RSS

Uzima wa Milele ni nini? Injili ni nini?

“Kama vile Baba alivyo na uzima ndani Yake, vivyo hivyo amempa Mwana kuwa na uzima ndani Yake.” (Yoh.5:26).

Uzima wa milele siyo jambo la muda! Kana kwamba, eti, utaishi kwa milele na milele, mwaka hadi mwaka hadi mwaka! Baba na Mwana tu wanao huo Uzima ndani Yao! Uzima wa milele ni jambo la hali, jambo la tabia!

Uzima (wa milele) ni hali au tabia ya Mungu Mwenyewe!  Uzima wa milele ni Utakatifu, Upendo, Wema, Huruma, Uvumilivu, Ufadhili, Nuru. Mungu anaweza kulifanya jiwe lidumu hata milele. Bado hiyo haimaanishi kwamba lile jiwe linao uzima wa milele! Ni vivyo hivyo kwetu!

“Huu ndio ushuhuda, ya kwamba, Mungu ametupa uzima wa milele, nao huo uzima umo katika Mwanawe. Yeye aliye naye Mwana, anao uzima, yeye asiye na Mwana hana uzima.” (1 Yoh.5:11,12).

Unaona? Uzima wa milele ni ndani ya Yesu! Unakumbuka Yesu alisema, ‘Mimi ni njia, na kweli na uzima.’ (Yoh.14:6). Yeye Mwenyewe ni Uzima! Hamna uzima, hamna uzima wa milile nje ya maisha na tabia ya Yesu Kristo. Haitoshi kuamini kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu. “Unaamini kwamba kuna Mungu mmoja. Vema! Hata mashetani yanaamini hivyo na kutetemeka.” (Yak.2:19). Lazima ninaye Yesu Kristo ndani yangu. Maisha Yake ndani yangu huo ndio ni uzima wa milele ndani yangu! “Yeye aliye naye Mwana, anao uzima, yeye asiye na Mwana hana uzima.” Uzima wa milele ni hali ya tabia ya Mungu, kwa hiyo Mungu hakuweza kutupa Uzima wa Milele bila kutupa Uzima Wake, bila kutupa Roho Yake. Kwa hiyo Petro anatufundisha,

“Kwa kuwa uweza Wake WA UUNGU umetukirimia vitu vyote vipasavyo UZIMA NA UTAUWA… Kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa WASHIRIKA WA TABIA YA UUNGU…”. (2 Petro 1:3,4).

Na tena katika Waebrania,

“…hao (baba zetu) kwa siku chache waliturudi kama walivyoona vema wenyewe; bali Yeye (Mungu Baba) kwa faida yetu, ILI TUUSHIRIKI UTAKATIFU wake.” (12:10).

Yohana anatutangaza kwa wazi ukweli huu mkuu, “Watoto wadogo, ninyi MMETOKANA NA MUNGU, nanyi mmewashinda kwa sababu YEYE ALIYE NDANI YENU ni mkuu kuliko yeye aliye katika ulimwengu.” (1 Yoh.4:4).

Kama umeokoka kweli kweli, umezaliwa na Mungu! (1 Yoh.3:9). Siyo unamini tu; siyo unakwenda kanisani tu; siyo kwa sababu unafanya mambo ya dini; umeokoka kweli kweli kwa sababu umezaliwa na Mungu, umezaliwa KUTOKA JUU! Yesu aliposema ‘hamna budi kuzaliwa mara ya pili’, (Yoh.3:7) maneno haya ‘mara ya pili’ yanaleta maana ‘toka juu’ pia. Yesu alisema katika sura hiyo hiyo, ‘Yeye ajaye kutoka juu…’ (3:31), na maneno haya ‘toka juu’ na ‘mara ya pili’ kwa Kigiriki ni neno lile lile (anothen).

Kuwa mkristo ina maana asili yako na chanzo chako ni Mungu. “Kwa hiyo kama mtu akiwa ndani ya Kristo, amekuwa kiumbe kipya, ya kale yamepita, tazama, yamekuwa mapya. Haya yote yanatokana na Mungu.” (2 Wakro.5:17,18). Labda unakwenda kanisani. Labda unafanya mambo mengi ya dini lakini yote ni bure kama hujafanywa kuwa kiumbe kipya katika Kristo Yesu, kama Paulo anasema, “Kwa maana katika Kristo Yesu kutahiriwa au kutokutahiriwa si kitu, bali kuwa kiumbe kipya!” (Wagal.6:15). Hiyo ni mwanzo wa maisha ya Mkristo! Sikiliza mwandishi wa waraka wa Waebrania asemalo!

“Yeye (Yesu) awafanyaye watu kuwa watakatifu na wale ambao hufanywa watakatifu, wote pia WATOKA KWA  MMOJA (yaani, Mungu). KWA AJILI HII haoni haya kuwaita ndugu Zake.”

Kumbe, sisi siyo ndugu ya Yesu Kristo kwa sababu, eti, tunaamini jambo fulani tu. Hapana. Sisi tu ndugu ya Yesu kwa sababu sisi na Yeye tunatoka kwa huyo Mmoja, yaani Mungu! Kwa sababu tumezaliwa toka juu, tumezaliwa na Mungu, Yesu Kristo haoni aibu kutuita ‘ndugu’! Kwa kweli, huu ni wokovu upitao fahamu kwa jinsi ulivyo mkuu!

Unaona, kuokoka ina maana kupata uzima mpya kutoka Mungu; ina maana tumebadilishwa kabisa kwa ndani sana. Mungu Baba anaweza kufanya hivyo kwa sababu Mwanawe Yesu Kristo aliteswa msalabani.

“Kwa maana Mungu alimfanya Yeye asiyekuwa na dhambi kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi TUPATE KUFANYWA HAKI YA MUNGU katika Yeye.” (Wakor.5:21). Mstari wa maana sana na mwenye uzito! Na tena imeandikwa, “Kwa maana kama vile kwa kutokutii yule mtu mmoja wengi walifanywa wenye dhambi, vivyo hivyo kwa kutii kwa mtu mmoja wengi WATAFANYWA WENYE HAKI.” (Warumi 5:19). Huu ni ukweli wa Mungu – kutokana na dhambi ya Adamu tulifanywa wenye dhambi. Kwa kuzaliwa kwetu kwa kwanza tulipata tabia ya mwenye dhambi, na sawasawa na tabia hiyo tunafanya dhambi. Sasa, VIVYO HIVYO kupitia utii na mateso ya Yesu Kristo msalabani TUMEFANYA WENYE HAKI! Kwa kuzaliwa kwa pili tunapata Roho ya Mungu na maisha ya Yesu ndani yetu na sawasawa na Uzima huo tumewekwa huru mbali na dhambi ili “tusitumikie dhambi tena.”

Yesu Kristo aliomba Baba, “kama inawezekana, kikombe hiki na kiniepuke.” Unaona, hakikuwa kitu cha urahisi kwake Yesu kuondoa dhambi zetu msalabani! Yeye ni Mwana Mungu. Yeye ni Mtakatifu; Yesu alikuwepo pamoja na Baba katika utukufu kabla ya ulimwengu haujakuwako! Yeye hajui dhambi! Lakini anajua atakiwalo apatie msalabani, yaani, “kuchukua dhambi ya ulimwengu.” Isaya inasema, “Na Bwana ameweka juu Yake maovu yetu sisi sote…alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu…ATAWAFANYA WENGI KUWA WENYE HAKI KWA SABABU ATAYACHUKUA MAOVU YAO.” (Isaya 53). Kwa sababu ya hiyo, Yesu alipokuwepo bustani aliomba Baba mara tatu, “kama inawezekana, kikombe hiki na kiniepuke…Naye akiwa katika maumivu makuu, akaomba kwa bidii, nalo jasho Lake likawa kama matone ya damu yakidondoka ardhini.” (Luka 22:24). Bwana Yesu hakuogopa mateso ya kimwili! Tabia Yake ya kiungu inachukia maovu kabisa, lakini msalabni atakuwa ‘kufanywa dhambi’ na kuondoa dhambi yetu ili ‘tufanywe wenye haki’! Kwa hiyo Yesu alisema bustani, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa!” Kwa ufahamu wetu hatuwezi kuingia katika mambo haya au kuyaelewa kwa urahisi! Lakini haya yote ni neno la Mungu! Yanapita ufahamu wetu, lakini tunaweza kusema kwamba Mungu hakuweza kutoa bei kubwa zaidi kwa ajili ya wokovu wetu! Baba alitoa Mwanawe msalabani. Mwana alitoa maisha Yake msalabani.Tumenunuliwa na gharama iliyopita ufahamu wetu! “Tazameni ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba sisi tuitwe wana wa Mungu!”

Mwana wa Mungu hakutoa maisha Yake msalabani, ili tupate baraka tu za nje! Bwana Yesu ‘hakufanywa kuwa dhambi’ ili tuendelee kufanya  dhambi, au kucheza na dhambi, au tufikiri si kitu kikubwa kama nikifanya dhambi kwa sababu, eti, kila wiki baada ya kuungama dhambi zangu, mtu wa dini ataweza kutamka dhambi zangu zimesamehewa (huo ndio udanganyifu kubwa sana ambao unabatiza watu katika giza ya kiroho!). Mwana wa Mungu hakuchukua dhambi zetu msalabani ili tufikiri kwa sababu ya neema ya Mungu na damu ya Yesu sasa haidhuru kama nikifanya dhambi!

“Tuseme nini basi? Tudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi? Hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi? (Warumi 6:1,2).

Nilisikia waumini wakisema, “Samahani ndugu, nilifanya dhambi, lakini mimi ni binadamu tu.” Watu hao wanongea kama hawajui Agano Jipya, au hawajui kwa nini Yesu Kristo alikufa msalabani, kama hawajui wokovu wa Yesu Kristo! Wanafikiri kama wakristo ‘tumeacha kutokubadilishwa kwa ndani’, tumeacha kama ‘binadamu’ na kwa hiyo tunafanya dhambi; wanafikiri kwa sababu ya hiyo Mungu alitoa Mwanawe ili sisi, ‘kama bindamu’, tunapata msamaha kila mara!’ Wanakosa sana kwa mawazo haya! Yesu alikufa kwa sababu hiyo hiyo, yaani, kwa sababu tulikuwa ‘binadamu’! Maana yake ya ‘binadamu’ ni ‘mtoto wa Adamu’! Mungu alitoa gharama kubwa mno ili atubadilishe kabisa kwa ndani, kuibadilisha hali ya kiroho yetu, kutufanya ‘kiumbe kipya’, kutufanya ‘wenye haki’ ambao tumezaliwa na Mungu! Mwana wa Mungu alitoa gharama kubwa mno ili niishe kuwa ‘mtoto wa Adamu’ na kuwa ‘mtoto wa Mungu’ kwa kuzaliwa mara ya pili! Mungu apewe sifa kwa neema hii kuu! Kuwa Mkristo ina maana mabadiliko kubwa sana yametokea ndani yetu! Mtume Paulo anasema tunajua neno mmoja, yaani,

“mkijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale (‘binadamu wa kale’ – kwa Lugha ya Kigiriki) ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena” (Warumi 6:6).

Paulo anawauliza Warumi, “Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.”(m.3,4). Unaona, kitu kikubwa sana kimetokea msalabani kutubadilisha kabisa ili ‘tusitumikie dhambi tena’ na tuenende katika upya wa uzima! Matokea ya kazi ya msalaba ni haya,

“dhambi haitawatawala ninyi, kwa sababu hamwi chini ya sheria, bali chini ya neema.” (War.6:14).

Kwa wale wafikirio kwa sababu ya neema haidhuru sana kama nikifanya dhambi, Paulo anandika, “Ni nini basi? Tufanye dhambi kwa sababu hatuwi chini ya sheria bali chini ya neema? Hasha!” (m.15). Kwa wakristo kisingizio kwa dhambi siyo ‘mimi ni binadamu tu’; kisingizio siyo neema; kwa msingi, kisingizio sio shetani! Hakuna kisingizio! Imebaki toba tu; tukiri tumekosa, tumefanya dhambi na kwenda mara moja na moja kwa moja kwa Yesu tupate msamaha na kutusafishwa kwa damu Yake! Kwa sababu ya kufa kwake Yesu msalabani hatuna kisingizio kwa ajili ya dhambi tena, kama, eti, wokovu wa Yesu haufiki kiasi cha kuniokoa kutoka katika jaribu hili! Neno la Mungu linatangaza,

“Naye…aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee.” (Waebrania 7:25). Mungu alifanya yote kupitia Mwana Wake ili tufanye mtakatifu.

Kwa damu ya Yesu tunapata msamaha wa dhambi. Kwa damu ya Yesu tunasafishwa na dhambi yote. Kwa kifo cha Yesu msalabani ‘tumewekwa huru mbali na dhambi na nguvu za dambi’ (Warumi 6:18).

Yesu amevunja ile nguvu za dhambi katika maisha yetu. “Kwa sababu sheria ya ROHO WA UZIMA ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti.” (Warumi 8:2). Sheria ya nje haina uwezo kuibadilisha hali ya kiroho yako au tabia yako. Kwa mfano, na tuweke sheria kwa ajili ya nyoka, na sheria hiyo inasema “uwe mwanakondoo!” Sasa, nyoka anaweza kujitahidi sana awe mwanakondoo; anaweza kujaribu kufanya hivi na hivi; anaweza kusali na kwenda kanisani, lakini anabaki nyoka! Hakuna mabadiliko! Kwa hiyo Yesu alisema, “Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye AWE NA UZIMA WA MILELE KATIKA YEYE.” (Yoh.3:14,15). Unakumbuka, Waisraeli walipofanya dhambi waliumwa na nyoka na wengi walikufa. Mungu alimwambia Musa atengeneze NYOKA WA SHABA NA AMWEKE JUU YA MTI, ye yote aliyeumwa na nyoka anaweza kumtazama NA AKAISHI TENA. (Hesabu 21:8). Neema kuu ya Mungu! Yesu Kristo kwa maneno Yake alijilinganisha Mwenyewe na nyoka mtini (msalabani)! Biblia ni ya ajabu! Kwa hiyo Biblia inasema, “utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye (msalabani), tusitumikie dhambi tena.” Nyoka hawezi kudai awe mwanakondoo, hawezi kuwa mwanakondoo! Ipo njia mmoja tu! Kuiua tabia ya nyoka na kufanya kiumbe kipya! Matendo ya mwili yanatokana na tabia au hali ya kiroho iliyomo ndani ya mwili! Kwa hiyo ‘sheria’ iliyo nje ya hali yetu haiwezi kutubadilisha! Lazime tubadilishwe kwa ndani kwanza! Yesu Kristo alisulibisha utu wetu wa kale, na nguvu wa dhambi, na nguvu wa shetani msalabani! Kwa hiyo Paulo anatangaza, “Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu!” (Wagal.2:20). Je, inakukwaza au ni chukizo kwako kulinganishwa na nyoka? Kama unasema ‘ndiyo’, ndipo ina maana hujui tabia yako; hujui kina cha dhambi ndani yako; hujui udanganyifu wa dhambi; hujafikia toba kweli kweli! Yesu alijilinganisha na nyoka msalabani ili kutuonyesha kwa wazi hali yetu ni mbaya ya namna gani! Yesu hakufa msalabani ili ‘kuboresha’ maisha yetu! Hakuna ‘kuboresha’ kwa maisha ya mwenye dhambi, kwa sababu “Sisi sote tumekuwa kama mtu aliye najisi, nayo matendo yetu yote ya uadilifu ni kama matambaa machafu!” (Isaya 64:6). Ipo njia mmoja tu – kusulibisha utu wetu wa kale na kufanya kiumbe kipya!

Sheria haikuweza kutufanya wenye haki na watakatifu, lakini, “yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili; ili maagizo ya torati YATIMIZWE NDANI YETU SISI, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.” (m.3,4).

Kwa kifo chake msalabani imeandikwa juu ya Yesu, “kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi” (Waebr.2:14). Na tena, “Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.” (! Yoh.3:8).

Kwa kifo cha Yesu msalabani, Mungu ‘ametugeuza tuiache giza na kuielekea nuru, tuziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu.’ (Matendo 26:18).

Kwa kufa na ufufuo wa Yesu, “Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; ALITUHUISHA pamoja na Kristo.” Na Paulo anasema maneno haya ya ajabu, “Kristo Yesu…aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili.” (2 Timotheo 1:10).

Tayari Yesu alibatili mauti! Tayari Kristo Yesu ametuletea uzima wa milele, sawasawa na alivyosema, “Mimi ndimi chakula cha uzima… Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ATAISHI MILELE.” (Yoh.6:48,58).

Unaona, kwa mkristo kweli kweli, uzima wa milele tayari umeshaanza kwa sababu Mungu alimhuisha na alizaliwa na Mungu. Kama nilivyosema kwenye mwanzo wa somo hili, kama tumeokoka kweli kweli Mungu ametupa uzima wa milele, na uzima wa milele ni nini? Uzima wa milele ni uzima au maisha ya Yesu Mwenyewe.

Kwa sababu ya mambo haya yote, neno la Mungu anatufundisha, “Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu… Kila akaaye ndani yake hatendi dhambi; kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtambua.” (1 Yoh.3:6,8). Kama nilivyosema hapo juu, matendo yetu yanatokana na hali ya kiroho yetu!

Yesu alikufa msalabani ili tuzaliwe na Mungu na tusitumikie dhambi tena! ‘Hawezi kufanya dhambi.’ Fundisho lenye uzito sana! Na nitoe mfano, labda itakusaidia. Mama mmoja yupo kando ya mto akimbeba mtoto mchanga wake anampendaye sana. Sasa je, mama huyo anaweza kumtupa mtoto wake mtoni? Hawezi! Maana ya ‘hawezi’ ni nini? Je, huna uwezo wa kimwili kumtupa mtoto wake mtoni? Ndiyo, anao uwezo wa kimwili kufanya hivi. Nguvu ya mwili ipo! Hata hivyo, mama huyo ‘hawezi’ kumtupa mtoto wake mtoni! Kwa nini? Kwa sababu ya TABIA YAKE ya umama! Yeye ni mama ya mtoto wake ampendaye! Tabia yake inamzuia kufanya tendo lile baya! Hawezi kufanya hivyo! Vivyo hivyo kwa mkristo kweli kweli siyo tabia au nia yake kufanya dhambi, siyo desturi yake kufanya dhambi, kwa sababu alizaliwa kutokana na Mungu. Kufanya dhambi ingemhuzunisha sana kwa sababu ni kinyume cha nia yake. Kama mama yule angedharau mtoto wake angehuzunishwa sana!

Kama mtu fulani akisema, ‘Nisamehe ndugu yangu, mimi nimefanya dhambi, lakini mimi ni mwenye dhambi tu, mimi ni binadamu tu…,’ ndipo yule mtu hajui Injili kweli kweli na anajaribu kutoa kisingizio kwa dhambi zake! Kwake dhambi ni kama jambo la kawaida tu. Kwa msingi anasema, ‘Mimi ni mwenye dhambi, na sawasawa na tabia yangu ya mwenye dhambi ni jambo la kawaida nifanye dhambi’! Mtu huyo anaongea kama hajui wokovu wa Yesu Kristo ndani ya moyo wake – dhambi haimhuzunishi kiasi cha kwenda mara moja kwa Bwana, kutubu na kupata kusafishwa dhambi yake tu, na zaidi ya hayo kuliitia jina la Bwana ili awekwe huru na dhambi hiyo! Kama hiyo ni nia yako; kama unaweza kufanya dhambi bila kuhuzunishwa mara moja, bila kwenda kwake Yesu mara moja kupata kusafishwa na dhambi zako; kama dhambi siyo jambo zito au la maana sana kwako, eti, kwa sababu unasema ‘mimi ni mwenye dhambi, mimi ni mwanadamu tu’ au ‘nalitegemea kanisa na mtu wa dini kusahihisha na kusawazisha yote kwa ajili yangu’, ndipo unakiri hujui au hutaki kujua wokovu wa Yesu Kristo katika maisha yako. Au ni nani aliyekudanganya – mtu mwingine au wewe mwenyewe?

Mkristo amfuataye Bwana Yesu hatafuti kisingizio kwa dhambi zake! Mkristo anaichukia dhambi; anashindwa kuivumilia dhambi katika maisha yake, kwa sababu amepokea ndani ya maisha yake uzima ule uliomo ndani ya Kristo Yesu, ambaye juu Yake imeandikwa, “Umependa haki, umechukia maasi”! (Waebr.1:9). Bwana Yesu aliondoa kila kisingizio juu ya dhambi kwa upande wetu. Tuliona hapo juu ya kuwa Yesu Kristo alivunja nguvu za dhambi, alivunja nguvu za shetani, ‘utu wa kale’ ulisulibishwa pamoja na Kristo na tumewekwa huru mbali na dhambi.

Mungu hajatufanya ‘kwa dhambi’. Mungu kupitia Mwanawe ametufanya kwa Yeye Mwenyewe. (God has not made us for sin. He has made us for Himself.) “Maana tu kazi Yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo… Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu, hata mkazitii tamaa zake.” (Waefeso 2:10; War.6:12).

Mwana wa Mungu alikufa kwa ajili yetu “ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo.” (Waefeso 1:4). Katika Matendo ya Mitume na Nyaraka zote ya Mitume, Wakrsito huitwa “watakatifu” kama mara hamsini – ni jina la kawaida kwa waumini katika Agano Jipya! Hamna mstari mmoja katika Agano Jipya ambapo Wakristo wameitwa ‘wenye dhambi’! Kama wewe ni mwenye dhambi, sikiliza neno la Mungu juu ya watu hao, “Lakini ikiwa sisi wenyewe, kwa kutafuta kuhesabiwa haki katika Kristo, tulionekana kuwa wenye dhambi, je! Kristo amekuwa mtumishi wa dhambi? Hasha! Maana nikiyajenga tena yale niliyoyabomoa, naonyesha ya kuwa mimi mwenyewe ni mkosaji.” (Wagal.2:17,18). Unaona, wao waliookoka kweli kweli waliacha kuishi kama mwenye dhambi, waliacha kutumikia dhambi! Kupitia toba kweli kweli na kuzaliwa kutoka juu, nilibomoa maisha ya dhambi, sasa je, inakuwaje nijenge tena matendo ya makosa, isipokuwa ninajifanya mwenye dhambi tena? Paulo anasema siyo kazi ya Kristo kutufanya tuwe wenye dhambi! Hasha!

Tumeshasoma juu ya kufa kwa Yesu kwamba, “kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki.” Kutokana na yale ambayo Yesu alifanya msalabani waumini wamefanywa wenye haki, kama Petro anasema, “Kwa maana wakati umefika wa hukumu kuanza katika nyumba ya Mungu; na ikianza kwetu sisi, mwisho wao wasioitii injili ya Mungu utakuwaje? Na mwenye haki akiokoka kwa shida, yule asiyemcha Mungu na mwenye dhambi ataonekana wapi? (1 Petro 4:17,18). Basi kama mimi ni mwenye dhambi, nitaonekana wapi? Mamilioni ulimwenguni wamedanganywa na dini – wanafikiri kwamba mtu mmoja wa dini tu aliyepo Rumi anayo mamlaka afanye mtu aitwe ‘mtakatifu’! Hiyo ni udanganyifu na makufuru. Ni Mungu tu anayeweza kufanya hivyo na neema Yake kuu ameshakufanya hivyo kupitia kufa kwake msalabani, “Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu… Maana kwa toleo moja amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa.” (Waebr.10:10,14). Wakristo wametakaswa na damu ya Yesu iliyomwagika msalabani kwa ajili ya wokovu wetu!

Kwa sababu ya hayo, wakristo huitwa ‘watakatifu’ katika Agano Jipya. Hapo chini ipo mifano michache tu,

“Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao… Kwa hiyo, ndugu watakatifu, wenye kuushiriki mwito wa mbinguni ….Nawaapisha kwa Bwana, ndugu watakatifu wote wasomewe waraka huu… tangu nilipopata habari za imani yenu katika Bwana Yesu, na pendo lenu kwa watakatifu wote.” (Wakol.3:12; Waebr.3:1; Wathes.5:27; Waefeso 1:15).

Wao wasisitizao kuwa, ‘Ahhh, mimi ni mwenye dhambi tu’, kwa ujumla wanamaanisha kwamba wamezoea kufanya dhambi na hawatafuti mabadiliko katika hali ya kiroho yao! Au hawajasikia Injili!

Kama nilivyosema, Uzima wa milele kwa msingi siyo jambo la muda, ni jambo la hali ya kiroho au tabia, ni jambo la Yesu Kristo ndani yetu. Uzima wa milele ni uzima wa Mungu ndani yetu!

Unakumbuka Bwana Yesu alisemaje, “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?  Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.” (Mat.7:21-23). Unaona? Wanamwite Yesu ‘Bwana’, na kwa jina Lake walifanya ‘miujiza’, lakini Yesu hakuwatambua, hakuiona tabia Yake ndani yao! Lakini kwa upande mwingine kabisa, Yohana anaidhirisha sababu ya ujasiri wa waumini kweli kweli siku ya hukumu, “Katika hili pendo limekamilishwa kwetu, ili tuwe na ujasiri katika siku ya hukumu; kwa kuwa, kama yeye alivyo, ndivyo tulivyo na sisi ulimwenguni humu.” Unaona, ni maisha mmoja! Ni maisha yale yale, ndani Yake na ndani yangu kutokana no Roho niliyoipokea! Kwa hiyo Yohana anatufundisha na kutuonya ya kuwa, “Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda.” (1 Yoh.4:17; 2:6).

Tusicheze na mambo haya. Kwa sababu ya ‘dini’ watu wengi siku hizi wamepotea. Kuwa mkristo ina maana maisha yangu yamebadilika kabisa kwa ndani na niliacha kuitumikia dhambi. Labda unafikiri Paulo anajiita ‘mwenye dhambi’ katika 1 Timotheo 1:15, “Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi.” Ndiyo, Yesu alikuja kumwokoa Paulo. Kwa nini alisema ‘ambao wa kwanza wao ni mimi’? – ni kwa sababu ya mistari kabla ya mstari 15 ambapo anasema, “hapo kwanza nalikuwa mtukanaji, mwenye kuudhi watu, mwenye jeuri” (m.13). Paulo alikuwa mwenye kuliudhi Kanisa la Bwana, kwa hiyo alisema alikuwa ‘wa kwanza’ kwa wenye dhambi – inahusu maisha yake kabla ya hajaokoka, kama vile mstari wa 16 unavyotuonyesha, “Lakini kwa ajili hii nalipata rehema, ili katika mimi wa kwanza Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote; niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini baadaye, wapate uzima wa milele.” Kumbe! Maisha ya Paulo yamebadilishwa kabisa kwa sababu ya neema na rehema ya Mungu! Kama unataka kulinganisha na Paulo na kudai wewe ni ‘kwanza wa wenye dhambi’, ni sawa – kwa masharti ya kudai pia sasa maisha yako ni kielelezo kwa wale waoamini!

                                                       ——————————————

Kama ukitenda dhambi na dhambi hii haikuhuzunishi sana, ni wazi huna uhusiano na Mungu au hujaokoka. Kama ukitenda dhambi na unaweza kungoja mpaka mwisho wa juma kukiri dhambi zako mbele ya mtu wa dini ili upate uthibitisho wa msamaha wa dhambi zako, tena ni wazi huna uhusiano na Mungu au hujaokoka. Umedanganywa. Kama ukiwa na uhusiano na Mungu ingekuhuzunisha sana kama ungalifanya dhambi, na ungekwenda mara moja kwake Yesu upate msamaha. Kama ilivyoandikwa, “…nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu…” (1 Yoh.2:1,2). Yote Mwokozi wetu aliyoyafanya na yote yaliyoandikwa katika neno la Mungu ni kwa lengo ‘tusitende dhambi.’ Lakini ikiwa mtu ametenda dhambi tunaye Mwombezi – siyo mtu wa dini – kwa Baba naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu! Hakuna mtu mwingine kusimama kati yangu na Mungu ila Yesu Kristo tu! “Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu.” (1 Tim.2:5). Ndiyo, naijua ile mistari Yohana 20:23 na Yakobo 5:16, lakini mistari hii haifundishi ni lazima muamini aende kwa mtu rasmi wa dini kwa ajili ya kuungama dhambi zake ili mtu wa dini athibitishe msamaha wa dhambi zake! Biblia inaeleza! Katika Biblia nzima haupo mfano mmoja ambapo muamini mmoja alikwenda kwa mtu mwingine apate uthibitisho wa msamaha wa dhambi zake! Katika Biblia nzima haupo mstari hata mmoja unaofundisha lazima niende kwa mtu wa dini ili nipate uthibitisho wa msamaha. Huwezi kwenda kwa ‘kuhani’ kwa ajili ya dhambi zako! Kwa nini? Kwa sababu waumini kweli kweli WOTE ni makuhani!

“Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa muwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo… Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu (1 Petro 2:5,9).

Kama unafikiri mchungaji au padre ni ‘kuhani’ wako kwa ajili dhambi zako mbele ya Mungu, umedanganywa. Umenyang’anywa na uhusiano na Mungu. Wakristo ni ukuhani matakatifu watoao dhabihu za roho zinazokubaliwa na Mungu!

Hakuna kuhani kati yangu na Mungu! Je, ni jambo halisi katika maisha yako kufanya kama mtume alivyotusisitiza, “Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu…Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.” (Waebr.4:14,16). Unaona? Hatuna kuhani kati yetu na Mungu! Tunamfuata Kristo Yesu tukaingia patakatifu kwa Roho Mtakatifu. Kama Paulo anavyoeleza, “Kwa maana kwa Yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja.” (Waefeso 2:18). Je, unajua hivi katika maisha yako ya kila siku? Je, maisha ya kiroho yako yanaonekana kama hivyo? Kupitia damu ya Yesu hatupati msamaha za dhambi tu, bali tumesafishwa kwa ndani kwa damu ya Yesu nasi tumewekwa huru mbali na dhambi ili tuweze kuingia katika uwepo wa Mungu. Yesu Kristo alikufa ili atulete kwa Baba na kwa hiyo neno la Mungu linatusistiza, “Basi, ndugu, kwa kuwa tuna UJASIRI wa KUPAINGIA patakatifu kwa damu ya Yesu, njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake; na kuwa na kuhani mkuu (yaani, Yesu) juu ya nyumba ya Mungu; na tukaribie wenye moyo wa kweli, kwa utimilifu wa imani, hali tumenyunyiziwa mioyo tuache dhamiri mbaya, tumeoshwa miili kwa maji safi.” (Waebr.10:19-22). Maneno ya ajabu na ya maana sana! Kwa damu ya Yesu tunaingia pale Mungu alipo – katika mahali pa patakatifu!

Kutoka Adamu alipofanya dhambi mpaka kufa kwa Kristo msalabani mtu hakuweza kuingia pale Mungu alipo – angalikufa kufanya hivyo! Kuonyesha jambo hili Mungu alimuagiza Musa Waisraeli wajenge hema jangwani na katika hema hili walitenga chumba kimoja kilichokiitwa ‘Patakatifu pa Patakatifu’ na kuhani mkuu aliingia mara mmoja tu kwa mwaka kwa ajili ya dhambi ya watu. Kitabu cha Waebrania kinatueleza kwamba ‘kuhani mkuu’ wa Agano la Kale anawakilisha Yesu Kristo (kuhani mkuu wetu sasa) na patakatifu pa patakatifu panawakilisha uwepo wa Mungu na kiti cha neema mbinguni! (Waebr.9:11,12, 24). Ilitokeaje Yesu alipomwaga damu yake pale msalabani? Imeandikwa, “Pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini.” (Marko 15:38). Jambo la ajabu sana! Kwa mara ya kwanza katika historia ya binadamu njia ya kumkaribia Mungu (katika Roho) pale pale alipo imefunguliwa kwa sababu Yesu alitusafisha kwa damu yake naye aliziondoa dhambi zetu! Mwandishi wa Waraka wa  Waebrania anaeleza kwa uwazi, “Roho Mtakatifu akionyesha neno hili, ya kwamba njia ya kupaingia patakatifu ilikuwa haijadhihirishwa bado, hapo hema ya kwanza ilipokuwa ingali ikisimama…” (Waebr.9:8). Lakini kutokana na toleo la Yesu msalabani lile pazia hekaluni lilipasuka ili sisi tuweze kuingia kwa damu ya Yesu na kwa Roho Mtakatifu pale Mungu alipo, kama Petro alivyoandika, “Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili ATULETE KWA MUNGU.” (1 Petro 3:18). Neema kuu ya Mungu kwetu! Huo ndiyo ukweli mkuu sana!

Wokovu katika Kristo Yesu ni jambo kubwa zaidi kuliko msamaha wa dhambi tu – wokovu katika Kristo unatusafisha kiasi cha kutubadilisha kwa ndani sana kupitia kuzaliwa kutokana na Mungu! Na kwa sababu tunatokana na Mungu, Yeye ametuita twende pale alipo ili tushirikiane naye, kama Yohana anavyotufundisha, “na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo,” na ushirika huu ni katika nuru, “tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.” (1 Yoh.1:3,7). Kama tulivyosoma hapo juu, Mungu alituita, “tutoke gizani TUKAINGIE katika nuru yake ya ajabu.” Je, unao ushirika wa namna hiyo na Baba na Mwana katika maisha yako ya kila siku? Je, unaenenda nuruni na unajua moyoni mwako ya kuwa damu ya Yesu inakusafisha, au unahitaji kwenda kwa mtu wa dini kuthibitisha hayo kwa sababu huna ushirika, huna uhusiano na Mungu?

Lakini kwa sababu ya ushirika huo, Mkristo anakwenda mara moja kama mtoto mbele ya Baba kama akikosa na akatubu mbele Yake! Na Roho Mtakatifu atashuhudia moyoni mwake pamoja na neno la Mungu kwamba dhambi zake zimesamehewa na amesafishwa na damu Yake! (1 Yoh.2:2). Wao ambao wametubu kweli kweli na wamepokea Roho Mtakatifu wanajua ukweli wa mstari huu: “Roho Mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu.” (Warumi 8:16).

Kama umezaliwa na Mungu wewe unao uhusiano kwa ndani sana na Bwana: “Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye… Mungu ni mwaminifu ambaye mliitwa na yeye muingie katika ushirika wa Mwanawe, Yesu Kristo Bwana wetu..” (1 Wakor.6:17; 1:9). Yesu alikufa ili kutufanya wamoja na Baba na Mwana. “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako…hao nao wawe ndani yetu Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja…” (Yoh.17:21,23). Hilo ndilo kusudi la Mungu kupitia kufa kwa Mwana Wake msalabani, ili Yeye anaishi ndani yetu na sisi tuishi ndani Yake! (Yoh.14:20,23). Wokovu huo siyo jambo la dini; siyo jambo la nje, siyo jambo la sheria; siyo njia ambayo inaniruhusu kuendelea kuishi katika dhambi; wokovu wa Yesu Kristo ni nguvu ya Mungu ya kuniokoa kabisa kutoka katika dhambi na kunisafisha kabisa, kunibadilisha kabisa, kunifanya niwe kiumbe kipya kwa kuzaliwa tena kutokana na Mungu! Ninao uzima wa milele kwa sababu ninatokana na Mungu. Uzima wa milele ni maisha Yake ndani yangu, na Yeye hutuita kushirikiana sisi kwa sisi ili ‘tumjue’; ili ‘tupate kuwa washirika wa tabia ya Uungu’. Paulo anaeleza kwa maneno haya, “Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho.” (2 Wakor.3:18). Je, unajua ukweli wa mstari huo katika maisha yako ya kiroho? Ni halisi katika maisha yako? Huo ndio ushirika katika Roho ambao kupitia ushirika huo tunabadilishwa!

“Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima.” Uzima wa milele siyo jambo la muda; ni jambo la hali ya kiroho; ni jambo la kufanywa mwenye haki; ni jambo la tabia (kuzaliwa na Mungu); ni jambo la umoja; ni jambo la ushirika; ni jambo kumjua Baba na Mwana. Siku hizi wengi wanafuata ‘ndoto’ zao, au ‘mafanikio’, lakini huo ndio wokovu wa Yesu Kristo; huo ndio mwito wa Mungu.

Kama mambo yale niliyoyaandika yanaonekana kama kitu kigeni kwako, kama hujui ukweli au uhalisia wa mambo hayo katika maisha yako, ndipo inawezekana huujui wokovu huo wa Yesu Kristo.

Yohana Mbatizaji alishuhudia mambo mawili ya msingi juu ya huduma ya Yesu. la kwanza, “Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!” Na la pili, “yeye (Yesu Kristo) atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.” (Yoh.1:29 ; Luka 3:16). Kujua wokovu wa Yesu Kristo lazima utubu kwa ajili ya dhambi zako. Lakini toba ya kweli siyo jambo la kupokea kanuni za dini au kufuata sheria ya dini. Toba ya kweli inatokana na mambo haya: unatambua siyo unafanya dhambi tu, lakini unafanya dhambi kwa sababu ya tabia yako, na unajua kwa sababu ya dhambi hizo na tabia yako upo mbali na Mungu. Ndipo unakuja kwa Bwana Yesu kukiri dhambi zako na kuacha dhambi zako. Kama Yohana Mbatizaji alivyosema, “Basi zaeni matunda yapasayo toba.” (Math.3:8). Ina maana lazima maisha yako yatabadilika kupitia toba ya kweli – huwezi kubaki mtu yule yule kwa sababu, “Na shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.” (Math.3:10). Toba ya kweli inafika ndani sana ya moyo wako kusababisha mabadiliko kwa neema ya Mungu. Kupitia toba tunapokea msamaha wa dhambi zetu moja kwa moja kutoka kwake Yesu – siyo kupitia mtu wa dini – na Roho Yake itashuhudia moyoni mwako ya kuwa dhambi zako zimesamehewa! Baada ya hapo ni lazima ubatizwe kwa maji mengi, kwa sababu ‘batiza’ kwa lugha ya Agano Jipya (Kigiriki) ina maana “kuzama”, “kutosa”. Na zaidi ya hayo mtume Paulo anafundisha, “Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake.” (Warumi 6:4). Hapo Paulo analinganisha ubatizo na ‘kuzikwa’. Kama vile ‘kuzikwa’ inamaanisha kufunikwa kabisa na udongo, vivyo hivyo ‘kubatizwa’ inamaanisha kufunikwa kabisa na maji.

Na sasa tunakuta na jambo muhimu sana! Huduma ya Yesu Kristo ni kutubatiza kwa Roho Mtakatifu – huna budi kubatizwa na Roho Mtakatifu! Petro aliweka wazi kabisa njia, “Petro akawaambia, TUBUNI MKABATIZWE kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi MTAPOKEA KIPAWA CHA ROHO MTAKATIFU.” (Matendo 2:38). Ilikuwa vivyo hivyo kwa waumini waliopo Samaria (Matendo 8); waliiamini Injili ya Yesu Kristo na walibatizwa kwa maji. Baada ya hapo, mitume walikuja na waliwaombea wapokee Roho Mtakatifu na walipokea Roho wa Mungu! Kwa hiyo Paulo aliwauliza wanafunzi ambao alikutana nao huko Efeso, “Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini?” Paulo alitambua wanafunzi hao walikuwa hawajapokea Roho Mtakatifu na baada ya kuwaombea walijazwa na Roho Mtakatifu na wakanza kunena kwa lugha na kutabiri! (Matendo 19:1-6).

Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, aliimwaga damu Yake ili tuweze kupokea Roho Mtakatifu! Tunao ushirika na Baba na Mwana katika Roho Mtakatifu. Tusipopata nguvu ya Roho Mtakatifu kupitia ubatizo huo, hatuwezi kuwa mashahidi kweli kweli ya Bwana Yesu. (Matendo 1:8). Bila kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu hatuwezi kumwabudu Baba katika Roho na kweli. (Yohana 4:24; 7:38,39). Kutokubatizwa katika Roho Mtakatifu ina maana unakosa ‘ahadi ya Baba’ (Matendo 1:4), lakini Yesu alikufa ili atupe ahadi ya Baba, yaani, kipawa cha Roho Mtakatifu! Hilo ndilo Agano Jipya! Huwezi kuelewa au kujua maana ya ‘Agano Jipya’ katika maisha yako bila kubatizwa katika Roho Mtakatifu na moto.

Kwa wakristo mambo haya hayamaanishi sasa tunayo sababu kujivuna au kujisifu! Hapana! Tunategemea neema ya Mungu kabisa kwa wakati wote! Kama Paulo anavyosema, “Tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu.” (2 Wakor.4:7). Amina!

Na tuishie sasa kwa maombi ya Mtume Paulo:

“Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu…”

“Kwa hiyo nampigia Baba magoti…awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake katika utu wa ndani. Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu. Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo….” (Wefeso 1:17-20; 3:14-20)!

© David Stamen 2015

Kudownload somo hili bonyeza link: UZIMA WA MILELE NI NINI

Kusikiliza zaidi juu ya mambo haya bonyeza links zifuatazo:

https://somabiblia.wordpress.com/ubatizo-kwa-roho-mtakatifu-na-moto/

https://somabiblia.wordpress.com/ufalme-wa-mungu-1-shoka-limekwisha-kuwekwa-mizizi/

https://somabiblia.wordpress.com/ufalme-wa-mungu-2-semina-ya-casfeta/

https://somabiblia.wordpress.com/kuwekwa-huru-mbali-na-dhambi/

https://somabiblia.wordpress.com/msiupende-ulimwengu/

https://somabiblia.wordpress.com/ushirika-na-umoja/

Kusoma zaidi juu ya mambo haya bonyeza links zifuatazo:

https://somabiblia.wordpress.com/siku-ile-ni-siku-ya-nini-yohana-1420/

RUDI KWA HOMEPAGE

 

 

 

One response to “Uzima wa Milele ni nini? Injili ni nini?

  1. SAMSON EDWIN MBIJE

    November 30, 2015 at 10:45 am

    nimebarikiwa sana MUNGU awabariki

     

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

 
%d bloggers like this: