RSS

JE, IPO NGUVU KWENYE MANENO YAKO?

Niliwahi kumpatia pesa rafiki yangu mmoja ili anunue mbegu akapande kwenye shamba lake iweze kumsaidia kutoka katika hali ya shida sana aliyokuwa akipitia. Nilimpa sharti moja tu kutokana na zawadi hiyo niliyomsaidia. Nilimwomba angalau awe ananitumia taarifa fupi tu – hata kama ni sentensi moja tu – iwe mara kwa mara ili kuniwezesha mimi kufahamu jinsi gani mambo yanavyoendelea ili kwamba nipate kuomba Mungu pia. Yule rafiki alinijibu,” Ndiyo, kwa vyovyote vile nitafanya hivyo.” Lakini baada ya wiki nyingi tu kupita hakuwasiliana nami hata mara moja. Alikosa kabisa kuwasiliana nami juu ya jambo hili. Ilionyesha kana kwamba maneno tuliyokubaliana hayakubeba maana /umuhimu wowote ndani yake.

Watu husema maneno au kuahidi mambo pasipo hata kutambua wala kujisikia wanalo jukumu ya kile walichokisema au kuongea, na pasipo kuelewa kuwa sisi tu watu wa Mungu hivyo yatupasa tuwe waaminifu. Tunapaswa kuwa waaminifu kwa yale tunayoyasema kwa watu.

Neno la Mungu linasemaje? Tunasoma,

“Mwenye haki huchukia kusema uongo; Bali mtu mbaya…hupatwa na aibu…Shahidi mwaminifu hatasema uongo; Bali shahidi wa uongo, pumzi zake ni uongo.” (Mithali 13:5; 14:5).

Hebu achilia jambo hili lizame ndani ya mioyo yetu! Tunapaswa tutafakari sana ukweli huo. Watu wengi husema na kuahidi mambo, lakini maneno yao yanakosa nguvu ndani yake. Wanasema au kuahidi kitu lakini wanakosa kusudi la dhati na uaminifu kutimiza walichokisema na kuahidi. Kwa hiyo, wanachosema hayana maana yoyote kwao.

Je, na wewe maneno uyasemayo yana nguvu? Maneno yako yana maana / thamani yoyote?

Siamini kuwa huyu rafiki yangu kwa makusudi alinidanganya. Ninafikiri hili ni jambo lililozama sana kwa kina na lenye nguvu kuliko hilo. Baadaye nilifanikiwa kuongea na huyo rafiki yangu kuhusiana na upungufu wa uaminifu, na mwisho wa mazungumzo yetu alikubali kuwa watu WAMEZOEA kusema mambo PASIPO HATA KUJISIKIA JUKUMU LOLOTE LA KUTIMILIZA KILE WALICHOKIAHIDI. (Hapa siongelei kuhusu mambo madogo madogo ambayo mtu yeyote anaweza kuyasahau – lakini tunapofanikiwa kukumbuka, basi hata hayo mambo madogo madogo tunapaswa kuwasiliana na mtu yule mara moja na kumwomba radhi na kisha kuyaweka mambo vizuri). Hapa naongelea kuhusu mambo muhimu ambayo watu huyaahidi au huyasema ya kuwa watayafanya dhahiri kwa ajili yako na hata baada ya kusema hayo bado hawawasiliani nawe, wananyamza kimya kwa muda mrefu – hadi mwishoni wewe ndiwe unayemtafuta. Hata hivyo haionyeshi kuwa watu hawa wanapata woga wowote wala wanajisikia aibu kwamba maneno waliyoyasema hawakuyajali au hawakuyatunza. Badala yake kwa urahisi na haraka wanabaki na kisingizio kwamba wamekuwa wakihangaika kwa shughuli nyingi! Na hata hivyo baada ya hao, wengi wao hawatimilizi kile walichokiahidi mwanzoni.

Tunasoma, “Walakini mwisho wa agizo hilo ni upendo utokao katika moyo safi na DHAMIRA NJEMA, na imani isiyo na unafiki. Wengine wakiyakosa hayo wamegeukia maneno ya ubatili.” (1 Tim. 1:5,6).

Katika maisha ya Mkristo kuwa na DHAMIRA NJEMA ni jambo la muhimu na maana sana. Lakini kwa wengi inaonekana dhamira yao haiwasumbui hata kidogo! Dhamira yao imelala! Au wamezoea kuishi na dhamira mbaya. Paulo alimwagiza Timotheo awe dhamiri njema, “Mwanangu Timotheo, nakukabidhi agizo hilo liwe akiba…ili katika hayo uvipige vile vita vizuri; uwe mwenye imani na DHAMIRI NJEMA, ambayo wengine wameisukumia mbali, wakaangamia kwa habari ya Imani.” (1 Tim. 1:18,19). Na Tena tunasoma, “Tuombeeni; maana tunaamini kwamba tuna DHAMIRI NJEMA, tukitaka kuwa na mwenendo mwema katika mambo yote.” (Waebr. 13:8). Hatuwezi kuwa na ushuhuda mzuri mbele ya watu pasipo kuwa na dhamiri njema! Mtume Paulo alifurahia sana juu ya jambo gani? Tumsikilize:

“Kwa maana kujisifu kwetu ni huku, USHUHUDA WA DHAMIRI YETU, ya kwamba kwa utakatifu na weupe wa moyo utokao kwa Mungu.” (2 Wakor. 1:12).

Je, umewahi kutafakari juu ya USHUHUDA wa dhamira yako? Ushuhuda wa dhamira yako ni nini juu ya mambo yale ambayo unawaahidi na kuwaambia watu wengine? Je, neno la Mungu na Roho ya Mungua wanaweza kuigusa dhamira yako?

Nilialikwa kwenye semina ya wanachuo kwa siku tatu. Siku ya kwanza nilifika kwenye chuo pamoja na mtafsiri wangu nusu saa kabla ya mwanzo wa semina. Baada ya dakika chache tulipata text message kutoka kiongozi wa wanafunzi ili kutujulisha kwamba wamefuta semina ya siku ile kwa maelezo wanafunzi wanafunga siku ile! Hakuna mtu ambaye alikutana nasi pale wala kutupigia simu – tulipata text message tu. Hata hivyo tuliendelea na semina kwa siku mbili nasi tulibarikiwa. Nilipoongea na kiongozi yule kumwuliza kwa nini hakutuambia taarifa hayo mapema, alijibu alikuwa anayo shughuli nyingi siku ile! Nilishangaa kwa sababu kutumia text au kupiga simu juu ya jambo muhimu kama hili inachukua dakika moja tu. Lakini kile kilichonishangaza zaidi ni kwamba jambo hili halimsumbua cho chote wala hakujisikia aibu yo yote. Ilionekana kwamba kwake kitendo hiki ni cha kawaida kabisa na jambo la kubalika.

Wanafundisha nini kwenye makanisa mengine kama vijana wanaweza kufikiri kuwa kitendo hiki ni cha kawadia tu na tabia hiyo inakubalika.

Katika somo hili silalamiki jinsi watu walivyonitendea mimi. Hapana, silalamikii hilo kabisa. Na hili sio kusudio la somo hili, na wala sio nia ya moyo wangu. Mzigo wangu ni kuona kuwa tunakuwa ni mashahidi wazuri sisi kwa sisi na mbele ya wasioamini ili kwamba jina la Bwana na kazi ya Mungu isiteseke na isilaumiwe kutokana na kukosa uaminifu kwetu.

Watu wengi wamezoelea kuwa wavivu katika mambo kama haya. Hawapendi kujisumbua na kutunza kile walichoahidi. Inaonekana kipaumbele chao ni kuendelea na mambo wanavyopenda wenyewe bila kujali mtu yule mwingine anayemsubiri kutimiza neno lake! Kwao huo ndio mfumo wa maisha yao na ndiyo mifumo ya kufikiri kwao.

Nimepata kukutana na mambo haya mara nyingi kuhusu mambo ya muhimu, sio tu kutoka washirika lakini na kwa wachungaji pia.

Vipi wanavyoweza kuhubiri juu ya Mungu wa Agano wakati wanapovunja ahadi zao kwao wengine? Jambo hili sili jambo ndogo. Ni jambo la maana na muhimu sana! Unawezaje basi kuhubiri Injili iwapo wewe mwenyewe kirahisi tu huyatunzi yale unayoyasema.

“Mungu si mtu, aseme uongo; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?” (Hesabu 23:19).

Vipi kuhusu wewe? Mtume Paulo anasema, “nilipokusudia hayo, je! Nalitumia kigeugeu? Au hayo niyakusudiayo, nayakusudia kwa jinsi ya mwili kwamba iwe hivi kwangu, kusema Ndiyo, ndiyo, na Siyo, siyo?” (2 Wakor. 1:17). Vipi sasa kuhusu wewe. Je, unatumia kigeugeu kwa yale mambo unayosema?

Sasa je, inakuwaje mumini analipuuza neno la Mungu kiurahisi namna hii? Inakuwaje basi kwamba dhamira zao HAZIWASUMBUI au kuwakumbusha? Je, hii mifumo yetu ya maisha ina nguvu kuliko nguvu ya neno la Mungu ambalo ndilo linapaswa kutubadilisha ili kwamba tusifuate vijitabia vya mila zetu au mifumo ya maisha yetu ya kale/ zamani? Mtindo huu wa kutokuwa mwaminifu unakuwa ni tatizo baya sana kwa kazi ya Mungu.

Rafiki mwingine alinialika kwa ajili ya kupata chakula cha jioni nyumbani kwake – aliniambia iwe jumanne jioni. Ilipofika siku ya jumatatu kabla ya hiyo nilikuwa namtembelea mchungaji wake na kupata chakula cha mchana pamoja naye. Mchungaji huyu alikuwa haishi mbali saana kutoka nyumba ya yule mshirika. Hivyo, aliposikia kuwa nimemtembelea yule mchungaji wake, MARA MOJA yeye naye alifikiri kuwa nitamtembelea siku hiyo hiyo jumatatu badala ya jumanne kama tulivyokubaliana. Hivyo alimjulisha mkewe kununua vyakula haraka haraka na kupika chakula cha wageni jioni ile. Wakati huo huo nilikuwa tayari nimemaliza kula chakula nyumbani kwa Mchungaji, ilikuwa kama muda wa saa tisa jioni hivi.

Kunako kama saa kumi yule mshirika akaja pale nyumbani kwa mchungaji wake, huku akiendesha pikipiki yake. Akitaka kuja kunichukua ili anipeleke nyumbani kwake kwa ajili ya kupata chakula. Nilimwambia kuwa nilikuwa nakuja nyumbani kwake siku inayofuatia, yaani, jumanne sawasawa na makubaliano yetu, na hata hivyo tayari wakati huo nilikuwa nimeshiba chakula ambacho nilikuwa nimekula hapo kwa Mchungaji wake muda mfupi tu uliopita. Naye akanijibu, “Sawa, basi kwa kuwa tumeshakutana na kuonana leo hakuna haja tena ya wewe kesho kuja nyumbani tena”. Kisha akaondoka baada ya kuongea nae kwa muda wa dakika kumi tu.

Hii ilinishtuka sana, sikuelewa kwa nini aliamua kufuta ratiba ya mwaliko kwenda kumtembelea kesho yake kama tulivyokubaliana mwanzoni. Jambo hili lilinifanya nifikiri kuwa bila shaka nimemkosea sana! Baadaye (siku ile ile) nilimwuliza imekuwaje mambo hayo yote kuwa hivyo. Ndipo alinisimulia akasema aliposikia kuwa nipo nyumbani kwa mchungaji wake siku ile ya jumatatu mara moja yeye alifikiri kwamba NIMEBADILISHA mipango yetu ya mimi kumtembelea nyumbani kwake ile siku ya jumanne. Hivyo akafanya haraka kumwambia mkewe kununua chakula na kuandaa mlo, wakati huo nilikuwa hajajua chochote juu ya mabadiliko hayo ya ghafla aliyoyafanya. Hivyo nilipomwambia kuwa mimi nitaendelea kujali mpango wetu wa kumtembelea siku ya jumanne naye akajisikia kuwa hivyo sasa itakuwa ni mzigo mzito sana kwa upande wa mkewe na pia kwa gharama za matumizi ya pesa kwamba amwombe tena mkewe kupika kesho yake kwa ajili ya wageni lakini alikuwa anasumbuka kunijulisha hivyo. Badala yake akatumia dakika 10 tu pale njiani kuniambia kuwa ilikuwa hakuna haja tena ya mimi kumtembelea nyumbani kwake jumanne maadamu tumeonana pale eti ilikuwa inatosha tu. (Lakini hadithi hii ilikuwa na mwisho mzuri).

Aliponiambia hivyo nikamwambia, “Tazama, ninapobadilisha mipango yangu NINGEKUAMBIA kabla MAPEMA. Nisingewasili tu siku mapema pasipo kwanza kukujulisha.” Ndipo akaniambia ifuatavyo, “Lakini watu huwa wanafanya hivyo mara nyingi, na ni jambo la kawaida. Mtu anasema jambo fulani na tena anabadilisha tu ovyoovyo pasipo sababu yoyote ya msingi au pasipo kuomba radhi.” 

Inaonyesha kana kwamba maneno hayabebi maana yoyote kati ya watu wengi.

Je, maneno yako unayoyasema yana nguvu yoyote ndani yake? Maneno yako yanabeba maana yoyote? Je, unalo kusudio na nguvu ya kutimiliza mambo unayoyasema kwa watu – sio tu yanapokuwa mepesi kwako bali kila wakati? Kwa uzoefu nilionao katika mashauri mbalimbali, watu hawajayajali maneno yao wayasemayo kwa sababu lile ambalo waliahidi halikuoanisha na mipango yao ya binafsi wenyewe – hawakutaka kujisumbua wenyewe!

Wanapendelea kuwa mvivu badala ya kuwa mwaminifu.

Sisemi wanafanya hivyo kwa makusudi kila mara, ila wamezoealea kufanya hivyo. Tabia hii ya kutokutunza maneno yasemwayo yanamadhara mengineyo. Nilikuwa naendesha semina sehemu fulani nchini. Nilinunua kifaa cha kamera kwa ajili ya kumpatia ndugu ambaye alikuwa akiishi eneo la mbali kutokea pale nilipokuwa nikihubiri. Nilimtaarifu kuwa ningemtumia kifaa kile kwa bus, ili kwamba asisumbuke kuja pale nilipokuwepo na nilimwambia mara mbili kwamba sitalipia nauli ya kurudi kwake kutokea pale nilipo. Lakini baadae nikamwona akaja kwenye semina ile hivyo nikafikiri kuwa huenda amemudu kujilipia nauli yake mwenyewe. Basi nilifurahi kumwona na tulikuwa na muda mzuri na ushirika kwa pamoja. Basi, alikuwa anaondoka kurudi kwao, tukaagana, lakini alipoona simpatii nauli ili kusafiri kurudi nyumbani kwake, mara moja akakasirika sana. Akageuka na kuondoka kwa taabu ya kuchukizwa. Akaenda kumlalamikia ndugu mwingine kuwa eti sijampatia nauli ya kumrudisha nyumbani kwake. Na huyo alikuwa mchungaji!

Sasa, inakuwaje kwamba ndugu huyu atarajie nimlipie nauli ya kurudi kwao wakati tayari nilikwisha kumtahadharisha mara mbili kabla hajafunga safari yake kwamba sitalipia nauli yake ya kurudi?

Sio tu kwamba watu wengi hawajali maneno yao wayasemayo, bali kwa sababu ya tabia hii kadhalika mara nyingi hawaamini kile akisemacho mwingine! Tunatambua kuwa jambo hilo ni la maana sana na lenye uzito kutokana na maneno ya Paulo yafuatayo:

“Wakrete ni waongo siku zote… walafi wavivu. Ushuhuda huo ni kweli. Kwa sababu hiyo uwakemee kwa ukali, ili wapate kuwa wazima katika Imani.”  (Tito 1:12,13).

Hapa tunaona kuwa kile kilicho nguvu kwenye mila na desturi za watu inaweza ikapata nguvu kwenye maisha ya watu baada ya kumgeukia Yesu ikiwa hawataruhusu neno la Mungu liwabadilishe. Wakrete walikuwa ni watu walio na mazoea ya uongo na pia wavivu, na baadhi ya waamini wa huko waliendelea kuishi kwenye tabia hii. Ushauri wa Paulo kwa Tito kuhusu jambo hili ulikuwa ni wenye nguvu sana!

Paulo anasema hivi kwa waumini wa huko Efeso juu ya namna zao za kuishi maisha ya kale, “mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli. Basi UVUENI UONGO, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake.”  (Waefeso 4:24-25).

Unaona? Tunapaswa kuyavua mambo yetu yote ya ukale, ya maisha yetu yaliyopita kama kwenye dhambi, na sasa badala yake tumvae Kristo. Kwa mfano, kama mtu alikuwa ni mvivu katika kuzitunza ahadi zako pale zamani kabla hujawa Mkristo, basi Paulo anasema, “badilika”, kwa sababu Kristo alikufa ili kwamba usiishi namna ile tena! Je, wewe unawahubiria watu neno la Mungu lakini wewe mwenyewe hutunzi ahadi zako kwa watu na wala hutimizi ahadi zako ulizoahidi kuzifanya?

Katika muktadha mwingine, mtume Yakobo alikuwa akifundisha juu ya madhara yanayotoka kwenye vinywa vyetu. Na anasema hivi, “ndugu zangu haifai mambo hayo kuwa hivi…”. ( Yak. 3:10).

Tunapasa kumheshimu Bwana kwa yale tunayosema; tunatakiwa tuwe na ahadi nzuri kwa watu wale tunaowaahidi mambo; tunapaswa kuwa na ushuhuda mzuri na baraka kwa watu wengine – sio kuleta kukatishwa tamaa ambayo humletea mtu mwingine matatizo tu.

“Wanadamu hutangaza kila mtu hisani yake mwenyewe; Bali mtu aliye mwaminifu, ni nani awezaye kumpata?” (Mithali 20:6).

Jamani, ebu na tuishi kulingana na neno la Mungu. Basi neno lake Mungu libadilishe jinsi ya kiongea kwetu na namna tunavyotenda. Ni matumaini yangu kuwa maneno haya yanaweza kukusaidia na kukubariki iwapo unahitaji kubadilisha mambo katika eneo hili la maisha yako.

Kama nilivyosema, katika somo hili silalamiki jinsi watu walivyonitendea mimi. Lakini nilitoa hadithi hizo ili msomaji aelewe vizuri muktadha na maana ya mistari uliyoinukuu hapo juu.

©   DAVID STAMEN  2018   somabiblia.com

 

Comments are closed.

 
%d bloggers like this: