RSS

KWA MUJIBU WA BIBILIA, JE, NI SAHIHI UPATE KIBALI CHA MCHUNGAJI WAKO KWANZA KABLA YA KUMTAFUTA MCHUMBA WAKO UMPENDAYE?

Hakuna chochote katika haya yaliyoandikwa katika makala hii, yanayolenga kumtia moyo yeyote yule ili awe mkaidi, au mtu mkorofi kuhusiana na kile anachokitaka au katika kujitafutia mapenzi yake binafsi zaidi kuliko mapenzi yake Mungu. Na wala hakuna chochote katika haya yaliyoandikwa katika makala hii yanayowatia moyo vijana kudharau au kutokujali mashauri wanayopewa na wachungaji, marafiki zao wa karibu, au hata jamii ya familia zao ambao wanaweza kuwa na mambo ya msaada ya kuyasema.

Tunapaswa kumtambua Mungu analofanya katika maisha yetu. Yeye ndiye anayepaswa kuwa ni Bwana wa maisha yetu nasi tunapaswa kumheshimu!  Ni Mungu ndiye aliyelipa gharama kubwa kwa kumtoa mwanae pekee kwa ajili yetu, ili kwamba tufanyike kuwa watoto wake na kwamba ili tupate kutafuta na kuyafanya mapenzi yake katika mambo yetu yote! Maisha yetu sio mali yetu wenyewe bali ni mali yake yeye! (1 Wakor. 6:19,20; 2 Wakor. 5:15). Yeye mwenyewe anaendelea kufanya kazi ndani ya maisha yetu ili kutimiza kusudi lake jema. (Wafilipi 2:13). Je, umekwisha kupata ushirika pamoja naye? Unaamini kuwa yeye anafanya kazi ndani ya maisha yako na kukuongoza? 

Mbali na wokovu wako ulioupata kupitia Kristo Yesu, kuolewa/kuoa ni mmoja ya maamuzi makubwa unayokwenda kuyafanya katika maisha yako. Unaweza kuchoshwa na kazi yako kisha ukaamua kuiacha na kwenda kutafuta kazi nyingine, lakini huwezi kufanya kama hivyo kwa mkeo – hii ina maana kuwa huwezi kufanya tendo kama hili kwa mkeo iwapo wewe ni mtu unayemfuta Yesu Kristo. Unaweza kufanya makosa mabaya unapoendesha gari, pikipiki hata baiskeli na ikakusababishia kupoteza mguu wako kwa kuvunjika, lakini ikiwa utamwacha mkeo kwa sababu tu wewe ‘unafikiri’ kwamba ulifanya makosa, basi unaweza kupoteza roho yako! Kuoa ni moja ya mambo ya maamuzi muhimu sana katika maisha yako! Kulifanya jambo fulani kwa kukosea, ujue hapa haliwezi tu kukuletea hasara na maumivu pekee kwako katika maisha yako ya leo tu, bali ni katika maisha yako yajayo pia!

Je, unafikiri kuwa Mungu anafurahia juu ya mtu yule utakayemwoa? Ndiyo kwa vyovyote vile anafurahia! Je unafikiri jambo hili linakwenda kutokea tu kwa bahati au kwa uchaguzi wako mwenyewe? Je, Bwana ni Mungu wako? Au je, mchungaji wako ndiye Mungu wako? Napenda kuuliza tena, je, tayari unao uhusiano na Yesu Kristo? Unatafuta mapenzi yako mwenyewe, au mapenzi ya mwanadamu au je, mapenzi ya Mungu? Je, hayo ndiyo maombi yako ya kina kwenye moyo wako kila pumzi yako unayoendelea kuivuta ukimwambia Mungu “mapenzi yako yatimizwe!” Unaamini kuwa yeye Mungu anaweza kukuongoza hatua zako na kukulinda? Tunawezaje kujua sasa mapenzi ya Mungu na maongozi yake katika maisha yetu? Warumi 12:1, 2, inasema,

“basi ndugu zangu nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, yakumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana, wala msiifuatishe namna ta dunia hij, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu, yaliyopo mema ya kumpendeza na ukamilifu”.

Somo hili ni somo gumu. Kwa nini hili ni somo gumu? Ni somo gumu kwa sababu kila kitu kinategemea na hali ya kiroho ya mtu mhusika  – juu ya hali ya moyo! Je, unamtaka Mungu na mapenzi yake kwa hakika au wewe ni mtu wa dini tu? Je, unautoa mwili wako kuwa dhabihu iliyo hai kwa Mungu, katika misingi yako ya maisha ya kila siku, kuishi maisha matakatifu ambayo yanampendeza yeye? Au unatafuta kujipendeza mwenyewe, kufurahia tamaa ya macho na ya mwili?  Je, upo kimwili au kiroho?  Shetani huwajia vijana na kuwaambia “umesubiria vya kutosha! Mchague huyu hapa awe mume wako, awe mke wako! Kwapua fursa hii, kabla hujachelewa zaidi!” (1Timotheo 5:11,12,15, inatupatia mfano wa namna hii.) Hivyo wanafuata matamanio yao wenyewe, tamaa ya mwili, na kisha huteseka kwa maumivu makubwa sana katika maisha yao!

Wengine hawajitoi maisha yao kama dhabihu iliyo hai, badala yake wao huenda na kujiingiza katika kutenda mambo ya zinaa. Ushauri wa aina yoyote mtu awezao kukupatia, haijalishi ushauri huo unakuwa mzuri kiasi gani, kimsingi hautakusaidia wewe hadi pale moyo wako uwe mnyofu mbele ya Mungu. Mpaka pale unapokuwa na mahusiano mazuri na yeye Mungu! Kwa hiyo hakuna chochote hapa katika yale ninayoyaandika yanayoweza kukuhakikishia kuwa eti utafanya uchaguzi nzuri, utaenda katika njia nzuri, mpaka tu kwanza pale moyo wako utakapokuwa sawa mbele za Mungu.

Kwa hiyo, ikiwa kwa dhati kabisa unataka mapenzi ya Mungu katika maisha yako, ndipo basi utakupasa kujitoa mwenyewe, na mwili wako kwake kama dhabihu iliyo hai, takatifu, ukisubiri kutoka kwake na sio kupaparika juu ya njia anayokuongoza. Kama vile maandiko tuliyoyasoma hapo juu yasemavyo, usijifananishe mwenyewe na dunia hii, wala usifuatishe vitabia vibaya na mifumo ya maisha ya vijana wengine wapendao dunia hii. Bali wewe utatumia muda wako ukiwa mwenyewe mbele zake Mungu, utasoma neno lake ili kwamba uweze kufanyika upya nia yako au akilini mwako, ili kwamba upate kujua katika moyo wako ni nini kilicho bora chenye kukubalika, kikamikifu katika mapenzi ya Mungu kwako. Na hii inahusisha pia mke wako ajaye katika maisha yako ya baadaye.

Kadiri unavyoendelea kutembea na Bwana, yeye atakupatia ufahamu wa mapenzi yake – ambayo ni mazuri, yenye kukubalika mbele zake! Baba yako na mama yako hawezi kukuambia wewe mapenzi ya Mungu katika jambo hili ni nini. Kadhalika mchungaji wako hapaswi kukunyoshea kidole chake na kukuambia yule binti ndiyo kusudi la Mungu kwako, basi umwoe yule. Hapana, hatakiwi akuambie hivyo, hahusiki katika jambo kubwa na muhimu kama hili. Hili ni jambo moja kati ya mambo ambayo yanakutaka ufanye uchaguzi muhimu sana sana katika maisha yako – penginepo ni jambo la muhimu zaidi! Ni wewe mwenyewe ndiye unapaswa kufahamu mapenzi yake Mungu katika jambo kama hili -wala si mtu mwingineo yoyote yule; ni wewe mwenyewe tu. Ni Mungu pekee ndiye atakayekuongoza wewe katika jambo kama hili linalogusa maisha yako ya baadaye – kwa sababu yeye ndiye Baba yako, kadhalika ni Mungu wako. Ikiwa tutamtegemea mtu mwingine kututolea maamuzi katika jambo kubwa na muhimu kama hili, yaani, la kutuchagulia nani awe mchumba wako, basi hii inamaanisha kuwa sisi wenyewe hatuna mahusiano yoyote na Baba yetu Mungu kupitia Yesu Kristo. Tunawategemea wanadamu kana kwamba sisi wenyewe hatumjui Mungu. Mwanadamu kamwe asichukue nafasi ya Mungu katika maisha yetu – hata wawe mchungaji wako, au wale wanaojiita manabii au mitume! Hao wote hawana nafasi hiyo. Biblia haijawapatia jukumu hili. Yesu Kristo mwenyewe hakuwakabidhi wajibu kama huo.

Ikiwa wewe utamwendea mchungaji wako na kumwuliza kama unaweza kumfuatilia binti fulani hapo kanisani au hata mahali penginepo ili umwoe awe bibi harusi wako, basi hapo ndipo unapomfanya mchungaji wako huyo kuwa ndiye Mungu wako. Au yeye anajifanya kuwa kana kwamba ni Mungu wako. Kama mchungaji wako atakuambia, ‘Hapana usiseme chochote na binti yule”, hapo ndipo mchungaji huyo anajifanya mwenyewe kuwa ni mbadala wa Mungu. Hii ni dhambi, ni kuabudu sanamu! Mwanadamu – mchungaji – anachukua mahala pa Mungu katika maisha yako! Ninajua jambo kama hili linaweza likawa ni utamaduni au sheria katika kanisa unaloabudu, lakini haijalishi, bado hiyo ni dhambi kinyume na kanisani, na washirika kanisani hapo kwamba eti uamuzi wa nani unayekwenda kumwomba awe bibi harusi wako utegemee kile ambacho mchungaji wako atakachokuambia!  Hapana. Hakuna maelekezo yoyote yanayoagiza hivyo kwenye Biblia yote. Kwa hakika hakuna fundisho lolote la namna hiyo katika Agano Jipya lote. Na hiyo ndiyo sababu utamaduni/desturi ya aina hiyo haijulikani katika baadhi ya sehemu nyingi ulimwenguni humu. Haijawahi kutokea na haijafanyika hivyo kwa washirika wengi zaidi ya miaka 2000.

Mchungaji hana mamlaka yoyote kutoka katika Biblia au hata kutoka kwa Mungu mwenyewe eti, akuelekeze wewe nani wa kumwoa! Nataka ujue ndugu msomaji wangu, hakuna maelekezo yoyote toka kwa Mungu wanayopewa wachungaji, mitume, manabii hata wainjilisti na walimu kwamba wakuelekeze wewe mtu wa mzuri wa kumwoa, au yupi usimwoe, eti tu kwa sababu yeye ni mchungaji!  Biblia ipo kimya juu ya wajibu huu wanaoudandia wachungaji. Kwa ujumla hakuna yeyote anayeweza kukuambia hivyo! Na mwishoni hakuna akuambiaye kufanya hivyo! Unapaswa kuwa na ufahamu wako wewe mwenyewe ni nani awe bibi harusi wako kutokana na mahusiano yako mwenyewe na Mungu. Jambo hili ni vilevile kwa mwanamke wa kikristo; ni lazima awe na ufahamu kutoka kwa Mungu mwenyewe kuwa mwanamume ambaye anakwenda kuoana naye anatokana na mapenzi ya Mungu kwa ajili yake (yaani, Mungu ndiye anaye mshuhudia moyoni mwake kuwa huyo ndiye mumewe aliyemwekea kwa ajili yake).

Nakusihi uelewe muktadha wa fundisho hili. Naandika kuhusu uchafuzi wa mamlaka ambao baadhi ya wachungaji wanautenda makanisani mwao nyakati hizi. Ndiyo kwa vyovyote vile, katika mila na desturi za utamaduni nyakati hizi wazazi wa mwanamke umpendaye awe bibi arusi wako anaweza asikubaliane na wewe kumwoa binti yao, lakini hili ni jambo la tofauti kabisa na kile ninachokisema hapa, na kuhusiana na tamaduni za ulimwengu huu. Na wala mimi siwezi kuingia katika somo kama hili kwenye fundisho hili ambalo linahusu tu madaraka wanayojitwalia wachungaji huko wa kanisani mwao kwa mambo kama haya.

Pengine waweza ukasema, “Lakini mchungaji anayo majukumu ya kuiangalia hali ya afya yangu kiroho kwamba inaenda vizuri”. Nakubaliana na jambo hili kabisa! Na neno la Mungu bado linaunga mkono na kuthibitisha jambo kama hili – Matendo 20:28; Waebrania 13:17. Kulikuwepo na mwanamke mmoja kanisani ambaye nilitaka nimwoe. Baada ya muda fulani wa kufahamiana vizuri na kusubiria kwa Bwana, niliamini kuwa hili lilikuwa ni maongozi ya Mungu na ni mapenzi yake Mungu. Hata hivyo, nilikwenda kwa mchungaji kumshirikisha kile ambacho Mungu alikuwa akikifanya katika maisha yangu na kuona kama alikuwa na ushauri wowote wa busara wa kumpatia kijana kama mimi. Sikwenda kwake ili kuomba ruhusa ya kumwoa binti yule – kwa sababu, kwa mujibu wa neno la Mungu, hawezi kunipa au kukataza ruhusa hiyo – lakini nilikuwa tayari kusikiliza ushauri wowote ule au maonyo ambayo angekuwa nayo kwa ajili yangu. Na ndiyo, na hata yeye hakufikiria kuwa anayo mamlaka ya kuniambia mimi, ni nani wa kumwoa au nani nisimwoe eti tu kwa kuwa yeye ni mchungaji. Kama yeye angekuwa amepata mashaka yoyote juu ya maamuzi yangu, basi angenishirikisha mimi mwenyewe nami ningeweza kufikiria kuwa ni wajibu wangu mbele za Mungu kufikiria juu ya mashaka na maonyo aliyoniambia mchungaji yule. Lakini mwishoni mwa yote maamuzi yangelipaswa kukaa katika msingi wa kile ninachoamini kuwa Mungu alikuwa anakifanya ndani ya maisha yangu. Lakini yule mchungaji alifurahishwa tu na maongozi ya Mungu katika maisha yangu!

Nilinukuu Waebrania 13:17 hapo juu, lakini tunatakiwa kuelekezwa na kusudi lote la Mungu basi hebu tuangalie katika 1 Petro 5:2,3,  sehemu ambayo mtume Petro anatoa maelekezo kwa wachungaji.

“Lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. WALA SI KAMA WAJIFANYAO MABWANA juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya VIELELEZO kwa lile kundi. “

Haya ni maelekezo ya aina ileile ambayo Paulo aliwapa wachungaji wa huko Efeso, yaani, alisema, “Lisha watu wa Mungu kwa neno la Mungu.” Hivyo ndivyo Bwana Yesu alivyomwambia Petro, “Lisha kondoo wangu.” Hili ndilo jukumu na wajibu mkubwa wa wachungaji. Wanapaswa kufanya hivyo pasipokujifanya kama mabwana dhidi ya watu wa Mungu. Haiwapasi wachungaji kutumia nafasi zao kutawala au kuwamiliki maisha ya watu wa Mungu. Haiwapasi kuwa na au kutumia mamlaka zao juu ya watu wa Mungu, kana kwamba wao ni machifu wa vijiji, kama rais wa nchi – hili ndilo fundisho la neno la Mungu! Hebu msikilize Yesu mwenyewe asemavyo hapa,

“Yesu akawaita, akawaambia, Mwajua yakuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa mataifa HUWATAWALA (KAMA MABWANA), na wakubwa wao huwatumikisha. LAKINI HAITAKUWA HIVYO KWENU. . . ” (Marko 10:42, 43).

Unaona hapo?  Bwana Yesu alisema ‘haitakuwa hivyo kwenu’; hivyo basi, jambo hili likoje huko kanisani kwako? Jambo hilohilo linapatikana kwenye Biblia tafsiri ya Kiswahili, inasema, “hutawala kwa nguvu”, lakini maneno ‘kwa nguvu’ haionekani katika tafsiri halisia ya asili. Wale watafsiri waliongeza neno hill. Neno lililotumika katika kigiriki/kiyunani halisia ilimaanisha ‘kutawala juu ya mwingine kama bwana…’! Na katika kiyunani/kigiriki halisia kwenye Agano Jipya neno hili ‘hutawala’ ilivyoainishwa katika Injili ya Marko 10:42, ni neno LILELILE kama ‘wajifanyao mabwana juu ya. . . ‘ katika 1 Petro 5:3 (neno ‘katakurieuo’). Neno hili linamaanisha, ‘ kutawala kama bwana’ – na Bwana wetu Yesu Kristo ametuagiza kuwa wachungaji wasiishi maisha ya mfumo wa aina hiyo! Yesu anasemaje sasa kuhusu wale wanaoongoza watu makanisani?  Anasema, “bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa MTUMISHI wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza kwenu, atakuwa MTUMWA wa wote”. (Marko 10:43, 44). Haya basi jambo hili linaonekanaje kanisani kwako? Je, inafanana na hili tunaloliongelea hapa? 

Kipengele cha msingi cha mchungaji ni kuwatumikia waumini kama mtumishi wao (Mathayo 20:25-27; Yoh.13:14,15). Anawahudumia na kuwalisha neno la Mungu, anawahudumia kwa upendo na kuwajali, na wala hatumii cheo chake kunifanya kana kwamba yeye ni bwana juu ya waumini wale, au juu ya maisha yao, au juu ya imani yao. Paulo analiweka jambo hilo kwa uwazi kabisa pale anapowaambia Wakorintho, “si kwamba tunatawala imani yenu, bali tu wasaidizi wa furaha yenu”. (2 Wakor.1:24). Hata pale Paulo alipowasahihisha na kuwakemea Wakorintho, hakufanya hivyo ili kutafuta kuwamiliki na kuwatawala maisha ya kila siku ya Wakorintho. Hata pale baadaye katika nyaraka zake anasema, “kwa maana hatujihubiri wenyewe, bali Kristo Yesu yakuwa ni Bwana, na sisi wenyewe kuwa tu watumishi wenu kwa ajili ya Yesu” (2 Wakor.4:5). Unaona hapo! Paulo anajitangaza mwenyewe kuwa yeye ni mtumishi wao! Anapowaandikia Wathesalonike, Paulo anasema, “Hatukutafuta utukufu kwa wanadamu, wala kwenu, wala kwa wengine tulipokuwa tukiweza kuwalemea kama mitume wa Kristo. bali tulikuwa wapole katikati yenu, kama vile mlezi awatunzavyo watoto wake mwenyewe. Vivyo hivyo nasi tukiwatumaini kwa upendo mwingi, tuliona furaha kuwapa, si injili ya Mungu tu, bali na roho zetu pia kwa sababu mumekuwa wapendwa wetu.” (2 Wathesalonike 2:6-8). Mchungaji wa kweli nia yake si kuhubiri tu, bali ni kuyatoa maisha yake kwa ajili ya kondoo anazozichunga! Mtume Paulo alimhubiri Kristo, na maisha yake yalimwishia Kristo mbele ya waumini.

Hebu sasa turudi kwenye kitabu cha Waebrania ile sura ya 13, lakini safari hii tuuangalie ule mstari wa 7, ambao unasema kuwa, “wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowambia neno la Mungu, na iigeni imani yao, kwa kuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao.”  Wachungaji  ‘hawatawali’; wachungaji ‘huongoza’. Nyakati zile za Yesu katika nchi ya Israel, ilikuwa ni tabia ya wachungaji kutembea mbele ya kundi la kondoo analolichunga, akiwaongoza, kama vile Bwana Yesu (yule Mchungaji Mkuu wetu) alivyoeleza (Yoh.10:4). Hakuwa akiyaswaga makundi ya kondoo kutokea nyuma ya kundi! Katika mstari wa 7, tunaagizwa kufuata imani ya hao wanaotuongoza na wanaotuhibiria neno la Mungu – kwa kufikiria kwa uangalifu mkubwa mwisho wa mwenendo wao. Maneno haya, “mwishoni mwa mwenendo wao” linamaanisha nini? Maneno haya yanatuomba sisi kufikiria kwa uangalifu mkubwa matunda ya jinsi gani yanayojifunua katika maisha ya hao wanaotuhubiria. Je, matokeo yao ya mwisho katika kuhubiri kwao na kuishi kwao wanabeba matunda ya maisha ya Kristo katika maisha yao? Hebu tuuweke mstari wa 7 na 8 pamoja. Sasa tunasoma, “…kwa kuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao. Yesu Kristo ni yeye yule jana, leo na hata milele.” Unaona? Yatupasa kufuata imani na mafundisho ya hao ambao wanadhirisha uzima wa Kristo Yesu ndani ya maisha yao – yaani mwisho wa mwenendo wao aonekane Yesu Kristo ndani ya maisha yao! Kuhubiri kwao na imani yao izalishe uzima wa Kristo ndani yao. Hiyo ndiyo sababu inayotufanya tufuate imani yao na mahubiri yao ili yazilishe uzima wa Kristo ndani yetu pia!

Kwa hiyo sasa tunaweza kuuelewa vizuri zaidi mstari wa 17 wa sura hii: “Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi.” Kwanza, hebu tutambue kwamba, inasema kwamba tunapaswa ‘kuwatii’ na kujikabidhi kwa hao ‘watuongozao’, haisemwi hapo kuwa, “kwa hao wanaotutawala”. Nakushauri kwa nia njema na kwa mapenzi yake Mungu, usimfuate yeyote yule anayetafuta kutawala wewe katika maisha yako!  Kwa kufanya hivyo, itakuwa ni jambo la hatari sana katika maisha ya kiroho yako na kwa maisha yako kwa ujumla! Tunatakiwa tujikabidhi kwa wale wanaofanya kazi kwa ajili ya kutunza roho zetu, anaoyajali maendeleo yetu ya kiroho! Huduma zao zirandane na ukuaji wetu kiroho katika Bwana, na hiyo ndiyo sababu inayotufanya tujikabidhi kwao – hairandani na wao wafanyapo maamuzi kwa ajili ya mambo muhimu katika maisha yetu badala yetu!

Yesu alisema juu ya mchungaji wa kweli, “Naye awatoapo nje kondoo wake wote, huwatangulia; na wale kondoo humfuata…” (Yoh.10:4), na tumeshaona Petro aliyowaambia wachungaji, yaani, “lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi.” Hayo yote pamoja na Waebrania 13:7,17, inatufundisha kwamba tunapaswa kuwafuata wale ambao ni kielelezo cha Yesu Kristo mbele ya macho yetu. Cheo cha mchungaji hakimpi mchungaji yeyote ruhusa wala nafasi kutawala juu yako au kujifanya bwana, kana kwamba lazima umtii katika kila kitu cha maish yako.

(Ya mwisho niseme kitu juu ya neno ‘watiini’ kwenye Waebrania 13:17. Hapo kwa lugha ya asili, ya Kigiriki, mwaandishi alitumia neno ‘peitho’ – linatafsiriwa ‘watiini’ – lakini kwa ujumla Agano Jipya halitumii neno hili na maana ‘kutii’, linatumia neno ‘hupakouo’. Kwa ujumla neno ‘peitho’ lina maana ‘kushawishi’ (Angalia Luka 16:31), au ‘kutegemea’ (Marko 10:24), au ‘kutumaini/ kuamini’ (2 Wakor.1:9; Matendo 28:24). Kwa hiyo, katika muktadha wetu tungeweza kusema neno ‘peitho’ lina maana ‘kufanya au kufuata jambo fulani kwa sababu umeshawishwa au unaamini ni sawa au vizuri kufanya hivyo’. Sasa kwenye Waebrania 13:17 kwa maana hiyo tunaelewa tunapaswa kuwafuata, kuwatumaini – au kuwatii – waliotuongoza kwa sababu tumeshawishiwa na mwendo wao, tabia yao. Kama huutumaini au huujashawishiwa na mwendo wa mchungaji wako, kwa nini unamfuata?! Lakini siyo lazima tuelewe mambo hayo ya Kigiriki, kwani tayari maandiko yameweka maana hayo hayo wazi pasipo kutulazimu kujua Kigiriki!)

Niache niweke wazi hapo: mchungaji akikuambia ukafanye unyang’anyi kwenye duka fulani, je, utamtii mchungaji huyo? Kwa vyovyote vile huwezi kumtii huyo. Mfano huu upo wazi tu. Hebu basi tuuchukue mfano mwingine ambao ni wa kawaida tu. Unaamini kuwa Mungu anakuongoza uhamie katika mji mwingine, halafu hapohapo mchungaji wako anakukataza anakuambia, hayo sio mapenzi ya Mungu, na ya kwamba ni lazima ubakie katika mji huu huu na katika kanisa lake. Utafanyaje hapo? Je, mara moja utamtii mchungaji huyo, kwa kuwa yeye ni mchungaji wako? Sasa, najua kuwa wakati mwingine tunamwamini Mungu kutuongoza katika njia fulanifulani, lakini wakati mwingine tunakuwa hatuna uhakika kikamilifu na wakati mwingine tunakuwa tumekosea. Hiyo ndiyo sababu katika maamuzi ya namna hii ni vema kumsubiria Bwana, hali kadhalika na kusikiliza ushauri wa watu wengine pia, ikiwa ni pamoja na ushauri utokao kwa mchungaji wako pia, kwa maana wanaweza wakawa na jambo la kusema ambalo laweza kutusaidia kutambua mapenzi ya Mungu. Hii ni hali ya kawaida na kwa ujumla ni nzuri. Hakuna jambo lolote baya kumsikiliza ushauri wa mchungaji wako -mradi tu uelewe kuwa huo ni ushauri wake!  Wajibu wako sasa ni kukileta kile anachokuambia mbele za Bwana, ili kuhakiki kama jambo hili ni kweli ndivyo asemavyo kwako. Kisha ni lazima ufanye uchaguzi wenye msingi wa kile unachokiamini, kwamba Mungu anachosema nawe na namna gani anakuongoza wewe.

Kama hufanyi hivyo, na wewe mara moja unamtii tu kwa kile akuambiacho mchungaji, kwa kuwa yeye ni mchungaji wako, ndipo hapo utakuwa unamwinua na kumhofia mwanadamu zaidi kuliko kumwinua na kumhofu Mungu. Utakuwa humtii Mungu au kumumiza Roho wa Mungu. Au ni sawa na kwamba utakuwa humjui Mungu, kwamba hata huna mahusiano naye na kwamba unamuhitaji mwanadamu akuambie wewe jinsi gani Mungu anavyokuongoza katika maisha yako? Neno la Mungu linasema,

“wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu.” (Warumi 8:14).

Je, wewe ni mwana wa Mungu?   Basi uongozwe na Mungu katika maisha yako wala usiruhusu mwanadamu atawale maisha yako. Mchungaji hawezi kukuamulia maamuzi wewe.

Mchungaji hapaswi kukufanyia wewe maamuzi muhimu au badala yako. Hilo sio jukumu lake, wala hiyo siyo huduma yake. Yeye amhubiri ‘Yesu Kristo naye amesulubiwa.’ Afundishe utakaso, neema, upendo, imani na utakatifu ili kwamba upate kukua katika Kristo ili kwamba WEWE ufanye maamuzi yaliyo sahihi katika maisha yako! Mchungaji hana mamlaka yoyote ya kuyatawala maisha yako kwa maamuzi yake anayoyatoa kwako. Kufanya hivyo itakuwa kana kwamba ni namna ya uchawi. Anapaswa kutunza ukuuaji wako mzuri kiroho – hili ndilo jukumu au wajibu wake. Ndiyo, kwa sehemu jukumu lake lingine ni kutoa ushauri kwako, hata na maonyo pia, lakini bado atakuwa hana mamlaka yoyote kibiblia wala kiroho kukufanyia wewe maamuzi kwa ajili ya maisha yako. Kwa hakika hana mamlaka hayo ya kukuamuria nini ukifanye au kipi usikifanye katika mambo yako ya kila siku katika maisha yako. Ikiwa atakupatia ushauri mzuri nawe ukautambua upo kwa jinsi hiyo na ukaufuata, basi hapo utabarikiwa. Lakini kama atakupatia ushauri wake kisha na wewe unaubeba tu ushauri huo na kuufuata eti kwa vile tu ni ushauri unaotoka kwa mchungaji wako, kwa jinsi hiyo utakuwa unatembea katika hali ya hatari sana. Kwa sababu kufanya hivyo ni kumwabudu mwanadamu.

Tafadhali, usinielewe vibaya, mimi mwenyewe nimetumika kama mchungaji, na ndiyo, nimewahi kukutana na waumini ambao wamejiamulia tu kuwa Mungu amewaambia kufanya jambo fulani, na hawatakuwa tayari kusikiliza toka kwa mtu yeyote yule. Kimsingi wanataka kile wanachokitaka, na wala hawapo tayari kuruhusu yeyote awazuie! Katika haya ninayoyaandika hakuna lolote ambalo linakusudia kuwatia moyo watu wenye tabia ya ukaidi na ukorofi ya namna hiyo! Watu wa aina hii hujisababishia maumivi na hasara kubwa katika maisha yao ya kiroho na kimwili pia.

Hebu sasa tuliangalie suala la kutafuta bibi harusi/ mchumba. Katika jambo kubwa na muhimu katika maisha yako kama hili, mchungaji, nabii, mtume, hawa wote hawana mstari wowote kimsingi katika Biblia, wala hawana mamlaka yoyote kiroho yupi wa kumwoa, na yupi usimwoe. Huu ni ukichaa. Hii ni udanganyifu na kukaribisha majanga na uchafuzi! Kwa sababu hali kama hiyo haijafundishwa popote pale katika Biblia nzima, na wala hatuna mfano hata mmoja katika maisha ya kibiblia unaoelezea jambo kama hili. Hii ni kweli yenye msingi ulio wazi kabisa ambao tunapaswa kutambua.

Hata hivyo waweza ukaniambia, kwamba mchungaji anao wajibu wa kuwaangalia washirika. (Tayari nimekwisha lishughulikia eneo hili kwa kina kikubwa, lakini wacha tulijadili jambo hili zaidi kidogo.) Ndiyo, ni kweli kuwa mchungaji anao wajibu wa kulichunga kundi nami nimekwishaelezea kuwa mchungaji anaweza akashauri na wakati mwingine hata kuonya pia. Lakini pamoja na wajibu huo alionao, bado hawezi ni nani umwoe na ni nani usimwoe.

Tatizo linaloonekana hapo la kimsingi ni hili:

baadhi ya wachungaji hujifanya kuwa wao ni kama miungu mtu au kama ni bwana katika makanisa yao, jambo ambalo ni kinyume na fundisho lake Yesu Kristo, wala mtume Petro. Na wala sio hivyo tu bali hata washirika wenyewe nao, wapo na taabu ya kumhofu mchungaji wao kana kwamba ni Mungu! Inakuwa kama vile watu vijijini wanavyomhofia chifu wa kijiji!

Huo ndio mzizi wa matatizo yanayotokea.

Matokeo ya hofu hiyo ni yafuatayo: sasa washirika wanaogopa kusema chochote kile ambacho mchungaji wake atakikataa, au kitaweza kumfanya mchungaji huyo asione raha navyo au akakasirika. Hiyo sasa inageuka kuwa ni mila yenye hatari sana kanisani yenye kuleta hofu, na kuabudu sanamu (yaani, kumheshimu mwanadamu kuliko Mungu), na inatuzalishia uovu msingi na dhambi. Hiyo haiwakilishi Kanisa la Bwana; inafanana au inawakilisha udikteta wa biashara.

Kutokana na mila na desturi hizi, kijana anaweza kutamani kwenda kumwona mchungaji wake na kumweleza kuwa angependa kumwona msichana fulani kanisani humo ili kuanzisha mahusiano ya kiuchumba pamoja naye, na mchungaji anaweza tu kusema, ‘Hapana, na hutakiwi kwenda kumwona.’ Na kijana huyo anaishia tu kuikubali ‘sheria’ hiyo ya mchungaji huyo, ‘kanuni’ hiyo, wala hakuna ushauri wowote au hata maelezo yoyote yanayoweza kutolewa na mchungaji huyu! Unakuwa ni uamuzi tu wa mchungaji, kwisha! Hakuna chochote kinachotokea! Yule kijana anabaki peke yake tu pamoja na uamuzi wa mchungaji! Huo ni uonevu mkubwa katika nafsi ya kijana yule! Hii ni kinyume na Biblia; ni mila na desturi za uovu! Mchungaji hiyo anamtendea dhambi kijana yule kwa mgongo wa kichungaji. Hakuna kitu chochote kinacho halalisha tabia ya jinsi hii kwa sababu mchungaji wako yeye sio Mungu! (Tafadhali naomba unielewe, naongelea kuhusu hali ya kawaida huko makanisani, ambayo washirika wengi wanapitia kwa maumivu makubwa sana mioyoni mwao. Siongei juu ya mambo ya dhambi kubwa – hiyo inakuwa ni suala nidhamu ya kikanisa, na hiyo sio jambo tunaloliangalia hapa).

Kinachoumiza zaidi sio tu kwamba mchungaji anajifanya yeye ni kama ‘Bwana’ juu ya waumini, lakini hata washirika wenyewe nao mahala hapo wanamwona mchungaji wao kuwa kama ni bwana au chifu – ni kana kwamba hawajasoma Biblia. Katika hali hii na hasa katika jambo kama hili ni wazi mahali hapo, yaani kanisani hapo panaupungufu mkubwa wa kulielewa neno la Mungu.

Bwana Yesu ALILINUNUA kanisa LAKE kwa damu yake mwenyewe (Matendo 20:28 – na Paulo anawakumbusha wachungaji wale juu ya ukweli huu kwenye mstari huu!), na Yeye ni KICHWA na BWANA wa kanisa lake, na sisi si mali yetu wenyewe, wala si mali ya mchungaji au mtu mwingine, bali mali ya Bwana Yesu tu! (1 Wakor.6:19,20). Lakini badala yake, wachungaji wengi wanawamiliki washirika kama ni mali yao!

Kwa hiyo tabia wanayoionyesha wachungaji wengi kwa vijana wao haitupatii mfano mzuri wa utunzaji mzuri wa kundi kiroho au utimilizaji majukumu ya kiroho – hiyo ni umiliki wa MTU mmoja kwa watu wa Mungu! Ni chukizo mbele za Mungu. Tazama, badala ya watu wa Mungu kuongozwa na Roho wa Mungu katika mapenzi yake (ndiyo, kwa hapa anaweza pia kuhusisha ushauri wa mchungaji lakini sio kuwamiliki watu wa Mungu), mchungaji sasa anachukua utawala wa eneo hili la maisha yao!  Anaichukua nafasi ya Mungu ndani ya maisha ya watu hawa. Mchungaji sasa anakuwa kama ndiyo nabii, anatengeneza utaratibu ili watu wamfuate yeye kuuliza wanapokuwa na hitaji fulani, na hata kuuliza ni nani nimchumbie. Unaona, jinsi ambapo vituko kama hivyo vinavyoweza kuharibu mahusiano yetu na Mungu kwa sababu tu mchungaji wako anachukua nafasi ya Mungu katika maisha ya washirika! Na kama nitajavyozidi kuonyesha wazi, mila na desturi hizi zimekwisha kuumiza na kuharibu maisha ya washirika wengi hasa vijana makanisani.

Tafadhali kumbuka kuwa tangu mwanzoni mwa makala hii nilishasema kuwa sipo hapa ili kumtia moyo mtu yeyote yule ili awe mkorofi au akimbilie katika hali hiyo, wala simtii moyo yoyote yule ili kwamba aache kusikiliza ushauri wa watu wengine ambao utakuwa ni wenye msaada, au kutokuheshimu wengine wanaotaka kumsaidia kwa dhati! Pia najua kuwa vijana hufanya makosa katika eneo hili la maisha kwa sababu 1), wanakosa uvumilivu na hawaungojei muda wa Bwana ili kumpa nafasi Bwana awaletee mtu wa kweli; au 2), wanaupenda ulimwengu zaidi kuliko kumpenda Kristo, na wanafuata matamanio ya mwili na kumbilia kwenye mahusiano mabaya, au katika dhambi; au 3), wanachanganya kati ya kuvutiwa kimwili na upendo, na kadhalika. Ndiyo, mambo haya yote pamoja na mengine zaidi yaweza kuwa ni kweli. Hiyo ndiyo sababu nasema kuwa kilicho cha muhimu ni kwamba mchungaji anapaswa kumhubiri ‘Kristo, naye amesulubiwa’, na nguvu ya msalaba itutakasayo na kutuokoa kutokana na nguvu ya dhambi. Tukijumlisha na hilo, mafundisho ya kibiblia na ushauri wenye busara unaweza kutolewa kwa vijana kuhusu namna gani wanapaswa kuishi, na jinsi gani wanapaswa kujizuia dhidi ya hatari ya dhambi ili kuzikwepa katika maisha yao. Hayo yote ni mema. Lakini kwa mchungani yule kujifanya kwake aonekane kana kwamba yeye anayo maarifa maalum kuhusu ni nani wewe na mimi wa kumwoa, huo ni udanganyifu mkubwa.

