RSS

DHAMBI ZA TAIFA (MAKALA)

KUTUBU KWA AJILI YA DHAMBI ZA TAIFA    

(Kupakua bonyeza link: KUTUBU KWA AJILI YA DHAMBI ZA TAIFA)

SEHEMU YA KWANZA

Paulo na Sila walipofika Beroya katika Matendo 17:10, tunaambiwa kwamba watu wa Beroya walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike kwa sababu walilipokea neno kwa utayari wote wa moyo na wakayachunguza maandiko kila siku waone kama mambo yalikuwa ndivyo. Hakika hii ndiyo taratibu ambayo hupendekezwa na maandiko, yaani kwamba kwanza tuone katika maandiko mafundisho yoyote mapya kabla ya kuyaamini na kuyapokea mioyoni mwetu. Huku si kutoamini lakini inaonyesha kuwa tunapendezwa na mambo kama hayo kama Mungu alivyoyafunua kupitia Neno lake. Tunatakiwa kuheshimu na kumpenda Mungu kwa kuyafuata mambo yale ambayo ameyaonyesha kwetu kwa uwazi. Hii pia ni ulinzi kwetu –tutalindwa toka madhara na udanganyifu kwa kulitunza Neno lake kwa unyenyekevu.

Vivyo hivyo, kama tukimsikia mtu anahubiri na kutuambia tuamini hili au kufanya lile, lakini hatuvioni vitu hivyo kufundishwa katika maandiko, basi tusipokee mafundisho hayo kabisa. Haijalishi kama mafundisho yanatufikia kupitia msemaji wa kimataifa anayetukuka, kitabu cha kikristo ambacho kimeuzwa nakala mamilioni ulimwengu mzima, au mtu ambaye tunaweza kuwa tunamheshimu. Haijalishi hata kama imetoka kwa Mtume au hata malaika kutoka mbinguni (Galatia 1:8), tusiamini wala kupokea kama jambo hilo hatuwezi kuliona kwenye maandiko. Mtume Paulo alishangazwa kwamba Wagalatia walikuwa wameiacha haraka namna hiyo Injili ambayo walikuwa wameiamini na kuipokea, na kufuata mafundisho mengine ambayo yalikuwa mageni kabisa na yaliyokuwa kinyume na kweli. Leo, pia tunaweza kushangazwa na jinsi watu wa Mungu wanavyopokea mambo haraka na kirahisi rahisi, ambayo hayajafundishwa katika Biblia. Hatuchunguzi biblia kuona kama mambo hayo yako hivyo.

Hakuna kitu kipya chini ya jua. Kama ilivyo katika nyakati za Agano Jipya, ndivyo ilivyo leo kuna upinzani kati ya ukweli wa Injili na mafundisho ambayo yanataka kututia katika kongwa la mawazo ya Agano la kale ambayo yamemalizwa katika Kristo. Mafundisho haya si sehemu ya Agano jipya na wala hayamo kabisa. Watu hutumia maandiko, hasa kutoka Agano la kale, na kuanza kuyajengea hoja. Mafundisho haya hutuibia kweli, kama ilivyo katika Kristo Yesu na uhuru tulio nao katika yeye (Gal.3:1, 5:1). Wanataka waturudishe katika mawazo ya Agano la kale ambayo yameondolewa katika Kristo na mafanikio aliyoyapata Kalvari. Katika moyo wake na mwisho wake, mafundisho haya yote huwakilisha mashambulizi juu ya kweli ya Injili ya Kristo naye amesulibiwa. Huvuruga kweli ya Injili na kutupofusha tusiweze kuiona nguvu ya kweli na utoshelevu wote wa mahubiri ya msalaba. Wanaoyainua sana mawazo hayo hawana habari kama wanapingana na kweli, lakini bado mafundisho hayo si sahihi na ya hatari. Paulo alipigana kwa nguvu kuwafungua watu wa Mungu toka uongo kama huo na kuonyesha kuwa waalimu kama hao walisumbua kanisa na watabeba hukumu kwa kufanya hivyo. (Galatia: 1:8,9; 5:10-12).

Sasa tufikirie juu ya wazo hili ambalo limesifika sana siku hizi kwamba tunapashwa kutubu juu ya dhambi za nchi ambayo tunaishi ndani yake. Kufuatana na fundisho hilo, Mungu huumizwa kwa sababu ya uovu katika nchi “yetu”, na uovu unamzuia Mungu asibariki nchi na watu wake kama ambavyo angependa. Na pia nchi inakuwa chini ya laana au hukumu. Kwa sababu hiyo tunapashwa kuungama na kutubu kwa sababu ya maovu katika nchi yetu na kwa sababu ya dhambi ambazo watu wanazifanya, ili kwamba Mungu asamehe uovu huu na kutuma baraka zake – inabidi tupokee upatanisho kwa ajili ya nchi yetu na watu wake. Wanaendelea kufundisha kwamba ni lazima pia kutubu kwa ajili ya dhambi zilizofanywa na vizazi vilivyopita katika nchi yetu – dhambi za kitaifa kabla Mungu hajaleta baraka kweli kweli au kuleta uamsho. Katika insha hii ninajaribu kusema juu ya mafundisho haya. Lakini kadri mafundisho haya yanavyoendelea kuzunguka ulimwenguni, dondoo zingine zinaimalishwa zaidi au kusisitizwa zaidi kuliko nyingine, na yale ambayo watu huamini yanaweza kutofautiana kwa namna fulani. Kwa hiyo katika insha hii si kwamba namjibu mwandishi mmoja tu bali jibu langu ni kwa mawazo mbalimbali ambayo yameendelea na kupata sifa kati ya mengi ulimwenguni. Kwangu binafsi, ninaamini kuwa mtu anaweza kwa haraka haraka na kirahisi kuonyesha kwamba mawazo haya yako kinyume na maandiko, lakini kwa sababu watu wengine wameshawishika kwa kina sana kwa mafundisho haya mbalimbali, nimegusia karibu kila vifungu, kama si vyote ambavyo hutumiwa katika jaribio la kuunga mkono mawazo yao, ili mtu asije akadhani kuwa mafundisho haya yana maana yoyote ya kibiblia.

Sasa, watu wanaofundisha vitu hivi hawavileti vitu hivi kama mawazo yao au tafsiri zao lakini husema kwamba vimefundishwa katika maandiko kwamba tunapaswa kuvifanya vitu hivi. Hili ni jambo la kutisha. Ni mamlaka gani waliyonayo ya kuwabebesha wakristo mzigo huo? Tutaona kwamba hawana mamlaka yoyote kufundisha vitu hivi. Ni utunzi wao mpya kabisa. Ni udanganyifu unaotuondoa kutoka kwenye kweli na nguvu ya msabala. Haimtukuzi Kristo na kazi yake ya Kalvari lakini matokeo yake ni kuzitukuza baadhi ya sehemu za sheria na kwa njia hiyo kuwaleta watu wa Mungu kwenye udanganyifu na kongwa. Haifundishwi hasa hata katika Agano la kale, ingawa hapa ndipo wanapo kimbilia ili kuhalalisha mafundisho haya. Wanatafuta tukubaliane na taswira za baadhi ya watu na Agano la kale kama Eliya, Yeremia, Yona au Daniel (ingawa kuna vitu tunavyoweza kuvisifia juu yao), badala ya kutuletea mfano wa ufunuo wa Yesu Kristo, ambaye yu juu ya hao wote, katika asili yake ya uungu na pia huduma yake. Mafundisho haya yanataka kuturudisha katika namna ya Agano la kale ya kufikiri juu ya laana na hukumu juu ya mataifa, badala ya kutambua, kukiri na kuutangaza kutolewa kwa msamaha katika siku hizi za neema. Lakini zaidi ya haya, wanaishia katika kuwatumbukiza watu katika mawazo na maombi ya kishirikina, kwa kulielewa vibaya hata Agano la kale. Hii haina maana kwamba tusiombe juu ya baadhi ya hali za kijamii ambazo zina athiri saana jamii zetu au uenezaji wa Injili. Tutagusa juu ya jambo hili baadaye, lakini mawazo haya ya kisasa yanaenezwa zaidi ya haya.

Swala ni rahisi tu, ni hili, kama vitu hivi vinahitajika na watu wa Mungu, yaani kuungama au kutubu dhambi ambazo hutokea katika nchi yao, mji au sehemu, ili kwamba hukumu ya Mungu au laana juu ya nchi iondolewe na baraka kuja, sasa kwa nini jambo hili halifundishwi kaatika Agano Jipya? Kwa nini hakuna hata aya moja ambayo inafundisha au kuelekeza tufanye jambo hili? Hata haikutajwa wala kuashiriwa. Kumbuka, wanataka kutuambia kwamba baraka za kweli au uamsho katika nchi yetu huzuiliwa kama hatuungami na kutubu kwa ajili ya dhambi za vizazi vya sasa na vilivyopita! Ni kwa vipi jambo la maana kama hili kwa ajili ya maendeleo na kuenea kwa Injili lisiwepo kabisa katika mafundisho ya Agano Jipya? Hakuna kabisa katika Agano Jipya kitu ambacho kingetuongoza ingalau kufikiria vitu kama hivyo. Tutaona pia jinsi ambavyo walimu hawa hulitafsiri visivyo Agano la kale katika jaribio lao la kuhalalisha mafundisho haya.

Mitume Hawakutumia Mtazamo Huu

Fikiria matendo ya mitume. Ni wapi mtazamo huu ulikuwa mkakati wa mitume, wakifikiri au kufundisha wasafiripo kuizunguka dunia wakihubiri Injili? Ni wapi wanawaelekeza wakristo au watu wengine wowote watubu dhambi za nchi zao, mkoa au mji ili baraka za Mungu zije. Tunasoma wapi kuwa wao wenyewe walifanya kitu kama hiki? Lakini haya ndiyo tunaletewa katika mafundisho haya – kwamba wakristo waungame na kutubu kwa ajili ya dhambi za ulimwengu, yaani kwa dhambi za wasioamini katika maeneo yao, ikiwa ni pamoja na vizazi vilivyopita. Hakuna mahali popote katika matendo ya mitume jambo hili linaonekana. Mitume na wengineo husafiri kama Mungu anavyowaongoza; kuhubiri Habari Njema kwa watu kwamba wamesamehewa bure kwa dhambi zao zote kupitia kifo na kufufuka kwa Yesu Kristo; watu huokolewa na makanisa kuanzishwa na wakristo hupokea mafundisho. Lakini hakuna kuungama au kutubu kwa ajili ya dhambi za nchi yoyote au eneo na wakristo (au mtu awaye yote!) kabla ya kuipeleka Injili mahali pale kwa uwezo – bila shaka Mungu alibariki kazi na kuongeza watu wengi katika Kanisa pasipo mafundisho haya – wala hapakuwa na mafundisho kama haya yakitolewa na mitume kwa wakristo wafanye hivyo baada ya makanisa kuanzishwa ili kazi ya Mungu kati yao istawi na kuenea. Ilienea na kukua kwa ajabu na kulikuwa na uamsho, pasipo watu wa Mungu kujiweka katika nafasi ya wasioamini kati yao na kutubu dhambi zao. Pia ilienea kuwa ajabu kwa neema ya Mungu pasipo wenye dhambi kuambiwa watubu juu ya dhambi (zilizopita au za wakati huo) za miji yao mikuu au nchi zao, kabla ya Mungu kuwabariki kweli kweli na kutenda kazi kati yao kwa nguvu! Mahali popote, mtu yeyote aliambiwa atubu kwa ajili ya dhambi zake! Jambo hili kwa kweli ndilo fundisho na pia mfano tunaoukuta katika Biblia yote, kama ambavyo tutaona.

Vivyo hivyo, kumekuwa na uamsho mara kadha ulimwenguni kote na Injili imeenea na kuwa na mizizi tangu nyakati za mitume hata leo pasipo watu wa Mungu kufanya vitu hivi, kujua au kufundisha. Kwa hiyo nani anaweza kutuambia kwa nini mafundisho haya yameonekana mara kuwa ya lazima kwa kanisa na kwa mafanikio na kuenea kwa Injili katika siku hizi?

Mitume Hawakufundisha Juu ya Mtazamo Huu

Mafundisho haya huwezi kuyakuta mahali popote katika maandiko ya mitume katika Agano Jipya. Kitu kama hicho hakitajwi hata kidogo. Je tunaweza kusema basi kuwa palikuwa na dhambi pungufu, uchawi na kuabudu sanamu kupungufu katika nyakati za Agano Jipya kuliko zilizopo sasa na kwamba kwa hiyo wakristo wa nyakati hizo hawa kuhitaji mafundisho haya kama tunavyohitaji leo. Hii ni wazi si kweli. Na simjui mtu yeyote ambaye anayesema jambo hili. Maandiko ya Agano Jipya pamoja na kumbukumbu za kihistoria zinahakiki wazi na kwa msisitizo kwamba kulikuwa na ufisadi mkuu na dhambi za kutisha, uchawi, kuabudu sanamu na ugandamizaji katika nyakati za Agano Jipya. Kwa mfano, Mdo 8:9-11; 13:6-8; 17:16; 19: 18,19,23-28. Tunafahamu pia toka kumbukumbu za kihistoria kwamba jiji la korintho lilikuwa ni mahali pa uzinzi mwingi na hii inaweza kusaidia kutoa maelezo kwa nini kanisa la Korintho lilihitaji mafundisho maalum na kukemea kwa mtume Paulo. Vita vingi vilikuwa vimetokea katika eneo hili la ulimwengu na dhuruma nyingi zilikuwa zimetokea. Kidokezo hiki ni kikubwa kwamba hakihitaji ufafanuzi zaidi.

Kwa hiyo kwa nini mitume hawa hawawaambii wakristo watubu kwa ajili ya dhambi ambazo nchi zao na maeneo yao yalikuwa yametenda katika kizazi hicho ama vilivyopita? Je nchi zilikuwa hazijatenda uonevu wowote au ugandamizaji? Bila shaka zilikuwa zimetenda lakini hakuna mahali popote mitume waliwaelekeza watu wa Bwana waombe au watubu kwa sababu ya dhambi za Athene au kwa sababu ya uchawi na uabdu sanamu wa Efeso au kwa sababu ya uzinzi wa jiji la Korintho, au kwa sababu ya ugandamizaji wa Rumi juu ya nchi zingine hasa Yudea. Hakuna mahali ambapo tutaona wakitia mkazo au kuwashinikiza wakiristo waungame na kutubu kwa ajili ya dhambi za kitaifa au za vizazi vilivyopita. Hawawaambii wayahudi kwamba lazima waungame na kutubu kwa ajili ya dhambi za mababa zao katika mwili; wala hawawaambii waamini wa Kirumi, Kigiriki au Waarabu au wakristo wa nchi nyingine yeyote au eneo lolote watubu kwa ajili ya dhambi za zamani za nchi zao. Hakika wakristo mjini Rumi walikuwa na sababu lukuki za kuungama dhambi za himaya ya Kirumi kama mafundisho haya yangekuwa kweli! Lakini hawapewi maelezo kufanya hivyo. Hakuna aya hata moja, mkazo hata mmoja kwa wakristo wafanye hivyo mahali popote katika Agano Jipya. Kulikuwa na dhambi nyingi mno, kuabudu sanamu, uchawi na ugandamizaji katika siku zao na katika vizazi vilivyopita, kiasi kwamba mitume walikuwa na kila sababu na fursa ya kutosha kuwakazia wakristo waungame au kutubu kwa ajili ya dhambi za wale waliokuwa wamewazunguka – lakini kamwe hawakufanya namna hiyo. Kwa hiyo tena tunaachiwa swali: kama kutubu kwa ajili ya dhambi za wasioamini katika maeneo yetu au nchi ilikuwa lazima kwa ajili ya “upatanisho” wa nchi na kwa ajili ya kuenea ufalme wa Mungu kwa nini mitume hawatuelekezi kufanya hivyo? Je wamepuuza kutufundisha kitu ambacho kanisa linahitaji kujua ili Injili isitawi na kuenea? Je walikuwa wajinga wasioweza kujua mafundisho muhimu kama hayo, kama ni mafundisho muhimu kweli? Kama kanisa limejengwa juu ya msingi wa Kristo, mitume na manabii, Je waalimu hawa wa kisasa wanajua zaidi ya wao? Bila shaka wasingesema hivyo na wasingetaka kuwa hivyo, lakini naweka swali hili ili kuonyesha wazi upotofu mkuu wa mafundisho haya na hatari ambayo waalimu hawa wanajiingiza ndani yake. Hawajengi juu ya Kristo. Wanajenga juu ya tafsiri zao juu ya Agano la kale. Wanabadilisha imani katika kristo na dini ya ushirikina!

Yesu Hakufundisha Mtazamo Huu

 

Yesu mwana wa Mungu hakuwaelekeza wafuasi wake wafanye hivyo mahali popote katika Injili hata katika ufunuo. Yesu alikuja akihubiri habari njema za ufalme wa Mungu kwa watu na kuwaambia watubu – na si kuwaambia watubu kwa niaba ya wengine! Wala hakuwaambia waungame au kutubu kwa ajili ya dhambi za vizazi vilivyopita kama kwamba hivyo ilikuwa lazima kwa ajili yao wapokee msamaha kamili na baraka toka kwa Mungu. Hasha. Na tuelewe kuwa kwa ajili ya Kalvari, mtu yeyote atubuye dhambi zake, hugeuka kumwelekea Bwana na hufanyika mwana wa Mungu, dhambi zilizopita za mababa zake au za taifa haziwezi kuweka mpaka au kuzuilia baraka kamili za Mungu katika Kristo Yesu kwa mtu huyo. Kalvari ni kukatwa kikamilifu toka dhambi, hukumu, toka kuhukumiwa moyoni na toka Adamu wa kale, hii ni pamoja na maisha yetu ya nyuma na mababu zetu nyuma. Mungu Asifiwe! Watu wa Mungu hawako kwenye kongwa lolote kwa ajili ya dhambi za mababu kama wako katika kristo! Hakuna kitu kama hiki kimafundisho ya Yesu au mitume. Angalia 2 Kor 5:17. Mawazo haya hayako ama sawasawa na maneno au Roho wa Kristo. Neno la Mungu huja kwa watu wenyewe, moja kwa moja kuwashawishi juu ya dhambi zao na kuwaongoza katika toba. Marko 1:14,15; 2:17 (Anawataka wenye dhambi watubu, wala si watakatifu watubu kwa dhambi za wenye dhambi!).

Neno la Mungu sasa linakuja kwa mtu binafsi na mmoja mmoja kwa kila mtu likiwatia hatiani kwa dhambi zao wenyewe: Luka 13:1-5; Mdo 2:38, 3:19; 8:22; 17:30; 26:20. Ni kwa njia gani wake kwa waume husikia kuhukumiwa kwa ajili ya dhambi zao kutubu na kumgeukia Mungu kwa imani na kupokea msamaha wa dhambi? Ni kwa njia gani baraka hii na neema ya Mungu inaloijia mioyo yao! Huja kwa kusikia neno la Mungu linalokuja mioyoni mwao wenyewe! Rumi10:10–17. Ndiyo, Yesu huwaambia wanafunzi wake waombe – lakini si kwa ajili ya dhambi za wenye dhambi katika miji mikuu, lakini badala yake waombe Bwana wa Mavuno atume watenda kazi (kuhubiri juu ya ufalme wa Mungu ili wenye dhambi wenyewe wasikie neno la Mungu na kwa njia hiyo kuamini na kutubu). Pia anawafundisha waombe ufalme wa Mungu uje na kwa mapenzi yake yatimizwe hapa duniani kama huko mbinguni, na ili kwamba tusamehewe kama tunavyowasamehe wengine. Lakini hakuna mahali popote katika Agano Jipya na hakuna mahali popote katika Biblia tunapoambiwa kutubu kwa niaba ya wenye dhambi, au kuungama dhambi zao ili kufanya upatanisho au mapatano kwa ajili yao kitendo ambacho kitamfanya Mungu awabariki! Yesu anaweza kutambua hukumu juu ya Kapernaumu na anaweza kulia juu ya Yerusalemu kwa sababu walifanya mioyo yao migumu kwa neno la Mungu na hawakutubu, lakini hawaombi wafuasi wake waungame na kutubu kwa dhambi za watu hao. (Bila shaka mifano hii inahusiana na Israeli kuikosa au kuikataa fursa ya kumpokea masihi wao).

Pia ona kwamba katika Uf.2:8-11, Bwana hakulitaka kanisa katika jiji la Smirma liombe na kutubu kwa ajili ya maovu yaliyokuwa yakitendwa na baadhi ya watu wa Smirna ambao ni wa Sinagogi la shetani, ili kwamba msamaha wa Mungu na baraka zake zije kwenye eneo: nasema tena, hakuna mahali popote katika biblia watu wa Mungu wametakiwa kufanya hivyo.

Lakini watu wengine huenda hata mbali zaidi katika kufundisha kwao, kwa kuwaambia watu wa Mungu kwamba watubu kwa ajili ya dhambi za mji au nchi, kama uchawi, uzinzi na ulevi na kuungama kwamba wao watu wa Mungu wanahusishwa katika dhambi hizi na wamemtenda Mungu dhambi! Watakatifu huambiwa wahusike na dhambi za wasio amini kama kwamba dhambi hizo ni zao! Huambiwa basi watumie damu ya Yesu katika hali hiyo ili kuleta upatanisho na kuomba msamaha wa Mungu! Lakini damu ya Yesu hutumika kwa moyo uaminio. Huwezi kuitumia damu ya Yesu kupitia maombi kwa mwenye dhambi asiyetubu! Huu ni  kama uchawi katika ukamili wake ambao hutafuta kuchukua nafasi ya kristo ambaye ndiye mpatanishi pekee kati ya Mungu na Mwanadamu. Yesu katika jumuisho na hitimisho amejihusisha na dhambi za ulimwengu wote pale Kalvari, kwa njia ambayo ameleta msamaha kwa wote wanaoamini Injili. Usitafute kuongeza katika kazi ya Mungu katika Kristo.

Bila shaka wanaamini kuwa wanafuata mifano ya Agano la kale (na tutaona hayo baadaye kwa kirefu) lakini tayari tumekwisha kuona wazi kwamba hakuna wazo kama hilo katika Agano Jipya (na hata katika Agano la kale kama tutakavyo ona pia). Hakika sasa tunaweza kulia pamoja na Paulo na kusema,

“Enyi wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu yakuwa amesulubiwa?”

Na isitoshe, mafundisho haya yanafanana na ulozi, mwishowe watu huamini mambo ambyo, sio tu yako kinyume na maandiko, bali pia kinyume na kufikiri ipasavyo.

Wanao ushawishi wa kiuchawi juu ya watu wa Mungu wanaoyafuata mafundisho haya pasipo kuhakikisha kwenye Biblia. Mafundisho haya yanaonyesha yanakubalika kwa watu wengi kwa sababu walimu wao hutumia maandiko yaliyochaguliwa kwa uangalifu sana (lakini kama walivyofanya kati ya makanisa ya Galatia, hasa kutoka katika agano la kale) ambayo pengine huonyesha tarajio la ukweli ambalo linalingana na la wakati ule; lakini hapo huongezea mawazo yao katika hilo. Na hii ndiyo hatari na hila ya makosa ya aina hii, huku inatajwa kwamba wanatumia maandiko, lakini hapo hapo wakiyakataa maandiko mengine – hivyo hujitokeza ukweli – lakini wanatafsiri vibaya mistari hiyo ya neno la Mungu, wakiweka maana yao wao wenyewe juu yake na ndipo huishia kupata kitu fulani ambacho kwa uhakika ni mbali na ukweli na hata huwa kinyume cha ukweli. Kwa kukataa ushuhuda wote na maandiko, wakijenga mtindo wao wa mafundisho, ingawa huwa hawanzii na Biblia hata kidogo. Wanadai kuwa wanao ufunuo maalum au huduma – hata mitume kutoka kwa Mungu. Wanaanza na mawazo ya aina fulani yaliyo ya kwao ambayo wao hufikiri labda yanaweza kufanya kazi na pia ni ya kibiblia na baada ya hapo, wanajaribu kuyatafutia mistari ya neno la Mungu, mstari wowote ambao unaweza kuonyesha kuunga mkono mafundisho yao. Na wanapogundua kuwa kumbe biblia haiwaungi mkono kwa dhahiri, wanaanza kujisomea maana zao wenyewe katika mistari hiyo waliyoichagua. Na wengi wamedanganyika kwa njia hii, kwa sababu hawayachunguzi maandiko, wamesahau ile thamani ya usafi na wepesi wa Injili ulivyotolewa kwao toka mwanzo.

Agano la Kale – Kwa Ujumla

Sasa, hebu tufikirie juu ya maandiko ya Agano la Kale, ambayo kwa hakika ni neno la Mungu lenye uvuvio kwetu. Ndani yake tunagundua mambo ya utendaji wa Mungu kwa wanadamu na hasa kwa watu wake aliowachagua, Israel, na maagano aliyoyaanzisha pamoja nao. Zaidi ya yote anatupatia picha ya mambo yanayokwenda kutokea hapo baadae na kutupatia mfano wa ufufuo wa wokovu ambao Mungu anakwenda kuuleta kwa wanadamu kupitia Yesu Kristo.

Ingawaje maandiko ya Agano la Kale yana mifano mingi inayomwonyesha Yesu katika namna yake na wokovu atakao uleta – matarajio ya mwenendo wa maisha ya Yusufu yanamdhihirisha Yesu k.m.f. Musa akiongoza wana wa Israel kupitia bahari ya Shamu ni picha ya ubatizo wetu katika Kristo. Lakini ili alisimamishe Agano Jipya na kuwaingiza waume na wake ndani ya ufalme wa kiroho wa Mungu, kwa hakika Mungu alipaswa kumleta Kristo mwenyewe na kumtuma afe katika msalaba. Kabla Kristo hajaziondoa dhambi za ulimwengu pale Kalvari (Yoh. 1:20), Mungu asingeleta au kuzaa chochote katika maisha ya ndani ya kiroho na uweza wa maisha yake yeye mwenyewe na ufalme. Agano la Kale linatupatia picha ya nje ya yale ambayo Mungu alipenda kutufanyia kiroho. Kwa kweli kifo cha Yesu pale Kalvari, kilikuwa ni kielelezo muhimu cha tukio la kihistoria ikiwa sio la umilele. Kifo chake kilibadilisha mambo kwa njia ya msingi kabisa. Alilia, “Imekwisha!”, na papo hapo pazia la hekalu likapasuka vipande viwili. Hii inaonyesha kuwa, watu kwa imani kupitia Kristo, sasa wangeweza kuingia patakatifu pa patakatifu kwa damu ya Yesu; katika roho; pasipo matendo ya sheria tena. Sheria ilitolewa na Musa, lakini neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. Mungu habadiliki. Hata kidogo! Rehema zake kwa ajabu kabisa zinaonyeshwa kwa matendo yake na watu katika Agano la kale. Halikadhalika, haki yake na hukumu. Lakini sasa kwa sababu ya kifo cha Yesu pale Kalvari, uhusiano wa Mungu na wanadamu umepitia katika msingi wa mabadiliko makubwa. Yesu alikuwa ni mwanakondoo wa Mungu azichukuaye dhambi za ulimwengu, aliihukumu dhambi katika mwili wake hivyo kuivunja nguvu yake ndani ya maisha ya watu, alizichukua hukumu za dhambi za wanadamu, kwa hiyo akatupatia msamaha bure, akatupatia uzima, uzima wa milele kwa roho na haki yake (Rumi 8:1-4). Kwa ajili ya msalaba Mungu ameweza kufanya yale ambayo sheria isingeweza kufanya, na amewapa wale wanaoamini katika Kristo haki ya kufanywa kuwa wana wa Mungu na kuingia katika uwepo wake.

Kwa hiyo kati ya mambo mengine, mawili ya msingi na muhimu yamebadilika. Kile ambacho Mungu amekifanya kwa ajili yetu, ni kile ambacho Mungu amekifanya ndani yetu. Katika hii ya mwanzo, watu sasa wanashiriki haki ya Mungu kwa imani, kwa sababu ya utajiri wa neema yake na sio kwa kazi zipatikanazo kwa sheria, na hii inatupatia sisi haki ya kufanyika kuwa wana wa Mungu.

Na kwa sababu Mungu amekwisha kutuondolea vyote viwili, dhambi na uadui wa sheria (Efeso 2:15; Kol. 2:14), sasa kunakuwa na muungano wa kweli kiroho kati ya Mungu na wanadamu. Hutufanya sisi tuwe watoto wake kwa kutupatia roho wa mwana wake Yesu Kristo akaaye ndani yetu. Kutokana na hali hiyo basi, sasa maisha yetu yanaonyesha tabia yake kwa njia ambayo haikuwezekana katika Agano la Kale (2 Petro 1:3-4). Kwa hiyo, iwapo tutarudia ili kuzitunza baadhi ya sehemu ya sheria kama walivyofanya kule Galatia, hivyo basi, tutakuwa tunaikataa imani yetu katika Kristo na wokovu wake aliotununulia, au kama tutakuwa tunarudi kuzifuata njia za tabia za kale, ndipo basi tutakuwa tunakataa ufunuo wa tabia yake ndani ya mioyo yetu.

Kwa mfano, katika Agano la Kale watoto wa kiume walilazimika kutahiriwa, kama ni sehemu ya agano kati ya Mungu na watu wake. Hii ni aina au picha ya ndani ya kazi za kiroho ambazo Kristo alizikamilisha kwa wale ambao wanamwamini yeye, (Kol. 2:11). Lakini yeye ni utoshelevu wa kweli ambao kutahiriwa kwa nje katika agano la kale ilikuwa inaelezea (Heb.10:1). Kwa hiyo, mtu yeyote kwa sasa, iwapo anaamini kuwa pamoja na kuamini katika Kristo, ni lazima pia kwa nje utahiriwe ili kuokoka, basi mtu wa jinsi hiyo atakuwa anaiondoa imani yake na wokovu aliopewa (Gal. 5:3-6).

Ni ujinga ulioje jamani kuacha kitu muhimu na kubakia na kivuli chake! (Heb.10:1). Je, unaweza kula kivuli cha tunda la ndizi? Kivuli kinaweza kukushibisha njaa yako na kukuacha hai? Ebu – jaribu kula kivuli kwa kadiri uwezavyo. Lakini utaishia na vumbi mdomoni mwako! Na jambo hili linafanana na mafundisho ya aina hiyo yanavyofanya. Wanayaacha ya kiroho na kung’ang’ania ya kimwili, ya mbinguni na wanang’ang’ania ya duniani, ingawaje mtu anaamini kuwa Yesu ni mwana wa Mungu na kwamba anao msamaha kupitia damu yake; ingawa anaamini mambo mengineyo mengi yaliyo ya kweli, bado mtu huyo, ikiwa anatafuta kuongezea chochote kwa yale Kristo aliyoyafanya, iwapo anatafuta kuturudisha nyuma kwenye vitu ambavyo kwa kweli Kristo alikuja kuviondosha au kutimiliza, hapo basi mtu huyo anasababisha kuukataa wokovu wa Kristo. Kristo, na imani katika Kristo havina faida yoyote kwake mtu huyo na hivyo imani ya mtu huyo ni bure. (Gal.4:19,20; 5:3,4). Hata kama anajifikiria kuwa anamfuata Kristo, amejidanganya, (Gal. 3:1). Mtu wa jinsi hiyo kwa jumla, anachanganya agano la kale na jipya, wanachanganya yale ya ndani na ya nje; kivuli na kitu halisi, ya mwilini na ya rohoni ya duniani na ya mbinguni. Inafanana pia kama Mkristo anafikiri ni lazima kutunza sherehe za Agano la kale. Anaikataa Imani!

Kwa mtazamo wa yote ambayo Mungu ameyafanya kwa ajili yetu kwa Kristo Yesu, haikushangaza kuona Mtume Paulo akihuzunishwa kutoka ndani ya moyo wake, akijitahidi kadiri alivyoweza kwa maombi na maelekezo ili kuwakomboa Wagalatia kutokana na ujinga wao wa madanganyo.

Je, unapaka damu leo katika miimo ya milango yako ili kuzuia hukumu ya Mungu? Unaleta ng’ombe au mbuzi au kondoo pamoja nawe kanisani ili kumtolea Mungu kama dhabihu ya dhambi zako? Haya, pengine labda unatabasam, kama mwitikio kwa maswali haya! Lakini makosa ya jinsi hiyo hiyo yanafundishwa na kujitokeza siku za leo; watu wanatafuta kuturudisha nyuma kwenye fikra, na matendo ya agano la kale. Na wengi wa watu wa Mungu wanapokea na kuyafuata mafundisho hayo. Sasa, mafundisho tunayoyaona ndani ya makala hii yanahusiana na aina hii ya makosa.

Niliyoyaelezea hapo juu ni mambo ya msingi ambayo Mungu amefanya kwa ajili yetu katika Kristo – ambaye ndiyo njia ya wokovu wetu. Sasa vipi kuhusu huduma na tabia ya Wakristo – Mungu anafanya nini ndani yetu na kupitia kwetu. Je, mambo yanaendelea katika Agano jipya kama ilivyokuwa katika agano la kale? Kwa kiasi tu. Lakini lazima tukiri juu ya mzizi wa mabadiliko ya msingi kwa sababu ya Kristo na yale aliyoyafanya. Hebu fikiria Matayo 5: n.k. Sasa je, utambomoa mwenzako jino lake, kwa sababu eti yeye amelibomoa lako? Je, utawachinja watu wasioamini kwa upanga? Kanisa lako litampiga kwa mawe yeyote ambaye amefumaniwa katika uzinzi? Au utamwita Mungu atume moto toka mbinguni uwajilie hao wanaompinga Mungu? Haya yote yaliruhusiwa na kutakiwa ndani ya agano la kale. Lakini kwa sasa hatuwezi; hatuwezi kuthubutu kufanya lolote kati ya hayo. Kwa sababu sisi tumezaliwa upya kwa roho wa Mungu na wala hakuna kati ya hayo yanayofanana na tabia yake Yesu ndani yetu.

Tunaweza kufikiri kwamba, haya yote ni rahisi na yaliyowazi kabisa, lakini ebu umchukulie Yakobo na Yohana ambao kwa uwazi kabisa walipenda harufu ya uweza wa kuwa na Yesu aliowapa. Hata hivyo walimwomba iwapo, angeweza kuita ili kushusha moto chini, juu ya wasamaria kwa sababu wamekataa kumpokea Yesu. Aliwakemea mara moja, na akawaambia, hawajui ni roho ya aina gani walinayo. Wao hawakuelewa yote mawili, kati ya tabia na huduma ya mwana wa Mungu.

Na mpaka pale tu tutakapokuwa tunatembea katika Roho ya Kristo kufuatana na neno lake, bado tutakuwa tu tukifanya makosa hayo hayo. Na hivyo ndivyo ilivyo leo watu hawaelewi tabia ya Kristo na wokovu wake kadhalika na huduma ya kanisa. Kutokana na uchaguzi wao kutafuta tabia ya ubinafsi wa madaraka, baadhi ya walimu wao wamechagua maandiko kutoka katika Agano la Kale kwa kadiri yanavyowafaa wao na vile wanavyotaka kuamini. Wanaumba mfano wa Mungu unaochipua toka katika fikra zao, ambazo huzichochea baadhi ya nyaraka za Agano la Kale. Huu ni sawasawa na kuabudu sanamu na hunyan’ganya mfano halisi wa Mungu kama ulivyofunuliwa kwetu na katika Kristo.

Kwa hiyo, hii inatokana na watu hawa ambao huja mjini, na badala ya kuhubiri Injili na utajiri usiochunguzika wa Yesu Kristo, wanawaambia watu kwamba eti laana na hukumu za Mungu ni juu yao na miji yao na kwamba sasa wanatakiwa kutubu kwa niaba ya dhambi za (wengine katika) miji hiyo au taifa hilo; ili kwamba Mungu aweze kughairi na kuindoa hukumu yake na badala yake atume baraka (watu wengine karibu wapumue moto na hukumu kama Yakobo na Yohana walivyotaka kufanya). Tunawezaje kujua kuwa tumekwisha kuomba kwa ajili ya dhambi zote zinazotakiwa kuungamwa? Lakini jee, watu wataendelea kutubu kwa jinsi hiyo hadi lini? Nani atakaye waambia kwamba hukumu na laana hiyo sasa imeondolewa kwa toba ya jinsi hiyo? Wahubiri hawa hawaonyeshi kabisa kuwaambia watu bali wanawataka tu wakristo waaendelee kutubu na kutubu na kutubu kwa ajili ya mambo ya aina zote ambayo hao wahubiri na wapelelezi wao pamoja na waombezi wao huendelea wakitafuta makosa katika taifa!

Kwa kawaida, wanafurahishwa sana na ushahidi wowote ule juu ya mambo yahusuyo siri za ulozi au uchawi katika nchi hiyo. Na kisha hutangaza waliyoyagundua ndani ya makala zao na barua za maombi kwa maelezo makubwa. Wanazingatia sana katika mambo ya aina hiyo na huzijaza akili za watu wa Mungu kwa masomo yasiyofaa ambayo huelekea kwenye kutukuza kazi za shetani, badala ya kuiendeleza Injili ya Bwana Yesu au kuleta baraka. Hayo ni madhara makubwa yanayowaingiza watu katika ujinga wa kutomjua Kristo na wokovu wake wa tabia na huduma yake.

Tafadhali usielewe vibaya, hapa sisemi kuwa hatuwezi kuomba kuhusu mambo yatokezayo katika miji au nchi zetu bali ninachosema ni kwamba tusifanye mambo ambayo hayamo katika maandiko ya neno la Mungu; na tusiwe na mawazo ya ushirikina ambayo kwa hayo watu wengine huyachanganya na Injili ya kweli hata kuwatumbukiza watu katika vifungo na giza kwa mafundisho yao hayo. Katika siku hizi, kwa hakika tunaweza kuumizwa kwa yale yanayotutokea pia yanayotokea katika kanisa, na tungependa kunyenyekea mbele za Mungu na kuomba kuwa anaweza kugeuza mioyo ili imgeukie na kuwaongoza watu kuelekea toba. Lakini hii inatofautiana sana na aini hii ya maombi ya Ushirikina.

Agano la Kale – Daniel

Lakini sasa, kwa kadiri tunavyo yatazama maandiko ya Agano la Kale, kwa uhakika tunagundua kwamba kumbe mafundisho ya jinsi hiyo hata hayamo humo!

Wapi katika Agano la kale ambapo Mungu au hata manabii anawainua watu wake ili kuungama na kutubu kwa ajili ya dhambi ya yeyote yule asiyeamini au taifa lolote? Au ni wapi tunaweza kuupata mfano wa jinsi hii katika Agano la Kale? Haupo wowote; haupo; haupo hata mmoja.

Daniel ambaye hunukuliwa mara nyingi, alikuwa akiishi Babel, lakini pia huko nako hatumkuti akiomba kwa ajili ya maovu ya mji ule. Hakuna popote ndani ya Agano la Kale ambapo watu wa Mungu wanatubu kwa ajili ya dhambi za wasiomini, ili kwamba laana ya Mungu ipate kuondolewa, na badala yake baraka na msamaha upate kutolewa? Kwa kweli, hakuna yeyote aliyetubu kwa ajili ya dhambi za mtu mwingine katika Biblia. Tunaona mifano ya watu wa Mungu wakiungama dhambi za vizazi vilivyowatangulia – lakini hiyo ilitokea tu wakati ule Waisraeli walipopelekwa uhamishoni na jambo hilo lilifanyika kwa niaba ya watu wa Mungu, na kamwe sio kwa ajili ya wasioamini.

Je, Mungu amewatoa watu wengine au mataifa mengine kutoka katika baraka zake? Hapana, ndani ya Agano la Kale tunayakuta yaleyale kama yalivyo katika agano jipya. Mungu hulituma neno lake kwa watu wenyewe na huwainua ili kutubu juu ya dhambi zao wao wenyewe. Wao wenyewe binafsi ndio wanaopaswa kutubu dhambi zao, ndipo Mungu hujionyesha yeye mwenyewe kuwa yeye ni Mungu mwenye Neema isiyo na ukomo na fadhili zake na baraka zake hufuatia mara moja! Lakini ikiwa ni watu wenye kujaa majivuno na kufanya uovu ndipo hujulikana kuwa hukumu inawangojea watu hao. Au ni kwa kupitia imani, ushuhuda, upendo na utiifu wa watu wa Mungu katika Agano la Kale, ndipo watu huona kuwa jina la Bwana linatukuzwa katikati ya mataifa na hivyo ndipo wengine hujiunga wenyewe pamoja na watu wa Mungu, au huja kumwamini. Lakini wazo ya kwamba eti watu wa Mungu wanahitajika kuungama na kutubu kwa ajili ya dhambi za mataifa yasiyoamini hivyo ndivyo iwe kama utangulizi kwa Mungu ili aweze kubariki watu hao au taifa hilo, huo ni udanganyifu na ni mambo ya kubuni ya kibinadamu na wala hayapatikani katika maagano yote mawili ya kale na jipya. Sio hivyo tu bali hata wazo la aina hii linaweza kunyang’anya wokovu wa bure alioununua Yesu Kristo pale Kalvari kwa ajili ya wanadamu. Mahala ambapo alifananishwa na dhambi zao kiasi kwamba, dhambi zao zikawekwa juu yake na akazichukua pamoja akafanywa dhambi, ili kwamba tufanywe wenye haki kwa Mungu katika yeye. (Joh. 1:29; Rum.5:8-10; 2 Wakorinto 5:19-21; 1 Joh. 2:2.). Na hii ndio sababu, katika siku hizi za Neema, Habari Njema inapaswa ihubiriwe kwa watu wote, bure. Tumeambiwa katika sura hii kwamba, tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu, na kwamba tulipokuwa bado ni maadui, tukapatanishwa na Mungu, kutokana na kifo cha mwanae. Haya ni maneno ya ajabu ya wokovu wetu wa bure, ambapo Mungu alipoanzisha hatua ya kwanza, na akazishughulikia dhambi zetu zote (wakati tulipokuwa tungali ni wenye dhambi), hata kabla hatujazijali au kuzitambua. Sasa kwa nini basi tunahimizwa kutubu kwa ajili ya dhambi hizi za watu wasioamini ambazo kwazo Kristo alishawafia? Kristo alizichukua dhambi zetu zote ili kwamba kulingana na mtazamo wa Mungu, haliwi tena ni kizuizi kwake katika kutupatia wokovu na uzima wa milele. Kwa hiyo inasemwa kwamba Mungu katika Kristo hakutuhesabia dhambi yetu! Hayo yote ni kwa sababu ya Kalvari, na sasa ni juu ya watu wenyewe kuiamini Injili na kutubu ili kwamba waweze kujua na kupokea neema hii ya ajabu ya Mungu. Mungu amekwisha kufanya kila kitu kwa upande wake – kwa jinsi ya ajabu na kwa fadhili zake; sehemu yetu sasa ni kuiamini Injili na kutubu kwa ajili ya dhambi zetu binafsi na kuutafuta msamaha wa bure katika na kupitia Kristo. Sehemu yetu sio kuzifufua dhambi za watu wengine ambazo Kristo amezifilia na tayari amekwisha kupokea upatanisho ili kusudi tuweze kutubu kwa ajili ya hizo na kupokea upatanisho tena! Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumembadilisha Kristo pamoja na kifo chake kwa maombi yetu ya kutubu kwa ajili ya Taifa!

Au, watu hawa wanatutaka tuamini kwamba Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi za ulimwengu mzima, kwa kila roho ndani yake, bali kwamba kifo chake pale Kalvari hakijatosha kiasi na kile wanachokiita “ushiriki wa dhambi kitaifa”!? Kwa maneno mengine hapo wanataka kusema – Kalvari haitoshi kiasi kwamba ni lazima tutake hii nyongeza maalum “maombi ya upatanisho” ya kanisa ili kukileta kile wanachokiita wao “suluhisho kwa taifa” ambalo Yesu hakuweza kumaliza pale msalabani! Kama hivyo ndivyo ilivyo, basi tunaona kuwa kuingiliwa kwao kwa ubunifu wao unawalazimisha zaidi kuingia ndani kabisa ya makosa na udanganyifu. Ni kama ilivyo katika kanisa la Wagalatia – hawasemi kuwa ni Yesu tu, yeye pekee kasulibiwa kwa wokovu wetu; bali wanasema, “Yesu pamoja na kutahiriwa kwa ajili ya wokovu.” Kwa hivyo mafundisho hayo yanasema, “Yesu pamoja na kushirikisha kwa maungamo na toba” ili kuleta wokovu kwa watu. Kwa hiyo wamezua wokovu katika hatua mbili – wanasema, ndiyo Kalvari kwa hakika ni lazima lakini pia unahitaji toba ya upatanisho ili kusababisha suluhu ya kitaifa na Mungu, kabla watu hawajapokea faida halisi ya Kalvari. Hili ni kosa kubwa sana.

Na iwapo bado, wanasema kwamba maungamo na toba ya dhambi za taifa ya aina hii kwa hakika hayamsababishi Mungu kusamehe taifa na dhambi zake, bali kwamba inafungua tu njia ya Injili hii ya neema ili kuwabariki watu. Bado huo nao ni udanganyifu mtupu, kwani aina hii ya maungamo na toba wala haifundishwi kabisa katika maandiko ya neno la Mungu. Inaharibu tu ukweli uweza na wepesi wa Injili ndani ya akili za watakatifu na wenye dhambi wote pia; inasababisha kuchanganyikiwa na ushirikina ndani ya nchi.

Lakini wengine wa waandishi wao wanasema kuwa maungamo ya dhambi za kitaifa, na kuomba msamaha, ina maana kwamba, shetani hawezi tena kuwashitaki watu hao na kwa hiyo hawezi kuwaweka nje ya neema ya Mungu au kuwazuia kusikiliza Injili! Kwa hakika ikiwa unaweza kusadiki hivyo, basi unaweza pia kuamini chochote kile! Ni nini? Je, shetani anayo haki ya kuiweka nchi nje ya neema ya Mungu na kuwazuia kusikiliza Injili mpaka hapo kanisa litakapoungama dhambi za taifa na kutafuta suluhisho kwa ajili ya dhambi hizo? Hili ni kosa lenye ubaya uliokithiri; hivi kweli hawa walimu hawajawahi kusikia juu ya Kalvari, na uweza wake! Kwa sababu ya Kalvari, Mungu hawahesabii watu makosa yao, bali ametia ndani yetu neno la upatanisho (2 Kor. 5:19). Amefungua mlango wazi! Yesu amefanya njia Kalvari na shetani hana haki ya kuiweka roho nje ya neema ya Mungu, isipokuwa roho hiyo yenyewe iasi neno la Mungu.

Ni wapi katika Agano jipya ambapo pameonyesha au kufundisha kwamba kanisa linahitaji kuungama dhambi za mikoa ili lipate suluhisho kwa ajili ya dhambi hizo kabla Mungu hajawabariki kwa neno la wokovu? Jambo hili linakaribia sana ya kuwa kufuru! Kwa sababu ya kifo chake Kalvari, Yesu anayo haki kuwabariki na kuwaokoa watu sawasawa na kusudi lake na kadiri ya neema yake!

Sasa tukifuatilia jambo hilo kwa undani zaidi, wanatuambia kuwa eti kwa sababu Daniel aliziungama dhambi za taifa lake (Daniel 9), kwa hiyo basi, sisi nasi tunahitaji kuungama na kutubu kwa ajili ya dhambi za taifa “letu” – hii ni kwamba kwa ajili ya taifa lile tunaloishi, na kwa mji ule unaotuhusu.

Hakuna chochote kile kinachoonyesha kwa uwazi zaidi, kwa jinsi gani watu hawa wanaofundisha hivyo hata wanavyochanganya mambo ya kimwili na ya kiroho; ulimwengu na kanisa. Namna wanavyosoma ndani ya maandiko ni mawazo yao, na wala kwa kweli; hawajali kuona kuwa Biblia inafundisha nini juu ya jambo hilo. Ndiyo, Danieli alikuwa ni Mwisrael, akiomba kwa ajili ya taifa la Israel. Lakini katika Agano la kale Israel ni watu wa Mungu, na wanawakilisha kanisa. Na Daniel alikuwa ni mtu wa Mungu alikuwa akiwaombea watu wa Mungu (kanisa). Na maombezi yake yanahusika na agano kati ya Mungu na watu wake na namna ambavyo watu wa Mungu walilivunja Agano hilo na kupoteza urithi wao. Inafanana na jinsi ambavyo watu hao wanavyonukuu mistari ya Biblia kama ile Ezekiel 22:30, na wanatuambia kwamba, hii sasa inahusisha huduma ya kanisa katika kuomba kwa ajili ya dhambi za nchi tunamoishi. Lakini tena mstari huo huo wa Biblia unamweleza Mungu, akitafuta mtu kati ya watu wake aombaye, ameumizwa kwa ajili ya hali ya watu wa Mungu (kanisa) na yeye ambaye anajali vyakutosha kuhusu heshima na utukufu wa Mungu ili aweze kuomba mbele za Mungu kutokana na hali mbaya ya watu wake Mungu ambao kwao aliwatengenezea agano (mapatano).

Lakini, ili waweze kuyahalalisha mafundisho yao, watu hao wanaitumia vibaya mistari hiyo ya Biblia, wakiyabadilisha maombi yao kutoka kanisa (ambalo ni watu wa Mungu waliokombolewa kwa agano na yeye) kwa ulimwengu, kama vile hivyo ndivyo ilivyo au ingeweza kuwa sasa!

Ingawaje tunaweza au kutakiwa kuomba kwa ajili ya jamii tunayoishi, (kama vile 1Timotheo 2:1,2) -tutaliangalia hilo hapo baadae – katika mafundisho haya, na kile tunachopaswa kukifanya, hakina msingi wa kibiblia. Hawaupati mfano wote wa mafundisho haya ndani ya agano jipya; na kwa hiyo, wanamnukuu kwa wingi sana kutoka katika Agano la Kale – lakini baadae tu huishia katika kushindwa katika kuitumia mistari hiyo, na kwa ujumla kulichanganya agano, na hasa kushindwa kuelewa haswa Agano Jipya linahusu nini!

Kwa hiyo mmoja wa waandishi wake amesema kuwa, mji na nchi eti vinawakilisha mchanganyiko wa miili na maendeleo yao kiroho imefungwa kwa dhambi zao. Kulingana na mwandishi huyu, nchi hizo zimepewa kanisa ili kwamba eti liwawakilishe wao mbele za Mungu na kisha kuwaongoza kwenye kutubu na suluhisho! Anapozilinganisha nchi na miji anatumia usemi kama vile “binti bikira wa Ufaransa” au “binti wa New York”, analinganisha Ufaransa na mji wa New York. Kwa maneno mengine anajaribu kutumia maneno ambayo Mungu aliyatumia kwa watu wake aliowachagua, (“bikira, binti wa watu , watu wangu, binti bikira wa Israel”) ambaye kwake amemwanzishia agano la uhakika na kwa yeye aliye mkiri. Na kwa ajili yake mtumishi wake alifanya maombezi. Na mwandishi wao anatumia maneno hayo hayo kwa nchi na miji ya ulimwengu leo! Kana kwamba leo taifa au mji huo ungeweza kutazamwa kama vile ndio watu wa Mungu walimotendea dhambi kama ilivyo kuwa katika Agano la Kale; na kana kwamba kanisa linapaswa kuomba kwa ajili ya mji ule au nchi kana kwamba ilikuwa ni taifa la Mungu au watu wa Mungu! Inataka kuonekana kana kwamba kanisa linawakilisha manabii ambao huwaombea watu wa Mungu! Je, taifa la Uingereza au Tanzania linawakilisha watu wa Mungu au kanisa la Mungu? Na, je kanisa la Bwana leo linapaswa kutenda kama baadhi ya manabii wa Agano la Kale ili kupata upatanisho kwa ajili ya taifa kwa kuungama na kutubu dhambi zake?! Mambo haya yote ni mchanganyiko kabisa, na ni upotoshaji na yanalinyang’anya kanisa huduma lake la kweli. Kama tulivyosema tayari, matunzo na maombi kwa ajili ya jamii tuishimo ni ya muhimu (yanahitajika) na ni ya kimaandiko. Lakini tunapaswa kufuata maandiko yanavyofundisha kuliko kufuata upotoshaji huu.

(Upo mstari mmoja katika agano la kale unaoongelea kuhusu bikira binti wa Babeli, Isaya 47:1, lakini hii inahusu tu mambo ya hukumu na wala sio maombezi! Na kwa hakika, katika mstari wote huo, Babeli inachukuliwa kama alama ya utawala wa kidunia au shetani, ambapo kwake hukumu ya Mungu itatujilia. Soma Isaya sura ya 13 na 14 hasa mistari ya 4-24, hii inaweza kuelezea lugha iliyotumika katika 47:1. Hakika hakuna mahali popote pale katika Biblia ambapo maungamo au toba vimefanywa kwa ajili ya dhambi za watu wasioamini; Daniel na manabii wengine waliwaombea watu wa Mungu! Wanalichanganya kanisa na ulimwengu kabisa.)

Ni nini basi, kwa sababu eti mimi ni Mwingereza, kwa hiyo ninawajibika kuungama na kutubu kwa ajili ya dhambi ya Uingereza, kama Daniel alivyofanya kwa Israel? Ni nini basi, kutubu kwa ajili ya lile ambalo Waingereza walilowatendea Wajerumani, Waispania, Wamarekani, Wa-Irish na wengine wengi katika karne hii, halikadhalika miaka 100, 200, 500 na 800 ijayo? Inaishia wapi hiyo? Hii, kwa ujumla ni jukumu lisilokuwa; wanatufundisha kwamba tunapaswa kufanya utafiti wa kihistoria kwa uangalifu sana na uchuguzi juu ya dhambi kubwa zote, na matendo yasiyo ya haki ambayo nchi “yetu” imeyatenda, kwa sababu, eti tusipofanya hivyo na kuliongoza taifa katika kuungama na kutubu kwa dhambi hizo, basi hukumu za Mungu itaendelea kukaa juu ya nchi yetu na itazuia baraka za Mungu au uamsho kutujia kwa kweli. (Jambo hili ni udanganyifu). Na kama tutauliza na kwenda mbali kiasi gani nyuma katika historia, walimu hawa wanatuambia tunahitajika kwenda nyuma mpaka pale ambapo nchi “yetu” au taifa “letu” lilipoumbwa kwa mara ya kwanza na kugundua maovu yote makubwa liliyokwisha yafanya toka wakati huo hadi sasa. Kama ni hivyo, eti twende njia nzima nyuma mpaka kwa Adamu na kutubu kwa ajili ya dhambi zote ambazo mwanadamu ametenda hadi kufikia wakati huu. Hii inaweza kutimiza kosa lao la hatari na udanganyifu wao wa kufikiri ambao bado kwa namna fulani tungali (kupitia maombi ya upatanisho) weza kufidia makosa ya wanadamu, ambayo tayari Yesu alikwisha yabeba msalabani! Na tukiwaachilia mbali watu wa Mungu Israel, kabla ya Kalvari, ni wapi katika Agano Jipya ambapo Mungu anahitaji taifa zima litubu? Hili ni kosa au hitilafu nyingine na udanganyifu. Kama vile wanafundisha kwamba katika siku hizo za Injili ya Neema, Mungu anatuhitaji tuzingatie ukombozi wa mataifa kama mataifa, wanafikiri Mungu anashughulika na mataifa leo sawa sawa na jinsi alivyofanya kwa Israel katika Agano la Kale! Wanafundisha kuwa eti kanisa linayo haki kutumia damu ya Yesu Kristo kwa dhambi za mataifa, na wangependa kututaka sisi tuombe kwamba Uingereza kama nchi iweze kupatanishwa na Mungu kupitia damu yake. Tumekwisha kuona tayari kuwa hakuna kitu chochote kama hicho ambacho kimefundishwa katika Agano Jipya. Hii si kitu kingine isipokuwa ni matumizi ya kiushirikina ya damu ya Yesu Kristo.

Hii kwa kweli inaleta upuuzi wa Agano Jipya na ya Injili ambayo ni uweza wa Mungu uokoao roho wa kila roho na kila mmoja amgeukie Bwana kutoka katika nguvu za giza na kuibatiza roho hiyo iweze kuingia katika ufalme wa kiroho wa Mungu wa uzima, furaha amani na haki. Hicho ndicho kinachoelezwa na Agano Jipya – kuzileta roho katika uzima wa Mungu. Lakini nchi au mji hauwezi ukabatizwa katika ufalme na uzima wa Mungu. Ndiyo, Injili inaweza kuhubiriwa kwa mataifa yote, lakini mafundisho na mafunuo ya Agano Jipya ni kwamba mtu ataokolewa kutoka katika kila kabila na taifa. Haifundishi wala haionyeshi kuwa mataifa hayo yataokolewa kama taifa pekee katika siku hizi za Injili kama kwamba Mungu analo agano na Uingereza au nchi nyingine yoyote ile iwayo kama alivyofanya kwa Israel katika Agano la Kale.

Kanisa siyo ulimwengu; Uingereza siyo Kanisa; na wale wasioamini sio watu wa Mungu – Danieli aliomba na kuungama kwa ajili ya dhambi za watu wa Mungu, na wala si kwa ajili ya dhambi za watu wasioamini. Lakini wao wanachanganya yote pamoja. 

Paulo hakwenda Mekedonia na kuliambia taifa la Mekedonia kutubu kwa ajili ya dhambi zake na vita vilivyopita. Hakuwaita maafisa wa Serikali ili watubu kwa ajili ya dhambi za nchi yao au mji wao ili kwamba kusababisha upatanisho kwa mji huo au nchi hiyo. Alitembelea sehemu fulani fulani katika Mekedonia na aliwaambia watu waishio humo kuwa wanahitajika kutubu dhambi zao na kumgeukia Yesu Kristo ambaye ndiye atakayewafanya wawe wenyeji wa nchi nyingine, yaani, mbinguni! Wataweza kuongezwa katika kanisa la Mungu ambao ndio mwili mmoja. Paulo hakuthubutu kuweza kujaribu kuwafanya Wakristo wa Mekedonia waweze kusababisha aina fulani ya upatanisho kwa ajili ya nchi yao.

Pasipo kuelewa wanachokifanya au nini hasa wanakisema, wanabadilisha huu wokovu wa ajabu ambao unawaingiza wake kwa waume wengi katika uzima na uweza wa ufalme wa Mungu wa mbinguni, kwa mawazo yao ya uanzishaji wa aina ya mambo fulani fulani ya kiinje tu ya kitaifa au ufalme wa kikirsto.

Baadhi ya waandishi wao wanasema, inapotokea mkristo anatubu dhambi za taifa lake aishilo, eti hiyo ni hatua ya mwanzo tu; kwa ujumla wasemacho hapo ni kwamba unapaswa kuwa na maombezi kama Daniel ambaye anazitambua dhambi hizi na kisha anamuomba kwa ajili ya taifa, hii pia inapaswa kufuatwa na ujumla wa kanisa ambalo pia linaombwa kuhusu dhambi hizi za taifa. (Wanadai kuwa hii ililetwa na Ezra ambaye aliwaongoza watu katika maungano ya pamoja); na jambo la tatu na ambalo, ndiyo hatua ya mwisho ni pale ambapo jamii au maafisa wa kiulimwengu katika mji ule au taifa wanaziungama dhambi hizo hizo, na hii pia huwakilisha toba ya kweli ya kitaifa na pia kwamba, kwa taifa hilo! (Na hii nayo wanasema eti imeletwa na Nehemia katika Agano la Kale ambaye anauwakilisha ulimwengu au uongozi wa kiserikali!).Wanafundisha hayo ijapokuwa hakuna chochote kile kama hicho ndani ya Agano Jipya, na kwa ujumla wanalitumia vibaya Agano la Kale katika kusudi lao la kuunga mkono ubunifu wao. Wakiwa na nia ya kuunga mkono mambo yao mageni, inaonyesha dhahiri kuwa upotoshaji wao hauna mwisho.

Ni janga la jinsi gani kuona viongozi wa wakristo wengi wakjidanganya wao wenyewe na tena wakidanganya maelfu ya wengine kwa kufikiri na kufundisha kwamba eti wanasababisha aina fulani ya upatanisho na kufungua baraka za Mungu kwa taifa lao pale wanapoungana na kutubu dhambi za taifa lao zilizopita na zilizopo! Waumini wa Kiingereza waende Australia na kuziungama dhambi zilizopita za waingereza walizowafanyia waumini wa Australia; kadhalika wakirsto wa Australia waje hadi Uingereza na kuungama dhambi za Australia walizowafanyia waingereza! Wabrazil waje Uingereza, Waamerika nao waende Japan, na Wajapan waombe msamaha toka kwa wakristo wa Marekani na hivyo kuendelea zaidi na zaidi! Wakristo wakizunguka ulimwengu mzima wakiungama kwa wakristo wengine dhambi zilizopita za “taifa” lao, ambazo kwa hakika kanisa la Yesu Kristo halina chochote cha kufanya kwake!

“Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa?”

Kama tulivyokwisha kuona, hakuna popote katika agano jipya ambapo mkristo anaenda akizunguka kule na kule kuungama na kutubu kwa ajili ya dhambi za kitaifa za aina yoyote ile. Hatuuoni mfano wa jinsi hiyo hata mmoja, na wala hayapo maagizo ya kufanya hivyo yalivyoagizwa na Yesu au hata mitume.

Wakristo toka Roma hawapaswi kwenda Mekedonia kuziungama dhambi za Warumi, wala kwa Waathemi, kwa Wayahudi au kwa yeyote yule mwingine. Waumini toka Mekedonia, Athene, bara la Asia au sehemu nyingine hawaendi wakizunguka kuziungama dhambi zilizopita za watu wao na kuombana msamaha kati yao au nchi nyingine hata kama walikuwa na historia ndefu ya mapigano kati yao. Ujumbe wa wakristo wa kirumi hawakwenda Yudea kuomba msamaha toka kwa wakristo wa kiyahudi kule! Ni hakika kuwa kulikuwepo na mambo mabaya katika eneo lile, kama vile ilivyo katika karne hii, lakini ukitazama jinsi ambavyo Yesu Kristo amefanya pale Kalvari, basi kwa kweli ingekuwa ni ukichaa wao kufanya hivyo, ndio maana haishangazi kuona kuwa hatusemi chohcote cha jinsi hiyo ndani ya Agano Jipya. Na kama ulitaka kufanya hivyo, utawezaje basi pasipo shaka yo yote kuwa na uhakika kuwa umeungama dhambi zote ambazo nchi yako imezitenda dhidi ya nchi nyingine? Hata mtaalam wa historia tu asingeweza kuyaelewa mambo yote ambayo yangeweza kuwa yamemchukiza Mungu.

Kama watu wa Bwana, sisi sote tu wenyeji wa mbinguni, na tunafahamu kuwa vita na matendo yasiyo ya haki ya nchi tuishimo hayana chochote cha kulifanyia kanisa la Yesu Kristo, lakini bado utaona wakristo wengi wakizunguka wakiomba msamaha wa wakristo wengine kwa ajili ya dhambi za ulimwengu, kwa mfano, dhambi za mataifa “yao”; wakristo hao je wanaumizwa mioyoni mwao kwa yale ambayo nchi nyingine zimelifanyia taifa lao? Kwa nini basi waumizwe? Tungepaswa kuwasamehe kama vile sisi tulivyowasamehe iwapo tunaona kuna ugumu wowote mioyoni mwetu. Mimi sihitaji mkristo wa nchi yoyote kuomba msamaha wangu kwa ajili ya makosa yaliyofanywa na nchi aliyotokea kuishi, wala mimi au hata kanisa langu hatuwakilishi Uingereza kana kwamba tunao uhusiano wa kiagano maalumu na Mungu. Ninajua kuwa wao wanafikiri kwa kufanya hivyo watakuwa wanasaidia kuleta aina fulani ya mapatano, lakini hiyo inaishia tu kwenye maungamo mabaya kiroho na kimaandiko ya Neno la Mungu – bila kutofautisha kati ya ulimwengu na kanisa. Hii ni tafsiri ya mwili ambayo inakataa kuudhalilisha ukweli kuwa mimi ni uzao wa kutoka juu, tumezaliwa na Mungu na kwamba wenyeji wetu sasa uko mbinguni (Philipi 3:20). Nimekombolewa kutoka dhambini na mimi sio wa ulimwengu huu tena, kwa ufahamu wa ndani na ukweli; mimi sio Mwingereza na wala wewe sio Mtanzania, au Mhehe wala Mmasai; sisi ni mali ya Mungu (watu wa Mungu). Sitajaribu kujilinganisha na ulimwengu kama vile mimi ni wake. Hii sio kujifananisha na mahitaji ya wengine, hii ni kuchanganyikiwa, hii ni udanganyifu mtupu. (Hata kama maelekezo ya dini yanaweza kubeba jina la ukristo, bado kama watabeba uovu na ukatili watajionyesha kuwa hawana lolote lile mbele ya kanisa la kristo. Na katika mtiririko wa kuhubiri Injili kwa watu fulani fulani katika maeneo fulani ya ulimwengu, ukweli huu utahitajika kutolewa wazi, lakini hii haihalalishi ujumla wa mambo yasiyo ya kibiblia na ya tabia za ushirikina wa makosa haya ya kisasa.) Kama tulivyokwisha ona, hatuoni mfano wa aina hii hata mmoja ndani ya biblia yote! Hii haimaanishi kuwa sisi hatujali au hatuhusiki; la hata kidogo; haimanishi vilevile kwamba hatuwezi kuomba kwa ajili ya hayo, kwa ajili ya jamii zetu au nchi. Na tutaweza kuona baadaye jinsi kanisa linavyopaswa kuomba kwa njia za aina gani ili kwamba wale ambao hawajaamini wapate kufikiwa na Injili! Lakini ulimwengu, na zaidi sana kanisa halisaidiwi kwa mawazo hayo potofu ya kibinadamu, ambayo yanatumikia tu mambo magumu yasiyofahamika na kuharibu ukweli na uweza wa Injili.

Lakini waumini hao wanaendesha mikutano hii ya maungamo na kutubu, wao wanasema kuwa, eti wametembelewa kwa macho na wanaamini kuwa eti ni Mungu anayetembea katikati yao na kuguswa mioyo yao. Lakini wakiwa wakidanganyika kwa kuamini kwao wenyewe. Ndio maana haishangazi kuona kuwa wanapokusanyika pamoja wanazidi kujidanganya kwa mambo yanayodhihirishwa na kujisikia. Na kwa hakika hii ni jambo la hatari na sisemi mambo haya kiurahisi rahisi tu. Lakini aina hii ya makosa na udanganyifu yanapatikana nyakati hizi za Agano Jipya ambapo waumini kwa kutaka kukidhi nia zao na mawazo yao, kwa kweli kwa kufanya hivyo wanakuwa wanajifungulia wenyewe mlango ili kupokea Injili ya tofauti, Yesu wa tofauti, na Roho wa tofauti – na wao wanafikiri kuwa hayo ni ya Bwana! Lakini mtume Paulo anaonyesha hatari ya jambo hili kwa kusema kuwa kwa kweli wanadanganywa na malaika wa nuru, ambaye mtume Paulo anamlinganisha na shetani (2 Kor.11:1-15). Na hivyo ndivyo ilivyo leo kwa waumini hawa. Ni waumini, lakini wanauacha ukweli na wepesi wa Injili ya Yesu ambayo walikwishaipokea hapo mwanzoni. Wanajiweka wazi wao wenyewe kwenye udanganyifu. Haishangazi kuona kuwa wanaweza wakawa na aina zote za ujuzi ambao utawaendeleza kudanganywa tu. Bali kujisikia huko wanakojisikia pamoja na kudhihirishwa kwake kunatokana na pandikizo la Injili nyingine na roho mwingine.

Kaka zangu na dada zangu katika Kristo ninawasihini kwa ajili ya faida ya nafsi zenu ambayo kwayo Yesu Kristo alikufa Kalvari ili kukomboa na kuwaweka huru na kutufanya tuwe wake mwenyewe: mjihadhari na mafundisho hayo na madanganyo yake.

Biblia na kile inachosema ni cha muhimu zaidi kuliko shirika lolote kubwa la kikristo au wanenaji. Haijalishi jinsi gani wanenaji hao wanafahamika au kujulikana. Na kama basi ni bora uchukue mwelekeo wa Kristo, kuliko kufuata kile ambacho kinajulikana lakini na hakifundishwi katika maandiko ya neno la Mungu, na kile unachofikiri kuwa kitatueletea umaarufu na kufahamika zaidi.

“Ushahidi” wa Maandiko Yao

Maandiko ya neno la Mungu kwa uhasa ni kitu gani basi? Je, hawa walimu wanatupatia sisi ili kuonyesha kuwa kanisa linapaswa kuungama na kutubu kwa ajili ya dhambi (zilizopo na zilizopita) za nchi tuishiyo? Tumekwisha kuona nukuu fulani kutoka Daniel. Wengine wananukuu mistari inayoonyesha fadhili za Mungu katika kuwabariki wamataifa kwa wokovu, kama vile, Mwanzo 12:3, Zab. 22:27, Isaya 56:7, Yona 4:11 na Warumi 15: 9. Kwa hakika tungeweza hata kuongezea mistari hiyo na mingineyo inavyoonyesha, kama vile, kwamba tokea mwanzo Mungu alipanga kuwabariki watu wote katika dunia, lakini hakuna hata mstari mmoja kati ya hiyo, inayoonyesha kwa namna yoyote ile kwamba watu wa Mungu wanapaswa kuungama na kutubu kwa ajili ya dhambi za mataifa hayo, kabla Mungu hajawabariki kana kwamba hiyo ndiyo inayomfungulia Mungu mlango wa kuja kuwabariki! Ingawaje Mungu ameahidi kupanua wokovu wake kwa watu wote, lakini jambo hili haliwakilishwi ndani ya maandiko ya neno la Mungu kwa njia ya vifungu vipya vya kisheria kama ile ya pale Sinai na ambayo mataifa yasiyoamini yanapaswa kuitunza – na kanisa kuombea kwa ajili yao iwapo hawayatunzi! Hapana! Makubaliano ya Agano Jipya ambayo Mungu anayapanua kwa mataifa yote sasa, ni kwa ajili ya yeyote yule aaminiye, waume kwa wake wanaokolewa kwa imani katika Kristo Yesu, huru kwa neema ya Mungu. Huu ndio msingi wa Agano Jipya; toleo la Yesu Kristo ni kwa ajili ya waume na wanawake na ya kwamba, yeye ndiye aliyesulubiwa na akafufuka ni mlango wa agano hili, wala hayapo kabisa masharti ya kutimizwa kabla na kubarikiwa kwa wokovu wake.

Hayupo mpatanishi wa agano awaye yoyote yule na wala halipo agano lingine! (Mstari niliyoielezea hapo juu, haiwakilishi aina fulani ya uhusiano wa agano ambapo Mungu anasema, “kwa sababu nimekuahidi kukubariki wewe kwa wokovu kupitia Kristo tangu milele (Tito 1:2) basi, sasa umo katika uhusiano wa kiagano na mimi na kutokana na agano hilo kwa kweli huwezi kupokea wokovu kamili mpaka kwanza nchi unayoishi itakapotubu dhambi zake, zilizopita na zilizopo).

Kwa hakika yapo Agano la Kale na Agano Jipya tu. Hakuna lingine! Je, wewe umo ndani ya agano lipi kati ya hayo mawili? Aina hii ya kuomba kwa ajili ya dhambi za taifa zilizopita ni makosa, baadaye tutaangalia kwa karibu zaidi, jinsi Mungu anavyotimiza kusudi lake ili kubariki wale wasioamini.

Wanaonyesha vidole kwa Yona, alipokuwa akihubiri kwa watu wa Ninawi, lakini hapo anathibitisha tu yale tunayoyasema katika makala hii, yaani, ni kwa kulileta neno la Mungu kwa watu wenyewe, ndiyo inayowapatia fursa kwa imani na toba. Yona aliongea moja kwa moja na mioyo yao na akawaambia watubu. Nao watu wote pamoja, yaani, mji mzima, walitubu kwa ajili ya dhambi zao. Walitambua na wakakiri dhambi zao mbele ya Mungu. Yona hakuwaambia kwamba, kwanza watubu katika ujumla wao kwa ajili ya dhambi za wengine (wenzao waliomo mjini) kabla hajawabariki na kuwasamehe.

Wananukuu Kut.10:16-18, wakisema eti mbona Musa aliwaombea kwa Farao, na kwa hiyo kanisa nalo linapaswa kujitambulisha na dhambi za taifa na kutubu kwa niaba yao! Ndiyo, ni kweli kwamba, Musa aliomba kwa ajili ya Farao kwa sababu alizikiri dhambi zake na akamsihi Musa aombe kwa ajili yake. Hiyo inatofautiana sana. Musa alikuwa hatubu kwa ajili ya dhambi za mtu asiyeamini, na cha muhimu zaidi kwa wakati huo, Yesu alikuwa hajafunuliwa kuwa ndiye mwombezi kati ya wanadamu na Mungu. Hivyo ilikuwa ni jambo la kawaida kuona kuwa Farao amsihi Musa ili aombe kwa ajili yake, hasa pale ambapo Musa alipokuwa akifanya na kuongea kwa niaba ya Mungu kwa ajili ya watu (Ku. 4:16). Kwa hiyo huu hauwezi kuwa ni mfano wa mafundisho yao hayo, agano lisilosahihi, iwapo wataendelea kana kwamba Yesu hajafunuliwa kutoka mbinguni kuwa kama mwokozi na mpatanishi wa wanadamu. Hapa pia tunaona jinsi mafundisho hayo yanavyojaribu kumweka mpatanishi mwingine zaidi ya Yesu Kristo kati ya Mungu na wanadamu kwa ajili ya toleo la dhambi.

Wanafanya hivyo hivyo, pale wanapotaja kuwa Musa alipokea msamaha kwa ajili ya dhambi za Waisrael katika (Hes.14:17-21), na wanazidi kutuambia kwamba eti kanisa linaweza kupokea msamaha wake kupitia maungamo ya dhambi za kitaifa, kwa ajili ya dhambi za mataifa hayo, kama vile Musa alivyofanya kwa Israel! Hapa wanajifanyia kosa la kidole, wanachanganya tena ulimwengu na kanisa, wala hawawezi kutambua kama iwapasavyo kutambua kuwa leo yupo mpatanishi mmoja tu kati ya Mungu na mtu, na huyo ni KRISTO YESU. Tunaelewa kuwa huduma ya Musa ilikuwa ni picha ya kielelezo cha awali cha Kristo na kwa maana hiyo alikuwa ni wa namna ya pekee kabisa kama tunavyoona katika Kut. 4:16; Hes.12:6-8 na Kumb. 18:15.

Katika Agano Jipya, wanamnukuu Yesu, akimwomba Baba awasamehe wale waliomsulibisha (Luka.23:34), lakini pale Yesu alikuwa hafanyi lolote zaidi ya lile alilofundisha yeye mwenyewe kufanya.; kama vile, kuwasamehe wale wanaotutendea mabaya kwa makusudi, hasa pale wanapokuwa hawana wazo kuwa wanatufanyia ubaya. Ninafahamu kuwa, sisi kama wakristo, sote tumemfuata Kristo katika hili; lakini hata hivyo hii haiwakilishi ushahidi wa Agano Jipya kwamba kanisa sasa linapaswa kujishughulisha na kutubu kwa ajili ya dhambi za miji au nchi yao! Zaidi ya kushangaza, ni pale tunapoona wanamnukuu pia 1Yoh.1:9, “…tukiziungama dhambi zetu…”, na wanasema bila woga au hofu ya Mungu kuwa eti mstari huo unatuonyesha kwamba, kanisa la kwanza lilikuwa linajishughulisha na Ibada za maungamo ya dhambi za jamii! Wanadai kuwa, wakristo hapo walikuwa wanabeba mila /desturi za Agano la Kale zilikuwa ni mfano wa pekee kwao walioufahamu na kuusikia! Zile “mila” ambazo wanazizungumzia, ni mfano wa pekee wa mtu kama Danieli au Nehemia akiomba wakati ule wa kutawanywa na kupelekwa uhamishoni kwa Israeli. Lakini hii ilihusiana tu na Israeli na kwa wakati ule wa pekee katika historia yao! Nini? Baada ya Kalvari na baada ya kumpokea Roho Mtakatifu Wakristo walikuwa bado hawajapata ufahamu wa ndani zaidi kuliko tukio hili la pekee la Agano la Kale? Hii inaweza kuwa ni kweli kabisa kuhusiana na walimu hawa wa siku hizi lakini sio mitume wa kanisa la kwanza. Hii ni aina ya rushwa ya Neno la Mungu na kwamba sisi hatulazimiki kuukubali. Lakini labda inatosha kusema kuwa, Yohana anatumia uwingi, kama vile asemapo “sisi ” na “zetu” katika barua zake zote akimaanisha kuwa, watu wa Mungu – au je, tunapaswa kusema kwamba jamii ya watu wasioamini wale wanaotuzunguka, wanao ushirika pamoja na Baba na Mwana? (1Yoh 1:3)!!?

Na hii ndiyo baadhi ya mistari yao muhimu sana ambayo kila mara hutolea mifano yao, au kuthibitisha mafundisho yao. Lakini pia hii inatuonyesha sisi wazi tu kwamba, hata hao walimu hawawezi kutoa mfano, kwa kweli hapana hawana hata mfano mmoja ambao watu wa Mungu wameonekana sehemu fulani wakiungama au kutubu kwa ajili ya dhambi za nchi nyingine au kwa ajili ya dhambi za wasioamini wowote wale. Sasa kumbe tunaona kwa uwazi zaidi hapa kwamba kwa hakika wanakuwa hawapendezwi na kuelekezwa kutoka katika maandiko ya neno la Mungu katika mambo haya; bali wao wanatumia andiko lolote lile wanalofikiri kuwa litaweza kutimiza kusudi lao, na iwapo halitimizi kusudi lao, basi wao hulilazimisha ili liweze kutimiza, kwa kuyumbisha maana halisi ya Neno lile ili kwamba lipate kulingana na mtindo wa mafundisho yao.

Baadhi ya Waraka wa Msingi

Sasa, hebu tuyaangalie mambo ambayo wao huyachukulia kama msingi wa mfumo wao wote wa kufikiri na kufundisha kuhusiana na habari hii ya maungamo ya dhambi ya kizazi kilichopita. Mstari wanaoupenda sana kuutumia kama msingi wa mafundisho yao, unapatikana katika Mambo ya Walawi 26:40.

“Nao wataukiri uovu wao na uovu wa baba zao…” (Hapa unatakiwa usome sura nzima wewe mwenyewe).

Ukitazama kwa makini. Katika sura hiyo, Mungu anatamka hukumu atakayoileta kwa Israel, iwapo tu kama watakuwa wakirudiarudia kutomtii. Na hukumu ya mwisho itakuwa ni kuwa Mungu atawafunua wazi kutoka katika nchi yao na kuwatawanyia katika nchi nyingine mbalimbali; lakini hata hivyo, atakuwa bado na huruma juu yao na kukumbuka agano lake iwapo watatubu na kuziungama dhambi zao (mstari wa 40-41).

Kwa mapana zaidi ndani ya mstari huu walimu hawa wa kisasa wanajaribu kusimamia na kutengeneza mawazo ya “upatanisho wa maungamo na toba” na maungamo na toba ya dhambi za kihistoria, kwa pamoja, wao wanafundisha kuwa, Mungu kwa hakika eti hawezi kumbariki mtu au taifa mpka kwanza taratibu hizo ziwe zimekamilishwa. Kama vile kanisa linaongoza njia kuelekea kwenye kuungama na kutubu kwa ajili ya dhambi za taifa na wanaamini kuwa hii itaweza kusafisha njia kwa maungamo ya kiulimwengu kwa ajili ya hizo dhambi za kitaifa. Lakini hayo yote pengine hapa hatuna nafasi ya kuzitazama sababu zake kwa nini iwe hivyo.

Wanawanukuu baadhi ya watu kama mifano ya aina ya maungamo na toba; haishangazi kuona wanawataja akina Daniel, Ezra, Nehemia na Yeremiah (kama vile katika Daniel 9:;16) ambapo wote wanazikiri dhambi za mababa zao ndani ya maombi yao. Mstari tulioutaja hapo juu unapatikana pia katika kitabu cha Mambo ya Walawi pamoja na mifano ya maombi ya watu hao, yanawakilisha jiwe la msingi la mafundisho hayo hayo. Lakini kwa nini tunasema, haishangazi kuona kuwa wanawanukuu watu hawa maalumu. Ni wazi kuwa iwapo tutaisoma sura hiyo – Walawi 26 – na mistari hiyo katika mtiririko wa habari zao, ni wazi kutoka kwa Mungu mwenyewe kwamba aina hii ya maungamo (ya dhambi za pamoja na vizazi vilivyopita) ingeweza kutokea katika muda maalum ndani ya historia ya Israel, yaani, wakati Mungu alipowanyanganya na kuwatapanyatapanya mbali katika nchi nyingine, (Walawi 26: 27-42). Hivyo ndivyo tunavyogundua kwa uhakika pale, tunaposoma sura hiyo na kuiacha Biblia ijitegemee (isema nasi) badala ya kuitumia ili kuunga mkono mawazo yetu wenyewe tu. Kwa hiyo haishangazi kuona kuwa hawamnukuu mtu mwingine awaye yote, anayeomba kwa jinsi hiyo kabla ya wakati wa Jeremiah, (ambaye yeye katika wakati wake, Mungu alikwisha anza kutimiliza hukumu yake dhidi ya Israel, kwa kuwatapanyatapanya), kwa sababu hakuwepo yeyote alifanya hivyo, kwa kuwa Mungu hakutazamia hayo kabla ya utawanyo!

Katika mazingira ya namna hii, kukataliwa na kupelekwa uhamishoni, ambavyo vinawakilisha kuvunjika kwa agano, kungekuwa ni nini tena cha kawaida zaidi ya hii, yaani, Mungu angewataka wao kutambua na kukiri kama vile kuungama kwa sio tu dhambi za kizazi kimoja bali kule kurudiarudia na kutokuwa na utii kwa vizazi vingi vilivyoanzia kwa Israel wakifukuzwa kutoka katika nchi yao. Mungu aliwataka waelewe kuwa hii haikuwa tu adhabu kali na ya ghafla kwa sababu ya kizazi kimoja; bali kwamba vizazi vingi vinageuza migongo yao kutoka katika toleo la neema yake ya uvumilivu wao wa muda mrefu.

Iwapo tutasoma Walawi 26 tutaweza kuona namna gani Mungu alivyokuwa mvumilivu na mwenye rehema kwa Israel. Anawaambia kuwa ikiwa atakataa kumtii na kumfuata, ndipo atatuma aina fulani ya hukumu juu yao. Kwa nini? Ni kama adhabu tu na laana inayoendelea? Hapana! Tunapoangalia ugumu wa mioyo yao, Mungu angeweza kutuma hukumu kuwafanya wao wafikirie upumbavu wa njia zao na hivyo iweze kuwapa fursa ya kutubia dhambi na uovu wao; ili yamkini, waweze kumvumilia yeye. Na kama watakataa kuchukua tahadhari ndipo atazidisha ugumu au ukali wa hukumu hizo, katika kujaribu kuwafanya watambue kuwa walikuwa mbali toka Mungu na baraka zake za ajabu. Hivyo, kutokana na hukumu hizi Mungu alitaka kuona kuwa Waisrael wanarejea katika ufahamu wao kisha kurudi kwake, kama vile yule mtoto katika Luka 15. Tazama walawi 26:14,18,21,23,27. Katika hayo yote, tunaona kuwa hukumu zote hizo kwa kweli zilikuwa ni njia ya Mungu ya kuelezea Rehema zake, katika maana ya kuwa alitaka kutengeneza fursa ya aina fulani kwao ili waweze kujitambua upumbavu wao (upuuzi wao) ili watambue na watubu na kisha wamrudie yeye.

Kwa hiyo tunagundua hapa kuwa , kabla ya wakati wa Uhamishoni, ikiwa ikitokea mfalme yeyote wa Israel au Yuda pamoja na watu kama vile kizazi kizima chochote, wakatubu na kurejea kwa Mungu ndipo Mungu aliwabariki na ndipo waliweza kubarikiwa, pasipo maungamo au kutaka kuungama dhambi za vizazi vilivyopita. (Ijapokuwa ingewezekana kuonekana kama ni jambo la kawaida kuzitaja dhambi za aina hii kama wangekuwa wamefuta hizo dhambi zao binafsi; sio tu ili kuomba waweze kupata msamaha zaidi au kuachiliwa, bali tu kama utambulisho wa yale yaliyowahuzunisha kwa hakika, na pengine yalihitajika kusafishwa kutoka nchi iliyoanza mapema.) Hata hivyo, hatuoni mfano wowote wa aina hii ya maombi kabla ya mtawanyiko, kwa mfano, nyakati za mfalme Asa, Uzia, Hezekia na Josia. Tunawaona hapo wakimrudia Bwana pasipo hata kuzikiri dhambi za mababa, na hiyo ndiyo tunayo iona ndani ya Biblia yote. Hii ndiyo kipimo chenyewe kuwa mtu azitubie dhambi zake mwenyewe, sio za mtu mwingine. Na ingawaje Yeremiah anaonekana kuziungama dhambi za mababa ndani ya muda huo wa mahangaiko ya Israel, mzigo wake mkubwa na maelezo ya ujumbe wa Mungu kwa watu wake Mungu kwa wakati huo ni kwa ajili ya mioyo yao wenyewe, ikiwafunga, ikiwahimiza na kuwainua ili watubu na kumrudia Bwana.

Tukirudia kwenye maelezo ya mwanzoni tunaona kuwa Mungu hakuwatawanya Waisraeli kwa sababu ya dhambi za kizazi kimoja, bali alichoshwa na vizazi vingi vilivyo mgeuzia mgongo Mungu; na mwishoni mwake kulikuwa hakuna chochote ambacho Mungu angeweza kufanya, bali ni kuwaondoa katika nchi kama alivyokwisha kusema. Mungu alimwita Israel, “mtoto wake” ambaye amemkomboa kutoka Misri (Hosea 11:1). Naye alifanya agano pamoja nao pale Sinai, walikuwa ni taifa moja na ni watu wake, naye alijishughulisha nao kama wana wake au kama bibi arusi wake, na alikuwa amewaahidi na akawapa nchi ya Kanaani kama sehemu ya agano lake pamoja nao. Lakini baada ya kuvumilia dhambi na ibada yao ya sanamu kwa muda mrefu, ilimbidi Mungu awatoe katika nchi yao. Na kwa kweli jambo hilo lilikuwa na maana kubwa kwa sababu wao kumiliki nchi ile ilikuwa ni sehemu ya agano ambalo Mungu alikuwa amelifanya na Israeli na sasa hili agano likawa limevunjwa na Waisraeli kukosa uaminifu. Na sasa baada ya kuwa wametawanywa nchi nyingine, walipaswa kutambua kuwa kuendelea kwao kukosa uaminifu kwa vizazi vingi kulikuwa kumepelekea wao kutolewa kutoka katika nchi ya ahadi. Watu kama Daniel, Ezra na Nehemia (Ezra 9:1-10, hasa mstari 7, pamoja na Hezekiah katika 2 Mambo ya Nyakati 30:6-9) walitambua mambo hayo, yaani, ilikuwa ni uasi wa mara nyingi wa Waisrael (wakati wa vizazi vingi) ndio uliowapelekea kwenda uhamishoni. Na kufuatana na Walawi 26, wakaungama kule kutokuwa na utiifu kwao kwa vizazi vingi. Aina hii ya maungamo ilionekana pia katika Kumb. 30:1-5, 1 Falme: 8:46-50, ingawaje katika sura hizo hatuoni popote wanapotaja maungamo ya dhambi za mababa.

Kwa hiyo, hapa katika Agano la Kale, walichokifanya akina Daniel na wengineo ni kuungama au kukiri dhambi zilizopita za kisraeli zilizosababisha uhamisho na kutokumilikishwa, ambazo kwa sababu wanazigundua wao wenyewe. Hata nyakati za Nehemia, Israel na Yuda walikuwa ni watu waliotapanywa na ile nchi ya ahadi ilikuwa inakaliwa. Kama nilivyokwisha sema, hapo juu, kile tunachokiona katika nyakati za misukosuko ni kuziungamia sababu ya misukosuko hiyo. Kwa hiyo tunaona kuwa kukiri uasi uliofanywa na Waisraeli kwa vizazi vingi kulihusishwa haswa na wakati ule Waisraeli walipotawanywa na kupelekwa uhamishoni, muda ambao waisrael walikuwa hawamiliki nchi. Hata hivyo, wengine wao waliruhusiwa kurudi. Hii ilifanana na wakati ambapo agano lilivunjwa – agano maalum lililofanywa kati ya Mungu na Israel, sio kati ya Mungu na mataifa nyingine!

Hebu sasa tulielewe vizuri jambo hili. Kwenye Biblia ndani ya Agano la Kale na Jipya hakuna po pote pale ambapo watu wa Mungu wanaungama au kutubu kwa niaba ya dhambi za watu wasioamini – za zamani au za sasa, huko vijijini kwao, mjini au katika Taifa – ili waweze kupata aina fulani ya Upatanisho kwa ajili ya nchi. (Tumekwishashughulika na Musa akiomba kwa ajili ya Farao). Hakuna mfano wo wote, hakuna maagizo yo yote ya kufanya hivyo. Hakuna mahali po pote pale ambapo watu wa Mungu wanatubu kwa ajili ya dhambi za kizazi kilichopita, iwe kwa ajili ya waaminio au wasioamini. Hili ni jambo lisilowezekana. Ni katika mazingira ya aini moja tu ambapo Mungu anawategemea kuungama dhambi za vizazi vilivyopita vya watu wa Mungu – na huu ulikuwa ni wakati wa Uhamishoni na Utawanyiko. Hakuna wakati mwingine wo wote ule wala katika aina yo yote ile ya mazingira ambapo tunasoma kuwa watu wa Mungu walipodiriki hata kuungama tu dhambi za vizazi vilivyopita; ili kupata aina fulani ya Upatanisho au baraka. Ukweli huu pekee ni zaidi ya kutosha, kuonyesha jinsi mafundisho haya ya kisasa yaliyokosewa na jinsi yalivyosimamia katika hila.

Kama tukitafakari 2 Mambo ya Nyakati 7:14, ambao wananukuu sana, tena tunatumba kwamba Mungu anaongea juu ya watu WAKE na dhambi ZAO. Hasemi wakiri dhambi za taifa la wapagani fulani au watubu kwa ajili dhambi zao. Ukweli huo ni wazi kabisa lakini wengine hawajali ukweli huo, nao wanafuata hisia zao kuliko neno la Mungu katika tafsiri yao ya mstari huo.

“Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.”

Ni wazi kabisa mstari huo unahusu dhambi za watu wa Mungu tu, na kama tulivyoona, sharti hilo au ahadi hiyo ilihusu tu kipindi cha pekee katika historia ya Israel. Katika Biblia nzima hakuna mfano moja wala mstari moja ambao unatuonyesha watu wa Mungu wa nchi yoyote walitubu kwa ajili ya dhambi za taifa fulani la wasioamini wanapoishi.

Fundisho la Ezekiel: Sura ya 18

Kwa nini Israel walichukuliwa uhamishoni? Je ni kwa sababu tu ya dhambi za vizazi vilivyopita? Je walikuwa wakiadhibiwa kwa ajili ya dhambi za mababu zao? Mungu akizungumza kupitia Ezekiel katika sura ya 18 anatuambia waziwazi kwamba walikuwa hawaadhibiwi kwa ajili ya dhambi za mababu zao! Kupitia Ezekiel, Mungu hasa alikuwa akiwakemea watu wake kwa kufikiri na kusema kitu kama hicho! Kila mtu hubeba hukumu kwa dhambi zake tu. Kama Yuda wangekuwa wametubu na kumgeukia Bwana na moyo wao wote wakati wa Yeremia, basi Mungu angekuwa amewabakiza na kuwabariki kama ambavyo alikuwa amefanya kabla – Yeremia 26:1-7, hasa ya aya 3. Lakini ukweli ni huu, kwamba kizazi kile kiliendelea katika miungu na uasi kinyume na neno la Mungu, kama vile vizazi vingine vilivyokuwa vimefanya. Ulikuwa ni uasi ulioandikwa wa vizazi vingi, ikiwa ni pamoja na hiki, kilichosababisha uhamisho.

Lakini hata kwa Israel mwenye kurudi nyuma, Mungu katika wema wake atangaza rehema zake na kuwataka wamgeukie na warudishwe katika nchi yao, Yeremia 3:12-14. Katika mafungu haya ya maneno na katika mengi mengine katika Biblia yote, Mungu anasema na watu juu ya dhambi zao na jinsi gani wazitubie njia zao na kumgeukia. Mungu hataji kamwe toba juu ya dhambi za mababu zao. Hakuwaamuru kukiri dhambi za mababu zao kama kitu ambacho wangetakiwa kukifanya kwa kawaida. Kama tulivyoona katika Lawi 26:40, Mungu aliwategemea kuungama dhambi zilizokuwa zikirudiwa na zilizolundikwa kwa wingi kwa vizazi vingi ambazo zilisababisha wafukuzwe toka nchi ya ahadi. Huo ulikuwa wakati pekee na kwa sababu maalum ambazo tayari tumezitaja.

Ilikuwa ni watu wa Israel wenyewe waliofikiri vibaya kuwa walikuwa wanabeba uovu wa babu zao – kwamba walikuwa wanaadhibiwa kwa ajili ya dhambi za baba zao; “Baba wamekula zabibu mbichi, na watoto wakatiwa ganzi la meno.” – Ezekiel 18:2. Haya ndiyo maneno Israel walikuwa wanasema, na hata walibishana na Mungu juu ya hayo katika Ezekiel 18! Mungu hakufurahishwa hata kidogo na mawazo yao hayo maovu. Na kila kitu ambacho tumekisema hapo juu kinaungwa mkono pia katika sura hii, na kuwekwa hasa katika muhtasari katika mstari 19-23. Na mstari wa 20 unatangaza:

“…..Mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanae…..”.

Na katika sura hii tunaona lile ambalo ni kweli katika Biblia yote, yaani kwamba, kila mtu anawajibika kwa dhambi yake na anaweza tu kutubu dhambi yake. Hakuna haja ya kutubu kwa ajili ya dhambi ya babu zetu, kwa sababu hatubebi uovu wao au hata adhabu kwa ajili ya dhambi zao. Katika Biblia hii ndiyo kawaida – kwamba watu watubu dhambi zao, na si za mwingine! Ingawa Yeremia anaungama dhambi za mababa wakati wa kutawanywa Israel, mzigo uliolemea na kilichokuwa kwenye ujumbe kwa watu wa Mungu kwa wakati huo ni kwa mioyo yao wenyewe, akiwataka waache ugumu wa mioyo, akiwasihi waache dhambi yao, akiwakazia watubu na kumrudia Bwana. Haya ndiyo yaliyomo katika huduma yake – kuonyesha Israel, wakati huo, dhambi na kutangazwa kwa rehema na hukumu ya Mungu. Na tunakuta hili ni sawa katika Biblia yote. Ukisoma Yeremia na manabii wengine; ukisoma Wamuzi, Wafalme na Mambo ya Nyakati; ukisoma Agano Jipya; utakuta neno la Mungu huja kupitia watumishi wa Mungu wakiwasihi watu waliotenda dhambi warudi, au warudi kwa Bwana; neno huja kwa watu wenyewe juu ya dhambi zao wenyewe, likiwashashiwi juu ya dhambi zao na kuwataka watubu na si kuwataka watubu dhambi za mwingine awaye yote. Na kwa hiyo tunaona mtu mmoja mmoja na jamii wakitubu dhambi yao na kupokea baraka za Mungu pasipo kutajwa kwa dhambi za vizazi zilivyopita – wakiwa waaminio au wasioamini! Hii ndiyo hali ya kawaida. Lakini mafundisho haya mapya yanachukua kile kisicho cha kawaida (kilichohusu wakati wa utawanyiko), inavuruga kabisa, na kufanya iwe kanuni – inafanya iwe sheria na kongwa kwa watu wa Mungu! Lakini tena katika hali zote hapo juu, tuone kuwa ni swala la manabii wakiweka mkazo na kuwaombea watu wa Mungusi kwa ulimwengu, si kwa wasioamini. Je hawa waalimu wetu wa kisasa hupata kutoka wapi mawazo yao hayo? Hasa katika Agano jipya, kifo cha Kristo pale Kalvari kinashughulikia maisha yetu ya nyuma na kutukomboa toka wakati uliopita – 2 Kor.5:17,18; Rumi 6:6; 1Pet 1:18 – tunapomgeukia na kuzaliwa mara ya pili. Msalaba wa Kristo kukatwa kwetu kutukufu toka dhambi, toka hatia yake, hukumu kututawala katika maisha yetu, na kutoka kuhukumiwa kote. Ni mahali pa kukatwa toka dhambi za baba zetu – hadi mpaka Adamu – na hukumu zote zinazoendana nazo. Nguvu ya msalaba ni kuu kuliko tunavyofahamu, Efeso 1:16-23. Ni nguvu ya Mungu kila aaminiye, na hakika hakuna haja au hitaji la kutubu kwa ajili ya dhambi za baba zetu, kwa sababu kifo cha Kristo kimeshughulikia dhambi zote na hatuwezi kujipatia upatanisho zaidi kwa toba ya jinsi hiyo – si kwa ajili yetu na wala si kwa mji au nchi tunayoishi. Na dhambi ya mababu zetu na hukumu kwa ajili yake haiwezi kutugusa kama sisi ni wa Kristo. Tuko huru kwa sababu Mwana ametuweka huru. Mafundisho haya mapya yanataka tu kuturudisha nyuma kwenye kongwa.

Katika Yeremia 31:29-34, Mungu anasema kitu kilekile ambacho alisema kupitia Ezekiel 18. Mungu anawaambia kwamba siku inakuja ambapo hawatatumia mithali hiyo tena, ambayo ni, watoto wakatiwa ganzi la meno kwa sababu baba walikula zabibu mbichi. Mungu alitaka wasiendelee kulaumu vizazi vilivyopita kwa ajili ya dhambi zao! Sasa Mungu anawaambia juu ya Agano Jipya ambalo anakwenda kuweka ambapo katika hilo atasamehe uovu wao na asikumbuke dhambi yao tena. Hii ni ajabu na wazi, lakini akizungumza kuhusu mistari hii, mmoja wa wasomi hawa wa kileo anasema kwamba Kalvari na Agano Jipya haviondoi haja ya kuungama dhambi za baba zetu na zile za miji na nchi tunazoishi ndani yake! Hata licha ya yaliyosemwa katika 1 Pet 1:18, anafundisha, sambamba na wengine, kwamba wana na jamii bado wanaathirika na hukumu ambazo zinahusu dhambi za mababa na vizazi vilivyopita na kwamba kwa hiyo tunaweza tu kujipatia upatanisho kamili na kupata baraka kamili za Mungu kupitia kutubu dhambi hizi za wakati uliopita!

Msomaji mpendwa, ni nini kinachoweza kufanywa au kusemwa watu wanapompinga Mungu na kweli yake moja kwa moja. Mungu anasema kitu kimoja nao wanasema,”Hapana si hivyo”.

Kutoka 20: 3-6

Sasa tumefikia fungu lingine la maneno ambalo waandishi hawa wa kileo wanalihesabu kuwa lenye umuhimu wa msingi wa mafundisho yao, si kuhusu kutubu dhambi za kitaifa na za mababu peke yake, lakini pia kuhusu laana na kile wanachokiita “roho za eneo”. Sehemu wanayoilenga hasa ni pale wanapozungumzia dhambi za mababa zikiwafikia wana hadi kizazi cha tatu na cha nne. Toka fungu hili, pamoja na Lawi 26:40, wanaanzisha usemi mpya ambao haupo kwenye Biblia. Wanaita dhambi hii, “dhambi ya vizazi”. Kwa usemi huu hawafanyi rejea kwenye sheria ya dhambi na mauti ambayo imekuwa ikitenda kazi katika kila mtu tangu anguko la Adamu, na kwa hiyo Kristo alikufa na kutusafisha na kutuweka huru. Hapana. Kutokana na fungu hili hufundisha kuwa kama kizazi kimoja au mtu akitenda dhambi au kuabudu miungu, basi dhambi hiyo na hukumu yake, huendelea katika kizazi kinachofuata, kwa njia ambayo itazuia baraka za Mungu na kuleta hukumu. Na kwa sababu ya Lawi 26:40, wanasema kwamba dhambi hizi za vizazi vilivyopita zinatakiwa zitubiwe! Wanasema mistari hii miwili toka Kutoka na Walawi, inahusu watu wote – Myahudi au Myunani, mtakatifu au mwenye dhambi – tangu Mungu alipoweka sheria kwa Israel pale Sinai, mpaka siku ya leo! Wanafundisha pia kwamba Kalvari haijabadilisha hitaji la kuzitubia dhambi za vizazi vilivyopita. Kama hatufanyi hivyo, basi dhambi za vizazi vilivyopita na hukumu zake, bado zinatuathiri na bado zinatufanya tukose baraka kamili za Mungu na pia hutupatia msingi wa kisheria wa Ibilisi kufanya kazi katika maisha ya watu na jamii zao! Lakini yote hii ni tafsiri isiyozekana ya mafungu haya.

Tumekwisha kuona tayari kiasi gani jambo hili ni kosa kabisa na utunzi. Tumeona pia jinsi ambavyo wanatumia vibaya kabisa Lawi 26:40. Sasa, tunapoendelea kutazama fungu la Kutoka 20, tunakuta hakuna amri kwa watu wa Mungu kutubu kwa ajili ya dhambi za mababa. Wazo hili wala halijatajwa katika kutoka 20. Mungu anatangaza kwa Israel kwamba yeye ni Bwana Mungu wao aliyewatoa Misri. Mungu anawaonya wasiwe na miungu mingine zaidi yake kwa sababu yeye ni Mungu mwenye wivu, ambaye huwapatiliza wana mabaya ya baba zao hata kizazi cha tatu na cha nne cha wamchukiao. Nguvu na uzito wa maana ya mstari wa tano (ang. Kumbu. 5:9), iko juu ya hao wamchukiao. Wale wanaondelea kumkataa Mungu na neno lake kwao, na wanaochagua kufuata dhambi za baba zao. Wale wamchukiao wamenaswa na kupotoshwa na dhambi za baba yao, na dhambi hii na uasi inaweza kuwa matokeo na nguvu inayoongezeka kwa kila kizazi kinachofuata na kinachochagua kumkataa – na kwa sababu hiyo, bila mashaka watahukumiwa. Lakini mtu anaweza kugeuka kutoka dhambi za mababa zake, na kama atafanya hivyo, Mungu anaweza kumsamehe dhambi zake na kumpokea pasipo hata kuhitaji kutubu kwa ajili ya dhambi za mababa zake.

Lakini ni muhimu sana pia kutambua kwamba haisemwi kuwa Mungu huleta adhabu au hukumu ya dhambi za baba kwa wana! Na Ezekiel 18 inathibitisha. Wana hawauchukui uovu au adhabu ya dhambi za baba zao, isipokuwa kama wamechagua kuendelea katika hizo. Wanapatilizwa dhambi za baba zao, ambacho ni kitu tofauti. Ni wazi kuwa ikiwa mwana amelelewa na wazazi ambao wanatenda dhambi na kumwasi Bwana, hapo mwana yu katika hatari ya mvuto wa maovu yao na baraka za Mungu hazipo katika familia. Kwa hiyo dhambi ya wazazi inakuwa mtego kwa mtoto na bila shaka atajaribiwa kufuata mfano mbaya, badala ya kumfuata Bwana. Kutoka 20 na Ezekiel 18 zinasimama katika makubaliano kamili mmoja kwa mwingine katika kutoa kielelezo kwamba watoto wanaweza kuvutwa vibaya na kunaswa na dhambi za baba zao. Lakini Mungu wakati wote hutuchukulia kama mtu mmoja mmoja na humruhusu kila mmoja kufanya mwitikio wake mwenyewe kwa Mungu. Kwa hiyo, hata kama dhambi za wazazi zitakuwa mtego kwa watoto wao, bado wana uhuru wa kuchagua – wanaweza kuchagua kuziacha njia mbovu za baba zao na kumgeukia Bwana. Hii imewekwa wazi na Ezekiel 18 na pia na kusihi kwa Mungu akiwasihi Israel tena na tena katika vizazi vyao vinavyofuatana waache uovu wao na uovu wa baba zao na kurudi kwake kwa moyo wao wote. Hakuwaacha tu watu wake kwenye dhambi za baba zao. Alilitumia neno lake kwa kila kizazi kupitia manabii wake, akiwataka watu wake wamrudie kuna mifano mingi ya jinsi hii, kama Isaya 1:18,19. Tunaona pia jinsi ambavyo Asa, Hezekia au Yosia (2 Nyakati 14:29 na 34) walivyoacha dhambi za waliotangulia na kumrudia Mungu, ndipo watu walipobarikiwa sana na Mungu. Uwepo wa Mungu ulikuwa pamoja nao tena, na baraka na ulinzi wake. Na hakuna wakati tunapoona mmoja kati ya Wafalme hawa kabla ya utawanyiko wakikiri dhambi za baba zao. Walitubu kwa ajili ya dhambi zao wenyewe, ambazo bila shaka zingekuwa zilezile kama za baba zao – lakini ilikuwa ni toba yao wenyewe tu ndiyo iliyotakiwa. Na walipofanya hivi, hapo hapo na kwa wingi Mungu aliwasamehe na kuwabariki. Na haya yote yanaendana na mstari 6 wa Kutoka 20 (ambapo tunaona kwamba rehema ya Mungu ni kuu mno kuliko hukumu yake kwa wale wampendao na kumtii), na katika Ezekiel 18, ambapo tunaambiwa kwamba mwana baada ya kufikiria njia mbaya za baba yake, anaweza kugeuka toka uovu huo na kujinasua kutoka dhambi za baba yake anapomgeukia Bwana, ambaye atawasamehe kabisa na asiwe na kinyongo chochote naye. Tunapozungumzia uhusiano wa mtu na Mungu, Mungu haziweki dhambi za baba yake juu ya mtu huyo wala hamuadhibu kwa ajili ya hizo! Mwana husamehewa na kubarikiwa pasipo kutubu kwa ajili ya dhambi za baba yake! Waalimu hawa wa siku hizi wanataka tufungiwe ndani ya dhambi za baba na wahenga wetu kwa njia ambayo hata katika Agano la kale haikujulikana, na kwamba kwa hakika haina uhusiano na Agano jipya.

Sina budi kusema kwamba fungu la kutoka 20:4,5 lina vitu ambavyo si rahisi kuvielezea, na siwezi kusema kwamba nimeeleza kwa utimilifu. Lakini kwa kuwa Biblia ndicho kitabu peke yake chenye fafanuzi nzuri kuliko zote juu ya Biblia, tunapoliangalia fungu hili katika mwanga wa mafungu mengine, ingawa tutashindwa kueleza kwa utimilifu, bado kuna maandiko mengi ya kutosha ambayo yameangalia, kuona kwamba yale yanayofundishwa na hawa waandishi wa siku hizi, ni kitu ambacho hakifundishwi na neno la Mungu. Tafadhali rejea kwenye makala ihusuyo “Laana” kwa ajili ya mafindisho zaidi kuhusu sura hii ya Kutoka 20.

Msemo wa “dhambi ya kizazi” umebuniwa na waandishi hawa wa kisasa kwa ajili tu ya kuunga mkono mawazo yao ambayo si ya kibiblia. Msemo huo haumo ndani ya Biblia; huutumia kuunga mkono mawazo ambayo hayapatikani ndani ya Biblia. Ni kweli kwamba maisha maovu na mfano wa wazazi na jamii yanaweza kushawishi na kuathiri wengine ambao wanaendelea kukua, na kwa njia hiyo kama ambavyo ingesaidia kufanya mioyo yao iwe migumu kwa Injili. Hii ni kawaida na hakuna jipya. Lililo jipya, ni haya mafundisho yanayosema kwamba anapomgeukia Bwana, na pia kutubu dhambi zake, mtu au jamii inahitaji pia kutubu dhambi za baba zao au vizazi vilivyopita.

Wanatafuta “mifano” ya “dhambi za vizazi” katika Agano jipya! Je, “uthibitisho” wa maandiko ni upi? Wanadai ni Mathayo 23:32-35 na 1 Thesalonike 2:16! Hutuambia kuwa mistari hii “huthibitisha” kuwa Agano Jipya hufundisha juu ya dhambi ya vizazi na kwa sababu hiyo tunahitaji kutubu juu ya dhambi za vizazi vilivyopita! Mimi sidhani hivyo. Mistari hii haitufundishi kwamba tunapaswa kutubu juu ya dhambi za wahenga wetu! Wanarejea kwa wayahudi na jinsi wanavyochagua kupingana na Mungu. Swala si kwamba wanalazimishwa kuendelea katika dhambi za baba zao, lakini ni kwamba wanachagua kufanya hivyo. Hii ndiyo sababu Yesu aliulilia mji wa Yerusalemu. Alikuwa anawategemea wampokee lakini wakachagua kutokumpokea. Hii inaweka msingi wa hukumu yao isiyokwepeka. Mstari mwingine wanaounukuu kama uthibitisho ni ule wa I Petro1:18. Lakini mstari huu wa ajabu unathibitisha kinyume na vile wanavyofundisha. Mstari huu unatuambia kile ambacho nimekuwa nikisema katika makala hii, kwamba damu ya Yesu Kristo, Mwana kondoo wa Mungu, ina uwezo kamili na inatosha kutukomboa kutoka mwenendo wetu usiofaa tulioupokea kutoka nyuma na kutoka mapokeo batili ya baba zetu. Tumekombolewa! Tumenunuliwa na kurudishwa kwa damu ya Yesu. Hakuna tena hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Mungu Asifiwe! Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki! Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea! (Rumi 8: 33,34).

Lakini mafundisho haya mapya yangetuletea hukumu sisi sote, yakituambia kuwa si sisi wala jamii tunazoishi ndani yake tuko huru kikamilifu toka hukumu ya Mungu mpaka hapo tunapokuwa tumetubu dhambi za baba zetu! Hili si jambo la kushangaza. Kwa sababu kama ukimleta mtu chini ya sheria, mtu huyo hana budi kuwa chini ya hukumu. Na hii ndiyo asili ya mafundisho haya.

Wanachanganya Kanisa na Ulimwengu

Ingawaje ni kitambo cha vizazi vingi, bado historia ya Waisrael inachukuliwa kama ni Mungu alikuwa akishuhgulika na mtoto mmoja mmoja. Ni taifa moja pekee na historia moja. (Kanisa ni mwili mmoja kiroho lakini linahusisha makanisa madogo madogo ya aina nyingi katika maeneo mengi mbalimbali pamoja na watu wake, wanaotokea katika mataifa mengi ya aina mbalimbali. Na hii bila shaka haishirikishi historia ya aina moja au maendeleo ya kiroho, kama ilivyo katika Agano la Kale – tazama nyaraka za Agano Jipya na Ufunuo sura 2-4.)

Sasa, ikiwa yeyote yule kama Akani (Joshua 7:1) au Sauli (2 Samweli 21:1) alifanya dhambi, hii ingeweza kuleta madhara kwa wote, watu pamoja na baraka za Mungu zingezuiliwa. Tena hayo mafundisho yao mapya yanasema, “Haya, unaona, kwa sababu watu hawa walifanya dhambi, Mungu alizuia baraka zake hivyo tunahitaji kutubu dhambi za nchi yetu!” Lakini kwanza, nchi yetu ipo mbinguni, na pili nyaraka hizo hazitufundishi eti kanisa linapaswa kuungama na kutubu kwa ajili ya dhambi za ulimwengu, kama vile nchi tunamoishi. Kinyume chake kwa urahisi tu, inamaanisha tu kuwa, iwapo watu wa Mungu wakitenda dhambi watapata madhara katika maisha yao au katika maisha ya kanisa (Rumi 8: 13, 1Kor 5:6, Ufunuo 2:5), na kama tulivyokwisha tangulia kutaja hapo juu. Agano Jipya linatofautiana na Agano la Kale, ndani yake kiasi kwamba, watu waliochaguo la Mungu katika Agano la Kale, wanawakilishwa na taifa moja linalojulikana na historia yake ni moja wakati ambapo, kanisa la Agano Jipya linahusika na watu wengi wa aina mbalimbali katika maeneo mengi mbalimbali.

Hawa walimu wanataka kulinganisha na dhambi ya Akani – jinsi dhambi ya mtu mmoja inavyoweza kuidhuru jumuia nzima. Akani alikuwa ni mmoja wa watu wa Mungu na alifanya dhambi; dhambi yake iliwanyima waisraeli – watu wa Mungu – ulinzi wa Mungu na baraka zake. Je, sasa wanataka kutufundisha kwamba, ikiwa mkristo atatenda dhambi sehemu nyingine ya ulimwengu kwenye kanisa fulani, ndipo Mungu huzuia baraka zake kwa wakristo wote ulimwengu mzima, hadi pale wote watakapogundua nani aliyetenda dhambi hiyo, na kisha kanisa lote ulimwenguni kote litubu kwa ajili ya dhambi ya mtu huyo? Kama ni hivyo basi, kanisa lote ulimwenguni kote litahitaji kujua na kutubu kwa ajili ya dhambi alizokuwa akizitenda mkristo mmoja mmoja au anazozitenda, kabla hatujaweza kuishi katika baraka zake Mungu. Mpendwa msomaji unaweza ukaona wewe mwenyewe, matatizo yanayosababishwa na hayo mafundisho yao, jinsi yanavyojaribu kupindisha maana ya maandiko ili kukidhi mawazo yao.

Wanachanganya mafundisho ya Biblia yahusuyo kanisa na ulimwengu. Na wala haupo mfano wowote katika Agano Jipya ambapo kanisa likiomba kwa vizazi vingine vilivyopita; na wala haliwakilishwi na nchi yoyote iliyopo duniani. Kanisa linahusu Roho iliyookolewa kutoka katika kila koo za makabila na mataifa.

Sasa katika makala hii nimekuwa nikitumia maneno mawili: “kuungama” na “kutubu”, kwa sababu maneno hayo yote mawili yamekuwa yakitumiwa kwa uhuru sana katika mafundisho haya ya kisasa kana kwamba yangeweza kutumika katika mazingira yale yale, lakini mmoja wa waandishi wao wenyewe anakubali wazi wazi na kwa usahihi, kwamba, hakuna njia yoyote ambayo watu wowote wa Agano la Kale kama vile Daniel au Nehemia, kwamba wangeweza kutubu kwa ajili ya dhambi za vizazi vilivyopita. Huwezi kutubia uovu wa aina yoyote ile ambao hujahusika nao. Kwa sababu toba ni badiliko na kugeuka kutoka katika uovu ulioutenda. Kwa hiyo, ingawa je, Daniel angeweza kutubu kwa ajili ya dhambi yoyote aliyoitenda, lakini yeye asingeweza wala asingetubu kwa ajili ya dhambi za baba zake. Ndiyo, asingeweza, kwa sababu, kwanza hazikuwa dhambi zake mwenyewe, (aliungama na kutubu kwa ajili ya dhambi zake yeye mwenyewe, hata hivyo, dhambi za kumwasi Mungu hazikuwa zake). Na pili, hakuna njia yoyote ile ambayo mtu yeyote anaweza kupokea msamaha toka kwa Mungu kwa ajili ya watu ambao wamekufa. Hivyo kwa kweli ingeweza kuwa ni unajimu na matendo ya tabia zisizo za ki-mungu.

Sasa, ijapokuwa walimu hawa wanaweza kukubali kuwa ni kweli, lakini bado katika yote mawili, yaani ndani ya maandiko yao pamoja na mahubiri yao, wanazungumzia kutubia dhambi za baba zetu, (jambo ambalo haliwezekaniki), au kuimwagia damu ya Yesu katika dhambi za mji au taifa na hapo hapo eti upokee upatanisho kwa ajili ya watu wa hapo (hii ni unajimu kama sio kufuru). Hakuna maombi yetu yoyote ambayo yanaweza kusababisha msamaha toka kwa Mungu kwa ajili ya watu waishio au waliokufa. Na bila shaka hatuwezi kuitumia damu ya mwokozi wetu kwa njia ya jinsi hiyo. Damu yake Yesu sio aina fulani ya Hirizi.

Sasa yale ambayo bila shaka tunaweza kuona Daniel pamoja na wenzake wangeweza kuyafanya ni kuumizwa juu ya dhambi za watu wa Mungu wanaomhusu. Upendo wake kwa Mungu na kwa watu wa Mungu kwa kawaida ungeweza kumpelekea kuumizwa sana, pale aonapo kwamba Waisrael wamemwasi Mungu, na kwamba watu wa Mungu wao wenyewe wameondolewa utajiri wa baraka zake.

Isitoshe, ule ufahamu wetu wa umoja pamoja na watu wa Mungu, ungeweza kutupelekea kuumizwa na kujinyenyekeza wenyewe mbele za Mungu, inapotokea kanisa haliishi tena katika urithi wake ambao Kristo Yesu alinunua kwa ajili yetu pale Kalvari. Badala ya kulihukumu kanisa, tunapaswa kujinyenyekeza wenyewe na kuiomba rehema zake zitusaidie wakati wa uhitaji na kwa hakika hii inaweza pia ikajulisha kuungama mambo mengine kama yalivyosababisha hitaji hili kubwa katikati yetu. Kwa kweli, Roho wa Kristo atatuongoza katika hiyo (Rumi 8: 26,27, Efeso 6:19), lakini hii haifanani kabisa na kutubu kwa ajili ya dhambi za wengine. Mtume Paulo aliwaombea watakatifu (Wagalatia 4:19) bali yeye hakutubu kwa ajili ya dhambi zao. Alitafuta Bwana kwa ajili yao, lakini baadaye alihakikisha wazi kabisa neno la kweli linawajia ili kuwaongoza wamrudie Kristo.

Kwa hiyo tunaona kwamba, kuungama na kutubu kwa ajili vizazi vilivyopita hata katika Agano la Kale, ili watu waweze kuzichukua baraka za wakati huo, hakufanywi na watu wa Mungu kwa niaba ya watu wasioamini – katika miji au taifa. Halikadhalika, aina hii ya maombi, hayakuwa na kawaida kwa watu wa Mungu, wanapozifikiria dhambi zao wenyewe, bali aina hii ya maungamo ilikuwa inalingana tu na wakati wa kuondoshwa kwa Waisrael na uahmishoni na inahusu Israel tu, kwa sababu ya agano zuri na Historia yake nzuri ya matendo alivyojishughulisha nayo kwao kutokana na Agano hili. Na pengine, lililo la maana zaidi ya yote, ni hili kwamba, aina hii ya maungamo ya dhambi za vizazi vilivyopita yalifanyika kabla ya kifo na ufufuo wa Kristo Yesu pale Kalvari, ambaye yeye pekee ndiye mpatanishi kati ya Mungu na mwanadamu, kwa kuwa yeye ndiye amezichukua dhambi za wanadamu wote kwa yeyote amwaminiye (1 Yoh 2:2).

Mafundisho haya mapya yanawakilisha kitu fulani cha tofauti kwa ukamilifu wa Neema ya Mungu ambayo imeelezwa katika kumhubiri Kristo na kuwa yeye pekee ndiye aliyesulubiwa.

Agano na Mataifa?

Kuna jambo lingine ambalo itakuwa ni vema ni kulielezea kutoka katika maandiko. Tayari tumekwisha taja kuwa wangetutaka sisi tuamini kwamba, tunapaswa kuomba kwa ajili ya miji na nchi tuishimo (ulimwengu) kama vile Daniel alivyofanya kwa Israel (watu wa Mungu). Na kwamba Mungu alikuwa na maagano na mataifa ambayo yaliruhusu aina hii ya maombi; wanawezaje basi, “kuruka” namna hii, toka kwa watu wa Mungu hadi kwa watu wasioamini? Wao wananukuu mistari kama Kumb.32:8 ambao unasema kwamba Mungu, “… alipowapa mataifa urithi wao, alipobagua wanadamu…”, na hii inarejea kwenye migawanyiko ya kijiografia katika dunia. Sasa haya mafundisho mapya yanasema kuwa Mungu angeweza hayo tu kwa misingi ya agano la kisheria na mataifa hayo na kwa hiyo wao pia walikuwa au wanaweza kuwa na uhusiano wa Agano na Mungu kama Israel walivyofanya nyakati za agano la kale, na kwa hiyo kanisa linaweza kuomba kwa ajili ya dhambi zilizopita na nchi wanayoishi? Inaonyesha kuwa huu udanganyifu haufahamu mipaka ya upotoshaji wa kweli! Yesu Kristo alileta jipya ili kuliondoa la kale (Heb. 7:12, 18,19,22; 8:13; 10:9). Lakini walimu hao wanaanzisha maono ya kale yao wao wenyewe, na hatua yake inalichana jipya. “Oho! Enyi wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga?” Hayo yote kwa kweli ni ubunifu wa ushirikina.

Tumekwisha ona kuwa maungamo ya Daniel yalihusu na uasi wa kurudiwa na Israel kinyume na Mungu, kinyume na mafunuo yake, maalum ambayo aliwapa; pia ni kinyume na agano ambalo alilifanya maalum kwa ajili yao kupitia Abrahamu na pale Sinai. Agano hilo haliendi sambamba na taifa lolote katika maandiko. Mungu amepanga na kuahidi zaidi na sio tu mgawanyiko wa urithi wa dunia hii. Kwa fadhili zake Mungu amepanga kwa ajili ya wokovu wa watu wote watakaomwamini kutoka kwa taifa au kabila la jinsi gani lolote lile watakalo. Hii ni uwazi wa ajabu kutoka katika maandiko ya neno la Mungu na tunafurahia katika hilo kwa mioyo yetu yote! Lakini hamna popote ambapo Mungu hata anapopataja, achilia mbali kuwataka, wakristo au yoyete yule ahusike katika hatua za ushirikina huo wa kuungama au kutubu kwa ajili ya dhambi za kitaifa za vizazi vilivyopita, kana kwamba hiyo inaweza kutupatia baraka za Mungu na wokovu kwa ajili ya miji na nchi yetu.

Ni wazi kabisa kutoka katika Neno la Mungu, kwamba Mungu ametupatia baraka na wokovu kwa watu wote kupitia kifo cha mwanae pale Kalvari. Tunaweza kuomba kwa ajili ya kueneza Injili ili kwamba watu wapate kusikia ujumbe wa Kristo na kwamba yeye kusulubiwa ili wapate kumgeukia toka katika dhambi zao, ambazo kwa uhuru kabisa atawasaheme.

Ule mstari halisi ambao mwandishi wao mmojawapo anaunukuu, kutoka katika Kumb. 32:8 pia unanukuriwa na Paulo Mtume katika Matendo 17: 24-31 (mstari wa 26). Hapa Paulo Mtume anaongea na watu wa Athene kuhusiana na ibada ya miungu yao. Hawaambii kuwa laana ya Mungu iko juu yao kwa sababu ya Kutoka 20:5, na kwamba wanapaswa kutubu kwa ajili ya ibada ya miungu yao uliopita kabla ya kubarikiwa na Mungu. Hapana, hasemi hivyo, isipokuwa anawaambia kuwa Mungu aliweka mipaka ya nchi yao ili kwamba watu wapate kumtafuta Bwana (mstari wa 27). Hauelezi chochote kuhusu uhusiano wa agano kutoka katika agano la kale, ambalo sasa linawahitaji wao watubu dhambi zao nyingi zilizopita za miji na nchi ya Athen, vita vyake, na ibada ya sanamu yake! Hapana! Isipokuwa yeye badala yake anawaambia kuwa, Mungu alifanya kama haoni katika enzi za ujinga wao, lakini sasa anawaagiza watu wote watubu. Ndipo anaanza kuwaelezea kuhusu Yesu na ufufuo wake.

Inafanana pia na katika Matendo 14:16, ambapo watu wa Listra walitaka kumtolea dhabihu Paulo na Barnaba, wala Paulo hakuwakaripia na kuwaambia kuwa walikuwa chini ya laana ya Mungu, kwa sababu ya ibada ya sanamu yao mbaya na hivyo walitakiwa watubu dhambi za mababa zao kwanza, kabla Mungu hajawabariki wao bali pamoja na nchi yao; Hapana! Aliwaambia kuwa yeye alikuwa ni mtu kama wao, na kwa uwazi kabisa lakini kwa fadhili aliwahitaji wageuke na kuyaacha mambo hayo ya ubatili wamrudie na kumwelekea Mungu aliyehai, ambaye Mtume Paulo anasema “….ambaye zamani zilizopita aliwaacha mataifa yote waende katika njia zao wenyewe, lakini hakujiacha pasipo ushuhuda; kwa kuwa alitenda mema akiwapa mvua kutoka mbinguni, akiwashibisha mioyo yenu chakula na furaha…”. Hii ingeweza kuwa ni fursa ya pekee kwa Mtume Paulo kuweza kuhalalisha mafundisho haya mapya; lakini badala yake, hafanyi chochote cha aina hiyo, wala hazunguki huko na huko akihubiri laana na hukumu kwa sababu ya dhambi za vizazi ambavyo watu wanahitaji kuungamia na kutubuia; mpendwa msomaji wangu; tafadhali angalia jinsi ambavyo maandiko ya Neno la Mungu yanavyowakilisha karibu ni kinyume kabisa cha picha halisi ya yale mafundisho wanayoyatengeneza wao.

Katika mipangilio ya kuhubiri Injili, Mungu haweki majukumu yoyote juu ya taifa kwa ajili ya dhambi za vizazi vilivyopita (Rumi 3:24). Kwa kweli Mtume Paulo anasema, Mungu alifanya kama haoni katika nyakati zao za ujinga, ni vema kuliko kuongelea kuhusu ujumla wa mibaraka za Mungu ambazo kwa fadhili zake Mungu ameendelea kuzitoa chini ya nyakati zote kwa watu wote.

Na hii haishangazi kwa sababu kinyume na hayo mafundisho yao mapya, Mungu hajajifunua mwenyewe kwa namna ya pekee kwa mataifa kabla ya Kristo, kama alivyofanya kwa Israel. Hajafunua kwa mataifa haki yake na tabia yake takatifu kupitia sheria zake za manabii, na alijitokeza kwa mafunuo maalum. Hajalianzisha agano pamoja nao, ambalo kwa hilo sasa aweza kuwahukumia. Hapana, mbali ya kutambua uasili ambao unapaswa kuwa ndani ya moyo wa mume na mwanamke, kumhusu Bwana wao (Rumi 1: 19,20), kimsingi, walikuwa hawajapata mafunuo maalum kuhusiana na tabia ya haki yake na matakwa ya haki yake; na kwa hiyo Mungu kwa ujumla alikuwa hawakabi kuhusika na yaliyopita (yeye aliyepewa machache, machache yatahitajika) kinyume chake, anaendelea kuwa mwema kwao na anawabariki. Lakini kama Mtume Paulo alivyosema, sasa anawaagiza wote watubu dhambi zao wao wenyewe, na kumrudia Mungu aliye hai! Haleluya! Hii ndiyo Injili!

Mstari maalum wanaoutumia ili kufunga mkono mafundisho (Kumb. 32:8), unanukuliwa na kuelezwa na Mtume Paulo, kufundisha kinyume cha mawazo yao!

Wanasema unapaswa kuungama na kutubu kwa ajili ya dhambi za “nchi yako” kwa sababu eti ya uhusiano wa Agano (!?) kati ya Mungu na nchi ile, kabla Mungu kwa hakika hajakubariki wewe na nchi yako. Mtume Paulo anasema kuwa, Mungu alijua kuwa mataifa yalikuwa katika ujinga kwa tabia yake na haki, na kwa hiyo katika wema wake na rehema yake alifanya kama haoni, zilikuwa ni kama vizuri kwao, lakini kwa sasa anawaagiza wote kutubu, kwa sababu ya wokovu unaotolewa katika Kristo Yesu!

Hii ndiyo neema, maajabu na wepesi wa Injili. Hebu tuipokee hazina hii, tuitunze na kuitangaza.

Sasa tunaweza kuona jinsi wanavyofanya makosa makubwa. Msingi halisi wa mafundisho yao umesimikwa juu ya makosa ya kuwabadilisha au kuwachanganya watu wa Mungu na wasioamini. Wanawajali wenye dhambi na wasioamini kana kwamba ni watu wa Mungu waishio chini ya Agano la Kale – ambapo kanisa linapaswa kuomba kwa ajili ya ulimwengu kama vile Danieli alivyofanya kwa ajili ya Waisraeli! Kwa hiyo wanatenda makosa mawili makubwa na ya kumsingi. Kwanza, wasioamini sio watu wa Mungu waliokombolewa na hawawezi kutendewa au kuhesabiwa kama hivyo katika mahubiri au kuomba (ijapokuwa kwa vyo vyote vile tunapaswa kuomba na kuihubiri Injili kwao). Jambo la pili, Yesu Kristo alipokufa pale Kalvari alilia “Imekwisha!” Hii ililijumlisha na Agano la Kale. Imekwisha, kwa kuwa Kristo ametukomboa kutokana na sheria (Rum 7:6). Torati na manabii vilikuwapo mpaka kipindi cha Yohana, lakini sasa Ufalme wa Mungu unahubiriwa (Mt 11:12,13; Luka 16:16) au angalau ingekuwa hivi. Hatupo chini ya Agano la Kale tena, lakini hapo ndipo wangependa kutuweka sisi kama wangeweza kufanya hivyo! Mbaya zaidi, yale wanayoyafundisha ni mtindo wa uchafu wa Agano la Kale. Tumekwisha kuona jinsi ambavyo mafundisho yao yote yalivyo; yanapatikana kutokana na tafsiri yao wenyewe ya kitabu cha Kutoka 20:3-5 na Walawi 26:40. Je huo ni ufunuo wa Agano Jipya? Hapana!

SEHEMU YA PILI

Tukiangalia kwa makini maandiko yasemavyo:

Injili

Kama vile ilivyokuwa huko Galatia, vivyo hivyo leo mafundisho ya aina hii yanapora mahubiri ya Msalaba, uweza wake na utimilifu wake. Hii ni kasoro ya aina ya kizamani sana ni ya kienyeji. Inapotosha ukweli wa Injili, na inaturudisha nyuma hadi kwenye mtazamo wa aina ya Agano la Kale; wakielezea kwa jinsi hiyo, kwa uhakika, inawakilisha mashambulizi dhidi ya Injili ya Kristo na kile alichokipata pale Kalvari. Inatuondolea mtazamo wetu mbali na Kristo na inalikuza Agano la Kale. Hali kadhalika inafunua ukosefu wa ufahamu wa kile kilichomo ndani ya Agano Jipya. Ili kuonyesha kuwa hivyo ndivyo ilivyo, litakuwa ni jambo la faida kwetu sasa iwapo tutayatazama maandiko yanasema nini juu ya baadhi ya mambo haya. Tumekwisha onyesha wazi kuwa Agano Jipya halina hata mfano mmoja wa aina hii mpya ya mafundisho.

Hebu basi tuone katika Agano Jipya linatufundisha nini katika 2 Kor 5:19, tumesoma kuwa,

“…Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao…”

Warumi 5:8 inasema, “…bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu tulipokuwa tungali wenye dhambi.”

Waefeso 2:11 nayo inatuambia, “…akawapatanisha wote wawili na Mungu, katika mwili mmoja kwa msalaba, akishaufisha ule uadui kwa huo msalaba. Akaja akahubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na amani kwao wale waliokuwa karibu.”

Hii ni mistari ya thamani na ya muhimu, kwa sababu inafunua moyo halisi wa Injili, msingi wa wokovu wetu na neema ya Mungu ya ajabu kwetu sisi katika Kristo Yesu. Tulipokuwa bado tungali wenye dhambi, kabla hata hatujaweza kufikiria juu ya Mungu au kujali juu yake au hata juu ya amri zake, kabla hatuja mkaribisha kwa njia yoyote ile; yeye mwenyewe Mungu Baba, kupitia mwanawe Yesu, alikusudia kutujia na kwa niaba yetu kupokea msamaha wa dhambi hizo katika maisha yetu na kuziondoa hukumu zake juu ya maisha yetu kwa ajili ya hizo dhambi zilizopita, (Rumi: 3:24-28). Hivyo ndivyo alivyofanya pale Kalvari. Pasipo gharama yoyote alizichukua dhambi zetu na kuziharibu nguvu zake. Hili halikuwa tu ni wazo la baadae isipokuwa hayo yote yalitokea kulingana na kusudi lake la milele na kufurahishwa kwema kwa nia yake. Mungu asifiwe!

Mungu alitimiza yote kwa niaba yetu pasipo hata kutaka tulipe gharama (ni bure). Ni kwa neema, na kwa sababu ya neema ya Mungu, watu wanasamehewa na kuokolewa. Ilifanywa kwa ajli yao, hata walikuwa wafu katika makosa na dhambi, (Efeso 2:4-9). Na sasa Mungu huwapa haki watu wasio wanyofu kwa imani peke yake (Rumi 5: 4,5). Na pasipo hata kujitahidi kwa watakatifu wenyewe ili kujaribu kupata msamaha na upatanisho kwa ajili ya wenye dhambi, miji au Taifa; kwa kutubu kwa ajili ya dhambi zao. Kwa maneno mengine, pasipo hata kuwataka watakatifu kuongezea chochote kile juu ya neema na kazi za Mungu aliyoipata pale Kalvari kupitia Kristo!

Tumekombolewa kutoka katika mwenendo usiofaa ambao tuliupokea kutokana na mila na desturi za mababa zetu, kupitia damu ya thamani yaa Yesu Kristo; hapa sio kwa kupitia maombi ya watakatifu wala maungamo yao, (1 Petro 1:18,19). Hatuoni haja yoyote ya kuendelea kuzichambua dhambi zilizopita, yaani za mababa zetu ili kwamba sisi tupate kupokea wokovu huu kamili na ili tupate kuwa huru kabisa! Ni nini au ni nani atakayetuhukumu, atakayetushitaki, au kutuweka katika vifungo? Je, ni dhambi za mababa zetu? Hapana! Damu ya Kristo imetukomboa! Kwa maana damu ya Kristo imetufaa kabisa na ni kwa wakati wote; na wokovu wake upo wazi na ni kamili kwa yeyote atakayetubu na kuamini. Baadhi ya hao walimu wao wa kisasa wanasema kuwa, eti mstari huu unaopatikana katika Petro wa kwanza unathibitisha mawazo ya dhambi za vizazi, na kwamba, kwa hiyo sisi twapaswa kuungama na kutubu kwa ajili ya dhambi hizo za mababa zetu! Lakini katika sura ile, Petro hawaelekezi kufanya jambo lolote la aina ya mawazo yao hayo. Ni wapi basi anapokazia hitimisho lake, kwamba tunapaswa kuomba kwa ajili ya hilo, na kutubu kwa ajili ya dhambi za mababa zetu? Kwa hakika, hapo anatufundisha kinyume kabisa cha dhana ya mapokeo yao. Yaani, hapo anatufundisha kwamba, damu ya Kristo imefanya kazi yake, ametukomboa sisi kutokana na mila na desturi za mababa zetu. Kwa hiyo, mapokeo na maelekezo yao, kwa hakika ni mapokeo yanayoendeleza mashambulizi juu ya utimilifu wa uhuru ambao Mungu ameutoa katika huyo Kristo kwa ajili ya wanaume na wanawake wote.

Ukweli huu, uhusuo wokovu wetu kamili unafafanuliwa vizuri zaidi katika Warumi 5:15-21, ambapo tunasoma kwamba, dhambi na hukumu iliyowajilia watu wote kwa sababu ya Adamu wa kwanza, sasa kwa Kristo ambaye ndiye Adamu wa pili ametuondolea pasipo malipo yoyote; bali ni kwa kifo chake pale Kalvari, akitupatia msamaha na haki kwa wote watakaomwamini. Kwa maneno mengine, tungeweza kusema kuwa dhambi zao zote zisingeweza kuwashikilia kwa kuwa Kristo amewaondoa mzigo wa uwajibikaji kwa ajili ya hilo, kama vile Isaya anavyotutaarifu, katika ile sura ya 53. Na hii ndiyo maana halisi ya 2 Kor 5:19.

Hii ni habari njema ya Injili na sasa wanaume kwa wanawake wanaitwa ili kuziamini habari njema hizi na kugeuka kutoka katika dhambi zao. Imani hii ndiyo wokovu wao; kwa sababu hiyo tunasoma kwamba, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, asiwahesabie makosa yao (kwa vile yeye mwenyewe angeyaondoa). Kwa hiyo, Yesu alimwambia mtu yule aliyepooza ambaye alipelekwa kwake kwa ajili ya kuponywa, (kama ilivyo katika Injili ya Luka 5), kwamba, dhambi zake zimesamehewa pasipo malipo (bure) kwa sababu tu aliamini. Katika Injili ya Yohana sura 8 anamwambia mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, kwamba, hamhukumu, isipokuwa aende zake na asifanye dhambi tena. Katika Injili ya Yohana 4, anatoa maji ya wokovu bure kwa mwanamke Msamaria – kwa hakika msamaha sasa uilikuwa ni bure, na Mungu mwenyewe alikuwa akipatanisha wanaume na wanawake na nafsi yake mwenyewe. Kwa sababu alikuwa akienda kuliondoa lile pingamizi kuu la dhambi, ambalo limewashikilia watu wote katika vifungo vya dhambi na mauti; kuanzia wakati ule wa Adamu. Misingi yote ya mambo ilikuwa inaenda kubadilika kwa sababu ya Kalvari – “… kwa maana manabii wote na torati walitabiri mpaka wakati wa Yohana…”, Mathayo 11:13. Katika Luka 13:1-5, Yesu analiweka wazi zaidi kwa hao anaoongea nao, kwamba hawapo watu wengine ambao wao ni watenda dhambi wakubwa kuliko wengine; bali wote wamekufa katika makosa na dhambi; hata kama kwa nje wanaonekana wanatenda dhambi nyingi au kidogo; hapo hakuna tofauti, hali ya kila mmoja wao ni (Rumi 3:10,12,23). Sio wingi wa yale wanayoyafanya watu, isipokuwa ni ile hali yao. Hali ya watu wote (wanaume kwa wanawake) ni moja, ni ya dhambi na kifo na kutengwa kutoka kwa Mungu. Jambo hili halikufunuliwa kwa uwazi zaidi ndani ya Agano la Kale, kwa sababu hapakuwepo na matengenezo kwa ajili ya hali hii ya dhambi katika wakati ule. (Gal.3:22-25 ; 4:3-5; Rumi 3:19-22; Heb 1:1-2 ; 9:6,9 ; 10:1 ; 4:9,10). Lakini kwa sasa, kutokana na kujidhihirisha kwa Yesu, ukaja ufunuo wa kudumu, wenye kina cha uozo wa mwanadamu, kwa sababu, Mungu sasa alikuwa akitoa matengenezo kamili juu ya hali hiyo na alikuwa akifanya hivyo bure nje ya upendo na neema yake isiyo na ukomo.

Yesu hakuja kuwahukumu kwa ajili ya dhambi zao ambazo alipaswa kufa kwa ajili ya hizo (Yohana 3:17; 12:4), bali kuwapatia wokovu bure wale wote watakaotubu na kuamini Injili. Hii ndiyo maana halisi ya ile mistari mikuu inayopatikana katika Yoh. 3:16 –18. Mungu alifahamu wazi kuwa watu wote walikuwa katika vifungo kwa dhambi na kwamba kifo kilitawala ndani yao kwa sababu ya dhambi. Alikuwa hawalaumu kwa jambo hilo kwa maana hayo yote yalikuwa ni matokeo ya dhambi ya Adamu, na yeye Yesu, alikuwa anaenda kuzibeba dhambi hizo zote pamoja na hukumu zake pale Kalvari. Kuendelea kung’ang’ania juu ya dhambi moja na kuukataa msaada wa bure wa msamaha na wokovu; jambo hili linawakilisha dhambi ambazo watu watahukumiwa nazo.

Kile ambacho kinafanywa na mafundisho hayo yao mapya ni kuzifufua dhambi zile ambazo Yesu alikwisha mwaga damu yake kwa ajili ya hizo, na wakati huo huo kuwataka watakatifu kuomba kwa ajili ya dhambi hizo! Walimu hao wa kisasa wangekataa hizo; lakini wao hawajali madhara ya mafundisho yao. Hii inatoa mifano pia ya jinsi wanavyotumia vibaya ile 2 Kor 5:19. Wao wanasema kuwa, huduma hii ya upatanisho ni sehemu muhimu ya huduma ya kanisa.

Ndiyo, kwa kweli ni sawa, lakini je, maana yao hasa ni nini? Wanaharibu maana halisi ya sura hiyo; pale wanaposema kuwa ni sehemu ya huduma ya kanisa, kuupatanisha ulimwengu (mji, au nchi inayotuhusu) kwa Mungu! Na ni kwa jinsi gani basi? Kwa kuungama na kutubu dhambi za Nchi “yetu” na kujitwalia damu ya Yesu kwa dhambi hizo? Lakini maana hii waitoayo, hatupewi popote pale na Mtume Paulo! Hasemi kuwa Mungu yupo katika kanisa na akiwaongoza watakatifu leo kuungama na kutubu kwa ajili ya dhambi za jumuia ili kwamba apate kuwasamehe! Isipokuwa yeye anasema kuwa, Mungu alikuwa ndani ya Kristo na katika huyo Kristo alikuwa akiupatanisha ulimwengu na yeye mwenyewe asiwahesabie makosa yao; sasa kwa nini kuzifufua dhambi ambazo Mungu hazihesabii kwa ulimwengu? Ili kwamba eti kanisa liweze kutubu na kuungama kwa ajili hizo? Huu ni utata na mkanganyiko mkubwa! Katika sura hiyo yote tokea ule mstari wa 14 mpaka wa 21 kimsingi inaelezwa yale ambayo Mungu aliyafanya kupitia Kristo pale Kalvari kwa niaba ya wanadamu. Imefanywa! Mungu amefanya! Imekwisha na wala hakuna yeyote awezaye kuongezea lolote lile juu ya hilo!

Katika ule mstari wa 18 anatuambia kuwa Mungu alitupatanisha na yeye mwenyewe kupitia mwanae Yesu Kristo; wala kamwe haikuwa ni kanisa lililofanya hilo kwa kupitia maombi ya kuungama na kutubu! Mafundisho hayo yanajaribu kuongeza au kupunguza utimilifu wa Kalvari kupitia ubunifu wa hizi kazi zao za upatanisho, ambazo kanisa lililazimika kutimiliza kupitia kile wanachokiita wao maombezi ya utambulisho. Lakini Paulo haungami wala kutubu kwa ajili ya dhambi za yeyote yule katika waraka huu! Hii ni nini basi “Neno” au “huduma ya neno ya upatanisho” ile ambayo mtume Paulo ameitaja katika mstari ule wa 18,19? Ni sawa kuwa anatuambia sisi, “…naye alitupa huduma ya upatanisho yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake asiwahesabie makosa yao”. Tangazo la ujumbe huu ni “Neno”au “huduma ya upatanisho” – kutangaza kwa watu kile ambacho Mungu amekifanya katika Kristo kwa niaba yao, ni ujumbe wa neema uletao amani, kuwa upatanisho wanaume kwa wanawake kwa Mungu. Tazama kwa makini kile ambacho Paulo amekifanya ndani ya waraka huu, tunaona kuwa hajaribu kupata upatanisho kwa ajili ya tabia za kimwili walizo nazo wakorintho kwa kupitia maombi ya toba kwa niaba yao.

Tunamwona Mtume Paulo akitangaza kwa wakorintho kile ambacho Mungu amekwisha kifanya ndani ya Kristo kwa niaba yao, na ili baadae waweze kuelewa kuwa yawapasa kuwa ni watu wa aina gani katika hali ya ukweli huu wenye utukufu; ndipo sasa anawaagiza kupatana na Mungu, “…kana kwamba Mungu alikuwa akiwasihi (sio kuomba maombi ya toba kupitia kwetu sisi)….tunawasihi ……mpatanishwe na Mungu”. Ametangaza neno la Mungu lenye neema kwao ili kwamba ikibidi wapate kurejea na kutubu.

Hebu basi tuangalie kwa ufasaha zaidi jambo hili. Ni kweli kwamba unaweza kuhuzunishwa hadi kufikia kutoka machozi na maumivu ndani ya maombi, pale tuonapo ndugu zetu wakitenda dhambi au wakienda mbali na Mungu, 2 Kor 2:4; Gal 4:19; kwa ujumla tunapaswa kuguswa na mambo yale yanayoumiza mwili wa Kristo na hivyo kuombeana mbele ya kiti cha enzi cha neema ya Mungu na wema wake upate kuwaongoza wale waliofanya dhambi wapate kutubu na kwamba rehema zake zipate kurejesha tena mioyo yao kwake. Lakini sasa, jambo hili lipo tofauti kabisa na hayo mafundisho yao ya kisasa. Wao wanatusihi tuyafanye yale wanayotufundisha, kwamba wanatutaka tutubu kwa ajili ya dhambi za dunia, yaani, dhambi za watu wasioamini! Lakini kwa chochote kile tunachoweza kuombea, tusisahau kabisa kwamba yupo mpatanishi mmoja tu kati ya Mungu na wanadamu, na huyo ndiye mwanadamu Yesu Kristo; na sasa hayo mafundisho yao ya kisasa yanapoteza mwelekeo wao katika ukweli huu.

Tunaliona hili mara nyingi katika Biblia kwamba neno la kweli la Mungu huja kwa mtu binafsi likimtaka kugeuka toka dhambini kwenda kwa yeye; na katika Agano Jipya hili ni neno lenye utukufu, limejaa neema na kweli, likiwataka waume kwa wake wokovu wa bure katika Kristo. Dhambi zao zilizopita haziwezi  kuwatenga wala kuwazuia katika kupokea wokovu. Mungu hawahesabii tena dhambi hizo zilizopita ndani yao (kwa sababu ya Kalvari). Lakini kwa hakika sehemu ya wokovu huu mkuu ni kwamba, watu wanapokea msamaha wa dhambi zao zote zilizopita kupitia damu ya Kristo, pale tu wanapokea habari hii ya upatanisho.

(Rumi10:9-10, ukisoma kwa makini katika mistari hiyo, utaona kuwa Mungu anamtaka mtu binafsi amwamini Yesu na kumpokea moyoni mwake ili aweze kuokolewa; na wala si vinginevyo).

Lakini ili kuendelea na ujumbe wetu; tatizo halisi hapa sio kwamba watu wanafanya wizi, kuua n.k. bali tatizo ni kwamba, kuhukumiwa kwao ni kuwa mtu haiamini habari njema na hachukui hatua ya kuondoka kutoka katika giza. Katika Injili ya Yohana 16:9 tunasoma kwamba, hivyo Roho Mtakatifu atakapokuja atauhakikishia ulimwengu kwa habari ya dhambi. Sasa ni jambo la maana sana kugundua na kuelewa kuwa, ni kwa nini auhakikishie ulimwengu kwa habari ya dhambi?

Kwa hatua ya kwanza, haiwi hivyo kwa sababu ya kudanganya, kuiba, uchawi, uzinzi na kuua, bali Roho Mtakatifu atawashawishi juu ya dhambi kwa sababu hawakuamini. Hivyo ndiyo sababu ya msingi inayowazuia watu kuokoka – kule kutokuamini kwao. Ufahamu kuwa, Kalvari imekwishaishughulikia dhambi pamoja na nguvu yake. Waache watu sasa watubu na kuamini Injili. Mafundisho hayo yahusuyo kutubu kwa ajili ya dhambi za wenye dhambi, yanashambulia na kudhalilisha ukweli – iwapo mtu atakuwa amejihusisha katika uchafu, ulevi au uchawi, atahitaji pia kupata ukombozi maalumu ili kuondokana na mambo hayo; katika namna ambayo sio lazima wote waipitie hiyo. Mambo hayo yanaweza na yanafanya madhara makubwa na uharibifu katika maisha ya mtu iwapo atayaendea na kuyafanya. Lakini jawabu la hilo sio, kwa wengine kuanza kutubu kwa ajili ya dhambi za hao, badala yake ni kuomba, kwa mfano, mlango wa kuingia Injili upate kufunguliwa kwa ajili ya watu hao – hilo tu linalotupasa kufanya kwa ajili yao.

Katika Agano Jipya tatizo kubwa lililokuwepo la kueneza na kuipokea Injili, haionyeshi kuwa ni “dhambi” ya watu, dhambi zile wanazozitenda watu! Isipokuwa ni kule kutokuamini kwao. Katika Injili, tunaona kuwa, ilikuwa ni watenda dhambi ndio waaliokuwa wakimiminika kwenda kwa Yesu: wanyang’anyi, makahaba, watu wachafu na wale waliopagawa na mapepo; na wala sio watu wenye dini; hawa watu walikuwa ndio wale ambao hawakumuamini! Ndani ya mji wake mwenyewe, Yesu hakuweza kabisa kufanya miujiza mingi, sio kwa sababu ya uovu wa mji ule, isipokuwa ni kwa sababu ya kutokuamini kwao (Mty 13:58).

Tunaona pia katika Matendo ya Mitume, kwamba, kimsingi haikuwa ni kwa sababu ya dhambi za watu kama vile uchawi wao, ulevi wao na uuaji, ambavyo viliwakilisha kuzuiwa kwa Injili. Kwa mapenzi ya Mungu mwenyewe, Mtume Paulo na wengineo walitembea moja kwa moja katika mazingira ya miji ya jinsi hiyo, kama vile mji wa Samaria na Efeso, na Mungu alifanya kazi ya ajabu huko (wala pasipo hata kuomba au kuhubiri kwamba mmoja anapaswa kutubu kwanza kwa ajili ya dhambi za mji ule). Tatizo lililokuwa hapo ni kutokuamini, ugumu wa mioyo kuelekea ukweli, mara nyingi kutoka kwa watu wa dini; haijalishi kama wao walikuwa ni Wayahudi au kutoka kwa hao waliojishughulisha na kuabudu sanamu. Unapoendelea kusoma Matendo ya Mitume utagundua kuwa tatizo halikuwa ni dhambi ya watu, isipokuwa ni ugumu wa mioyo yao kuelekea ukweli – kutokuamini (kwa ajili ya sababu yoyote ile iwayo). Ndilo litakalo wahukumu watu siku hiyo, sawasawa na kazi zao kama maandiko ya Neno la Mungu yaonyeshavyo – kwa uwazi sana; na watu wanapaswa kuambiwa hayo. Lakini kwa mujibu wa tangazo la Injili tunapaswa kuanza kueleza kwa watu wote ule msamaha wa Mungu utolewao bure kwa njia ya Kristo ambaye alifufuliwa kutoka kwa wafu kwa ajili ya haki yao. Kutokuamini na kutokupokea. Hiyo ndiyo dhambi ya wanadamu.

Katika uwazi wa ukweli huu wote na ufunuo, mitume wangewezaje basi kutubu au kuwaambia wengine ili watubu kwa ajili ya dhambi za wasioamini katika nchi na miji yao? Yesu Kristo tayari alikwishawafia kwa ajili ya dhambi zao, na amekwisha lipa bei ya upatanisho wao (1Yoh.1:2)! Msamaha wa wokovu tayari umekwisha patikana katika Kristo, watu wanapaswa sasa kuamini habari njema, na wao wenyewe, yaani wao binafsi, ndio wenye dhambi zao. Kristo aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, na sasa je, tunafikiria kuongelea chochote juu ya kazi yake aliyoimaliza kwa kutubu kwa ajili ya dhambi hizo mbele za Mungu na kuomba msamaha kwa damu ya Yesu Kristo –wakati ambapo damu yake iliyomwagika pale Kalvari tayari imepokeo hayo?

Je, mateso yetu tunayo yapata tuombapo na kutubu yanaweza kutupatia msamaha zaidi kwa ajili ya wenye dhambi? Au tunadhani kuwa toba yetu kwa ajili ya dhambi zao kwa namna nyingine, labda sasa inamwezesha Mungu kuibariki mikoa na miji yetu pamoja na watu wake kwa Injili? (Watu wanaweza kudhani kuwa wao ni kama Daniel, wafanyapo hayo, lakini kwa masikitiko makubwa na kwa ubaya zaidi wamekosea). Ni nini? Mungu aliwasamehe waume kwa wake bure pale Kalvari; kisha eti watakatifu watubu kwa ajili dhambi hizo hizo ndani ya maombi yao ili kwamba Mungu apate kuwasamehe na matendo yao maovu? (Afanye hivyo kwa mara nyingine tena?). Na kwamba hii eti imzuie Mungu kuibariki miji au mikoa ili kwamba wenye dhambi wenyewe wapate tena kuzitubia dhambi hizo hizo na kupokea msamaha pia. (Je, mara nyingine tena?). Ni mchanganyiko wa jinsi gani huu? Ni aina gani ya mchanganyiko wa mawazo yasiyo na afya ya Agano la Kale na Jipya, ambayo yanaweza tu kuwadanganya watu kuhusiana na ukweli? Linaloshangaza zaidi, ni ule ukweli kuwa baadhi ya wahubiri wanasafiri huko na huko katika miji na kuhubiri hadharani kwa watakatifu pamoja na wenye dhambi, wakiwaeleza kwamba ni lazima watubu kwa ajili ya dhambi za nchi zao badala ya kuwapatia ukweli wa Injili wale wasioamini – kuwapa pia ujumbe wa Kristo na kwamba yeye ndiye aliyesulubiwa, kwamba Kristo alikufa na amefufuka kutoka kwa wafu na ameziondoa dhambi zetu zote, kwa ajili ya kutupatia msamaha na haki!

Wanatujia kwa mtindo wa baadhi ya manabii wa Agano la Kale, kama vile Yona au Yeremia wakiitangaza hukumu ya Mungu juu ya Taifa kwa ajili ya dhambi zake; wakati ambapo tumekwishaelezwa kwa uwazi kabisa kuwa nyakati za zamani Mungu aliongea na baba zetu kwa vinywa vya manabii; nyakati hizi za mwisho ameongea nasi kwa njia ya Mwana wake. Waebr.1:1,2. Sio tu kwamba Mungu amemchagua Mtu wa tofauti kabisa na wapokee mtu halisi wa kutuunganisha; bali ni kwamba ujumbe na huduma sasa ni mpya kabisa kwa sababu ya Mtu mwenyewe aliyechaguliwa na Mungu – Yesu Kristo, na kile alichokwisha kukifanya! Torati ilitolewa na Musa, lakini neema na kweli zilikuja kwa njia ya Kristo Yesu. Lakini hawa wahubiri wengineo wanahubiri kitu cha tofauti kabisa, na kitu kingine ambacho kipo jirani kabisa na torati na hukumu kuliko Injili na neema. Hata kama katika suala la Yona, yeye aliwaambia watu wa Ninawi wao wenyewe watubu, (wao binafsi). Hakuwataka kutubu kwa ajili ya dhambi za watu wengine katika mji ule! Na bila shaka Yona hakutubu kwa ajili ya dhambi zao.

Hebu niseme hapa, kwa vyovyote vile tunaweza na pengine tumehuzunishwa na yale yanayoendelea kufanyika katika jamii zetu au jamii na kwa hiyo tunaweza kuomba kuhusiana na vitu vya namna hiyo ambavyo ni vya wazi na vinavyotuhuzunisha na ambavyo vinaweza kutumika pia kama vizuizi vya watu kuisikia na kuipoke Injili. Na kwa hakika, tunaweza pengine kufikiri kuwa mambo yameenda mbali zaidi kiasi kwamba tunafikia hatua inayoonyesha kuiva kwa hukumu ya mwisho ya Mungu juu ya dunia. Na kwa hivyo, hiyo inaweza kutushurutisha kuomba kwa bidii sana, kwa ajili ya hali na huduma ya kanisa kwa ulimwengu huu uliopotea na wenye machukizo, hivyo kutangaza kwa bidii haja ya waume kwa wake kutubu. Hata hivyo, hiyo nayo tena hailingani kabisa na haya makubaliano ya kisasa yanayopenda kututaka sisi tufanye; katika kutubu kwa ajiliya dhambi za ulimwengu na katika jamii yenye kushutumiwa kama baadhi ya manabii wa Agano la Kale na wakiwasihi wauamini kutubu kwa ajili ya dhambi za jamii yao, kana kwamba jamii ni kama Israel ya Agano la Kale. Tunapaswa kuendelea kuhubiri Injili ya Yesu Kristo hadi mwisho utakapotujia.

Watu wanapokea msamaha na wokovu ambao tayari Kristo amekwishaununua kwa ajili yao, pale wanaposikia na kuamini habari njema. Lakini kabla watu wenyewe hawajatubia dhambi zao na kusikia habari njema, maombi yetu wala toba haviwezi kumshawishi kusamehe dhambi hizo, au kuleta upatanisho kwa ajili yao au kwa ajili ya nchi yao. Kuyafikiria hayo au kuyatenda, huu ni ushirikina wa kidini na wala sio vinginevyo! Hayana msingi wowote katika neno la Mungu. Ni sawa, Mungu amewasamehe dhambi zao katika Kristo kwa sababu ya Kalvari, lakini hata kama ni hivyo, hiyo haileti manufaa yoyote katika maisha yao mpaka tu pale watakapotubu na kuaimini Injili.

Kwa hiyo, hebu basi kwa hakika tuombe, ili kwamba Mungu atume watenda kazi wake ili Neno la Mungu lipate kuletwa kwa waume kwa wake na kuwaongeza katika kanisa lake. Tuombe kwamba Mungu afungue mlango wa usemi kwa wale wadumuo kwa jina lake, kwamba Injili hiyo ipate kuifikia mioyo ya watu wengi na kuwarejesha kwa mwokozi.

Ni jambo moja la kuombea nalo ni kwamba Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake (Luka 10:2); au kuwawezesha watumwa wake kuihubiri ile siri ya Injili kwa ujasiri (Efeso 6:19), au kwamba aweze kufanya maajabu kupitia watu wake ili wasioamini waweze kufikiwa (Mtd 4: 29,30); au kuhuzunishwa kwa sababu ya ugumu wa mioyo ya wale tunaowajua na wengineo pia na kwa hivyo kuomba ili kwamba Mungu aweze kuwaokoa (1 Tim 2:3,4; Rumi 9:1-3; 10:1); au kujinyenyekeza wenyewe na kuomba na kuombea katika kiti cha neema kwa ajili ya rehema ya Mungu iweze kuwafikia na kurejesha mioyo yao kwake pale ambapo wengine hutenda dhambi au kupotelea mbali (Gal. 4:19). Hayo yote ni mambo ambayo tunaweza na tunapaswa kuyafanya; lakini badala yake tunaona ni jambo la kinyume kabisa, pale tunapoanza kutubu kwa ajili ya dhambi za wenye dhambi na wakati huo huo kufikiri kuwa labda tunaweza kupokea msamaha na upatanisho kwa ajili yao na kwa nchi yetu pia!

Ni mchanganyiko wa kimawazo na upuuzi wa jinsi gani huu! Tumepotelea mbali kiasi gani na Biblia na mawazo yake. Kwanza, eti tuombe kwa jambo ambalo tayari Mungu amekwisha lifanya – kwa mfano, amewasamehe watu katika Kristo, na hii ameifanya bila malipo, bure – na kisha kujaribu tena na kusababisha msamaha huu ndani ya maisha yao kwa njia ya ujumla isiyofaa, kwa mfano, kwa kupitia maungamo na toba ya ushirikishwaji! Je, tunamjaribu Mungu kwa kulikataa neno lake na kupinga ukweli wake? Je, sio kwamba ni watu kwa makusudi kabisa ndio wanaoupinga ukweli wa Mungu lakini bila mashaka yoyote yale, hayo ni matokeo na mambo yaliyo sababishwa na mafundisho; pale wanapoongezea maombi yao ili kupata msamaha kwa ajili ya wenye dhambi.

Kwa ujumla, wanaushambulia ukweli huu, kuwa msamaha ulikwishapatikana kwa ajili ya wanaume na wanawake katika Kristo, kadhalika kwa kufanya hivyo wafanyavyo, wanapotosha ukweli juu ya asili ya dhambi na ukamilifu wa msamaha wa Mungu ndani ya Kristo, wanapofikia kuwa ni dhambi mbaya kama vile uchafu, uchawi, n.k. ambavyo ndiyo inayozuia Injili kuenezwa katika mkoa, kuliko kutambua kuwa:

1. Watu wote wamekufa katika makosa na dhambi.

2. Kristo amekwishazishughulikia dhambi hizo kikamilifu na bure na kwa hiyo kimsingi ni kutangaza habari njema kwamba watu wameletwa katika uzima na toba; kuliko kutujia na kuihubiri hukumu juu ya dhambi za watu kama ilivyokuwa kwa baadhi ya manabii wa Agano la Kale; na tena papo hapo kuwataka watu watubu kwa ajili ya dhambi za watu wengine, hata kama ni mjini au nchi na kwamba.

3. Ni kule kutokuamini, hiyo ndiyo dhambi ambayo watu watahukumiwa nayo na ndiyo inayowazuia watu kupokea msamaha na wokovu.

Ni ipi basi iliyo njia ya Mungu ya kuleta ukweli wa msamaha katika maisha ya watu? Ni kwa njia ya kuhubiri Injili – Kristo ndiye aliyesulibiwa – akiwataka watu kutubu na kuamini Injili. Hapa, tunaweza labda wote kusema kuwa hii ni wazi zaidi, ni pale watu wengine wanashindwa kuona kuwa mafundisho hayo mapya, yanaondoa ukweli uliopo kutoka katika Agano Jipya na kujaribu kutubatiza ndani ya fikra za kiagano la kale. Lakini hata hayo mawazo yao nayo, hayajatafsiriwa kwa usahihi. Kwa hiyo, ulinganifu huu unawapa wasio amini sura potofu ya Injili.

Injili ina maana gani? Ina maana kuwa ni “Habari njema” au “Ujumbe mwema”. Bwana asifiwe! Hivyo ndivyo anavyouelezea ujumbe wa Agano Jipya kwa wenye dhambi! Na msisistizo wake ni “kuihubiri Injili”. Katika Biblia zetu kuhubiri Injili inatafsiriwa kwa neno moja la kigiriki (uangelizo), ambalo linaweza kutafsiriwa zaidi kama “kuelezea, kutangaza, au kuhubiri habari njema”. Tangu mwanzo, Yesu alipofika hapa duniani, malaika walitangaza ujio wake kuwa ni habari njema yenye furaha kuu, (Luka 2:10). Yesu mwenyewe anaianza huduma yake kwa kutangaza habari njema ya ufalme wa Mungu, (Luka 4: 43), kisha anaendelea kuihubiri habari hii njema kwa wakati wote wa huduma yake, (Luka 8:1). Na anawaamuru wanafunzi wake kuitangaza kwa kila kiumbe. Na katika Agano Jipya lote, Neno hili kweli, linafananishwa kama ni habari njema, Efeso 1:13, na linatangazwa kwa wote – Kolosai 1: 5,6; 2 Tim 4:17. Na katika Injili hiyo, Mtume Paulo wala hakuona aibu kuitangaza kwa sababu ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye, (Rumi 1:16). Mtume Paulo yupo wazi na dhahiri kabisa na jambo hili anawaambia Wakorintho kwamba, “…Kristo hakunituma ili nibatize, bali nihubiri habari njema, wala sio kwa hekima ya maneno, msalaba wa Kristo usije ukabatilika.” (1Kor: 1:17). Hivyo alidhamiria asijue kitu chochote kingine, isipokuwa Yesu Kristo naye amesulibiwa. Kote alikokuwa akizunguka alieleza hayo. Kwa sababu yeye anaeleza kuwa, mahubiri ya msalaba ni uweza wa Mungu kwa hao wanaookolewa (1 Kor 1: 18-22). Hivyo, kwa nini basi watu hawakomi kutujia nakuhubiri kwa mtindo wa baadhi ya manabii wa Agano la Kale wakitangaza laana na hukumu juu ya miji na nchi kwa sababu ya dhambi. Kwa nini pia hawakomi kuongezea ujumbe wao wenyewe juu ya Injili na ambao unatolewa tu kulingana na matakwa na busara zao wenyewe ambao kwa huo huunyang’anya ukweli na uweza wa Injili mioyoni mwa jamii. Kwa nini wanahubiri Injili hii nyingine?!

Katika magazeti ya aina mbalimbali na kwenye mikutano ya hadhara, badala ya kutuhubiria Kristo, wao wanajaribu kudhihirisha maovu ya jamii na kisha kuwaambia watu watubu kwa ajili ya dhambi za jumuiya ili kusudi Mungu apate kuiondosha laana na hukumu kutoka katika mikoa yao. Aha! Ni upuuzi wa jinsi gani huu jamani! Aha! Ni madanganyo gani ya jinsi gani hayo? Aha! Jamani, ni huzuni ya jinsi gani hiyo? Tangaza jambo hili juu ya paa la nyumba, ili kila mmoja apate kusikia na kuelewa ya kwamba Yesu amekwisha kuziondoa laana zote na hukumu zake kwa niaba yetu sote. Sasa, tunapokea msamaha na wokovu bure iwapo tu, tutaamini na kutubu – dhambi zetu wenyewe. Toba yetu tuifanyayo kwa ajili ya dhambi za watu wasioamini, haiwezi kutusaidia kupata aina yoyote ya upatanisho na Mungu wala msamaha, zaidi ya lile ambalo damu ya Kristo imeupata pale Kalvari. Mty 13:38,39; Rumi 5:18; Kol 2:13-15.

Katika mahubiri ya mwanzoni yaliyonakiliwa na Mtume Paulo katika Matendo ya Mitume 13, anawaambia kwamba, Mungu ametuma, “Neno la wokovu huu” kwao, (Mstari wa 26). Hawaombi Wayahudi watubu kwa ajili ya ugumu wote wa viongozi wao waliopo kule Yerusalem na sehemu nyinginezo; hali kadhalika hawaambii wacha Mungu wasio wa kiyahudi kutubu kwa ajili ya dhambi za kule Antiokia, kusudi kwamba Mungu apate kuwabariki pamoja na mikoa yao! (Hebu niseme hapa kitu kidogo; ijapokuwa ni kitu kingine kidogo pale inapotokea mtu wa Mungu anakuja kulionya kanisa linapaswa kujisafisha lenyewe; basi inapotokea jinsi hiyo, ndipo tunayo mifano ya kutosha ndani ya Agano Jipya).

Kutoka katika maandiko mengi ya Neno la Mungu, tunaona kuwa kiini cha Injili hii ni, “Kumhubiri Yesu Kristo ” kwa watu, Mt 5:42; Mdo 8:12,25; 11:20, na kuutangaza ufufuko wake kama msingi na uthibitisho wa msamaha wa Mungu na wokovu. Mtd 2: 22,23; 4:410-12; 5:30,31; 10:40-43; 13:30-33; 17:18. Hii ndiyo Injili, huu ndiyo utume wa mfano wa Agano jipya. Ni kifo na ufufuo wa Kristo ndiyo kiini na uzima halisi wa ujumbe wa Injili, kwa sababu watu wamepata msamaha kutokana na hilo tu. Hatari kubwa inayoonekana na hapo, ni pale mtu mwenyewe (binafsi) anapokataa kuamini kuzipokea habari njema. Mtd 13:40, 41-46. Lakini Injili hii inaleta ujumbe wa amani mioyoni mwa waume kwa wake, Mtd 10:36. Ni Injili ya Neema ya Mungu, Mtd 20-24; na inatangazwa kuwa ndiyo Injili ya wokovu wetu, Efeso 1:17. Ni Injili halisi na ni yenye neema ya ajabu inayotupatia uweza wa uzima wa milele, 2Thes 1:9,10. Ni Injili yenye utukufu wa kweli 1Thes 1:11; kwa hakika, Injili ni Injili ya Mungu, 1Thes 2: 2,9, na ya Mwana Wake, Bwana wetu Yesu Kristo – 2 Kor 2: 12; 9:13?! Lakini watu sasa, wanaibadili na kuifanya ni ujumbe wa sheria, laana za ushirikina.

Kutokana na maandiko ya Neno la Mungu yote hayo, tunaweza sasa kuona kuwa ujumbe wa Injili ni tangazo la neema na rehema za Mungu isiyo nakifani kwa wanadamu wote ambayo walipatiwa kabla ya misingi ya ulimwengu huu, (2 Timotheo 1:19), na sasa inadhihirishwa wazi kwa kufufuliwa kwake mwokozi wetu Yesu Kristo – Mwanae. Kwa sababu hiyo, wao pia ni “habari za furaha”. Na huu ndio ujumbe, huu ndio mkazo wake kwamba kwa kadri tupatavyo nafasi (fursa) twapaswa kulitangaza hilo kwa wanadamu wote – kwamba tunapaswa kutubu na kumwamini Kristo ambaye amewakomboa kutokana na dhambi na hukumu; na kule kutokuamini ni dhambi kuu inayostahili hukumu ya binafsi – ambayo kwa kweli ndiyo watakayohukumiwa kwayo.

Sasa inaweza kusemwa kuwa haya yote tayari yaeleweka lakini ni ukweli na Injili hii ndivyo vilivyopotoshwa (Gal1:7), na imetiwa giza kwa mafundisho mengineyo ya kisasa. Wanatuletea ujumbe wenye laana na hukumu wanawahusisha watu mizigo ya uongo; wanawaelekeza watu kwenye mambo yasiyofaa kabisa yasiyo ya kibiblia kwa makusudi na uchunguzi usio na mwisho wa dhambi na maovu katika jumuia zao, miji na nchi zao. Kisha wanaweka matangazo ya uovu huu ndani ya nyaraka za maombi yao na mara zote wanajisikia kuwa kwa hakika wanapata maendeleo fulani pale wanapofanikiwa kuzigundua nyendo fulani za kiuchawi na unajimu ambapo baadae wanaendelea kufafanua na kutoa mifano yenye ujumbe wenye kupotosha maana katika maandishi yao. Wanakimbilia kuijaza mioyo ya watakatifu na akili zao kwa mambo hayo yasiyofaa na hatimaye hupenda kuishikilia mioyo yetu pia, kwa kututaka tutubu na kuomba juu ya maovu haya kana kwamba ni dhambi zetu wenyewe (binafsi) na kuiweka damu ya Yesu katika mazingira ya jinsi hivyo ili kuleta upatanisho ili kwamba laana ya Mungu na hukumu zipate kuondolewa. Hayo yote ni matendo ya ushirikina zaidi kuliko hata ilivyo Injili yenyewe. Ni vitendo vya kuwabatiza watu katika mazingaombwe yenye mawazo ya kidini ambayo huwaondoshea mbali ule ukweli uliomo ndani ya Kristo.

Inaonekana wazi kuwa siku hizi yapo makundi ambayo yanatafuta njia mpya ya kuieneza Injili kwa “mafanikio” zaidi, lakini matarajio yao nayo ni ya kupita kiasi, kwa ajili ya mafanikio na ufanisi pamoja na utayari wa kupokea kwa urahisi (mambo yao) uzoefu wao usio wa kawaida; hata kama ni vipawa kama inavyoitwa; au aina tofauti ya maono – imewapatia kwa haraka roho zidanganyazo. Hivyo wanapenda kuzingatia maandiko machache ya neno la Mungu, yanayoonyesha kuwa pengine yanaweza kuunga mkono mambo ya kihisia, wakati huo huo wakiukataa ushuhuda mzima wa maandiko ya neno la Mungu; hivyo katika kufanya hivyo wanawasilisha kitu kilicho tofauti na Injili. Hata hivyo Injili tunayohubiriwa hailingani na matakwa ya kibinadamu (Gal.1:16), mwanadamu hawezi kuibuni, wala hawezi kuibadilisha, wala hawezi kuongeza chochote juu yake au kugundua mandari mpya ya Injili. Ni Injili ya Mungu na ni ya kudumu.

Ingawa hao wanaoamini kanuni hizo za kisasa, wanatumia pesa nyingi, muda na nguvu nyingi katika kukuza mawazo yao na kujaribu kuonyesha jinsi gani mipango yao imeweza kufanikiwa ulimwenguni, lakini bado uthibitisho wake sio kamili na wala sio wa mwisho. Kinyume chake, ndio sababu makala hii imeandikwa. Katika nchi nyingine tofauti na zile nyingine, mafundisho haya ya kisasa yanasababisha kuchanganyikiwa na ghasia bila kugeuza mageuzo ya mkondo wa uovu kwa namna yoyote ile. Na katika maeneo mengine mengi hayaleti faida yoyote ila isipokuwa ni kuwafadhaisha watakatifu kutoka katika wito wa kweli. Wanachukua mahala pa Injili kuihuibiri kwa watu wote sehemu za hadhara kwa wasioamini na kwa watakatifu makanisani; matokeo yake ni kuwa, akili za wote, watakatifu pamoja na wapagani zinajazwa mawazo yenye maagano ya kisheria, hukumu na laana, ambazo huwaongoza kuingia katika aina ya ushirikina na toba isiyo na manufaa na vijitabia vya udanganyifu. Injili ya Bwana wetu Yesu Kristo hapo inabadilishwa.

Siamini kuwa watu wanayafanya hayo kwa makusudi, wala sisemi kuwa walimu hao sio watu wa Mungu. Mtume Paulo aliwaandikia watu wa Mungu katika makanisa kule Galatia na Korintho, wao waliamini katika mambo ya msingi ambayo sisi sote tunayaamini kuhusiana na Kristo na damu yake. Lakini wao baadae walipokea vingine, nyongeza ya mafundisho (Galatia) au walizingatia zaidi katika mambo ya nje wakiwa na nia ya kimwili kwa ajili ya kupata uwezo wa madaraka na utukufu (Wakorintho). Paulo amewaandikia akijaa huzuni ya kweli kwa jili yao, anapowaona wakiwa nje ya Imani kwa Mungu na kweli yake ndipo anawaonya kuwa, wanakaribia kuiacha Imani ya kweli, ambapo Kristo kwao sio wa faida tena, (Gal 3:4 ;4:11. 20:5:4). Anawaonya wakristo wa huko Korintho kuwa, kutokana na tabia zao za kimwili na kupeana utukufu wao kwa wao, wapo ukingoni kabisa kuelekea kudanganywa na shetani katika kumpokea Yesu mwingine, roho nyingine, na Injili nyingine; kwa sababu hata shetani hujigeuza ili afanane na malaika wa nuru, basi sio neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki. Kwa ajili ya hilo wakorintho walikaribia ukingoni mwa kudanganywa! (2 Kor. 11:1-20). Ikiwa mambo yaliweza kuwa hivyo katika kanisa la mwanzo; haitatushangaza sisi leo, kuona yanatukia pia ijapo kuwa yatatuhuzunisha sana. Na mambo hayo yanatokea siku hizi – watu wamo ukingoni kabisa kupokea Injili nyingine, Yesu mwingine na Roho mwingine – inawezekana kuwa tayari wamekwisha kuzipokea! Basi na hii makala ndogo hata kama haijawa kamilifu, ni kilio cha kurejea kwa wepesi uliomo katika Kristo, na kwa tangazo la umilele, Injili ya Mungu isiyobadilika, ambayo ni uweza utupatiao wokovu, ambao hutolewa bure kwa wanadamu!

Hebu tujikumbushe, ni nini mafundisho haya yasemavyo; ili kwamba asiwepo mtu atakayeelewa vibaya yale tunayoyasema hapa.

Mafundisho hayo yanawaambia wakristo kuwa wanalazimika kuungama na /au kutubu kwa ajili ya dhambi (zilizopo na zilizopita) za wenye dhambi wanaowazunguka katika miji na maeneo yao pamoja na nchi yao. Na hata kuungama kuwa wamemtenda Mungu dhambi za kwa ajili ya dhambi hizo. Wanapaswa kufanya hivyo ili kupokea msamaha wa Mungu na kuleta upatanisho kwa ajili ya nchi; kwa maneno mengine, wanataka kutuambia kuwa, kanisa linapaswa kutubu kwa ajili ya dhambi za ulimwengu na hata kuziungama dhambi hizo kana kwamba ni zao binafsi ili wapate msamaha wa Mungu! Vinginevyo eti laana ya Mungu na huku yake itaendelea kubakia juu ya nchi. (Mafundisho haya yanaweza kutofautiana kidogo kati ya nchi na nchi).

Sasa tunaelewa kuwa, kumbe Mungu hutazama mioyo, na bado anasikia kilio cha mioyo yetu hata kama ufahamu wetu na maneno yetu katika maombi tuombayo hayako sawa, lakini hiyo siyo sababu ya kuruhusu akili zetu zijawe mawazo ambayo kwa hakika siyo ya kibiblia katika kutupofusha ili tusione ukweli kama ulivyo katika Kristo Yesu. Hakuna lolote lile ndani ya Agano Jipya ambalo lingeweza kutuongoza ili tufikiri au kuamini lolote lile la mawazo hayo.

Maombi Katika Agano Jipya

Agano Jipya linatufundisha nini kuhusu maombi? Tunaipata mifano gani pale? Hebu basi tuanze na mwana wa Mungu mwenyewe. Katika Yoh.17 Yesu anaomba mambo ya ndani kabisa moyoni mwake, hata tunaweza kusema kuwa ni mambo fulani ya moyo wa Mungu yanafunuliwa katika maombi hayo. Tukiangalia kwa makini sana katika maombi hayo tutagundua kuwa, Yesu haombi mahitaji mengi hapo, isipokuwa moja ya mambo anayoyasema ni hili:

“Mimi siuombei ulimwengu bali hao ulionipa…”

Je, umewahi kumsikia mtu yoyote yule akihubiri juu ya jambo hili? Ni mstari ambao mara nyingi unapuuzwa, lakini unayo maonyo yenye maana yaliyozungumzwa na Kristo mwenyewe. Yesu alikuwa akiwaombea wale ambao Mungu amempa Wafuasi wake. Alikuja kuwaita watu wenye dhambi ili watubu, na alikuwa akienda kufa kwa ajili ya dhambi za ulimwengu. Baba aliupenda ulimwengu kiasi kwamba alimtoa mwanae pekee, kwa sababu hakusudii yeyote aangamie, (1 Tim.2:4). Kwa hiyo tunaona kuwa Mungu anao moyo unaojihusisha na wanadamu wote. Yesu alipokuwa akiomba kwa Babaye alikuwa haombi kwa ajili ya walimwengu hata kidogo, bali alikuwa akiomba kwa ajili ya wale walio wa Mungu. Hii ndiyo ilikuwa ni haja yake kubwa pale alipokuwa akiomba na inabakia kuwa haja yake kubwa siku ya leo pia. Yesu Kristo anafanya nini pale alipoketi kuumeni mwa Baba yake? Katika Warumi 8:34, tunaelezwa kuwa anatufanyia maombezi sisi – watakatifu. Na katika Waebrania 7:25 tunaambiwa kuwa yu hai siku zote ili awaombee wao wamjiao Mungu kwa yeye. Hiki ndicho kielelezo cha huduma yake yenye kuendelea katika maandiko, sio tu kwamba ni jambo ambalo alilifanya katika Injili ya Yohana 17. Lakini cha kushangaza, leo tunao walimu ambao wanatuambia kuwa, tuwe tunaendelea kuomba na kutubu kwa ajili ya dhambi za ulimwengu! Kwa hakika jambo hili ni kinyume kabisa!

Yapo maandiko mengine ambayo kwa hakika yatupasa kuyaangalia ili tupate picha pana kuhusu mstari wa Yohana 17 ili usimame na mistari mingine, au sijaribu kuweka tafsiri nyembamba (hafifu) juu yake kana kwamba kulikuwa na jambo moja tu la kuomba; sifanyi hivyo hata kidogo! Bali hebu tuangalie maandiko mengine zaidi yanasemaje kuhusu hilo na nini hasa mwelekeo na mkazo wake mkuu; ndipo itatuweka katika nafasi nzuri ya kuyafahamu mambo haya na msingi wake na nini, na ni kipi hakipo hivyo.

Tunafahamu nini basi juu ya huduma ya Roho Mtakatifu ndani ya maombi? Kumbe, kama ilivyo pamoja na Yesu Kristo ndivyo ilivyo pamoja na Roho Mtakatifu.Tunasoma katika Warumi 8:26,27,34, kwamba Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Mtume Paulo anaendelea kutuambia kuwa Roho Mtakatifu huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu.

Lolote liwalo laweza likawa ni kweli, maandiko ya Neno la Mungu yanatufunulia kwamba huduma kuu ya Mwana na ya Roho Mtakatifu katika maombi ni kwa ajili ya watakatifu. Ni vipi kuhusu watakatifu wenyewe? Wanapaswa kuomba kwa ajili ya nini? Jambo la kwanza na lililo kuu, kulingana na maandiko ya Neno la Mungu tunalolipata katika somo hili, tunaona watakatifu wanaomba, na pia wanapaswa kuombeana wao kwa wao kama vile Mwana na Roho Mtakatifu wanavyofanya. Katika Waefeso 6:10-18, tunaambiwa kuwa, “Tuzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake, kwa maana kushindana kweli sisi si juu ya damu na nyama, bali ni juu ya falme na mamlaka n.k.”, kwa maneno mengine yule adui sio wa kimwili bali ni wa kiroho. Ikiwa hivyo ndivyo ilivyo, mtume anatutaka tufanye nini? Je, hapo anatuambia kuwa, kwa hiyo tuwe tunaomba dhidi ya mamlaka na uweza, dhidi ya ulimwengu huu na dhidi ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho na kuwafunga? Hapana! Huo sio ushauri wake! Sio hivyo hata kidogo! Hafundishi hivyo mahala hapa wala sehemu nyingine yoyote ile ndani ya nyaraka zake kwa watakatifu. Hali kadhalika Petro naye, hafundishi hivyo. Yakobo na Yohana hawawaagizi wakristo kufanya hivyo kwa sababu wanajua kuwa adui yako ni mwenye nguvu za kiroho. Mtume Paulo anawaagiza waumini kuvaa silaha zote za Mungu, hiyo ni kwamba, wanahitajika kuishi na kutembea kiroho wakiwa na silaha za kiroho. Katika sura hiyo tunafundishwa kuwa, kwa sababu adui yetu ni wa kiroho, kwa hiyo mwendo wetu, maisha yetu ya kila siku yawe ni ya kiroho ili kwamba tupate kusimama kinyume na hila zote za shetani na mapepo yake, ambayo yanataka kutujaribu ili tuwe mbali katika kumtegemea na kumwamini Mungu; ili yeye (shetani) aweze kupata nafasi ya kupanda mbegu za mashaka, kukata tamaa, uongo na tamaa mbaya mioyoni mwetu.

Tunapaswa kuishi katika utii wa Imani na upendo kwa Mungu, tukiukataa uongo wote wa yule adui toka mioyoni na akilini mwetu. Hii ni vita ya kiroho; kwa hiyo sasa, tukiwa tumezivaa silaha za kiroho, Paulo anatuagiza tuombe juu ya nini pale katika mstari wake wa 18? Je, juu ya uweza na mamlaka n.k.? Hapana! Anatuambia tunapaswa kuomba kwa maombi na sala zote kuwaombea watakatifu wote. Kusimama tukiwa tumevaa silaha zetu, yaani, kuishi na kutembea kiroho ili tuweze kuombeana wenyewe kwa wenyewe kwa utaratibu na kwa mafanikio. Katika mienendo yetu binafsi mbele za Mungu, tunapaswa kuyapinga majaribu ya shetani, kusita juu ya Mungu au kuwekwa naye mbali; na kutokana na kukaa katika mwenendo huo ndipo tunawezeshwa kuomba vizuri kwa ajili ya watakatifu. Hayo ndiyo mafundisho yake, lakini watu wanatupoteza kwa kutufundisha vitu vingine; wakituhimiza kuzingatia kuomba dhidi ya mamlaka na uweza au kutubu kwa ajili ya dhambi za ulimwengu, jambo ambalo hiyo siyo maana ya Mtume Paulo kabisa, katika jambo hilo hapa. Kwa Mtume Paulo hili ni jambo muhimu sana, hatuagizi kuomba tu kwa ajili ya watakatifu, isipokuwa, “kukesha katika jambo hilo kwa bidii na kudumu katika sala”, kwa maana nyingine, tunapo ombeana, tunatakiwa kuwamacho na kuwa waangalifu kwa mahitaji ya watakatifu na matokeo ya maombi yetu kwao (watu wengine wangependa kututaka tuendelee kuwa macho na makini kwa kila aina ya uovu, dhambi na matendo ya uchawi yanayotuzunguka).

Paulo mwenyewe binafsi anafanya nini? Anaombaje? Zaidi sana anaomba kwa ajili ya watakatifu akidumu kuomba kwamba wapate kukua na kuongezeka katika upendo na ufahamu wa urithi wao wa wokovu katika Kristo jinsi ulivyo; karibu maombi yake yote katika Agano Jipya ni ya tabia hii. Hivyo anawaambia Wafilipi kuwa, anawakumbuka kila wakati anapoomba, na anapowaandikia wanawajulisha juu ya maombi yake kwa Mungu kwamba upendo wao upate kuwa mwingi sana, (Wafilipi 1:4-9). Huo ndio ushuhuda wake wa kawaida uhusuo maombi yake, kama tunavyoweza kuona kutoka katika mistari ifuatayo: Rumi 1:9; Gal.4:19; Efeso 1:16-20, 3:14-19; Kolosai 1:3,9-11; 2:2,3; 1Thes.1:2,3; 3:10; 2Thes 1:3, 11,12; 2Tim.1:3; Philemon 1:4. Epafra anaomba maombi ya jinsi hiyo hiyo (Kol. 4: 12).

Kwa hiyo tunaona kwa uwazi kuwa, mifano na kumbukumbu nyingi za maombi katika nyaraka za Agano Jipya yanajishughulisha na maombi kwa ajili ya watakatifu kutoka kwao ndani ya Kristo – na kwa ajili ya huduma ya kanisa kwa wengineo. Iko mistari mingine ambayo ni kama mausia ya maombi – kama vile Kol.4:2 na 1Thes.5:17; wengine wanafanya marejeo kwa mambo maalum kwa ajili ya kuwaombea, na tutaangalia katika jambo hilo kwa karibu zaidi. Lakini tena hapo napo hatuoni hata andiko moja ambalo linatusihi tuungame au kutubu kwa ajili ya dhambi za wasioamini katika maombi yetu.

Hii sasa inatupeleka mbali zaidi katika jambo lingine ambalo Kristo aliomba katika Yoh. 17:20,

“…wala sio hao tu ninaowaombea, bali na wale watakaoamini kwa sababu ya neno lao.”

Kwa hiyo, Yesu anaendelea kuomba sio tu kwa ajili ya wanafunzi wake, bali na kwa wale watakaoamini kwa neno lao, hapo anawaombea wale ambao baadae wataongezeka kwa kanisa. Kwa hiyo Kristo anategemea kuona wengine wakiokolewa pia kwa kupitia huduma ya watumishi wake. Hadi kufikia mwisho bado anawasihi kuomba kuwa, Bwana wa mavuno atume watenda kazi, na kwa hakika yeye mwenyewe anawaagiza kuihubiri Injili kwa kila kiumbe, Luka 24:46-47 na Mark 16:15-16. Na pale yanapotokea matatizo tunaliona kanisa likiomba sio dhidi ya mamlaka na uweza wala sio kuzitubia dhambi za hao waliomo katika miji hiyo, isipokuwa ni kulingana na mfano wa Yesu Kristo mwenyewe katika Yohana 17 – wanaomba ili Bwana awape ujasiri kulinena neno lake, na kuwa Bwana atende ishara na maajabu katikati ya watu (Mtd. 4: 29-30). Katika Warumi 15:30-32, Paulo anawaomba wakristo wa kirumi kuungana naye katika kuomba kwa ajili ya kazi ya huduma na kwamba ili apate kuokolewa kwa ajili ya wasioamini katika Yudea.

Hakuna sehemu yoyote inayotaja kutubu kwa ajili ya wanaoipinga Injili. Angalia kwa makini sana hapo, utaona kuwa sio hapo wala penginepo popote pale katika nyaraka zake kwa Warumi (pamoja na sura ya 9-11) ambapo Paulo anajaribu hata kuelekeza tu wale wakristo wa kirumi kwamba eti watubu kwa ajili ya dhambi za Rumi na ufalme wake – ambao umeshinda na kukaliwa na nchi ya Israel na sasa wanaitawala. Katika nyarak zake hizo, alikuwa na fursa ya kifalme ya kuwaambia kuwa Rumi imetenda dhambi dhidi ya watu wa Israel, na kwamba kama lilikuwa ni jukumu lao la kiroho, kama wenyeji wa Rumi, kuzitambua dhambi za nchi yao na kisha kuzitubia dhambi hizo dhidi ya Israel. Zaidi ya hayo yote, bila shaka kama ilivyo kwa ye yote yule anayajua maandiko ya Agano la Kale yahusuyo toba na umuhimu wa taifa la Israeli, lakini Paulo bado hawaagizi wakristo wa kirumi watubu kwa ajili ya dhambi za Warumi au za wengine – hafanyi hivyo hata kidogo! Hatuioni kabisa aina hii ya mafundisho yao ndani ya nyaraka zake, kama vile ilivyo ndani ya Agano Jipya lote, hivyo, kwa sababu ingekuwa ni udanganyifu kufanya hivyo. Anawaonya kwa uangalifu sana wasio na watu wenye kujivunia akili, kinyume na wayahudi (sura 11), lakini bado hakuwaomba watubu kwa ajili ya dhambi za watu wengine. Sasa iwapo mitume wenyewe hawafundishi hivyo, je, hawa walimu wa kisasa wanachukua kutoka wapi hizi mamlaka na ufunuo huo? Kwa masikitisho makubwa, hawaupati toka kwa Mungu.

Mtume Paulo anapowaandikia Wakorintho, anawaandikia katika moyo huo huo (2 Kor 1:11), anawaomba wamwombe yeye mwenyewe pamoja na wale wote walio naye. Tumekwisha kuona katika Efeso 6 jinsi Mtume Paulo anavyowasihi ili waombe kwa ajili ya watakatifu. Kadhalika katika ule mstari wa 19 (kulingana na kielelezo au moyo wa Yesu unaopatikana katika Yoh.17), anawaomba kuwa apate kupewa usemi ili kuihubiri Injili yenye nguvu, anayaomba makanisa mengine kuomba vivyo hivyo. Kwa mfano, kuomba kwa ajili yake na huduma ya Neno la Mungu lipate kuendelea. Wafilipi 1:18,19; Kol. 4: 2,3; 1Thes.5:25; 2Thes3:1. Tafadhali, hapa usijaribu kufikiria kuwa labda tunatafuta tu baadhi ya mistari michache, tuliyoichagua. Mafunzo haya yanahusiana na karibu kusihi kote kwa maombi katika Agano Jipya. Zaidi ya yote kumbukumbu zote zinazohusiana na “toba” hazielezei chochote kile kuhusu eti mwamini atubu kwa ajili ya dhambi za kitaifa au miji. Hali kadhalika anawaelezea wafilipi kuwa wayafanye mambo yote pasipo manunguniko na kushutumiana. Kwa nini basi anafanya hivyo? Ili kwamba wawe ni watu “…wasiolaumiwa na wasio na madhara, wana wa Mungu…wale waliomo katikati ya taifa linaloenda kombo na lenye ukaidi, ambamo ninyi mnawaka kama nuru ulimwenguni, mkilishika kwa ukamilifu lile neno la uzima”.

Ni jambo la muhimu kwa Mtume Paulo kwamba anapaswa kumweleza Kristo kwa namna zote mbili, kwa tabia yao na kupitia ushuhuda wao. Hayo yote yanafanana na maombi ya Yesu katika Yoh.17 ambapo anaomba kuwa wapate kutakaswa kwa ile kweli kama vile yeye alivyotumwa hapa ulimwenguni, ili wengine wapate kuamini kupitia Neno lao (mstari ule wa 17-20), na kwamba wote wapate kuwa kitu kimoja.

Kama vile nilivyokwisha eleza hapo mwanzoni, kuwa kuna mistari mingine ambayo inatuagiza zaidi jinsi itupasavyo kuomba. Katika 1Tim 2:1-4, tunasihiwa kuwaombea watu wote, na Mtume Paulo anawataja rasmi, kuwaombea wale waliopo katika mamlaka na kadhalika anataja kusudi la maombi ya jinsi hiyo, sala na maombezi yaani tunapaswa kuwa na tabia za aina hiyo, za kijamii, ambayo itatupelekea sisi kuishi maisha ya kimungu katika amani. Mstari wa 3 na wa 4 inaoonyesha kuwa tunapaswa kuomba kwa mtinndo huo, kwa sababu itawezesha pia kujenga nia ya kuieneza Injili kwa wanaume na wanawake.

Hivyo inatupasa kuwaombea wale walimo katika mamlaka serikalini, kwamba tuwapate watu wa jinsi hiyo ambao wanaweza kukuza uaminifu, haki na hali ya amani ambavyo ni msaada mkubwa katika kuenenza Injili ili kuifikia mioyo ya watu; kuliko kuwa na mashambulizi, vita na masharti mengi yasiyo ya haki. (Ijapokuwa tunaelewa kutoka katika kitabu cha matendo ya mitume kuwa tunapaswa kuieneza Injili hata katika hali ya mateso).

Kwa hali hiyo, naona ni vema kuitaja Warumi 13:1-7, na Tito3:1,2, ambapo sehemu zote mbili tunasisitiziwa kujinyenyekeza kwa wenye mamlaka na kuwapa heshima wanayostahili, na wala tusinene mabaya juu ya mtu yeyote, ijapokuwa mtiririko wa aya hizo zinaweza kutofautiana kidogo, hata hivyo mstari unaopatikana kutoka katika 2 Petro2:10-12 umebeba mambo yanayofanana hapa pia; katika ukweli kwamba mafungu yote mawili ya maneno yanatusisitizia na kutuonya tusiwakemee na kuwashutumu wale waliomo katika mamlaka. Kwa maneno mengine, usijifikirie kuwa wewe unayo haki ya kuja na kusuta, kulaumu na kutamka hukumu dhidi ya hao waliomo katika mamlaka kama walivyofanya baadhi ya manabii wa Agano la Kale, eti kwa sababu tu wewe ni mkristo na wao ni watu wa dunia. Tena, hitilafu nyingi na michanganyiko inatujia kutoka kwa watu wanaoitumia vibaya mifano ya Agano la Kale – wao wanafikiri kuwa kama manabii wa Bwana walivyowakemea watu wa Bwana katika Agano la Kale, kwa hiyo wakristo wanaweza kuwakemea walio kwenye mamlaka na walio katika jamii. Mitume wa Bwana hawakufanya hivyo!

Lakini hayo yote, kwa ujumla ni mambo ya kulichanganya kanisa na ulimwengu, neema na sheria. Haupo mstari au mfano wowote wa Agano Jipya, wala hayapo mafundisho yoyote yatakayo tupeleka sisi na kufanya au kusema kwa jinsi hiyo. Hebu ujifunze kitabu cha Matendo ya Mitume kwa wakati wako mwenyewe, utagundua kuwa kulikuwepo na uovu na udhalimu mwingi katika jamii katika siku hizo; lakini je, watakatifu walijiheshimu namna gani? Kwa hakika, hebu tuihubiri Injili, lakini tuwe macho sana na hao wanaochanganya matengenezo ya jamii na Injili. Msingi mkuu wa huduma ya kanisa kwa ulimwengu ni kuleta mabadiliko ya ndani kwa waume na wake; kutoka katika mauti kuelekea uzimani. Kutoka katika dhambi kuelekea haki. Lakini iwapo utazidisha kukazia zaidi juu ya matengenezo ya jamii, watu watashindwa kuelewa kuwa Injili inahusu nini hasa?

Bila shaka tunaweza kuchagua kuzitumia haki zetu za kidemokrasia, ikiwa tunazo na dhamira zetu na imani; lakini kuhubiri na uwasilishaji wa Injili nyakati hizi za neema ni, na inapaswa kuwa tofauti kutoka katika namna ambayo manabii wa Agano la Kale walikuja kulisema neno la Mungu. Zipo siku nyinginezo ambapo wanayachanganya mambo haya na kutaka kuturudisha nyuma kwenye njia za kufikiri na kutenda za kiagano la kale; ambazo kwa hakika hizo zilikwisha kuondolewa katika Kristo. Hapa sisemi kuwa tusiwaambie watu juu ya hukumu inayokuja, isipokuwa ninachokisema hapa ni kuwa hakuna awezaye kutushurutisha kufanya lolote lile ambalo hatuamriwi kulifanya katika maandiko ya neno la Mungu. Kwa mfano, si Yesu wala Mitume waliipinga mamlaka ya utawala kwa ajili ya matengenezo ya kisiasa au jamii ijapokuwa kulikuwa na maovu mengi nyakati hizo. Watu wengine wanadai kuwa eti hawakuweza kufanya upinzani huo, kwa vile kulikuwa hakuna uhuru wa kufanya hivyo wakati huo. Lakini iwapo hilo ni jukumu la Mkristo kufanya kampeni kwa ajili ya kuleta mabadiliko, je, lisingekuwa ni jukumu la mitume kufanya hivyo pia kwa hali yoyote iwayo kwa jamii? Hata hivyo, cha muhimu zaidi ya hilo ni kwamba hatulioni agizo lolote lile kutoka kwa Bwana Yesu mwenyewe, wala kutoka maandishi yao mitume wenyewe (kwa ajili ya kizazi chochote kijacho ambacho kitakuwa na uhuru zaidi wa kupinga) kiasi kwamba tunapaswa kufanya kampeni kwa ajili ya matengenezo ya kijamii au kuwashutumu wale waliomo madarakani. Hapa sisemi kuwa wakristo hawawezi kujishughulisha na matengenzo ya kijamii wanapopata fursa ya kufanya hivyo; lakini kile nisemacho ni kwamba, hakuna yeyote yule aliye na haki au mamlaka kutoka katika Agano jipya linalosema kuwa Mkristo anapaswa kujihusisha katika siasa kwa jinsi hiyo. Kila mtu ashawishike na dhamira yake mwenyewe na hivyo atende ipasavyo pasipo kulazimishwa na kuhukumiana. Bila shaka katika mambo makubwa zaidi pale ambapo uovu wa haki au watu waovu wanaweza kutushurutisha kufanya mambo kinyume kabisa na mapenzi ya Mungu, lazima tuweke msimamo. Katika tukio lolote lile nia yetu kuu iwe ni kuwaona watu waume kwa wake wakizaliwa katika ufalme wa Mungu wa haki, furaha na amani; ambayo historia pia imeonyesha kuwa ni mambo yenye mafanikio makubwa katika kuibadilisha jamii kuliko aina yo yote ile ya kampeni ilivyoweza kufanya.

Mwisho hebu tutazame katika maelezo ya Mtume Paulo kwa Warumi, (Warumi 9:1-3 na 10:1). Hapa anaelezea hamu yake waziwazi, ya kusikia kuwa Israel inaokolewa na kwamba anayo huzuni nyingi isiyokoma kwa sababu ya ugumu wa ndugu zake kwa jinsi ya mwili wanaosimama kinyume na Injili. Huzuni zake ni kubwa kwa sababu ya wao waliofanywa kuwa wana wa ule utukufu na maagano (mstari wa 4). Na kwa sababu hiyo, vile vifungo vyake na huzuni yake kwa ujumla zingeweza kuwa ni kubwa kuliko ambavyo raia yoyote wa nchi nyingine angeweza kujisikia kwa ajili ya watu wa nchi yake, ambao, kwao kule kufanyika wana wa maagano haikutumika mwanzoni kama vile ilivyofanywa kwa Wayahudi.

Ili kwamba watu wapate kuokolewa ni jambo jingine tena lililo wazi katika mioyo yetu – linaonyesha nia yake Mungu ndani ya mioyo yetu – hasa kwamba kuomba kwa ajili ya watu walio jirani nasi kwa namna fulani inaweza kuwa ni familia au jumuia. Lakini tafadhali uangalie hapa kuwa, hakuna sehemu yoyote ile ambayo Mtume Paulo anaonyesha akitubu kwa ajili ya ugumu wao, kule kukaa kwao kinyume na Injili. Ijapokuwa hilo limehuzunisha, bado yeye maombi yake ni kwamba, “ili wapate kuokolewa”. Angalia tena tafadhali, kwamba Paulo angeweza kupata fursa nzuri sana hapa ya kuwasihi wauamini katika Urumi, kutubu kwa ajili ya dhambi za mji wao mkuu na viongozi wao, ambao majeshi yake yalikuwa yakikalia mji wa Israel pamoja na maeneo mengine ya ulimwengu. Lakini bado hatuoni fununu yoyote ya mafundisho ya jinsi hiyo hapa wala katika Agano Jipya. Jambo moja tu linalopatikana hapa kwa ajili ya Wayahudi ni kuomba wapate kuokolewa, ambapo kwa ajili ya hilo Biblia inatupatia sababu za kutosha kutuwezesha kufanya hivyo.

Lakini ni jambo la tofauti kabisa leo kuwaambia watu kwamba wanapaswa kuunga mkono Serikali ya kisiasa ya Israel. Hakuna mstari hata mmoja katika Agano Jipya unaotusihi tufanye hayo. Niko mwangalifu sana juu ya maandiko ya neno la Mungu, na mistari mingi iliyomo ndani ya Agano la Kale ihusuyo Israel; lakini jambo Mungu mwenyewe alipendezwa nalo ni vile uhusiano wake yeye mwenyewe na Israel, kwamba wawe ni watu watakatifu, wamtumikie yeye pekee. Israel waliposhindwa kutimiza hilo Mungu naye hakuweza kuuheshimu unyoofu wa Taifa lao. Wakati ambapo manabii wengine walipokuwa wakitoa unabii nyakati zile za Yeremiah alisema kuwa kwamba Israel watakuwa na amani, na wala hawataona vita. Bali Yeremiah alisema maneno ya Mungu kwao kama vile, Taifa lao litaangamizwa na kwamba watatapanywa mbali utumwani (lakini baadae baadhi yao wangerudi kulingana na neema yake). Kwa hiyo, tunaona wazi kuwa hata katika nyakati hizo Mungu hakuwa akiunga mkono Serikali ya nje ya kisiasa wakati ambapo mioyo yao ilipokuwa mbali naye.

Jambo hili halitofautiani kabisa na nyakati hizi za leo, lakini tena watu wengine nyakati hizi hizi za leo wanachanganya kwa matamko yao kuelewa kwao juu ya Agano Jipya na Agano la Kale, hali kadhalika hawafahamu jinsi gani Kalvari ilivyobadilisha mambo haya, lakini wao wangetamani kuwataka watu leo, ili waombe na kufanya mambo yanayounga mkono mambo ya kimwili ya kiinje ya serikali ya kisiasa ya Israel ambayo wala haimtambui Mungu. Ni taifa la kidunia tu; wapo pia Wayahudi wa Othodox ndani ya Israel ambao wanakataa kulitambua taifa la kisiasa la Israel ni kutokana na sababu hiyo ya msingi wao wanafanya hivyo. Wanaamini kuwa, kwa vile Mungu amewarejesha katika nchi yao, hata hivyo atawashughulikia tu – iwapo wataweka matumaini yao kwake Mungu na sio katika nchi nyingine. Ninarudia tena kusema kuwa, ni jambo moja tu tupaswalo kuomba nalo ni kwamba wapate kuweka matumaini yao katika Kristo ya kwamba ni mwokozi wao. Lakini, badala yake, sasa tunawaongoza watu waende mbali na Mungu pale tunapojaribu kuwaambia kuwa eti wanapaswa kuunga mkono taifa la kisiasa la Israel.

Je, Yehoshaphat hakukemewa na manabii wa Mungu kwa ajili ya sababu hiyo? Kama pale alipounga mkono ndugu zake waisrael wakati ambapo kwa kupitia kwa Ahabu walikuwa wamempa Mungu mgongo, 2Nyk.18:3 na 19:2 – uaminifu wa kimwili kwa kweli unapingana na kusudi la Mungu. Siyo kwamba najihusisha katika mjadala kuhusu kanisa na Israel, bali jambo pekee ambalo ninalifanya kwa kiasi fulani ni hili kwamba; wazo kuwa tunapaswa kuunga mkono Serikali ya kisiasa ya kiinje ya taifa la Israel, halijawahi kufundishwa na Yesu wala manabii. Kulingana na Injili, ni sawa kuwa tunaweza kuomba kwa ajili ya Wayahudi, lakini ukienda ndani zaidi hadi kufikia hatua ya kuunga mkono serikali yao ya kisiasa ambayo ni ya kiinje tu, basi hapo yakupasa uwe mwangalifu ili kuona kuwa huungi mkono kitu ambacho kinakataa kumtambua Mungu na kujikabidhi katika kweli na neema yake.

Tafadhali sana, unaweza kwenda sana katika maombi yako kadiri unavyoamriwa na maneno ya Mungu, lakini uwe makini kuona kuwa huvuki mipaka ya maandiko ya neno la Mungu na bila shaka usiwashurutishe watu wa Bwana na kufanya hivyo. Pia ukumbuke kupambanua kuwa yeye ni Myahudi aliye Myahudi kwa ndani, na sio Myahudi aliye Myahudi kwa nje. Rumi 2:28,29. Usije ukachanganya mwili na Roho, ulimwengu na kanisa, Agano la Kale na Agano Jipya.

Mambo ya Kufikiria Mwishoni

Mwisho, hebu tuangalie ni jinsi gani fundisho hili, kwa kweli, linavyoiinua torati ya Agano la Kale juu ya neema ya Agano Jipya, na linavyotafuta kutuweka kwenye utumwa kwa hoja zinazopingana na Injili. Labda kwa kutambua kuwa hii hoja ya “dhambi za vizazi” na kuzitubia haifundishwi katika Agano Jipya, mwalimu mmoja anajaribu kuhalalisha fundisho hili kwa njia ya ajabu kabisa. Na haya yafuatayo ndiyo majibu yake akisema, “Inapaswa kuwa wazi kuwa hatujaokolewa kwa kutunza torati ya Agano la Kale, isipokuwa tumeokolewa kwa imani na kwa toleo la damu yake Yesu kwa ajili ya dhambi zetu. Anaendelea kusema zaidi kuwa, hii haimaanishi kuwa chimbuko la kina la amri kumi zilizotajwa katika Kut. 20:3-17 na Kumb. 5:7-21, ilibatilishwa kwa imani katika Kristo. Wanadai kuwa Mtume Paulo anatuonyesha hayo yote kwa uwazi kabisa katika Warumi 3:31, pale ambapo Paulo anasema, “hatuibatilishi sheria bali tunaithibitisha sheria kwa imani katika Kristo”; na hivyo huyo mwandishi wao anahitimisha kuwa imani ya Agano Jipya inatilimilizwa na kuthibitisha chimbuko la kina la sheria ya Agano la Kale (torati) kama ilivyo katika Rumi 8:4, 13:8! Na ni chimbuko gani la kina la Agano la Kale ambalo Agano Jipya linatimiliza sasa?

Kwanza kabisa, katika makala hiyo yake ijapokuwa ananukuu hizo sehemu 3 za maandiko ya Agano la Kale, kimsingi na kama sio kipekee, mwandishi huyo anahusika kabisa na kule kuyathibitisha mawazo ya dhambi na vizazi; ambayo imejitokeza tu katika mstari mmoja ndani ya kila habari kama nilivyokwisha kutangulia kusema hapo juu. Hupenda kuthibitisha yale mawazo yake tu ya dhambi za vizazi, kama vile, kwamba – eti, dhambi inaweza kuendelea toka kizazi hadi kizazi na kwa hiyo inatupasa kuungama na kutubu kwa ajili ya dhambi hizo ili kwamba tupate kuachiliwa kutoka katika laana na hukumu. Hapo haelezi mengineyo (uhakika au utukufu) yahusuyo tabia ya Mungu anapo ya Mungu kumbushia katika nyaraka hizo. Hivyo anachotaka kutueleza hapa ni kwamba, kutokana na Warumi 3:31 na 8:4, imani katika Kristo inathibitisha kweli ya dhambi za vizazi na ushirikishwaji! Imani ya Agano Jipya inathibitisha torati; na dhambi za vizazi zimetajwa katika torati; kwa hiyo dhambi ya vizazi ni sehemu ya kweli ya Agano Jipya! Eti hiyo ndiyo sababu yake ya msingi anayoitoa. Tohara ilikuwa ni sehemu ya torati, na iwapo imani ya Agano Jipya inaithibitisha torati kwa namna anavyosema, je, si sote tunapaswa tutahiriwe?! Je, unaweza kufikiria kuwa Paulo alikuwa anawaza hivyo alipokuwa akiandika mistari hiyo katika waraka wa Warumi? Ikiwa ndio hivyo, kwa nini fundisho hili haligusiwi hata kidogo mahali popote katika maandishi yake?

Jambo la pili: Je, umewahi kusikia kuhusu chimbuko la ndani kabisa lihusulo tabia ya Mungu ambayo ilijitokeza katika Agano la Kale na jinsi ilivyolinganishwa na ile iliyomo katika Agano Jipya? Je, hii ina maana gani? Mpendwa msomaji, napenda kukualika usome Amri kumi katika Kut. 20; kisha usome Matayo sura ya 5 mpaka ya 7. Unafikiri nini hapo? Je, ni sura ipi ambayo inakupatia kwa kina zaidi juu ya ukuu na zaidi ya yote pamoja na utukufu wake – ule mwanga wa tabia ya Mungu pamoja na torati? (Ikiwa tunatumia neno torati hapa kwa ukweli ambao Yesu anauelezea ndani ya sehemu yake katika Mathayo, huo ni mwanga wa kutosha wa maisha halisi ya Mungu ndani ya mtu; sio maisha yale ambayo mtu anayapata kwa kujitahidi kwake mwenyewe katika kutunza torati. Hii ndiyo sababu inasemwa kwamba torati ilikuja kupitia Musa, lakini kweli na neema imekuja kupitia Yesu Kristo). Yesu alisema, “Yeyote anionaye mimi amemwona Baba.” Je, kulifunuliwa nini kwa sehemu au kwa aina, na zaidi sana kwa nje katika Agano la Kale? Jambo hili kwa sasa limefunuliwa kwa utukufu zaidi na kwa njia ya ukamilifu kupitia Kristo, ambaye hutupatia utukufu huu na ukamilifu ndani yetu kwa Roho. Ni kweli tunayo kila sababu ya kumshukuru Mungu na kuitukuza Injili yake ya neema na kweli.

Hebu sasa utazame katika, 2Wakor.3:6-18; 4:6; Wakol.1:27; 1Petro1:10-12; Waebr.1:1-3; 7:18,19;10:1. Kutokana na maandiko hayo, wanawezaje kusema kuwa Agano la Kale linayo hali yenye kina zaidi ihusuyo tabia ya Mungu kuliko Agano Jipya? Mungu habadiliki, na upendo wake, upole na uvumilivu wake, hali kadhalika na hukumu zake zimejitokeza wazi kabisa katika Kristo, utukufu wa tabia yake, neema ya kusudi lake la umilele kwa ajili yetu na kina cha wokovu imefunuliwa kwa njia yenye utukufu na ya ndani zaidi. Paulo anatuambia kwamba utukufu wa Agano Jipya ni mkubwa zaidi kuliko ule wa zamani, ndiyo kusema kuwa kwamba ya zamani haina utukufu kwa kulinganishwa!

Jambo la latu: wananukuu warumi 8:4 ili kusudi kuhakikisha kuwa mawazo ya dhambi za vizazi katika torati yametimilizwa au kuthibitishwa ndani ya Agano Jipya; pengine hakuna chochote kinachoweza kuonyesha kwa uwazi jinsi ambavyo, siyo tu kwamba hawaelewi Agano Jipya bali pia hulinyang’anya uweza wake na maana yake halisi, kwa kupitia mafundisho hayo yao. Warumi 8 inayo mistari muhimu na yenye utukufu katika Agano Jipya, ukijumlisha mstari 1-4 kwa kupitia kifo na ufufuko wa Kristo – sasa tumewekwa huru kutokana na sheria ya dhambi na mauti. Ni mara ya kwanza katika historia ya mwanadamu; toleo la sheria halikuweza kutupatia haki, isipokuwa kwa ujumla liliweza tu kututhibitishia kwamba sisi hatuna haki; na kisha tupo katika vifungo vya dhambi, hivyo hatuna uwezo wa kukaribia katika uwepo wa Mungu (Rumi 3: 10-12,19,20; 7: 7-11; Gal 3:19; Heb 9:8); na kwamba tuna haja ya wokovu, njia pekee ya kutupatia uzima. Uzima wa milele ni kutufanya tuwe wenye haki; hakuna tofauti ya hakika kati ya uzima kama ulivyo katika Mungu na haki (Gal. 3:21; Rumi 5:21). Basi tena kwa kupitia Adamu wengi walifanywa kuwa wenye dhambi, hali kadhalika kwa kutii kwake Kristo wengi walifanywa wenye haki, kwa sababu Mungu alimfanya kuwa dhambi ili kwamba tupate kufanywa wenye haki kwa Mungu katika yeye. Rumi 5:19; 2Kor.5:21. Huo ndiyo uwezo na utukufu wa Habari Njema!

Ni sehemu gani ya sheria katika Agano la Kale ambayo Mungu alipenda kuikamilisha ndani yetu? Sio sehemu za wonyesho wa Ibada! Wala hakuna chochote kiwezacho kuleta laana na hukumu! Ilikuwa ni haki ya sheria – hiyo ndiyo iliyotuletea mwanga wa hali yake ya utukufu na haki ya ile tabia yake. Hicho ndicho alicho nacho toka katika umilele. Alipenda kukileta kwetu, kama vile, ile haki yake yeye mwenyewe na maisha ya utukufu wake! Ilikuwa ni njia pekee ya kutupatia uzima wa umilele kutufanya kuwa wana wake kulingana na tabia yake yeye mwenyewe. Ni Injili ya jinsi gani hiyo? Je, ni neema ya jinsi gani hiyo? Ni upendo wa jinsi gani huo? “Tazama ni upendo wa jinsi gani ambao Baba ametupatia kwamba tuitwe wanawa Mungu”, 1Yoh. 3:1; na pia tazama Gal.3: 21; Efeso1:4,5; Rumi 8: 15-17; 29; 2Kor 4:10 ,11; 2Tim 1: 9; Heb 12:10, 1Petro 1:15, 16; 2Petro 1:3,4; 1Yoh. 4:17.

Mpendwa msomaji, ukiitazama mistari hiyo hapo juu kwa makini sana, utagundua kuwa hii ndiyo ile, ambayo Rumi 8:4 inaelekeza yale ambayo torati haikuweza kuyatimiza, yale ambayo damu ya mafahari ya ng’ombe na mbuzi hayakuweza kuyafanya; yale ambayo jitihada nzuri kabisa za watu wazuri kabisa hawakuweza kuyafanya – Mungu ameyafanya sasa ndani ya Mwana wake; mwanakondoo wa Mungu ameziondoa dhambi zetu, akihukumiwa katika mwili wake na hivyo pia hakiharibu uweza wake na mashutumu yake juu yetu ili kwamba ile haki inayopatikana kwa sheria ipate kutimilizwa ndani yetu sisi ambao hatuenendi kwa sheria bali katika Roho. Hii ina maana kwamba, uzima wake upate kudhihirishwa ndani yetu, pamoja na haki yake, neema yake, upendo wake, upole na uvumilivu wake.

Hivyo ndivyo inavyohusika na ile Warumi 8, kama vile, kuwa na uzima wake Yesu ndani yetu. Nashangaa wanawezaje basi kuchukua mstari huu wenye utukufu wa namna hii na kuanza kuutumia vibaya namna hii, ili tu kukidhi udanganyifu wao! Naona bila shaka hawafanyi hivyo kwa kusudi, hata hivyo wanahusika kwa ajili ya kuyakataa na kuyapinga yale ambyo yanaelezwa na maandiko ya neno la Mungu, kama wafanyavyo katika mafundisho yao kama tulivyoeleza katika makala hii. Hakuna chochote kile kinachoelezea kwa undani kama Kalvari wala hakuna lolote lenye ukuu kama Kalvari; katika matukio yote yaliyopo ya kihistoria pamoja na mafunuo ya Mungu kwa wanadamu – Kalvari inaelezea kila kitu na kwa kweli imepata kila kitu.

Tafsiri zao katika mistari hii ya Warumi, pamoja na kufasiri kwao bado inaonyeshwa wazi jinsi wanavyozingatia maandiko ya Agano la Kale, wakiyatengeneza na kuyatukuza zaidi kinyume na Agano Jipya. Wanatangaza mistari ya Agano la Kale kiasi kwamba inadharirisha na kuuharibu ukweli wa Agano Jipya -sawa sawa kabisa kama ilivyokuwa katika makanisa ya wagalatia!

Hii ni hitilafu na udanganyifu wa aina ile ile ya wagalatia; hii ni ulozi. Hata kama wanakubali ukweli mwingineo juu ya Yesu Kristo kama walivyofanya wale walimu waa uongo kule Galatia, hata hivyo yale wanayoyaongezea katika ukweli, kwa hakika waliutangua ukweli.

Na hii ndiyo sababu ya kuandikwa kwa makala hii. Watu ambao walisumbuliwa, walichanganywa au kwa kiasi fulani kusita kuhusishwa na mafundisho haya waliniomba niweke kitu fulani katika maandishi ili kuwaelezeni mambo hayo jinsi yalivyo kutokana na maandiko ya neno la Mungu. Ni matumaini yangu kuwa nimefanya itoshayo kuonyesha wazi kuwa mafundisho haya mapya hayana nafasi yoyote katika Agano Jipya (na wala hayatakuja kuwa na nafasi yoyote katika nyakati zijazo hata milele) na kwa hiyo, yasipewe nafasi yoyote katika mioyo yetu. Tumeweza kugusia sehemu za ndani na kubwa kuhusiana na somo hili (kama vile mambo ya maombi, maombezi na wokovu) ndani ya makala hii. Lakini hatukufanya hivyo kwa nia ya kutoa ufahamu wa undani wa mafunzo juu ya kila mmoja wapo, bali kusudi haswa la makala hii ni kutazama kwa kina juu ya maandiko ili kuona yanavyoenda pamoja na mambo yanayohusiana na muungano, maombi na toba; kisha kuyapambanua kwa uwazi zaidi kuwa yanasema kitu tofauti sana na mawazo yale wanayoyafundisha katika mafundisho yao ya kisasa.

Kungekuwa na mambo mengi sana ya kusema juu ya somo hili, na kwa hakika sijaelezea kila jambo moja moja ambayo hawa walimu wa kisasa huyafanya – kama nisingefanya hivyo ingebidi makala hii kuwa ndefu zaidi kuliko ilivyo sasa, lakini bila hata kuongezea kitu chohote juu ya yale mambo ya kimsingi ambayo ninaamini nimeweza kuyaelezea.

Mpendwa, naomba nikuachie mstari kutoka katika Gal. 5:1,

“kwa hiyo simameni wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa”.

Neema ya Bwana Wetu Kristo iwe nanyi!

© David Stamen 2013

RUDI KWA HOMEPAGE

 

11 responses to “DHAMBI ZA TAIFA (MAKALA)

  1. Osward Mbwile

    July 4, 2014 at 9:10 am

    Mungu akubariki mtumishi tatizo ni kwamba wakristo tumekuwa wavivu wa kusoma maandiko , hivyo somo hili ni msaada mkubwa sana

     
    • dsta12

      July 12, 2014 at 9:02 pm

      Asante. Kwa kweli ni matumaini yangu kwamba masomo yatawasaidia watu.

       
  2. NAFTAL OBONDO KISSIRI

    August 24, 2014 at 8:25 am

    huu ni ufunuo wa ajabu sana kwa wote watakaousoma

     
  3. dsta12

    August 24, 2014 at 3:51 pm

    Haya ni matumaini yangu! Nafikiri unajua unaweza kupakua makala na kuigawa na wengine.

     
  4. EMANUEL OMARI

    April 30, 2015 at 5:43 am

    Kwa kwel atakayesoma ufunuo huu atabarikiwa sana kama mm nilivyo barikiwa baada ya kuusoma.

     
  5. Anonymous

    July 26, 2015 at 5:26 am

    ahsante sana mtumishi kwa hili somo

     
  6. deograthius

    August 26, 2015 at 9:41 am

    nahitaji ufafanuzi zaidi maana kuna vitu sijakuelewa kibblia

     
    • dsta12

      August 26, 2015 at 2:13 pm

      Deograthius kama ukiwa na maswali, unitumie email (dsta12@hotmail.co.uk). Au kama ukiwa na facebook account, nipe jina lako ya facebook.

       
  7. Anonymous

    March 11, 2016 at 11:44 am

    Haki huinua taifa bali dhambi ni aibu kwa kila mtu, uelewa wangu mdogo ninafahamu taifa linaweza kunajisika na likamfanya Mungu alipige kwa laana

     
    • dsta12

      March 11, 2016 at 12:50 pm

      Inaonekana hukuelewa somo vizuri. Uliandika, “taifa linaweza kunajisika na likamfanya Mungu alipige kwa laana.” Sasa, unapata wazo hili wapi katika mafundisho ya Mitume ya Agano Jipya? Kosa ni hili, wengi wamebaki katika mafundisho ya Agano la Kale na hawaelewi vizuri Injili ya Yesu Kristo.

       
  8. Robert J. Zingu

    August 22, 2019 at 7:49 am

    Aisee, asante sana mtumishi wa Bwana.

    Nimebarikiwa na nimeelewa mambo mengi sana kupitia somo hili

    Nikiri wazi kuwa, hata mimi hapa nilikwisha kuathiriwa sana na mafundisho haya na kwa kweli labda ndiyo sababu nilikuwa simwoni Mungu akitenda kazi ktk maisha yangu

    Sasa nimejua kuwa, kumbe imani yangu ilikuwa imejengwa juu msingi wa mafundisho dhaifu

    Mungu ktk Yesu Kristo anisamehehe na kuniokoa na kunipa moyo mpya ili nishike mwenendo mpya ktk yeye. Amina

     

Leave a Reply