RSS

Kusudi la Majaribu

Je, baada ya kubatizwa kwake, Yesu aliongozwa na nani nyikani? Neno la Mungu linatufundisha aliongozwa na ROHO MTAKATIFU nyikani. Aliongozwa nyikani kwa sababu gani? Biblia inatusema kwa wazi! “Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ILI AJARIBIWE NA IBILISI.” (Math.4:1).

Na Luka anasema, “Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu…akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani, akijaribiwa na Ibilisi.”

Basi, Yesu alikuwa hali AMEJAA ROHO alipoongozwa na Roho Mtakatifu nyikani ili ajaribiwa na Ibilisi, lakini baada ya kujaribiwa na shetani, Biblia inasema kwamba, “Yesu akarudi KWA NGUVU ZA ROHO, akenda Galilaya…” (Luka 1:1-14).

Aliingia nyikani amejaa Roho, alitoka kwa nguvu za Roho!

KUSUDI la majaribu ni TUKUE katika maisha ya kiroho yetu, katika imani, haki, utakatifu na katika upendo wetu kwake Mungu – tuchague yaliyo mema na tukatae yaliyo mabaya; tuchague Yesu na tujikane wenyewe; tumpendeze Mungu badala ya kutupendeza wenyewe, siku hadi siku katika mambo yote. Kwa njia hiyo tunakua katika Kristo Yesu na tunaanza kuishi kwa nguvu za Roho. Tunaweza kuanzisha vizuri, lakini tunaendeleaje?

Tutapita majaribu. Lakini majaribu siyo adui yetu. Tatizo lenyewe siyo tatizo. Tatizo kwa dhati linatokeza usipojidhughulisha na tatizo kama unavyopaswa! Ndiyo maana Yakobo anasema,

“Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni FURAHA tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. SABURI NA IWE NA KAZI KAMILIFU, MPATE KUWA WAKAMILIFU na watimilifu bila kupungukiwa na neno.” (Yakobo 1:2-4).

Mungu anataka tuwe na mtazamo wa namna huo.

Je, unafikiri Bwana alishtuka kuona kwamba Ibilisi aliingia bustani ya Edeni? Sidhani! Mungu alimpa Ibilisi nafasi kuingia bustani ili awajaribu Hawa na Adamu, vile vile alivyomruhusa Shetani kumjaribu Yesu nyikani. Sikiliza neno la Mungu kwao watu wake jangwani, “Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze, KUKUJARIBU, KUYAJUA YALIYO MOYONI MWAKO, kwamba utashika amri zake, au sivyo. Akakutweza, AKAKUACHA UONE NJAA, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; APATE KUKUJULISHA ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana.” (Kumbu.8:2,3).

Unaona? KWA KUSUDI Mungu aliwaacha watu wake waone njaa! Kwa nini? Kuyajua yaliyo moyoni mwao, kama wangeshika amri zake au sivyo; kama wangemwamini Mungu au sivyo; kama wanampenda Mungu KULIKO MAMBO YOTE MENGINE, haijalishi yanayotokea au yasiyotokea katika mazingira yao! Na Bwana Yesu alipita jaribu lilelile nyikani naye hakunung’unika – alinukuu mstari uleule ya Kumbu.8:3! Aliishi KWA NENO LA MUNGU! Alisimama kwa neno la Mungu; alikataa kushawishiwa na maongo ya Shetani; hakulalamika ili Mungu amwondoe Shetani au mazingira yale ambyo MUNUG MWENYEWE ALIPANGA KWA AJILI YAKE MAJIRA ILE! Kwa hiyo Biblia inasema, “Basi mtiini Mungu (au umnyenyekee Mungu). Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.” (Yakobo 4:7).

Inawezekana watu wengi hawatumbui mkono au uongozi wa Mungu katika maisha na mazingira yao, katika majaribu yao. Wanalalamika kana kwamba Bwana amewaacha au wanapenda kumlaumu Shetani badala ya kumpinga! Badala ya kujitoa kwake Mungu na kujikana, wanachagua kujipendeza, kujifurahisha au kujihurumia! Badala ya kupinga maongo ya Ibilisi na kuizima mishale yote yake yenye moto, wanalalamikia mazingira yao tu.

Tatizo katika bustani ya Edeni, tatizo katika jangwa la Sinai kimsingi halikuwa shetani, halikuwa upungufu wa vitu au chakula – lilikuwa kutokuamini na kutokutii ya Adamu na Hawa, ya Waisraeli! Walilalamika na kushindwa NA MAMBO YALEYALE AMBAYO MUNGU MWENYEWE AMESHAYAPANGA KWA AJILI YAO ILI WAKUE – katika maisha ya kiroho yao – KUPITIA YAO NA KUIMARISHIWA NAYO!

Ndiyo maan imeandikwa, “na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi, na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini; na tumaini halitahayarishi…” (Warumi 5:3-5). Lengo la dhiki na majaribu ni kuwa tukue katika maisha ya kiroho yetu.

Miaka mingi iliyopita nilipofundisha katika kanisa fulani huko Dar Es Salaam juu ya Warumi 5:3, mtafsiri wangu alinidakiza akiniambia, “Watu hawapendi kusikiliza ujumbe wa namna huo!” Kumbe! Watu wa Mungu huchukizwa na neno Lake! Na sisi? Lakini hata mfalme Daudi katika Agano la Kale alikiri, “Umenifanyizia nafasi wakati wa shida…” (Zaburi 4:1).

Na neno hili lenye maana sana liingie mioyoni mwetu, “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo KAWAIDA ya wanadamu; ILA MUNGU NI MWAMINIFU; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.” (1 Wakor.10:13). Hasemi ataliondoa jaribu lile haraka haraka. Anasema ‘pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea’, basi tukumbuke Yakobo alilosema, “Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno.”

Lakini Mungu hajatuacha peke yetu! Neno la Mungu linatutia moyo kwa kutufundisha,

“Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.” (Waebr.4:14-16).

Kwa hiyo tusishangae ila tuyatafakari na kuyapokea maneno ya Petro aliposema, “Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali; ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, AMBAYO INA THAMANI KUU KULIKO DHAHABU ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa KWA MOTO, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, KATIKA KUFUNULIWA KWAKE YESU KRISTO.

Mungu atubariki na neno Lake.

© David Stamen 2017   somabiblia.com

UNAWEZA KUDOWNLOAD SOMO HILI  KWA KUBOFYA LINK IFUATAYO:     KUSUDI LA MAJARIBU   

 

 

 

Comments are closed.

 
%d bloggers like this: