RSS

NA KATIKA KUTAMANI WATAJIPATIA FAIDA

“NA KATIKA KUTAMANI WATAJIPATIA FAIDA (YAANI, PESA) KWENU KWA MANENO YALIYOTUNGWA; AMBAO HUKUMU YAO TANGU ZAMANI HAIKAWII, WALA UVUNJIFU WAO HAUSINZII.” (2 Petro 2:3).

MISTARI HII INAMHUSU NANI SIKU HIZI?

INAMHUSU YE YOTE (aitwe mtume, nabii, askofu au mchungaji) ANAYEMLAZIMISHA au KUMSHAWISHI mshirika (au mtu ye yote) AMTOE/AMLIPE PESA KABLA YA KUMWOMBEA, yaani, ampe pesa kwa ajili ya maombi yake, au huduma yake ye yote aliyodai ameipokea kutoka kwa Mungu.

Pia inamhusu ye yote ambaye anafanya ‘huduma’ ya maombi kwenye redio (kwa dakika 15 au zaidi) na MARA anapomaliza maombi anatangaza numba ya Mpesa yake ili wasikilizaji wamtumie pesa kwa ajili ya maombi yake!

Hivi karibuni niliambiwa juu ya kanisa moja lilopo Dar Es Salaam. Walitangaza kwamba magonjwa yote yanatibika pale. Lakini kabla ya kuombewa ilikuwa lazima kujaza fomu ya maombi. Lakini kujaza fomu hiyo walitaka ulipe sh. elfu kumi! Sasa je, hatusomi Biblia? Kwa nini watu wanadanganywa kwa njia rahisi sana?

Viongozi wengine wanawaweka waumini kwenye fedheha zaidi. Katika mkutano mmojawapo kiongozi alisema, “Tengenezeeni mistari mitatu hapa mbele.” Kisha akawa anaelekeza  akisema, “Simama foleni katika mstari huu hapa kama wewe unataka kutoa sh. 1000; na wewe unayetaka kutoa sh 10,000, tafadhali njoo hapa mbele na upange foleni hapa katika mstari huu wa pili. Lakini kama unayo laki moja nawe unataka kutoa njoo usimame katika foleni hii ya tatu.” Ndipo sasa kiongozi yule anazidi kuwasihi wasikilizaji wake akiwadanganya kwa kusema, “naenda kuomba maombi mazito. Maombi mazito ya wale waliotoa laki moja yataanza, kisha wataombewa wale waliotoa sh. elfu kumi, na wewe uliyetoa elfu moja utaombewa mwishoni!” Sasa kutokana na kiu yao ya kupenda pesa, na uchoyo walio nao viongozi kama huyo, wanaligeuza kanisa liwe biashara, hivyo wanamtenda dhambi Mungu, na pia wanawatendea dhambi watu wa Mungu.

Haya yote ni dhambi kubwa sana! Hiyo ni biashara. Wanajaribu kutumia ‘karama’ ya Mungu au huduma yao kujipatia pesa. Kila afanyaye hivyo upo chini ya hukumu ya mstari huu wa hapo juu! Haupo hata mfano mmoja katika Biblia ambapo mtumishi wa Mungu ye yote anasema, “Nipe pesa kwanza kabla sijakuombea.”

Kwa mujibu wa neno la Mungu HIYO NI KAZI YA SHETANI na wale wanaofanya hivyo ni WATUMISHI WAKE.

Mtume Paulo anaeleza jambo hili kwa wazi. Paulo alihudumia washirika wa Korintho bure, bali Wakorintho HAWAKUWEZA kuelewa TABIA yake, HAWAKUWEZA kutambua PENDO la Mungu wala HUDUMA ya Mungu kweli kweli! Hawakuelewa kuwa Paulo angeweza kuwa mtume kwa sababu HAWAKULAZIMISHWA na Paulo wampe pesa kwa ajili ya huduma yake!  Kwa hiyo Paulo aliwauliza, “Je! NILIFANYA DHAMBI kwa kunyenyekea ili ninyi mtukuzwe, kwa sababu naliwahubiri Injili ya Mungu BILA UJIRA?” (2 Wakor.11:7). Kwa nini waumini wa Korintho walikosa sana katika fikra zao? Kwa sababu mitume wa UONGO walikuja na WAKAJIINUA na WALIWALAZIMISHA washirika wawalipe pesa kwa ajili ya huduma yao. Kwa hiyo Paulo aliwaambia, “Maana MWACHUKULIANA na mtu akiwatia utumwani, akiwameza, akiwateka nyara, akijikuza, akiwapiga usoni.” (2 Wakor.11:20). Katika 2 Wakorintho 11 Paulo anajishughulisha na swali la pesa na huduma, hasa juu ya wahubiri ambao waliwalazimisha kuwatoa pesa kwa ajili ya huduma yao. Na Paulo anasema nini juu ya wahubiri hao? Hebu tusome maelezo ya neno la Mungu:

“Maana watu kama hao ni MITUME WA UONGO, watendao kazi kwa hila, WANAOJIGEUZA wawe MFANO wa mitume wa Kristo. Wala si ajabu. Maana SHETANI mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru. Basi si neno kubwa WATUMISHI WAKE nao WAKIJIGEUZA wawe MFANO wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao. (2 Wakor.11:13-15).

Unaelewa? Hatupaswi kucheza na mambo hayo! Ni hatari sana! Hatupaswi kutekwa nyara na dhambi hiyo na udanganyifu huu. Haijalishi ikiwa anaitwa mtume, nabii, askofu au mchungaji!

USISHIRIKI DHAMBI ZAKE! Ni kazi ya shetani tu, na yeye mtumishi wake!

Dhambi hiyo inaharibu ‘sura’ ya Mungu mioyoni mwa watu! Inasababisha wauumini wasiitambue tabia ya Mungu, hata wasimtambue Mungu mwenyewe! Kwa matendo hayo mabaya wanatangaza ‘Mungu ndivyo alivyo!’ Lakini Mungu SIYVO ALIVYO kama wanavyofanya mbele ya macho ya watu! Kwa dhambi hiyo wanazuia waumini wasimjue Mungu wala tabia yake! Hiyo ni kazi ya shetani toka mwanzo kama tunavyoona katika bustani ya Edeni! Kwa hiyo Paulo anasema katika sura ile ile ya 2 Wakrointho,

“Lakini nachelea; kama YULE NYOKA ALIVYOMDANGANYA Hawa kwa hila yake, ASIJE AKAWAHARIBU FIKIRA ZENU, MKAUACHA unyofu na usafi kwa Kristo. Maana yeye ajaye akihubiri YESU MWINGINE ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea ROHO NYINGINE msiyoipokea, au INJILI NYINGINE msiyoikubali, mnatenda vema KUVUMILIANA naye! Maana nadhani ya kuwa mimi SIKUPUNGUKIWA na kitu walicho nacho mitume walio wakuu.” (2 Wakor.11:3-5).

Unaona? Kazi ya wahubiri hao ni kuwaharibu fikira za watu kwa matendo yao mabaya na kuwadanganya ili wasijue Mungu. Haya yote ni hila ya shetani mwenyewe. USIVUMILIANE nao! Kwa uchoyo wao wa kupenda pesa wanahubiri ‘yesu mwignine’ na ‘injili nyingine’ kupitia ‘roho nyingine’! Ni hatari sana! Unaona? Waumini wengi wa Korintho walifikiri Paulo alikupungukiwa na kitu kikubwa KWA SABABU hakuwalazimisha waumini wampe pesa kwa ajili ya huduma yake!!! Katika sehemu nyingine Paulo aliwaambia, “kwa maana wengine HAWAMJUI  Mungu. Ninanena hayo NIWAFEDHEHESHE.” (1 Wakor.15:34).

Usishiriki na matendo ya wale watakao pesa yako kwa ajili ya maombi yao! Haijalishi ikiwa ni wengi! Haijalishi ikiwa anaitwa askofu au nabii. Ukumbuke mstari ule uliosema, “Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, KWA KUWA UMEDHANIA YA KUWA KARAMA YA MUNGU YAPATIKANA KWA PESA… moyo wako si mnyofu mbele za Mungu.” (Matendo 8:21,29).

Juu ya karama au huduma tuliyoipewa na Mungu, Yesu alisema, “Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; MMEPATA BURE, TOENI BURE.” (Mathayo 10:8).

Ushuhuda wa Paulo ulikuwa ufuatao: “SIKUTAMANI FEDHA WALA DHAHABU, WALA MAVAZI YA MTU….Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, NI HERI KUTOA KULIKO KUPOKEA.” (Matendo 20:33,35).

Lakini naomba usinielewe vibaya. Tafadhali uelewe muktadha ya somo hili kwa makini! Sijaandika juu ya msaada kwa ajili ya kazi ya mchungaji wa kanisa au mtumishi mwingine wa Bwana kwa ujumla. Kama mchungaji wako ni mwaminifu, mtu asiyelaumika, mpole, mwenye haki na SIYO “MWENYE KUPENDA FEDHA” (1 Tim.3:2,3), akifanya kazi ya upendo kwa ajili ya kanisa la Bwana, basi ni jambo la upendo na haki kuwa kanisa wamsaidie sawasawa na MAHITAJI yake na familia yake, sawasawa na neno la Mungu: “Wazee watawalao VEMA na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha. Kwa maana andiko lasema, Usimfunge kinywa ng’ombe apurapo nafaka. Na tena, Mtenda kazi astahili ujira wake.” (1 Tim.5:17,18). (Maana ya ‘wazee’ hapo ni sawa na ‘wachungaji.’) Lakini mchungaji ye yote anayetaka pesa yako kwa ajili ya maombi yake, huyo siyo mchungaji wa kanisa la Bwana Yesu.

Inaonekana wengi wanajiruhusu kudanganywa kwa urahisi kwa sababu hawajui Biblia au hawajaacha mila ya uchawi. Kumlipa mtu fulani pesa ili akuombee, ni jambo la uchawi kabisa!

Usishiriki na dhambi yao. Usivumiliane nao! Hata kidogo! Mfuate Bwana Yesu! Some neno la Mungu. Jitafutie mchungaji mzuri ahubiriye neno la Mungu na kuishi kadiri ya neno la Mungu.

© David Stamen  2016              

 

Comments are closed.

 
%d bloggers like this: