RSS

JE, UNAIFUATA DINI YA USHIRIKINA AU UNAMFUATA YESU?

Kama ukiishi hali ya kufikiri kwamba baraka za ‘nje’, za kimwili ni alama Mungu anapendezwa nawe, unakosa sana. Huo ndio ushirikina. Unatembea gizani.

“…uzima wa mtu HAUMO KATIKA WINGI WA VITU VYAKE ALIVYO NAVYO.” (Luka 12:15).

“Basi msihukumu hukumu YA MACHO TU, bali ifanyeni hukumu iliyo ya haki.” (Yoh.7:24).

“Mungu… huwaangazia jua lake WAOVU NA WEMA, huwanyeshea mvua WENYE HAKI NA WASIO HAKI.” (Matt.5:24).

Wapo watu wengi wanaodhani kimakosa kwamba kubarikiwa na mambo ya nje (mavazi mazuri, pesa, gari, nyumba nzuri, kufanikiwa katika biashara) KWA UHAKIKA inaonyesha baraka za Mungu katika maisha yao, na hiyo ndiyo ALAMA YA MAISHA YA KIROHO YENYE MAFANIKIO! Na wanajaribu kushawishi na wengine kufikiri hivyo. Kwa upande mwingine, wanadhani kwamba kama unapungukiwa na ‘baraka za nje’ ina maana humpendezi Mungu. Huo ndio ushirikina. Wamedanganywa.

Nilimsikia mshirika mmoja wa kanisa fulani akasema kwamba yeye anataka kumfuata muhubiri aliyefanikiwa, ambaye ana fedha nyingi, avaae nguo za gharama na kutembelea magari ya kifahari. Anasema anataka kumfuata mtu ambaye amefanikiwa kupata kitu maishani mwake kwa sababu na yeye pia anataka apate kitu na awe mtu mwenye mafanikio! Mawazo kama hayo yanaonyesha kwamba mtu huyo hajui Injili wala hamjui Yesu alivyo. Uchoyo unawakula watu wengi siku hizi na uchoyo huo unawaongoza kudanganywa wasielewe Injili wala Yesu Kristo.

“Akawaambia, Angalieni, JILINDENI NA CHOYO, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo.” (Luka 12:15).

Unaona? Uchoyo moyoni mwako unakupelekea hali ya kufikiri wingi wa vitu vyake alivyo navyo ni alama ya kumpendeza Mungu! Ni wazi, Mungu anaweza kutubariki rohoni na mwilini, LAKINI kupima maisha ya kiroho yetu kulinganisha na ‘baraka za nje’ tulizozipata ni ushirikina (superstition). Kufikiri baraka za nje ni sawa na kumpendeza Mungu, na kupungukiwa na baraka za nje ina maana Mungu hapendezwi nasi, ni dini ya ushirikina (religion of superstition).

Mungu aliwalisha watu wake kwa mana jangwani na mavazi yao hayakuchakaa, wala miguu yao haukuvimba kwa miaka arobaini. (Kumbuk.8:3,4). Hayo yote yalikuwa MIUJIZA na BARAKA za Mungu kwao kwa miaka arobaini, lakini neno la Mungu linatujulisha juu ya watu hao jangwani, “wengi sana katika wao, Mungu HAKUPENDEZWA NAO!” (Soma 1 Wakor.10:1-5)! Kwa kweli Mungu alitangaza juu ya watu wake maneno hayo, “…nilichukizwa na kizazi hiki, Nikasema, Sikuzote ni watu WALIOPOTOKA MIOYO hawa; HAWAKUZIJUA NJIA ZANGU.” (Waebr.3:10).

Ni jambo la kuhuzunishwa sana kwamba wengi wanaokwenda kanisani siku hizi hawazijui njia wala tabia ya Mungu. Wanapima maisha ya kiroho yao kadiri wanavyobarikiwa na mambo ya nje. Waisraeli walipotoka Misri walifurahi sana kwa ajili miujiza na baraka za Mungu – waliamini Mungu yupo upande wao. Baada ya siku tatu walipungikwa na maji ya kunya (baraka ya nje) na MARA MOJA waliamini Mungu yupo juu yao na dhidi yao. Kila mara watu wa Mungu jangwani walipokutana na shida na kupungukiwa na ‘baraka’ walinung’unika na wakasema, “Ni kwa sababu Bwana AMETUCHUKIA, ndipo akatutoa katika nchi ya Misri, apate kututia katika mikono ya Waamori, ILI KUTUANGAMIZA.” (Kumbuk.1:27).

Unaona? Walimpima Mungu kulinganisha na matendo yake katika mazingira yao tu! Walikosa kabisa. Waisraeli hawakutambua tabia ya Mungu – waliweza kuelewa Mungu kupitia hali ya mazingira yao tu, kupitia matendo yake ya nje tu, kadiri ya baraka za kimwili tu! Hiyo ndiyo dini ya ushirikina na kwa hiyo maandiko yanasema, “Alimjulisha Musa NJIA zake, Wana wa Israeli MATENDO yake.” (Zab.103:7). Ni vile vile siku hizi – wengi hawazijui njia ya Bwana, ‘wanahukumu hukumu ya macho tu’; hawawezi kutambua Mungu wala tabia yake ila kwa mazingira yao, ila kwa matendo ya Bwana katika mazingira yao! Kutokana na ushirikina wao na kutokuamini kwao wanasema, “Kama ukipungukiwa na baraka (za nje), ina maana huishi karibu na Mungu. Kama umebarikiwa na mambo ya nje, ya kwimili, ni alama ya mafanikio ya maisha ya kiroho yako!” Wengi sana wanaokwenda kanisani wanafikiri vivyo hivyo.

Na turudi kwa maneno ya Yesu, “…uzima wa mtu HAUMO KATIKA WINGI WA VITU VYAKE ALIVYO NAVYO.” Katika sura hiyo ya Luka 12 Yesu anaendelea kuongea juu ya kunguru na maua, juu ya tutakula nini au tutavaa nini, naye alisema, “Ninyi msitafute mtakavyokula wala mtakavyokunywa; wala MSIFANYE WASIWASI,… Bali utafuteni ufalme wa Mungu, na hayo mtaongezewa.” Anasema ‘hayo’ mtaongezewa – kwa muktadha ya sura hiyo, ‘hayo’ inamaanisha chakula na mavazi (ila tunajua anaweza kukutana na mahitaji mengine pia katika maisha yetu!). Ni jambo la ajabu jinsi andiko linavyokubaliana na andiko, jinsi maneno ya mtume Paulo yalivyounga mkono na maneno ya Yesu anaposema, “tukiwa na chakula na nguo TUTARIDHIKA na vitu hivyo.” (1 Tim.6:8). Sawa, tunajua Mungu anaweza kutubariki zaidi ya hayo, hata hivyo, Paulo anachosema hapo je, kwa msingi ni mwelekeo wa moyo wako, ni mtazamo (attitude) ya moyo wako? Je, unaishi kwa ukweli huo?  

Unaridhika na nini? Lazima ubarikiwe na mambo ya nje, ya kimwili KIASI GANI kabla ya hujaridhika? Ujiulize na jibu mwenyewe kwa ukweli moyoni mwako. Neno la Mungu linatutangaza, “UTAUWA pamoja na KURIDHIKA ni faida kubwa.” (1 Tim.6:6). HALI YA MIOYO YETU ni muhimu, siyo wingi wa vitu vyetu tulivyo navyo! Uhusiano wetu na Yesu ni muhimu, siyo mambo yanayotokea au yasiyotokea katika mazingira yetu! Kwa hiyo Paulo anaweza kusema,

“nimejifunza KUWA RADHI na HALI YO YOTE niliyo nayo. Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; KATIKA HALI YO YOTE, na katika MAMBO YO YOTE, nimefundishwa KUSHIBA na KUONA NJAA, kuwa na vingi na kupungukiwa.” (Wafilipi 4:11,12). Hayo ni manano ya mtu anayetembea karibu na Mungu!

Unaona? Baraka za kweli za Mungu hazitegemei na mazingira yetu, na vitu tulivyo navyo au na vitu tusivyo navyo! Haijalishi inachotokea au isichotokea katika mazingira yetu. Muhimu ni jambo moja, yaani, “Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.” (Warumi 5:8). Unataka kujua Mungu anavyokupenda kiasi gani? Hutazami mazingira yako, tazama Mwana wa Mungu, Yesu Kristo, msalabani akifa kwa ajili yako! Halipo pendo kuu kuliko hilo!

Najua Ibrahimu alibarikiwa kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu. Najua hayo vizuri sana. Najua pia kwa ajili ya uchoyo wa mioyo yao, wapo watu wanaotaka kutokujali mafundisho ya Bwana Yesu na Agano Jipya kwa kudai baraka za mambo ya ulimwengu huo ni alama ya maisha ya kiroho yenye mafanikio – lakini wanajidanganya. Hatari ni hiyo – inawezekana watu hao hawatamtambui Yesu Kristo atakaporudi! Hawataitambui tabia Yake kwa sababu tabia yao inatofautiana na tabia ya Yesu.

Wazo la Mwisho.

Ilikuwa vivyo hivyo siku ya Paulo. Paulo aliwaandikia waumini wa Korintho, “Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo.” (2 Wakor.11:3). Waumini hao walikaribia kudanganywa na shetani. Kwa nini? Kwa sababu ya hiyo: “Yaangalieni yaliyo MBELE YA MACHO YENU.” (Wakor.10:7). Yaani, Paulo alihubiri Injili BURE kwao! Zaidi ya hayo alifanya kazi kwa mikono yake mwenyewe (1 Wakor.4:12). Ingawa alikuwa mtume, Paulo hakuwashuruthisha wala hakuwataka wampe pesa kwa ajili ya huduma yake kwao! (1 Wakor.9:4-18). KWA SABABU YA HIYO sehemu ya kanisa la Korintho walifikiri Paulo hakuwa mtu muhimu sana, zaidi ya hayo, wengine hawakuamini Paulo alikuwa mtume wa Bwana! Inaonekana wengine walisema, “Kumbe! Alifanya kazi kwa mikono alipokuwepo miongoni mwetu! Haiwezekani kwamba yeye ni mtumishi muhimu au maarufu!” Walihukumu hukumu ya macho tu; walimpima kwa mambo ya nje tu! Kwa sababu ya hiyo aliwaandikia, “Maana nadhani ya kuwa mimi sikupungukiwa na kitu walicho nacho mitume walio wakuu.” Unaona? Alilazimishwa kuutetea utume wake na huduma yake kwao! Anasema tena, “Mtu akijitumainia mwenyewe ya kuwa ni mtu wa Kristo, na afikiri hivi pia nafsini mwake, ya kwamba kama yeye alivyo mtu wa Kristo, vivyo hivyo na sisi…. Wao ni wahudumu wa Kristo?… mimi ni zaidi… Maana nadhani ya kuwa mimi sikupungukiwa na kitu walicho nacho mitume walio wakuu.” (2 Wakor.10:7). Wuamini wengine kati ya Wakorintho walikuwa na shaka juu ya huduma yake kwa sababu Paulo hakuwataka wampe pesa kwa ajili ya huduma yake! Kwa hiyo aliandika, “Je! Nilifanya dhambi kwa kunyenyekea ili ninyi mtukuzwe, kwa sababu naliwahubiri Injili ya Mungu BILA UJIRA?” (2 Wakor.11:7).

Waumini wengi waliopo Wakorintho waliyapima na kuyahukumu mambo kwa yale yaliyo ‘mbele ya macho’ yao tu, kwa ‘mambo ya nje’ (outward things). Waumini wa Korintho waliwapokea wale ‘waliojisifu kwa jinsi ya mwili.’ (2 Wakor.11:18). Kwa hiyo walikuwa tayari kumpokea mtu aliyejiinua miongoni mwao, kujifanya mwenyewe awe mtume au nabii, kujidai ni mtu maarufu, na kuwalazimisha watu wampe pesa kwa ajili ya huduma yake! “Maana mwachukuliana na mtu akiwatia utumwani, akiwameza, akiwateka nyara, akijikuza, akiwapiga usoni.” (2 Wakor.11:20). Ukweli huo ni muhimu sana kwani mambo haya yanatokea siku hizi na wengi wanadanganywa. Kwa sababu Wakorintho wengi waliyapima mambo kwa macho ya kimwili tu (Ohhhh! Anavaa mavazi mazuri ya gharama kubwa; amekuja kwa magari yenye fahari. Tazama jinsi Mungu alivyombariki! Nkd. nkd. nkd.) HAWAKUWEZA KUTAMBUA HUDUMA YA KIROHO, huduma ya kweli kweli, na walikuwa tayari kuwapokea mitume wa uongo na watumishi wa shetani! Kwa sababu ya hali ya kiroho yao walikaribia kudanganywa kabisa. Sikiliza mtume Paulo, “Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo. Maana yeye ajaye akihubiri Yesu mwingine ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea roho nyingine msiyoipokea, au injili nyingine msiyoikubali, MNATENDA VEMA KUVUMILIANA NAYE!… Lakini nifanyalo nitalifanya, ili niwapinge hao watafutao nafasi wasipate nafasi; ili kwamba katika neno hilo wajisifialo waonekane kuwa kama sisi. Maana WATU KAMA HAO NI MITUME WA UONGO, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo. Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru. Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao.” (2 Wakor.11:3,4;12-15).

Na mambo hayo yanatokea siku hizi. Sio tu kwamba waumini wanakosa, bali wahubiri wa uongo wanawashawishi wasikilaji kufikiri ya namna hiyo, wawe watu wa kimwili badala ya watu wa kiroho. Wote wanaanguka pamoja gizani.

Kumbuka na tunza ukweli huu, “Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo… Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema.” (Waefeso 1:3; Warumi 8:28).

Mambo hayo ni ya maana sana siku hizi. Nimeandika somo hili ili litusaidie tupo tayari kumkutana na Yesu atakaporudi, na tusishtuke wala tusiaibike kwa kufunuliwa kwake. Mungu atufumbue macho yetu tutambue ukweli kama ulivyo katika Yesu. Amen.

© 2016  David Stamen    somabiblia.com

Unaweza kupakua somo hili kwa kubonyeza link hapo chini:

Ushirikina au Injili

 

Comments are closed.