RSS

INJILI YA MAFANIKIO INAVYOLIANGAMIZA TAIFA.

Ni saa sita za mchana Jumapili nikiwa katika kanisa moja jijini Dar es Salaam. Ghafla waumini ambao walikuwa wakiimba nyimbo za kumsifu Mungu huku wakiwa wamekaa, wanasimama na kuanza kuimba wimbo ambao unamsifu kiongozi wa kanisa hilo ambaye kwa muktadha wa makala hii jina lake tutamwita ni nabii Malamula wa Malamula. Muda huo ndio anaingia kuongoza ibada.

Ninamwona Nabii Malamula amevaa suti ya kijivu inayongaa, anatembea kwa ukakamavu kama askari vile, haraka haraka anaruka juu katika madhabahu ambayo imenakishiwa kwa gharama kubwa. Sasa anakuwa mbele ya waumini ambao kwa makadirio ni kati ya 1,000 na 1,500 hivi. “Haleluya wapendwa, Bwana asifiwe sana!”, anasalimia kusanyiko Nabii Malamula, na waumini nikiwemo mimi niliyehudhuria ibada kanisani hapa kwa mara ya kwanza, tunaitikia ameeeeni baba!

Baada ya maneno machache ya utangulizi, Nabii Malamula mwenye umri unaokadiriwa kuwa miaka 56 hivi anasema siku hiyo Bwana, yaani Mungu, alikuwa amemwongoza kuendelea kufundisha somo linalosema Kuchunguza njia za kumiliki fedha, ambalo alisema alianza kulifundisha Jumapili iliyopita. Alisema ili kuendana na kasi yake katika kufundisha, na ili waumini waweze kuelewa vizuri zaidi somo hilo ameandaa kanda za audio za mafundisho ya somo hilo, hivyo akawataka wote tununue kwa Shilingi 7,000.

“Watu wengi ni wajinga sana, hawajui ukweli kwamba Mungu ameishawatengenezea watoto wake mazingira ya kuwa matajiri hapa duniani. Ninaposema kuwa matajiri, ninamaanisha kuwa matajiri kweli kweli. Usipoteze fursa hii! Nunua kanda hiyo, na jambo la msingi ambalo unapaswa kufahamu kama muumini ni kwamba, sio dhambi kutamani kuwa tajiri,” anasema kwa namna ya kuunguruma Nabii Malamula wa Malamula.

Nabii huyu ambaye pia ndiye askofu mkuu wa kanisa hili lenye matawi katika baadhi ya mikoa hapa nchini, anatuambia tunaomsikiliza kuwa tunapaswa kuwa na ndoto kubwa, lakini pia ni lazima tujue kuwa kuna watu wanaoua au kuziiba hizo ndoto. Kuna watu wengi ambao kazi yao ni kuua ndoto zenu, kuna watu wengi tu ambao kazi yao ni kuiba ndoto zenu, msiwaruhusu waue na kuiba ndoto zenu, anasema nabii huyo kabla ya kutupatia unabii kama ifuatavyo:

“Kesho yako itakuwa nzuri zaidi. Mwaka 2017 utafika ulipokuwa unapataka. Wasichana waliokuwa wanahitaji kuolewa wataolewa, wengi wenu mtanunua magari mapya, na wanawake tasa watajifungua mapacha.”

Unabii huo ulipokelewa kwa shangwe na vigelegele na waumini, lakini wakati shangwe zikiendelea, Nabii Malamula wa Malamula aliliambia kusanyiko kuwa watu ambao wangependa kumwagikiwa na baraka hizo wapite mbele ya madhabahu na kumtolea Mungu sadaka iliyonona itakayomfurahisha. Kundi kubwa la watu lilijitokeza mbele na nabii akaanza kuwapanga kulingana na kiasi cha fedha ambacho muumini angetoa au kuahidi kutoa. Nabii alitoa angalizo kuwa kiasi cha kutoa hakitakiwi kuwa chini ya Shilingi laki mbili. Baada ya dakika chache mamilioni ya fedha yalikusanywa na mengine kuahidiwa.

Hii ni sehemu tu ya vionjo vinavyopatikana katika kile kinachojulikana kama Injili ya Mafanikio. Na aina hii ya injili ambayo imekuwa na kishindo kikubwa ikikokota idadi kubwa ya watu, imesambaa na kukita mizizi katika nchi nyingi maskini, Tanzania ikiwemo. Ni injili inayoahidi mtu utajiri na afya njema, lakini nyuma ya pazia ni injili inayosababisha madhara makubwa katika jamii, kama utakavyoona huko mbele.

Injili ya Utajirisho inatokana na neno la Kiingereza – Prosperity theology, au Prosperity gospel. Kwa Kiswahili hujulikana pia kama Injili ya Utajirisho. Kwa mujibu wa Wikipedia, Injili ya Mafanikio inasimamia zaidi mafanikio ya kiafya na utajiri wa fedha na mali. Ni injili ambayo inaaminisha watu kuwa kadri muumini anavyochangia kanisani ndivyo anavyojiongezea utajiri. Ni injili yenye mtazamo kuwa Biblia ni mkataba baina ya Mungu na wanadamu. Kwamba kama mwanadamu atakuwa na imani kwa Mungu, atakuwa salama kiafya na atakuwa na mafanikio katika kila kitu.

Injili hii ina historia yake, lakini lianza kuenezwa zaidi kwenye miaka ya 1950 huko nchini Marekani kufuatia kuibuka kwa Uamsho wa Uponyaji, baadaye miaka ya 1980 injili hii ilishika kasi kwa kuwatumia wahubiri waliokuwa wakitumia zaidi televisheni. Injili hii ya mafanikio imekuwa ikikosolewa na watumishi kutoka madhehebu mbalimbali ya Kikristo, wakiwemo Wapentekoste, ambao wamekuwa wakisisitiza kuwa injili hii ni sawa na ibada ya sanamu, na iko kinyume na maandiko matakatifu.

Kutokana na kukosolewa sana baadhi ya watumishi wanaoendesha injili hiyo hawapendi kutambulishwa kama watumishi wanaohubiri injili ya mafanikio, wala hawapendi makanisa au huduma zao zijulikane kuwa ni kwa ajili ya injili ya aina hiyo, lakini wawapo madhabahuni wanahubiri injili ya aina hiyo. Kama ambavyo wahubiri nchini Marekani walitumia zaidi TV kueneza injili hiyo, hapa Tanzania nako televisheni imetumika zaidi kama njia ya kueneza injili hii. Mbali ya televisheni, injili hii inaenezwa kupitia vitabu vinavyoandikwa na watumishi, ambavyo hupigiwa debe madhabahuni ili vinunuliwe kwa wingi.

Kama nilivyoahidi huko juu, zifuatazo ni sababu zinazochangia ujumbe unaotokana na injili ya utajirisho kuiangamiza Tanzania:

 1. Ni mchanganyiko wa imani potofu. Kabla ya Ukristo haujaingia nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla, watu walitegemea zaidi waganga wa kienyeji ambako walifanyiwa matambiko wakiambiwa watoe kuku au hata mbuzi, ili wapate uponyaji au baraka katika shughuli zao za biashara au kazi. Walimwaga pombe kama sadaka kwa miungu ili wasikie maombi yao. Leo mambo ya namna hiyo hiyo yanaendelea, kilichobadilika tu ni kwamba mambo hayo yanafanywa na wahuburi ambao ni waganga wa kienyeji lakini waliobadili majina na kujiita wachungaji, manabii au mitume. Kuna wachungaji au manabii ambao wamezika wanyama katika nyumba za ibada. Kuna manabii ambao wanawaambia waumini wapeleke mchanga wanaochota walipokanyaga wabaya wao. Kuna manabii wanawauzia maji na mafuta waumini ili wakanyunyize majumbani mwao waweze kubarikiwa. Waumini wanaotii ulaghai huu wanaambiwa kuwa pamoja na kutumia vitu hivyo mambo yao hayawezi kunyoka hadi watoe michango mikubwa ya fedha au mali.

Hapa maana yake ni kwamba, tunakuwa na taasisi ambazo zimesajiliwa na serikali zikiaminika kuwa zinafanya kazi ya kikanisa, na serikali pamoja na jamii inaona hivyo, lakini ukweli ni kwamba ni taasisi zinazotumia usajili wa makanisa, kuhalalisha mambo yaliyo kinyume na kanisa la Mungu.

 1. Inachochea tamaa. Mtu yeyote anayemjua Mungu anaweza kujifunza uzuri wa kutoa au kusaidia wengine. Lakini Injili ya Mafanikio inawafundisha watu kuangazia zaidi katika kupata, na sio kutoa. Ni ubinafsi wa kiwango cha juu na hali hii imesababisha kuwa na idadi kubwa ya Wakristo bandia. Waumini wanaendelea kutakiwa kupanda mbegu nono ili wavune baraka juu ya baraka. Katika baadhi ya makanisa hiki kinachoitwa makongamano hukusudiwa kutumika kujipatia utajiri kwa watumishi, na mwisho wa siku utawasikia wanatamba kuwa wanavaa nguo za gharama, wana majumba ya gharama; nakadhalika.

Na utawasikia wakiwaambia waumini kuwa ukiroho wa mtu hupimwa kulingana na thamani ya vitu anavyomiliki, jambo ambalo ni kinyume kabisa na mpango wa Mungu kwa mwanadamu. Utawasikia wakisema eti mtu aliyeokoka hawezi kushindwa kujenga nyumba nzuri ya kisasa, hawezi kukosa gari zuri. Kwa kuwa namna ya tamaa ninayoizungumzia hapa huandaliwa madhabahuni basi husambaa na kuwaingia waumini kwa kiwango kikubwa.

 1. Inatengeneza kiburi na majivuno. Hali hii haifichiki katika makanisa yetu. Ni rahisi kuiona ukipenda. Makanisa yanayohubiri injili ya Mafanikio yanatengeneza wajasiriakanisa. Watumishi wanapanda makanisa sio kwa sababu wana mzigo wa kufikia roho zilizopotea bali kwa sababu wameona kiashiria cha kuwa na fedha iwapo watakuwa na makanisa na viti katika makanisa hayo vikajaa watu.

Na watumishi wa namna hii wana viburi vya ajabu na hawawezi kuwasikia hata baba zao wa kiroho. Ujumbe wa kiburi na majivuno unaotumwa kupitia injili ya mafanikio unazalisha wasaka fursa ambao hawana kiongozi wa kiroho anayeweza kuwashauri au kuwarekebisha wanapoonekana kukosea.

Wahubiri wa injili hii waliofanikiwa zaidi ndio hatari zaidi maana hawaoni aibu kuliambia kusanyiko kuwa Yesu alikufa msalabani ili walokole waweze kumiliki benzi!

 1. Inafanya kazi kinyume na tabia ambazo ameumbiwa Mkristo. Ujumbe wa mafanikio utokanao na injili ya mafanikio hautoi nafasi ya kutosha kwa unyenyekevu, hautoi nafasi kwa kuchelewa ambako Mkristo anafahamu kuwa Mungu hapangiwi na hutenda kwa wakati wake, wala haikubaliani na ukweli kwamba mtu anaweza kuugua.

Injili ya Mafanikio huahidi njia ya mkato ambayo ni kinyume na mpango wa Mungu. Wahubiri wa injili hii huahidi matokeo ya hapo kwa hapo. Kuna nabii mmoja eneo la Mbezi, Dar es Salaam, yeye aliwaambia waumini kanisani kwake kuwa katika kipindi cha miezi sita kama kuna muumini ambaye hatakuwa amebarikiwa kuwa na gari kanisani hapo yeye ataacha kuhubiri! Ingawa matokeo yalikuwa tofauti kabisa lakini mtu huyu anaendelea kuhubiri. Anachokifanya, anaendelea kuwaambia wafuasi wa kanisa lake kuwa, kama hujabarikiwa ni kwa sababu hukutoa fedha nyingi katika matoleo. Wakati Yesu anatutaka tujikane ili tumfuate Yeye, lakini wahubiri wa injili ya mafanikio wao wanatutaka tumkane Yesu ili tufuate matamanio yetu ya kimwili.

 1. Inawafanya watu waendelee kuwa masikini.

Ulaghai huu hauwafanyi watu kuwa matajiri. Badala yake huwaibia watu pesa zao na hivyo kuwafanya wawe masikini zaidi.

Yesu alipowazungumzia manabii wa uongo kama mbwa mwitu waliovaa ngozi ya kondoo, alikuwa akituonya akitutaka tuwatambue kwa matunda yao. Mathayo 7:17 inasema, “Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya.” Ni matunda yapi yanatokana na kuhubiri injili ya mafanikio?

Na Jackson Malugu

http://www.mwanzonews.com/2016/12/24/injili-ya-mafanikio-inavyoliangamiza-taifa/

 

4 responses to “INJILI YA MAFANIKIO INAVYOLIANGAMIZA TAIFA.

 1. Noel Balama

  October 26, 2017 at 10:27 am

  Ujumbe huu ni mzito sana.Nataka nipate zaidi

   
 2. Noel Balama

  October 26, 2017 at 10:40 am

  Wewe mtu ubarikiwe sana ndugu yangu yaani haya ni ya kweli kabisa.Sijui tutafanyaje ndugu maana hao watu wana wafuasi wengi mno.Lakini si hivyo tu bali wanaweka ufa mkubwa katika huduma…maaana muumini akitenda dhambi ukamtenga usishangae…… kama hajaanzisha kanisa basi anaenda kuwa kiongozi wa kanisa tena mara nyingine ni la jirani tu..

   
  • dsta12

   October 26, 2017 at 11:35 am

   Asante Noel. Unaweza kusoma masomo mengine kwenye tovuti hiyo hiyo. Je, unayo facebook account, whatsapp namba au email ili tuweze kuwasiliana?

    
 3. Zakayo Sylvester James

  February 20, 2019 at 10:34 am

  Ubarikiwe sana mtumishi kwa ujumbe mzur kwel nimebarikiwa na umenifungua macho ila naomba unisaidie material zaid yanayohusu injili ya mafanikio na miujiza maaana mm ni mwanachuo wa masomo ya uchungaji ndy nafanya utafiti juuu ya maswala hayo by zakayo s.james

   

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

 
%d bloggers like this: