RSS

NENO KWA AJILI YA VIONGOZI WA IBADA WAIMBAJI NA WANAMUZIKI

KANDO YA MITO YA BABELI: NENO KWA AJILI YA VIONGOZI WA IBADA WAIMBAJI NA WANAMUZIKI NDANI YA KANISA LA BWANA.

“Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi, Tukalia tulipoikumbuka Sayuni. Katika miti iliyo katikati yake Tulivitundika vinubi vyetu. Maana huko waliotuchukua mateka Walitaka tuwaimbie; Na waliotuonea walitaka furaha; Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni. Tuuimbeje wimbo wa Bwana Katika nchi ya ugeni? Ee Yerusalemu, nikikusahau wewe, Mkono wangu wa kuume na usahau. Ulimi wangu na ugandamane Na kaakaa la kinywa changu, nisipokukumbuka. Nisipoikuza Yerusalemu Zaidi ya furaha yangu iliyo kuu. (Zaburi 137: 1 – 6).

Kabla hatujaangalia hii mistari ambayo tumetoka kuinukuu natamani tuangalie mistari michache mingine kama utangulizi, alafu tutakuja kwenye moyo wa ujumbe wangu wa leo kwa Kanisa la Yesu Kristo kwenye nchi yetu, hususa viongozi wa ibada, waimbaji na wanamuziki.

Naomba ieleweke kuwa hapa sizungumzi na tasnia ya Muziki wa Injili, maana huo sasa ni biashara kama muziki wa aina nyingine yoyote na nisingependa kuingilia wanachokifanya. Sizungumzi na matamasha na makongamano ya muziki wa Injili. Nisingependa kukubaliana nao au kuwapinga. Labda siku nikiwa na uhakika kuwa nimesikia neno wazi na bayana toka kwa Bwana kuwahusu ndo nitazungumza.

Nataka nizungumze na Kanisa, viongozi wa ibada, waimbaji na wanamuziki hasa mkazo wangu ukiwa kwenye uimbaji na muziki kama ibada ambayo ndo tunauita Sifa na Kuabudu. Kabla sijasema kile ambacho ninaamini Mungu ameniwekea moyoni katika nuru ya mistari ambayo nimetoka kuinukuu, embu tupite kwenye mistari michache ili kwanza tuone nguvu ya Sifa na Kuabudu kama ikifanyika vile Mngu amekusudia ifanyike.

 “Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao, Na upanga mkali kuwili mikononi mwao. Ili kufanya kisasi juu ya mataifa, Na adhabu juu ya kabila za watu. Wawafunge wafalme wao kwa minyororo, Na wakuu wao kwa pingu za chuma. Kuwafanyia hukumu iliyoandikwa; Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wake wote. Haleluya.” ( Zaburi 149: 6 – 9).

Pale tutakapofika mahali ambapo Sifa Kuu za Mungu zipo vinywani mwetu, na upanga mkali (Neno la Mungu kwa mujibu wa Waebrania 4:12 na Efeso 6:17) upo mikononi mwetu, Kanisa la Yesu kupitia Kusifu na Kuabudu litaanza kufanya kisasi cha Mungu juu ya mataifa, yaani maadui wa Mungu, na kuachilia adhabu ya Mungu juu ya kabila za watu. Kanisa kupitia sifa na kuabudu litaanza kuwafunga wafalme kwa minyororo na wakuu kwa pingu za chuma. Tutaanza kuwafanyia mapepo na nguvu za giza katika ulimwengu wa roho hukumu iliyoandikwa. Hii ndo heshima ambayo Mungu ameiweka kwa ajili ya Kanisa kupitia Sifa na Kuabudu.

Maandiko yanatuambia:

“ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho.” ( Efeso 3:10).

Mungu kwa njia ya Kanisa anataka kuwajulisha falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho hekima yake iliyo ya namna nyingi na mojawapo ya hekima hiyo ni wajue nguvu za Mungu za ajabu zinazoachiliwa kupitia Sifa na Kuabudu.

Wakati Mfalme Yehoshafat alipovamia na mataifa matatu, mkakati wa kivita ambao Mungu alimpa Yehoshafat wa kumshinda adui ulikuwa na kipengele cha Sifa na Kuabudu ndani yake.

“Naye alipokwisha kufanya shauri na watu, akawaweka wale watakaomwimbia BWANA, na kumsifu katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi, na kusema, Mshukuruni BWANA; kwa maana fadhili zake ni za milele. Nao walipoanza kuimba na kusifu, BWANA akaweka waviziao juu ya wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja juu ya Yuda; nao wakapigwa. Kwani wana wa Amoni na wa Moabu waliwaondokea wenyeji wa mlima Seiri kuwaulia mbali na kuwaharibu; nao walipokwisha kuwakomesha hao wakaao Seiri, wakajitia kuharibu kila mtu mwenziwe. Hata Yuda walipofika mnara wa kulindia wa jangwani, wakalitazama hilo jeshi; nao, angalia, walikuwa maiti walioanguka nchi, wala hapana aliyeokoka. (2 Nyakati 20: 21- 24).

Pamoja na kwamba Yehoshafati na Yuda walikuwa wamevamiwa na Wamoabu, Waamoni na Wameuni, mataifa matatu makali mno katika vita, waliambiwa na Mungu kuwa hawatakuwa na haja ya kupigana bali wajipange na wasimame katika zamu yao na walifanya hivyo kwa njia ya kutanguliza mbele vitani waimbaji na wapigaji watakaomwimbia Bwana katika kumsifu na kumshukuru. Walipokuwa wakifanya hivyo, kumsifu Bwana katika uzuri wa utakatifu Wake, maandiko yanasema kuwa Mungu aliwatuma waviziao (malaika), maadui wakaanza kujimaliza wao wenyewe kwa wenyewe. Yuda walipofika kwenye kambi ya adui wakakuta maadui zao wamekuwa maiti wote na wala hapana hata mmoja aliyeokoka. Hii ndo nguvu ya ajabu ya Sifa na Kuabudu kama Mungu alivyoikusudia.

Shida ibada yetu, sifa yetu, na kuabudu kwetu kumeingiliwa na udunia mwingi kiasi kwamba nguvu iliyo ndani ya ibada, sifa na kuabudu imepotea katika kanisa.

Tumebaki na mapokeo ya ibada, sifa na kuabudu ambayo yamenyang’anya hii kitu nguvu za Mungu zilizo ndani yake. Wana wa Israeli walipovuka mto Yordani kuingia nchi ya ahadi, ngome ya kwanza ambayo walikutana nayo ni ngome ya Yeriko. Huu ulikuwa ni mji ambao umezungushiwa ngome kubwa sana na adui na ilikuwa ni muhimu sana kwa wana wa Israeli kuuteka huu mji kwanza kabla ya mji mwingine wowote katika nchi ya ahadi. Bibilia inatuambia kuwa:

“Basi Yeriko ulikuwa umefungwa kabisa kwa sababu ya wana wa Israeli; hapana mtu aliyetoka wala hapana mtu aliyeingia. ( Yoshua 6:1).

Pamoja na kwamba huu mji ulikuwa umefungwa kwa kiwango hiki, mkakati ambao Mungu aliwapa wana wa Israeli kuuchukua huu mji ulikuwa ni mkakati wa sifa. Aliwaambia wauzunguke huu mji mara moja kwa siku sita wakiwa kimya, siku ya saba wauzunguke mara saba, na mara ya saba wapige kelele za shangwe. Walipofanya hivyo kuta za ule mji zilididimia kuingia ardhini na wana wa Israeli wakauchukua huo mji. Haikuwa tu zile kelele za shangwe ambazo ziliwapa kuuchukua ule mji, sanduku la Agano, yaani uwepo wa Mungu ulikuwa pamoja nao. Sifa na kuabudu ni kitu kimoja cha nguvu sana kama kikifanyika katika uzuri wa utakatifu Wake.

Paulo na Sila walipotupiwa gerezani, mnapo usiku wa manane wakaanza kusali na kumwimbia Mungu nyimbo za sifa, na bibilia inasema wafungwa wote wakawa wakiwasikia. Maandiko yanasema mara kukaja tetemeko likatikisa misingi ya gereza, milango ikafunguka na vifungo vya wote vikalegezwa. Hii sasa ndo sifa na kuabudu inavyotakiwa kuwa miongoni mwa watu wa Mungu. Sifa na kuabudu inatakiwa kumleta Mungu katikati yetu, na ajapo misingi ya kila gereza itatikiswa, milango itafunguka na vifungo vya wote vitalegezwa. Sio hivyo tu, wokovu ulikuja kwa mkuu wa gereza pamoja na familia yake nzima kupitia Sifa na Kuabudu. Pale tunapomsifu Mungu katika uzuri wa utakatifu Wake tutaona misingi ya magereza mengi ambayo imekamata wanadamu ikitikiswa na malango yake yakifungula na vifungo vya wote vikifunguka. Wakuu wa haya magereza ambao mara nyingi ni wachawi na waganga na mawakala wa shetani, watamjua Mungu wetu na kuokoka.

Kuna maandiko mawili nikiyasoma yananipa faraja sana:

“Siku hiyo nitaiinua tena maskani ya Daudi iliyoanguka, na kuziba mahali palipobomoka; nami nitayainua magofu yake, na kuyajenga kama siku za kale; wapate kuyamiliki mabaki ya Edomu, na mataifa yote yaitwayo kwa jina langu, asema BWANA, afanyaye hayo.” (Amosi 9:11,12).

“Baada ya mambo haya nitarejea, Nami nitaijenga tena nyumba ya Daudi iliyoanguka. Nitajenga tena maanguko yake, Nami nitaisimamisha; Ili wanadamu waliosalia wamtafute Bwana, Na mataifa yote ambao jina langu limetajwa kwao.” (Matendo ya Mitume 15:16,17).

Ukiiangalia hii mistari miwili unaona Mungu akisema kuwa ataenda kuinua tena maskani ya Daudi na kujenga maanguko yake. Mungu anasema kuwa ataenda kuisimamisha tena kama ilivyokuwa katika siku za kale. Atakapofanya hivyo anasema watu wake wataenda kuyamiliki mabaki ya Edomu. Kitu kitakachoenda kuachiliwa wakati maskani ya Daudi itakapojengwa tena ni uwezo wa kumiliki milki zetu kama Kanisa pamoja na mmoja mmoja. Sio hivyo tu lakini mataifa ambayo Jina Lake limetajwa kwao watainuka na kuanza kumtafuta Bwana. Kwa maneno mengine kutaachiliwa wimbi kubwa sana la wokovu.

Tunasoma katika maandiko wakati Roho Mtakatifu alipoanguka juu ya Kanisa, sifa na kuabudu ilipata nguvu sana na ikawa ni moja ya chachu kuu za kuachilia ongezeko katika Kanisa.

“wakimsifu Mungu, na kuwapendeza watu wote. Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa.”  (Matendo 2:47).

Unaona jinsi ambavyo walipokuwa wakimsifu Mungu walipata kibali kwa watu wote? Na kwa sababu hiyo, Bwana akalizidisha Kanisa kila siku kwa wale waliyokuwa wakiokolewa na chachu iliyosababisha mavuno hayo ya ajabu ilikuwa ni sifa na kuabudu. Tunapozungumzia Maskani ya Daudi, tunazungumzia moja ya majengo matatu ya ibada ambayo yalikuwepo katika Agano la Kale. Wengi tunaifahamu hema au maskani ya Musa na Hekalui la Sulemani, lakini wachache sana tunaifahamu maskani ya Daudi. Daudi aliinua hii maskani ili dhabihu ya sifa na ibada iweze kufanyika hapo masaa 24 kwa siku. Tofauti kubwa ambayo ilikuwepo kwenye jengo hili ukilinganisha na mengine mawili, hapakuwa na dhabihu za wanyama na sadaka za unga na vyakula bali dhabihu zilizotolewa hapo zilikuwa za Sifa na Kuabudu masaa 24 kwa siku.

Kulikuwa na familia tatu ambazo zilipewa wajibu wa kusimamia hilo. Asafu na wanawe, Hemani na wanawe, na Yeduthuni na wanawe. Hawa hawakuwa tu wastadi katika kuimba na kupiga vyombo vya muziki bali pia walikuwa wanaimba kinabii na kupiga vyombo kinabii. Maskani ya Daudi ilikuwa imezungukwa na uimbaji na upigaji wa vyombo wa kinabii. Roho wa Mungu alikuwepo katika uimbaji wao na upigaji muziki wao. Walitabiri kwa kuimba na kwa kupiga vyombo vya muziki. Uimbaji na upigaji wa muziki ulishikilia uwepo wa Mungu uliyo dhahiri hapo kwenye maskani ya Daudi. Kulikuwa na mpangilio na kila kitu kilifanyika kwa uzuri na utaratibu bila ya kuupoteza uwepo wa Mungu uliyo dhahiri.

Sasa hiki kitu ndicho Mungu anataka akirudishe katika siku hizi za mwisho.

Kanisa tumepita mahali ambapo waimbaji na wapigaji muziki wamekuwa na ujuzi na ustadi kuliko wakati mwingine wowote lakini kiwango cha uwepo wa Mungu ambacho kinaachiliwa na uimbaji wetu na upigaji wetu wa muziki au ni mdogo sana au hakuna kabisa. Mungu anataka uimbaji wetu na muziki wetu upelekee kutikiswa kwa misingi ya magereza, kufunguliwa kwa milango ya magereza ambayo watu wamefungwa, na vifungo vya kila namna na aina vya wote ikafunguliwe. Lazima turudi katika kumsifu na kumwabudu Mungu katika uzuri wa utakatifu Wake ili tuanze kuona tena wingu la utukufu wake likiachiliwa miongoni mwa watu wake. Maandiko yanatuambia:

 “Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu, Ya kwamba atatujalia sisi, Tuokoke mikononi mwa adui zetu, Na kumwabudu pasipo hofu, Kwa utakatifu na kwa haki Mbele zake siku zetu zote.” (Luka 1:73-75).

Mungu akatujalie tuokoke kutoka katika mikono ya adui zetu ili tumwabudu pasipo hofu, kwa utakatifu na kwa haki, mbele Zake siku zetu zote. Baada ya kusema hayo ngoja turudi kwenye moyo wa huu ujumbe.

Bibilia inawazungumzia wana wa Israeli kuwa kando ya mito ya Babeli ndipo walipoketi na Biblia inasema kuwa walilia hapo walipoikumbuka Sayuni. Kwa wana wa Israeli, Babeli ilikuwa na mahali ambapo walichukuliwa mateka na kupelekwa huko kama watumwa. Kwetu sisi Kanisa Babeli sio mahali bali Babeli ni mfumo. Ni mfumo wa kidunia wa kufanya vitu. Kanisa limechukuliwa mateka na huu mfumo na kupelekwa huko kama mateka. Kanisa zaidi na zaidi linaiga namna ya dunia ya kufanya vitu na kwa kadiri linavyovutwa kufanya vitu kwa namna ya dunia linazidi kupoteza uwepo wa Mungu uliyodhihirishwa katikati yake.

Mimi napenda sana vitu vifanyike kwa ubora, uweledi, kiuvumbuzi na kwa ustadi lakini natamani vyote hivi vifanyike pasipo kuupoteza uwepo wa Mungu ndani ya Kanisa. Tumeridhika na hali ya kufanya tu vitu kwa ubora, uweledi, kiuvumbuzi na kwa ustadi bila ya kujali uwepo wa Mungu ambao ndo huo unatikisa misingi ya magereza, unafungua malango ya magereza na kufungua vifungo vya wote kama upo. Hawa wana wa Israeli kuna wakati waliridhika kabisa na kufanya ibada zao huko Babeli lakini kuna wakati wakaanza kupakumbuka Sayuni, mahali pa uwepo wa Mungu. Mfumo wa Babeli umeondoa uwepo wa Mungu katikakti ya watu wa Mungu kuliko kitu kingfine chochote. Wana wa Israeli wakaamua kutundika vinubi vyao. Wakasema kuwa hawataendelea tena kuimba nyimbo za sifa huko Babeli. Biblia inasema wale watu waliyowachukua mateka wana wa Israeli walitaka wawimbie na walitamani kufurahi na nyimbo za Sayuni.

Utakubaliana nami kuwa hata katika shughuli za watu ambao sio wa Mungu wanapiga nyimbo zetu na wanazicheza sio kwa sababu wanamchezea Mungu wetu bali kwa sababu ni nyimbo nzuri ambazo zimepigwa na kuimbwa kwa ustadi na uweledi mkuu. Kwenye mabaa na madisko siku hizi, hizi nyimbo ambazo zinaitwa za Injili zinapigwa.

Wana wa Israeli wakasema hapana.

Hawakukubali tena kuuimba wiimbo wa Bwana katika nchi ya ugeni. Wakafika mahali pa kusema kama nikikusahau wewe ee Yerusalemu, mkono wangu wa kuume usahau. Vyombo vingi vya muziki hupigwa kwa kutumia mikono. Mkono wa kuume unazungumzia nguvu. Tupo vizuri sana katika upigaji wa muziki. Ukitaka wapigaji bora wa muziki njoo kanisani utawakuta na ndiyo maana hata wanamuziki wa duniani huko wanakuja kuchukua wanamuziki kanisani huku wakiwalipa fedha nyingi wakawapigie huko na wanamuziki wa kanisani wanajitetea kuwa wanaenda kufanya kazi. Kipawa cha muziki walichopewa na Mungu wanenda kukipatia hela tena kwenye kambi ya adui.

Ni sawa tu na msichana mzuri au mwanamke mzuri aamue kutumia kipawa cha uzuri alichopewa kujipatia fedha kwa kulala na wanaume mbalimbali. Wanamuziki wa Kanisani wamekubali kulala na dunia ili waweze kujitengenezea hela na sababu yao kubwa na ugumu wa maisha. Hakuna mtu anayekubaliana na kwamba ugumu wa maisha unampa uhalali mwanamke mzuri kwenda kuuza mwili wake kwa ajili ya kupata kipato. Watauita huo ni uasherati, uzinzi, ukahaba na umalaya. Lakini hakuna mtu hata anafikiria na kuona kuwa kuchukua kipawa cha Mungu na kwenda kumwuzia shetani ili tupate hela, ni uasherati wa kiroho, uzinzi wa kiroho, umalaya na ukahaba wa kiroho. Mungu atusaidie tufunguke macho yetu na kuona uzito wa yale tunayoyafanya kwa jina la kukabiliana na ugumu wa maisha.

Wana wa Israeli wanajitamkia kuwa ulimi wao ugandamane na kaakaa la kinywa chao wasipoikumbuka Yerusalemu na kuikuza Yerusalemu zaidi ya furaha yao kuu. Tukitaka kurudi kwenye mstari embu huu ukichaa ambao umetuvamia wa kuhakalisha matumizi ya vipawa vya Mungu katika kambi ya adui uondoke. Ni kweli wanamuziki na waimbaji wanawekeza muda, fedha na mali kuweza kuwa na kiwango cha upigaji na uimbaji ambacho wanacho. Mwanamke mzuri anawekeza muda, fedha na mali ili awe na urembo aliyo nao lakini haihalalishi yeye kujiuza au kuuza huo uzuri aliyo nao. Kuwekeza kwake muda kufanya mazoezi ili mwili wake uwe vizuri, awe hana tumbo, awe na hips zilizokaa vizuri, miguu na mapaja ambayo imekaa vizuri, shepu lililokaa vizuri haimpi uhalali hata kidogo wa kwenda kujiuza ili aweze kufidia gharama za kujitunza.

Vivyo hivyo hakuna sababu nzuri ya kutosha ya kuhalalisha waimbaji na wanamuziki kwenda kuzini na shetani na dunia ili kufidia gharama za kunyanyuka kwao. Walipokuwa chini walikuwa wanyenyekevu wanaompenda Mungu sasa vipawa vyao vimeinuka na kung’aa wanaona ni sawa kwenda kumwuuzia shetani hivyo vipawa. Hii sio sawa na tukitaka kuona hili tulilolizungumza humu la nguvu ya sifa na kuabudu kurudi ndani ya Kanisa, lazima kuwe na marekebisho makubwa sana hapo. Kanisa lirudi tena kuangalia maslahi ya hawa watu maana ni watumishi kama watumishi wengine wowote. Ni watenda kazi katika mavuno kama watenda kazi wengine wowote. Wanatumika madhabahuni kwa hiyo wanahitaji pia kuwa na fungu lao hapo madhabahuni.

Maandiko yanasema kuwa mtenda kazi anastahili ujira wake. Wachungaji na viongozi wa huduma tuondoe ubinafsi wa kujiangalia tu sisi na kutowaangalia wao. Kama tunawaambia wamwamini Mungu kwa ajili ya maisha yao ya kila siku basi nasi pia tumwamini Mungu kama mfano kwao. Waimbaji na wanamuziki waangaliwe na kwenye zile huduma ambazo bado ni changa na ni ndogo basi Mungu afungue mlango kwa ajili ya watumishi hawa kupata kipato mbadala lakini sio kwenda kumwuuzia shetani vipawa vyao.

CARLOS RICKY WILSON KIRIMBAI.

 

Comments are closed.

 
%d bloggers like this: