RSS

JUU YA KUIMBA NA KUCHEZA (DANCING) MAKANISANI

         “WAMEMWONDOA BWANA WANGU, WALA MIMI SIJUI WALIKOMWEKA”

                             JUU YA KUIMBA NA KUCHEZA (DANCING) MAKANISANI

Neno la Mungu linasema, ‘Mwenye mwili awaye yeyote asijisifu mbele za mungu.’ (1 Wakor.1:31)

Lipo eneo ambalo watu hutukuza mwilini katika nyakati hizi za siku hizi. Ni sehemu ya uimbaji. Utawaona watu wanakuja mbele ya washirika ili kuimba, na wanasema wanafanya hivyo kwa utukufu wa Mungu! Mara nyingi sio kweli. Wanafanya hivyo kwa sababu wanajiridhisha wao wenyewe katika nafsi zao kule kuimba mbele za watu. Ukiwatazama na kusikiliza nyimbo zao utaona kuwa wanaimba vile vile kama dunia waimbavyo, hakuna tofauti – uimbaji wao, unenguaji viuno vyao. Wanatamashisha mbele ya watu kanisani kama vile dunia inavyofanya matamasha yao. Wanataka kujionyesha wenyewe ule uwezo wao wa kuimba, na kunengua viono vyao hadharani na kuwafurahisha watu. Utawaona wengine wanabeba CD zao ili ziimbwe kanisani, na kisha wimbo uleule unaoimba na CD na wao wanaigiliza kwa kuuimba tena wakati CD zao zinapoimba! Baada ya semina moja, mwimbaji mmoja aliniuliza kama napenda kununua CD yake! Jamani, kwa nini hivyo! Tunawezaje kuyaamini mambo kama hayo! Kwa nini tunajifanyia hila wenyewe katika kujifikia kuwa mambo haya yanafanyika ili kumpa Mungu utukufu!

Usinielewe vibaya! Ndiyo, nimewahi kuwasikia watu wakiwa wamesimama mbele ya kanisa na wanaimba kwa sababu wanampenda Mungu, na ni tendo la kuabudu na waumini wanaokuwemo katika ibada hiyo wanabarikiwa. Lakini jambo ambalo ni la kawaida siku hizi za leo (na linazidi sana), wachungaji wakiruhusu vijana kulitumia kanisa ili kujitangaza wao wenyewe pamoja na uimbaji wao. Ni nani sasa anayepaswa kuwajibika katika mambo kama haya? Wachungaji na viongozi wengi wanashindwa kutoa mafunzo ya kweli ya uongozi katika nyakti kama hizi. Kwa nini? Hawataki waonekane kuwa ni watu wasiojulikana na jamii?

Tulikuwa na semina fulani ya siku mbili na wanachuo, semina iliyoandaliwa na Huduma ya Shirika la kikrisho la wanachuo. Kiongozi wao aliniambia, ‘Kama tusingewaruhusu wanachuo kuja mbele kuimba, basi wasingekuja kuhudhuria semina.’ Hayo ni maneno yake yeye mwenyewe! Uimbaji ulikuwa mzuri nami niliufurahia lakini kuna jambo pale ambalo sio sahihi iwapo tutaiachilia bali hiyo kuwa ndiyo tabia yetu.

Mambo ni mabaya zaidi kwa nyakati hizi tulizo nazo, kwa sababu wachungaji wananyenyekea kwa vijana, kuimba na kucheza (dance) na kiasi katika mikutano ya hadhara. Ni mfano mmojawapo mbaya wa kujitukuza katika mwili ambao tunauona nyakati hizi. Waimbaji wanajitokeza mbele ya washirika wakiwa katika kundi kubwa na wanacheza kwa unenguaji mbele ya waumini.  Watu hawa wanautumia muda wao mwingi wakifanyia mazoezi ya aina hiyo ya unenguaji. Je, wanautumia muda wa aina hiyohiyo ya mazoezi kwa kuomba ili kwamba Mungu aweze kuleta neno lake na kuwabariki watu wake katika mikutano hiyo? Bila shaka unajua jibu la jambo hili! Eti, wao wenyewe wanasema kuwa wanayafanya hayo yote kwa utukufu wa Mungu. Ni wazi kabisa kuwa hii sio kweli kwa mambo yote niliyoyashuhudia mwenyewe kwa kuyaona. Mambo haya yananihuzunisha sana!

Huo ni mfano mwingine wa wazi unaoonyesha maana nyingine ya kujitukuza katika mwili. Wanacheza kwa sababu wanafurahia kuigiza kutoka ulimwenguni na kuyaingiza kama tamasha ndani ya kanisa. Basi, kwa ujumla ni makosa kufikiri kuwa watu hao wanafanya hivyo kwa kulifaidisha kanisa! Wananengua minenguo yao kwa muda hata wa dakika 10 na zaidi huku wakitokwa na majasho kwenye miili yao na kisha wanapomaliza kucheza hivyo wanaenda kukaa wamejichosha. Je, hilo ndilo kanisa mpendwa! Je, mifumo kama hii ndiyo inamwakilisha Kristo kwa waumini wake? Je, na wale watu wanaokuwa ameketi kanisani wakiwaangalia hao wanenguaji, huwa wanafikiri nini hasa wakati huo? Je, hayo yanawafanya wanafikiri juu ya utakatifu wa Bwana? Je, hiyo inawaongoza kumpenda Kristo zaidi? Je, hii inaliinua kanisa? Kwa vyovyote matukio hayo hayawezi kulijenga kanisa. Matokeo ya vituko hivyo vyote vinavyoonyeshwa humo kanisani vinasaidia tu kuchochea matamanio ya kimwili.

Kwa sababu ya mambo hayo ninajisikia vivyo hivyo kama Mariamu alivyojisikia alipolia na nataka kusema alilosema bustani, “wamemwondoa Bwana wangu, wala mimi sijui walikomweka.”

Lakini pamoja na hayo yote bado wachungaji na viongozi wa kanisa hawana ujasiri wa kuwaelekeza vijana wao kulingana na neno la Mungu kwa namna ambayo itawasababishia wao kukua katika Kristo wakiwa ni wakristo walioimarika. Badala yake wao wanayaruhusu mambo kama hayo yatokee, yaendelee kufanyika kanisani mara zote – kisha hatimaye wanakuja kushangaa kwa nini tendo la dhambi ya uzinzi inakuwa ni tatizo kubwa la kanisa kati ya vijana katika makanisa!

Tulikuwa na mkutano wa siku tatu huko kwenye milima ya Udzungwa mkoa wa Iringa. Kila mara mwishoni mwa mkutano watu huimba na kusalimiana pale nje ya mlango wa kanisa kama ilivyo desturi ya mila za kanisa huko. Walikuwa wamekoka moto nje ya kanisa kwa sababu ni inchi ya baridi. Watu huota moto huo, basi watu waliendelea kucheza na kuimba kwa nguvu wakiuzunguka moto ule, na shughuli hii iliendelea kwa muda wa dakika kama 15 hivi. Kisha nikamweleza mzee wa kanisa kuwa angefunga uchezaji ule sasa vinginevyo vijana wale wangejiingiza kwenye matatizo. Alinielewa nilivyosema na mara moja akasema, “Tulishawahi kupata matatizo!” Mwenendo kama huu hauwaongozi vijana wa kiume na wa kike kwenda misituni kuomba maombi! Mwenendo huo unasababisha dhambi tu!

Je, hatuwapendi vijana wetu! Kwa nini kunaonekana kuna upungufu au kukosekana kabisa kwa mafundisho ya Kimungu na miongozo katika makanisa!

Nafahamu kuwa mfalme Daudi alicheza walipolirudisha sanduku la Bwana Jerusalem, lakini ebu tusijidanganye wenyewe kwamba eti, kinachotokea leo makanisani kinaweza kulinganishwa kwa namna yoyote ile na alichokifanya Daudi. Daudi alikuwa haleti matamasha ya kidunia kwa watu wa Mungu kila wiki!

Tunaharibu vijana wetu na kizazi hiki na mwenendo huu. Je, vipi hatutambui tunatayarisha sehemu ya kizazi hiki cha waumini itekeleze neno lile la Mungu lisemalo, “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani.”?

Na kimsingi, mambo hayo sio kosa la ulimwenguni, hayasababishwi na wasioamini, ni kosa la kiongozi na wachungaji wa makanisa mengi.

Ni wakati turudi kwenye kumhubiri Kristo naye AMESULIBIWA! Kama Daudi alivyosema, “Wakati umewadia Bwana atende kazi; Kwa kuwa wameitangua sheria yako.” (Zaburi 119:126).

Sipendi kuandika ya namna hiyo, jamani, lakini yanayotokea ni hatari sana na ni lazima kuandika kwa uwazi juu ya mambo hayo.

Jambo hili linafanana pia na mambo ya muziki na vikuza sauti vya muziki makanisani. Vijana wanaruhusiwa kutawala uimbaji na kuabudu na wanafanya hivyo kwa sauti kubwa ya juu kwa kutumia vyombo vya muziki vilivyokuzwa sauti kubwa hata inawafanya washirika wenyewe wasisikie hata sauti yao wenyewe. Ndiyo vijana wanapenda kutumia fursa kama hizo kuigiza ulimwengu na kutamashisha hivyo hivyo makanisani. Sikiliza hii nayo! Nilikuwa katika kanisa fulani huko Dar Es Salaam, ambapo mchungaji alimwambia yule anayesimamia muziki wa kwaya ili ajaribu kupunguza sauti ya vyombo maana ilikuwa juu mmno. Japo kuwa mchungaji huyu alimwomba kijana yule mara mbili zote kupunguza sauti ile lakini kijana yule hakupunguza sauti, aliendelea kuburudisha kwa sauti ya juu ya vyombo vile. Hivyo mchungaji yule alilazimika kwenda kwenye eneo la vyombo vya muziki na kupunguza sauti ya vyombo vile yeye mwenyewe!

Ndiyo, hata mimi nawapenda sana vijana na kwa ujumla ni kutokana na kule kuwapenda vijana kiasi kwamba inaniumiza mimi sana kuona wachungaji wengi wanawaharibu vijana kiroho.

Unijalie niseme kitu zaidi. Unafikiri ingetokea nini kama mwislamu kijana angependa kuanzisha mambo ya kukuza sauti kwa ajili ya kuimbia msikitini mwao kama vile kijana huyo angetamani kuleta bendi kwa ajili ya kuabudu msikitini humu kwa kutumia vyombo vya muziki vya umeme?! Jibu liko wazi, liko wazi kabisa! Kulingana na uaminifu walionao kwa lile wanaloliamini, basi vijana wao wa kiislamu hata hawawezi kupata muda wakufikiria kufanya jambo kama hili. Ikiwa ingetokea wakapeleka ombi lao kama hili kwa viongozi wao wa msikitini, je, wasingeweza kukemewa kwa ukali!

Kama leo utaenda kuingia msikitini, hutakipata kitu chochote kinavyo kuburudisha wewe kama tamasha humo, au kuvutia mwili wako. Wao wanakaza na kuonyesha unyenyekevu wao kwa kile wanachokiamini. Niacheni niseme hili kwa masikitiko makubwa kuona waislamu wanaonyesha heshima yao kwa kile wanachokiamini kuliko wachungaji wengi wafanyavyo kwa Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ili tupate kuwavutia watu makanisani mwetu tunamuuza Mungu wetu kwa urahisi. Je, hatuna hata chembe ya aibu kweli pale tunapoacha kumheshimu Mungu kwa kuyaruhusu mambo kama haya yatokee makanisani?

Labda unashtushwa na maneno hayo, lakini hili si wazo langu tu – Ilikuwa ni Mungu mwenyewe alisema kuhusu watu wake kupitia nabii Jeremia, “Je! Taifa wamebadili miungu yao, ingawa siyo miungu? Lakini watu wangu wameubadili utukufu wao kwa ajili ya kitu kisichofaidia. Enyi mbingu, staajabuni kwa ajili ya jambo hili, mkaogope sana, na kuwa ukiwa sana, asema Bwana. Kwa maana watu wangu hawa wametenda maovu mawili; wameniacha mimi, niliye chemchemi ya maji ya uzima, wamejichimbia mabirika, mabirika yavujayo, yasiyoweza kuweka maji.” (Jeremia 2:11-13).

Hapa Mungu anashangaa kuona kuwa mataifa mengine yanaheshimu miungu yao – ni watu hawa Wake pekee ndio wanaomwacha na kufuata mifumo mingine ya kuabudu!

Yesu Kristo ndiye anayesimama katikati ya kanisa ambaye macho yake yanawaka kama mwali wa moto akiangalia moja kwa moja kwenye hamasa ya kweli na hali ya mioyo huku akiona kila jambo lililofichika. Na ndiye anayepima thamani halisi ya kile anachokiona kwetu. Na mara zote hayapimi mambo kama tufanyavyo wanadamu! Analiambia kanisa mojawapo, wasipotubu atakiondoa kinara, ambayo inamaanisha kuwa kanisa hilo halitakuwa tena kanisa lake (Ufunuo 2:5). Kanisa lingine ambalo lenyewe lilijiona kuwa ni tajiri, yeye analiita kanisa hilo kuwa ni nyonge, na ni fukara, na yuko tayari kulitema kanisa hilo kutoka katika kinywa chake (Ufunuo 3:15-17). Na hivyo ndivyo ilivyo hata leo. Washirika wanakutana mahala pamoja kwenye jengo kisha wanajiita wenyewe kuwa ni kanisa la Kikristo, lakini Kristo halitambui kuwa ni kanisa lake! Hawang’ali kwa utukufu wake! Wamebadilisha utukufu wa Mungu (ambao ndiyo tabia yake Mungu) na jambo jingine linalotokana na mwanadamu, jambo ambalo sasa linamtukuza mwanadamu na kazi zake tu!

Je unaweza kuiona sura halisi ya jambo hili hapa? Tukutanikapo pamoja basi mkazo wetu uwe ni Kristo. Anapaswa kukuzwa na kutukuzwa katikati ya kusanyiko letu. Haipaswi kuwepo na wivu au mashindano wala kusiwepo na kujiridhisha binafsi. Hatuji kukusanyika ili kukidhi furaha yetu wenyewe, yaani kujifurahisha wenyewe au kujipendeza wenyewe. Tunakuja ili kumpatia sifa na kumtukuza kisha kumwacha Mungu aongee ndani ya mioyo yetu! Tunakuja kumheshimu na kumwonyesha heshima yetu. Kila tukifanyacho kinapaswa kifanyike kwa utukufu wake peke yake, na wala isiwe kwa ajili ya utukufu wetu sisi. Kila jambo linalosemwa na kufanyika liwe ni la kumfurahisha yeye na wala sio sisi!

Ni Kristo ndiyo anayepaswa kudhihirishwa na kuonekana katikati yetu. Neema yake inayofanya kazi kwa kila mshirika ndiyo kwa hakika inayolibariki kanisa zima. Kanisani sio mahala pa kujisifu au kujionyesha uwezo wetu wa kupiga vyombo, kuimba, kucheza na hata kuhubiri! Tunapaswa kuwa na mioyo inayoabudu ambayo inainama mbele zake. Wala tusitafute kumnyang’anya Mungu utukufu wake kwa kuwafanya watu waanze kutupongeza  kwa kile tunachokifanya. Heshima yetu kwa Mungu mwokozi wetu ijaze mioyoni mwetu, na ndiye anayepaswa kusujudiwa nasi kiasi kwamba hakuna mwili unaomtukuza mbele ya uwepo wake. Anasimama katikati ya kanisa lake! Je, kwa kweli tunautaka utukufu wake pamoja na uwepo wake? Kama jibu ni ndiyo, hii inamaanisha ni kifo cha aina zote za matangazo hayo na kujinadi huko.

Tunasoma haya katika kitabu cha matendo ya mitume, “Na kwa mikono ya mitume zikafanyika ishara na maajabu mengi katika watu; nao wote walikuwako kwa nia moja katika ukumbi wa Sulemani; na katika wote wengine hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao; ila watu waliwaadhimisha; walioamini wakazidi kuongezeka kwa Bwana, wengi, wanaume na wanawake.” (Matendo 5:12-14).

Je, unakiona kile tulichonacho hapa? Washirika wanapokusanyika pamoja, hapakuwepo hata mtu mmoja aliyethubutu kujiunga nao! Kwa nini? Je, ni kwa sababu Wakristo walijifanya kuwa ni watu muhimu na wenye kuwalaani wale wasioamini? Hapana! Je, ni kwa sababu Wakristo walikuwa ni wanafiki ambapo walijifanya kuwa ni watakatifu kuliko wengineo? Hapana! Watu wengine waliwatukuza! Sasa, kwa nini basi hata mmoja hakuthubutu kujiunga pamoja nao walipokuwa wakikutanika? Hii ni kwa sababubu watu hao walipokuwa wakikusanyika mkazo wao wote na upendo wao wote, na ibada yao ilielekezwa kwa Mungu tu ambaye amewaokoa kutoka katika dhambi zao! Hivyo upendo wao, ibada yao kuabudu kwao na heshima yao kwa Mungu ilijaza mioyo yao na ilidhihirishwa kwa uwazi pale walipokutanika pamoja.  Walikuwa wamekazia katika ibada yao kwa Bwana Mungu wao, kiasi kwamba kama wewe bado hujabadilishwa kwa wokovu huo huo, ungefahamu kuwa upo nje ya kile kilichokuwa kinajaza mioyo ya waumini. Mara moja ungetambua kuwa humjui Mungu wao, na kuwa nawe usingekuwa na njia nyingine ya kuabudu Mungu kama wanavyofanya wao! Ungetambua kuwa kile kilichokuwa kikiwasukuma wao kuomba, kuabudu kwa namna ya mtindo huo, haina nafasi kabisa katika maisha yako!

Ungethubutu tu kwenda pale iwapo tu kama ungekuwa na jambo maalum linalo kuvutia ili kubadilishwa na wokovu huu ambao umewabadilisha wengine wengi! Ibada yao kwa Mungu ilikuwa ni kamilifu kiasi kwamba ni kwa Mungu mwenyewe ndiko nyimbo zao, maombi yao na kuhubiri kwao walimwelekezea. Na kutokana na sababu hii ndiyo maana watu wengine walitambua ni waumini wa dhati, na hiyo waliwaadhimisha. Je, kutokana na hayo kanisa liliendelea kusinyaa? Hapana! Inasemwa kuwa waumini wengi waliongezeka kwa Bwana na makundi makubwa ya wanaume na wanawake!

Watu wengi wameacha hali hiyo ya kanisa la kwanza siku hizi za leo.

Nilinukuu kutoka katika kitabu cha Yeremia ambapo Mungu analalamika kuwa ni watu wake tu ambao wamemwacha ili kuabudu mambo mengine. Katika sura ileile ya neno la Mungu, Mungu anasema kuwa, “Makuhani hawakusema, Yuko wapi Bwana? Wala wana-sheria hawakunijua; wachungaji nao waliniasi, nao manabii walitoa unabii kwa Baali, wakafuata mambo yasiyofaidia kitu.” (Yeremia 2:8).

Unaona? Sasa, badala ya kuhubiri ‘Yesu Kristo, naye amesulibiwa’ na ‘neno la msalaba’, badala ya kutambua kutokuwepo kwa uwepo halisi na nguvu ya Bwana katika makanisa yetu, badala ya kutambua hitaji letu la kumhitaji yeye kwa kuliita jina lake, kuomba kwake yeye, na kumngojea yeye ili kwamba yeye apate kufanya kazi katika maisha yetu na katikati ya kanisa, sasa viongozi wanageukia kwenye namna nyingine nyepesi za mtindo wa kuwavutia watu kanisani. Na matokeo ya hayo yote ni kwamba wachungaji, viongozi, manabii, maaskofu na mitume wa aina hiyo wanaohubiri kutoka kwenye Biblia hawamjui Mungu kweli kweli.

Wachungaji wanafurahia kuwaruhusu vijana kusherehesha watu kanisani, kwa nyimbo zao nakucheza kwao. Wachungaji wengi wanapenda kuhubiri juu ya uamsho, upako, na nguvu au wanahubiri kuhusu mafanikio na mapesa, lakini mengi ya mafundisho ya aina hii hayana maana yoyote – ‘Hawa ni visima visivyo na maji, na mawingu yachukuliwayo na tufani”. Kwenye mahubiri yao wanawaahidi watu mambo mengi lakini ukiuangalia mwisho wake unagundua kuwa hakuna lolote wanalopokea watu – ni maneno matupu ambayo yanawahamasisha watu kwa muda mfupi tu, lakini wamenyimwa neno la Mungu katika maisha yao. Hapa tena Mungu analalamika zaidi dhidi ya watu wake kwenye Yeremia,

Jambo la ajabu, la kuchukiza, limetokea katika nchi hii! Manabii wanatabiri uongo, na makuhani wanatawala kwa msaada wa hao; na watu wangu wanapenda mambo yawe hivyo. Nanyi mtafanya nini mwisho wake? (Yeremia 5:30-31).

Siku hizi viongozi wengi hawahubiri tena neno la Mungu. Wanahubiri mambo yanayo wafurahisha watu. Tena tunayo maeelezo yenye kuhuzunisha sana ambapo Mungu anasema kuwa, “na watu wangu wanapenda mambo yawe hivyo!’ Na ndivyo ilivyo leo katika makanisa mengi. Watu wanapenda na kuridhia kushereheshwa makanisani; wanapenda kusikia ahadi kubwa kubwa zinazohusu maisha yao zinazotolewa na wahubiri. Na sasa mwishowe watafanya nini? Na matokeo ya mambo kama hayo itakuwa nini?

Mtume Yohana alimwona mwanakondoo alionekana kana kwamba amechinjwa, katikati ya kiti cha enzi cha Mungu. (Ufunuo 5:6).

Je, tunapenda Yesu Kristo asimame katikati yetu? Je, tunampatia nafasi ndani ya mioyo yetu na katika maisha yetu, katika kanisa letu? Yeye anasimama kama mwanakondoo aliychinjwa; yeye ambaye hajitafutii mambo yake mwenyewe lakini badala yake yeye huyaweka chini maisha yake kwa ajili ya kanisa. Nasi tunapaswa kufanya vilevile! Yeye apendaye maisha yake atayapoteza, lakini yeye apotezaye maisha yake atayapata tena! Kama wewe unatafuta madaraka na vyeo kanisani na kuonekana na watu wengine katika yale unayoyafanya, basi hapo utapoteza maisha yako. Hapo utakuwa humtumikii Bwana Mungu bali unajitumikisha mwenyewe tu, unajipendeza mwenyewe tu. Ikiwa makanisa leo yanataka yahesabiwe kuwa ni kanisa lakeYesu, basi hapo makanisa mengi yatapaswa yafanye mageuzi kwa kiasi kikubwa – ambapo pasipo mashaka yoyote mageuzi hayo yatahusisha na kutubu!

Mungu ageuzie mioyo yetu kwake, nyakati hizi ili kwamba apate utukufu ambao ni stahiki ya jina lake! Kama Daudi alivyoomba, “Ee Mungu, uturudishe, Uangazishe uso wako nasi tutaokoka.”  (Zaburi 80:3).

© David Stamen 2016        somabiblia.com

 

 

 

Comments are closed.

 
%d bloggers like this: