RSS

DAMU YA YESU SIO HIRIZI.

Katika Agano Jipya hutakutana na mafundisho ambayo yalienezwa na watu wengi, yaani, yakiagiza kuwa ni lazima, halali au vizuri ‘kuitumia’ damu ya Yesu ili kuweka ulinzi kwenye nyumba yako, shamba lako, gari lako, ofisi yako, biashara yako au kuwafunika watu wa nyumba yako kila wakati nk! Watu wengi wa leo wanadai eti, ukifunika vitu vyako kwa damu ya Yesu kwa imani adui hawezi kuja kuvigusa, maana huo ni ulinzi wa hali ya juu. Mambo hayo yote siyo kweli. Hamna msingi katika Agano Jipya. Ni jambo la ushirikina tu. Maombi ya namna hiyo ni matupu na bure. Hamna hata mstari mmoja unaofundisha juu ya jambo kama hili katika Agano Jipya. Ni wapi? Tafuta katika Agano Jipya, chunguza – na ukipata mstari mmoja na fundisho hili katika Agano Jipya, tuambie. Watu hawasomi Biblia vizuri. Wanachanganya Agano la Kale na Agano Jipya kabisa bila kufikiria maana ya mambo yale wanayoyasoma.

Yesu Kristo alimwaga damu yake kwa ajili ya ukombozi wetu – tumekombolewa na damu ya Yesu. (Waefeso 1:7; Wakol.1:20; 1 Petro 1:19; Ufunuo 5:19; Waebr.9:12).

Tumehesabiwa haki katika damu yake (Warumi 5:9).

Yesu ni upatanisho wetu kwa njia ya imani katika damu yake (Warumi 3:25).

Yesu alituosha dhambi zetu katika damu yake (Ufunuo 1:5).

Kupitia damu ya Yesu tumesamahewa dhambi zetu zote (Mathayo 26:28; Warumi 3:25).

Kwa damu yake Yesu ameziondoa dhambi zetu zote (Mathayo 26:28; Waebr.10:4).

Damu ya Yesu yatusafisha dhambi yote.(Waebr.9:14; 1 Yoh.1:7; Ufunuo 1:5; 7:14).

Bwana Yesu ametutakasa kwa damu yake (Waebr.13:12).

Kwa damu yake mwenyewe Yesu aliingia mara moja tu katika patakatifu, ndio maana sisi tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu, yaani, uwepo wa Mungu katika Roho. (Waebr.9:12; 10:19).

Kutokana na mistari hiyo hapo juu ni wazi damu ya Yesu inahusu wokovu na ukombozi wetu tu, hasa inahusu kuondolewa kwa dhambi zetu ili tusamehewe, tusafishwe na tutakaswe. Waandishi wa Agano Jipya hawataji wala hawafundishi juu ya kuitumia damu ya Yesu, au ‘kuvifunika vitu, ili kuweka ulinzi kwenye nyumba yetu au mashamba yetu! Hamna! Wakristo hawakufanya hivyo. Hawakuitumia damu ya Yesu kama hirizi!

Lipo fundisho mmoja zaidi juu ya damu ya Yesu katika Agano Jipya, yaani, Yesu alisema, “Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu… Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake.” (Yoh.6:53,56). Hatuna nafasi sasa kuingia katika maelezo ya mstari huo, lakini nanukuu mistari mitatu zaidi ili itusaidie.

 “Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi”

“Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo?”

“bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.” (Mathayo 26:27,28; 1 Wakor.10:16; 1 Yohana 1:7).

Sawasawa na maneno hayo tunatambua kuwa damu ya Yesu inawakilisha uzima Wake (ndani yetu). Sitasema mengi juu ya mistari hiyo sasa, lakini mistari hiyo inagusa ukweli wa ushirika wetu wa kiroho na Bwana. Kwa nini watu wanapenda sana kusisitiza mambo ya nje, ya kimwili, yasiyofaa badala ya kuwalisha waumini chakula cha kiroho!!!

Lakini wazo kuwa tunaweza kufunika nyumba yetu, vitu vyetu, watu wengine au sisi wenyewew na damu ya Yesu ili itulinde na adui, hamna! Hiyo ni jambo la ushirikina tu.

Je, Agano la Kale linasemaje kuhusu jambo hili muhimu? Je, watu wa Agano la Kale walikuwa na desturi katika maisha yao ya kila siku kuweka damu ya mwanakondoo katika miimo ya milango yao ili kuwalinda dhidi ya maadui zao au kutoka kwa shetani? Hapana, wao hawakufanya hivyo hata mara moja. Kulikuwa hakuna kabisa desturi kama hiyo wala kulikuwa hakuna kabisa fundisho la aina kama hiyo katika Agano la Kale. Haikutokea hata mara moja katika maisha ya kila siku ya Waisraeli ambapo waliweka damu ya kondoo katika nyumba zao au hata mashamba yao, ili kuwalinda dhidi ya maadui zao au dhidi ya nguvu ya shetani.

Watu wanachanganya maandiko na wanashindwa kuyaelewa. Tazama hivi ndivyo ilivyotokea katika Agano la Kale. Usiku ule Mungu alikuwa anaenda kuwahukumu watu Wamisri kwa kuwaua watoto wao wa uzao wa kwanza na kuwakomboa Waisraeli wapate kutoka Misri na kuondokana na nguvu za Pharao. Mungu aliwaagiza watu wake Israel kupaka damu ya kondoo kwenye miimo ya milango ya nyumba zao, ili kuwaonyesha kuwa hiyo ilikuwa ni alama kuwa Israel ni watu wake Mungu. Ilikuwa sio shetani anayekwenda kuipiga Misri! Alikuwa ni Mungu anaenda kuipiga Misri kwa kuwaua wazaliwa wa kwanza wote katika nchi yote ya Misri katika hukumu. Basi pale Mungu alipoiona damu ya mwanakondoo katika miimo ya milango ya nyumba zao aliiacha au aliipita nyumba ile na wala hakuwachinja watu wake katika nyumba hiyo. (Tukio hili liliitwa ‘pasaka’, yaani, ‘kupita’, kwani Mungu ‘alipita’ nyumba za watu Wake.) Wayahudi walipaswa kuchinja mwana kondoo na kuioka nyama yake na kuila pamoja na mkate usiotiwachachu, waile nyama hiyo usiku huohuo, na kujiandaa au kukaa tayari kwa kuondoka usiku huo kutoka Misri. Hiyo ndiyo ilikuwa ni mara yao ya pekee kwa Waisraeli kupaka damu ya mwanakondoo katika miimo ya nyumba zao. Na hiyo haikuwa ni kinga yao ya kujilinda dhidi ya adui, au kuwalinda dhidi ya nguvu za shetani, bali ilikuwa ni ulinzi wao dhidi ya hukumu ya Mungu ambayo ilikuwa inapita juu ya nchi nzima ya Misri! Waliweka damu hiyo ya kondoo katika miimo ya milango ya nyumba zao siku hiyo tu ya pasaka na wala hawakuweka hivyo tena siku nyingine yoyote – na hii ilikuwa inawalinda tu dhidi ya hukumu ya Mungu siku ile tu.

Siku ile Mungu alikuwa anaenda kuangamiza uwezo na nguvu za Pharao (kwetu sisi leo jambo hili ni picha halisia au ni mfano wa ukombozi wetu kutoka nguvu za shetani). Mungu alikuwa anaenda kuwakomboa watu wake kutoka kwenye utumwa na vifungo (kwetu sisi leo inawakilisha ukombozi kutoka katika utumwa na vifungo vya dhambi – Kutoka 13:3). Hii iliitwa ni ‘pasaka’ na ilikuwa inawakilisha kile ambacho Mungu alikuwa anaenda kukifanya kupitia kifo cha Mwanae pale Kalvari! Siku ile wana wa Israel walikombolewa kutoka kwenye hukumu ya Mungu na wakakombolewa kutoka kwenye nguvu za Pharao (shetani) kwa kupitia kifo cha mwanakondoo na kupitia damu ya mwanakondoo. Kwa kupitia matukio hayo yote Mungu alitutaka sisi tuone na kuelewa kwa njia iliyo ya wazi zaidi kile ambacho angalikwenda kukifanya kupitia mwanae Yesu Kristo katika kutukomboa dhidi ya nguvu ya shetani na utumwa wa dhambi.

Hivyo ndivyo tunavyosoma kwenye Warumi 5:9, “Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye.” Kama tulivyoonyeshwa kupitia mifano ya Kitabu cha Kutoka, vivyo hivyo sasa tunaelewa Bwana Yesu ametuokoa na hukumu ya Mungu na ghadhabu itakayokuja. (Warumi 5:16,18; 1 Wathess.1:10).

Na tena tunasoma, “Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, awaache huru wale ambao kwamba maisha yaoyote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa” (Waebramia 2:14,15).

Kwa vyovyote vile tungeweza kunukuu mistari mingi kadiri iwezekanavyo, lakini hii michache tuliyoionyesha ifae tu kutuonyesha sisi jinsi gani siku ile ya Pasaka inavyoshabahiana na ukombozi wetu katika Kristo. Hakuna popote pale katika Bibilia ambapo watu wa Mungu wanatumia au wanaomba damu iweze kufunika mali zao ili kuwalinda dhidi ya adui yoyote yule au dhidi ya shetani. Hapapo mahala popote ambao jambo kama hili lilifundishwa, ilikuwa ni siku ile ya Pasaka tu, damu ilipakwa kwenye miimo ya milango ya nyumba zao, ili kuwalinda watu wa Mungu kutokana na hukumu yake Mungu mwenyewe juu ya Wamisri – lakini Waisraeli wao wenyewe waliokolewa!

Damu haikuendelea kutumika tena katika matumizi ya maisha yao ya kila siku ili kujilinda dhidi ya adui. Hapana, haikutumika hivyo! Na sasa, hatutakiwi ‘kuvifunika’ vitu vyetu kwa damu ile ambayo sisi tulikombolewa nayo kana kwamba ‘itavilinda’. Imeandikwa, “Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo.” (1 Wakor.5:7). Kwa hiyo, usitumie damu ya ukombozi wetu kufunika vitu vya dunia! Yesu mwenyewe ameshamwagika damu yake msalabani kwa ajili yetu!

Katika kitabu ya Waebrania mwandishi pale anatuambia hivi, “basi si zaidi damu yake Kristo, …itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu…? Na kwa sababu hii ni mjumbe wa Agano Jipya, ili, mauti ikiisha kufanyika kwa kukomboa makosa yaliyokuwa chini ya agano la kwanza, hao walioitwa waipokee ahadi ya urithi wa milele. Maana agano la urithi lilipo, lazima iwepo mauti yake aliyelifanya. Kwa maana agano la urithi lina nguvu palipotukia kufa kwa mtu; kwa kuwa halina nguvu kabisa, akiwa yu hai yeye aliyelifanya. Kwa hiyo hata lile la kwanza halikuanzwa pasipo damu. Maana kila amri ilipokwisha kunenwa na Musa kwa hao watu wote, kama ilivyoamuru sheria, aliitwaa damu ya ndama na ya mbuzi, pamoja na maji na sufu nyekundu na hisopo, akakinyunyizia kitabu chenyewe, na watu wote, akisema, Hii ni damu ya agano mliloamriwa na Mungu. Na ile hema nayo na vyombo vyote vya ibada alivinyunyizia damu vivyo hivyo. Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo.” (Waebr.9:14-22).

Hapa mwandishi anamrejesha msomaji nyuma katika kitabu cha Kutoka 24:6-8, mahala ambapo Mungu alianzisha Agano lake na watu wake kupitia Musa. Ili kulikamilisha Agano lile, damu ya dhabihu zilizotolewa ilinyunyizwa, sio juu ya nyumba zao wala mashamba yao ili kuwalinda dhidi ya maadui, bali ilinyunyizwaa maeneo mbalimbali ya hema au hekalu ili kuwasafisha watu wale tayari kwa ajili ya huduma ya Mungusiyo ili kuwalinda dhidi ya adui!  Hapa tena hayo yote yanawakilisha kwetu kuona kile ambacho Kristo alikuwa anaenda kukikamilisha kwa ajili yetu kupitia kifo chake. Kupitia damu yake Yesu na kifo chake sisi tumepokea msamaha yaani tumesamehewa na kusafishwa. Tumeingizwa katika mahusiano ya kiagano na Mungu mwenyewe, kupitia damu ya Mwanawe! Kama vile Yesu mwenyewe alivyosema, “hii ndiyo damu yangu ya agano jipya, imwagikayo kwa ajili ya wengi.” (Marko 14:24).

Mahali pa kukaa kwake Mungu ni kitu gani kwa sasa! Je ni lile hekalu! Hapana! Sisi tuliokombolewa na Mungu tumefanyika kuwa ndio makazi ya Mungu kupitia Roho wake Mtakatifu, na tumefanywa kuwa hekalu lake takatifu (Waefeso 2:22, 1Wakor. 6:19). Tumeoshwa kwa damu ya Yesu Kristo. Hapo sasa Agano la Kale linatupatia picha ya uwazi kabisa juu ya kile Mungu alichokuwa anaenda kukifanya kwa ajili yetu kupitia Mwanae. Mungu alikuwa hawaagizii maelekezo Waisraeli jinsi au namna ya kutumia hirizi (ushirikina) katika kulinda mali zao. Lakini sasa, hivyo ndivyo ilivyo leo, watu wanafundisha hivyo! Wanajaribu kuitumia damu ya Yesu kama vile ni Hirizi ya uchawi fulani au dawa ya ushirikina. Jambo hili hatulioni popote katika Biblia. Kwa nini sasa watu wanafundisha mambo hayo ambayo hayaleti maana yoyote, mambo ya ujinga tu? Aina hii ya maombi, eti kuitaka damu ya Yesu ifunike kulinda na kufunika mali zetu, haina maana yoyote ile katika kizazi hiki cha Agano Jipya na wala katika ulimwengu wa Bibilia  na wa historia ya watu wa Mungu – hiyo ni uchafuzi na ni matumizi mabaya tu ya damu ya Yesu.

Kwa nini watu hulifanya jambo kama hili? Je, itakuwa ni kwa sababu katika fikra zao wanashawishiwa na mifumo ya desturi ya uchawi ambayo wengi wao wamekulia huko? Sijui! Lakini hii ni uchafuzi wa kile Biblia yenyewe inavyofundisha.

“Mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo.” (1 Petro 1:18,19).

Damu ya Yesu ni yenye thamani. Yesu Kristo alilipa gharama kubwa sana kwa ajili ya wokovu wa roho zetu – na sio kwa ajili ya wokovu wa nyumba yako, mashamba yako au biashara yako. Tumekombolewa, tumesamehewa, na kutakaswa kwa damu yake ya thamani. Mpendwa msomaji wa makala hii, usiongozwe na mawazo ya kiushirikina kwa kuyafuata mafundisho ya uwongo wa namna hiyo unayofundishwa. Mafundisho ambayo yanaibadili damu ya Yesu ionekane kana kwamba ni aina ya Hirizi ya maisha ya watu, mashamba, nyumba au biashara zao!

Kama wewe umekwisha kombolewa kwa damu yake Yesu, basi sasa wewe u wake Yesu Kristo! Kisha upo salama ndani yake yeye! Damu yake ambayo ilitukomboa yatufanya tuwe salama katika yeye dhidi ya yule mwovu – Ufunuo 12:11. (Usisahau kuwa damu ya Yesu ni inawakilisha pia ushirika wetu naye na uzima Wake ndani yetu kama tulivyoona hapo juu.) Mungu ni Mungu, na Yeye anaweza kutulinda na kututunza sawasawa na Neno Lake – bila sisi kutumia mambo yale ya ushirikina ambayo hayafundishwi katika neno lake na ambayo hayampendezi! Kuna ahadi nyingi zenye thamani kwenye neno la Mungu, zikuhusuzo wewe na mimi! 

“Naye ni nani atakye wadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema…..Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?” (1 Petro 3:13, Warumi 8:31). Na tena, “Kwa maana ulikuwa kimbilio langu, Ngome yenye nguvu adui asinipate… Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. (Zaburi 61:3; 46:1).

Kuna mistari mingine mingi ya neno la Mungu ambayo inatutia moyo kuhusiana na upendo wa Mungu na ulinzi wake kwetu. Basi, ni vema kumwamini Mungu na kutii neno lake kuliko kufuata mambo ya kishirikina ambayo kwanza hayaungwi mkono popote katika Biblia na wala hayawezi kukusaidia chochote katika mali zako pia.

Kama wewe unatembea na Bwana na katika ushirika na yeye na kuyakabidhi maisha yako kwake (Warumi 12:1,2), ndipo sasa hakuna tena sababu ya KUOMBA ulinzi wake kila siku kwa ajili yako na kwa ajili ya vitu ulivyo navyo. Kumtegemea kwetu Mungu kuwe ni tabia ya mioyo yetu, na hili tegemeo letu, hii imani tuliyonayo mioyoni mwetu ihusuyo wema wa Mungu ni jambo la pekee linalomfurahisha yeye (Waebr 11:6). Ndiyo, kwa vyovyote vile tunapokuwa tunakutana na aina fulani ya hatari au hali ngumu katika mapito yetu, basi inakuwa ni vema kujikabidhi sisi wenyewe na vile tulivyonavyo kwa Bwana, lakini haitupasi kufanya hivyo kwa kuifanya damu ya Yesu kuwa kama hirizi yako ili kupona dhidi ya magumu unayopitia au kulinda maisha yako, nyumba yako, na mali zako. Kwa kufanya mfumo wa namna hii katika maisha ya ukristo basi linakuwa ni tendo la ushirikina.

Pia uwe mwangalifu, kwa sababu kuomba kwako kutokane na matumaini yako kwa Mungu. Ninachomaanisha hapa ni hiki – watu wengine wanaweza wakawa waoga kila siku wakidhania kuwa jambo fulani baya linaweza kuwatokea na kwa hiyo wanakimbilia kuomba kwa ajili ya ulinzi wao mara zote wanageuka na kuonekana kama vile ni aina fulani ya utumwa. Maombi ya aina hii ni kuomba kunakotokana na hofu yako tu! Na huko ndiko kutokuamini. Mungu alishasema wazi kuwa, “Mnalindwa na nguvu za Mungu aliye hai.” Na Paulo anaomba kwa ajili ya waumini, “Basi Mungu wa tumaini na awajaze ninyi furaha yote na amani katika kuamini, mpate kuzidi sana kuwa na tumaini, katika nguvu za Roho Mtakatifu.” (Warumi 15:13). Kwa sababu ya kupungukiwa na mahusiano yako na Mungu na kumtegemea Mungu kwa ukweli, ndipo hofu na kutokuamini kunachukua nafasi katika maisha yako kisha inakufanya uombe kwa ajili ya ulinzi nyakati zako zote. Kama jambo hili liko namna hiyo katika maisha yako, basi namna ya kufikiri kwako kunapaswa kubadilika.

Jikabidhi kwa Mungu na umtegemee yeye! Na amani yake pamoja na furaha ijazwe ndani yako kadiri unavyoendelea kumpenda na kumtumikia.

© David Stamen 2016    http://www.somabiblia.com

KUPAKUA SOMO HILI BONYEZA LINK HAPO CHINI:

damu-ya-yesu-sio-hirizi

 

Comments are closed.

 
%d bloggers like this: