RSS

KANISA TUKUFU LA YESU KRISTO TURUDI TENA KWENYE KUMHUBIRI KRISTO.

Na Carlos Ricky Wilson Kirimbai.                                                                                                                             kirimbai

Mpendwa wangu, ninakusalimu katika Jina lipitalo majina yote Yesu Kristo, Mwana wa Mungu Aliye Hai.

Kuna jambo limekuwa likinisumbua kwa muda sana ila leo nimeamka nalo kwa nguvu sana na nimeona tu kama mtoto wa Mungu na raia wa jumuiya ya familia ya Mungu katika nchi yangu nilisemee hili. Imekuwa ikinisumbua sana katika nchi yangu vile ambavyo tunazidi kuondoka katika msingi wa wito mkuu wa kumhubiri Kristo, kuihubiri Injili kwa kila kiumbe na kuwafanya mataifa kuwa wanafunzi.

Pamoja na ukweli usiyopingika kuwa kila mmoja wetu ameitwa tofauti na kuwekewa kusudi tofauti la Mungu ndani yake lakini ukweli mwingine usiyoepukika ni kwamba bila ya kujali wito wa kila mmoja mmoja binafsi na kusudi la Mungu ambalo amelibeba, haliwezi kuwa nje ya Agizo Kuu la Bwana Yesu la kuhubiri Injili kwa kila kiumbe na kuwafanya Mataifa yote kuwa wanafunzi.

Nakumbuka kwenye Luka wakati Yesu anazungumza na wale wanafunzi wawili, Cleopa na mwenzie ambaye hakutajwa jina wakiwa wanatembea pamoja kwenda Emau, aliwaambia kuwa kwa Jina Lake msamaha na ondoleo la dhambi utahubiriwa kwa mataifa yote.

Nachelea kusema kuwa tunazidi kuondoka kwenye Agizo hili la msingi.

Hapa nakumbushwa maneno ya thamani sana ya Mtume Paulo katika waraka wake kwa Wakorintho:

“Kwa sababu Wayahudi wanataka ishara, na Wayunani wanatafuta hekima; bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi; bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu. Kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu.”       (1 Korintho 1: 22 – 25).

Inaonekana wazi kuwa kulikuwa na makundi mawili ya watu ambao Paulo alikuwa akikutana nao katika huduma yake na akaona ni vema awasemee. Kuna wale ambao walikuwa wanataka ishara na kuna wale ambao walikuwa wanatafuta hekima. Yaani ipo kana kwamba kulikuwa na kundi la watu walikuwa wanakimbizana na miujiza na lingine walikuwa wanatafuta zaidi mafundisho.

Makundi yote haya mawili yalikuwa yakivutia kila mmoja kwake.

Wa ishara walikuwa wanaona ishara ndo za muhimu kwa sababu ya uhitaji ambao ulikuwepo katikati ya watu na wale wa hekima walikuwa wanavutia kwao maana walitamani kuona badiliko la kimaisha na kitabia kwa watu. Kwa hiyo kila mmoja akawa anatukuza kile alichokuwa anaamini. Paulo akasema kuwa wao walikuwa wanamhubiri Kristo aliyesulubiwa ambaye kwa wale wa ishara alikuwa kikwazo na kwa wale wa hekima alikuwa ni upuuzi.

Huhitaji kulithibitisha hili katika nchi yetu maana ukifungulia tu radio za kikristo utasikia tu anayehubiriwa sio Kristo bali watu, huduma zao na pako na neema zao.

Watu wanatukuza makusudi waliyobeba na kumsahau aliye wabebesha hilo kusudi.

Paulo anaendelea kusema kuwa kwa wale waitwao Kristo ni Nguvu ya Mungu na Hekima ya Mungu au kwa maneno mengine kama Kristo akihubiriwa, kwa wale ambao wanahitaji ishara atakuwa Nguvu ya Mungu kwao na kwa wale wanaohitaji hekima ya maisha atakuwa Hekima ya Mungu kwao.

Akatuonya kabisa kuwa japo wale wanaotafuta hekima wanaona kama haitoshi kumhubiri tu Kristo lazima wafundishe na vitu vingine na kuhubiri vitu vingine maana ipo kana kwamba Yesu ni upuuzi fulani hivi anawaambia kuwa upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu.

Tumeacha kumhubiri Yesu Kanisa limevamiwa na “Motivational Talk.”

Sasa motivational talk haina shida kama ikibaki kwenye uwanja wake maana hiyo ni hekima ya kibinadamu lakini tunapopunguza au kuacha kabisa kumhubiri Kristo alafu tunabaki na “Motivational Talks” tu basi tumeshaudharau msalaba sana.

Kanisani siku hizi tunawanukuu watu maarufu kuliko tunavyolinukuu Neno la Mungu na ni hekima sawa, bali ni hekima ya kibinadamu ila Kristo Ndiye Hekima ya Mungu.

Kwa wale watakao ishara ndo imekuwa mbaya zaidi.

Tumehamia kwenye kutukuza maji ya upako, mafuta ya upako, sabuni za upako, chumvi ya upako, vitambaa na nguo za upako na kila aina ya vitu vya upako mpaka Kanisa Tukufu la Kristo linaonekana kama kituo cha waganga wa kienyeji maana mambo ambayo tunaelekezwa Kanisani sasa hayana tofauti kabisa na mambo ambayo watu wanaambiwa wakienda kwa waganga wa kienyeji.

Kanisani siku hizi wala hatuoni aibu tena kutoza sadaka kwa ajili ya huduma ambazo kimsingi kwa mujibu wa neno zinatakiwa kutolewa bure. Sijui tumejifunzia wapi hili maana kwenye maandiko halipo.

Mahali ambapo unaweza kwenda na kuzikuta hizi ni kwa waganga wa kienyeji.

Bila aibu Kanisani tumevamiwa na mambo ya kusafisha nyota na kuwadanganya watu kuwa nyota zao zinafifishwa, zinaibiwa, zinazuiliwa na tunaanza kutoa huduma za kusafisha nyota za watu, kuzirudisha nyota zilizoibiwa na mambo yanayofanana na hayo. Hivi vitu kwenye maandiko huvikuti ila ukienda kwa waganga wa leo utavikuta na inaninfanya nijiulize hivi Kanisa la Kristo tumejifunzia wapi haya mambo.

Kimsingi Kanisa Tukufu la Yesu Kristo linakwazika na kumhubiri Kristo, linafanya tu kumtaja kidogo asijisikie vibaya lakini kwa kweli tunahubiri vitu vingine na sio Kristo. Tunatafuta kwa darubini viandiko vya kuhalalisha upuuzi ambao tunaufanya huku tukiwa tumemwacha kabisa kumhubiri Kristo. Paulo kwa hili anasema kuwa udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya mwanadamu.

Ni kweli watu wana mahitaji sana katika zama zetu na huu uhitaji wa watu hautapungua utazidi kuongezeka maana Shetani ametupwa kwetu mwenye hasira nyingi akijua kuwa wakati wake ni mchache.

Lakini suluhisho la hawa watu sio hivi vitu tunavyovifanya bali ni Kristo Naye amesulubiwa.

Tukirudi kumhubiri Kristo na nguvu ya msalaba kimsingi tumerudi kwenye Nguvu za Mungu na kwenye Hekima ya Mungu na watu watatendewa makuu na Nguvu za Mungu na kubadilishwa maisha kitabia na kimwenendo na Hekima ya Mungu. Paulo katika kuendelea kuwaandikia Wakorintho aliandika:

“Basi, ndugu zangu, mimi nilipokuja kwenu, sikuja niwahubiri siri ya Mungu kwa ufasaha wa maneno, wala kwa hekima. Maana naliazimu nisijue neno lo lote kwenu ila Yesu Kristo, naye amesulibiwa.”    (1 Korintho 2:1, 2).

Paulo alipoenda kwa Wakorintho, hakuenda kuwahubiri siri ya Mungu kwa ufasaha wa maneno wala kwa hekima. Anasema kwanini.

Aliazimu asijue neno lolote kwao ila Yesu Kristo naye amesulubiwa.

Wokovu wa mwanadamu kutoka kwenye dhambi na kazi zote za shetani upo ndani ya Yesu na kazi Yake ya pale msalabani na kama Yesu akihubiriwa na kazi ya msalaba nayo ikahubiriwa italeta badiliko la maisha kitabia na kimwenendo kwa watu na pia itawatoa watu katika vifungo na mateso bila kuongezea na vitu vingine ambavyo kimsingi huondoa macho ya watu kwa Yesu na kuyaweka juu ya hivyo vitu na wanaovitumia.

Kuna haja kubwa ya kuirudia tena Injili ya kweli ambayo inamwinua Yesu na kazi ya msalaba.

Tusiionee haya Injili maana ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye.

Watu wakiiamini Injili itawaletea wokovu na kila kazi ya adui kinyume nao.

Kuna matamko ya ajabu sana Yesu aliwahi kuyatoa alipokuwa hapa duniani:

“Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi. (Mathayo 11:28-30).

Yesu aliwaita watu wanaosumbuka na kulemewa na mizigo waende Kwake naye atawapumzisha.

Yesu hajabadilika, ni Yeye yule, Jana leo na hata milele.

Hata leo anawaita watu wanaosumbuka na kulemewa na mizigo waende Kwake.

Turudi kwenye kuwaelekeza watu kwa Yesu na sio kwetu na wala sio kwenye “vitu vya upako.”

Watu wanahitaji kupumzika na mateso, maumivu na masumbufu ndiyo lakini ili wapumzike lazima waende Kwake awezaye kuwapumzisha Naye ni Yesu.

Turudi tena kuwaelekeza kwa Yesu.

Turudi tena kwenye kumhubiri Yesu.

Turudi tena kwenye kumtangaza Yesu.

Yesu akasema hao watu wanaosumbuka na kulemewa na mizigo watwae nira Yake na kujifunza kwake maana Yeye ni mpole na mnyenyekevu wa moyo nao watapata raha nafsini mwao maana taabu walizokuwa nazo zimewajia kwa sababu ya namna walivyokuwa wanaishi.

Namna walivyokuwa wanaishi ilifungua mlango kwa adui kuingia na kuwatesa.

Kwa hiyo sio tu anaweza kuwapumzisha na shida, maumivu na mateso waliyo nayo lakini kama wakiwa tayari kubadilika maisha yao na kumfuata na kujifunza Kwake atawahakikishia raha. Anawahakikishia kuwa nira Yake ni laini na mzigo Wake ni mwepesi.

Wakati ndugu wanne walipomleta kwa Yesu mwenzao aliyekuwa amepooza na Yesu alipoiona imani yao alimwambia yule mwenye kupooza dhambi zako zimesamehewa ndipo akamwambia jitwike godoro lako uende.

Hatuna namna ya kumhubiri Kristo pasipo pia kuhubiri msalaba. Msalabani hapo ndipo tatizo la msingi la mwanadamu liliposhughulikiwa. Dhambi ndo tatizo la msingi la mwanadamu ambao ndo mlango ambao unafungua kwetu kila aina ya mateso, masumbufu, shida, mizigo na nira. Msalaba wa Yesu ndo dawa ya shida ya msingi ambayo ikitatuliwa mengine yote yanaisha.

Nitoe tu mfano rahisi.

Mtu akiwa na malaria inaweza ikajidhihirisha kwa homa, maumivu ya kichwa, maumivu ya viungo, kuuma na kuvurugika kwa tumbo, kukohoa kusiko katika nk. Hizi zote ni dalili za tatizo la msingi ambalo ni malaria. Huna namna unaweza kushughulikia ipasavyo hizi dalili bila ya kushughulika na tatizo la msingi. Zipo dawa za kushughulika na hizo dalili zinazojidhihirisha lakini nguvu yake ikiisha mwilini hizo dalili zinarudi kwa sababu tatizo la msingi halijashughulikiwa. Kwenye lugha ya Sayansi Tiba wanaita Primary Infection na Secondary Infection. Ukishughulika na Secondary Infection ambayo ndo hizo dalili unakuwa hujatatua tatizo vya kudumu mpaka ushughulike na Primary Infection ambayo ni shida ambayo inasababisha hizo dalili.

Tunapomhubiri Kristo na msalaba tunaachilia nguvu ambayo inashughulika na vyote viwili, Primary Infection ambayo ni dhambi na Secondary Infection ambayo ni hizo shida ambazo zinajionyesha katika maisha ya watu.

Kuna siku Yesu alienda juu mlimani kuomba pamoja na wanafunzi wake watatu, Yakobo, Yohana na Petro. Akiwa huko juu mlimani huku kuna baba mmoja akamleta mtoto wake aliyekuwa anateswa na kifafa kwa wanafunzi wa Yesu lakini wakashindwa kumsaidia.

Yesu aliposhuka kutoka huko juu mlimani na wale wanafunzi aliyokwenda nao akakuta kama kuna zogo na alipotafuta kujua shida ni nini ndo akajua kilichojiri.

Napenda sana kitu Yesu alichofanya. Akasema, “MLETENI HUKU KWANGU.”

Wapendwa turudi kwenye kumhubiri Yesu na msalaba Wake. Tuwaelekeze watu kwa Yesu na kwa msalaba Wake ili wakasaidiwe matatizo yao na tatizo la msingi ambalo ndo kilisababisha shida walizonazo.

Nimalize kwa kunukuu maneno ambayo Yesu alimwambia mtu ambaye alimponya na shida aliyokuwa nayo iliyomtesa kwa miaka mingi sana:

“Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi.” (Yohana 5: 14).

Yesu waziwazi alimwambia huyu ndugu ambaye alikuwa amelala bila msaada kwenye birika la Bethzatha kwa muda wa miaka 38 mpaka pale Yesu alipokuja kumsaidia, kuwa ASITENDE DHAMBI TENA LISIJE LIKAMPATA JAMBO LILILO BAYA ZAIDI.

Watu wanamhitaji Yesu na wanauhitaji msalaba Wake maana shida walizo nazo zinasababishwa na jambo ambalo ni Yesu tu na msalaba wake ndo vitatoa suluhisho la kudumu kwao.

Unaweza kupona kabisa malaria lakini usipokuwa makini kuhakikisha nyumba yako madirisha yana nyavu za kuzuia mbu kuingia, na kutumia neti vitandani au kupiga dawa ya kuua mbu ndani ya nyumba na kufanya usafi wa mazingira wa kuharibu mazalio ya mende utakuwa kila siku unapata malaria.

Baada ya kufunguliwa watu na kuponywa ni muhimu sana wapate badiliko la maisha kitabia na kimwenendo na hilo linawezakana tu kama tukimhubiri Kristo naye amesulubiwa.

TURUDI KUMHUBIRI YESU NAYE KASULUBIWA.

TUACHE HAYA MAVITU MENGINE AMBAYO TUMEYATUKUZA SANA KATIKA ZAMA HIZI.

TURUDI KUMHUBIRI KRISTO NAYE KASULUBIWA.

MUNGU AWABARIKI SANA.

Na Carlos Ricky Wilson Kirimbai, 2016.  Senior Pastor Manna Tabernacle Bible Church. Dar Es Salaam

 

4 responses to “KANISA TUKUFU LA YESU KRISTO TURUDI TENA KWENYE KUMHUBIRI KRISTO.

 1. Anonymous

  February 5, 2018 at 6:43 pm

  Nimefulahi na mafundisho yako Mungu akubaliki naomba namba yako tuwasiliane

   
  • dsta12

   February 5, 2018 at 6:52 pm

   Nipe namba yako, rafiki.

    
   • Elibariki Mchau

    June 1, 2018 at 8:45 pm

    Barikiwa Pastor, nimependa somo ni nzuri ni Msaada kwa watumishi na kanisa pia . Namba yangu ni 0677708651

     
 2. Elibariki Mchau

  June 1, 2018 at 8:43 pm

  Barikiwa Pastor, nimependa somo ni nzuri ni Msaada kwa watumishi na kanisa pia

   

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

 
%d bloggers like this: