RSS

Bwana Yesu Kristo hakufa Msalabani ili atimize Ndoto Yako

LUGHA MPYA: Mtazamo wa ulimwengu, nia ya kibinadamu na ya wasioamini zimeingia fikra za waumini wengi sana.

Wapendwa wasomaji, wapi katika Agano Jipya tunasoma kwamba Yesu au mitume wanawasisitiza waumini wazifuate ‘ndoto’ zao? Haipo! Wapi katika maandiko ya Biblia waandishi wanatumia lugha ya ‘zifuate ndoto zako’? Haipo! Wapi Bwana Yesu alisema, “Nimekuja kuitumiza ndoto yangu.”? Haiwezekani! Yesu wala mitume wake hawakuitumia lugha hiyo au maneno haya! Wazo hili linapinga mafundisho ya neno la Mungu. Wazo hili linainua hamu yangu yenyewe au tamani yangu ya binafsi kuliko mapenzi ya Mungu kwa maisha yangu! Ni mafundisho ya hatari sana siku hizi.

Watu, na hata wahubiri, wanasema, ‘Fuata ndoto zako!’ Lakini Yesu alisema, ‘Nifuate mimi’. Ikiwa utafuata ndoto zako, unajifurahisha mwenyewe tu. Lakini ikiwa utamfuata Yesu, atampendeza Yeye. Kama utafuata ndoto zako, basi unajitumikia wewe mwenyewe. Ukimfuata Yesu, utamtumikia Yeye na kanisa lake. Kama utafuata ndoto zako, unajitengenezea njia yako mwenyewe. Kama utamfuata Yesu, Yeye ndiye atakayekuandalia njia – siyo kwa ajili ya maisha ya kiroho yako tu, bali kwa ajili ya KILA SEHEMU ya maisha yako.

Kama utajitahidi kutimiza ndoto zako au mtazamo wako, inaweza kabisa utakosa mapenzi ya Mungu. Lakini kama ‘utatoa mwili wako uwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu na hutaifuatisha namna ya dunia hii, bali kugeuzwa kwa kufanywa upya nia zako, ndipo utakapojua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, YA KUMPENDEZA NA UKAMILIFU’, siyo kwa ajili ya maisha ya kiroho yako tu, bali kwa ajili ya KILA SEHEMU ya maisha yako.

Hila iliyomo ndani ya fundisho hili inawaelekeza waumini kuzifuata na kujaribu kutimiza “ndoto” zao za kibinafsi bila kujitoa kwake Mungu kwa dhati ili wathibitishe kile wanachokitamani (“ndoto” zao) kinatokana na Mungu au la, kutambua kama ni mapenzi ya Mungu au sivyo!

Watu wengi siku hizi wanafuata ‘ndoto’ zao au wanajitahidi kuutengeneza ‘mtazamo’ wao ili ‘wafanikiwe’ wakati wakidai au wakifikiri hiyo ni sawasawa na mapenzi ya Mungu, lakini wanajidanganya au wanaruhusu mhubiri fulani kuwadanganya. Yesu hakuifuata ndoto yake – hiyo ni kinyume cha tabia Yake! Kinyume cha wazo hili la siki hizi Yesu alisema, “Kwa kuwa mimi SIKUSHUKA kutoka mbinguni ILI NIYAFANYE MAPENZI YANGU, bali MAPENZI YAKE aliyenipeleka.” (Yoh.6:38). Huo ulikuwa msingi wa maisha ya Mwana wa Mungu! Na kama Wakristo tunapaswa tuwe na msingi ule ule! Kumbe, kwa maneno machache Bwana Yesu amebomoa ndoto nyingi ya waumini ya siku hizi, ameharibu mafundisho haya ya udanganyifu! Je, ndoto yako ni sawasawa na mapenzi ya Mungu kwa maisha yako? Unajuaje? Kwa wengi, chakula chao ni kuota ndoto wafanikiwe, au wawe kitu, kama mwimbaji, mwenye biashara, mhubiri nchini au ulimwenguni – wanajisikia kiu sana kwa ajili ya tekelezo la ndoto ZAO au mtazamo WAO! Kinyume chake neno la Mungu lilimjia Baruku, “Je, utajitafutia mambo makubwa kwa ajili yako mwenyewe? Usiyatafute hayo.” (Yeremia 45:5).

Yesu alisema, “Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi YAKE aliyenipeleka, nikaimalize kazi YAKE.” Na wewe? Unafuata ndoto yako au unaifuata njia ya Yesu Kristo – yaani, hufuati mapenzi yako mwenyewe bali mapenzi ya Mungu? Udanganyifu ya siku hizi ni kwamba watu wanachanganyika kabisa kabisa ‘ndoto yangu’ na ‘mapenzi ya Mungu kwa maisha yangu.’ Bila kusoma Biblia, bila kuamini Biblia, bila kufiri hata kidogo juu ya yale Biblia isemayo, na hata bila kujitoa wenyewe kwake Mungu kwanza, watu wanasawasisha ‘ndoto zao’ na ‘mapenzi ya Mungu’, na wanaandika maneno bila maana kabisa kama, “Usikate tamaa. Mungu atatimiza ndoto yako”, au “bila ndoto hutapata cho chote!” au “Usimruhusu shetani aiharibu ndoto yako!” Watu hawa hawajali neno la Mungu, wanapuuza mafundisho ya Biblia, wanatangaza maneno matupu!

Na hapo tunakutana na udanganyifu ya mafundisho hayo; yaani, wahubiri hawafuati neno la Mungu bali badala yake wanachochea HAMU YA BINAFSI ya watu, TAMANI YA WATU WENYEWE wawe kitu au kuwa na kitu. Kwa mafundisho yao wanaacha lugha ya Biblia, wanaondoa wazo la ‘mapenzi ya Mungu’ na badala yake wanatumia neno ‘ndoto’ na wanasawasisha hamu ya binfasi ya mtu na mapenzi ya Mungu, yaani, hawatofautishiani kati ya ‘ndoto yangu’ na ‘mapenzi ya Mungu’. Matokeo ya mafundisho haya na lugha hiyo ni machanganyiko na udanganyifu. Ni wazi watu watafurahi kusikia mambo haya. Kwa nini? Kwa sababu sasa hamu yangu inawakilisha ‘mapenzi ya Mungu’ kwa maisha yangu, na sasa watu wanafikiri lazima Mungu atatimiza tamani yao wawe kitu kwa sababu ‘ndoto’ yao ni sawa na mapenzi ya Mungu! Kwa nini watu wanafurahia mafundisho haya? Kwa sababu yanaruhusu, na hata yanachochea tabia ya kujipendeza!

Hila ya fundisho hili ipo ifuatavyo: Kwamba kile ni lazima niwe nacho, nitakipata tu, kitatimizwa kwa vyovyote vile! 

Kumbe, sasa ‘njia’ ya Yesu inanipendeza kwa sababu ni njia kutimiza matamanio yangu! Hapana. Yesu alitangaza kwa wazi kabisa, “Akawaambia WOTE, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na AJIKANE MWENYEWE, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate… Kama mtu akija kwangu naye hamchukii …nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.” (Luka 9:23, 14:26).

Ni siku za hatari sana. Vijana wengi wamedanganywa kufikiri ndoto zao au mitazamo yao zinawakilisha mapenzi ya Mungu, kwa hiyo…

kwa wengi, ndoto zao hazitatimizwa.

Kwa wengine ndoto zao labda zitatimizwa lakini haimaanishi ni mapenzi ya Mungu kwa maisha yao! Inategemea kabisa!

Waumini wengine wanangojea ngojea matekelezo ya ndoto zao. Badala ya kufuata kwanza ufalme wa Mungu na haki Yake, akili zao zimejazwa na mawazo ya ndoto zao; badala ya kumpenda Yesu kwa mioyo yao yote, mioyo yao zimeshikwa na hamu zao kuona matekelezo ya ndoto zao; badala ya kuyatafuta mapenzi ya Mungu (ambayo inawezekana yatakatisha ndoto zao!), wao wanaongozwa na ndoto zao katika mawazo na matendo yao – wanajitoa kwa ndoto zao kuliko kwake Mungu. Lakini kwenye facebook au kwenye semina fulani wahubiri au waandishi watajaribu kuzimarisha ndoto zao kwa kuwatia moyo ili wasikate tamaa. Kwa wengi ndoto zao hazitatimizwa kwa sababu hazijajengwa juu ya mwamba wa neno la Mungu bali juu ya mchanga wa mawazo ya ulimwengu na juu ya ‘tamani’ ya watu tu! Waumini wengi hao watashindwa kuona tekelezo la ndoto zao, na kwa hiyo watakata tamaa sana na inawezekana wengine wao wataacha imani, wataacha kumfuata Yesu. Ni jambo la kuhuzunishwa sana na ninaandika mambo haya ili hata kijana mmoja tu ageuke na kuacha udanganyifu huo.

Yesu Kristo hakufa msalabani ili kutumiza ndoto zako!

Siyo kazi yangu kuota ndoto kwa maisha yangu! Jukumu langu ni ‘kutoa mwili wangu uwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu na kugeuzwa kwa kufanywa upya nia yangu, ndipo nitakapojua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza na ukamilifu kwa maisha yangu.’ Jukumu langu ni ‘niufuate kwanza ufalme wa Mungu na haki Yake NA HAYO YOTE MTAZIDISHIWA! Bwana asifiwe sana! Sisi hatuwezi kukosa cho chote ambacho kinahusu mapenzi ya Mungu kwa maisha yetu kama tukifuata neno la Mungu! Ni rahisi. Hatuhitaji kwenda chuo kikuu kuelewa ukweli wa Mungu! Inatosha kabisa tuwe kama watoto wachanga (Matayo 11:25). Kama tukitoa maisha yetu yawe dhabihu iliyo hai, Mungu Mwenyewe atatimiza mapenzi yake katika maisha yetu kwa wakati Wake, siyo kwa ajili ya maisha ya kiroho yetu tu, bali kwa ajili ya kila sehemu ya maisha yetu – nyumbani, ndoani, kazini na zaidi!

Usinelewe vibaya. Siyo kosa kuwa na hamu au lengo! Lakini lazima tuwe watumishi wa Bwana na kufuata neno lake lisemalo, “Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote wala usizitegemee akili zako mwenyewe, katika njia zako zote mkiri yeye, naye atayanyoosha mapito yako.” (Mithali 3:5,6). Mtumaini Bwana na siyo ndoto yako! Usizitegemee ndoto zako bali mtegemee Mungu! Katika njia zako zote usikiri (moyoni mwako au mbele ya watu) ndoto yako, bali mkiri Bwana, naye atayanyoosha mapito yako, ndugu yangu, rafiki yangu.

Najua katika Biblia watu wa Mungu (kama Yusufu mwana wa Yakobo katika Agano la Kale na mume wa Mariamu Agano Jipya) waliota ndoto, na imeandikwa “na wazee wenu wataota ndoto” (Mat.2:17), lakini ndoto hizo na maono yote ambayo watumishi wa Mungu walikuwa nayo katika Biblia yanahusu MAPENZI YA MUNGU kwa watu wake na mpango wa Mungu juu ya mambo yajayo – zinatokana moja kwa moja na Mungu Mwenyewe, hazitokani na hamu ya watu ili kuzitumiza ndoto zao!

Kwa mfano, Yusufu hakukaa chini ya mti fulani akiwaza, “Ah! Siku mmoja ningependa kuwa kiongozi wa Misri! Natamani kuwa mtu mkuu wa Misri – hiyo ndiyo ndoto yangu!” Yusufu hakuwa na hamu ya kuwa na mambo kama hayo, eti aje kuwa mtu mkuu wa Misri! Hapana. Mawazo hayo hayakuingia kichwani mwake hata kidogo! Yeye alipata ndoto ile moja kwa moja kutoka kwa Mungu mwenyewe. Na ndoto hiyo haikuhusika na kiu au hamu ya matamanio binafsi ya Yusufu mwenyewe BALI ilihusu MAPENZI YA MUNGU kwa ajili ya mpango Wake na kwa ajili ya watu wake na kazi yake duniani. Ndoto ile haikutokana na hamu binafsi ya Yusufu mwenyewe awe mtu mkuu katika nchi ya Misri, bali ilitokana na Mungu mweyenwe tu kutimiza mapenzi YAKE duniani, na mapenzi lake lilizingatia maisha ya Yusufu.

Sasa je, unawaonaje wahubiri wa siku hizi wanavyopotosha neno la Mungu kwa kuwafundisha vijana kile wanachokitamani wenyewe kilingane na ndoto iliyoletwa na Mungu? Kimsingi, KILA NDOTO iliyopewa na MUNGU katika Biblia haikuhusu mpango wala hamu wala matamanio za mtu binafsi – ilihusu mapenzi ya Mungu kwa ajili ya watu wake na kazi yake duniani. (Mwanzo 20:3, 28:12, 31:11, 31:24, 37:6, 42:9; Waamuzi 7:11-15; 1 Wafalme 3:5; Mathayo 1:20, 2:12,13,19, 22; Matendo 16:9; Mwanzo 40:5; Mwanzo 41:15,16; Daniel 2:36, 4:19). Ndoto ya Yusufu ilihusu mpango wa Mungu kuokoa familia ya Yokobo kutoka katika hali ya njaa na kutayarisha mahali pa usalama kwa ajili ya familia yake, pamoja na mambo mengine mengi! Ndoto ya Yusufu HAIWAKILISHI TAMANIO LA BINAFSI YAKE, eti aje kuwa Mkuu wa Misri! Jambo kama hilo halionekani na wala halijitokezi katika Biblia.

Vivyo hivyo Mungu hasemi, “Uwe na maono juu ya maisha yako ya baadaye.” HAKUNA SEHEMU YOYOTE ya Biblia inayokuhimiza “ujitengenezee maono ya maisha yako ya baadaye”.

Kama nilivyosema, mafundisho haya hayatofautishi kati ya “shauku zetu binafsi” (‘ndoto’ au ‘maono’ au ‘mtazamo’) kwa ajili ya maisha yetu yajayo na “mapenzi ya Mungu” kwa ajili ya maisha yetu. Na hiki ndicho wahubiri siku hizi wanachofanya – wanatumia kilichotokea, kwa mfano, kwa Yusufu, mwana wa Yakobo, kwenye haja na matamanio binafsi!

Rafiki, kama huelewi au hutambui utofauti kati ya mambo haya mawili, fuate onyo la mtume Paulo katika Warumi 12:1,2 na ujifunze ukweli wa maneno ya Mungu hayo:

“Hili ndilo asemalo BWANA: ‘Mwenye hekima asijisifu katika hekima yake au mwenye nguvu asijisifu katika nguvu zake au tajiri asijisifu katika utajiri wake, Lakini yeye ajisifuye na ajisifu kwa sababu hili: Kwamba ananifahamu na kunijua mimi, kwamba mimi ndimi BWANA, nitendaye wema, hukumu na haki duniani, kwa kuwa napendezwa na haya,’ asema BWANA.” (Yer.9:23,24).

Mungu alimuahidi Abrahamu mtoto. Abrahamu alisubiri kwa muda mrefu sana ili ahadi hiyo iweze kutimia. Alikuwa bado akisubiri hata pale Mungu alipomtokea kwenye Mwanzo 15 na kusema,

‘Usiogope Abramu: mimi ni ngao yako, na ni thawabu yako.’

Abramu alikuwa na hofu kwamba bado hakuwa na mtoto, lakini Mungu alimwambia, ‘Mimi ndiye thawabu yako.’ Je hii ni kweli kwangu mimi na wewe, mpendwa msomaji? Unamuhesabu Yesu Kristo kama thawabu yako kubwa, kuliko kitu kingine chochote? Je, Yeye ni wa thamani kwako kuliko hata karama zako au mwito wako? Je, Yeye ni thawabu kubwa kwako kuliko ‘ndoto’ na ‘matamanio’ yako? Kama sivyo, anawezaje kukutumia?

Mungu alimpa Ibrahimu mtoto, jina lake Isaka. Mungu alitimiza ahadi yake kwa wakati wake na kwa njia zake. Wakati Isaka bado akiwa mdogo, Mungu akamwambia Ibrahimu amtoe sadaka ya kuteketezwa. Ibrahimu hakusita. Asubuhi na mapema Ibrahimu aliamka kumchukua mtoto kwenye eneo la kutolea sadaka – eneo ambalo hapo baadaye Yesu Kristo alikuja kusulubiwa. Tunahitaji kuelewa ni jinsi gani ile dhabihu ilikuwa kubwa kwa Ibrahimu. Si tu Isaka mwanae wa pekee aliyepewa kimuujiza na Mungu, lakini Mungu aliahidi kutengeneza taifa kupitia kwa Ibrahimu na kwamba uzao wake utakuwa kama nyota za angani! Mungu alimuahidi Ibrahimu kwamba jamaa zote za dunia zitabarikiwa kupitia yeye na uzao wake! Kwa hiyo ahadi za Mungu kwa baraka zijazo ambazo zingekuja kukamilishwa kupitia Isaka, na Ibrahimu si kwamba tu alimtoa mwanae wa pekee, ambaye alimpenda, lakini pia kumtoa kama dhabihu ya ahadi zote ambazo Mungu alimuahidia, kama Isaka angekufa, ahadi ya Mungu pia ingekuwa imechinjwa!      

Inakuwaje kwako? Uko tayari kuweka kando mipango yako binafsi, matamanio ama ndoto yako kwa hili ama kwa lile ’kwenye madhabahu’ na kusema, si mapenzi yangu bali ya kwake ndiyo yafanyike! Je, uko tayari ‘kuachilia’ yale unayotaka kufanya, ama yale unayoyawaza kwamba Mungu amekupangia, na umuache yeye ‘afufue’ kile alichokichagua kwa ajili yako? Ibrahimu, alipokwenda kumtoa Isaka, aliwaambia wajakazi wake wasubiri wakati yeye anaenda ‘kuabudu’. Je, unaweza kumuabudu Mungu kwa njia hii – kumfanya yeye ngao yako na thawabu yako kuu, kumpenda yeye kuliko huduma yoyote ama mafanikio ambayo umekuwa ukiyaota? Je, mambo mengine yanaonekana kama si kitu kwako ukilinganisha na kumjua yeye na kumpenda yeye na kutembea katika njia zake? Kama sivyo, atawezaje kukutumia? Kama sivyo, Mungu atawezaje kuwabariki wengine kupitia wewe? Kama ‘tutamwabudu’ Mungu kwa jinsi hii, hatutapoteza! Mungu mwenyewe atatupa kile kitakachotubariki kwelikweli na kutupa njia tutembee na kubariki wengine!  

Wapendwa, nayaandika hayo kwa sababu tunaishi “wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo.” (2 Tim.4:3,4).

Hayo ni mambo potofu ya wahubiri wa leo. Uwe makini nao unapopata fursa ya kuwasikiliza. Usilipokee fundisho lao. Usifuate ukubwa wa muhubiri au umaarufu wake katika ulimwengu huu unapomsikiliza mhubiri yeyote yule, bali uangalie ukuu wa Mungu. Jihoji, je, asemavyo mtu huyu ndivyo inenavyo Biblia. Kwa tabia ya kujihoji namba hii utapona na uharibifu wa nyakati hizi za manabii hawa wadanganyao nyakati hizi za mwisho.

Mungu tusaidie tuwe wafuasi kweli kweli wa Bwana Yesu.

© David Stamen 2015  http://www.somabiblia.com

 UNAWEZA KUDOWNLOAD SOMO HILI KWA LINK HIYO: Yesu hakufa kuitimiza ndoto yako.

UNAWEZA KUSOMA MAKALA NYINGINE JUU YA NDOTO KWA LINK HAPO CHINI:

https://somabiblia.wordpress.com/je-unatafuta-ndoto-zako-au-mapenzi-ya-mungu/

 RUDI HOMEPAGE

 

2 responses to “Bwana Yesu Kristo hakufa Msalabani ili atimize Ndoto Yako

  1. Pingback: somabiblia
  2. ENOCK NGALLUPELAH

    October 6, 2015 at 5:38 pm

    Ilike this leson

     

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

 
%d bloggers like this: