NIDHAMU ZA MTUMISHI WA MUNGU
“Hata mtu akishindana katika michezo HAPEWI taji, asiposhindana KWA HALALI. Yampasa mkulima mwenye taabu ya kazi kuwa wa KWANZA wa kupata fungu la matunda (au ‘…kuwa wa kwanza KUONJA matunda yale…’). Yafahamu sana hayo nisemayo, kwa maana Bwana atakupa akili katika mambo yote.” (2 Tim. 2:5-7).
Ujuzi hautoshi katika huduma. Ujuzi tu hautawatosheleza wasikilizaji. Haifai mkulima kuuza matunda yake kwa wengine pasipo kwanza yeye mwenyewe kuyala matunda ya kazi yake ili atambue kama yanafaa au la! Kama matunda ya maisha yako hayafai, utawafundishaje wengine? Haifai kuwalisha watu wa Mungu na ‘ujuzi’ wangu tu; kuwalisha na fikira na nadharia (ideas and theories) tu pasipo kwanza neno la Mungu kutimizwa katika maisha ya binafsi yangu kwa kadiri ipasavyo! Lazima mimi mwenyewe kwanza niwe ninaishi maisha ya Kristo kadiri ipasavyo. Matunda ya kiroho ambayo ni kupitia Yesu Kristo lazima yatokeze katika maisha yangu kwanza ili nisiwalishe watu wa Mungu na ujuzi tu! Hapo hamna njia ya mkato (short cut) katika huduma ya Bwana – au hata katika maisha ya Mkristo. Yesu mwenyewe alijaribiwa jangwani! Aliongozwa na Roho nyikani hali AMEJAA Roho Mtakatifu ili ajaribiwe na Ibilisi, lakini tutambue kuwa baada ya siku arobaini akarudi Galilaya kwa NGUVU za Roho! Hali kadhalika, lazima sisi sote tupite au kutembea katika njia ya nidhamu ya kiroho na majaribu. Tusiposhindana kwa halali, hatupewi taji. Na maisha hayo ya nidhamu ya kiroho na kimwili hayaishii baada ya muda tu, bali lazima yawe sehemu ya maisha yetu mpaka mwisho, kama Paulo alivyosema,
“Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio WOTE, lakini apokeaye tuzo ni MMOJA? Pigeni mbio NAMNA HIYO, ili MPATE.Na kila ashindanaye katika michezo HUJIZUIA KATIKA YOTE; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika. Hata mimi napiga mbio VIVYO HIVYO, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa; bali NAUTESA mwili wangu na kuutumikisha; ISIWE, nikiisha kuwahubiri wengine, MWENYEWE niwe mtu wa kukataliwa.” (1 Wakor. 9:24-27).
Mtumishi wa Mungu wa dhati, anawalisha watu wa Mungu na neno la Mungu – ila ni lile neno la Mungu ambalo linatokana na uhusiano wake na Mungu! Kimsingi inapaswa lile analolihubiri litokane na maisha yake ya kiroho mbele ya Mungu na nidhamu yake ya kiroho na kimwili – kimsingi analohubiri lisiwe ni jambo la ‘ujuzi’ ambao ameukusanyika kutoka katika vitabu tu au kwenye shule ya Biblia! Hafai kuwajaza watu ujuzi tu! Mtumishi wa Mungu wa kweli amefanywa na Mungu kuwa mhudumu wa Agano Jipya – SIYO WA ANDIKO BALI WA ROHO. (2 Wakor. 3:6). Anahudumia kwa nguvu za Roho, na kwa Roho, sio tu kwa sababu ameshabatizwa na Roho Mtakatifu bali kwa sababu anatembea na Bwana kila siku naye anabadilishwa siku hadi siku kutokana na uhusiano wake na Mungu (2 Wakor.3:18).
Sisemi lile neno analohubiri ni tofauti na mafundisho ya Biblia, hapana, hata kidogo; ila analohubiri limejaribiwa katika maisha ya binafsi yake na kwa hiyo kwake kimsingi siyo jambo la ‘ujuzi’ bali linatokana na uzoefu wake wa dhati MBELE YA BWANA. Mwishoni, ‘kipawa’ au ‘karama’ peke yake havitoshi (Mathayo 7:22,23)! Lazima huduma yetu inatokana na nidhamu ya kiroho, ya kimwili na majaribu vivyo hivyo ilivyokuwa katika maisha ya Kristo Yesu! Kwa hiyo Paulo alimwandikia Timotheo,
“Usiache kuitumia KARAMA ile iliyomo ndani yako, uliyopewa kwa unabii na kwa kuwekewa mikono ya wazee. UYATAFAKARI hayo; UKAE katika hayo; ili KUENDELEA KWAKO kuwe DHAHIRI kwa watu wote. JITUNZE nafsi yako, na mafundisho yako. DUMU katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako NA WALE WAKUSIKIAO PIA.”
Na tukumbuke kuwa Daudi aliweza kumshinda kwa uhodari tele Goliathi kwa sababu KWANZA kutokana na uzoefu wake mwenyewe alishamwua simba na dubu – na hayo hayakutokea ‘mbele ya watu’ bali katika maisha yake ya binafsi ‘mbele ya Bwana’! Na Daudi hakutumia mavazi ya Sauli ya vita kumshinda Goliathi, alitumia ustadi na silaha ambazo ALIJIFUNZA MWENYEWE KUTOKANA NA IMANI YAKE KWA MUNGU!
Sisemi ni lazima muumini asubiri miaka mingi kabla ya kufanya huduma, hapana, lakini inapaswa mtumishi wa Mungu awalishe waumini na neno la Mungu litokanalo na uhusiano wake na Mungu na muda wake mbele ya Bwana!
© DAVID STAMEN 2018