Unaweza ukaniambia, “Oho, lakini waumini wachanga watakuwa hawajakua kiroho vya kutosha kiasi cha wao wenyewe kujiamulia mambo katika suala hili, hivyo wanahitaji miongozo na maamuzi ya mchungaji wao, kwa sababu yeye ndiye anawajua vizuri washirika wote”. Tayari jambo kama hili ninekwisha litolea maelezo hapo juu. Lakini hebu tuliangalie jambo hili zaidi kidogo kutoka katika kipengele kingine cha kibiblia – kipengele cha ukiroho wa mchungaji. Je, wewe unafikiri kuwa mchungaji wako ni wa kiroho kwa sababu tu yeye in mchungaji, au hata ni askofu? Kama unafikiri hivyo basi umesimama kwenye mtazamo wa hatari sana! Yesu alituambia kuwa watatokea mbwa mwitu waliovaa mavazi ya kondoo, nasi tutawatambua kwa matunda yao! Kuwa mchungaji hakuaminishi ukiroho wako!  Mtume Paulo aliwaandikia wachungaji waliopo huko Efeso akisema, “Najua Mimi yakuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa mwitu wakali wataingia kwenu wasilihurumie kundi, tena katika ninyi wenyewe watainuka watu wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi, wawaandame wao.” (Matendo 20:29-30). Kwa hiyo,tunaona kuwa kutokana na mambo haya, mchungaji anaweza akaanza vema lakini baadaye anachafuka kwa sababu ya yale madaraka ambayo cheo chake kinampatia. Anakuwa hawakilishi tena Roho ya Kristo, bali anaanza kulitawala lile kusanyiko kana kwamba yeye ni bwana wa watu wake badala ya Kristo!

Tunayo mifano ya wazi kabisa ya haya yanayotokea, tunayaona katika nyaraka za Yohana wa tatu: “Naliliandikia kanisa neno, lakini Diotrefe, apendaye kuwa wa kwanza kati yao, hatukubali. Kwa hiyo, nikija, nitayakumbuka matendo yake atendayo, atoavyo upuzi juu yetu kwa maneno maovu; wala hatoshwi na hayo, ila yeye mwenyewe hawakaribishi hao ndugu, na wale watakao kuwakaribisha, huwazuia, na kuwatoa katika kanisa.” (m. 9,10). Mistari hiyo hapa inaweka ukweli wazi mbele yetu. Watu wengine, ina maana wachungaji wengine – kama sio wengi – hupenda ukubwa makanisani, jambo ambalo Yesu alisema usitokee kati yetu. Mambo haya hayapaswi kuwa hivyo. Je, unaona? Diotrefe alilimiliki kanisa lote na akalitawala kama vile dikiteta, akijifanya yeye ni bwana juu ya watu wa Mungu! Yeyote yule ambaye hakukubaliana au kuongea kinyume chake hiyo alifukuzwa kanisani. Je, mambo hayako namna hiyo katika baadhi ya makanisa huko Tanzania? Hata wazee wa kanisa hawataki kujisogeza kupinga au kukosoa chochote anachokisema mchungaji yule. Kwa nini basi? Je, wanafanya hayo kutokana na kwamba wanamheshimu mchungaji yule? Jawabu hapa ni, “Hapana”. Wengi wanafanya hivyo kwa sababu wanamwogopa kumsogelea, hawathubutu kusema chochote kinyume cha maneno au mawazo yake – wanaogopa lile ambalo mchungaji huyo anaweza kulifanya dhidi yao. Na kwa hakika washirika hawasemi lolote lile moja kwa moja kutokubaliana na mchungaji wao. Na hii inatokana na hali ya mchungaji yule ya kutawala kama bwana, na watu sasa wanamhofu na kumwogopa. Inafanana kama vile vijijini wanakijiji wanavyoweza kumhofia mganga wa kienyeji – wanaogopa mganga yule anaweza kufanya jambo baya kwao! Mwenendo wa jinsi hii makanisani hauwakilishi Kanisa la Kristo!

Uovu huu umezama ndani kabisa ya fikra za watu wakifikiri kuwa mfumo huu na tabia ya jinsi hiyo ndiyo hali ya kawaida makanisani! Nakuhakikishia kuwa mwenendo wa jinsi hiyo siyo hali ya kawaida katika kanisa la Mungu! Huo ni udanganyifu mtupu. Waumini kule Korintho waliamua au kupima mambo kwa kuangalia mwonejano wa inje (2 Wakor.10:7). Ikiwa mtu yoyote ajifanyae mwenyewe kuwa ni nabii, mtume na kujifanya mwenyewe kuwa ni mtu muhimu, kisha Wakorintho waliwakilisha kwake chochote alichokifanya katikati yao, na wakampatia pesa alipowadai wampe! Wakorintho walimruhusu mtu huyo awamiliki na kuwatawala juu yao – hadi kufikia hatua hata ya kuwapiga!  Sikiliza sasa Paulo anavyosema,

“Maana mwachukuliana na mtu akiwatia utumwani, akiwameza, akiwateka nyara, akijikuza, akiwapiga usoni.” (2 Wakor.11:20).

Na hivyo ndivyo inavyotokea nyakati hizi pia. Huo ni udanganyifu na ni hatari kubwa. Na kutokana na mambo haya Paulo anawaonya Wakorintho, kwamba wapo katika hatari ya kuzipokea roho nyingine tofauti, yesu mwingine, na injili nyingine. Kama nilivyokwisha kusema kuwa mambo kama hayo hayamwakilishi Kristo au kanisa lake.

Hebu niambie, je, utawapenda mbwa mwitu wa aina hii, au wachungaji wa binafsi wawe ndio wachungaji wako?  Au je, wewe unawahesabu wachungaji wote kuwa ni wa kiroho?  Sikiliza maelezo ya kushangaza toka kwa mtume Paulo, katika Wafilipi 2:20-21, ambapo yeye humwongelea Timotheo.  Anasema, “maana sina mtu mwingine mwenye nia moja nami atakaye iangalia hali yenu kwelikweli, maana wote wanatafuta vyao wenyewe sivyo vya Kristo Yesu”. Hii in ajabu! Huo ndio ushuhuda wake kwa watu wengine baada ya kutumika katika huduma kwa miaka mingi. Anasema kwamba wengi hutafuta vyao wenyewe, na kiuhalisia hawalijali kundi!  Kwa nini iko hivyo! Hii ni kwa sababu watu wengi katika huduma hupenda madaraka, wapenda kuwa na mamlaka, wanapenda pesa, wanapenda umaarufu. (2 Wakor.11:20; 1 Wathes.2:5,6; 2 Tim. 4:10). Mambo hayo yote ndiyo yanayo chafua moyo wa mtu, na ndicho kimfanyacho ajifanye kuwa kama Bwana au Mungu kanisani kwake. Watu wa jamii hiyo kwa hakika sio watu wa kiroho, na wala hawawezi kiukweli kuwalisha au kuwaongoza watu wa Mungu kiroho ili wapate kuingia kwa Yesu na katika busara ya kweli ya Kristo.

Ukiroho wa mchungaji wako sio hakikisho, eti tu kwa sababu yeye amefanywa awe mchungaji.

Unakumbuka tulitazama mistari katika Waebr.13:7, na hapo tumeelezwa kuyaangalia kwa umakini mwenendo wao watuongozao na kuona ni namna gani mwenendo wao kimaisha unaweza kutuongoza sisi. Nasi tuliona kuwa mwisho wake au mwelekeo wa mienendo yao ya maisha ionyeshe maisha ya Yesu! Hao ndio aina ya wachungaji ambao tunapaswa kuwafuata na kujikabidhi kwao.

Kwa nini basi nayaandika mambo kama hayo! Siandiki hayo yote ili kusema kuwa wachungaji wote sio wa kiroho! Hapana sisemi hivyo hata kidogo! Ninayaandika hayo kujibu fikra za udanganyifu zinazofikiria kuwa mchungaji yeye ni mtu wa kiroho eti kwa sababu tu yeye ni mchungaji! Na jambo la pili nayaandika hayo ili kuzijibu zile fikra zilizopotoshwa wanaofikiria kuwa eti mchungaji ni mtu wa kiroho atoshaye kukuambia wewe ni mtu gani umchague kumwoa. Ikiwa mila na desturi ya aina hii itaendelea kuruhusiwa kustawi kanisani, basi inafungulia mlango aina zote za uovu ziingie ndani. Inampa mchungaji nguvu na uwezo ambao mwananadamu hapaswi kuwa nao. Hebu nikupe baadhi ya mifano halisia na pengine hata wewe unaweza kuongezea mifano yako mingine ambayo unaijua.

Mchungaji ambaye alikuwa na mkewe tayari alikuwa na mahusiano na mwanamke mwingine ndani ya kanisa. Mama huyo akashika mimba kwani wametenda uzinzi, lakini mara tu mchungaji alipogundua kuwa mwanamke yule ameshika mimba yake, akamfuata kijana mmoja kanisani hapo na akamwambia, “Kijana, huu ni wakati wako sasa wa kupata kuoa, kwa sababu umri wako tayari umeenda sana. Hebu tazama je, huoni kuwa binti fulani hapa kanisani ni mshirika mzuri? Ninafikiri huyo atakuwa mke wako mzuri!” Na kwa vyovyote mchungaji yule alitaja jina la yule mshirika pale kanisani ambaye tayari ameshampatia mimba. Ni wazi hapo kuwa mchungaji yule alimficha kijana yule taarifa zake za mahusiano yake na mshirika yule. Kijana huyo sasa akayaamini mawazo na ushauri wa mchungaji na akayafuata, na muda mfupi tu alimwoa binti yule ambaye amewekwa mimba na mchungaji wake. Kwa vyovyote vile, hatimaye, kweli ilijulikana mwishoni. Tukio kama hilihili lilitokea kwenye makanisa mawili tofauti – moja katika maeneo ya huko Iringa, na nyingine Morogoro, Tanzania. Kwenye kanisa la kwanza, kijana yule aliendelea kuishi na binti yule ambaye alimwoa ambaye alipewa mimba na mchungaji wake. Katika kanisani lingine, shauri hili lilipelekwa mahakamani na ndoa ile ikavunjwa! 

Jambo hili linaumiza sana moyo! Sio kwamba mchungaji anaharibu maisha ya mtu – ya yule mwanamke – lakini hii yote ni kwa sababu ya mila na desturi iliyopo makanisani, na mwenendo wake mchungaji kujifanya kama mfano wa Mungu kanisani humo, anaweza pia kuharibu maisha ya mtu mwingine pia – maisha ya kijana yule pia! Je, inakuwaje sasa juu ya wazazi wa vijana wa pande hizi mbili? Ni maumivu ya kichwa kiasi gani wanayapitia wazazi hawa!? Kwa hiyo desturi ya jinsi hii sio ya kibiblua tu, bali inaharibu mahusiano yetu ya ndani na Mungu, kwa kule kusambaza uwezo wa kiMungu kwa mwanadamu. Uwezo ambao mwanadamu hapaswi kuwa nao! Kwa sababu ya mambo haya, kama nilivyokwisha kusema, inafungua mlango wa aina zote za uovu na dhambi.

Hivyo kijana hapo kanisani anaweza kwenda kwa mchungaji wake na kumwomba kuanzisha uhusiano na mwanamke kanisani. Mchungaji anaweza kusema ‘hapana’, na katika makanisa mengine hata hasemi kwa nini. Kwa hakika hii ni makosa. Kwa nini mchungaji aseme hapana? Je, inakuwa hivyo kwa sababu yeye anadhaniwa kuwa ni mtu wa kiroho sana na kwamba anayo maarifa maalum kutoka kwa Mungu kuwa ndoa ya jinsi ile haita kuwa ya haki? Au kwa sababu kijana yule wa kike anaongoza kwaya kanisani hapo au anayo majukumu mengine humo kanisani na mchungaji wake hapendi ‘kumpoteza’ binti yule kwa kwenda kuolewa? Au kwa kuwa msichana yule ni mrembo, hivyo mchungaji yule anapendezwa naye ili awepo hapo kanisani kama binti asiyeolewa bado? Au ni kwa sababu binti ni mrembo sana na hivyo mchungaji wake anapanga kuanzisha mahusiano naye?  Au je, inawezekana ni kwa sababu mchungaji huyu aliwahi kukosana na kijana huyo hivyo humfanyia visa? Au ni kwa sababu mchungaji huyu hampendi kijana huyo?  Au ni kwa sababu. . . . au ni kwa sababu. . . . au ni kwa sababu. . .? Unaona? Mfumo huu hufungulia mlango wa aina zote za uchafuzi dhambi na mchanganyiko. 

Iwapo lipo dhehebu linalo mpatia mchungaji wake aina hii ya mamlaka na utoaji wa maamuzi, basi ndipo watakuwa wanamtendea dhambi kinyume naye kupitia desturi zake ambazo si za kiBiblia, kwa sababu watakuwa wanamweka katika hatari ya wazi ya kushikwa na majaribu ya nguvu na kuyatawala maisha ya watu ambayo asingekuwa nayo!

Ni hali gani ya kutisha hii! Kuna uwezekano kuwa Mungu mwenyewe anaamsha matamanio kwa vijana ili kumwongoza apate bibi arusi kwa maisha yake ya baadaye. Lakini sasa mchungaji anaweza kuvuruga na kuharibu kile akifanyacho Mungu bila mtu yoyote yule kufahamu sababu yake! Kwa ujumla ulimweguni mambo kama hayo hayapo – kwa sababu hata kwenye Biblia pia mambo kama hayo hayapo! Hayaja andikwa popote pale kwa sababu sio utaratibu wa ki-Mungu. Kutokana tu na uradhi wake na anavyopendelea mwenyewe mchungaji anaweza kuwazuia watu wawili kufahamiana. Tumekwisha taja ukweli mkuu ufuatao, “…kwa hiyo alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.” Najua wazi hii inahusu ndoa kati ya watu wawili, lakini ikiwa sisi tu watoto wake Mungu, je, yeye Mungu hafanyi kazi ndani ya mioyo yetu na kutuongoza kwa mtu ambaye ndiye atakuwa mume wetu au mke wetu? Ingawa bila shaka tukawa hatujasikia sauti yoyote toka kwa Mungu, kwa vyovyote vile itakavyokuwa, je, yeye hatupatii amani ndani ya mioyo yetu ambayo inatenda kazi ya kututhibitishia juu ya njia itupasayo kuiendea na yupi tuweze kuwa naye? Je, Mungu hawaleti watu wawili pamoja ili wapate kukaa pamoja sawasawa na mapenzi Yake? Nasikitika sana kuiona ni hukumu ya jinsi gani inayomsubiri mchungaji huyu, ambaye hata pasipo mamlaka yoyote ile au maongozi kutoka kwa Mungu, yeye anawazuia watu wawili wasifahamiane, watu ambao inawezekana Mungu angependa waunganike pamoja!

Kama tulivyokwisha kuona uovu huu unaweza kufanya kazi kwa namna nyingine pia, sio tu kwamba mchungaji aweza kuuzuia uhusiano halisia usiumbike kati ya wawili hao wapendenao, bali kutokana na nguvu zake na madaraka aliyojitwalia kanisani hapo, yeye aweza pia kuwaongoza vijana watumbukie katika mahusiano na mshirika mwingne hapo kanisani ambayo siyo sahihi wala yasiyo na muafaka. Jambo kama hili pia linayo madhara yake!

Kuna mifano mingine ambayo yenyewe hauhusishi tendo la dhambi kama mifano iliyopita hapo juu. Lakini maafa yake yanaweza kufanana. Mchungaji atamfuata kijana na kumwambia kuwa binti fulani kanisani hapo ni mzuri kwa kuolewa na atakakuwa ni mke mzuri kwa ajili ya kijana huyo! Na jambo kama hili kwa kijana kanisani hapo anaweza kufikiri kuwa ni jambo lenye mamlaka ya ki-mungu litokalo kwa mchungaji, na hivyo kijana huyo anafikiri ni sahihi na vizuri kumwoa binti yule. Na sasa ni nani ajuaye, na hasa ni kwa sababu zipi mchungaji huyu anafanya jambo kama hili! Je, hiyo haiwezi kuwa ndiyo sababu kwa baadhi ya ndoa – kama si nyingi – huishia katika kuvunjika na kupeana talaka baada ya muda tu tangu wafunge ndoa hiyo? Nimeambiwa kuwa hiyo ndiyo sababu kubwa inayopelekea kuvunjika ndoa mapema, na haishangazi kuona hivyo.

Watu wawili wamefahamiana kwa kuunganishwa na mchungaji, watu hao wawili wameunganishwa tu pasipo hata wao mwenyewe kujisikia kuwa wanapendana, na pengine hata hawajuani vizuri, wameelemezwa na mchungaji wao kujitumbukiza kwenye ndoa ambayo kimsingi na mwanzoni sio uchaguzi wa mpango wa matakwa yao. Kwa halj hivyo mara nyingi ndoa za jinsi hii zitazaa matatizo tu, tena ni matatizo makubwa katika ndoa za aina hii zisizo na muafaka wowote. Na matatizo hayo yatakuwa yamesababishwa na desturi hizi za uovu.

Hadithi zote pamoja na mifano niliyoielezea hapo juu inaleta ugumu kuelezea uharibifu na masumbufu yanayoumiza kichwa ambayo yanasababishwa tu na desturi hizi ambazo si za kibiblia kabisa! Mfumo huu wa uangalizi wa makanisa uliopitiliza/usiofaa kitu hauharibu tu uelewa wa kibiblia pamoja na mahusiano ya watu na Mungu wao tu, bali zaidi inawanyima watu uwezo wao wa kawaida wa kufikiri juu ya mambo yao yanayowahusu. Inalingana na maneno ya nabii aliyosema kwamba, “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, Mimi nami nimekukataa wewe usiwe kuhani kwangu mimi, kwakuwa umeisahau sheria ya Mungu wao.” (Hosea 4:6). Watu hawalifuati neno la Mungu wala kweli lake, wanapendelea kuyafuata mapokeo/desturi za kibinadamu kuliko kufuata maarifa ya Mungu!

 Hapa sisemi kwamba kila mchungaji anayehusika na mfumo huu ni mwovu, au sio wa kiroho! Kwa hakika inaweza ikatokea mahala fulani katika kanisa jambo hili likazoeleka kwa muda mrefu hata ikawa ndiyo desturi ya kanisa hilo, lakini wao wenyewe wakawa ni wa kiroho. Hawachafui mamlaka hiyo au vyeo vyao kama wachungaji, wala hawazuilii mambo ambayo Mungu angeyafanya katika maisha ya watu. Wanashauri na kutoa maelekezo, yawezekana hata kuonya lakini hawatafuti kutawala maisha ya watu. Bwana asifiwe kwa kuwa na watu wa kiroho wa aina hii mahala popote walipo!

Kwa mara nyingine tena, ningependa kuweka wazi kuwa siandiki mambo haya ili kwamba umdharau mchungaji wako, kwa vyovyote vile alivyo awe ni mtu wa kiroho au kimwili. Tayari nimekwisha kunukuu mistari ya neno la Mungu inayofundisha kwamba yatupasa tuwatii wale wanaotuongoza na wanaotuangalia kiroho.Lakini bado hii haimanishi kuwa tunapaswa kuwatii kwa kila jambo ambalo hata Neno la Mungu haliwapatii mamlaka ya kufanya hivyo. Nayaandika mambo haya ili kumpatia msomaji wangu ufahamu wa kibibilia kuhusiana na eneo hili la maisha ya kanisa ili kwamba wasitumbukie katika mitego ya kishetani! Nayaandika mambo haya ili kwamba vijana kwa natumaini makubwa waione njia ya kupita kuelekea katika mapenzi ya Mungu ndani ya maisha yao.

Nayaandika haya kutokana na matukio yafuatayo hapa chini ambayo yametokea mwaka huu (2017) huko Nigeria katika mji Wa Delta state, Warri, kwenye kanisa la mtu mmoja anayejiita mwenyewe kuwa ni nabii. Nabii huyo anamwita mwanamke aje mbele kutoka kwenye kongamano lake kisha anamwuliza kama mume wake yupo hapo kwenye hilo kongamano. Mama yule anajibu kuwa yeye hajaolewa, ndipo tena anamwambia azunguke kanisani mle ambalo ni kanisa kubwa na limejaa watu wengi, na katika mizunguko yake aangalie ni kijana yupi amchague kuwa mchumba wake ambaye ndiye ampendaye kuolewa naye. Baada ya kutembea akilizunguka kanisa lote, mama huyu anakuja mbele na kumwambia nabii yule kuwa hajamwona yeyote yule ambaye angependa kumchagua. Hapo ndipo nabii huyu anawakaribisha vijana toka kwenye kusanyiko lile wanaopenda kumwoa msichana yule waje mbele. Wanaume nane wanajitokeza kuja kusimama mbele, lakini bado binti yule haoni yeyote kati ya hao nane ambaye atafaa kumwoa. Ndipo nabii yule anamwambia mama yule kuwa analo tatizo la kiroho. Kisha anawaalika wamama ambao hawajaolewa waje mbele na wasimame nyuma ya vijana wale nane ambao wanawapenda na kwamba wangependa wawaoe. Wanawake wengi wanakimbilia mbele na kufoleni nyuma ya kijana ambaye angempenda, kwa hiyo kijana mmoja alikusanyikiwa na wamama 11 ambao walipenda waolewe naye. Kisha yule nabii akamweleza yule kijana kuwa anampa mwezi mmoja kuchagua mchumba kati ya wale wanawake waliokusanyika kusimama nyuma yake! Kisha akawaomba wachungaji wengineo waliokuwepo kwenye kongamano lile kuandika majina yao na akasema kuwa itakapokuwa kijana amechagua mchumba wake tayari yeye ataigharimia harusi ile siku ileile. Mtu awezeje kulielezea jambo kama hili kuwa ndio jambo la kikristo au ni la kibibilia!?

Ikiwa umeshitushwa na jambo kama hili, je, ikoje kanisani kwako, nchini kwako? Ikiwa mchungaji anatumia cheo chake kukuambia ni nani umwoe au ni nani usimwoe, au anakuambia unapaswa kumwoa fulani, basi kanisani kwako hakuna tofauti yoyote na mambo hayo yaliyotokea hapo juu. Yawezekana ikawa ni tofauti katika kiwango au namna inavyotokea, lakini kwa kiini chake huyo ni mfumo uleule wa desturi za uovu. Inaweza ikawa ikaleta ukubwa tofauti wa matunda yake, lakini mbegu ni ileile ya uovu, mizizi yake nayo ni ile ile ya uovu na uchafu.

Unaweza ukaniuliza nifanye nini sasa ninapojikuta niko katika kanisa la aina hiyo? Katika kujibu swali hili hebu kwanza nikuelezee mfano mwingine wa kweli uliotokea katika kanisa moja huko Tanzania. Walikuwepo vijana wawili ambao walipendana waliona kuwa wangeoana lakini mchungaji wao aligoma kuwapa kibali cha kuendelea kuchumbiana. Binti alimfuata mchungaji wake na kumwelezea kwa machozi mengi kuwa wao wanapendana na wangependa waoane, na pia wazazi zao pande zote mbili wamekubali kuwa na wameruhusu waoane, lakini mchungaji anamwambia yule binti, “Mungu hajasema nami juu ya uchumba wenu,” na mchungaji huyu hakutoa ruhusa kabisa juu ya kuendeleza uchumba wao! Je, ni nani anayeweza kuzitetea hoja za uovu kama huu anaoutenda mchungaji huyu kwa binti yule! Ni nani awezaje kutetea undanganyifu huu wa maamuzi yasiyo ya kibibilia yatendeke katika kanisa la Mungu? Ni sababu zipi zinazomfanya mchungaji huyu afikiri kuwa Mungu anapaswa azungumze na yeye kwanza kuhusu ni nani katika washirika alionao waoane au wasioane?

Hata hivyo vijana wao wawili waliamini kuwa Mungu anawaunganisha pamoja waliamua kuhama kanisa hilo na kwenda zao kujiunga na kanisa jingine. Kwa kufanya hivyo hawakufanya kosa lolote. Mahusiano yao binafsi na Mungu ni jambo kubwa na muhimu zaidi kuliko kujisalimisha mikononi mwa utawala wa uovu wa aina ile ya mchungaji. Kuhama kanisa kwa sababu ya kujipisha na uovu si dhambi. Sasa, mchungaji yule alipoambiwa kuwa vijana wale wamehama kanisani, mchungaji yule alitangaza kanisani siku ya jumapili kuwa, ‘Vijana wale wawili waliohama nawalaani, nayalaani maisha yao wote wawili’. Lakini laana hiyo haikuwapata! Zaidi ya yote, vijana walipokelewa vizuri katika kanisa jingine, wakaoana vizuri, hadi siku hii ya leo wanaishi vizuri. Ndiyo, wachungaji wengine wanapenda sana kukuambia utalaaniwa kama ukiachana na kanisa lao, na kwa hila na mbinu hiyo wanataka kukutisha ili usiache kanisa lao!

Vijana hao wawili walipata ujasiri wa kuachana na kanisa lile la kwanza lenye misukosuko ya uovu mwingi. Walimwamini Mungu zaidi kuliko kumwamini mwanadamu. Kumhofu Mungu zaidi kuliko kumhofu mwanadamu, walikuwa na hisia ya kile Mungu anakifanya katika maisha yao na wakachagua kufuata yale waliyoyaamini kuwa ni maongozi ya Mungu ndani ya maisha yao. Hata hivyo, kwa wengine ni tatizo, ijapokuwa nimetaja mwanzoni mapema, lakini hata sasa ningependa tuliangalie kwa undani na mpangilio zaidi.

Kwenye baadhi ya makanisa (sio makanisa yote) inafundishwa kuwa kanisa hilo ulilojiunga ni sehemu ambayo unakutana na Mungu mwenyewe. Na hapo ndipo huduma ya Roho Mtakatifu ilipo. Hapo ndipo ilipo madhabahu ya Bwana, na kwamba sasa hapo ndipo mahali ambapo mchungaji wako anaowajibu wa kutunza afya yako kiroho. Fundisho hilo kukaziwa sana, hurudiwa rudiwa kwenye vipindi vingi kiasi kwamba waumini wanafanyika kuwazia kuwa umehama kanisani hapo, basi watakuwa wanamwacha Mungu, watakuwa wanatembea na anguko mabegani mwao. Wanafundisha kuwa usipomtii mchungaji wako katika jambo lolote analokuambia kulitenda basi wewe utakuwa humtii Mungu, kuwa eti kama unahama kanisa basi utalaaniwa na Mungu. Ni udanganyifu wa ukatili wa jinsi gani huu! Huo ni uwongo mtupu, ni upotoshaji wa neno la Mungu. Mambo ya aina ya vitisho, hofu, hupatikana katika ufalme wa giza pekee, kwenye jumuia za wachawi na waganga wa kienyeji tu, pengine dalili zake tunaziona katika ulimwengu wa falme cha machifu wa vijijini! Huo ni msiba mkubwa kwa waumini wanaoendelea kufikiri fundisho la jinsi hiyo latoka kwa Mungu aliye hai! Fundidho hilo ni la uwongo kwa sababu halijafundishwa mahala popote katika Agano Jipya, na isipokuwa kinyume chake lipo fundisho katika Agano Jipya linalosema watajitokeza watu watakao wadhibiti na kuwatawala makongamano na kujifanya wao kuonekana kama ni mabwana juu yao!

Hivyo basi, ni nini matokeo ya mafundisho kama hayo? Kwanza, waumini makanisani humo hawatakuwa na heshima za kweli toka mioyoni mwao kwa wachungaji wao, kwa sababu wanamhofia mchungaji wao kutokana na hofu ya kibinadamu tu. Mchungaji pamoja na kile anachokisema karibu kina uzito uleule kana kwamba alikuwa ndio Mungu. Ni kinyume na neno lake Yesu na hata la Petro! Wachungaji wa namna hiyo wanatawala, yaani, huwatiisha watu chini yao. Huamuru huyu ‘nenda’ akaenda, na huyu ‘rudi’ akarudi kwa amri yao. Wao ni mabwana, wenye kuheshimiwa, wenye kutunzwa, kunyenyekewa, kuogopwa, nakuitwa baba. Wao kila mshiriki ni mtoto, na wengine wao huuza huduma kwa fedha. Hiyo sio kumheshimu mchungaji, hiyo ni utumwa! Inatengeneza desturi ya umiliki kwa sehemu ya mchungaji huyu, na pia mila na desturi ya hofu kwa upande wa makutaniko yale. Wala aina hii ya hofu haiwakilishi aina yoyote ile ya heshima kwa mchungaji – inawakilisha vifungo vya kiroho kwa watu wa Mungu. Hii haitii moyo ukuaji wa kiroho katika Kristo, badala yake inauzuia inauharibu! Hakuna lolote kati ya hayo yanayowakilisha Roho ya Kristo au kanisa lake.

Kwa hiyo matokeo ya haya yote ni nini kulingana na muktadha wa yale tunayoyafikiria katika somo hili? Matokeo yake ni kwamba sio kila mmoja anao uwezo au ujasiri wa kufanya kile walichokifanya vijana wale wawili walioelezwa katika habari ya hapo juu, kwa kulihama kanisa lao na kisha kwenda kujitafutia kanisa lingine mahala ambapo uongozi na uangalizi mzuri wa kiroho. Washirika wengi wamefungwa kwa utumwa wakifikiri labda nikihama kanisa langu kinyume na matakwa ya mchungaji wangu, basi watakuwa wanahesabika kuwa wanamwacha Mungu au wameanguka kiroho, au watakuwa wanapoteza baraka za Mungu. Kwa kweli hii ni aina ya mifumo ya kishirikina au uchawi. Na kama watu watakuwa wamefungwa kwa utumwa wa aina ya desturi hii, basi kuna uwezekano wa aina mbili tu ya uchaguzi unaotokea. Baadhi yao watajinyenyekeza kwa mchungaji wakimwona kavile ni Mungu wao, na pengine kumruhusu mchungaji kuvuruga hata yale ambayo labda Mungu anapenda kuyafanya ndani ya maisha yao. Wengine wao si kwamba watalihama kanisa hili tu, bali pamoja na haya yote, wataacha kumfuata Yesu. Kwa nini? Kwa sababu watu hao kwa ujumla wamedanganywa kwa mafundisho ya mahali pale ambapo ni kanisa wanaloshiriki, wameambiwa hapo ndipo mahali sahihi ambapo watabarikiwa na Mungu, na kwamba kuacha kanisa hili kinyume na ruhusa ya mchungaji, ni kama vile kutokutii au ni dhambi kwao mbele za Mungu! Hivyo wanapoamua kulihama kanisa hili kwa kuwa mchungaji wake amegoma kuwa ruhusa ili kuoana, wanaamini kuwa wakifanya hivyo basi watakuwa wamemwasi Yesu. Nimejulishwa kuwa watu wengi hasa vijana wameacha kumfuata Yesu Kristo kwa sababu ya mambo kama hayo. Inashangaza sana kuona jinsi udanganyifu huu ulivyozama ndani ya mioyo ya watu wengi. Inaniwia vigumu kusikia na kuona kuwa watu wanadanganyika kwa kiwango hicho wakati sisi wenyewe tunayo Biblia ambayo inatueleza kwa uwazi kabisa kuwa fundisho kama hili halijafundishwa katika sehemu yoyote.

Ninachosema ni nini? Ninasema kuwa ikiwa wewe ni mwana wa Mungu, unayo majukumu ya kujiangalia mwenyewe juu ya uhusiano wako na Mungu. Mwishowe, unapaswa kumtii Mungu kuliko kumtii mwanadamu – haijalishi hata kama mtu huyo ni mchungaji wako au hata anayeitwa ni mtume.

Wana wa Mungu huongozwa kwa Roho ya Mungu (Warumi 8:14).

Ndiyo, hili ni jambo la lazima! Nawe unapaswa kujijua Bwana afanyacho katika maisha yao na jinsi gani anakuongoza. Inakupasa kumsubiri Mungu na kujua ushuhuda wa Roho ndani ya moyo wako wewe mwenyewe. Iwapo unayo mahusiano na Yesu Christo basi itapaswa iwe namna hiyo, pasipo kujali gharama zozote zile. Usiende kinyume na ushuhuda wa Roho Mtakatifu ndani ya moyo wako wala usiende kinyume na kile unachokiamini kuwa Mungu anakifanya ndani ya maisha yako na anaongea nawe. Inatokea mara kwa mara katika maisha yetu kuna mambo ambayo Bwana anayafanya katika maisha yetu binafsi ambayo ni ya kimsingi kwetu kuyatambua na kuyajua, na sio tu mwingine fulani. Mungu hamwambii mtu mwingine yoyote yule. Anakutegemea wewe mwenyewe kujua na kutembea katika utii wa imani. Hii ni sehemu ya ukuaji ki Roho katika Bwana!

Kwenye 1 Wafalme sura ya 13, Mungu anamtuma nabii kwenda Betheli kutoa unabii huko dhidi ya madhabahu ya Jeroboam. Mungu pia alishamwambia nabii huyo kwamba asile chakula wala kunywa maji na wala asirudi kwa njia ileile aliyoijia wakati anaenda kutoa unabii huko Bethel. Baadaye mara tu baada ya nabii kufanya unabii, nabii mzee moja aliyekuwa akiishi katika mji uleule wa Bethel akamwendea nabii huyo na akamwomba arudi aje nyumbani kwake akapate kula chakula. Lakini nabii kijana akasema hawezi kufanya hivyo kwa sababu Mungu amemkataza. Yule nabii mzee naye akasema Mungu amesema naye pia kupitia malaika na kumwagiza kuwa nabii yule kijana arudi na kwenda nyumbani kwa huyu nabii mzee kula chakula. Basi yule nabii kijana alikubali na akaenda nyumbani kwa nabii mzee. Lakini Baada ya kula na kunywa, nabii mzee akatoa unabii dhidi ya mgeni wake (nabii kijana) kwa sababu hakumtii Mungu! Na mara tu nabii huyo kijana alipoaga na kuondoka kutoka kwenye nyumba ya nabii mzee alikutana na simba njiani na akauawa!  

Ni muhimu sana kufahamu Mungu anasema nini katika maisha yako! Mtu mwingine hapaswi kujifanya kama yeye ndio Mungu kwenye maisha yako! Ikiwa tutayaachilia mambo kama hayo yatokee katika maisha yetu, tutakuwa tunampa fursa shetani. (Ninaposema unahitaji kujua Mungu anasema nini katika maisha yako, simaanishi kuwa inakupasa kuisikia sauti ya Mungu kimwili, bali namaanisha kuwa Mungu anazungumza nasi kupitia maandiko ya neno lake, kupitia mazingira, kupitia hata watu wengine wanavyosema, na kupitia ushuhuda Wa Roho Mtakatifu ndani ya mioyo yetu.)

Je, wale vijana wawili waliotajwa hapo juu walikuwa sahihi kuhama pale kanisani? Ikiwa watu hawa walipendana, ikiwa wote waliamini kuwa yalikuwa ni mapenzi ya Mungu kwa ajili yao na iwapo kulikuwa hakuna sababu yoyote isiyo ya Ki-Mungu ambayo ingewafanya wakosee, hivyo basi jibu ni ndiyo, kwa hakika hakuna chochote walichokosea katika maamuzi yao ya kulihama kanisa lile, ili kujitafutia mahala pengine salama pa kuabudu. Mbali na swali kuwa je, ilikuwa ni sahihi kwa wao kuendeleza uchumba wao huko walikoenda hata kuoana, au la, kwa ujumla watu hao walifanya vema kujiondoa chini ya huduma ya mwanadamu anayejifikiria kuwa Mungu anapaswa kuongea na yeye kwanza kabla kijana haja hajaamua kuchumbiana! Kuwepo chini ya huduma ya mtu wa aina hii ni hatari. Hata hivyo, iwapo wao kwa ukamilifu kabisa waliamini kuwa Mungu amewaongoza waishi pamoja, basi kulikuwa hakuna kosa lolote kuamua kufanya walichokifanya kwa kulihama kanisa lile. Na kutokana na ushuhuda wa mtu anayewajua vijana wale, kuoana kwao kwa hakika kunaonyesha kuwa no uamuzi mzuri!

Neno la Mungu linasema, “kwa sababu Mungu ni mmoja na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, mwanadamu KRISTO YESU”(1 Tim. 2:5). Hii iko wazi kabisa! Ninajua kuwa mstari huu wa neno la Mungu kimsingi unaelezea kuhusu ukombozi wetu kupitia Yesu Kristo pekee na kibali chetu cha kumjia Mungu kupitia kwake. Lakini pia inakazia ile kweli kuwa tunayo mahusiano ya moja kwa moja na Baba kupitia Mwana! Hivyo basi kwa sasa hatuna kuhani wala mchungaji anayesimama katikati yetu na Mungu katika mahusiano hayo! Mkristo wa kweli amezaliwa upya kwa Roho wa Mungu, na anachokibali cha kumjia yeye kupitia Roho Mtakatifu kwa Yesu Kristo (Waefeso 2:18). Hiyo ndiyo tabia ya Agano Jipya iliyotangazwa na Mungu aliposema,

“Maana hili ndilo agano nitakaloagana na nyumba ya Israeli Baada ya siku zile, asema Bwana; Nitawapa sheria zangu katika nia zao, Na katika mioyo yao nitaziandika; Nami nitakuwa Mungu kwao, Nao watakuwa watu wangu. Nao hawatafundishana kila mtu na jirani yake, Na kila mtu na ndugu yake, akisema, Mjue Bwana; Kwa maana wote watanijua, Tangu mdogo wao hata mkubwa wao.” (Waebr. 8:10-11).

Je, hii ndio kusema kwamba sasa haitupasi kwenda kanisani au kusikiliza neno la Mungu linapohubiriwa? Kwa vyovyote vile hapana. Tunafanya hivyo na yatupasa kufanya hivyo! Isipokuwa hii inamaanisha kwamba tunayo mahusiano yetu binafsi pamoja na Mungu na kutokana na mahusiano hayo binafsi na Mungu wetu tunaweza kujua mapenzi yake mema, timilifu na yanayokubaliwa naye katika maisha yetu (Warumi 12:1,2).

Kwenye dhehebu moja inakupasa umwendee kuhani/padiri ili kupokea msamaha wako kwa ajili ya dhambi. Hivyo hivyo ni kinyume kabisa na maandiko. Kuhani/padiri yule sasa anageuka kuwa ndiye mpatanishi kati yako wewe na Mungu! Sasa kwenye dini nyingine inakupasa umwendee mchungaji ili kufahamu ni nani inanakupasa kumwoa. Hivyo, hiyo nayo ni kinyume kabisa na maandiko ya neno la Mungu. Mchungaji amekuwa mpatanishi kati yako na Mungu! Neno la Mungu linasema,

“Kwa maana ndiye KUSUDI LAKE MUNGU atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza jema.” (Wafilipi 2:13).

Je, unaona hapo? Mungu anatenda kazi ndani yako kwenye moyo wako na katika maisha yako ili kukuletea mapenzi yake na kusudi lake jema. Mungu anatenda kazi ndani yako ili kukuletea ufahamu wa kusudi lake ndani ya maisha yako! Hayupo kabisa mpatanishi mwingine anayesimama kati yako na Mungu isipokuwa mwokozi wako Yesu Kristo! Lakini usikimbilie kwa harakaharaka na kiurahisi tu kukosea kwa yale ambayo wewe mwenyewe unayataka kufanya. Kwa sababu maandiko ya neno la Mungu kabla ya andiko hili yanasema, “basi ndugu zangu…utimizeni wokovu kwenu mwenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.” ( mstari wa 12). Usianze kutumia ile misemo ya ushawishi, “Mungu ameniambia”, au “Roho wa Mungu ananiambia” ili uweze tu kufanya kile ambacho wewe binafsi unapenda ufanye.

Ndiyo Mungu anatenda kazi katika maisha yako ili kulitimiza kusudi lake. Hivyo wewe na mimi yatupasa kuitoa miili yetu kuwa dhabihu iliyo hai na kufanya upya ajili yetu ili kuhakikisha kuwa tunafikia katika kuyafahamu mapenzi yake kwa ajili yetu. Na haitupasi kufanya hivyo katika namna  ya njia ya urahisi na ya kawaida, bali ni katika hofu ya Mungu tukitafuta mapenzi/ kusudi lake na utukufu wake katika maisha yetu!

Sijui kama unamfuata Bwana kwa uhalisia kwa moyo wako wote, au labda tu wewe ni mtu wa Dini sana unayetaka kufuata matamanio ya mwili wako tu. Katika haya yote ninayoyaandika hapa hakuna lolote lile linalokusudia kuwatia moyo vijana kwa makusudi na kwa uchoyo wapuuze ushauri wanaopewa na watu wengine. Hakuna chochote katika yale niliyoyaandika hapa kwamba yawatie moyo vijana waanze kuyafikiria mambo kama haya kiurahisi tu au kutia maamuzi ya haraka na mepesi ambayo yana msingi wa matamanio yao kimwili kwa ajili ya mtu mwingine! Ninafahamu kuwa kuna watu fulanifulani na yawezekana umepata kukutana watu ambayo hupendelea kutumia kauli hizi za kuhofisha na kushawishi kwa kusema, “Mungu Ameniambia……”, au, “Roho wa Mungu ameniambia.” Na huku tunajua kutokana na hali na tabia ya kimwenendo wa maisha kwamba hivyo haina ukweli wowote, isipokuwa watu wa aina hiyo hutumia tu mfumo huu wa maelezo ya kushawishi na kuhofisha ili kuhalalisha kile wanachotaka kufanya.

Sasa mtu aweza kusoma habari hii kisha akafikiri, “Nifanyeje sasa? Kwa sababu kwenye ndoa yangu hii nilimwoa mke huyu, au niliolewa na mume huyu, haya yote sasa ni kwa sababu mwanzoni nilimfuata mchungaji wangu alivyoniamulia na kunipa maelekezo, wala binafsi sikushawishiwa moyoni mwangu juu ya jambo hili. Nilisukumizwa kwenye ndoa hii na mawazo ya mchungaji wangu tu, au na wazee wa kanisa.” Hasa mawazo kama haya humjia mtu ambaye katika ndoa yao wanapitia maisha magumu, usumbufu na taabu nyingi. Hebu kwanza niseme kupitia kwenye matatizo kwenye ndoa yenu haimaanishi kuwa ndoa yenu ina makosa. Jambo la pili ni hili, Mungu hutazama mioyo yetu na kama ulikuwa unafuata ushauri wa mchungaji wako kwa sababu ulifikiria kuwa hivyo ndivyo inavyompendeza Mungu, na ndilo Mungu atalijua jambo hili na yenye ni kwenye rehema aweza kukurehemu katika mapito yako yote! Mtume Paulo akisema alipata rehema kutoka kwa Mungu kutokana na kile alichokifanya – maana aliwatesa Wakristo – aliyafanya hayo kwa ujinga wake. “Ingawa hapo mwanzo nalikuwa mtukanaji na mwenyewe kuwaudhi watu, mwenye jeuri, lakini nalipata rehema kwa kuwa nalitenda hivyo kwa ujinga, na kwa kutokuwa na imani.” (1 Tim. 2:13). Mungu aliujua moyo wako wakati ule, na anaweza kukurehemu kwa undani zaidi ili tupate kutambua na kutengeneza njia kwa ajili yako katika hayo upitiayo kupitia neema na rehema yake.

Jambo la tatu na lenye umuhimu zaidi ni hili, Bwana ni Mungu. Yeye anaujua mwisho tangu mwanzo. Yeye ni Mkuu kuliko vitu vyote. Ni Mkuu kuliko makosa au kasoro yoyote ile unayoifikiria kuwa umeitenda, na ni Mkuu kuliko hukumu yoyote ile inayolenga kukutawala au kubakia katika moyo wako (1 Yoh.3:19,20). Je, mapenzi au kusudi la Mungu kwako ni lipi? Mapenzi ya Mungu kwako ni kwamba usiishi katika mambo ya kale yaliyopita, usitazame nyuma kwenye mambo yaliyopita, usiishi katika majuto kwa sababu unafikiri labda umekosa. Kama kuna jambo lolote ambalo unaamini kuwa yakupasa kulitengeneza liwe sawa kwenye mahusiano yako na Mungu, basi hebu wewe mwenyewe rekebisha na uweke sawa na Mungu mwenyewe. Lakini pia hili hapa ni neno la Mungu kwa ajili yako, “natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu. Basi sisi tulio wakamilifu na tuwaze hayo.” (Wafilipi.3:13-15). Ni hivyo ndivyo ikupasavyo kufanya.

Kama umeoa/ kuolewa unapaswa kumpenda mke wako, kumpenda Mume wako. Ikiwa wewe umeolewa basi ni mwili mmoja na hiyo mumeo, na mkeo pia – na muunganiko huu ni wa Mungu, ni kutokana na Mungu kwa sababu akisema, “Hata wamekuwa si wawili tena bali mwili mmoja, basi aliowaunganisha Mungu mwanadamu asiwatenganishe.” (Mathayo 19:6). Kwa hiyo, usiache mke wako, mume wako! Kimsingi jambo pekee linalovunja ndoa ni kifo cha mmoja wa wanandoa hao (Warumi 7:2,3; 1 Wakor.7:39). Na sababu pekee ya kuachana – kupeana talaka – ni iwapo mmojapo wa wana ndoa hao amefanya uzinzi: “Nami nawaambia ninyi, kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini, naye amwoaye yule aliyeachwa azini.” (Mathayo 19:9). Usimruhusu shetani kuharibu maisha yako ya sasa na ya baadaye kwa kukuelekeza utazame nyuma kwenye mambo yaliyopita na kwenye makosa unayofikiri kuwa ulifanya! ‘Neema yake yatosha.’ Pendo lake lina nguvu za kutosha kukuinua wewe upite vizuri na kukubariki pamoja na mume wako wa sasa au mkeo hadi siku ile mtakapokutana uso kwa uso na Bwana! Kaza moyo wako kwa Mungu, yeye ni mwaminifu atakupa kilicho chema.

Ili kukazia umuhimu wa somo hili na kile ambacho nimetoka kusema kuhusiana na mambo ya kuoana, basi sasa nakwenda kumalizia makala hii kwa kusisitiza umuhimu wake na umaana wake wa kuoana kama ilivyo katika Biblia. Tafadhali soma mambo ya muhimu sana yafuatayo ambayo itatuonyesha jinsi kuoana/ndoa ilivyo ni ya umuhimu na maana mbele za Mungu.

NDOA

Hili ni somo la muhimu na lenye uzito sana. Ni somo la lazima. Mahusiano ya ndoa ni mahusiano yenye umuhimu mkubwa kuliko mahusiano yote ya kibinadamu. Hapo mwanzo Mungu alimwuumba Hawa kutoka katika ubavu wake Adam. Sura ya kwanza ambayo Biblia inatupatia ihusuyo uhusiano wa kibinadamu, sio mahusiano ya wazazi, bali ni mahusiano ya mwanamume na mwanaamke, ya mume na mke wake! Alipokwisha kumuumba mke kwa ajili ya Adam, Mungu akasema, “kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja” (Mwanzo 2:24). Kutokana na mstari huu tunaona kuwa mahusiano ya ndoa yanakipaumbele zaidi dhidi ya mahusiano yaliyopo kati ya mzazi na mtoto – “kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake.” Ninayo mahusiano ya karibu sana na yenye nguvu , mahusiano yenye upendo kwa watoto wangu. Na hicho ndicho tunacho kitarajia kukiona toka kwa kila familia! Lakini sasa watoto wangu watatu walipoolewa, nilitambua kuwa sasa watoto wangu hao wanakwenda kuingia katika mahusiano ambayo yalikuwa ni “yenye nguvu” na hili lichukua kipaumbele kwao kuliko uhusiano uliopo kati yangu na wao – “Na hawa wawili watakuwa mwili mmoja.” Hapo Mungu anaongea juu ya mume na mke.

Alipoulizwa juu ya talaka, Bwana Yesu alinukuu maneno haya kutoka katika kitabu cha Mwanzo, kisha akaongeza, “kwa hiyo hawa si wawili tena, bali ni mwili mmoja, na kwa hiyo kile alichokiunganisha Mungu pamoja, mwanadamu asikitenganishe.” (Mathayo 19:6). Hili hapa ni jambo la ndani kabisa na la ajabu linalopaswa kulielewa!  Mungu ametuumba sisi kwa namna ambayo wanapooana, mume na mke huwa mwili mmoja – na huku ‘kuungana pamoja’ kunatokana na maamuzi ya Mungu mwenyewe! Umuhimu wa jambo hili umewekwa wazi kwetu na Mungu mwenyewe katika Agano la Kale ambalo linasema, ikiwa mtu aliyekwisha kuolewa akilala na mtu mwingine, yaani, watakuwa anafanya usherati, hivyo wote wawili wakikamatwa iliwapasa wapigwe mawe hadi kufa ikiwa itatokea wote wawili wakikubali na kitendo hicho. Watakuwa wameachana vipande kile ambacho Mungu alikiunganisha pamoja! Jambo gani linaloweza kuwa ni la hatari zaidi kuliko lile jambo ambalo unapaswa kufa kwa ajili ya hilo?  Hata hivyo ikiwa ni mwanamume ambaye hajaoa akajilazimisha mwenyewe kulala na mwanamke ambaye hajaolewa kinyume na matakwa ya mwanamke huyo, ndipo Mungu aliamuru kwamba yampasa mwanamume huyo amwoe mwanamke yule kwa sababu amemvunjia heshima mwanamke huyo. (Kumb. 22:22-29).

Kutokana na jambo hili tunaweza kuona kuwa ushirika wa kimwili kati ya mwanamume na mwanamke inao umuhimu mkubwa mbele za Mungu – ni umuhimu na ulazima ambao ni wa ndani sana kuliko tunavyotambua! Na kwa sababu ya umuhimu wake mbele zake Mungu, na kwa sababu kwa jinsi gani ushirika unavyowagusa mwanamume na mwanamke, Mungu ameteua aina hii ya ushirika wa kimwili utende kazi zake ndani ya ndoa tu – kati ya mwamamume na mwanamke.

Sasa sisi hatuishi chini ya Agano la Kale, hata hivyo umuhimu na uzito wa ukweli unabaki ni ule ule kwa ajili yetu kama vile tulivyokwisha kuona tayari kutoka katika maneno ya Yesu. Mtume Paulo naye vilevile anauweka ukweli huu kuwa wa wazi kabisa kwa ajili yetu kwenye 1 Wakorintho 6:15,16, pale anaposema kuwa, “Je, hamjui yakuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha, (Mungu apishe mbali). Au hamjui yakwamba yeye aliyeunganishwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, wale wawili watakuwa mwili mmoja.” Hili ni jambo linaloshangaza. Ni maelezo ameyatoa Paulo!  Anazungumzia dhambi ya zinaa au uasherati. Na hapo mtume Paulo anawakumbusha Wakristo kwamba miili yao ni viungo vya Yesu Kristo, kwamba vinamhusu yeye, na anasema kuwa ukilala na mwanamke ambaye siye mkeo hata kama mwanamke huyo ni kahaba, unajifanya mwenyewe kuwa ni mwili mmoja na kahaba huyo! Je, unaona hapo jinsi mambo hayo yalivyo ni yenye maana sana mbele zake Bwana? Paulo naye anaonyesha jinsi ilivyo ni dhambi ya hatari na ya kipekee pale anaposema, “ikimbieni zinaa, kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake, ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.” (1 Wakorintho 6:18).

Kwa ujumla, kulingana na neno la Mungu jambo pekee ambalo linafuta au kuondoa mahusiano ya kindoa ni kifo cha mwenzake wa ndoa ile. (Warumi 7:2,3;1 Wakor.7:39). Pamoja na kwamba imesemwa hivyo, bado Yesu amekazia kwamba ikiwa mmoja wa wanandoa hao ataanguka katika uzinzi, hiyo ndiyo itakuwa ni sababu nyingine ya kuvunjika kwa ndoa, yaani kuachana wanandoa hao. (Mathayo 19:9). Haya yote yanatusaidia kuelewa kuwa ule ushirika uliopo kati mwanamume na mwanamke ni mtakatifu, wenye thamani na wenye maana kuu mbele zake Mungu. Na ushirika huu, kwa mujibu wake Mungu, ni kati ya mwanamume mmoja na mwanamke mmoja kadiri wote wawili wanavyoweza kuishi – kuwa hai! Hii yote ni ya lazima zaidi kwa vile inawakilisha ukweli wa kiroho na wa milele!

Ile sura ya mahusiano ya wanandoa kati ya mume na mke inabeba muhimu mkubwa kuliko hata ubinadamu! Kile ambacho Mungu alikifanya pale bustanini Edeni kinatupatia kielelezo cha mwanzo cha kusudio la Mungu la umilele katika kumtayarishia bibi harusi kwa ajili ya Mwanae! Mungu akampatia Adam usingiziv mzito, kisha akachukua ubavu wake, na kutokana na ubavu huo akamwuumba bibi harusi wa Adam; mke wake Adam – Hawa! Askari walipokuja kumtoa Yesu pale msalabani, wakagundua kuwa tayari alikuwa amekwisha kufa, na wakamchoma ubavuni mwake kwa mkuki. Na damu na maji vikatiririka kutoka ubavuni hapo. Je, unauona usambamba wa kile kilichotokea katika bustani ya Edeni na kile kilichotokea pale Kalvari? Pale Kalvari, Vitu Vile ambavyo vingeweza kukomboa, kusafisha na kumtakasa bibi harusi wa Yesu ilitiririka kutoka ubavuni mwake Mwokozi! Tumekombolewa kwa damu ya Yesu Kristo, na sisi si mali yetu wenyewe bali ni mali yake yeye! Zaidi ya hayo yote, mtume Paulo anasema katika kitabu cha Waefeso 5:25-27,

“Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda kanisa, akajitoa kwa ajili yake, ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno apate kuliletea kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lolote kama hayo, bali liwe takatifu lisilo na mawaa. Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe.” 

Mungu alipomtoa Hawa kutoka katika ubavu wa Adam, inasemwa kuwa akamleta kwa Adam, alimkabidhi kwa Adam. Na ubavuni mwake Yesu yalitiririka maji na damu ili kwamba apate kuliwakilishia kanisa lenye utukufu na safi! Katika Waefeso sura ya 5, mtume Paulo anakamilisha ulinganisho wake anaposema kuwa, “kwa kuwa tu viungo vya mwili wake, mifupa yake na nyama yake, kwa sababu hii mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, na hawa wawili watakuwa ni mwili mmoja. Siri hiyo ni kubwa ila Mimi nanena habari ya Christo na Kanisa.” (Mistari wa 30-32). Je, sio jambo la kushangaza hilo? Mtume Paulo ananukuu kutoka katika kitabu cha Mwanzo, eneo ambalo linaongelea kuhusu uhusiano uliopo kati ya Adam na Hawa, na kisha anaitumia hiyo kama kielelezo kamili cha Kristo Yesu na kanisa!

Mahusiano yaliyopo kati ya mume na mkewe yanawakilisha mahusiano yaliyopo kati ya Kristo na kanisa lake, na hii ndiyo sababu inayompelekea Paulo kusema kuwa, “maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu, kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi. (2 Wakor.11:2).

Hii inatupatia mambo ya muhimu na ya kimsingi ya kibiblia kuhusiana na jambo hili lenye ukweli wa lazima sana, ambalo natumaini itatusaidia sana. Hebu basi tuangalie tena kile ambacho Yesu mwenyewe alikisema alipoulizwa iwapo mwanamume angepaswa kumfukuza au kumpatia talaka mkewe kwa sababu yoyote ile. Yesu ananukuu mstari unaopatikana katika kitabu cha Mwanzo ambao tayari tumeshauangalia hapo juu, na kisha anaumalizia mstari huo kwa kusema,

“…hata wamekuwa si wawili tena bali mwili mmoja, basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.”

KIMALIZIO

Watu wengine wanapenda kunukuu Mwanzo28:1-9, kana kwamba mistari hiyo sasa inawakilisha msingi wa fundisho kwamba mchungaji anaweza kukuelekeza au hata kukuambia umwoe binti yupi, au usimwoe binti fulani! Jambo la kwanza kuligunfua hapo no Isaka alimwambia Yakobo asioe binti yoyote kutoka katika makabila ya Wakaanani. Isaka hakumchagulia Yakobo mchumba, alichofanya ni kumwambia tu kwamba akachague mchumba wake kutoka miongoni mwa familia yake. Na ukweli wake hapo ni kwamba uwakilishi wa jambo hili tayari umeonyeshwa katika Agano Jipya pia. Inatajwa kuwa Mkristo anapwaswa kumwoa Mkristo mwenzake tu (1 Wakor.7:39; 2 Wakor.6:14). Jambo la pili kugundua hapo ni kwamba Isaka alikuwa ni baba wa Yakobo wala Isaka hakuwa ni mchungaji wa Yakobo. Lakini pia kama nilivyokwisha kusema kuwa ule ushauri ambao Isaka anampatia mwanae tayari umejumuishwa kwenye neno la Mungu katika Agano Jipya ambao unatueleza kuwa tusifungiwe nira pamoja na wasioamini.

Kama nilivyokwisha sema, mafundisho au desturi zinazoelekeza kwamba eti, yakupasa kwanza upate kibali kutoka kwa mchungaji ili kwanza uweze kumsogelea mwanamke fulani ambaye ungependa umwoe, mwenendo kama huo hauonekani popote pale kwenye Biblia – wala katika Agano la Kale au kwenye Agano Jipya.

Kuilazimisha desturi kama hiyo itawale makanisani inasababisha kufungua mlango kwa mambo mengi ya hatari na uovu mwingi. Kwa vyovyote kijana anaweza akakosea pia, lakini desturi hii ya uovu haifai na wala sio suluhisho linaloweza kuwasaidia na kuwaongoza watu kwenda katika njia ya haki. Kwenye makala hii, nimeelezea pia njia nzuri ambazo kijana anaweza kusaidiwa na kuelekezwa juu ya mambo kama haya.

Hata hivyo, hebu nitaje mifano miwili tuliyonayo kwenye Biblia, mahala ambapo mwanamke mmoja maalum alichaguliwa awe bibi harusi wa mwanaume mmoja. Ya kwanza ilitokea kwenye bustani ya Edeni, ambapo Mungu alichukua ubavu wa Adam na kutokana na ubavu huo akamwuumba Hawa. Mungu akamletea Adam mwanamke huyo. Katika mfano huu tunaona kuwa ni Mungu ndiye anayechagua mwanamke ambaye atakuwa ni mwanamke wa Adam!

Mfano wa pili ni ule wa Ibrahimu na Isaka. Ibrahimu alimpenda na kumtunza mwanae. Hakupenda mwanae apate mwanamke kutoka miongoni mwa mataifa. Kwa hiyo Ibrahimu ( ambaye ndiye mfano wa Baba) akamtuma mtumishi wake mkubwa (mfano wa Roho) kwenda kumtafutia mchumba kwa ajili ya Isaka (ambaye ni Mwana), akamtafute mchumba kutoka katika nchi yake yeye mwenyewe na katika ukoo wake.( soma Mwanzo 24). Na ikiwa utasoma hadithi hii nzuri ajabu, utaona jinsi Mungu alivyofanya kazi kupitia mazingira katika kumwongoza mtumishi wa Ibrahimu mwanamke sahihi! Na mara tu Rebeka alipoletwa mbele ya Isaka, akampenda.

Sasa katika mifano hiyo yote, Mungu alikuwa kazini akifanya kazi kwa jinsi ya ajabu ndani ya maisha ya watu hawa wawili ili kuwaletea wake zao wenye kufaa kwa ajili yao!

Hivyo basi, ningependa kukutia moyo ili ujikabidhi kwa Mungu, na kuweka matumaini yako kwake kikamilifu, na kumruhusu au kumwachia Yeye afanye kazi katika maisha yako; na kwa uvumilivu kuendelea kusubiria toka Kwake ili akuongoze kupata mwanamke atakayekufaa! Na ukumbuke kuwa katika mahusiano yote, itakupasa ukue katika neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na katika upendo Wa Mungu ili kwamba tuzijue baraka za Mungu ndani ya ndoa yetu.

Ni matumaini yangu makubwa kuona kuwa yale yote niliyoyaandika yatawasaidia baadhi ya wana wa Mungu wapate kuingia katika mahusiano ya kina na wafikie katika kuyaelewa vema makusudi na mapenzi yake kwa ajili ya maisha yao na njinsi wawezavyo kuyatimiliza.

©  David Stamen 2017

Unaweza kupakua/download somo hili kwa kubofya link ifuatayo (bofya kulia, chagua ‘save link as’): JE, NI SAHIHI UPATE KIBALI CHA MCHUNGAJI WAKO KWANZA KABLA YA KUMTAFUTA MCHUMBA WAKO UMPENDAYE

 

 

2 responses to “KWA MUJIBU WA BIBILIA, JE, NI SAHIHI UPATE KIBALI CHA MCHUNGAJI WAKO KWANZA KABLA YA KUMTAFUTA MCHUMBA WAKO UMPENDAYE?

 1. Jacob kiio

  February 5, 2018 at 9:54 am

  Inaambata na imani yangu ndani ya kristo. Muñgu akumbariki sana Mtumishi.Je ni lazima ndoa iunganishe kanisani na mchungaji.

   
 2. Robert J. Zingu

  August 16, 2019 at 2:05 pm

  Looh, asante mtumishi wa Mungu. Hakika umenisaidia sana kupanua ufahamu wangu na nimepata majibu ya mengi ya maswali niliyokuwa nayo ndani ya nafsi.

  Na kwa hakika mengi ya makanisa ama dini za siku hizi, wachungaji wanawatawala washirika kwa kuwatia hofu na kuwaogepesha wasiweze kutambua ajenda ya ya uovu wa shetani iliyo nyuma ya maongozi yao.

  Namshukuru sana Yesu Kristo kwa kuniongoza kuisoma makala hii iliyosheheni kweli ya Neno lake Mungu mwenyewe.

  Sina shaka hakika, hapa Mungu mwenyewe alikuwa akinifundisha kupitia kinywa chako ndugu David Stamen

  Bwana Akubariki sana, akulinde na kuindeleza huduma yako kuwafikia watu wengi zaidi.

   

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

 
%d bloggers like this: