RSS

Kuhusu Ulipaji wa Mahari

                                                     KUHUSU ULIPAJI WA MAHARI:

                           Matokeo ya kupanga gharama kubwa za mahari kupita kiasi.

“…lakini mimi nawaambia, kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa  mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini.” (Mathayo 5:32).

Hili ni fundisho la msingi.Tunaona hapa kuwa Yesu anatufundisha kwamba mwanamume ndiye anayesababisha mkewe kuwa mzinzi. Kwa hiyo ni mume ndiye anayebeba mzigo wa dhambi ya uzinzi ya mkewe. Ingawa pia, naye hufanya dhambi kwa kuolewa tena.Tunaona katika mstari huu kuwa Yesu hamshitaki mwanamke. Kwa nini?  Ni kwa sababu tendo la mwanamume kumwacha mkewe, linaweza kumweka katika hali ya kujaribiwa kupita kiasi.  Lakini ni kwa nini iwe kupita kiasi?  Ni kwa sababu, kwanza kabisa, tabia ya mwanamke kwa ujumla ni kuwa na hamu kubwa ya kuolewa. Soma 1 Timotheo 5:11-12. Sababu ya pili, mwanamke anapoachika na mumewe ndipo huachiwa hali ya kutokutoshelezwa.  Kwa hiyo amebakia kuwa mtu muhitaji sana.( Soma 1 Timotheo 5:9-10, na Matendo 6:1.Tunaona hapo kuwa ulikuwa ni wajibu wa kanisa kumtunza mjane wa kweli). Kwa hiyo atajaribu kuolewa tena ili aweze kupata njia ya kujitosheleza aweze kuishi. Na iwapo akiolewa, atakuwa anazini. Sawasawa na maneno ya Yesu, hali hii yote imekuwa hivyo kutokana na tendo la mume, yaani mke ameingia katika dhambi hii kutokana na mume kumwacha mkewe. Ni mume ndiye aliyesababisha hayo, kutokana na ugumu wa moyo wake.  Anamkwaza mkewe na kumkosesha.

Kadhalika tunasoma katika 1 Wakorintho Sura ya 8 yote, lakini hasa katika mstari wa 11, 12 na 13,

“…Na yule aliye dhaifu aangamizwa kwa ujuzi wako naye ni ndugu ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake. Hivyo mkiwatenda dhambi ndugu zetu……mnamtenda dhambi Kristo.  Kwa hiyo, chakula ikimkwaza ndugu yangu, hakika sitakula chakula hata milele nisije nikamkwaza ndugu yangu”.

Baadhi ya washirika wa kanisa la Koritho walikuwa wakila vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu. Wao walidai kuwa sanamu si kitu na hakuna Mungu ila mmoja tu. Kwa hiyo walisema kuwa ni halali kwao kula vitu hivyo. Lakini wale washirika wengine walio na dhamira ‘dhaifu’ walipoona hao wanakula, nao walifanya hivyo pia, lakini pasipo na imani kwa Mungu, yaani walikula vitu hivyo kana kwamba ni vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, huku dhamira zao zikinajisika, yaani, kwa kufanya hivyo walimkosea Mungu. Lakini pamoja na hayo kumbe Paulo bado hawakemei washirika hawa wenye dhamira dhaifu. Hawaambii wale wenye dhamira dhaifu kuwa, “Mbona mnafuata matendo yao?” Hapana! Hasemi hivyo hata kidogo! Bali Paulo anawakemea “wenye ujuzi” tu! Anakubaliana na ujuzi wao kwamba sanamu si kitu na chakula ni chakula bila kujali kama kimetolewa kwa sanamu au la. Paulo anaendelea kufundisha kuwa kula vitu vilivyotolewa kwa sanamu sio jambo la haki wala upendo isipokuwa ni jambo la ubinafsi tu. Kwa hiyo wale wenye ujuzi walipokula vyakula hivyo waliwakwaza ndugu zao, yaani, waliweka kwazo mbele ya miguu ya ndugu zao. Kwa matendo yao, hao wenye ujuzi, yaliwaingiza ndugu zao wenye dhamira dhaifu katika hali ya kujaribiwa hata wakamkosea Mungu. Hivyo ndugu hao walio dhaifu walianguka – walianguka katika dhambi. Paulo atufundisha kuwa yule aliye dhaifu huangamizwa kwa ajili ya matendo yao wao waliojiruhusu kula! Matendo ambayo hayakuambatana na upendo, yaliwatumbukiza wengine wamkosee Mungu.

Tena tunaona mafundisho ya Neno la Mungu kwamba, kama nikiweka kwazo njiani mwa ndugu yangu (kwa matendo yangu yasiyo na upendo kwao) basi yeye huanguka dhambini na ni kweli amekosea, lakini mimi ndiye mhusika wa kosa lile; kwa sababu ni mimi niliyemsababisha ndugu yangu afanye dhambi kwa matendo yangu ya ubinafsi, yaani nilimfanya aingie katika majaribu makubwa kupita kiasi. Basi, Paulo hufundisha kama ifuatavyo; “Hivyo mkiwatenda dhambi ndugu zenu….mnamtenda dhambi Kristo.” Kwa hiyo mimi nilikuwa nimetenda dhambi ninapomkwaza ndugu yangu.  Hayo ni mafundisho ya Biblia.

Paulo hutaja ukweli huu pia katika Warumi 14:10-21 hasa mstari wa 13 ,”…toeni hukumu hii, mtu asitie kitu cha kumkwaza ndugu au cha  kumwangusha.”  Tena katika mstari wa 15, Biblia inasema, “Kwa chakula chako (au kwa kutafuta fedha nyingi za mahari) usimharibu mtu yule ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake.”  Anatuonya tusijipendeze wenyewe, bali tufuate kielelezo cha Kristo Yesu (Warumi 15:2-3).

Mambo hayo yaliyo hapo juu yanahusikanaje na utoaji wa mahari?  Basi ni kama ifuatavyo:

Lakini yanahusika kwake ni pale tu wazazi wa binti ni Wakristo na kwa sababu wao ndio wanaoweza kuamua gharama za mahari. Kama wazazi wa binti sio Wakristo hawawezi kutarajiwa kuyafuata mafundisho hayo. Hata hivyo, na tuombe Mungu aiguse mioyo ya watu wengi.

Iwapo mwanaume maskini ametakiwa kulipa gharama kubwa ya mahari (au tuseme gharama kupita kiasi cha uwezo wake) hilo humsukuma mtu aweze kujitahidi ili apate pesa. (Labda atalazimika kuhama kwa muda ili atafute kazi ili aweze kuongeza mapato yake. Hapo kinachofuatia, mtu huyo ni lazima aache kijiji chake, familia yake na kanisa lake, hapo hataweza tena kumwona mpenzi wake kwa muda fulani). Labda anaweza kufanya kazi huko kwa muda wa mwaka mmoja au zaidi bila kufanikiwa kupata fedha za kutosha kulipia mahari inayohitajika, yawezekana akaomba msaada kwa wengine wamsaidie. Hata hivyo kwa kuwa yeye ni maskini atashindwa kupata fedha zote zilizohitajika, hapo ndipo hufikia kukata tamaa. Aidha, anaweza kujisikia aibu sana na kufikiri ni jinsi gani anaweza kupata pesa za kutosha, na je, lini ataweza  kuzilipa? Je, ni lini ataweza kuoa?  Hiyo sasa ni hatari sana!  Kwa sababu kijana huyo anaweza kuanguka majaribuni hadi kumkosea Mungu.Yawezekana ataamua kukimbia eneo hilo na kuacha kanisa pamoja na Mungu pia. Hali kadhalika kwa msichana aliyeposwa atapatwa na shida na majaribu mengi.

Sasa na tusome 1 Wakorintho 7:1,2 na 9,  “…ni heri mwanamume asimguse mwanamke. Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe.”  Katika sura hii Paulo anatoa maoni yake tu kwamba ni heri watu wakae bila kuoa (mstari 8). Ndipo anasema hivi, “.. lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe, maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa.” Basi, twaweza kuona katika sura hii kuwa ni tabia ya watu kuoana; sio dhambi, na zaidi ya hayo tunajua Mungu aliwaagiza wanadamu waongezeke. Kutokana na mafundisho ya Paulo tunatambua ya kuwa kama mtu apenda
kuoa lakini ikiwa ipo sababu fulani isiyofaa inayomzuia mtu kuoa; basi kwa muda fulani ndipo hali hiyo ya kuzuiwa inamumbia au kumtengenezea kuwaka tamaa sana nafsini mwake hata kujaribiwa vikali kupita kiasi.

Kisha kinachofuatia hapo mtu anaweza kuanguka dhambini, yaani kufanya uzinzi; kama vile Paulo anavyotueleza hapo juu. Na tukumbuke ya kuwa Paulo anawaandikia wakristo! Vivyo hivyo ikiwa tutawazuia vijana wasioe kwa muda usiofaa eti kwa sababu tu tunatamani kupokea fedha zote za mahari, ndipo tunaweza kumkatisha  tamaa kumwaibisha tena kumtia katika majaribu makali ambamo anaweza kuanguka dhambini.  Ni kweli kijana ametenda dhambi akifanya hivyo, bali sawasawa na Neno la Mungu ni sisi (wazazi) wenyewe ndio tuliomkosea kijana huyo, kwa maana tumemkosesha, tumemtia katika majaribu makali kupita kiasi na yasiyo ya kawaida hata amekuwa mateka wa dhambi. Na kwa ajili ya mambo hayo sisi tutahukumiwa na Kristo Yesu. Tumemharibu ndugu yetu.

Ndugu wapendwa, ambao kwa ajili yenu Kristo alikufa, ebu tujiulize, je, tumewaumbia au kuwafanyia ndugu wengine nafasi yenye kujaribiwa kupita kiasi na hata kuanguka dhambini? Je, tumeweka kwazo njiani mwa ndugu zetu ili waanguke na kuangamizwa?  Na ni kwa nini?  Je, ni kwa ajili ya kutaka pesa tu? Hatutaki tukapunguza gharama za mahari, kwa hiyo hufuatia tunawatia vijana wetu majaribuni kinyume cha maneno ya Yesu aliyewafundisha wanafunzi wake waombe “….usitutie majaribuni ….” ( Mathayo 6:13). Je, tumeweka mzigo mzito mno ulio kama mlima mabegani mwa ndugu kwa kisingizio cha kutafuta bei kubwa sana ya mahari, ambayo wengine hawawezi kuubeba mzigo huo ila huanguka dhambini?

Unaweza kusema kuwa ameanguka dhambini yeye mwenyewe.  Ni kweli. Lakini Neno la Mungu linatuhusisha na ukweli huu, kuwa wewe ndiye uliyesababisha kuumbika kwa hali ya kujaribiwa kupita kiasi kwa nduguyo, kwa sababu gani?  Ni kwa sababu ya uchoyo wa moyo wako umemwangamiza nduguyo, kama vile Biblia inavyofundisha.

Lakini labda utasema kuwa, kama kijana akianguka dhambini baada ya muda fulani, inatuonyesha ya kwamba moyo wake haukuwa thabiti na mnyofu na kwa hiyo ni afadhali kugundua hivyo mapema kabla ya kuoana kuliko baadaye. Lakini kama ni hivyo, ndipo basi tungeweza kusema nini kuhusu yule mwanamke katika Mathayo 5:32 kwamba hana moyo mnyofu wa kumtafuta Bwana kwa kuwa tu, kumbe, alioelewa tena baada ya kuachwa na akafanya uzinzi? Lakini hapa Yesu anatufundisha kuwa ni mumewe ndiye aliyemfanya mkewe awe mzinzi kwa tendo lake la kumwacha mkewe. Kadhalika ungeweza pengine kumwambia hata yule aliye na dhamiri dhaifu katika 1 Wakorintho 8 kuwa “Haya, kama ulidhania ya kuwa ni dhambi kula chakula kitolewacho kwa sanamu, kwa nini basi unafanya hivyo?  Kwa nini unaiga watu wengine ambao wanaweza kula kwa dhamira safi, ni bora kumcha Mungu na kutokula kuliko kufuata wengine na ukala huku ukiwa na dhamiri isiyo safi?”  Kuna maana!  Lakini tena mtume Paulo hafundishi hivyo, wala wale wanaokula huku wakiwa na dhamira dhaifu hawakemewi hata kidogo! Ndivyo, walifanya dhambi. Lakini Paulo anawakemea wale tu waliokula kwa ujuzi, yaani wakiwa na dhamira safi. Anawaambia kuwa wanawaangamiza ndugu zao kwa sababu wanawasababisha wengine watende dhambi kutokana na matendo yao ya ubinafsi, kwa maana hiyo, wao ndio waliofanya dhambi. Mtume Paulo anatupia jukumu la dhambi hii juu yao walio na ujuzi wa mambo yote. Hali kadhalika kama nikikataa kupunguza gharama za mahari kwa muda mrefu na yule kijana akijikwaa, yaani akianguka dhambini, mimi ndiye niliyemkosea na ni mimi niliyefanya dhambi. Ndiyo, yeye atapata hasara kubwa sana, lakini mimi nitahukumiwa na Kristo kwa ajili ya dhambi yangu ya kumharibu ndugu yangu. Haya ndiyo mafundisho ya Biblia.

Iwapo utasema ni desturi yetu kupokea mahari, basi jibu langu la kwanza ni kwamba, hapa mimi sitafuti kuondoa desturi hii, bali kuondoa nafasi kumkwaza kijana kwa kutaka bei kubwa ya mahari kuliko uwezo wake. Ya pili, ikiwa namna ya desturi yetu ni kinyume na Roho wa Kristo, basi na tukumbuke pia kwamba tumekombolewa kwa damu ya thamani tupate kutoka katika mwendo wetu usiofaa tuliourithi toka kwa mababa zetu (1 Petro 1:18,19).

Aidha, ukumbuke ya kuwa Mungu anawahurumia maskini, naye hutuonya na kututaka kufanya vivyo hivyo. Tunaweza kusoma katika Biblia jinsi Wayahudi walivyowasonga na kuwadhulumu maskini, wakati wao maskini walikuwa ni ndugu zao!  Walitumia shida ya maskini hao kwa ajili ya faida yao wenyewe, hasa wakati wa njaa. Tunaweza kusoma hayo katika kitabu cha Nehemia 5:1-13. Na Nehemia alikasirika sana.  Katika maneno yake aliwaambia Wayahudi hao “…Je, haiwapasi ninyi kwenda katika kicho cha Mungu wetu, kwa sababu ya mashutumu ya makafiri adui zetu? (mstari wa 9). Basi, aliwakemea kwa sababu waliwasonga na kuwaaibisha ndugu zao mbele ya wasioamini.  Jina la Bwana linalaumiwa kwa ajili ya matendo yao ya ubinafsi na kutokuwahurumia ndugu zao maskini. Sisi pia leo, tunaweza kufanya vivyo hivyo kwa ndugu zetu iwapo hatuwezi kujilinda na uchoyo. Yapo maandiko mengine mengi yanayotufundisha yanavyofanana na hayo hapa juu, kama: Kumbukumbu ya Torati 15:7-11 na Mithali 14:31 na 22:16.

Yawezekana wewe pia ni maskini sana, labda wewe ni baba na unaye mtoto wa kike. Sasa, kwa mara ya kwanza katika maisha yako utapata nafasi ya kupokea fedha nyingi sana kama baraka ili kukufariji na kukutuliza, labda umekuwa ukingojea baraka ya jinsi hii kwa muda mrefu na kwa hamu kubwa sana. Na sasa labda utafikiria kuwa mafundisho haya yanaweza kubatilisha sana baraka yako. Lakini huwezi kupoteza cho chote iwapo utafuata mapenzi ya Mungu na pendo la Mungu. Mkumbuke Ibrahimu, jinsi alivyongoja kwa maisha yake yote ili apate mtoto wa kiume, na akampata. Kisha hapo hapo Mungu alimwambia amtoe mwanae. Ibrahimu hakusita. Katika hali ya kumwabudu Mungu alikuwa tayari kumtoa mwanawe, ingawa mtoto huyu alikuwa yote kwake Ibrahimu. Pia ingawa ahadi zote za Mungu pamoja na baraka zote za Mungu kwake Ibrahimu zilikuwamo kupitia Isaka, bado angemtoa – kama Isaka angekufa, ndipo baraka zote ambazo Mungu alikuwa amemwahidi Ibrahimu, pamoja na ndoto zote za Ibrahimu nazo zingekufa pia. Ndiyo, kabisa! Lakini Ibrahimu alimwamini Mungu, naye alikuwa tayari kumtii na kumtolea yote, ndiyo, yote aliyo nayo. Lakini sasa Mungu hatafuti utoe mtoto wako afe, bali kuacha pesa ya uchoyo tu!

Sasa ndugu, mpendwa wa Mungu, iwapo ukimtii Mungu, yeye atakubariki rohoni na mwilini, sasa na hata milele. Usimwaibishe ndugu yako wala usimwangamize, kama ikiwa ni wakati wa kumhurumia ndugu yako basi punguza bei ya mahari kwa hiari ya moyo wako.

——————————————————–

KUHUSU KUHESHIMANA

Kwa wakati wote na katika mambo yote yawapasa vijana kuwaheshimu wazazi wao, hivyo ndivyo Biblia inavyotufundisha. Ni kosa kabisa kutumia ukweli huo hapo juu kutokuwaheshimu wazazi au kuwatisha au kuwahukumu kwa njia yo yote ile. Mungu pekee ndiye Hakimu. Ni vema kuomba na kusihi kwa upole na uvumilivu na ili kuleta heshima wakati wote. Kwa upande mwingine Neno la Mungu linasema “Ninyi akina baba msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.” (Wakolosai 3:21).

NA TUSIHUKUMIANE, NDUGU!

Paulo anasema, “Basi tusizidi kuhukumiana, bali afadhali toeni hukumu hii, mtu asitie kitu cha kumkwaza ndugu au cha kumwangusha.” (Warumi 14 : 13). Ndugu, mchukuliane katika upendo. Msihukumiane wala msiwadharau wengine. Mngojee Bwana atakayemlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. Bwana anajua yote naye atakuongoza na kukusaidia kama ukitembea mbele zake kwa unyenyekevu na upendo.  Atakupa neema ya kutosha. Hivyo na tupendane kulitukuze jina la Bwana kati yao wasioamini. Amina.

KUHUSU HEKIMA

Ikiwa kijana fulani akijidai kuwa ameokoka na akajiunga na kanisa, kisha baada ya muda mfupi asema anapenda kuoana na kijana kanisani, jihadharini! Labda alisikia kuwa Wakristo wanahurumiana juu ya ulipaji wa mahari, wakati kumbe yeye moyo wake sio mnyofu. Kama jinsi ilivyo kwa mashemasi wa kanisa, ndivyo hivyo iwe kwake kijana huyu, anapotaka kuoa; yaani “Hawa…na wajaribiwe kwanza, baadaye….” (1 Timotheo 3:10), yaani, inampasa kuonekana mnyofu kwanza kabla hajakubaliwa kuoa.

Tena kama mwanamume mkristo alipata idhini ya kuoa, kisha ameanza kuwa mvivu kwa sababu anafikiri pengine baada ya muda wazazi wanaweza kupunguza bei ya mahari, hapo ndipo atakuwa amejionyesha kuwa hafai na wala hastahili kuoa. Katika hali yo yote ile inampasa kijana ajionyeshe kuwa ni mnyofu, mwaminifu na ni mwenye bidii.

KWA UJUMLA

Kama ikiwezekana inawapasa wakristo kumtumia mkristo mwenzao kama mjumbe kati ya familia kwa ajili ya mawasiliano na matengenezo juu ya ulipaji wa mahari. Jambo hili lisiachwe mikononi mwa ulimwengu kwa kuwa ni jambo linalohusu waumini tu.

Siwezi kutaja mambo yote hapa, kwa mfano, gharama za mahari inapaswa kutegemea na uwezo wa kijana mwenyewe pia, na hali ya maisha pale mlipo bila kumlazimisha kufanya kazi kwa muda unaopita kiasi. Ni muda gani? Mungu akupe huruma na hekima!

Neema ya Bwana iwe kwenu!

© David Stamen 2015

KUPAKUA SOMO HILI BONYEZA LINK HII: KUHUSU ULIPAJI WA MAHARI

RUDI KWA HOMEPAGE

 

4 responses to “Kuhusu Ulipaji wa Mahari

 1. henry mazengo

  May 8, 2015 at 11:09 am

  asante kwa neno

   
  • Elizabeth M.John

   December 10, 2015 at 6:29 am

   Ni kweli maana wengi leo wamefikia pabaya lkn kama wakristo basi tuwe nuru kwa jamii ili ujumbe huu uwafikie wenzetu wa mataifa,ombi langu hebu sasa tubadilike kupitia mafundisho haya

    
 2. tumsifu mmari

  June 12, 2015 at 9:56 pm

  Mafundisho kwanza yamenibariki sana ifike mahali jamii ibadilike kwan ndoa sio kukomoana ni jambo la kimungu tena wazo langu yangeondolewa kabisa

   
 3. John wakuchalo.

  March 6, 2017 at 7:45 am

  Swala la mahali.Kwa mtazamo wangu si swala la kibiblia.Ni kati ya maswala ya kijamii,linategemea hasa mila za jamii husika.Kuna ambapo mume hutoa mahali.Mahala pengine mke na mume wazazi wao huchangiana mahali,nk.Mahali ni nini?Nijuavyo mimi mahali ni kitu chochote kitolewacho na muoaji kwa muolewaji kama ishara ya dhamira njema ya kujenga na kuanzisha familia.Kitu hicho lazima kitoe majibu ya maswali kadhaa ya familia ya anae olewa.1,Ananipenda kiasi gani?2,amejiandaa kuilea familia anayo taka kuiunda kiasi gani?nk.kadiri muoaji anavyo timiza mashariti ya mahali ndivyo familia ya muolewaji wanavyo anza kujua majibu ya maswali hayo hapo juu.Nia ya mahali si kumzuia kuoa la bali kumfahamu Dhamira yake na maandalizi yake,ktk kuamua kuwa na familia.Anaweza kuwa amekurupuka bila kujitafakari mabo kadhaa mfano je,naweza kulea familia?je,huyu ni mke ninaye mudu kumlea?nk.Mahali ndiyo itaonyesha hayo yote. ukishindwa mahali ni ishara kuwa si sahihi familia hizo kuungana.Kwani mahali si bei ni ishara ya kufahamiana.

   

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

 
%d bloggers like this: