Ufahamu wako wa neno la Mungu hautegemei akili yako ya kibinadamu, au elimu yako.
Kimsingi, ufahamu wako wa neno la Mungu – Biblia – hautegemei akili yako ya kibinadamu, au elimu yako.
Tunalijuaje jambo hili? Tunalijua kwa sababu Biblia ndivyo inavyotuambia hivyo! Kwa mujibu wa Biblia, kuna masharti ya msingi mawili ili kuielewa neno la Mungu, yaani, hali na mwelekeo wa mioyo yetu; na jambo la pili, kuwa na huduma ya Roho Mtakatifu katika maisha yetu.
Jambo la muhimu sana katika kulielewa neno la Mungu na kupata ufahamu wa ndani ni ile hali ya kiroho na ya mioyo yetu. Wenye kiburi wanaweza kukusanya maarifa mengi ya Biblia, lakini hawatafikia kumjua Mungu wala kulielewa neno lake. Kwa uhakika uelewa wetu wa neno la Mungu unategemea mahusiano yetu ya kiroho naye Mungu.
Hebu waangalie mafarisayo! Walikuwa ni watu walio na elimu sana na walikuwa ni watu wenye kuyaelewa vizuri sana maandiko – walikuwa ni watu wenye kuyaelewa zaidi karibu kuliko mtu mwingine yeyote yule! Walikuwa wanaelewa kila hoja ya sheria za Musa na walijua kuwa Kristo atazaliwa Bethelehemu, na kadhalika. Lakini bado watu hawa HAWAKUMJUA Mungu! Walimpinga Mungu! Kiburi na ugumu wa mioyo yao iliwatia upofu wasiijue kweli na neno la Mungu – hawakulijua maana ya dhati ya neno Lake. Watu hawa WALIJAZWA NA UJUZI wa maandiko, lakini Yesu aliwaita “nyoka, wana wa majoka” (Mathayo 23:33).
Mungu huwapa wanyenyekevu ufahamu wa neno lake, na wale wanaomhofu yeye na kujinyenyekeza wenyewe mbele ya neno lake,
“WENYE UPOLE atawafundisha njia yake… Siri ya Bwana iko kwao WAMCHAO, Naye ATAWAJULISHA agano lake.” (Zaburi 25:9,14).
“KUMCHA Bwana ni CHANZO cha maarifa…Maana mtu mkaidi ni chukizo kwa Bwana, Bali SIRI YAKE ni pamoja na WANYOFU…KUMCHA Bwana ni mwanzo wa hekima; Na kumjua Mtakatifu ni ufahamu.” (Mithali1:7; 3:32; 9:10).
Na hiyo ndiyo sababu iliyomfanya Yesu aseme maneno yafuatayo, “Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya ULIWAFICHA wenye HEKIMA NA AKILI, ukawafunulia WATOTO WACHANGA. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ILIVYOPENDEZA mbele zako.” (Mathayo 11:25).
Na haya mambo yote hayategemei elimu yetu tuliyo nayo (ijapokuwa inaweza kukusaidia kujifunza KUSOMA neno la Mungu!) au hata akili ya kibinadamu – inategemea na unyenyekevu, mahusiano ya kumtegemea Mungu. INAMPENDEZA Mungu kuwafunulia kweli yake WANYENYEKEVU wa moyo. Kwa nini Mungu anapaswa atoe uelewa wa kweli kwa wale wenye kiburi na wanao pinga tabia yake? Yesu anasema nini kwenye mistari michache tu baadae pale? Mwana wa Mungu anasema hivyo, “mjifunze KWANGU; kwa kuwa mimi ni MPOLE na MNYENYEKEVU wa moyo.” Hili ni jambo la kushangaza. Tunapaswa kujifunza toka kwake Yesu ambaye anakiri juu ya upole wake na unyenyekevu wa moyo! Na iwapo mwalimu Mkuu na Mwokozi wetu yeye ni mnyenyekevu, basi tunaweza tu kujifunza kutoka kwake iwapo tutajinyenyekeza wenyewe mbele zake na mbele ya neno lake!
Kwenye ule mstari wa 27 Yesu mwenyewe anaifunua kweli hii muhimu, “wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda KUMFUNULIA.” Unaweza kujisomea au kujifunza Biblia mara nyingi kadiri utakavyo, lakini haitakusaidia chochote ndugu iwapo moyo wako sio mnyenyekevu na haupo sawa mbele zake Mungu. Mungu hujifunua mwenyewe kwa wale ambao humhofu yeye na kujinyenyekeza wenyewe kwa neno lake. Kama Mungu anavyosema, “Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu.” (Isaya 57:15).
Hivyo ndiyo sababu mtume Paulo naye anawaandikia Wakorintho akisema, “Twajua ya kuwa sisi sote tuna UJUZI. Ujuzi huleta majivuno, bali upendo hujenga.” (1 Wakor. 8:1).
Tunaweza kuwa na ujuzi mwingi wa neno la Mungu, lakini kuwa nao huo ujuzi haitusaidii lolote ndugu ikiwa matendo yako yanapingana na tabia ya Mungu. Wakorintho ambao Paulo alikuwa anawaandikia walikuwa wameokolewa kupitia huduma yake na walikuwa wamebatizwa kwa Roho Mtakatifu; pamoja na hayo yote mioyo yao ilikuwa haipo sawa mbele za Mungu wakati alipowaandikia. Tabia yao na matendo yao walikuwa ni kinyume na upendo wake na tabia yake! Wakorintho walikuwa wakivutana na kubishana wao kwa wao na wakivurugana wenyewe kwa wenyewe. Ndipo ilimfanya Paulo awaandikie, “Amkeni! Anzeni kuishi vema, na acheni kutenda dhambi. Baadhi yenu HAWAMJUI Mungu. Hii nawaambieni, ni AIBU kubwa kwenu!” (1 Wakor. 15:34 na 6:6). Lakini tafsiri ya Biblia ya Kiswahili (SUV) imekosea pale kwenye mstari huo. Inasema, “Tumieni akili kama ipasavyo, wala msitende dhambi…”. Hakuna sehemu yoyote ile kwenye Biblia inayohimiza au kusema “tumieni akili.” Sawasawa na lugha ya asili ya Agano Jipya, yaani kigiriki, maneno yale (εκνηψατε δικαιως – eknepsate dikaios), yanamaanisha ‘Amkeni katika haki’ na siyo ‘Tumieni akili’.
Unaona sasa, Paulo anawaambia Wakorintho kuwa ijapokuwa wanao “ujuzi au maarifa” (1Wakor.1:5), lakini baadhi yao hawamjui Mungu kama ipasavyo, na mienendo yao haipo sawa! Maarifa au ujuzi wetu unakuwa sio mzuri ikiwa haubadilishi namna ya mienendo yetu na tabia zetu! Ikiwa tabia yetu haipothabiti, yaani, haizingatii neno lake Mungu pamoja na tabia yake, basi maarifa yetu yote ni bure na hayana maana yoyote ile. Neno la Mungu halipo pale ili kutuinua sisi na kutufanya tuwe na kiburi juu ya kile tunachokijua, wala halipo pale ili kukijaza kichwa chetu na mataarifa mengi; isipokuwa liko pale ili kuuongoza moyo wako uelekee kwa Mungu, kuifunua tabia ya Mungu na ili kukubadilisha wewe upate kuwa na tabia yake Mungu (2 Wakor. 3:18; 2 Petro 1:4,5).
Tatizo hili limeonyeshwa kwa uwazi sana kwenye mabishano yanayofanyika kwenye makundi ya kikristo kwenye kurasa za Facebook na za jamii za mitandao zingine. Watu wengine wanafikiri “wanaijua” kweli ya Mungu “vizuri Zaidi” ya wengine (ni vilevile ilivyokuwa kati ya Wakristo wa huko Korintho). Na kwa sababu hiyo sasa watu hao wanaojidhania wanao ujuzi wanawadhihaki, kuwakejeli, kuwadharau, kuwasingiza wengine na kutumia lugha ya matusi! Wao hufikiri kuwa kwa kufanya hivyo wanatangaza na ‘kuitetea’ kweli ya Mungu, lakini wanaandika kana kwamba hawamjui Yeye hata kidogo! Njia wanayoitumia kuandika INAPINGANA na ni tofauti kabisa na Roho ya Kristo mwenyewe. Wanaharibu ushuhuda wa Kristo katika maisha yao, na kujitia aibu wao wenyewe kutokana na mwenendo wao. Mijadala kwenye Facebook iwe ni jambo linalolenga kufundisha na kulishana sisi kwa sisi. Ndiyo, Paulo anatuagiza tushindanie Imani (Yuda 3), lakini isijichafue yenyewe kwa kujiingiza katika mifumo ya vita vya kiakili ambapo tunajitafutia kuwashinda wengine na kuwadhihaki!
Maarifa ya ukweli ya Mungu na tabia yake haina majivuno ndani yake! “Lakini HEKIMA ITOKAYO JUU, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki.” (Yakobo 3:17).
Uelewa na maarifa ya Mungu hayategemei elimu au akili zako, bali hutegemea sana hali ya moyo wako. Inategemea mahusiano yangu binafsi Kwake Mungu – je, nina njaa na kiu juu ya haki yake Mungu? Je, nipo tayari kujinyenyekeza mbele ya neno lake na kuyatafuta mapenzi yake pekee na kumpenda yeye kwa moyo wangu wote! Haya ndiyo masharti makuu ambayo maarifa ya ukweli wa Mungu hutegemea! Haitegemei kama wewe umemaliza form 6 au sivyo, au kama umefika hadi chuo kikuu, au hata chuo cha Biblia! Hizi ni habari njema ya ajabu kwa wapole na wanyenyejevu wa moyo! Mungu apewe sifa kwa neema na hekima yake katika mambo hayo! Hii ni ajabu na ni kweli yenye kutia moyo! Hii inafungua milango kwa ajili ya wote, na hivyo ndivyo Mungu alivyoyateua mambo kwa hekima yake! Hii ndiyo sababu neno la Mungu hutufundisha mambo yafuatayo, “Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa.” (1 Wakor.1:26). Bwana asifiwe kwa ajili ya neema yake kuu na hekima ya haki yake!
Mitume Petro na Yohana walikuwa ni wavuvi wasio hata na elimu iliyo rasmi lakini waliwashangaza Mafarisayo? Kwa nini? Sikiliza neno la Mungu lisemavyo. “Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu WASIO NA ELIMU, WASIO NA MAARIFA, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu.” (Matendo 4:13).
Hiyo ni mistari mizuri sana inayofunua kiini cha kweli inayohusu jambo tunalolishughulikia katika somo hili.
Jambo lililo kubwa na muhimu ni yale mahusiano yako na Yesu – na wala sio akili zako au elimu yako. Unaona! Mafarisayo “walitambua” kuwa mitume wamekuwa PAMOJA NA Yesu. Je, hivyo ndiyo ilivyo kwetu? Watu wanapotutazama wanatuona kwamba hakika mtu huyu amekuwa pamoja na Yesu, ya kwamba tumekuwa pamoja na Yesu, kwamba tunamfuata Yeye, na kwamba tabia yetu inatokana na upendo wetu kwa ajili yake pamoja na utii kwake? Je, nyakati zetu ya faragha pamoja na Yesu Kristo inagusa maisha yetu ya kila siku ili kwamba watu wapate kutambua kuwa kuna kitu cha tofauti kuhusu sisi? Mafarisayo hawakuelewa kuwa watu pasipo kuwa na elimu wangeweza kusema kwa ujasiri namna ile na kuwa tofauti kabisa. Walitambua kuwa jambo la aina hii linaweza tu kuelezwa vema na MAHUSIANO YA WANAFUNZI WALE NA YESU. “Waliwatambua kuwa watu hawa wamekuwa pamoja na Yesu”.
Sasa, hapa siidharau elimu. Hapana. Lakini wacha niseme tena kwamba, kumjua Mungu na kulielewa neno lake haitegemei elimu yako uliyonayo! Paulo alikuwa ni mtu msomi, lakini hebu umsikilize hapa anavyosema ushuhuda wake: “Kwa maana, ndugu zangu,Injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo.” (Wagal. 1:11,12). Kuhusiana na mambo yote ya mafunzo yake ya kidini na elimu, yeye anasema kama ifuatavyo, “Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu.” (Wafilipi 3:7,8).
Jambo kuu na lenye thamani kwa mtume Paulo ilikuwa ni KUMJUA Kristo, na wala hiyo haishangazi! Uzima wa milele ni mini? Hapa sasa Yesu mwenyewe anatujulisha kwa uwazi kabisa, “Na uzima wa milele ndio huu, WAKUJUE wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.” (Yohana 17:3). Lakini hebu tuweke wazi juu ya jambo hili tena – ikiwa tunamjua Mungu kiukweli, ndipo hiyo itajionyesha yenyewe katika MWENENDO wetu na TABIA zetu, katika UTII wetu kwa neno lake (1 Yoh 2:3,4). Tunakuwa hatuna maarifa ya kweli wala uelewa wa neno la Mungu ikiwa hatulitii neno lake Mungu. Sikiliza maneno asemayo Yesu hapa, , “Mafunzo yangu si yangu mimi, ila ni yake yeye aliyenipeleka. Mtu akipenda KUYATENDA mapenzi yake, ATAJUA habari ya yale mafunzo, kwamba yatoka kwa Mungu.” (Yohana 7:17).
Kuelewa kwa kweli ya neno la Mungu huja kutokana na kutembea kwetu kwa ukaribu na Mungu katika maisha yetu ya kila siku na kulishika neno lake.
Sasa tunaingia kwenye jambo jingine la umuhimu na lenye ulazima katika kutupatia ufahamu wa kweli ya neno la Mungu.
Tayari tumekwisha kuona kwamba Mafarisayo ambao walikuwa ma maarifa makubwa ya Agano la Kale hawakuwa na uelewa HALISI wa ujumbe wake uliobebwa ndani neno. Wao sasa walitumia maandiko kupinga na hatimaye kumwua Kristo! Neno la Mungu liko wazi kabisa kwamba pasipo msaada na huduma za Roho Mtakatifu hatutakuwa na uelewa wa kweli ya neno la Mungu:
“mambo ya Mungu HAKUNA ayafahamuye ILA Roho wa Mungu. Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate KUYAJUA tuliyokirimiwa na Mungu. Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho… Basi mwanadamu wa tabia ya asili HAYAPOKEI mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala HAWEZI kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.” (1 Wakor. 2:11-14).
Hapa tunaona wazi kuwa pasipo msaada wa Roho Mtakatifu wa Mungu basi tutaachwa mbali, tutatupwa mbali kabisa na uelewa wa neno la Mungu na makusudio yake. Katika tafsiri ya Kiswahili inasema kuwa, ‘mwanadamu wa tabia ya asili’. Lakini kwenye tafsiri ya lugha ya asili inasema ‘mwanadamu wa nafsi’. Hapa inaelezea juu ya ufahamu wetu wa kawaida (asilia). Kila kitu tulivyo ni kutokana na uzao wa kiasili, uzao wa kwanza. Tutaelewa nini basi iwapo tutaachwa pasipo mabadiliko yoyote katika maisha yetu na pasipo msaada wa Roho Mtakatifu? Inasemwa kwamba iwapo tutabaki na akili zetu tu tulizozaliwa nazo, basi ndipo hatuwezi kuyaelewa mambo ya Mungu, wala kupokea mambo ya Roho Mtakatifu wa Mungu. Hii ni yenye nguvu na jambo la maana sana! Ni wazi pia kuwa Mafarisayo pamoja na kujifunza kwao na uelewa wao hawakujua wala kupokea mambo ya Roho wa Mungu!
Kumbuka kuwa Paulo alikuwa akiwaandikia mambo haya Wakristo (kwenye zile nyaraka za Wakorintho) ambao walikuwa wamebatizwa kwa Roho Mtakatifu, lakini mbali na ubatizo huo wa Roho Mtakatifu hata hivyo walikuwa wakiishi katika mifumo ya ujinga wa kutokumjua Mungu wakati alipowaandikia mambo hayo (kama nilivyokwisha kuonyesha hapo juu). Ndipo sasa ilimpasa Paulo kuwatengeneza vizuri watu hawa kwa kuwawekea uelewa wa misingi iliyo bora ya kweli ya Mungu na ilimpasa kusisitiza kweli hiyo kwa kusema yafuatayo, “Basi, ndugu zangu, mimi nilipokuja kwenu, sikuja niwahubiri siri ya Mungu kwa UFASAHA WA MANENO, WALA KWA HEKIMA. Maana naliazimu NISIJUE NENO LO LOTE kwenu ILA Yesu Kristo, naye amesulibiwa.” (1 Wakor.2:1,2).
Akili za kibinadamu na elimu pekee hazitoshi kabisa! Ikiwa tutakuwa tukitumia busara zetu za kibinadamu tu ambayo ni busara tu za ki-dunia hii (namna ambavyo dunia nayo inavyofikiri) basi tutauvuruga ujumbe ule – ujumbe uleule tunaotaka kuutangaza sasa tunaufanya usiwe na nguvu na badala yake sasa unakuwa hauna matokeo yoyote! Paulo analionyesha jambo hili kwa uwazi kabisa: “Maana Kristo hakunituma ili nibatize, bali niihubiri Habari Njema; wala SI kwa hekima ya maneno, msalaba wa Kristo USIJE UKABATILIKA.” (1 Wakor.1:17).
Mungu mwenyewe, kwa Roho wake Mtakatifu ndiye anayepaswa kuwa ni chanzo au asili ya uelewa wetu. Na kama yeye ndiye atakuwa ni chanzo, hapo ndipo tutakuwa tunamtegemea yeye kwa kila kitu na kwa uelewa wa kweli. Mungu hatairidhia au kuikubali njia nyingine yoyote ile kwa sababu anasema, “Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, Na akili zao wenye akili nitazikataa. Yu wapi mwenye hekima? Yu wapi mwandishi? Yu wapi mlete hoja wa zamani hizi? Je! Mungu hakuifanya hekima ya dunia kuwa ni upumbavu?” (1 Wakor.1:19,20).
Hapo anazungumza juu ya akili na hekima ya kibinadamu, ya dunia hii. Na tutambue kuwa hata wanafunzi wake Yesu walipungukiwa na ufahamu wa maandiko. Ilimlazimu Yesu mwenyewe KUWAFUNUA AKILI ZAO: “Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko.” (Luka 24:45). Pasipo kazi ya Roho ya Mungu katika maisha yetu na katika akili yetu hatuwezi kuelewa maandiko kwa dhati, kwa hiyo Paulo anatuagiza, “na MFANYWE WAPYA katika roho ya AKILI zenu.” (Waefeso 4:23. Soma pia Warumi 12:2).
Katika kitabu cha Matendo ile sura ya kwanza tunaelewa kuwa wanafunzi wa Yesu hawakuelewa ni ufalme upi na ni wa aina gani ambao Yesu anakwenda kuuanzisha baada ya ufufuo wake. Wao walifikiri kuwa ufalme huo utakuwa ni ufalme wenye mamlaka YA KIDUNIA ambao Yesu angeuanzisha wakati uleule! Lakini siku ile ya Pentekoste walipokuwa wamebatizwa kwa Roho Mtakatifu, Petro hakupata taabu tena ya kuelewa wakati anawahutubia kongamano la watu kuhusu kwa niini Yesu alikufa!
Ni Roho Mtakatifu ndiye atupaye nuru katika ufahamu wetu na kuwasha nuru katika neno la Mungu ili kwamba tupate kuelewa neno hill linamaanisha nini. Na hii ndiyo sababa Paulo anaomba maombi yafuatayo kwa ajili ya waumini wa Efeso, “Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, AWAPE ninyi ROHO ya hekima na ya UFUNUO KATIKA KUMJUA yeye; MACHO YA MIOYO YENU YATIWE NURU, MJUE…utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo,” (Waefeso 1:17,18). Kwa hiyo sio tu kwamba mtu anahitaji kubatizwa katika Roho Mtakatifu, bali muumini huyo ni budi amtegemee Roho wa Mungu ili kumpatia uelewa wa maana ya andiko na Injili. Yohana naye anakazia kweli hii na kuifanya ueleweke vizuri pale anaposema, “Nanyi, MAFUTA yale mliyoyapata kwake yanakaa ndani yenu, wala HAMNA HAJA ya mtu kuwafundisha; lakini KAMA MAFUTA yake YANAVYOWAFUNDISHA habari za mambo yote, tena ni kweli wala si uongo, na kama yalivyowafundisha, kaeni ndani yake.” (1 Yohana 2:27).
Hili ni andiko la kushangaza hata hivyo ni ukweli mtupu. (“Upako” ndio Roho Mtakatifu tunayempokea tunapobatizwa kwa Roho). Kile anachokisema Yohana hapa ni kwamba iwapo tunaye Roho Mtakatifu katika maisha yetu, ndipo yeye anaouweza wa kutufundisha na kutusababisha kuelewa kweli muhimu ya wokovu wetu kwa uhakikisho mkuu. Ikiwa utaangalia muktadha anasema kwamba Roho wa Mungu anaouweza wa kututunza katika kweli na katika kuyatambua mafundisho ya uongo – ili mradi tu tushikamane naye. Yohana hapa anaongelea kuhusu mambo ya muhimu yahusuyo wokovu wetu. Lakini hii haimaanishi kuwa yasiwepo mafundisho kanisani! Ni wazi kuwa huwa tunakutana pamoja kama waumini kutiana moyo, kujengana na kufundishana sisi kwa sisi katika mambo ya Mungu. Na kwa hakika Mungu amelipatia kanisa watu wale wenye huduma ya kufundisha (Waefeso 4:11). Hivyo tunaweza kukielewa vizuri kile tunachokijua tayari au kuingia kwa undani zaidi.
Kuhusu huduma ya Roho Mtakatifu katika maisha yetu, Yesu Kristo anaithibitisha kweli hili kwa uwazi kabisa kwetu pale abaposema kuwa, “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, ATAWAFUNDISHA YOTE, na kuwakumbusha yote niliyowaambia… Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza AWATIE KWENYE KWELI YOTE.” (John 14:26, 16:13).
Ni Roho Mtakatifu wa Mungu ndiye atakayetufundisha na kutuongoza katika kweli yote! Yeye ndiye ayafanyaye maandiko yalete uzima ndani yetu. Ni Roho ndiye ambaye sio tu kwamba hutupatia uelewa tu wa kile tunachokisoma, bali yeye atatia kweli hiyo ndani ya mioyo yetu kwa namna ambayo inahusu maisha yetu ya kila siku.
(Ebu niweke WAZI zaidi hapa kuwa Roho wa Mungu atatupatia uelewa wa kweli na wa ndani zaidi ya kile kilichoandikwa katika maandiko matakatifu, ambayo yalivuviwa na Roho Mtakatifu wa Mungu mwenyewe! Roho Mtakatifu hatakupatia wewe ufunuo mpya ambao ni WA NYONGEZA kwenye Biblia au tofauti na kile ambacho tayari Biblia inafundisha – wala sio kwa ufunuo wowote ule au ndoto na hata maono. Hizi ndizo kasoro na udanganyifu mkubwa ambao wengi wametumbukia humo siku za leo. Yote tunayoyafundisha ni lazima yawe na msingi dhahiri na wazi kwenye maandiko, na ikubaliane na neno la Mungu. Roho wa Mungu aweza kumpatia mtumishi wa Mungu karama ya ufunuo wa kweli yake ili kwamba apate kutoa maelezo ya kina na ya wazi habisa yahusuyo mambo yaliyoandikwa katika Biblia, hata hivyo hiyo HAITAWAKILISHA FUNDISHO JIPYA.)
Tunapaswa kujazwa na Roho Mtakatifu, kutembea katika Roho na kuishi katika Roho. Tukisemezana sisi kwa sisi kwa Zaburi, tenzi na nyimbo za rohoni huku mukiimba na kumshangilua Bwana mioyo mwenu.( Waefeso 5:19).
Kimsingi Biblia sio kitabu cha shuleni, wala sio kitabu cha mambo ya kitaaluma. Ni zaidi ya kitabu chenye mikusanyiko tu ya taarifa mbalimbali ambayo ni lazima kujifunza, na wala hatusomi Biblia ili kujikusanyia ujuzi fulanifulani kichwani mwetu. Bali neno la Mungu ni chakula kwa ajili yetu. Neno la Mungu ni Roho na Uzima. Ni neno la Mungu lililo hai kwa ajili yetu. Biblia ni neno kamili la Mungu mwenyewe, limevuviwa kwa Roho Mtakatifu (2 Tim. 3:16). Basi hivyo ni kwa njia ya Roho wa Mungu pekee tunaweza kwa hakika kulielewa na kulitafsiri. Yeye aliyeivuvia Biblia ndiye yeye tunayemhitaji kututafsiria Biblia kwa ajili yetu!
Yesu Kristo alisema, “Maneno niwaambiayo ni Roho na uzima” (Yoh.6:63).
Inawezekanaje mwanadamu mwenye asili ya kimwili apokee au aelewe maneno ambayo yenyewe ni Roho na Uzima? Neno la Mungu huenda mbele zaidi ya ule ufahamu wetu na akili zetu za kimwili. Katika Yohana ile sura ya 6, wanafunzi wake Yesu wengi wao hawakumwelewa Yesu na kile alichokuwa akiongelea alipokuwa amewaambia kuwa inawapasa kuinywa damu yake na kuula mwili wake. Wanafunzi wake wakasema hii ni ngumu sana kuielewa na kuipokea! Matakwa ya akili zao za kawaida / za asili iliweka kipaumbeke dhidi ya kunyenyekea na kujikabidhi wao wenyewe mbele za mwana wa Mungu na kusubiri kwa muda wake ili kuwapatia uelewa. Matakwa ya maelezo yao yaliwaongoza kuacha kumfuata Yesu Kristo!
Kwa vyovyote huu ni mfano uliokithiri ijapokuwa bado unaweza kuwa ni mfano wenyewe kutufundisha kitu. Katika mstari huo huo tunamwangalia Yesu ambaye anasema haya yafuatayo,
“Roho ndiye atoaye uzima, mwili HAUSAIDII CHOCHOTE.”
Hebu achilia jambo hili lizame ndani ya mioyo yetu! Mwili hausaidii chochote. Hii ina maana gani? Hii inamaanisha kuwa uelewa wetu wa kawaida – pasipo msaada wa Roho wa Mungu – kwa hakika usomapo neno la Mungu haitakusaidia! Akili zetu za kawaida, za kibinadamu na werevu haitatosha! Neno la Mungu NI ZAIDI YA UJUZI AU MAARIFA ambayo tunayapata kutokana na kujisomea vitabu, ndugu! Neno la Mungu linafanyika uzima kwetu kupitia kazi ya Roho Mtakatifu pekee. Neno la Mungu hufanyika kuwa ni chakula chetu, linakuwa lenye kuhusika na maisha yetu ya kila siku na lilikusudiwa kutubadilisha!
Ni upendo wetu pamoja na utoaji wetu kwake Yesu Kristo ndicho kinachotuongoza kusoma neno lake na kujinyenyekeza wenyewe mbele zake na mbele ya neno lake. Ni shauku yetu kumpendeza na kumtii yeye. Hiyo ndiyo itakayotuhamasisha kuisoma Biblia. Kama mfalme Daudi alivyosema, “Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu, Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha…Ndiyo maana nimeyapenda maagizo yako, Kuliko dhahabu, naam, dhahabu iliyo safi… sheria ya Bwana ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.” (Zaburi 119:72, 127; 1:1,2). Ushauri Wa Paulo kwa Timotheo ulikuwa ni upi? Tunasoma namna hii,
“UYATAFAKARI hayo; UKAE katika hayo; ili kuendelea kwako kuwe DHAHIRI kwa watu wote. Jitunze nafsi yako, na mafundisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia. (1 Tim. 4:15-16)
Unaweza kujionea mwenyewe hapa kutoka kwenye kile ninachonukuu kuwa sikusudii kumtia moyo yeyote yule ili eti awe mvivu katika mambo hayo! Tunapaswa kuwa na mwendelezo wa kutafakari neno la Mungu na kujikabidhi wenyewe kwenye mambo yale tuyasomayo kwa namna kwamba inabadilisha maisha yetu na kutufanya tuwe wapya na pia kugusa maisha ya wengine pia.
Nilipokuwa nikihubiri huko kwenye milima ya Udzungwa, huko kulikuwa kuna baridi kali sana nyakati za jioni. Hivyo wenyeji wa huko walikoka moto mkubwa na watu wote waliuzunguka moto ule wakiwa wamekaa ili kujipatia joto. Ni wakati huo ndipo niliposikia na kujifunza usemi huu usemao “kuota moto”. Hii inamaanisha kuwa unasimama au kukaa KARIBU SANA na moto ili kwamba mwili wako UCHUKUE NA KUFYONZA lile joto la moto ule. Sasa hivyo ndivyo itupasavyo kuwa kufanya na sisi pia – kati yetu na neno la Mungu!
Ota neno la Mungu!
Ota moto (uzima) utokanao na neno la Mungu! Tembea karibu sana na Mungu.Tumia muda wako pamoja naye na katika kusoma neno lake ili kwamba neno lake lifanyike kuwa halisia ndani yako na katika maisha yako! Usiwe mvivu katika kufikiri kwako wala usiwe mvivu katika mambo unayotafanya. Neno la Mungu linatuhimiza kwa maneno yafuatayo, “Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu…kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana;” (Wakolosai 3:23; Warumi 12:11).
Katika kila jambo nililolisema hapo juu, huo ni ukweli wa kimsingi tuliouona kutoka katika Biblia. Ufahamu wa kweli wa neno la Mungu linategemea na haswa linakuja kutoka katika hali ya kiroho / ya moyo wako mbele za Mungu na mahusiano yako kwake; na katika kuwa na Roho wa Mungu na huduma yake ambaye hukuongoza katika kweli yake Kristo na neno lake, sio tu pale mwanzoni mwa maisha yako ya kikristo, bali ni endelevu. Sio sahihi kufikiri kuwa unahitaji kwenda kusoma chuo cha Biblia au kwenda kujipatia shahada, au kupata elimu ya juu ili kwamba uweze kuelewa kwa ukweli na kuhubiri neno la Mungu. La kwanza (kuelewa neno la Mungu) litategemea na mahusiano yako na Mungu, na la pili (kuhubiri neno la Mungu) kwa namna fulani angalau litategemea na wito wa Mungu katika maisha yako. Siyasemi haya ili kutoa fursa kwa yeyote yule ambaye kwa kiburi chake atafikiri kuwa anaweza kulihubiri neno la Mungu. Wapo watu wengi wanaofikiri kuwa wao wameitwa kuhubiri lakini ukiwatazama maisha yao hawatembei karibu na Mungu na wale hawana wito wa kweli wa Mungu. Wala SISEMI hapa kuwa elimu ya jinsi hii ni lazima ni mbaya – bali ninachokisema hapa ni kuwa ni lazima tutambue kuwa hiyo sio msingi wa kweli wa kulielewa neno lake Mungu.
Ndiyo, Mungu ametoa vipawa na huduma katika kanisa. Haijalishi ikiwa tunayo karama au huduma ya kufundisha au la. Haijalishi kama tunayo elimu ya juu au la. Kilichoandikwa hapa kinawahusu waumini wote na ni lazima iwakilishe chanzo cha na msingi wa uelewa wetu wa Mungu pamoja na neno lake kwa namna yoyote ile tuliyonayo. Hapa sisemi kuwa kuendeleza elimu hakutusaidii kwa namna fulani. Lakini yatupasa tujue kuwa hakuna kiasi vyovyote kile cha elimu ya juu ambayo inaweza kufanyika kuwa ndio mbadala wa kubadilisha msingi huu wa kumjua Mungu pamoja na neno lake. Ni lazima pia tutambue hatari iliyopo kuwa elimu inaweza ikawa ndiyo njia ya kufichia upungufu wa ufahamu wa kweli wetu wa neno la Mungu na hata upungufu wa kumjua Mungu mwenyewe. Inaweza ikawa ndio njia au mbinu ya kujaza vichwa vyetu na ‘ujuzi’ tu ambao hauna uzima ndani yake, haina upendo na wala haina nguvu za Mungu. Kwa mfano, shahada ya teolojia inaweza tu kujaza kichwa cha mtu na ‘mataarifa’ ambayo baadaye hayana chakula chochote wala nguvu ndani yake kwa ajili ya watu wa Mungu. Hiyo ni aina ya tatizo ambalo linaweza kutokea. Kama nilivyosema, faida inategemea uhusiano wa mwamini na Mungu.
Ikiwa wewe unapenda kujifunza na kuelewa mambo mbalimbali ya kijiografia yahusuyo Biblia, kwa mfano unataka kujua mji wa Antiokia upo wapi; ikiwa unapenda kujua Kiebrania na Kigiriki, na kama unataka kujua historia ya muktadha wa matukio mbalimbali katika Biblia na kadha wa kadha, basi ndipo utahitajika kujifunza mambo hayo kutoka katika vitabu vinginevyo au hata kwenda kujiunga na aina fulani ya chuo. Hata hivyo, katika mambo hayo yote utakayojishughulisha nayo, hakuna hata mojawapo linalohusiana na mwenendo wako wa kiroho wa imani yako mbele za Mungu na katika ulimwengu huu pia. Mambo hayo hayahusiani kabisa na maisha yako ya imani na utakatifu. Na pia uelewe kuwa hata ufahamu wako wa Mungu na ufahamu wako wa kiroho wa neno lake kamwe haitegemei ujuzi wa kuyajua mambo hayo. Naweza kushuhudia kweli ya mambo hayo katika maisha yangu.
Hakuna popote katika Biblia panaposema “tumia akili” (sawasawa na lugha ya kiasili ya Biblia). Kwa nini basi Biblia haisemi hivyo? Kwa sababu sisi sote tayari tunatumia akili zetu – kutoka muda unapoamka unatumia akili zako mfululizo kufikiri kuhusu mambo na kuyafanyia maamuzi ya aina mbali mbali.Tunatumia akili zetu kufikiri. Hivyo huwezi kuishi pasipo kutumia akili zako, yaani, pasipo kufikiri na ni akili zako ndizo zifanyazo kazi hiyo ya kufikiri. Na hii sasa ndiyo sababu inayoifanya Biblia isiseme “tumia mapafu yako.” Wote tunatumia mapafu ili kupumua, hivyo haihitajiki mtu fulani atuambie ‘tumia mapafu kipumua’! Na kwa ujumla wake huwezi kuishi bila kufikiri, na wala hutaishi pasipo kupumua! Kwa hilo la kwanza unatumia akili zako, na hilo la pili nalo unatumia mapafu!
Watu wengine wanasema eti, tunapaswa ‘kutumia akili zetu’, lakini huwa kwa hakika wanamaanisha nini hasa! Kwa baadhi yao ni jambo tu la kujitetea ili waweze kupenyeza matumizi ya mantiki zao binafsi kwenye matumizi ya maandiko ya neno la Mungu ili kupata majawabu wanayoyataka kuliko hata kupenda kufundishwa na kuongozwa na neno la Mungu. Wengine hupenda kutumia mwelekezo huo kwa sababu wanatafuta kukufundisha wewe mbinu za namna ya kuwa mtu mwenye mafanikio katika maisha hasa katika nambo ya biashara na pesa – wanatumia Biblia kana kwamba ni kitabu cha mwongozo wa biashara. Hili ni kosa kubwa sana.
Kama ulivyo kwenye lugha yetu ya kila siku, mtu mmoja anaweza kumwambia mwingine, “Fikiri tu!” au “Tumie akili yako!” Hiyo ina maana gani? Kimsingi inamaanisha kuwa yule mwingine anakosea kutafakari jambo fulani vizuri na atakutwa na hasara au madhara kwa sababu ya kosa hili. Kwa muktadha huo, Biblia haiongelei juu ya ‘kutumia akili’ au ‘kutokutumia akili’ ila inaongelea juu ya ‘wenye akili / busara’ na ‘wapumbavu’. Soma Mathayo 7:24-27; 25:1-8 na utaona hayo. Hapo tunaona kuna watu ambao wanalo lengo kufanya kitu lakini wanakosea kutafakari vizuri ni nini wanalotakiwa kufanya ili kutimiza lengo lao – Biblia inawaita ‘wampumbavu’. Kwa ujumla kwenye tafsiri ya Kiswahili ya Biblia linapotumika neno ‘akili’ kwa muktadha mwingi sana inamaanisha ‘busara’, ‘hekima’ au ‘ufahamu’ (‘mwenye akili’; ‘fanya akili’, ‘mtu wa akili’ nkd.). Hiyo siyo mada yetu katika somo hili, lakini ikiwa kwa hakika unataka kulielewa neno la Mungu, na kisha ukafikiri kuwa hiyo itategemea na elimu ya juu ili kulielewa neno hilo la Mungu, au ukategemea akili zako za kibinadamu kulielewa neno hilo, basi hapo neno hili ‘mpumbavu’ litakuhusu. Ndiyo, elimu ya juu au chuo cha Biblia zinaweza kutufundisha mambo mbalimbali lakini msingi wa ufahamu wetu wa neno la Mungu unabaki ule ule.
Kwa vyovyote vile, JINSI TUNAVYOZITUMIA akili zetu ni jambo jingine, lakini ukweli ni kwamba wote huwa tunatumia akili zetu nyakati zetu zote. Hili sio somo la ‘jinsi ya kuzitumia akili zetu’ lakini ni juu ya kile kinachotegemea kuielewa kweli ya Mungu kwa dhati na kwa ndani. Hiyo ndiyo moyo wa somo letu na tayari tumekwisha kuona kuwa wala si akili za kibinadamu pekee au elimu itoshayo kutupatia ufahamu wa kweli na kulielewa neno la Mungu. Tumeona wazi kuwa kumbe, kila kitu hutegemea na hali ya kiroho (ya mioyo) yetu na ya mahusiano yetu na Kristo. Kwa mujibu wa neno la Mungu yapo wazi pia kuwa tunamtegemea Roho Mtakatifu kutuongoza kwenye kweli yote.
Kama nilivyoandika, nilichokiandika sikuandika ili mtu awe mvivu. Kinyume chake, lengo la somo hili ni kutuongoza kusoma neno la Mungu zaidi na kumjua Mungu kwa dhati. Kama neno la Mungu linavyosema,
“Bwana asema hivi, Mwenye hekima asijisifu kwa sababu ya hekima yake, wala mwenye nguvu asijisifu kwa sababu ya nguvu zake, wala tajiri asijisifu kwa sababu ya utajiri wake; bali ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi, na kunijua, ya kuwa mimi ni Bwana.” (Yeremia 9:23,24).