RSS

‘Siku ile’ ni siku ya nini? Yohana 14:20

KUHUSU UBATIZO KWA ROHO MTAKATIFU

Yesu aliongea juu ya ‘siku ile’ (Yohana 14:20). Katika muktadha huo (hapo chini) ‘siku ile’ inahusu siku ya …… nini?

“Sitawaacha ninyi yatima, NITAKUJA KWENU. Bado kitambo kidogo ulimwengu hautaniona tena, ila ninyi MTANIONA, kwa kuwa Mimi ni hai, ninyi nanyi MTAKUWA hai. SIKU ILE MTAJUA ya kuwa Mimi niko ndani ya Baba na ninyi mko ndani Yangu na MIMI NIKO NDANI YENU.” (Yoh.14:18-20).

Wengine wanasema ni siku ya ukombozi, wengine ya wokovu, wengine ya ufufuo, tena wengine ya unyakuo. Kwa hiyo napenda sasa kutoa jibu na maelezo juu ya mistari hiyo kwa wale ambao hawana uhakika juu ya jambo hili.

Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Sasa Mimi NINAKWENDA Kwake Yeye aliyenituma…Lakini amin nawaambia, YAFAA Mimi NIONDOKE kwa kuwa nisipoondoka, huyo MSAIDIZI hatakuja kwenu, lakini NIKIENDA NITAMTUMA kwenu…” (Yoh.16:5-7). Basi, Yesu alieleza ilikuwa LAZIMA AONDOKE ili Msaidizi, yaani ROHO MTAKATIFU ATUMIWE kwao. Yaani, ilikuwa lazima Yesu afe msalabani na kumwaga damu yake na kufufuka ili wanafunzi wake wapokee Roho Mtakatifu.

“Kama mnanipenda, mtazishika amri Zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine akae nanyi milele. …Ninyi mnamjua kwa kuwa yuko pamoja nanyi naye ATAKAA ndani yenu.” (Yoh.14:15-17). Biblia ya Kiswahili nyingine walitafsiri Kigriki vibaya – walitafsiri ‘anakaa ndani yenu’, lakini sahihi ni ‘atakaa ndani yenu’.

Bwana Yesu alieleza lazima aondoke – kupitia Kalvari – ndipo Baba atawapa wanafunzi Roho Mtakatifu naye ATAKAA NDANI YAO (mistari 15-17). Mara moja Yesu aliendelea kueleza (mistari 18-20) hatawaacha YATIMA kwa sababu YEYE ATAKUJA kwao. Basi, Roho atakuja na Yesu atakuja na kwa sababu ya hayo watakuwa hai na SIKU ILE watajua kwamba wao wapo ndani Yake na Yeye yupo ndani yao! Siku gani? Siku ile ile watakapopokea Roho  Mtakatifu! Yesu aliongea juu ya ujio wa Roho Mtakatifu mara ya kwanza – maneno yake yanahusu ubatizo wa Roho Mtakatifu.

Soma kwa makini Yoh.14:15-26. Pia utaona unaposoma sura ya 14 na 16, Roho Mtakatifu anaitwa pia ‘Msaidizi’ (14:26), au ‘Roho wa Kweli’ (16:13). Katika Matendo ya Mitume Yesu anamwita ‘ahadi wa Baba’ (Matendo 1:4). “Msitoke humu Yerusalemu, bali ingojeni ahadi ya Baba, AMBAYO MMENISIKIA NIKISEMA HABARI ZAKE. Yohana aliwabatiza kwa maji, lakini baada ya siku hizi chache mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.’’

Basi, Yesu aliwaambia wanafunzi wake wangoje ahadi wa Baba, yaani, yule Roho Mtakatifu ambaye Yesu aliongea juu yake katika Yohana sura ya 14 na 16. Aliwaambia watabatizwa kwa Roho Mtakatifu baada ya siku chache. Ndipo Bwana Yesu aliinuliwa, wingu likampokea machoni pao.

Baada ya siku chache ilikuwa siku ya Pentekoste, “…Zikatokea ndimi kama za moto zilizogawanyika na kukaa juu ya kila mmoja wao. Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakaanza kunena kwa lughanyingine, kama Roho alivyowajalia.” (Mat.2:3,4). Walibatizwa kwa Roho Mtakatifu na Moto sawasawa na maneno ya Yohana Mbatizaji na sawasawa na maneno ya Bwana Yesu! Walipata ile ahadi ya Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste. Katika Yoh.7:38,39 Yesu alipaza sauti yake akasema, “ ‘Ye yote aniaminiye Mimi, kama maandiko yasemavyo, vijito vya maji ya uzima vitatiririka ndani mwake.’’ Yesu aliposema haya alimaanisha Roho Mtakatifu ambaye wote waliomwamini wangempokea, kwani mpaka wakati huo, Roho alikuwa hajatolewa, KWA KUWA YESU ALIKUWA BADO HAJATUKUZWA.” Sasa tunaelewa Baba angepa Roho Mtakatifu BAADA YA KUTUKUZWA KWA YESU KRISTO. Petro alieleza tukio la siku ya Pentekoste na maneno haya, “Mungu alimfufua huyu Yesu na sisi sote ni mashahidi wa jambo hilo. Basi IKIWA YEYE AMETUKUZWA kwa mkono wa kuume wa Mungu, AMEPOKEA KUTOKA KWA BABA AHADI YA ROHO MTAKATIFU, naye amemimina kile mnachoona sasa na kusikia.” (Mat.2:32,33). Neno la Mungu ni la ajabu! Mistari ya Biblia inakubaliana pamoja! Na unakumbuka, Yesu alisema katika Yoh.14:16 kwamba, “Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine..”, na Petro alitanganza hapo, “Yesu…amepokea kutoka kwa Baba ahadi ya roho mtakatifu”. Jambo lile Yesu alilolitanganza katika Yohana Sura ya 14 na 16 lilitimizwa (na lilianzishwa) siku ya Pentekoste.

Je, unafikiri ni lazima kungojea mpaka siku ya mwisho tujue kwamba Yesu ni ndani yetu? Hiyo haina maana! Sikiliza Paulo asemalo, “Basi ni Mungu atufanyaye sisi pamoja nanyi kusimama imara NDANI ya Kristo. Ametutia mafuta kwa kututia muhuri Wake na kutupa Roho wake mioyoni mwetu.” (2Wakor.1:21,22).Unaona, Paulo anasema tumewekwa katika Kristo Yesu kupitia kupokea kwa Roho ya Mungu – au anaweka ukweli huo mbili pamoja!  Kwa hiyo, ushuhuda wa waaminio katika Agano Jipya ni, “Nimesulibiwa pamoja na Kristo, wala si mimi tena ninayeishi bali KRISTO NDIYE AISHIYE NDANI YANGU.” (Wagal.2:20). Tumaini la utukufu ni nini? Neno la Mungu linatutangaza, “Kristo ndani yenu!” (Wakol.1:27). Bwana asifiwe! “Siku ile mtajua kwamba ninyi ni ndani Yangu!” Umuhimu wa ukweli huo Paulo anausisitiza kwa kusema, “Jichunguzeni wenyewe mwone kama mnaishi katika imani. Jipimeni wenyewe. Je, HAMTAMBUI ya kuwa Yesu Kristo Yesu yumo ndani yenu? Kama sivyo, basi, mmeshindwa kufikia kipimo hicho.” (2 Wakor.13:5). Unaona? Kuwa Mkristo ina maana Yesu Kristo yumo ndani yako! “Siku ile mtajua mimi ni ndani yenu.”

Zaidi ya hayo “mtajua ninyi mko ndani Yangu”! Je, tunajua tupo ndani ya Kristo? Ndiyo! Kupitia wokovu wa Bwana Yesu na kwa ubatizo wa Roho Mtakatifu ambao Yesu alikufa ili tupokee ubatizo huo, tunaambiwa kwamba, “Bali kwa Yeye (Mungu) ninyi mmepata kuwa ndani ya Kristo…” (1 Wakor.1:30). Baba ametuweka kuwa ndani ya Kristo Yesu, kama Paulo anatufundisha, “Kwa hiyo kama mtu akiwa NDANI YA KRISTO, amekuwa kiumbe kipya…”! Ukweli wa ajabu na mwenye nguvu!

Ukweli huo unaendela! Paulo anaweka wazi, “Kwa maana ninyi mlikufa, nao uhai wenu sasa umefichwa pamoja na Kristo KATIKA MUNGU (kwa Kigriki, ‘ndani ya Mungu’). Mambo haya ni ya maana sana na sipendi kwenda haraka, ningependa kubaki hapo na kuyatafakari lakini lazima tumalize somo! Katika Efeso inasema, “Katika YEYE (au ‘ndani Yake’ Kristo) ninyi nanyi mnajengwa pamoja ili mpate kuwa MAKAO ambayo MUNGU ANAISHI NDANI YAKE kwa njia YA ROHO WAKE.” (Waefeso 2:22). Unaona, katika mstari mmoja anataja Baba, Mwana na Roho. Ndani ya KRISTO YESU tunajengwa tuwe makao ya MUNGU kwa njia ya ROHO! Ukweli wa kina sana! Ilikuwa lazima mtume Paulo kuwakumbusha waumini waliopo Korinto, “Je, hamjui ya kwamba ninyi ni hekalu la Mungu na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?” Kuna mistari mingine ambayo tunaweza kuitaja lakini hiyo inatosha kuthibitisha ukweli huo.

Na turudi Yohana 14. Yesu alisema hatawaacha yatima lakini Yeye atakuja kwao. Tumeona Yesu anaongea juu ya ubatizo wa Roho Mtakatifu. Kwa ubatizo wa Roho Mtakatifu Yesu anakuja kwetu kwa Roho. Katika mstari 15 na 16 Yesu alisema, “KAMA MNANIPENDA, MTAZISHIKA AMRI ZANGU. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine akae nanyi milele.” Katika mstari 23 Yesu anatumia mawazo yale yale tena, yaani, “MTU YE YOTE AKINIPENDA ATALISHIKA NENO LANGU na Baba Yangu atampenda, NASI TUTAKUJA KWAKE na kufanya MAKAO YETU KWAKE.” Haya yote yanahusika siku ile ile. Aliwaambia wanafunzi wake kama wanaendelea kumpenda na kushika neno lake, Roho Mtakatifu atakuja kwao, na Yeye pamoja na Baba watakuja kwao – kwa njia ya Roho! Alisema Yeye na Baba watafanya makao yao kwetu! Kwa hiyo alisema hatawaacha yatima, kwa sababu wangepokea Roho ya Baba na Mwana! Tuseme nini kwa ajili ya wokovu wa nama huo? Unapita ufahamu! Unaona, sehemu hiyo kati mistari 15 mpaka 23 inaongea juu ya jambo lile lile, yaani, itakalotokea siku ile ya Pentekoste. Siku ile mtakapopata ubatizo wa Roho Mtakatifu mtajua, “Mimi niko ndani ya Baba na ninyi mko ndani Yangu na mimi niko ndani yenu.”

Kwa wanafunzi wale, siku ile ilikuwa siku ya Pentekoste, na maneno ya Yesu katika Yohana 14 yanahusu siku ya Pentekoste. Kwa sisi, siku ile ni siku tunapobatizwa kwa Roho Mtakatifu, kama Petro alitanganza, “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja wenu abatizwe kwa jina la Yesu Kristo, ili mpate kusamehewa dhambi zenu. NANYI MTAPOKEA KIPAWA CHA ROHO MTAKATIFU. Kwa kuwa AHADI HII NI KWA AJILI YENU NA WATOTO WENU NA KWA WALE WOTE walio mbali na kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita amjie.’’ (Mat.2:38,39). Kwa hiyo, baada ya watu wa Samaria walitubu na kubatizwa kwa maji, “…mitume waliokuwa Yerusalemu waliposikia kuwa Samaria walipokea neno la Mungu, wakawatuma Petro na Yohana waende huko. Nao walipofika wakawaombea ili wampokee Roho Mtakatifu, …Ndipo Petro na Yohana wakaweka mikono yao juu ya wale waliobatizwa, nao wakapokea Roho Mtakatifu.” Kwa hiyo pia mtume Paulo aliwauliza wanafunzi aliokutana nao Efeso, “Je, mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini?” (Mat.19:2). Paulo alitambua kwamba wanafunzi wale walikosa kitu katika maisha yao ya kiroho. Ndipo aliweka mikono yake juu yao na walibatizwa kwa Roho nao wakanaza kunena kwa lugha na kutabiri.

Lazima tutofautishe kati mambo yanayotofautiana! Yaani, ni kweli kwamba Roho ya Mungu alifanya kazi katika maisha ya watu wa Mungu katika Biblia nzima. Lakini tusijichanganye. Yohana alitangaza, “Mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba. Lakini nyuma yangu anakuja Yeye aliye na uwezo kuliko mimi, …Yeye atawabatiza kwa  Roho Mtakatifu na kwa moto.” Yohana alishuhudia mambo mawili juu ya huduma ya Yesu, yaani, Yeye ni Mwana-Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu, na Yeye atawabatiza kwa Roho na moto. Kwanza ilikuwa lazima Yesu aziondoe dhambi zetu msalabani kabla ya kutupa Roho Mtakatifu akae ndani yetu milele. Kwa hiyo ilikuwa haiwezekani kupokea karama au ahadi ya Roho Mtakatifu kabla ya kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo.

Na tusifikiri ubatizo wa Roho Mtakaifu ni jambo la karama tu, kama kunena kwa lugha. Yesu Kristo alikufa na alimwaga damu yake ili tupokee ukamilifu wa uzima Wake ndani yetu kupitia ubatizo wa Roho Mtakatifu! (Wakol.2:9,10).

Haya kwa ufupi tu na kwa msingi. Kuna mambo mengi kusema juu ya ukweli huo, lakini nilitaka kueleza juu ya jambo la ‘siku ile’ tu. Lengo langu siyo tubishane na maneno bali tufakari neno la Mungu kwa makini sana, tuwe mbele Yake ili aongee nasi kupitia neno lake na kutubariki kupita kiasi.

© David Stamen 2015                        somabiblia.com

Kupakua somo hili bonyeza link: Siku Ile

RUDI  HOMEPAGE

 

One response to “‘Siku ile’ ni siku ya nini? Yohana 14:20

  1. Pingback: somabiblia
 
%d bloggers like this: