Nyumba ya Mungu ni nini?
‘NYUMBA’ YA MUNGU NA ‘MADHABAHU’ NI NINI?
Hebu niseme neno linalowasumbua baadhi ya watu. Sasa sisi tupo katika Agano Jipya. Mambo yote ya inje yahusuyo sheria ya Musa, yalitolewa kwetu ili kutufundisha sisi kuhusu Yesu, kuhusu kifo chake, dhabihu na ufufuo wake kuwa umekamilishwa. Sasa ni kwamba Kristo amekufa na amefufuka tena, hakuna haja tena ya vielelezo vya inje vya uhalisia wa kiroho kuendelea. Kwa kweli vielelezo vya kiinje vimeondolewa kwa sababu ya kile kilichokuwa kikielezea kimekwisha timilika kwa kuja kwake Kristo Yesu. Hivyo ndivyo kitabu cha Waebrania kinavyotufundisha kwa uwazi kabisa (Waebr. 7:11,12,19,22; 8:3-8; 9:11, 24;10:1). Halipo tena hema! Sisi sasa, ambao ni watakatifu, ndio makazi, jengo na hema ambamo Mungu anaishi kwa Roho. (Kwa hiyo Agano la Kale ni mwalimu wa kutuleta kwa Yesu.)
“Sasa kwa hiyo. . . . bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho. (Waefeso 2:19-22).
Kwa hiyo kama kuna mtu yeyote atasema kuwa jengo au chumba ambacho Wakristo hukutanika siku za jumapili kuwa hiyo ni ‘nyumba ya Mungu’ au akisema “Karibuni kwenye nyumba ya Mungu,” basi watu hao watakuwa wanaupotosha ukweli mkuu wa Agano Jipya. Ni makosa na watakuwa wanawafundisha watu wa Mungu kimakosa – wanawafanya wafikiri kuwa ukweli huu wenye nguvu za kiroho unahusu tu mambo ya inje. Kama vile matofali na chokaa. Sisi tu kanisa. Sisi ni hekalu la Mungu kiroho. Mahali pale wanapokutanika watu wa Mungu hapo ndipo kanisa la Mungu lilipo – hata kama mahali hapo ni chini ya mti! Katika Agano Jipya makanisa mengi walikutanika kwenye nyumba (Warumi 16:5; 1Wakor. 16:9; Wakolosai 4:15; Filemon 2). Nyumba ya Mungu ni kanisa, na kanisa ni watu wa Mungu (1 Timotheo 3:15). Maana halisia ya neno ‘Kanisa’ imekuwa haieleweki kutokana na tafsiri katika lugha ya asilia ya kigiriki, ambayo hata mtume Paulo ameitumia katika kuandika nyaraka zake. Neno hilo (yaani ‘kanisa’) ni ‘ekklesia’ – hii inamaanisha ni watu ‘walioitwa’. Inatumika kwa kikundi cha watu waliokusanyika mahali pamoja kwa kusudi maalum, kwa kawaida ni kwa kusudi la kidini. Jambo muhimu kwetu kutambua hapa ni kwamba neno ‘kanisa’ kinahusu watu, na wala kamwe si majengo yanayotumiwa na watu kukutania.
Hakuna tena mwendelezo wa kuhani wala ukuhani kati yetu sisi na Mungu – kwa sababu tumefanywa kuwa ukuhani mtakatifu, ukuhani wa kifalme (1 Petro 2:5-9), na Yesu ndiye kuhani wetu mkuu (Waebr4:14). Na yeye pekee ndiye mpatanishi kati ya mwanadamu na Mungu. (1 Timotheo 2:5). Kwa hapa duniani sisi ambao ni watu wa Mungu, tu hekalu la Mungu. Kupitia Yesu Kristo tunayo nafasi ya kuingia katika uwepo wa Mungu, katika patakatifu pa patakatifu mbinguni (Waebr. 4:16,10:19).
Kwa mtu yeyote yule kudai kuwa jengo ndio nyumba ya Mungu, hilo ni kosa kabisa. Kwa mtu yeyote yule kudai kuwa bado ipo madhabahu hapa duniani ambayo inawapasa Wakristo kuiendea, huo ni udanganyifu kwa ujumla wake. Kusema au kudai kuwa kuna aina fulani ya madhabahu inayoonekana ambapo Wakristo wanakutana pamoja huko ni kulikataa Agano Jipya. Katika Mathayo 5:23-24 Yesu anazungumza juu ya kuleta sadaka /zawadi zao madhabahuni – lakini hapo yeye alikuwa anawaambia Wayahudi ambao bado walikuwa wakiishi katika sheria, ni sawasawa vilevile kama Yesu alivyomweleza mtu yulevaliyeponywa ugonjwa wa ukoma kwamba aende akajionyeshe kwa kuhani wake na akatoe sadaka ya njiwa wawili. Hivyo Yesu anazungumza kwa wayahudi katika Matayo 5; anazungumza katika mantiki ya mfumo wao waliouelewa na ambao ndio walikuwa wakiishi wakati ule. Na kama ilivyo leo kwa mtu ambaye ameponywa kwa ukoma haimhitaji yeye leo aende Yerusalem kumtafuta kuhani wa kiyahudi ili akatoe sadaka yake ya njiwa wawili kwa alili ya uponyaji wake, basi twaona kuwa siku za leo hatuna madhabahu zinazoonekana, ambazo tunaziendea.
Kuwafundisha watu leo jambo kama hilo ni kuwadanganya na kuwanyang’anya maarifa ya Mungu. Ndiyo, kulikuwepo na Wayahudi ambao waliendelea kutoa matoleo kwenye madhabahu kwa mujibu wa sheria za Musa. Mwandishi anasema kwamba wao waliokuwa wakitumika katika madhabahu za aina hizo, hawakuwa na haki ya kuvila vitu vitokanavyo na madhabahu hizo ambazo waamini wameshiriki katika hilo.
“Tuna madhabahu ambayo wale waihudumiao ile hema hawana ruhusa kula vitu vyake. Maana wanyama wale ambao damu yao huletwa ndani ya patakatifu na kuhani mkuu kwa ajili ya dhambi, viwiliwili vyao huteketezwa nje ya kambi. Kwa ajili hii Yesu naye, ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa nje ya lango. Basi na tutoke tumwendee nje ya kambi, tukichukua shutumu lake. Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao. Basi, kwa njia yake yeye, na tumpe Mungu dhabihu ya sifa daima, yaani, tunda la midomo iliungamayo jina lake. (waebr 13:10-15).
Kimsingi, anachokisema mwandishi hapa ni kuwa waumini hawahusiki na lolote lihusulo vitu vya kiinje, wala taratibu za ibada za sheria za Musa. Paulo anasema kwamba tunapaswa kwenda inje ya kambi, ambayo inamaanisha hatuna lolote la kufanya kwa madhabahu na mahekalu ya sheria za kiyahudi ambapo dhabihu zilikuwa zikifanyika. Yesu tayari alishatuondoa mbali na mambo kama hayo kwa kifo chake pale msalabani. Nasi tunapaswa sasa kumfuata Yeye inje ya kambi. Hii inje ya kambi inamaanisha nini basi? Katika mstari ufuatao unaelezwa, “hapa hatuna mji udumuo, bali tunautafuta ule utakao kuja.” Mahali pale tulipoletwa si pale kwenye madhabahu ya dunia hii, bali ni pale kwenye uhalisia wa kiroho wa mbinguni, ndiyo maana Paulo anasema kuwa uwenyeji wetu upo mbinguni (Wafilipi 3:20). Tumezaliwa kutoka juu. Ndiyo sababu Paulo anatangaza kuwa Yerusalem ambao uko juu ni mama wa sisi sote! (Wagal.4:26). Mungu ametuinua sisi juu pamoja na mwanae Yesu Kristo ili kwamba tupate kuketi pamoja naye mahala mbinguni. Hapo ndipo mahala ambapo Mungu ametubarikia sote kwa baraka za kimbinguni (Waefeso 1:3; 2:6).
Kwa kule kutubatiza kwake kwa Roho Mtakatifu, Mungu ametufanya sisi tuwe ni watu wa kiroho (Yohana 4:24; 1 Wakor. 2:15; Wagalatia 6:1). Mungu hutufanya sisi kuwa ni nyumba yake ya kiroho tupate kutoa dhabihu za kiroho (1 Petro 2:5). Sisi tu hekalu la Mungu, ni maskani ya kuishi Mungu (Waefeso 2:22). Nasi tunao uweza wa kupaingia kwenye uwepo wake wakati wowote (Waebrania 10:19). Hatuhitaji kutumia masanamu au picha za kidini ili kutusaidia kuomba au kutusaidia kufikiria mambo ya kiroho. Kufanya hivyo ni kuabudu sanamu. Hakuna jengo la hekalu lililojengwa kwa matofali ambalo litaitwa ni ‘nyumba’ ya Mungu. Huo ni uongo na ni fikra za kiushirikina. Halikadhalika hakuna madhabu inayoonekana kwa inje wala hakuna meza ya mkate wa wonyesho au madhabahu ya uvumba au kitu kingine chochote cha aina hiyo. Basi sasa, kuunda mambo ya aina hiyo, ni kutokuielewa Injili na Agano Jipya – ni kuunda dini ya uongo inayoturudisha nyuma kwenye Agano la Kale ambalo mtume Paulo anatuonya kwa nguvu sana tusifanye katika nyaraka zake kwa Wagalatia.
Lakini, ebu turudi kwenye mstari uliopo kwenye Waebrania 13, ambapo mwandishi anasema kuwa, “Tuna madhabahu ambayo wale waihudumiayo ile hema hawana ruhusa ya kula vitu vyake.” Hapa mwandishi anasema kuwa tunayo madhabahu ambayo hao waifuatayo sheria ya Musa hawana ruhusa ya kula vitu vyake. Mwandishi anaiongelea madhabahu kama ni mahali tunapotumia kula, na hii ni kweli halisi, ni kweli kabisa. Ndiyo, wanyama walitolewa dhabihu juu ya madhabahu zile lakini makuhani walikula sehemu ya dhabihu ile. Walikuwa ni washirika wa madhabahu ile. Hicho ndicho mwandishi anacho kiongelea hapo. Kweli hii imetajwa pia katika 1Wakor. 9:13. Basi ebu niambie, ni madhabahu gani wewe unaitumia kuila dhabihu yake, na kitu gani unachokula! Jibu la swali hili lipo wazi. Yesu Kristo ndiye aliyetolewa awe dhabihu ya dhambi zetu, nasi tuwashirika naye, tunamla yeye, kama Yesu mwenyewe alivyosema katika Injili ya Yohana sura ya 6.
“Basi Yesu akawaambia, Amini amini nawaambieni, msipoula mwili wake mwana wa adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu, anao uzima wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho, maana mwili wangu ni chakula cha kweli na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Yeye aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu, hukaa ndani yangu nami hukaa ndani yake” (Yoh. 6:53-56). Sasa wengi wa wanafunzi wake hawakuelewa na maneno haya ya Yesu, waliliona jambo hilo ni gumu sana kulielewa hata wakarudi nyuma katika kumfuata Yesu.
Tunajua kuwa Yesu hapo alikuwa haongelei juu ya mwili na damu hii ya nyama kwa sababu damu na nyama haviwezi kuurithi ufalme wa Mungu. Ninaamini maneno haya ya Yesu yanaelezea ushirika wetu wa kiroho pamoja na yeye. Alikufa ili tushiriki maisha yake. Jambo hili limeelezwa kwa wazi kabisa na baadhi ya waandishi wengineo katika Agano Jipya, “tumefanywa kuwa washirika wake Yesu. . . Kristo ambaye ndiye uzima wetu. . .yeye aliyeunganishwa na Bwana ni Roho moja. . . ili kwamba upate kufanyika kuwa mshirika wa tabia ya kiUngu.” (Waebrania 3:4; Wakolosai 3:4; 1 Wakor 6:17; 2 Petro 1:4). Maisha haya ya kiroho ya kuwa na Yesu Krist ndani yetu (Wakolosai 1:27) yanaimarishwa na ushirika wetu pamoja na Bwana. Akizungumzia juu ya mkate na kikombe tukinywecho, mtume Paulo anasema, “Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate ni mmoja na sisi tulio wengi tu mwili mmoja, kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja (1Wakor. 10:16,17). Damu na mwili wake Yesu vyanena juu ya uhai wake. Inawakilisha uhai wake. Usifananishe na kunywa damu ya kimwili. Jambo hili halipo hapa. Kinachomaanishwa hapa ni kufanywa mshirika wa uhai wake, wa jinsi alivyo.
Ushirika huu pamoja na Yesu ni lazima liwe ni jambo linalofanyika kila siku katika kaisha yetu. Ni kama vile yunavyohitaji chakula na maji ili kusalimika kimwili, tunahitaji kuwa na muda kushirikiana pamoja Kristo, katika maombi, katika kumwabudu, katika upendo, katika mahusiano pamoja naye, ili kwamba tupate kusalimika kiroho, ili kwamba maisha yetu yapate kuimarishwa kiroho. Sikiliza Yohana asemavyo, “Tukisema ya kwamba twashirikiana naye tena tukienenda gizani twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli; bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu mwana wake yatusafisha dhambi zote. (1 Yoh. 1:6,7). Unaona, ni pale tu tunaposhirikiana na Yesu Kristo ndipo tunapoweza kutembea katika nuru -katika ushirika huo damu yake Yesu inatenda kazi katika kututunza sisi tuwe safi kutokana na dhambi. Kushiriki kwa mkate na kikombe chake kunawakilisha ushirika wake kiroho ambao inatupasa kushiriki mara zote katika maisha yetu. Yohana anasema katika sura ile ile, “Kweli ushirika wetu ni pamoja na Baba na Mwana”, na Paulo anatangaza kweli hiyohiyo katika 1Wakor 1:9, “Mungu ni mwaminifu ambaye muliitwa na yeye muingie katika ushirika wa mwawe, Yesu Kristo Bwana wetu.”
Ni katika ushirika huu tunabadilishwa na kufanywa upya katika roho ya nia zetu, kama Paulo asemavyo, “Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho.” (2 Wakor 3:18). Tunabadilishwa tufanane naye, kadiri tunavyo shirikiana naye, na ‘tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo’ – hii ina maana kwamba tunapaswa kumtafakari Yesu, kumwangalia Yesu, kumpenda Yesu, kuchukua muda tuwe pamoja na Yesu, na kupitia hayo kugeuzwa, kadiri tunavyojitoa wenyewe kwake kwa imani, utii na upendo. Na kwa mfano upi ambao tunabadilishwa? Tunabadilishwa kwa mfano wake Bwana!
Je unafahamu lolote kuhusu ushirika huo katika maisha yako?.
Kwa hiyo madhabahu anayoizungumzia katika Waebrania 13 ni mahala tunapojikabidhi wenyewe kwa Yesu. Ni sehemu tunaposhiriki pamoja naye, tunapofanyika kuwa washirika wa Yesu. Hapo ndipo mahala ambapo anashirikiana pamoja nasi, ndipo anapotubadilisha kiroho. Hapo ndipo mahala tunapomtolea dhabihu yetu ya sifa. Maisha yetu hutolewa kwa Mungu kwa shukurani, ibada na kujitoa.
Mungu anatupatia maelezo ya ajabu pamoja na vielelezo kuhusiana na jambo hili kwenye kitabu cha Kutoka 29, ambapo Mungu aliamuru kwamba kila siku asubuhi na jioni, mwanakondoo apate kutolewa kama sadaka ya kuteketezwa kwenye madhabahu ya dhabihu.
“Basi sadaka utakazozitoa juu ya madhabahu ni hizi; wana-kondoo wa mwaka mmoja wawili siku baada ya siku daima. Mwana-kondoo mmoja utamchinja asubuhi; na mwana-kondoo wa pili utamchinja jioni …iwe harufu nzuri, ni dhabihu ya kusongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto. Itakuwa ni sadaka ya kuteketezwa milele katika vizazi vyenu vyote mlangoni pa ile hema ya kukutania mbele ya Bwana; hapo nitakapokutana nanyi, ili ninene na wewe hapo. Nami nitakutana na wana wa Israeli hapo, na hiyo Hema itafanywa takatifu na utukufu wangu.” (Kutoka 29:38-43)
Hii hapa sio matoleo ya sadaka ya dhambi, bali ni matoleo yote ya sadaka ya kuteketezwa. Matoleo ya sadaka ya kuteketezwa yalikuwa ni matoleo yatolewayo kwa uchaguzi wa hiari ya aabuduye (Mambo ya Walawi 1:3), ilipaswa kuwa ni yenye harufu tamu/nzuri kwa Bwana. Ilikuwa inawakilisha kujitoa kukamilifu kwa waabuduo kwa Bwana. Angalia pale anachokisema Mungu mahali pale – hapa ndipo Mungu atakapokutana nasi. Anakutana na watu wake mahala pale ambapo watu wake wanakutana kwa hiari zao kutoa maisha yao pasipo masharti ya aina yoyote ile na pasipo kubakiza lolote. Lakini ebu nasi tukumbuke kuwa mwana kondoo inamwakilisha Yesu Kristo. Kwa maneno mengine, Mungu anatarajia kupata harufu ya manukato ya maisha ya mwanae kutoka katika maisha yetu ya kujitoa. Kama tulivyoona hapo ndipo mahali pa matoleo, na ni mahala pa ushirika na Bwana. Mahala ambapo maisha yetu yanafanyika kuwa ndiyo maisha Yake hapa duniani – na hiyo humpendeza sana Mungu.
Paulo anaelekeza kwetu juu ya ukweli huu wa ajabu katika nyaraka zake akisema, “Ila Mungu ashukuriwe, anayetushangiliza daima katika Kristo, na kuidhihirisha harufu ya kumjua yeye kila mahali kwa kazi yetu. Kwa maana sisi tu manukato ya Kristo, mbele za Mungu, katika wao wanaookolewa, na katika wao wanaopotea katika hao wa pili harufu ya mauti iletayo mauti; katika hao wa kwanza harufu ya uzima iletayo uzima. Naye ni nani atoshaye kwa mambo hayo?” (2 Wakor. 2:14-16).
Je, sasa unaona jinsi ya ajabu kabisa ambavyo neno la Mungu linavyokaa vizuri kwa pamoja? Bila shaka Paulo alifikiria Kutoka 29 alipoandika mistari hiyo. Na je, unaona jinsi Warumi 12 inavyokaa kwa makubaliano mazuri na eneo hili?
“Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.” (Warumi 12:1-2).
Sasa hapo ndipo tunapokutana na ukweli wa jambo hili. Haipo madhabahu inayoonekana wala hakuna haja. Hakuna mahali popote panapoonekana ambapo tunapaswa kupaendea ili kusogelea penye madhabahu. Wala hakuna kuhani wa kibinadamu hata mmoja ambaye tunapaswa kumwendea.
Tunapasa kuendelea kumtolea Mungu maisha yetu iwe dhabihu iliyo hai ili kwamba tupate kumjua Yeye, na kuyajua mapenzi yake na tuweze kubadilishwa ili tufanane na Kristo ili kwamba tupate kuwa harufu ya manukato ya Kristo hapa ulimwenguni. Hiyo ndiyo madhabahu yako, ni mahala ambapo unajitoa mwenyewe kwa Mungu. Mahala ambapo wewe unashirikiana na Mungu, na Mungu naye anashirikiana na wewe. Mahali ambapo nyakati za tabu yako na magumu, huchagui kuamini uongo wa shetani wala kuufuata mwili wako, wala kuchagua kufuata njia zako au mambo yako unayoyapendelea, bali kuchagua kwa hiari yako kujitoa mwenyewe kwa ukamilifu kwa Mungu, ili akuelekeze na kukuongoza na akujaze ndani yako kwake mwenyewe.
Neno la mwisho. Ye yote asemaye lazima ulete pesa yako YOTE (ya zaka au kadhalika) mahali ambapo washirika wanakusanyika jumapili kwa sababu madhabahu yapo pale pale tu, asema uongo. Anajaribu kufanya kanisa liwe kama biashara! Hamna mafundisho hayo katika kanisa la Bwana katika Agano Jipya. Kinyume chake, wazo hili linajaribu kuuharibu ukweli wa Mungu tuliousoma katika somo hili. Usinelewe vibaya, kwa ujumla ni jambo la kawaida kuleta pesa ya sadaka yetu ‘kanisani’, hata hivyo hamna fundisho kuwa lazima utoe pesa yako yote kwa kanisa. Wazo hili inakaribia ushirikina. Upendo wa Mungu mioyoni mwenu utatuongoza kutoa pesa yetu kwa ajili ya mahitaji aina ya mbalimbali.
Hayo kwa ufupi!
© David Stamen 2016 somabiblia.com
Kupakua makala hiyo, bonyeza link hapo chini: