RSS

Nani atakaye kumtumikia Bwana?

Nani atakaye kuwa mtumishi wa Mungu na kuwafundisha na kuwaongoza wengine?

“…wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu.”

Imeandikwa, “Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu.” (Matendo 4:13). Napenda sana tena sana mstari huo! Kumbe! Tutambue, tutafakari kwa kina, Petro na Yohana walikuwa watu wasio na elimu na wasio na maarifa! Hata hivyo Bwana Yesu aliwachagua wawe mitume wa kanisa! Inatufundisha kitu cha maana sana! Watu wa dunia hiyo hawawezi kuelewa jambo hili! ‘Walistaajabu’ tu! (Na inawezekana hata waumini kadhaa hawaelewi jambo hili vizuri.) Maelezo au ‘siri’ ya huduma yao ni hiyo, “wakawatambua ya kwamba WALIKUWA PAMOJA NA YESU.” Amina! Je, kutokana na maisha yako na maneno yako, wengine wanaweza kutambua, ‘Yeye amekuwa pamoja na Yesu; anatembea na Yesu?’

Kama tukipenda kutumikia Bwana na Kanisa Lake, lazima tuchukue muda mwingi tuwe mbele ya Bwana, tuwe pamoja na Yesu! Kama tukilifuata kundi tu, tutashindwa kuwa mtumishi wa Bwana kweli kweli. Kama tukijitosheleza na wazo hili, “Ha, maisha yangu sio mbaya kuliko wengine kanisani,” ndipo hatuwezi kuwa mtumishi wa Mungu. Kiwango kilicho mbele yetu ni Bwana Yesu Kristo mwenyewe. (“Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda.” 1 Yohana 2:6). Kama tukichukua muda mwingi pamoja na marafiki yetu, kufanya mambo  na simu au kuwa mbele ya computa kiasi cha kutokuchukua muda mwingi pamoja na Yesu – peke yetu – ndipo hatuwezi kuwa mtumishi wa Bwana kweli kweli, au kumwakilisha mbele ya watu.

Shauku yetu kumpenda Bwana Yesu, kuwa pamoja naye peke yetu, kumjua Yeye, kufanana naye lazima izidi shauku zetu zote zingine. Na hiyo SIYO jambo la sheria. Lazima iwe jambo la moyo, tuwe na shauku kumpendeza Bwana kuliko yote mengine kwa sababu ‘alinipenda na alikufa kwa ajili yangu!’

Tukiri ukweli. Shida kubwa (katika maisha ya nidhamu ya kikristo) kwa wengi sana, hata kuliko shida nyingine yote, ni ifuatyo: kuchukua muda wa kutosha tuwe mbele ya Bwana peke yetu tu. Kwa nini? Kwa sababu jambo hili linahitaji na kutuongoza tujikane wenyewe! Ni jambo la kujikana mwenyewe. ‘Lazima nifanye hivi na hivi na …. Nafurahia kile na kile na… Ah, sasa nimechoka. Sipati muda kuomba.’ Kwa ujumla hutapata muda wa kuomba! Lazima ujikane mwenyewe  na kuchukua muda. Hiyo tu. Kusema kweli, wengi ni ‘mvivu’ katika jambo hili (juu ya nidhamu ya kiroho). ‘Mvivu’ hapo haina maani hufanyi kitu. Hapana! Labda unafanya mambo mengi kwa juhudi mpaka umechoka kabisa! Labda wewe unakosa kama Martha alivyokosa! ‘Jambo hili ni muhimu nilifanye, na jambo lile… na jambo lile…!’ Lakini Bwana Yesu alimwambia Martha, “KINATAKIWA KITU KIMOJA TU; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.” Kumbe! Lile tulilolifikiri ni ‘muhimu’ au ‘lazima’, linaweza kuondolewa siku ile kama hatujali kitu kile kimoja kinachotakiwa! Je, tunalipokea neno la Bwana, yaani, ‘kitu kimoja kinatakiwa’? Je, jambo hili limeingiza mioyo yetu na linawakilisha mtazamo wetu na nia yetu? Je, ukweli huo na shauku yetu inatupeleka kujikana wenyewe na kuchukua muda na Bwana? Hata hivyo, kama nilivyosema, siyo jambo la kujikana tu, ni jambo la kumpenda Mungu kuliko mambo mengine yote, na ni upendo huo huo ambao unatupeleka kwa Bwana.

Hilo siyo jambo la kusema maombi kadhaa tu kwa dakika chache. Hata siyo jambo la kusema maombi tu ingawa ni wazi tutafanya hivyo. Tunapaswa kuchukua muda kumsifu Bwana, kumwabudu, ‘kutoa miili yetu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yetu yenye maana.’ Jinsi tunavyoweza kuomba kama maisha yetu yasipokuwa dhabihu iliyo hai? Bila kufanya hivyo hatutajua mapenzi ya Mungu kwa maisha yetu, “(ili) mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.” (Warumi 12:1,2).

Nani aliyewaongoza watu wa Mungu waingie nchi ya ahadi? Ni Yoshua! Nidhamu yake ilikuwa ya namna gani? Tunasoma juu ya Yoshua yafuatayo:

“Musa, alitwaa ile hema, na kuikita nje ya marago mbali na hayo marago; akaiita, hema ya kukutania. Hata kila mtu aliyekuwa akitaka neno kwa Bwana, akatoka, akaenda hata hema ya kukutania, iliyokuwa nje ya marago…BALI MTUMISHI WAKE YOSHUA, mwana wa Nuni, naye ni kijana, HAKUTOKA MLE HEMANI.” (Kutoka 33:7,11).

Unaona? Wengi walijitosheleza kuishi maisha ya kawaida na walikwenda kwa Bwana walipotaka – labda kwa ajili ya ‘baraka’ au kwa sababu ya shida. Bali Yoshua – kwa kusudi – alikataa kulifuata kundi, alikataa kuishi maisha ya kawaida. Alipenda kuchukua muda mwingi na Bwana na kuishi maisha yasiyo kawaida! Kutokana na shauku yake kumjua Mungu na njia zake, alijitoa kwa Bwana na alitafuta uso Wake kwa ajili ya mapenzi ya Mungu na kazi Yake, na kwa jili ya watu wa Mungu! Aliamua ‘kuwa pamoja na Bwana’! Alijitenga na mazungumzo matupu, na watu wabaya; alikataa kupoteza muda kwa kujifurahisha na anasa ya maisha ya kila siku. (Lijalie neno la Mungu liguse moyo wako kuhusu maisha yako na usifikiri mambo haya yanamaanisha lazima kuacha nyumbani, elimu au kazi yako na kwenda jangwani! Lazima tujifunze mambo haya katika maisha ya kila siku.) Kama tukipenda kumtumikia Bwana na watu wake lazima tujikane na tujitenga siyo na mambo yasiyofaa tu, bali hata kujitenga na mambo ya kawaida ambayo yanataka kula muda wetu kiasi cha tusimtafute Bwana. Tafakari, Yoshua hakuishi mbele ya watu; hakutafuta ‘huduma’ au sifa ya watu. Aliishi mbele ya Mungu tu bila kujali wengine wafanyalo! Wengi wanapenda waonekane kutumiwa na Mungu mbele ya watu. Yoshua alimtumikia Mungu faraghani kabisa na hiyo ilimtosheleza! Ingekutosheleza? Yesu alisema, “Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.” (Mathayo 6:6). Mambo yale Mungu aonayo ni muhimu mno kuliko mambo watu waonayo! Maisha yako ya faragha – mahali ambapo watu hawakuona – ni ya namna gani? Kama hatuchukui muda ‘pamoja na Bwana Yesu’, hatutakuwa na kitu kuwapa watu.

Petro alihubiri kwa ujasiri, akijaa Roho Mtakatifu, na ‘wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu.’

Kama wewe unahubiri au kufundisha, je, washirika wanaweza kuona ‘umekuwa pamoja na Yesu’? Washirika wengi wanaweza kutambua kama unawalisha na ujuzi wako tu, kama unajifurahisha na mamlaka yako juu yao, au kama umechukua muda na Bwana Yesu na umepokea kitu kutoka Kwake  ambacho unaweza kuwapa! Washirika wengi wanaweza kutambua kama wewe ni mtu wa kiroho au sivyo. Bila kuchukua muda pamoja na Yesu na katika maombi, hamna huduma ya kweli!

Petro alisema, “sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.” (Mat.6:4).

Maombi na Neno la Mungu. Hayo ni muhimu na msingi; muhimu kuliko kwenda shule ya Biblia! Pasipo maisha ya kuchukua muda na Bwana Yesu, shule ya Biblia haiwezi kukufanya awe mtumishi wa Mungu – utajazwa na ujuzi tu ambao huleta majivuno. Ni wazi, kama ukiwa na uhusiano wa kina na Yesu katika maombi na neno lake, unaweza kukua kuwa mtumishi wa Mungu – kama ukienda shule ya Biblia au sivyo. Juu ya shule ya Biblia mimi sina la kusema – lazima kila mtu ajue uongozi wa Mungu katika maisha yake – ila kuwa mtumishi ya Bwana machoni pa Mungu, siyo lazima kwenda shule ya Biblia. Lakini madhehebu kadhaa yanataka uende pale. Lakini tambue vizuri sana, ‘shule ya Biblia’ ya kwanza au ya kweli, ni maisha ya kawaida – nyumbani, shuleni, kazini! Jihadhari! Kuwapo Shule ya Biblia siyo maisha ya kawaida, ni shule tu! Kumbuka pia Mungu alilolisema,

“Mwenye hekima asijisifu kwa sababu ya hekima yake, wala mwenye nguvu asijisifu kwa sababu ya nguvu zake, wala tajiri asijisifu kwa sababu ya utajiri wake; bali ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ANANIFAHAMU MIMI, NA KUNIJUA, ya kuwa mimi ni Bwana…” (Yeremia 9:23,24).

Maneno ya ajabu! Tafakari kwa kina sana Mungu analosema! Haifai kuwalisha kundi la Bwana na ‘ujuzi’ wetu au ‘elimu’ wetu au ‘maarifa’ yetu tu! Lazima mimi mwenyewe kwanza nimfahamu Bwana na kumjua – kupitia kuchukua muda kuwa pamoja naye, kumtafuta, kumpenda, kumtii, kumwamini na kuomba kwa ajili ya kazi Yake na kanisa Lake!

Paulo alipokea mwito wa Mungu mara alipookoka, lakini alitembea na Bwana Yesu mpaka Mungu alimtuma! Alikuwa anafanya nini wakati Roho Mtakatifu aliposema, “Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia,”? (Mat.13:2). Sikiliza!

“Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba… na Sauli (Paulo). Basi hawa WALIPOKUWA WAKIMFANYIA BWANA IBADA (AU ‘WAKIMTUMIKIA BWANA) NA KUFUNGA, Roho Mtakatifu akasema…”.

Unaona? Paulo hakutafuta ‘huduma’, alimtumkia Bwana; alichukua muda pamoja na Bwana; alimtumikia Bwana na maombi na kwa kufunga. ‘Hakuutangulia’ mwito wake! Hakukimbia kuokoa ulimwengu pasipo uongozi wa Mungu! Alikuwa mtu aliyejikana na kujitoa kwa Bwana wake. Alihudumia kanisa lililopo Antiokia akiwa mwalimu na nabii – kabla kuwa mtume! Lazima kumtumikia Bwana kabla ya kumtumikia watu! Siyo wengi wanaofanya hivyo. Kwa nini? Kwa sababu siyo mbele ya watu! Haipo nafasi kuonekana kuwa mtu maalum! Upo mbele ya Mungu! Kama hatuna uhusiano na Bwana Yesu hatuchukui muda kuwa pamoja naye. Wengi wanachoshwa kwa upesi. Lazima kujikana. Lazima kumpenda Yesu zaidi ya yote nyingine – kumpenda na kumwaabudu kwa mioyo yetu yote! Wengine wanaifurahia huduma yao. Wengine wanayo furaha kubwa sana inayotokana na ushirika wao na Bwana Yesu!

Yoshua alimtumikia Mungu faraghani, hakuchukua wala hakupoteza muda kwa nia ya kupendeza watu na kuwavuta watu kwake. Kwa wakati wake, Mungu alimwita kuongoza na kuwalisha watu Wake!

“Musa akanena na Bwana akisema, ‘Bwana, Mungu …aweke mtu juu ya mkutano, atakayetoka mbele yao, na kuingia mbele yao; atakayewaongoza watokapo, na kuwaleta ndani; ili mkutano wa Bwana WASIWE KAMA KONDOO WASIO NA MCHUNGAJI.’ Bwana akamwambia Musa, ‘Mtwae Yoshua, mwana wa Nuni… wekee mkono wako; …Nawe utaweka juu yake sehemu ya heshima yako, ili mkutano wote wa wana wa Israeli wapate kutii.” (Hesabu 27:15-20).

Amina! Unaona? Je, inakutia moyo? Je, inaichochea shauku ndani yako kumtumikia Bwana haijalishi analofanya nawe, haijalishi kama watu watakuona au sivyo, haijalishi itachukua muda gani?

Uliona Musa alilosema? Alikuwa na moyo kwa watu wa Mungu ili ‘wasiwe kama kondoo wasio na mchungaji’ – mchungaji ‘atakayeiangalia hali ya kundi la Bwana kweli kweli na asiyetafuta vyake mwenyewe bali vya Kristo!’ Paulo alisema, “Maana wote wanatafuta vyao wenyewe, sivyo vya Kristo Yesu – ila Timotheo tu!”  Na inaonekana sana ni vile vile siku hizi juu ya wengi. Siku hizi sisi pia tunahitaji viongozi, wachungaji na watumishi wa kweli. Wengi wanapenda sifa ya watu, wanapenda cheo, wanapenda mamlaka, wanapenda ‘mafanikio’, wanapenda pesa, wanapenda kuvuta vijana na muziki ya kisasa, wanapenda miujiza kupita kiasi. Matokeo ya hayo yote wengi wanazoea kutafuta ‘baraka’ (ya nje) badala ya kujikane wenyewe, wajitwike msalaba wao kila siku, wamfuate Yesu. Ni wachache siku hizi wanaohubiri ‘Yesu Kristo, naye amesulibiwa.’ Matokeo ya mambo hayo ni maisha ya wakristo yanazidi kufanana na maisha ya wasioamini. Lakini ni viongozi na wachungaji wengine wanaoruhusu hali ya namna hiyo kuingia katika kanisa la Bwana – kwa ajili ya kuwapendeza watu na kuvuta watu. Ni viongozi ambao wanachukua wajibu kwa kosa hili. Matokea ya mambo hayo yote ni baada ya muda washirika watashindwa wakati majaribu magumu yatakapokuja – hasa vijana ambao hawajalishwa na neno la Mungu kweli kweli, na neno la msalaba. Na mwishoni itatokeaje? Paulo alisema, “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani.” (1 Tim.4:1). Ni kwa sababu ya hiyo ninayaandika mambo haya. Siku hizi ni hatari sana, siyo kwa sababu ya mambo yale yanayotokea nje ya makanisa, bali kwa sababu mambo yale yanayotokea na yanayfundishwa katiak makanisa mengi!  

Ninayo shauku kubwa sana (pamoja na huzuni kwa kina sana) kutuchochea na kutuhimiza ili tujitoe kwa Bwana, kumfuata uso Wake, kuchukua muda sana kushirikisha naye, kusoma neno lake sana na kuomba kwa ajili ya kazi ya Mungu na kwa ajili ya watu wa Mungu. Tunahitaji watumishi kama hao siku hizi. Yoshua alikuwa tayari, au tunaweza kusema, alikuwa ametayarishwa ‘kwa ajili ya wakati kama ule’ kuwaongoza watu wa Mungu ili warithi ahadi ya Mungu! Na wewe? Na mimi? Mungu awainue watumishi wa kweli siku hizi – kama Timotheo – watakaoiangalia hali ya watu wa Mungu kweli kweli, watakaohubiri ‘Kristo Yesu naye amesulibiwa.’

Kama tulivyoona, Petro alisema, “sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.”

Najua sisi sote siyo mitume! Hata hivyo ili watu watambue ‘tumekuwa pamoja na Yesu’, sehemu mmoja ya hiyo ni tusome neno la Mungu, na siyo kusoma neno Lake tu, bali kulipenda neno Lake, kumtafuta Yesu kupitia neno Lake – tunasoma neno Lake kwa sababu tunayo shauku kubwa sana kumjua, na kwa neema na Roho Yake kufanana naye! Watu wanasema wanapojisikia baridi, “Ota moto!’ Mimi nawahimiza watu ninapohubiri, ‘Ota neno la Mungu!’ Maandiko yanasema, “Naye Neno alifanyika mwili.” (Yohana 1:14). Lazima jambo hili hutokea katika maisha yetu! Yaani, maneno tunayoyasoma kwenye Biblia lazima yafanyike ‘mwili’ katika maisha yetu – hayafai kama yanabaki kama ujuzi tu vichwani vyetu! Lazima tubadilishwe na neno la Mungu na kwa Roho Yake. Ota neno la Mungu!

Paulo alimhimiza Timotheo, “UYATAFAKARI hayo; UKAE katika hayo; ili kuendelea kwako KUWE DHAHIRI KWA WATU WOTE. Jitunze nafsi yako, na mafundisho yako. DUMU KATIKA MAMBO HAYO; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako NA WALE WAKUSIKIAO PIA.” 

(1 Tim.4:15:16). Maneno ya ajabu na ya maana sana! Pia yanawakilisha changamoto kwetu! Unona? Lazima tuwalishe watu na mambo yale yanayotokana na uhusiano wetu na Bwana Yesu, ambayo sisi tumeyajifunza kutoka Bwana, kwa sababu tunachukua muda ‘kuwa pamoja naye’; tuwalishe watu na neno lile ambalo limeshayabadilisha maisha yetu kutokana na utii wetu kwa Bwana Yesu – na siyo na maneno ya vitabu tu tulivyovisoma! Hatuhubiri kuwapendeza watu bali kama Biblia inasema, “Mtu akisema, na aseme kama mausia ya Mungu…” (1 Petro 4:11). Lengo la huduma yote ni kumtukuza Bwana Yesu na siyo huduma yetu, “mtu akihudumu, na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na Mungu; ili Mungu atukuzwe katika mambo yote kwa Yesu Kristo!” Amina.

Sehemu ya ‘kuwa pamoja na Bwana’ ni tumtafute Bwana na uso Wake. Daudi aliandika,

“Uliposema, Nitafuteni uso wangu, Moyo wangu umekuambia, Bwana, uso wako nitautafuta.” (Zaburi 27:8).

Daudi alikuwa na shauku kubwa kumjua Bwana! Shauku hiyo ilimchochea aamke mapema kuutafuta uso wa Bwana! “Ee MUNGU, Mungu wangu, nitakutafuta mapema, Nafsi yangu inakuonea kiu, Mwili wangu wakuonea shauku…Ndivyo nilivyokutazama katika patakatifu, Nizione nguvu zako na utukufu wako.” (Zaburi 63:1,2). Je, umejisikia vivyo hivyo? Je, tupo tayari kumtafuta Bwana namna ya hiyo? Je, tupo tayari kumtafuta kwa ajili ya utukufu wake, na ili nguvu ya Injili yake idhihirishwe kanisani na duniani?

Mungu mwenyewe alishangaa. Kwa nini? Imeandikwa, “kweli imepunguka kabisa… naye Bwana akaona hayo, akachukizwa kwa kuwa hapana hukumu ya haki. Akaona ya kuwa hapana mtu, akastaajabu kwa kuwa hapana MWOMBEZI.” (Isaya 59:15,16). Na ‘kweli’ imepunguka siku hizi na inaonekana ni wachache tu wanaohuzunishwa na jambo hili na ambao wapo tayari kuutafuta uso wa Bwana kwa ajili ya hali hiyo! Mungu alilalamika juu ya jambo hili, “Bwana asema hivi, Baba zenu waliona dhuluma gani kwangu, hata wakafarakana nami, wakafuata ubatili, nao wakawa ubatili? Wala HAWAKUSEMA, YUKO WAPI BWANA, aliyetutoa katika nchi ya Misri; akatuongoza jangwani… Makuhani hawakusema, Yuko wapi Bwana? Wala WANA-SHERIA HAWAKUNIJUA; wachungaji nao waliniasi, nao manabii walitoa unabii kwa Baali, WAKAFUATA MAMBO YASIYOFAIDIA KITU.” (Yeremia 2:5-8).

Wahubiri wengine wanachochea hisia ya watu tu. Wanaacha kufundisha neno la Mungu na wanawaahidi watu mambo makubwa kwa maisha na yao, na ‘mafanikio’, na watu wanasimama wakipiga makofi kama ni mambo majabu wakati wanapohubiri mamb hayo. Lakini mara nyingi sana ni ‘mawingu yasiyo na maji!’

Daudi aliandika, “Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao, Wakutafutao uso wako, Ee Mungu.” (Zaburi 24:6).

Sasa, labda ninakosa lakini mimi sidhani hiki ndicho kizazi cha wamtafutao Mungu na uso Wake kwa ajili ya kazi yake katika Kanisa lake; wapo wao wanaofanya hivyo lakini kwa sababu ya hali ya makanisa kwa ujumla, tunahitaji sana Mungu aichochee mioyo yetu wamtafute kwa ajili ya mambo yale ambayo Yeye mwenyewe anataka kuyafanya katika kanisa Lake na kupitia kanisa Lake! Kwa hiyo ninayaandika mambo hayo ili tujichochee kumtafuta Bwana ili Yeye awainue na ‘apeleke watenda kazi katika mavuno yake’. Watenda kazi ambao watajikana wenyewe na kuwalisha watu na neno la Mungu!

Tunasoma neno la kuhuzunisha kwenye 1 Samueli 3:1. “Na neno la Bwana lilikuwa ADIMU siku zile; hapakuwa na MAFUNUO DHAHIRI.” Kwa nini? Tusome mstari wa mwisho ya kitabu cha Waamuzi, “…kila mtu alifanya yaliyokuwa ni mema machoni pake mwenyewe.” Unaona? Kila mtu alifanya yaliyokuwa ni mema machoni pake mwenyewe na matokeo ya hayo yalikuwa ‘neno la Bwana lilikuwa adimu!’ Hakuwepo mtu mmoja aliyemtafuta Bwana na uso wake kweli kweli. Kwa huzuni naamini siku hizi zinafanana siku za Samueli. Wengi wanafanya yanayokuwa mema machoni pao na hawahubiri ‘Yesu Kristo naye amesulubiwa’. LAKINI… “mtoto Samweli akamtumikia Bwana.” Amina! Samueli alimtumikia Bwana hekaluni – siyo mbele ya macho pa watu bali faraghani mbele ya macho pa Mungu! Samueli alizuia taa ya Mungu isizimike! Amina! Alikuwa hekaluni wakati wote (je, unamkumbuka Yoshua alilofanya?) kumtumikia Bwana, na kupitia huduma hiyo alipata kumjua Bwana na neno la Bwana lilifunuliwa kwake! Amina! Na ilikuwa Samueli aliyeongoza watu wa Mungu na kuwalisha na neno la Mungu la kweli na la safi! Tunahitaji waumini kama hao siku hizi, ambao wanamjua Bwana kweli kweli na wawezao kuwalisha watu wa Mungu na neno lake ili wakue katika Kristo na kumjua!

Ni jambo la ajabu na la neema sana kwamba Mungu anataka tumtafute kwa ajili ya mambo yale ambayo Yeye mwenyewe anataka kuyafanya – katika maisha yetu, katika kanisa na katika ulimwengu! Haifai kumtafuta ovyoovyo tu. Yeye alisema, “Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta KWA MOYO WENU WOTE.” (Yeremia 29:12,13). Na Paulo anasema, “nakaza mwendo ili NIPATE KULISHIKA LILE AMBALO KWA AJILI YAKE NIMESHIKWA NA KRISTO YESU. Ndugu.. natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.” (Wafilipi 3:12-14).

Je, unataka kuwa mtumishi wa Mungu? Kumbuka mistari hiyo: “wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu,” na “kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia.” Lazima watu waone wewe siyo msemaji tu, lakini kwamba wewe unao uhusiano na Mungu na hubiri yako na mafundisho yako na maisha yako mbele ya watu YANATOKANA NA UHUSIANO HUO HUO!

Ninaandika mambo hayo siyo kwa viongozi, wahubiri au wachungaji tu, ni neno kwa wote.

© David Stamen   2015                

Unaweza kupakua somo hili kwa kubonyeza link hiyo:  Nani atakaye kumtumikia Bwana.

DALILI (KADHAA) YA MTUMISHI WA MUNGU:

– Mtumishi wa kweli wa Mungu HATAFUTI fedha zako. Hatamani pesa zako wala hatakulazimisha umpe pesa kwa ajili ya huduma au maombi yake.

“Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu.” (Mat.20:33).

– Mtumishi wa Mungu HATAFUTI kujifanya mtajiri kupitia huduma yake kwako.

 “Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho.”

(Mat.3:6). Mtume Petro pamoja na mitume wengine walipokea pesa kwa ajili ya waumini maskini lakini, kumbe, hawakuchukua pesa kwa ajili ya faida yao kujifanya matajiri! Hawakuishi kwenye nyumba ya fahari wala hawakuwa na walinzi wa binafsi. (Au unafakiri Petro au Paulo wangeweza kuwa na magari mengi ya gharama kubwa sana?) Walikuwa na moyo safi na walifanya huduma yao bila unyonyaji,

“Maana hatukuwa na … maneno ya juujuu ya kuficha choyo; Mungu ni shahidi.” (1 Wathes.2:5).

“Basi thawabu yangu ni nini? Ni hii, ya kuwa nihubiripo, nitaitoa Injili bila gharama, bila kutumia kwa utimilifu uwezo wangu nilio nao katika Injili.” (1 Wakor.9:18).

Neno la Mungu ni dhidi wachungaji ambao wanawahudumia watu Wake kwa ajili ya faida zao, kujitajirisha wenyewe,  “Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wachungaji wa Israeli, wanaojilisha wenyewe; je! Haiwapasi wachungaji kuwalisha kondoo? …Mnawala walionona, mnajivika manyoya, …lakini hamwalishi kondoo.” Ezekieli 34:2,3.

– Mtumishi wa Mungu HATAFUTI kuwapendeza watu, hasemi mambo kwa kusudi la kuvuta watu kanisani kwake ili ajenge kanisa kubwa kwa ajili ya sifa yake.

“Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza wanadamu, singekuwa mtumwa wa Kristo.” (Wagal.1:10). “Kama vile tulivyopata kibali kwa Mungu tuwekewe amana Injili, ndivyo tunenavyo; si kama wapendezao wanadamu, bali wampendezao Mungu. Maana hatukuwa na maneno ya kujipendekeza wakati wo wote, kama mjuavyo.” (1 Wathes.2:4,5).

– Mtumishi wa Mungu HATAFUTI sifa ya watu.

“Hatukutafuta utukufu kwa wanadamu, wala kwenu, wala kwa wengine.” (1 Wathes.2:6).

– Mtumishi wa Mungu HATAFUTI vyake mwenyewe.

“Maana wote wanatafuta vyao wenyewe, sivyo vya Kristo Yesu.” Tutambue, Paulo anasema ‘wote’! Basi, kwa uhakika maana yake ni idadi isiyopungua ‘wengi’! Ina maana, watumishi wengi/wote (ila Timotheo) walitafuta vyao wenyewe! Je, ni tofauti sana siku hizi?

– Mtumishi wa Mungu HATAFUTI vitu vya waumini. Anatafuta faida ya kiroho ya waumini.

“Maana sivitafuti vitu vyenu, bali nawatafuta ninyi.” (2 Wakor.12:14).  Maneno ya ajabu! Paulo alipenda waumini, siyo ‘vitu vyao’! Hatafuti vitu vyao, pesa zao, sifa zao au utukufu kwa watu! Mtumishi wa Mungu anajitoa kwa ajili ya faida ya wale awahudumiao. Anayo nia moja tu, “Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi.” (2 Wakor.11:2). Naye yupo tayari kujimwaga kwa ajili ya watu wa Mungu ili wapate faida ya kiroho,

“Nami kwa furaha nyingi nitatapanya, tena nitatapanywa kwa ajili ya roho zenu. Hata kama kadiri nizidivyo kuwapenda sana, ninapungukiwa kupendwa.” (2 Wakor.12:15).

Maneno ya kuchanga moto! Mtumishi ya Mungu huzidi kuwapenda waumini awahudumiao hata hivyo anapungukiwa kupendwa!

– Mtumishi anamtegemea Mungu kwa ajili ya mahitaji yake.

“Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; MAANA NIMEJIFUNZA KUWA RADHI NA HALI YO YOTE NILIYO NAYO. Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; KATIKA HALI YO YOTE, na katika mambo yo yote, nimefundishwa KUSHIBA NA KUONA NJAA, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.” (Wafilipi 4:11-13).

– Mtumishi wa Mungu hufurahi kwa ajili ya waumini wanapotambua ni jambo la haki na la pendo kumsaidia mtumishi ambaye anafanya kazi mbele ya Mungu kwa ajili yao.

“Nalifurahi sana katika Bwana, kwa kuwa sasa mwisho mmehuisha tena fikira zenu kwa ajili yangu, kama vile mlivyokuwa mkinifikiri hali yangu lakini hamkupata nafasi….Lakini mlifanya vema, mliposhiriki nami katika dhiki yangu…. hakuna kanisa lingine lililoshirikiana nami katika habari hii ya kutoa na kupokea, ila ninyi peke yenu. Kwa kuwa hata huko Thesalonike mliniletea msaada kwa mahitaji yangu, wala si mara moja. SI KWAMBA NAKITAMANI KILE KIPAWA, bali nayatamani mazao yanayozidi kuwa mengi, KATIKA HESABU YENU. Lakini ninavyo vitu vyote na kuzidi, tena nimejaa tele; nimepokea kwa mkono wa Epafrodito vitu vile vilivyotoka kwenu, HARUFU YA MANUKATO, sadaka yenye kibali, IMPENDEZAYO MUNGU.”

Ndiyo. Paulo alikuwa na mahitaji na alipokea kile kipawa kwa ajili ya MAHITAJI yake (siyo kwa ajili kumfanya mtajiri) kwa furaha, lakini siyo kutokana na uchoyo au tamani yake apate fedha, lakini alifurahi kwa ajili ya waumini. Katika utoaji wao Paulo alitambua matunda ya pendo katika maisha yao ambayo ni kama harufu ya manukato impendezayo Mungu! Alifurahi kwa ajili ya hayo tu! Tena ni wazi hapo kwamba mtumishi wa Mungu hawalazimishi waumini wamtoe pesa. Anafurahi waumini watoe kipawa kwa hiari kutokana na pendo la Mungu mioyoni mwao!

© David Stamen   2015                    http://www.somabiblia.com

UNAWEZA KUDOWNLOAD SOMO HILI KWA KUBONYEZA LINK IFUATAYO:  Nani atakaye kumtumikia Bwana.

UNAWEZA KUSIKILIZA ZAIDI JUU YA MAMBO HAYO KWA KUHUDHURIA SEMINA HAPO CHINI:

DAR ES SALAAM.  TAREHE   SEPTEMBA 15-17   2015

 

 

4 responses to “Nani atakaye kumtumikia Bwana?

  1. Fredy

    September 9, 2015 at 2:33 pm

    SHALLOM, I ASK IF I CAN GET AN OPPORTUNITY TO VOLUNTEAR ON SPREAD THE WORD OF GOD.

     
    • dsta12

      September 9, 2015 at 3:21 pm

      Please give me some information about yourself. Do you have a facebook account or email or phone number? What area do you live in? What is your job at the moment? Asante!

       
  2. John wakuchalo.

    March 13, 2017 at 6:30 pm

    somo zuri sana.Ubarikiwe.

     
  3. Anonymous

    March 19, 2017 at 1:16 pm

    Lushoto Tanga

     

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

 
%d bloggers like this: