RSS

Maana na Tafsiri ya Ndoto

MAANA NA TAFSIRI YA NDOTO: MAMBO YA HATARI SANA. NI WENGI WANAOKOSA JUU YA JAMBO HILI SIKU HIZI.

Biblia inatufundisha kwamba Mungu anaweza kuongea na nabii wake kupitia ndoto. (Hesabu 12:6).

Tutaangalia mistari ambayo inatuonyesha vipi Mungu alivyoongea na watu kupitia ndoto.

1. Mungu aliongea na watu MOJA KWA MOJA kupitia ndoto juu ya MPANGO AU MAPENZI YAKE, naye aliyeota ndoto ALIJUA MARA MOJA maana ya ndoto yake – alijua alikuwa Mungu aliyeongea naye. huyu hakuhitaji mwingine atafsiri ndoto yake! Tunaona hayo katika mistari ifuatayo: Mwanzo 20:3, 28:12, 31:11, 31:24, 37:6, 42:9; (Waamuzi 7:11-15); 1 Wafalme 3:5; Mathayo 1:20, 2:12,13,19, 22; (Matendo 16:9).

Mifano hiyo hapo juu haihusu moja kwa moja mada yetu kwa sababu ndoto hizo HAZIKUHITAJI MWINGINE atafsiri maana ya ndoto. Yule aliyeota ndoto ALIJUA MWENYEWE maana ya ndoto yake naye alijua alikuwa Mungu aliyeongea naye.

2. Kutimiza mapenzi yake kwa ajili ya taifa lake, au kutimiza mpango wake katika wafalme wa dunia, Mungu aliwapa watu wasioamini (Farao, na mkuu wa wanyweshaji na mkuu wa waokaji wa Farao, na Nebukadreza ) ndoto, naye aliwapa watumishi wake (Yusufu na Danieli) uwezo wa kutafsiri ndoto hizo (Mwanzo 40:5; Mwanzo 41:15,16; Daniel 2:36, 4:19). Kwenye mifano hiyo tunaona pia Mungu alifanya hivyo kuinua watumishi wake katika nchi walizokaa, yaani, kumuinua Yusufu na Danieli na kutimiza mapenzi yake wa ajili ya watu wake. (Yusufu aliweza kutafsiri ndoto ya mkuu wa wanyweshaji na mkuu wa waokaji wa Farao siyo kwa sababu ilikuwa kwa ajili yao, lakini kwa sababu ilihusu mapenzi ya Mungu kwa ajili ya Yusufu na kwa ajili ya mpango wa Mungu kwa ajili ya Israel! Mungu alitaka kumuinua Yusufu katika nchi ya Misri.)

Tunaona watu wawili katika Biblia, yaani Yusufu na Danieli, walioweza kutafsiri ndoto ya mtu mwingine.

Walitafsiri ndoto za nani? Ndoto za wasioamini. Je, zilikuwa ndoto za kawaida? HAPANA. Ndoto hizo zilitokana na Mungu. Na kila ndoto ilihusu mambo makuu AMBAYO MUNGU MWENYEWE ALIKUWA ANATAKA KUYATENDA kwa watu duniani. Bila kufikiri sana tunaweza kutambua mifano hiyo ni muhimu sana nayo kimsingi inahusu mapenzi au mpango wa Mungu kwa ajili ya watu wake au inahusu mpango Wake juu ya wafalme wa duniani.

Hapo juu tunayo mistari yote katika Biblia ambapo watu waliota ndoto pamoja na tafsiri yake.

Tunaona ndoto zote hapo juu ni ndoto za kipekee na maalum. Siyo ndoto za kawaida, za kila siku – zinayo tafsiri inayohusu mapenzi ya Mungu duniani.

Katika kila mfano tunaona kwamba muotaji ndoto…

– Alipewa moja kwa moja na Mungu. Yaani, haikuwa ndoto ya kawaida, ya kila siku. Ndoto zote hizo zilitokana na Mungu au zilisababishwa na Mungu na zilihusu tekelezo la mapenzi yake duniani.

– Alijua maana yake moja kwa moja kutoka kwake Mungu mwenyewe, au…

– Mungu alitumia mtumishi wake kutafsiri ile ndoto ili kutimiza mpango wake kuhusu watu wake au kuhusu mpango wake juu ya wafalme wa dunia.

Je, ndoto zako za kila siku ni za namna hiyo? Je, ndoto zako nyingi za kila siku zinatokana na Mungu kwa ajili ya mapenzi na mpango Wake duniani – na je, kwa hiyo unahitaji mtumishi wa Mungu (kama Yusufu) atafsiri ndoto zako nyingi?

Kwa maneno mengine, ndoto hizo za hapo juu (ambazo zilihitaji tafsiri) hazikuwa ndoto za kawaida, za kila siku. Ndoto hizo zote hazikuhusu maisha ya mtu binafsi tu! Zilikuwa ndoto za pekee au ndoto maalum. Ndoto zote za hapo juu zilitokana na Mungu! ZILIHUSU MAPENZI AU MPANGO WA MUNGU DUNIANI JUU YA WAFALME, HASA KUHUSU MPANGO WAKE KWA AJILI WATU WAKE.

Kwa ujumla, watu wanaota ndoto karibu kila usiku, hata wewe na mimi. Hizo ni ndoto za kawaida, za kila siku. Ndoto zetu kwa ujumla hazifanani na mifano tunayosoma kwenye mistari ya hapo juu. Namaanisha hivi, katika Biblia nzima HAUPO HATA MFANO MMOJA unaotuonyesha kuwa mtu fulani alikwenda kwa mtumishi wa Mungu apate tafsiri ya ndoto yake ya kawaida, yaani, apate tafsiri ya ndoto yake kwa ajili yake binafsi tu! Katika Biblia kila ndoto iliyotafsiriwa na mtumishi wa Mungu ilihusu mpango wa Mungu kwa ajili ya watu wake au kuhusu mpango wa Mungu kwa ajili ya falme za dunia! Katika Biblia nzima haupo hata mfano mmoja ambapo mtumishi wa Mungu alitafsiri maana ya ndoto ya kawaida ya mtu! Katika Biblia nzima haupo hata mstari mmoja unaotufundisha kuwa ipo karama ya Mungu ambayo inamwezesha mtu kutafsiri maana ya ndoto ZA KAWAIDA za watu, kana kwamba anaweza kutafsiri ndoto mbalimbali za kila mtu!

Kulinganisha Yusufu au Danieli walilotenda katika huduma yao ya kutafsiri ndoto za Farao au Nebukadreza (au hata za watumishi wa Farao) na ‘huduma’ ya mtu fulani siku hizi anayedai kuwa na kipawa cha kutafsiri ndoto za kila siku za watu kwa ujumla ni jambo la kupotosha neno la Mungu! Ni udanganyifu.

Wapo watu wanasema wanacho kipawa kinachotokana na Mungu kutafsiri maana ya ndoto ZA KAWAIDA, ZA KILA SIKU. Wanadai wanaweza kukuambia maana ya ndoto zako. Wanadai wanaweza kutoa maana ya kiroho ya ndoto zako ili kukusaidia katika maisha yako ya kiroho! LAKINI KATIKA BIBLIA NZIMA HATUNA MFANO HATA MMOJA WA JAMBO HILI. KATIKA BIBLIA NZIMA HATUWEZI KUONA KIPAWA HIKI. Hili ndilo jambo la ushirikina na udanganyifu tu.

Hamna ‘kipawa cha kutafsiri ndoto za kila siku’ katika Biblia kinachohusu watu wa Mungu. Wapi mtumishi wa Mungu katika Biblia alisema – kama wadanganyifu wa siku hizi wanavyosema – “Ukiota kitu chako, kimeibiwa au kuvunjika – maana yake, ulinde moyo wako, kuna roho ya uharibifu.” NA WANADAI TAFSIRI HIVYO INAHUSU WATU WOTE WANAOOTA NDOTO HIYO! Hamna mstari hata mmoja katika Biblia ambapo mtumishi wa Mungu anafanya kazi hiyo. Au sema, ni wapi? Kwa kweli tukiamini mambo hayo hatujapoteza ufahamu wetu wa kiroho tu, bali nguvu ya giza imeshatufanya tuwe vipofu juu ya mambo yaliyo wazi kabisa!

Kwa tafsiri yao wanachochea HOFU mioyoni mwa watu kwanza, ndipo wanadai kutoa ushauri wa Mungu ili tujilinde! Sikiliza. Kama fulani akikuambia, “Ukiota baiskeli yako imevunjika, ina maana kuna roho ya uharibifu”, huu ni ushirikina, ni uongo, haijalishi nani aliyesema. Lakini kama wewe unaamini hayo, unakosa, unafanya dhambi mbele ya Mungu. Unatafuta ‘ujuzi wa kiroho’ juu ya maisha yako ya kiroho nje ya neno la Mungu. (Soma Warumi 8:31-39; 1 Petro 3:13). Kama ukiamini uongo huo ina maana unaacha kuishi kwa neno la Mungu na unafungua mlango kwa Ibilisi kudhuru maisha yako! Kwa njia gani Ibilisi anaweza kudhuru maisha yetu ya kiroho? Anataka kufanya hivyo kwa kutudanganya ili tuamini uongo wake! Alifanya hivyo mwanzoni kwa Hawa, naye atajaribu kufanya hivyo kwako. Unaona, yeye anayedai kutabiri ndoto yako kwa ajili ya ‘faida’ yako, kwa kweli ni yeye anayekupeleka sehemu ambapo unaacha usalama na ulinzi wa Mungu (kwa kuliacha neno lake) na kujiweka sehemu ambapo Shetani anaweza kudhuru maisha yako ya kiroho – bure, na bila maana yoyote!

Kwa kawaida, siku hizi watu wanakwenda kwa ‘psychologists’, au kwa wapagani wanaodai wanacho kipawa cha pekee kuingia katika ulimwengu wa kiroho, kwa wapiga ramli na hata kwa wachawi kwa huduma hiyo. Kusema kazi hiyo ni kipawa cha Mungu ni kosa kubwa sana.

Pia, wanadai wanaweza kutabiri litakalotokea katika maisha yako punde hivi, kwa kusema, kwa mfano, ‘kama ukiota hivi au hivi, inamaanisha utabarikiwa sana katika maisha yako.’

Kazi hii ni kama kazi ya kupiga ramli. Kama ukijishughulisha na jambo hili, ni sawasawa kama umekwenda kwa mbashiri, muaguzi au mchawi. Katika Biblia pia tunasoma juu ya watu waliodai wanacho kipawa cha kutafsiri ndoto za watu. Wapagani walitumia njia zisizo halali mbele ya Mungu ili waweze kuelewa linalotokea katika maisha yao, na kutabiri yatakayotokea katika maisha yao. Walitaka kutumia ‘ujuzi huo wa siri au wa pekee’ kupanga maisha ya watu au kuharibu adui zao. Walifanya hivyo kwa kutazama bao, kwa kupiga ramli, kwa tumia wabashiri na waaguzi au wachawi, kama tunavyosoma katika Biblia. Hayo yote ni dhambi na uasi mbele za Mungu, yaani, watu wanapenda kutumia na kutegemea njia zingine kupanga maisha yao badala ya kumtegemea Mungu tu. Wanataka kupata ‘ujuzi wa pekee’ juu ya maisha yao kupitia wabashiri au wapiga ramli badala ya ‘kuishi kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.’ Hawataki kuishi kwa neno Mungu alilolidhihirisha, wanataka kitu kingine, kitu zaidi, na udadisi huo uliwaongoza dhambini.

Mungu aliwaonya watu wake, taifa la Israel, wasifuate njia za mataifa, ya wapagani’,

“Maana mataifa haya utakaowamiliki huwasikiliza wanaoshika nyakati mbaya na kutazama bao; bali wewe, Bwana, Mungu wako, hakukupa ruhusa kutenda hayo.” (Kumbu.18:14.)
Maisha ya wapagani waliongozwa na mambo ya uchawi na kadhalika, kama kupiga ramli na kwenda kwa wabashiri. Lakini baadaye Waisraeli wenyewe walimwacha Mungu nao walifuata njia ya wapagani. Lakini Mungu aliwakemea watu wake walipofanya hivyo,

“Lakini, katika habari zenu, msisikilize manabii wenu, wala wabashiri wenu, wala ndoto zenu, wala watambuzi wenu, wala waganga wenu…” (Yeremia 27:9).

“Kwa maana vinyago vimenena maneno ya ubatili, nao waaguzi wameona uongo; nao wameleta habari za ndoto za uongo, wafariji bure; kwa sababu hiyo waenda zao kama kondoo, wateswa, kwa sababu hapana mchungaji.” (Zekaria 10:2).

Ni nani aliyekuwa na watu maalum waliodai wanaweza kutafsiri/kutabiri ndoto ZA KILA SIKU? Wapagani tu! (Mwanzo 41:8; Danieli 2:2, “Ndipo mfalme akatoa amri kuwaita waganga, na wachawi, na wasihiri, na Wakaldayo, wapate kumweleza mfalme ndoto zake.”).

Tunapaswa kulifuata neno la Mungu, na kufundishwa mambo yaliyoandikwa kwenye Biblia TU juu ya maisha yetu ya kiroho, na tusitafute ‘ujuzi wa siri’ kutoka kwake anayedai anaweza kutafsiri ndoto zetu. Kwa nini waumini wengine wanapenda sana kusoma na kumwamini yule anayedai anaweza kutoa maana ya ndoto zao? Ni kwa sababu NENO LA MUNGU HALITOSHI KWAO! Wanachoshwa na neno la Mungu. Badala ya kuishi kwa neno la Mungu, kuliamini neno la Mungu na kulitii neno la Mungu, wanaitafuta njia rahisi, njia nyingine kuboresha maisha yao. Lakini hayo yote ni bure, ni dhambi. Wao hawajali neno la Mungu. Au wamejiruhusiwa wadanganywe.

Ukisema, “Lakini mimi nimesaidiwa kupitia ‘huduma’ hiyo!” Kweli? Ni wengi pia wanaoweza kusema, “Mimi nimesaidiwa na mchawi wangu!” Sasa je, kama ndio hivyo, tuende kwa mchawi akatusaidie katika maisha yetu ya kiroho?

Mungu ndiye ajuaye mambo yajayo naye alijua watu wake watachoshwa na neno lake, akisema, “Na wakati watakapokuambia tafuta habari kwa watu wenye pepo na kwa wachawi walio na ndege na kunong’ona je! haiwapasi watu kutafuta habari kwa Mungu wao? Je, waende kwa watu waliokufa kwa ajili ya watu walio hai?” (Isaya 8:19).

Katika Biblia nzima hamna kipawa cha kutafsiri, cha kutabiri ndoto za kila siku za watu, ila ni kazi ya ushirikina, ni tendo la kutokumwamini Mungu na neno Lake.

Tumfuate Bwana Yesu katika maisha yetu ya kila siku. Na tuishi kwa neno la Mungu. Hatuhitaji mwingine kutafsiri ndoto zetu za kila siku. Tukimpenda na kumtii Bwana wetu Yesu Kristo katika maisha yetu, Yeye Mwenyewe ndiye atakayeweka kwako usalama mchana na usiku!

Neno la Mungu linatangaza, “Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema?” (1 Petro 3:13).

© David Stamen  2016   somabiblia.com

 

Comments are closed.

 
%d bloggers like this: