RSS

‘HU BARIDI WALA HU MOTO’

“Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu. Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi. Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona. Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu. Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.” (UFU. 3:14-22 SUV).

Huu ujumbe wa Yesu kwa Kanisa la Laodikia kila nikiusoma naona kama unasema nasi sana Kanisa la leo hasa la Tanzania me included. Kwa kweli sisi sio baridi wala sio moto. Yaani hatusomeki kabisa. Huwezi ukasema hatujaokoka na wala huwezi kusema tumeokoka. Huwezi kusema hatujaokoka maana tunamkiri Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yetu lakini pia huwezi kusema tumeokoka maana maisha yetu, tabia zetu, mienendo yetu haiakisi kabisa kile tunachodai kwa vinywa vyetu.

Maandiko yapo wazi kuwa msingi wa Mungu wasimama imara muhuri hii kuwa Bwana anawajua walio Wake na tena kila alitajae Jina la Bwana na auache uovu. Ni heri ingejulikana moja kama tu wa baridi au wa moto.

Tumeokoka au laa.

Udunia umejaa kanisani mpaka tunashindwa kutofautisha kati ya watu wa dunia na wa Kanisa. Yaani haitusumbui hata kidogo kile ambacho Biblia inasema kuwa rafiki na dunia ni kujifanya kuwa adui na Mungu. Haitusumbui kabisa maandiko yanaposema kuwa haiwezekani kuipenda dunia na wakati huo huo upendo wa Mungu uwepo maishani mwetu. Hatuwezi kabisa kutiririka na dunia wanavyotiririka na bado tukawa na Mungu. Hilo haliwezekani hata kidogo.

Udunia wetu umemfukuza Mungu toka miongoni mwetu tumebaki na nadharia ya Mungu na maelezo mengi ya kisomi kuhusu Mungu ila Mungu Mwenyewe tushampoteza siku nyingi sana. Na Yesu yupo wazi, bayana, kinaga ubaga akisema kuwa kwa kuwa sisi sio baridi wala sio moto atatutapika tutoke kinywani Mwake. Nawaza hapa hivi nini maana ya kutapikwa tutoke kinywani Mwake? Je, ataacha kututaja mbele za Baba Yake? Sijaelewa kwa undani na uzuri anachosema Yesu hapa lakini ndani yangu ninajua kuwa kutapikwa tutoke kinywani Mwake haiwezi ikawa kitu kizuri hata kidogo.

Kanisa la leo tunajisifia utajiri wa mali hizi za huku duniani tu. Nyumba nzuri. Nguo nzuri. Samani nzuri kwenye nyumba zetu. Magari mazuri. Yaani, utajiri tu huu wa kupita ila Mungu sasa!

Tunajiona hatuna haja ya kitu hata kidogo ila Mungu anatuona tu maskini, wanyonge, wenye mashaka, vipofu ambao hatuwezi kabisa kuona uhalisia wa hali mbaya tuliyo nayo kama Kanisa na tupo uchi, tunaaibisha na kufedhehesha. Yesu anatupa shauri tununue Kwake dhahabu iliyosafishwa kwa moto tupate kuwa matajiri kweli kweli. Utajiri kweli kweli ni ule wa kiroho na tukishakuwa na huo hamna shida kabisa tukiwa na huu wa mwilini kama itampendeza Mungu kutupa huo. Ila kuwa na utajiri wa mwilini pekee bila ule wa rohoni ni umaskini kuliko umaskini wenyewe maana Yesu anatuambia itatufaidia nini tukiupata ulimwengu wote lakini tukapoteza nafsi zetu. Itakuwa hasara sana.

Bado neno la Yesu la kuutafuta kwanza Ufalme Wake na haki Yake na hayo mengine yote tutazidishiwa yapo wazi kwetu hata leo. Tumeacha kuutafuta Ufalme wa Mungu na haki Yake but tunatafuta hayo mengine. Hali ni mbaya mpaka watu wasiookoka wamekuwa reference authority ambao tunarefer kwao namna ya kutajirika. Kuna kitu tu hakijakaa sawa mahali maana mambo ambayo tunayakubali leo Kanisani baba zetu na babu zetu hawakuyakubali. Tunawacheka kuwa walikuwa washamba lakini katika ushamba wao walikuwa na Mungu na sisi katika ujanja wetu tuna vitu ila Mungu ndo shida sasa.

Naamini kwa mahali tulipofika kanisa tulitakiwa kuwa na both Mungu na vitu ila kuna mahali tu tumefanya suluhu na tukabaki na utajiri usiyo yakini huku utajiri yakini ukiwa umetuepuka. Yesu sio tu anatushauri tununue Kwake dhahabu iliyosafishwa na moto tupate kuwa matajiri bali pia anatushauri tununue Kwake mavazi meupe tupate kuvaa aibu ya uchi wetu isionekane.

Mavazi meupe ni matendo ya haki ya watakatifu. Uchi ni dhambi iliyopo ndani ya Kanisa. Kanisa lipo uchi na halitaki kuambiwa huu ukweli. Ukituambia tutakuambia unatuhukumu. Tuache tu na udunia wetu. Tuache na dhambi zetu. Acha tu tuzini ovyo na kuzaa ovyo bila agano la ndoa. Acha tuendelee kupiga madeal mjini bila ya kujali namna tunavyopata fedha. Usitusemeshe kabisa. Acha tujichanganye na dunia na bado tuwepo kanisani. Acha tu tufanye umalaya na ukahaba na usituambie maana ukituambia unatuhukumu. Unatakiwa kutupenda na kutuombea ila usituambie kitu cha kuacha dhambi.

Ndiyo tupo uchi, tumechafuka, tunatoa harufu, tunanuka ila usituambie. Tabiri tu juu yetu. Tuambie tutafanikiwa. Tuambie tutainuka ila usituambie hali yetu nyonge, dhaifu, chafu, inayoaibisha. Usituambie ukweli. Tudanganye. Tupake chokaa ambayo haijakorogwa sawasawa. Hatutaki kuisikia kweli inayotuchoma na kutegeuza tupate kutubu. Tuambie tu kuwa Mungu anatupenda haijalishi tunaishi vipi. Dah!

Yesu anasema tusiponunua Kwake mavazi meupe ya kufunika aibu ya uchi wetu ipo siku inakuja itakuwa aibu kweli kweli. Yesu anasema tununue Kwake dawa ya macho tupate kupaka macho yetu ili tuweze kuona maana ipo kama hatuoni hali mbaya ya kutisha ya maisha yetu ya kiroho. Hakuna utisho na uwoga kwa ajili ya vitu vya Mungu. Tupo so casual na Mungu na tunamzungumzia Mungu na mambo ya Ufalme Wake kiuwepesi wepesi tu. Iko kana kwamba hatuoni hali mbaya ya kutisha tuliyo nayo. Yesu anatuambia kwa sababu anatupenda anatukemea kwa hiyo tukawe na bidii tukatubu.

Tugeuke kabisa na tukaache tunavyokwenda na tugeuke kurudi katika njia iliyo sahihi. Alafu anasema kuwa anasimama mlangoni anabisha. Hazungumzi na wasioamini hapa. Anazungumza na wanaoamini. Hii inatisha sana. Kumbe Yesu hata hayupo ndani. Yupo nje. Anasema tukisikia anabisha tukamfungulia ataingia kwetu, sio ndani yetu bali kwetu. Anataka kuanza kujihusisha na maisha yetu. Akiingia kwetu atakula pamoja nasi na sisi pamoja Naye. Hapa anazungumzia ushirika. Anazungumzia fellowship. Anazungumzia mahusiano.

Tumebaki na Jina la kuwa hai lakini wenyewe tumekufa. Mahusiano yetu binafsi na Mungu yapo at an all time low. Yesu amesimama katika mlango wa maisha yako anabisha. Kama utaisikia sauti Yake na kumfungulia anataka kuwa na ushirika na wewe tena.

Mtu wa Mungu, ikiwa Watu wa Mungu waliyoitwa kwa Jina la Mungu watajinyenyekeza, yaani watakubali kuwa kuna kitu hakipo sawa hata kidogo, na kuutafuta uso wa Mungu na kuomba na KUACHA NJIA ZAO MBAYA, ndipo Mungu atasikia toka mbinguni, atatusamehe dhambi yetu na kuiponya nchi yetu.

Kama tunaona mambo yapo sawa na hivi tunavyokwenda basi tuendelee tu hivi hivi lakini kuna aibu kubwa sana inakuja juu yetu siku ile tutakaposimama mbele Zake. Charles Spurgeon aliwahi kusema kuwa Kanisa limeshindwa kabisa kuiathiri dunia iliyoizunguka kwa sababu dunia iliyoizunguka imeiathiri mno Kanisa.

Yesu alisema sisi ni chumvi ya ulimwengu lakini kama chumvi ikipoteza ladha yake yafaa nini isipokuwa kutupwa jaani na watu waikanyage chini ya miguu yao. Ndo maana kanisa tunakayagwa tu chini ya miguu ya watu. Ni chumvi ambayo imepoteza ladha. Nuru yetu haiangazi tena, watu hawayaoni matendo yetu mema na watu hawamtukuzi tena Baba yetu aliye mbinguni. Tumekuwa wa kuchekwa, kudharauliwa na kubezwa.

Niishia hapa.

Carlos Ricky Wilson Kirimbai

 

Comments are closed.

 
%d bloggers like this: