabali akawatukana tu. Mara moja Daudi aliamua kumwua Nabali – lakini mtumishi mmoja wa Nabali aliweza kumwambia Abigaili mambo hayo. Alifanyaje Abigaili? Je, alifurahia tukio hilo? Je, aliwaza, “Hii sasa ni fursa yangu kwa Mungu ya kuniondoa toka kwa mume huyu! Sasa nitakuwa huru kutokana na mume huyu mkorofi! Bado mimi ni mrembo – kwa nini niolewe na mume kama huyu? Abigaili alifanyaje sasa ili awe huru kutokana na mume wake mwovu? Hakuna chochote! Yeye hakupaswa kusema wala kufanya lolote lile! Yeye angeweza kutulia TU pale na kumwacha Daudi aje pamoja na watu wake kumwua mumewe Nabali! Na wewe ungefanyaje?

Lakini Abigaili ALIMCHA Mungu! Hakujipendeza. Hakujitumikia. Alitaka kumpendeza Mungu na kumtumikia! Hakujifikiria yeye mwenyewe, au ajiokoe mwenyewe kutokana na hali hiyo ngumu. Hapana. Yeye alifikiria tu kumsaidia Daudi asilete hukumu juu yake kwa kujilipiza kisasi mwenyewe na kumwua mumewe. Alimwamini Mungu. Kwa hiyo alinyenyekea chini ya mikono ya Mungu na hakufikiri juu ya faraja yake mwenyewe au hali yake ngumu wala hakutafuta njia ya kutoroka kutoka katika mazingira yake ngumu. Na wewe? Aliamini kuwa kila kitu kilikuwa mikononi mwake Mungu, na kwamba iwapo mumewe inampasa kufa, basi huo ulikuwa ni wakati wake Mungu mwenyewe na wala sio kwa mkono wa mwanadamu. Hivyo Abigaili alifanyaje? Yeye aliandaa zawadi ya vyakula kwa ajili ya Daudi na hao watu wake Daudi alioandamana nao. Abigael akaondoka na kumfuatilia Daudi hukohuko njiani, “Ndipo hapo Abigaili alipomwona Daudi, … akainama mpaka nchi. Akamwangukia miguuni pake, akasema, Juu yangu, bwana wangu, JUU YANGU MIMI NA UWE UOVU; tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako.”

Kumbe, Abigaili alikuwa yu radhi kuyatoa maisha yake kwa ajili ya mumewe mwovu! Kwa kuwa alimwamini Mungu, alitaka kumwokoa mumewe, na pia Daudi mwenyewe kutokana na hali ya kujilipiza kisasi. Abigaili hakujitafutia mlango au njia ya kutoka ili awe huru kutokana kwa mumewe mwovu. Na wewe? Aliamini kuwa kila kitu kilikuwa mikononi mwake Mungu. Ndoa yake ili kuwa mikononi mwa Mungu. Na alikataa kufanya cho chote kubadilisha hali hiyo ya maisha yake!

Je, mumeo au mkeo ni mtu mgumu sana hata unafikiri ungeshindwa kuendelea kuishi naye? Jaribu kufikiria hali ilikuwaje kwa mwanamke kuishi na mume kama Nabali!

Je, wewe ni mwamini? Je, unayo Biblia? Je, unakiamini kilichoandikwa ndani ya Biblia? Unampenda Mungu na unaamini kuwa yeye yuko pamoja nawe katika mazingira yoyote yale? Je, unatafuta kumpendeza yeye au kujipendeza wewe mwenyewe? Je, umepatwa na ubaridi au ugumu dhidi ya mumeo au mkeo kwa sababu unajisikia kuwa yeye ni mtu mgumu? Je, unamshughulikia kwa dharau na chuki? Yawezekana unataka kuniambia, “Lakini…” Lakini nini? Unataka kusemaje hapa? Unatakaje kujipa haki wewe mwenyewe – hapa hatuongelei juu ya dhambi kubwa, lakini ni kuhusu kile unachokifanya pale unapojisikia kuwa mumeo au mke wako ni mtu mgumu kwako. Je, unatafuta njia ya kuikwepa hali unayoipitia kuliko kuitafuta njia ya Mungu katika hali hiyo? Yesu ndiyo njia. Tabia yake ndiyo njia na uzima. Kama umeingiwa na ubaridi au umekuwa mgumu juu ya mumeo au mke wako, na ikiwa wewe ni mkristo, usimlaumu – sio mapenzi ya Mungu kwako uwe baridi au mgumu bali huo ni uchaguzi wako mwenyewe. Usimlaumu MTU yeyote. Utubu badala ya kuuachilia moyo wako uwe mgumu. Jinyenyekeze mwenyewe chini ya mkono wa Mungu wenye nguvu na upokee neema izidiyo – ambayo itakubadilisha WEWE  kwanza, na kisha umpende mumeo, mpende mkeo.

Abigaili hakuwa na Biblia isemayo kuwa, “mke ajinyenyekeze kwa mumewe”, wala hakuwa na Biblia inayosema, “waume wapendeni wake zenu”. Hakuwa na Biblia inayowaambia waumini wanaojikuta kwenye hali ngumu, , ‘Neema yangu YAKUTOSHA; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu.’ (2 Wakor. 12:9). Je, wewe unaamini mstari huu? Je utalipokea neno hili? Abigaili aliishi maisha ya namna hiyo. Je, wewe unaamini kuwa mume wako au mkeo ni mtu mgumu mno au ni mgumu kupita kiasi kwako? Lakini sikiliza neno la Mungu lisemavyo, “Lakini hutujalia sisi neema ILIYOZIDI; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu.” (Yakobo 4:6).

Ikiwa utapungukiwa na neema ya Mungu katika mahusiano yako, waweza kupata sababu toka katika mistari hii ya neno ka Mungu.

Waweza kujisomea vitabu vingi vihusuvyo ndoa, waweza pia kwenda kuhudhuria semina nyingi zihusuzo ndoa, lakini kama humwendei Mungu na kujinyenyekeza mwenyewe mbele zake kwanza, hakuna hata jambo moja kati ya hayo ufanyayo yatakayo kusaidia.

Daudi alimwambia Abigaeli, ‘ubarikiwe wewe’! Nawe pia utabarikiwa, na utafanyika kuwa baraka kwa wengine nyumbani mwako ikiwa unampenda Kristo na kumtumikia kuliko kujipendeza mwenyewe tu, ikiwa unamfuata Yeye na ‘kuipoteza nafisi yako’ kwa ajili Yake kuliko kujaribu kujiokoa maisha yako kwa kujaribu kuikimbia hali ngumu au kulalamika kuhusu hali hiyo, na kuwa mgumu na mwenye uchungu.

Kumfuata Kristo Yesu na kujikana mwenyewe kutayafanya “machungu” kuwa “matamu” katika maisha yetu. “Kujitwika msalaba wako” haimaanishi kubeba mzigo nzito! Inamaanisha kujikana mwenyewe na kumchagua Yesu na njia yake, na huku kunaleta MABADILIKO katika maisha yako. Kama neno la Mungu linavyosema, “Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito”, na tena, “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni NIRA YANGU, mjifunze KWANGU; kwa kuwa mimi ni MPOLE na MNYENYEKEVU wa moyo; nanyi mtapata RAHA nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni LAINI, na mzigo wangu ni MWEPESI. (1 Yoh. 5:3; Mathayo 11:28-30).

Abigaeli hakujaribu kumbadilisha mumewe, alikabidhi uhai wake mikononi mwa Mungu na alikuwa anaridhia hukumu ya mumewe imwangukie yeye. Ikiwa Abigael angeweza kufanya hayo na kuwa kama hivyo nyakati za Agano la Kale, je, haitupasi sisi kuonyesha hata upendo mkuu na dhabihu katika mahusiano yetu sisi kwa sisi – sisi ambao tumeipokea neema na upendo wa Mungu kupitia Yesu Kristo ili kwamba uzima wake upate kudhihirishwa katika maisha yetu.

Inawezekana kabisa neno hilo siyo neno kwa wote, hata hivyo inawezekana ni neno kwa wengine.

Mungu alibariki neno lake kwa mioyo yetu.

©  David Stamen  2019  somabiblia.com

RUDI KWA MWANZO

 

Comments are closed.

 
%d bloggers like this: