RSS

JE, MUNGU HUTOA MAFUNUO MAPYA NYAKATI HIZI?

UTARATIBU RAHISI SANA WA KUEPUSHA MAFUNDISHO YA UONGO

Kuna mafundisho mageni na ya hatari sana nyakati hizi. Kuna wale wanaosema kuwa, kama vile Mungu alivyosema na watumishi wake kwa Roho Mtakatifu nyakati hizo zilizopita, hali kadhalika nyakati za leo Mungu husema mambo mapya kwa Roho wake kupitia manabii na watumishi wake. Kwa maneno mwingine, watu hao wanaweza kuleta na kufundisha mambo ambayo hayapatikani kabisa kwenye Neno la Mungu. Hii sasa ni mafundisho yenye hatari sana na yanafungua mlango wa udanganyifu na vishawishi vya kiushetani.

Jambo lolote tunalofundisha, sio tu kwamba lazima kuwa na msingi wake kwenye Biblia, bali likubaliane na kile kinachofundishwa na Biblia yenyewe.

Kile tunacho kifundisha lazima kipatikane ndani ya Biblia kwa ufasaha wa wazi kabisa. Ni wazi kuwa “kufundisha” kunahusu kuelezea mambo yanayo patikana ndani ya neno la Mungu, lakini maelezo hayo hayatazalisha fundisho jipya ambalo halipatikani ndani ya Biblia!

Na nikushirikishe kitu fulani chepesi ambacho kilinisaidia mimi kwa kiwango kikubwa kwa miaka mingi: Kama mtu ye yote akifundisha kitu kipya ama tofauti ama hukitambui toka kwenye Biblia, JIULIZE TU, ‘Hii imeandikwa wapi kwenye Biblia?’ Huhitaji kwenda Shule ya Biblia; huhitaji kusoma ‘Teolojia’, huhitaji kuamini kila jambo yeye aitwaye nabii unalikuambia! Soma Biblia, soma neno la Mungu na jiulize, “Ni wapi kwenye Biblia napata wazo au fundisho hili?” Fanya vile vile kama watu wa Beroya alivyofanya (Matendo 17:11) na utapata baraka na usalama!

Kwa mfano, nimewahi kukutana na watu zaidi ya mmoja ambao wanadai kuwa wanayo karama toka kwa Mungu ya kutafsiri ndoto aina yoyote za kawaida tu ambazo watu tunaziota siku kwa siku!

Sasa, hili sio jambo gumu kulielewa. Jiulize tu wewe mwenyewe, ni mahali gani kwenye Biblia ambako tunaweza kumkuta mtu wa Mungu aliye na karama ya kutafsiri ndoto za kawaida za watu  wanazoziota siku kwa siku? Jibu hapo liko wazi na ni jambo rahisi tu! Kwamba hayuko hata mtu mmoja ndani ya Biblia aliyekuwa na karama ya jinsi hiyo na aliyepata kuitumia karama ya aina hiyohiyo.

Hivyo basi, yakupasa mara moja kuyakataa mafundisho ya aina hiyo moja kwa moja.

Ukisoma neno la Mungu utatambua kuwa ndoto ambazo tunazisoma habari zake ndani ya Biblia zilimjia mtu moja kwa moja kutoka kwa Mungu mwenyewe, na mara moja mtu yule aliweza kufahamu maana ya ndoto ile, na kwamba ndoto ile imetoka kwa Mungu. Au walipewa tafsiri yake mara moja baadae kupitia kwa mtumishi wa Bwana.

Jambo la muhimu hapo ni kwamba ndoto zote zile zilikuwa ni NDOTO ZA PEKEE kabisa zilizotokea moja kwa moja TOKA KWA MUNGU mwenyewe, ili KUTIMILIZA KUSUDI LAKE KATIKA MAISHA YA WATU WAKE NA KWA MAKUSUDI YAKE KATIKA ULIMWENGUNI. Haupo hata mfano mmoja ndani ya Biblia unaoelezea kuwa mtu wa Mungu alikuwa na huduma au karama ya kutafsiri maana ya kiroho ya ndoto za kawaida aotazo mtu siku kwa siku!.Lakini watu hawa wanadai kuwa unaweza kuwaendea na ndoto yako yoyote ile wakati wowote ule na wao watakupatia tafsiri ya kiroho kuhusiana ndoto yako hiyo KWA AJILI YA MAISHA YAKO YA BINAFSI. Hilo ni jambo labda la saikoloji lakini kwa Wakristo ni jambo la udanganyifu na kutokutii kwa sababu watu wanaenda huko nje ya neno la Mungu wapate ushauri juu ya maisha ya kiroho yao. Na kwa hakika kwa ujumla wake wanakuwa wanalipinga neno la Mungu.kwa sababu wao huliacha neno la Mungu na kuamua kuifuata aina ya kupiga ramli!

Nilipowaandikia watu hao nikiwataka angalau wanipe basi mstari mmoja tu wa Biblia unaoonyesha kumfuata mtumishi yeyote wa Mungu ambaye alikuwa na huduma ya aina hii kama wanavyodai wao kuwa wanayo. Hakuna hata mmoja kati yao aliyeweza kunipa mstari huo. Na hii haishangazi kwa sababu hata wao wenyewe wanajua kuwa haipo tena hata mfano mmoja wa aina hiyo au fundisho la aina hiyo kwenye Biblia.

Badala yake walijaribu kunishawishi mimi kwamba nisiwe nakomea kwenye mambo yaliyoandikwa kwenye Biblia tu kwa sababu eti ni Roho Mtakatifu ambaye aliivuvia Biblia iweze kuandikwa, na vivyo hivyo Roho Mtakatifu anaweza kutufundisha mambo mapya YASIYOFUNDISHWA KWENYE BIBLIA – hasa kama yamefundishwa na mtu anayejiita nabii! Wazo kama hilo ni la uwongo kabisa na udanganyifu mtupu unaotuongoza tuwe mbali na neno la Mungu, tusiishi kwa neno Lake.

Kama udanganyifu huo ungekuwa sawa, mtu yeyote angeweza kufundisha fundisho lolote kama  mwenyewe atakavyo kwa kudai ni ufunuo wa Roho Mtakatifu! Huo ni njia ya kufungua mlango kwa kila fundisho baya na roho baya!

Watu wengine eti hudiriki kufundisha kwamba hata kama mtu amepokea wokovu wa Kristo Yesu, basi lolote lile kama shida, taabu au hata ukipatwa na ajali yoyote ile, basi eti mambo hayo yanakupata kutokana na laana ya mambo ya huko nyuma – wanadai kuwa hayo yanakupata kutokana na laana itokanayo na maisha yako mwenyewe, au ni laana ya mababa nkd.  Hapa tena, UJIULIZE WEWE MWENYEWE, kuwa ni wapi katika Agano Jipya ambalo Yesu au mitume wanatufundisha au hata kutaja kuwa tatizo lolote ambalo tunaweza kulipata katika maisha yetu kama watoto wa Mungu litakuwa linatokana na aina yoyote ile ya laana? Mara moja utafahamu tu kwamba HAKUNA MAHALA POPOTE katika Agano Jipya ambapo laana inatambuliwa kuwa ndiyo chanzo cha matatizo yanayompata mkristo katika maisha yake!

Fundisho hilo halipo katika Agano Jipya lote, hivyo yakupasa na inakubidi kulikataa moja kwa moja bila kusita. Tunaposoma Agano Jipya tunaona wazi kuwa kutokana na kile alichokikamilisha Yesu pale Msalabani kinyume cha hayo wafundishayo ndiyo kweli. Bwana asifiwe! (Jisomee mwenyewe katika kitabu cha Waefeso 1:3 na Wagalatia 3:13-14). Watu hujaribu kuyahalalisha mafundisho haya kwa kuyatumia vibaya maandiko kutoka katika Agano la Kale tu, kama kwamba Yesu asingalikufa msalabani!

Tena, iwapo muhubiri yeyote yule akijaribu KUKUUZIA wewe chumvi, maji ya upako, au kitambaa akidai kuwa vitu hivyo ndivyo vitakuletea baraka na uponyaji au mafanikio, basi mtu huyo atakuwa anajiweka yeye mwenyewe kwenye eneo lenye hatari sana. Ikiwa na wewe utalipa pesa zako ili kununua uongo wa vituko kama hivyo, ndipo na wewe utakuwa umejiweka mwenewe katika eneo la hatari pia. Biblia inatupatia maonyo yenye kutuokoa na yenye usalama kutokana na mwenendo mbaya huo na mtazamo wa kiuchawi kama huo pale Petro anapomwambia Simoni, “Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali.” (Matendo 8:20). Je, na wewe unapenda kuwa kwenye kundi lilelile kama Simoni aliyekuwa amekuwa mpiga ramli? Hebu basi fikiri na ujiulize wewe mwenyewe, NI SEHEMU GANI katika Agano Jipya au hata ndani ya Biblia nzima ambapo alitokea mtu kumlipa mtumishi wa Mungu pesa ili apokee uponyaji au baraka? Jawabu la swali hili ni wazi kwamba hakuna popote pale! Hakuna kitu kama hiki kinachofundishwa na Biblia. Na kwa sababu hiyo basi yakupasa moja kwa moja kukataa fundisho hili na vitendo vyake wanavyofanya!

Petro anatangaza, “Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa KAMA APENDAVYO MTU fulani tu. Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.” (2 Petro 1:20,21). Na paulo anatujulisha, “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ILI MTU WA MUNGU AWE KAMILI, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.” (2 Tim.3:16,17).

Mistari hii inatuambia kile ambacho wakristo walikuwa wamekwisha kukiifahamu na kukiamini tangu siku za Mitume, ya kwamba maandiko ya neno la Mungu YANATOSHA na yanafaa kutufundisha/kutuhekimisha  KILA KITU tunachohitaji kukijua ili mtu wa Mungu awe mkamilifu!  Neno la Mungu LINATOSHA. Hili ni jambo la muhimu sana kiasi kwamba Mtume Paulo anatuonya kwa kutumia laugha nzito/kali zaidi kuhusu jambo hili la kubadilisha au kuongeza kitu chochote kile kwenye neno la Mungu ambalo tayari limekwisha tangazwa kwetu, “Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe.” (Wagal.1:9).

Aidha, Mistari hii ya neno la Mungu haihusiki tu na maandiko ya Agano la Kale pekee, lakini inahusu pia maandiko ya Agano Jipya – unaliona jambo hili vizuri kwenye mistari ifuatayo: 2 Petro 3:15.16; Wakolosai 4:16; 1 Tim. 4:15,16; 6:2,3; 2 Tim.2:2.

Na ukumbuke jambo hili kuwa Mungu yuko juu ya mambo yote. Kama vile ilivyo kwa Mungu mwenyewe kupitia maongozi yake aliyaleta pamoja na akatupatia vitabu vya Agano la Kale kwa ajili ya watu wake, VIVYO HIVYO vitabu vya Agano Jipya navyo HAVIKULETWA kama ajali au kwa njia ya ovyoovyo na baghalabaghala, lakini MUNGU KUPITIA MAONGOZI YAKE MWENYEWE ametupatia sisi vitabu hivyo ambavyo kwa sasa tunaviita Agano Jipya – naye amefanya hivyo KWA USALAMA WETU – na kwa wokovu wetu na baraka zetu sisi wenyewe. Yatupasa kuwa waangalifu sana, kwa sababu ya kile kilichoandikwa mwishoni mwa kitabu cha Ufunuo kuhusiana na kuongeza au kupunguza neno, yawezekana ikawa ni ukweli unaoihusu Biblia nzima! (Ufunuo 22:18,19).

Imeandikwa juu ya watu wa Beroya kwamba, “Watu hawa … walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, WAKAYACHUNGUZA MAANDIKO KILA SIKU, WAONE KWAMBA MAMBO HAYO NDIVYO YALIVYO.” (Matendo 17:11). Tunapaswa kufanya vilevile ili mafundisho mapya ya siku hizi yasitufanye mateka, ili “tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.” (Waefeso 4:14).

Fuata utaratibu huo ya kuepusha mafundisho ya uongo na ya mashetani na utabarikiwa. Usifikiri unahitaji elimu ya juu kufundishwa na neno la Mungu! Kumbuka kile Yesu alichokisema, “Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako.” (Mathayo 11:25,26).

 

Comments are closed.

 
%d bloggers like this: