RSS

MTAIFAHAMU KWELI, NAYO HIYO KWELI ITAWAWEKA HURU

Yesu alimaanisha nini aliposema hivi? Alikuwa akimaanisha uhuru wa namna gani?

Wacha tuone kwanza alikuwa akisema maneno haya kwa nani. Katika mstari wa 31 inatuambia alikuwa akiongea na wale Wayahudi waliomwamini. Ni muhimu kutambua hili. Anazungumza na wale ambao walikuwa wameamini maneno yake. Lakini wakati Yesu alipowaambia kwamba kweli itawafanya kuwa huru, walichukia na kumkasirikia, “Wakamjibu, Sisi tu uzao wake Ibrahimu, wala hatujawa watumwa wa mtu wakati wo wote; nawe wasemaje, Mtawekwa huru?” (mstari 33). Na hapa ndipo tunahitaji kutambua kitu muhimu na la maana sana). Watu hawa walikuwa wa DINI. ‘Walimwamini’ Yesu (mstari 31) na waliamini kuwa walikuwa watu wa Mungu kwa sababu walitoka kwa Abrahamu. Lakini ni tabia yao ya KIDINI iliyowafanya wapinge mafundisho ya Yesu. Walifikiri kwamba, “Hatuko kwenye kifungo. Sisi ni watu wa Mungu. Ibrahimu ni baba yetu.” Kwa sababu tayari walimwamini Mungu, hawakukubali ujumbe kwamba kuna kitu kinachohitajika kubadilika katika maisha yao. Walikubali kile Yesu alichokuwa akisema hadi alipowaambia kwamba mabadiliko makubwa yanahitajika kufanyika katika maisha yao. Na Yesu aliweka wazi kabisa ni nini kinachohitaji kubadilika katika mioyo yao. Alikuwa amekuja kuwaweka huru kutoka dhambini, “Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. Wala mtumwa hakai nyumbani sikuzote; mwana hukaa sikuzote. Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.” (Mistari 34-36).

Yesu alikuwa akiwaambia kuwa bado hawakuwa huru toka dhambini na kwamba bado walikuwa watumwa wa dhambi. Alikuwa amewaambia kwamba ikiwa wataendelea katika neno lake basi watakuwa wanafunzi wake wa kweli na wataijua kweli ambayo itawaweka huru (mstari 31). Yesu alikuwa akiwaambia wao – na sisi – kwamba KAZI YAKE NDANI YETU ni kutufanya tuwe huru kutoka dhambini, ili tusitumikie dhambi tena (Warumi 6:6).

Lakini kwa sababu hao Wayahudi waliamini kuwa tayari walikuwa ‘waumini’ na watu wa Mungu, walikataa mafundisho ya Yesu. Walimkataa Yesu. WALIKATAA KAZI YAKE maishani mwao. Walichukizwa kwamba mtu yeyote angeweza kupinga imani yao. Walichukia wakati Yesu alipofunua hali halisi na msukumo wa mioyo yao! Wayahudi walimpinga Yesu, wakisema kwamba Mungu ndiye baba yao (mstari 41). Lakini Yesu anawaambia kwamba wao ni wa baba yao shetani, na kwamba mawazo yao na nia yao ni ovu!

Na hivyo ndivyo ilivyo leo. Watu wanaweza kuwa waumini sana. Kwa sababu ‘wanaamini’ mambo fulani na hufanya mambo fulani, wanafikiri ni sawa. Watu wanaweza kusema kwamba wao ni Wakristo, kwamba ‘wanamwamini Yesu’, kwamba wanaenda kanisani, kwamba wamesamehewa, kwamba wamehesabiwa haki, nk. Hii inaweza kusababisha watu kupinga ukweli wa Yesu na nguvu ya Injili katika maisha yao. Kama Wayahudi katika Yohana sura ya 8, hawataki dhambi kupingwa au kufichuliwa katika maisha yao; wanapinga mabadiliko katika maisha yao yaliyoletwa na kufa kwa Yesu. Watu wanaweza kusema na kudai wanachotaka, lakini kazi ya Mwana wa Mungu maishani mwetu ni kutuweka huru tusitumikie dhambi tena. Huu ndio ukweli wa Injili. Hii ni nguvu ya msalaba na ya Injili.

Mtaijua kweli na itawaweka huru kutoka kwenye utumwa wa dhambi! Ikiwa Mwana atawaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli! Na huu ni uhuru ulioje!

Yesu alisema, “Wala mtumwa hakai nyumbani sikuzote; mwana hukaa sikuzote.” (Mstari 35).

Ni nani atakayekaa nyumbani (mwa Mungu) sikuzote (milele)? Ni yeye aliyeacha kutumikia dhambi maishani mwake – kupitia wokovu mkuu uliomo ndani ya Yesu Kristo; ni yeye aliyewekwa huru kutokana na kutenda dhambi. Huu ndio wokovu mkuu ambao Yesu alikufa ili atulete mimi na wewe.

“Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.”

Je, unajua uhuru huu katika Kristo Yesu?

Au, je, ni kawaida kwako kusema uwongo? Je, unasema uwongo bila dhamiri yako kukusumbua? Je, watu wanaweza kuamini kile unachosema? Au unaahidi vitu na kisha unasahau tu?

Je! Wewe hutazama ponografia (picha au video za ngono) kwa siri kwenye simu yako au kwenye tovuti? Je! Uko katika kifungo cha dhambi hii mbaya? Je! Unatumikia dhambi kwa kutazama picha zisizo safi. Yesu alisema kwamba ukimtazama mwanamke kwa kumtamani, basi tayari umekwisha kuzini moyoni mwako. Kwa kutazama picha chafu kwenye simu yako au kompyuta, unafikiri unafanya nini? Je! Mwana amekuweka huru? Je! Umeliitia jina la Yesu ili afanye kazi hii ya wokovu ndani yako?

Je. Unasema uongo na kudanganya ili upate pesa?

Je! Una husuda, wivu, uchungu moyoni mwako? Una kutosamehe moyoni mwako? Moyo wako ni mgumu na wa baridi kwa mtu yeyote?

Je! Unasingizia watu? Je! Unapambana kuwa wa ‘kwanza’ na kukosoa wengine ili uinuliwe? Je! Unajaribu kutaka utambuliwe na wengine badala ya kuwatumikia wengine.

Yesu alisema, “Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu YATOKA NDANI, nayo YAMTIA MTU UNAJISI.” Yesu alikuja sio tu kutusamehe dhambi zetu, bali kutusafisha kabisa na kutuokoa na dhambi zetu. Akizungumza juu ya kuja kwa Yesu, Yohana Mbatizaji alisema, “Na sasa hivi shoka limekwisha kuwekwa PENYE SHINA LA MITI” (Luka 3:9). (Kwa lugha ya asili ya Agano Jipya imeandikwa “shina” na siyo “mashina”).

Je, shoka hii limekwisha kuwekwa penye shina la moyo wako?

Na hii ndio iliyofanyika kwenye msalaba wa Kalvari. Sio tu kwamba tunasamehewa na kusafishwa kabisa kwa damu ya Yesu, bali kwa kifo chake na ufufuo, Yesu ameweka shoka kwenye shina la uovu katika maisha yetu; ameharibu nguvu ya dhambi na ya Shetani ili tusitumikie dhambi tena, bali kuishi maisha matakatifu na kutumikia haki.(Warumi 6:1,2,6,18; Waebr. 2:14; 1 Yohana 3:5-9; Luka1:74,75).

 Je! Unaamini hii? Je! Unajua nguvu ya Injili hii maishani mwako – kukuweka huru na dhambi? Je! Hii ndiyo Injili inayohubiriwa kanisani kwako?

Yesu Kristo alikufa kwa ajili hii. Mwana akikuweka huru, utakuwa huru kweli kweli.

 

Comments are closed.