RSS

EPUKA MTEGO WA ADUI

EPUKA MTEGO WA ADUI WA KUTAKA KUJITAJIRISHA KWA NJIA YA NJILI

 

Katika hotuba ya Yesu ya Mlimani kuna jambo nyeti sana alilizungumza ambalo natamani tulitupie macho hapa:

 

“Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.” (MT. 6:24 SUV).

 

Hili ni neno la kuzingatiwa sana na watumishi wa Mungu na wengine wote ambao wameamua kuyatoa maisha yao kwa ajili ya kumtumkia Mungu. Utumishi sio mahali pa kukimbilia kwa sababu maisha yamekushinda na shughuli zingine zote za kujipatia kipato zimekwama kwa hiyo unakuja kwa mfuniko wa kumtumkia Mungu kumbe kiuhalisia umekuja kuchumia tumbo.

 

Injili sio chanzo cha kipato. Injili ni kwa ajili ya watu wenye wito ambao wameamua kuyatoa na kuyadhabihu maisha yao kwa Mungu sawasawa na kusudi la kuzaliwa kwao ili watu wengine wapate habari njema za Mwokozi na Ufalme wa Mungu. Ni ngumu mno kudai eti unamtumikia Mungu wakati huo huo unaitumikia mali au unatafuta kutajirika kifedha na kimali kwa njia ya Injili. Hata Yesu alipowatuma wanafunzi Wake aliwaonya mno kuwa wamepewa bure watoe bure.

 

Hii ndo Injili.

 

Majibu ya ajabu ambayo Injili inaleta kwa maisha na changamoto za watu zinaweza zikamweka mtumishi, mhudumu na mdau wa Injili katika jaribu la kutaka kujineemesha binafsi kwa njia ya Injili.

Inasikitisha ni kwa kiwango gani watu wanatafuta kujitajirisha kwa njia ya Injili matokeo yake wanaanza kuishi maisha ya kijanja janja ndani ya Injili na kila siku kuja na uvumbuzi wa sadaka mpya za kutoza watu kwa ajili ya huduma mbalimbali. Haijalishi utaiitaje. Gharama kamili ya Injili ilishalipiwa na Yesu msalabani na kuwadanganya watu watoe sadaka fulani ili jambo fulani litokee ni kuwapiga, kuwatapeli na kuwaibia.

 

Katika Agano hili la neema sijaona hata jambo moja toka kwa Mungu likiachiliwa kwa yeyote kupitia sadaka. Lingekuwepo uwe na uhakika ungesoma Yesu akilifanya au mojawapo ya mitume baada Yake. Lakini huyasomi haya kwenye maandiko maana hamna kitu kama hicho. Kanuni ambayo mimi naiona ikijirudia rudia katika maandiko kwa habari ya utoaji katika Agano Jipya, ni utoaji ni wa hiari, kama ambavyo mtu ameguswa moyoni mwake, sio kwa huzuni wala kwa kulazimishwa na kwa kadiri ya kufankiwa kwa mtu na baraka za Mungu maishani mwa mtu husika. Utoaji wa sadaka ni sehemu ya ibada na wala sio tozo au ada ya aina fulani wala sio kodi au mchango wa lazima.

 

Paulo alipokuwa anaandikia Kanisa la Filipi aliwaonya na kwa njia hiyo anatuonya sisi sote kuhusu watu ambao matumbo yao ni miungu yao. “Maana wengi huenenda, ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia hata kwa machozi, kuwa ni adui za msalaba wa Kristo; mwisho wao ni uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedheha yao, waniao mambo ya duniani.” (FLP. 3:18-19 SUV). Haya maneno ya Mtume Paulo ni mazito mno maana ni kama anaona siku ambazo tunaishi leo japo alikuwa akizungumzia jambo ambalo lilikuwa linaendelea katika siku zake.

Aina hii ya maisha ya kutafuta kutajirika kwa njia ya Injili imekuwa na athari kubwa kwa Injili kuliko faida. Imezalisha wahanga wengi na majeruhi wengi kuliko ambavyo tupo tayari kukubali. Tunapotafuta kutajirika kwa njia ya Injili inatufanya tuingize ujanja ujanja kwenye kazi ya Injili ambayo mwisho wa siku hii tabia inageuka tu kuwa adui wa kazi ya msalaba wa Kristo.

 

Inasikitisha sana kuwa tunapotafuta kutajirika kwa njia ya Injili tunageuka kuwa maadui wa msalaba.

Injili sio tasnia ya kuzalishia watu kipato. Injili ni Habari Njema za Wokovu kwa watu wote. Huku kutafuta kutajirika kwa njia ya Injili imegeuka kuwa kikwazo kikubwa mno kwa Injili ya Yesu Kristo na watu wengi mno hawataki hata kuisikia Injili kwa sababu ya hii tabia inayosikitisha na kuuhuzunisha moyo wa Mungu. Wengi wetu tunatumikia mali na fedha. Tulishaachaga kumtumikia Mungu siku nyingi. Bahati mbaya sana hata hatujui ni kwa kiasi gani tumetoka kwenye njia. Injili siku hizi sio watu wangapi wamefikiwa na Injili ya Yesu Kristo na tumewafanya wangapi kuwa wanafunzi wa Yesu bali ni mashindano ya unavaa nini, unaishi kwenye nyumba ya namna gani, unaendesha gari gani, una pesa kiasi gani na mambo yanayofanana na hayo yasiyo na uhusiano wowote na Injili ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.

 

Paulo akiandika ili kumwonya na kumpa usia mwanae katika imani Timotheo anaandika:

 

“Mtu awaye yote akifundisha elimu nyingine, wala hayakubali maneno yenye uzima ya Bwana wetu Yesu Kristo, wala mafundisho yapatanayo na utauwa, amejivuna; wala hafahamu neno lo lote; bali ana wazimu wa kuwazia habari za maswali, na mashindano ya maneno, ambayo katika hayo hutoka husuda, na ugomvi, na matukano, na shuku mbaya; na majadiliano ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, huku wakidhani ya kuwa utauwa ni njia ya kupata faida. Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa. Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.” (1 TIM. 6:3-10 SUV).

 

Haya maneno ya Mtume Paulo ni mazito mno na yanastahili kuzingatiwa sana na sisi tuliyopo katika utumishi katika zama hizi. Anaanza kwa kuwaonya kuhusu watu wanaofundisha elimu nyingine tofauti na maneno yenye uzima ya Bwana wetu Yesu Kristo. Je hujaona katika zama zetu mafundisho ya ajabu ajabu ambayo yanamtukuza shetani na kuweka hofu ndani ya watu alafu kinachofuata ni kuwaambia watu watoe sadaka maalum ili wasafishiwe nyota, wakombolewe na madhabahu za kwao, wawekwe huru na ibada za kuabudu miungu ya kifamilia, kiukoo na kikabila, wakombolewe na laana na msururu mwingine mrefu wa sadaka, tozo, malipo, ada na michango ya lazima ambayo inaambatana na mafundisho ambayo usahihi wake unatia mashaka.

 

Yesu yupo wapi katika kiini cha mafundisho yote haya? Kama inabidi nitoe hela ili haya yafanyike, Yesu alienda msalabani kwenda kufanya nini hasa? Hivi sio ninamtukana na kumfedhehi kwa dhahiri?

Kwanini Yesu asiseme kwa sehemu kubwa kazi ya kumkomboa mwanadamu imekwisha bali alisema imekwisha? Tunapowatoza watu hizi sadaka aina aina lile andiko la I Petro linalosema hatukukombolewa kwa vitu viharibikavyo kama fedha na dhahabu ili tutoke katika mwenendo usiofaa ambao tuliurithi kwa baba zetu tunalitupa wapi? Imekuwaje ghafla sio Damu ya Yesu ilitukomboa bali ni maji yaliyo kwenye chupa yenye picha ya nabii fulani au mtume fulani? Inakuwaje sasa ukombozi na ulinzi hupatikana sio kwa kuwa na Yesu maishani mwako bali kuwa na sticker za wahubiri mashuhuri? Tangia lini Yesu na Damu Yake viliacha kuwakomboa watu na sasa wahubiri na pako zao na mbwembwe zao sasa ndo zinahudumu ukombozi kwa watu?

 

Ni wapi hasa kanisa la Karne ya 21 limepoteza mwelekeo?

 

Paulo anaonya kuwa utauwa sio njia ya kujipatia faida au kwa maneno mengine Injili sio njia ya kujipatia faida. Anatukumbusha kuwa utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa mno. Anaendelea kusema kuwa hatukuja na kitu duniani wala hatuwezi kuondoka na kitu. Hizi mali na fedha tunazojilimbikizia kama wahubiri wa Injili ni ili iweje? Tukiwa na chakula na mavazi tutaridhika navyo. Alafu anasema kwa kuonya kuwa wale watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi na tamaa nyingi zisizo na maana zenye kudhuru ziwatosazo watu katika upotevu na uharibifu.

 

Mimi na wewe tunapokuwa wahudumu wa Injili alafu tukatafuta kuwa na fedha na mali kwa njia ya hiyo Injili itatupelekea kuanguka katika majaribu na tanzi na tamaa nyingi zisizo na maana zitakazo tutosa katika upotevu na uharibifu.

Bahati mbaya sana hii ndo hali ya wahubiri wengi na wahudumu wengi wa Injili wa dotcom. Paulo alipokuwa anayaandika haya ni kama alikuwa anatuona kwenye karne ya 21. Kupenda fedha na mali ni shina moja ya mabaya yote. Yaana mabaya yote yameshikamanishwa na hiyo hali ya kupenda fedha na mali. Wengi wa watumishi na wahudumu wa Injili hali wakiwa wamekamatwa na hii hali ya kupenda fedha na mali na kuitamani wamesha farakana na imani na wamekuwa kama waganga wa kienyeji na walozi kwa namna wanavyofanya huduma. Yesu sio kiini tena cha ujumbe wao.

 

Watu hawambebi tena Yesu ndani yao bali wanabeba vichupa vya maji, mafuta, mapakiti ya chumvi, huku wakivaa mikufu, bangili na yafananayo ambavyo wanavipata kwa kuvinunua toka kwa wahubiri na wahudumu wa Injili. Imepelekea wengi kufarakana na imani na kujichoma na maumivu mengi.

Huu uwendawazimu tutauacha lini? Mbona tunaukwaza msalaba wa Yesu Kristo na tunafanyika kizuizi cha watu kumjua Yesu?

 

Na Carlos R. W. Kirimbai          Pastor Manna Tabernacle Bible Church, Dar Es Salaam

 

Comments are closed.

 
%d bloggers like this: