RSS

Maagano ya Mungu

Hapa kwa ufupi nimeandika kwa kugusia na kutoa muktadha wa maagano ambayo Mungo amefanya na mwanadamu.

Biblia inaundwa na kile kinachoitwa Agano la Kale na Agano Jipya. Lakini Biblia ni moja. Kuna vitabu sitini na sita 66 kwenye Biblia (39 vikiwa ni vya Agano la Kale na 27 vikiwa vya Agano Jipya)  lakini Biblia yenyewe kama ilivyo, ni kitabu kimoja. Biblia nzima inaonyesha ni kwa jinsi gani Mungu anavyojihusisha na mwanadamu – kuanzia pale alipowaumba mwanaume na mwanamke hapa duniani mpaka siku ya mwisho ya hukumu na uzima wa milele kwa watoto wa Mungu. Ni habari moja. Hakuna mvutano, mgogoro wala mkanganyiko baina ya Agano la Kale na lile Jipya. Ni habari kuhusiana na sababu za Mungu kumuumba mwanadamu na ni kwa namna gani analitimiza kusudi lake kwa mwanadamu aliyemuumba. Ni Mungu Yule Yule katika maagano yote na anatimiza lengo na makusudi yake kupitia kitabu hiki hiki Biblia.

Biblia inadhihirisha kusudi la Mungu kumuumba mwanaume na mwanamke, “ Mungu akasema, Na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu….” (Mwanzo 1:26). Kususdi la Mungu la milele lilikuwa, na hata sasa lipo ni kutufanya sisi tuwe kama alivyo Yeye na ‘kuingiza wana wengi zaidi kwenye utukufu wake’ (Waebrania 2: 10), ili sisi kama watoto wake, wenye asili moja naye, tumtumikie na kuishi pamoja naye milele kama bibi harusi wa Kristo. Hili ndilo kusudi kuu la Uungu la milele kwa kila kitu. (Warumi 8:29; 2 Petro 1:4; Waefeso 5:25- 27; 1 Yohana 3:2).

Lakini tatizo lilikuwa ni dhambi. Dhambi ilisababisha kuzaliwa kwa Agano zaidi ya moja kati ya Mungu na wanadamu. Maagano hayo yanaonyesha madaraja tofauti tofauti ambayo Mungu anayatumia kuidhihirisha dhambi kwa kina na mapana yake katika moyo wa mwanadamu na ni kwa jinsi gani mwishowe Mungu atakavyoshughulika na hiyo dhambi iliyomo moyoni mwa mwanadamu na wokovu mkuu wa kweli. Kupitia kutokutii kwa Adamu katika bustani ya Edeni pale mwanzo, dhambi na mauti vilizaliwa katika maisha ya mwanadamu. Kimsingi kwa mtazamo mmoja, maagano yote makuu ambayo Mungu aliyafanya baina yake na mwanadamu, yalikuwa ni njia ya Mungu ya kushughulika na dhambi na kutimiza kusudi lake la kumfanya mwanadamu afanane naye. Habari ama historia ya Biblia inaonyesha ni kwa jinsi gani dhambi ilikuja duniani na ni kwa jinsi gani Mungu aliweka njia kwa wanaume na wanawake kuokolewa toka kwenye dhambi ili waweze kuishi pamoja naye milele. Maagano tofauti yanawakilisha madaraja tofauti ambayo Mungu aliyatumia kuleta ukombozi kwa mwanadamu. Ni ‘habari’ moja. Ni historia moja – yenye madaraja ama hatua tofauti, ndio; lakini bado, historia ni moja. Ni mpango wa Mungu wa wokovu tangu mwanzo wa nyakati hata siku ya mwisho ya hukumu na baada ya hapo. Si sahihi hata kidogo kuwaza ama kufikiri kwamba Agano la Kale na Agano Jipya yako tofauti kwa namna fulani, yakiongelea habari tofauti na kuna mvutano ama mkanganyiko  kwenye vifungu vyake ama  mtu anatakiwa kuchagua mojawapo! Biblia nzima inawakilisha neno la Mungu. Mungu hakubadili mawazo yake kuhusiana na mambo alipofika katikati. Yesu alilihesabu Agano la Kale kama limehamasishwa ama kuhuishwa na Roho Mtakatifu (Mathayo 22:43; Yohana 10: 35).

Ngoja nijikatishe mwenyewe hapa, kuweka jambo moja vizuri. Wakati mwingine watu hujichanganya na huchanganya wengine pia kwa kuongelea mambo tofauti pale wanapofikiri wanazungumzia jambo moja! Kuhusu wokovu, kuwekwa huru mbali na dhambi na kuishi maisha matakatifu, ni wazi kwamba Agano Jipya linatufundisha kuwa hatuwezi kuhesabiwa haki kwa matendo ya sheria (sheria ya Musa) wala sheria haiwezi kutufanya tuwe watakatifu. Haiwezi kwa sababu ya nguvu ya dhambi iliyomo ndani ya maisha yetu. Tunahitaji nguvu mpya maishani mwetu! Tunahitaji kuzaliwa upya toka juu! Hii huja kwa imani na kwa kupitia neema. Ukamilifu unaohitajiwa na sheria, unakamilishwa kwa Mkristo kwa imani ya kile Mungu alichokifanya kupitia mwanawe pale Kalvari na kupitia uzima wa Kristo ndani yake. Haukamilishwi na sisi wenyewe, kwa juhudi zetu binafsi, kwa kujaribu kutenda sawa sawa na jinsi sheria ilivyoagiza na ambayo iliandikwa ‘kwa nje ya maisha yetu sisi’. Mungu anafanya kitu ndani yetu ambacho kinatupa uwezo wa kuishi sawa sawa na maagizo yake kwetu. Kwa sababu ya kusafishwa kwa damu ya Yesu, kwa ushindi wake wa kuishinda dhambi, kifo na shetani, wokovu ni kwa imani kwa kile ambacho amekifanya. Bila shaka tunatakiwa kuishi maisha matakatifu, hii ndiyo sababu ya Yesu kufa, ijapokuwa ni kwa imani na kupitia neema. Hata hivyo, kusema kuwa bado tunahitaji ‘kushika sheria’ kama Wakristo, kufanya hivyo ni sawa na kwenda kinyume na mafundisho ya Agano Jipya. Kwa sababu ndani ya Agano Jipya, sheria ya Musa imekuwa ikionekana kama ni kitu kilichoko nje ya maisha yetu kama itabidi tujaribu kuishika kwa juhudi zetu binafsi! Kupitia kifo cha Yesu na Agano Jipya, Mungu anaweka Roho wake kwetu na kutupa neema na nguvu ya kuishi maisha matakatifu kwa imani katika yake! Kwa maana hii hatuko tena chini ya sheria, wala kuishi kwa matakwa ya sheria. Agano Jipya lote limekuwa wazi katika hili. Ingawa, kusema kuwa vitabu vya Agano la Kale havina umuhimu tena, si sahihi kabisa. Biblia ni neno la Mungu, lililovuviwa na roho Mtakatifu. Wakristo ulimwenguni kote wanatambua ya kuwa hili si swala linalohitaji mjadala (ni kwa jinsi gani baadhi ya mambo katika Agano la Kale yaelezewe, ni swala la mjadala kwa baadhi ya watu tu).

Je, ni kwa nini Agano Jipya linaitwa Agano Jipya? Ni kwa sababu limekuja badala ya Agano la Kale. Upo muunganiko hapa! Tutakwenda kuona punde, kile Mungu alifanya kwenye Agano la Kale (hasa kwa kuwaokoa wana wa Israel kutoka katika utumwa wa Misri na swala la sadaka za kuteketezwa) kutuonyesha kwa njia ya mfano ama picha kile ambacho angekuja kukifanya kupitia kwa mwanawe Kristo! Kwa njia hii, Agano la Kale linatupa sisi uelewa mkubwa na wa kina wa kazi na huduma ya Yesu Kristo. Zipo jumbe za kinabii za kustaajabisha katika Agano la Kale zinazomuhusu Yesu Kristo ambazo zinaonyesha ni kwa jinsi gani Mungu alimchagua mwanawe awe Masiha na mwokozi wa ulimwengu. Maandiko haya kutoka katika Agano la Kale ni chanzo kikubwa cha baraka, faraja na mafundisho kwa Wakristo. Aidha basi, ni kwa jinsi  gani naweza kulifuata neno la Yesu na kuelewa kile ambacho kimeandikwa katika kitabu cha Danieli bila kusoma kitabu cha Danieli (Mathayo 24:15)? Je, ninahitaji kulifahamu Agano la Kale ili niweze kuokoka? Sihitaji. Lakini kama mwanafunzi wa Yesu utahitajika kulisoma neno la Mungu na kujifunza vile uwezavyo kuhusiana na Kristo na wokovu wako katika Kristo.

Ni kama vile nilivyotangulia kusema hapo awali, tatizo ni dhambi. Mungu alimuumba Adamu kutoka mavumbini kwa mfano Wake Yeye Mwenyewe, lakini kupitia huyu ‘mtu mmoja dhambi iliingia duniani’ (Warumi 5:12 ‘kwa hiyo, kama vile kupitia mtu mmoja dhambi iliingia duniani, na kifo kupitia dhambi; na hivyo kifo kikawafikia watu wote, kwa hiyo wote wametenda dhambi’). Dhambi ilibadili hali ya kiroho ya Adamu (Mwamzo 2:17) na ikapelekea kufukuziwa nje ya bustani na mkewe Eva. Kwa sababu ya dhambi hata mazingira ambayo Adamu alikuwa akifanyia shughuli zake yalibadilika (Mwanzo 3:18).

Matendo maovu na dhambi viliendelea kushamiri duniani mpaka Mungu akatuma mafuriko kuangamiza kila mtu isipokuwa Nuhu na familia yake ambao waliingia kwenye safina ambayo Mungu alimwamuru Nuhu kuitengeneza. Mungu aliweka Agano na Nuhu ya kwamba hataiangamiza nchi tena kwa mafuriko ya maji.

Baadaye, Mungu aliweka Agano na Abrahamu, ambaye alimchukua kati ya mataifa na kutokea kwake ambaye taifa la Israel lilizaliwa. Agano hili na Abrahamu lilionyesha ni kwa jinsi gani Mungu atakwenda kuyabariki mataifa ya dunia. Mungu aliahidi kwamba atafanya taifa kubwa toka kwa Abrahamu na kupitia yeye mataifa yote ya dunia yatabarikiwa. Ijapokuwa ilionekana kama ni jambo lisilowezekana, ‘Abrahamu alimwamini Mungu na Mungu alimuhesabia haki.’ (Mwanzo 15: 6) Ukweli huu na ahadi hizi kwa Abrahamu zinaweza kuwa ama kufanyika msingi wa wokovu katika Agano Jipya. Agano Jipya na wokovu kupitia kwa Yesu ni utimilifu wa ahadi ya Mungu kwa Abrahamu. Lakini bado.

Mungu alimwambia Abrahamu kuwa uzao wake utachukuliwa utumwani katika nchi ya ugeenini, lakini atawakomboa na kuwapeleka katika nchi aliyowaahidia. Mungu alifanya hivyo kupitia Musa na Yoshua (katika hatua hii yapo mengi yawezayo kusemwa lakini nitaendelea kutilia mkazo katika swala la maagano.) kwa kuwatoa wana wa Israel toka katika nchi ya Misri na kuwafanya warithi wake mwenyewe, Mungu anawapa Torati au Sheria katika mlima Sinai ambayo inazingatia zile amri kumi. (‘Naye akaandika katika hizo mbao, hayo maneno ya agano, hizo amri kumi’ Kutoka 34:28. ‘Sheria ilitolewa na Musa’ Yohana 1:17). Agano Jipya linaelezea makusudi ya sheria. Tunaambiwa ya kuwa sheria iliongezwa kwa sababu ya dhambi. ‘Torati ni nini basi? Iliingizwa kwa sababu ya makosa, hata aje huyo mzao aliyepewa ile ahadi’ (Wagalatia 3:19). Mungu alikuwa anakwenda kufunua mapana na marefu ya dhambi kupitia sheria. Sheria ilifunua ni kwa jinsi gani ambavyo tusingeweza kuishi maisha matakatifu na ya haki. Sheria inafunua hali yetu ya udhambi ya ndani na vile ambavyo dhambi inatutumikisha kama watumwa, ‘lakini sheria iliingia ili kosa lile liwe kubwa sana’ (Warumi 5: 20). Je, Mungu alitaka tutende dhambi? Hapana! Lakini kupitia sheria alituonyesha vile ambavyo hatuna nguvu ya kuishika sheria kwa sababu ya nguvu ya dhambi iliyopo ndani yetu. Agano Jipya linatufunilia kwamba lengo la sheria ni kutushawishi kwamba tuna hatia mbele za Mungu na hatuna haki kabisa ukitupima kwa asili ya Mungu, ‘basi twajua ya kwamba mambo yote inenayo torati, huyanena kwa hao walio chini ya torati, ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu’.(Warumi 3: 19) Umeona hapa kuwa Paulo anasema “ulimwengu wote”. Kwa maneno mengine, ijapokuwa sheria walipewa wana wa Israel, mtu yeyote anayejaribu kuishi maisha ya haki atajikuta anashindwa! “Kama ilivyoandikwa, ya kwamba,’ hakuna mwenye haki hata mmoja.’” (Warumi 3: 10). Paulo mbeleni anaandika, ‘kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria.’ (Warumi 3: 20). Kwa mara nyingine tunaona ya kwamba lengo kuu la sheria ni kutufanya tutambue kuwa sisi ni wenye dhambi. Sisi hatuwi wenye dhambi kwa sababu tumefanya dhambi; bali tunafanya dhambi kwa sababu ni wenye dhambi, kwa sababu nguvu ya dhambi imo ndani yetu. Kama ukimwambia nyoka atembee kwa miguu minne, aote manyoya, na kupiga makelele ya aina ile ile kama ya mwana kondoo, nyoka anaweza kujaribu kwa jitihada nyingi vile anavyoweza, lakini atashindwa kabisa kuwa mwana kondoo. Nyoka hawezi kujibadilisha awe mwana kondoo! Hivi ndivyo hasa inavyotokea kati ya sheria na mwanadamu. Sheria inatuambia kile tunachotakiwa kufanya na vile tunavyotakiwa kuwa, lakini haitupi nguvu ya kuishi hivyo, lakini inaishia kutufunulia tu ni kwa jinsi gani dhambi imetukamata pale tunapojaribu kuishi sawa na viwango vya Mungu. Hili ndilo hasa kusudio la sheria kutokana na tafsiri ya Agano Jipya. Lakini Mungu alidhamiria kuleta ukombozi toka dhambini, ‘na kama vile Musa alivyomuinua Yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye.’ (Yohane 3:14,15).

Hivyo basi, lengo la torati, ambayo inajumuisha amri kumi zilizoandikwa kwenye jiwe, ilikuwa ni kumfanya mwanadamu atambue ni kwa jinsi gani anahitaji wokovu! Torati (au mawe yaliyopo ‘nje’ yetu) haina nguvu ya kutufanya wenye haki wala kutupa uzima (Wagalatia 3:21). Kwa kutufanya tutambue ni kwa jinsi gani tu wadhambi, torati inatuandaa kwa ujumbe wa Kristo wa wokovu. Hivyo, ndio maana Paulo akasema, ‘Hivyo torati imekuwa kiongozi (au mwalimu) kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani. Lakini ipo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi’. (Wagalatia 3:24-25). Hivi sasa bila shaka, kwanza kabisa, hii inaturejeza kwa Waisrael ambao walikabidhiwa torati. Lakini inakwenda mbele zaidi ya hapo, inakwenda kwa kila mtu ambaye anafanya jitihada zake binafsi kuishi maisha matakatifu bila ya kuwa na imani katika Yesu Kristo. Katika kile kitabu cha Warumi sura ya pili inatueleza kwamba, kwa sababu tuliumbwa na Mungu, upo utambuzi wa viwango vyake vya utakatifu katika mioyo yetu na dhamiri zetu pia. Yeyote ambaye anajaribu kuishi kwa haki, na awe na maisha matakatifu, punde tu atatambu a ya kuwa lipo giza nene, uchungu, uchafu, chuki na husuda moyoni mwake – kama atakuwa mkweli na nafsi yake na kama pia ataisikiliza dhamiri yake! Kama sisi ni wayahudi kwa kuzaliwa ama si Wayahudi, jaribu letu kubwa ni kudhania ama kufikiri ya kuwa tunao uwezo wa kujifanya watakatifu sisi wenyewe ama kwamba tayari sisi ni watakatifu. Hasa kabisa kwenye eneo la imani, inaweza kuwa ni rahisi sanaa kujikuta umeangukia kwenye mkumbo wa kufikiri kuwa dini inajaribu kutufanyia mambo mazuri kwa nje tu. Hii ndiyo sababu Paulo alipata shida na baadhi ya makanisa, wao walitaka kurudi kwenye kushika torati badala ya kumfuata na kumwamini Yesu kwa ajili ya utakatifu. Ni rahisi sana kuyaamini matendo ya kidini ya nje kuliko kumfuata Kristo! Paulo anasema ‘kwa maana wakiwa hawaijui haki ya Mungu, na wakitaka kuithibitisha haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu’. Paulo anaandika haya kwa Wayahudi, lakini hii ni kweli kwa mtu yeyote tu, hata kama ni mkristo! Na hili bila shaka, ndilo tatitzo hasa alilokuwa akipambana nalo katika makanisa kule Galatia. ‘Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlimpokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kutokana na imani?….. baada ya kuanza katika Roho, mnataka kukamilishwa sasa katika mwili? (Wagalatia 3:2,3).

Hivyo basi, Paulo anasema, tulikuwa chini ya sheria (tuliachwa ambapo juhudi zetu ndizo zilikuwa njema kwetu) mpaka pale imani ilipokuja, ‘kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwwa mpaka ije ile ile imani itakayofunuliwa’. (Wagalatia 3:23). Lakini sheria haikuweza kuzuia ahadi ambayo Mungu aliifanya kwa Abrahamu kwamba mataifa yatakwenda kubarikiwa kupitia yeye na ‘uzao’ wake ambao ni Kristo (Wagalatia 3:17,18). Wokovu na ukombozi kutoka katika dhambi ungeweza kuletwa kwa njia ama namna nyingine kwa njia tofauti, si kwa njia ya mwanadamu mwovu kujaribu kwa juhudi zake binafsi kushika na kutenda sheria takatifu ambayo haimo ndani yake, lakini kupitia kwa Yesu Kristo (ambae ndiye hasa ‘uzao’ wa Abrahamu ulioahidiwa) na kupitia kuweka imani kwake. Kitabu cha Agano jipya kinatufundisha kwamba si kwa njia ya sheria bali kwa imani, kupitia imani kwa Kristo, kwamba mataifa yatakwenda kubarikiwa. Hii ndiyo sababu hasa Paulo anasema, ‘Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu… ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikie mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani’. (Wagalatia 3:13,14)

Agano Jipya linatufundisha kwa uwazi  kwamba tunafanywa wenye haki na kuokolewa kwa imani, na kwa namna hiyo, ‘sisi ni watoto wa Abrahamu’ (Wagalatia 3:6,7). Abrahamu alimwamini Mungu, na akahesabiwa haki. Na sisi tunaamini nini? Tunaamini katika Yeye ambaye Mungu alimuahidi Abrahamu, Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. Na ni kwa kupitia imani tunapokea ile ahadi ya Roho.

Huu ni ukweli muhimu sana! Kwa sababu ya damu ya Yesu ambayo ilimwagika pale Kalvari, tunapokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani (Wagalatia 3:2). Tangu wakati ule Adamu alipofanya dhambi, kila mwanadamu aliondolewa kwenye nafasi ambayo Mungu alikaa. Hema ya kukutania ya jangwani ilituonyesha kwamba hakuna mtu hata mmoja aliyeweza kuingia penye uwepo wa Mungu kwa sababu ya dhambi. Kuhani mkuu pekee tena mara moja kwa mwaka alitakiwa kupeleka damu kwenye kiti cha rehema. Yesu Kristo alipokufa alilia ‘Imekwisha’ pale Kalvari, pazia la hekalu lilipasuka vipande viwili! Hii iliashiria kwamba, sasa njia ya kuuendea uwepo wa Mungu iko wazi kwa kila aaminiye katika Kristo. Waebrania sura ya tisa na ile ya kumi inatufundisha haya kwa uwazi mkubwa. ‘Basi ndugu kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu, njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake’ (Waebrania 10:19,20). Huu ni ukweli wa kustaajabisha! Ni kazi kubwa kiasi gani Mungu amefanya ya kutusafisha na kutuokoa na kutuleta kwake, pale yeye alipo! Sisi ambao, ‘ waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu’. Huu ni ukweli mkubwa wa Agano Jipya. Mungu anafanya kwetu kiumbe kipya! ‘…mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya. Lakini vyote pia vyatokana na Mungu.’ (2 wakorintho 5:17,18).

Hivyo Paulo akasema, ‘…kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutotahiriwa, bali kiumbe kipya’ (Wagalatia 5:15). Tunatakiwa kuzaliwa upya kwa mara ya pili; tunatakiwa kufanyika viumbe vipya, nje ya hapo kazi yetu ni bure na juhudi zetu zote za kuwa watakatifu zitakwama!  ‘Siku ile ninyi mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu’. (Yohana 14:20) Hili ni Agano Jipya! Limekuja badala ya lile la kale lililotolewa pale katika mlima Sinai! Waebrania 8:7-13 inaelezea vizuri haya, hasa pale inaposema, ‘Maana hili ndilo agano nitakaloagana na nyumba ya Israeli baada ya siku zile, asema Bwana; nitawapa sheria zangu katika nia zao, na katika mioyo yao nitaziandika; nami nitakuwa Mungu kwao, nao watakuwa watu wangu’ (huu ni mstari wa 10).

Si kwamba tu Mungu kupitia kwa Roho wake ameweka sheria yake katika mioyo yetu, lakini Kristo na Baba sasa wamekuja kuishi ndani yetu! (Yohana 14:23). Paulo anatamka, ‘Nimesulubiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, Bali Kristo yu hai ndani yangu’.  Na anatoa kauli hii ambayo inaonyesha mipaka ya sheria ambayo ilitolewa pale mlima Sinai, ‘Siibatili neema ya Mungu; maana ikiwa haki hupatikana kwa njia ya sheria, basi Kristo alikufa bure’. (Wagalatia 2:20,21).

Wako watu leo, kama vile ilivyokuwa wakati ule wa Paulo, wanasema inatupasa kuishika torati ijapo Agano Jipya linatuelekeza kwa uwazi kinyume na maneno ama mawazo hayo. Wanasema inatulazimu kufuata sheria aliyopewa Musa na kama hatutoifuata itaonyesha kwamba hatuna umakini wowote kuhusu kuishi maisha ya utii katika utakatifu. Haya ni mashitaka yale yale ambayo aliwekewa Paulo (Warumi 3:8). Paulo anaweka wazi kuwa wanakosea. ‘Ni nini basi? Tufanye dhambi kwa sababu hatuwi chini ya sheria bali chini ya neema? Hasha? (Warumi 6:15). Mwishoni mwa kitabu cha Warumi katika sura ile ya tatu, Paulo anaainisha kwamba ni kupitia imani kwa Yesu kristo tu tunaithibitisha sheria! ‘Basi je! Twaibatilisha sheria kwa imani hiyo? Hasha! Kinyume cha hayo twaithibitisha sheria’. Ni kama vile nilivyoelezea hapo juu, swali sio kwa swala la tuishi maisha matakatifu au la, bila shaka inatupasa tuishi kwa utakatifu. Lakini ni kwa nini Agano Jipya linatufundisha kwamba sisi hatuko chini ya sheria? Ni kama vile ambavyo nimeonyesha hapo juu, ni kwa sababu sheria ya Musa alipewa na Mungu ili kuonyesha ni kwa jinsi gani mwanadamu hawezi kushika sheria, kumuonyesha mapungufu yake na dhambi. Alichukuliwa mateka na dhambi na sheria ilikuwapo nje yake na kwa hiyo haikuweza kumbadilisha. Hivyo Biblia inatufundisha ya kuwa hatuwezi kuokolewa wala kufanyika wenye haki au watakatifu kwa kujaribu kushika torati. Maisha haya, ambayo Mungu anatutaka tuishi, yametimizwa ndani yetu kwa sababu ya neema yake ituwezeshayo na kwa sababu ya uzima Yake ulio ndani yetu. Haya yote huweza kupatikana tu kwa njia ya imani. Warumi 8:2,3 inaelezea haya yote kwa uwazi mkubwa. (Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili;  ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.’)

Kwa hiyo Paulo anafafanua ya kwamba utakatifu unaohitajiwa na sheria umekwisha jazwa ndani yetu ambao tunaishi kwa neema na katika Roho. Si kwamba viwango vya utakatifu vimefanywa vidogo kwenye Agano Jipya, kinyume chake, lakini ile njia ya kutufanya watakatifu ama kuufikia utakatifu ndio imebadilishwa! Tumezaliwa na Mungu! Ndani ya Kristo tumewekwa huru mbali na dhambi! Haki ya torati (the righteousness of the Law) inatimizwa ndani yetu, siyo kwa sababu ‘tunashika torati la Musa liliandikwalo kwenye mawe’, lakini kwa sababu sasa kupitia Agano Jipya Mungu anasema ‘Nitawapa sheria zangu katika nia zao, na katika mioyo yao nitaziandika.’ Yesu ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu! (Yoh.1:33). Kristo amekuja aishi ndani yetu kwa Roho Yake ili ‘tuenende vile vile alivyoenenda Yeye’ (1 Yoh.2:6).

Sasa ni kwa nini baadhi ya watu wamekuwa wakisisitiza ‘ni lazima tuishike torati’.  Sote tunatambua na tunakubali kwamba inatupasa kuishi maisha matakatifu ya kimungu na imani hiyo haimaanishi kwamba tunaweza kufanya dhambi kwa sababu tu neema ipo. Je hayo ni mabishano ya maneno tu lakini kimsingi maana ni ile ile. Labda, lakini inawezekana isiwe. Ni ajabu sana kuanzisha mabishano ya matumizi ya maneno (“kuishika torati”) pale Agano Jipya inapokataa wazo hili! Ni kama tu ilivyokuwa wakati ule wa siku za Paulo, ndivyo hivyo ilivyo hata leo, wapo wale wanaokuwa ‘wadini sana’. Wameweka mkazo sana kwenye mambo ama vitu vya nje tu na katika kushika kanuni. Paulo alisema akiwaambia Wagalatia, ana wasiwasi ama ana hofu kwamba imani yao inaweza ikawa bure tu na kwamba tayari wameshatoka kwenye neema na kuangukia kule kule walipotoka kwenye torati ama sheria. Je! Tatizo hapa liko wapi? Tatizo hapa ni hili – inaweza kumaanisha kwamba upo upungufu ama ukosefu kabisa wa badiliko la kweli la ndani katika maisha ya mtu, au ni lile badiliko la wokovu halijatokea kabisa ndani ya mtu  ambalo ndilo hasa humpa mtu nguvu ya kuishi kama Yesu katika dunia hii. Hiki ndicho hasa Agano Jipya limeleta! Kama mtu atakosa kitu hiki, bila shaka atakuwa akitegemea tu mambo ya nje na kusisitiza hitaji la ‘kushika torati’. Wanajaribu kushika ama kufuata kitu ambacho ‘hakimo ndani’ yao! Kwa mfano, mtu anaweza kusema, ‘Ninakwenda kanisani. Ninamwamini Yesu. Ninajaribu kuzishika amri’. Na hata wanaweza kusema, ‘Ninakwenda kwa kuhani kuungama dhambi zangu na ananiambia kuwa zimesamehewa’. Mtu anaweza kusema haya hata hajaokoka. Hili swala linagusa mamilioni ya watu ulimwenguni kote leo. Hili pia lilimgusa dereva mmoja ambaye alinichukua kunipeleka katika vijiji huko Tanzania ambapo nilikwenda kuhubiri injili. Alinieleza kuwa yeye alikuwa ni mkristo na pia ameokoka. Nilitambua kutokana na maelezo yake na mwendo wake kuwa hakuwa. Nilijaribu kumpima lakini akasema kwamba anamuamini Yesu na kanisani anakwenda na aliamini kile kuhani alikuwa akisema na kwamba kuhani angeweza kuzisamehe dhambi zake pale anapozikiri! Nilimwambia wazi kuwa hakuwa ameokoka, ilionyesha yale yote niliyoyasema hayakumuingia. Lakini miezi kadhaa baadaye nilipompigia simu, alisema amekwenda katika kanisa lingine na kwamba maisha yake yamebadilika na sasa alikuwa ameokoka!  Alitambua ya kwamba kile alichokuwa nacho mwanzo ilikuwa ni dini tu ya nje ambacho hakikuweza kubadili maisha yake aweze kuishi kwa utakatifu. Sisemi kwamba hili ni swala la kila asemaye kwamba inatupasa ‘kushika torati’, lakini inainua swali kwamba ni kiasi gani cha nguvu iletayo badiliko ya Roho wa Mungu watu wao wanaijua ambao wanasema mambo hayo. Nguvu ya Injili hii hutuweka huru mbali na dhambi na inatupa nguvu ya kuishi kama vile ambavyo Yesu aliishi! Ni wokovu mkuu namna gani na ni upendo mkuu namna gani ambao Mungu ameonyesha kwetu ya kwamba tuitwe wanawe! Kama ukisema ni lazima kushika ‘sheria ya Musa’, hakikisha kuwa hukosi nguvu ya uzima wa Yesu ndani yako.

© David Stamen 2014    somabiblia.com

Kupakua somo hili bonyeza link hapo chini:

Maagano Ya Mungu

RUDI KWA HOMEPAGE

 

 

5 responses to “Maagano ya Mungu

  1. Samwel Amon

    August 26, 2014 at 7:53 am

    Am so glad for your bible teaching

     
  2. Shukrani Ngwangwalu

    October 20, 2014 at 6:10 am

    Nimebarikiwa na kujua ambayo sikuyajua juu ya somo hili

     
  3. David anyanda

    February 28, 2016 at 8:35 am

    nimebarikiwa somo hili

     
  4. Eunice

    July 5, 2016 at 12:43 pm

    Amen mtumishi nmekupata vizuri. Tupo pamoja. Bwana akuinue zaidi.

     
  5. Anonymous

    July 3, 2020 at 11:29 am

    Glory to God

     

Leave a Reply