RSS

TUMESHINDWA KUTOFAUTISHA UKWELI NA UCHOCHEZI

Kaika gazeti moja waliweka makala na kichwa kifuatacho:

‘TUMESHINDWA KUTOFAUTISHA UKWELI NA UCHOCHEZI.’

Hiyo inatokea katika makanisa mbalmbali pia. Watu wanashindwa kutofautisha kati ya jambo la kuchochea hisia za waumini, na kuwalisha kwa dhati na ukweli kama ulivyo katika Kristo Yesu!

Inazidi siku hizi. Je, umewahi kuona au kuhudhuria mkutano wa kikristo ambapo mhubiri / mchungaji / nabii ANAPAZA SAUTI na kuchochea HISIA za watu na maneno yanayoonekana kuwatia moyo, na kutokana na maneno hayo au na ‘uchochezi’ huo, baada ya kila dakika moja au mbili waumini kwa ghafla wanasimama na kupiga makelele na vigelegele, kupiga makofi au kupunga mikono  na kushangilia – kwa sababu mhubiri amesema mambo makubwa au ameahidi mambo makubwa kwa ajili yao? Inafanana na mkutano wa kisiasa! Inafanana na tabia ya mwanasiasa.

Jambo hili halijengi kanisa, haliwaongoza watu wakue katika Kristo.

Hata kama wahubiri wa namna hiyo kwa kiasi wanafundisha mambo yaliyo kweli, hata hivyo hawatoi nafasi ya kuliruhusu neno la Mungu liingie mioyoni mwa watu kwa ndani sana; hawatoi nafasi ya kutosha kwa waumini watafakari ukweli wa Mungu kwa makini, kwa taratibu ili neno  litie mizizi chini mioyoni mwao – ILI BAADAYE LIZAE MATUNDA MAISHANI MWAO.

Wahubiri hao wanapaza sauti, wanapiga makelele na wanakimbiakimbia toka wazo moja hadi lingine, bila kupumzika na kuchukua nafasi ya kuwalisha watu na neno la Mungu ambalo linaweza kuwajenga juu ya imani yao iliyo takatifu – wanachochea hisia ya watu tu. Wanahamasisha watu waamini kitu kwa njia ya kuchochea hisia yao badala ya kuwalisha na neno la Mungu kwa taratibu. Wanafanya hivyo hasa wanapotaka kukushawishi utafanikiwa. Hiyo ni jambo la saikolojia, siyo la kiroho! Aidha, mhubiri wa aina hiyo anavuta watu kwake na kwa huduma yake, siyo kwake Yesu!

Tatizo ni hili. Baada ya mkutano, huwezi kuishi sawasawa na hisia zako – lazima uishi kwa neno la Mungu! Hisia zako zinaweza kupanda juu sana kanisani, lakini kwa wengi wanapofika nyumbani au kesho yake, tayari wanajisikia ‘chini’ au kujisikia ‘kikombe changu ni kitupu’. Ndiyo maana wengi wanategemea sana na huduma hiyo! Lazima warudi kumsikiliza mhubiri yule ili wajazwe tena na hisia  ya juu! Unaona?

Kondoo wangu waisikia SAUTI yangu…. Tazama mtumishi… hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njia kuu. (Yoh.10:27; Isaya 42:1,2).

Hapo Yesu hakusema kondoo zake zayasikia MANENO yake – alisema waisikia SAUTI yake. Je, tunaweza kujifunza kitu hapo? Unafikirije?

SAUTI ya Yesu ni sauti ya mchungaji wetu, ni sauti ya Mwanakondoo wa Mungu; ni sauti yake aliyejitoa maisha Yake kwa ajili yetu; sauti ya upole, ya unyenyekevu, ya neema, ya upendo ya uwezo. Tabia Yake inatambuliwa na SAUTI YAKE. “Kondoo wangu waisikia sauti yangu.”

Wahubiri wengi wanapaza sauti (hata kwa hasira) wanapohubiri siyo kwa sababu wanao upako wa Roho Mtakatifu bali kwa sababu wanapungukiwa na upako wa Roho Mtakatifu. Wahubiri wengi wanapiga makelele wanapohubiri siyo kwa sababu wanahubiri kwa nguvu ya Roho ya Mungu bali kuficha ukosefu wa nguvu wa Roho ya Mungu katika huduma yao.

SISEMI hatuwezi kupaza sauti tunapohubiri, lakini karama na karama ya Mungu ni tofauti kabisa na kipaji au uwezo wa binadamu!

Wakorintho walikuwa na hamu kubwa sana kuona ‘nguvu ya Mungu’ na ‘huduma yenye upako wa Roho ya Mungu.’ Lakini walitafuta mambo hayo KUPITA KIASI na KWA HIYO wengi wao HAWAKUWEZA kutambua tabia ya Yesu katika huduma ya mtume Paulo! Paulo aliwaandikia, “mimi Paulo mwenyewe nawasihi kwa UPOLE na utaratibu wa Kristo; mimi niliye MNYENYEKEVU nikiwapo pamoja nanyi.” (2 Wakor.10:1).HAWAKUTAMBUA huduma na tabia ya Yesu katika huduma ya Paulo kwa sababu ‘waliyaangalia yaliyo mbele ya macho yao.’ (2 Wakor.10:7). Kuhusu huduma ya Paulo walisema, “akiwapo mwenyewe mwilini ni dhaifu, na maneno yake SI KITU.” Unaona?

Watu wengi siku hizi wameshindwa kutofautisha kati huduma ya Roho ya Mungu na huduma ya kimwili. Tungeweza kusema juu ya watu hao “wana juhudi kwa ajili ya Mungu, lakini si katika maarifa.”

Wakorintho walianza kudanganywa kiasi cha hatari kubwa sana kwa ajili ya hayo (2 Wakor.11:1-4). Walidanganywa kiasi cha kumpokea mtumishi wa Shetani kana kwamba ni mtume wa Mungu! (2 Wakor.11:13-15;19,20).Kwa sababu walikuwa na hamu kupita kiasi kuona huduma yenye ‘upako wa Roho ya Mungu’, waumini wa Korintho walidanganywa kiasi cha kufikiri wale ‘wanaojisifu kwa jinsi ya mwili’ ni mitume wa kweli wa Mungu (2 Wakor.11:18)! Na itatokea vivyo hivyo kwetu kama tukifuata mfano wa waumini wa Korintho! Kuwa na hamu KUPITA KIASI kuona ‘miujiza’ au ‘upako wa Roho Mtakatifu’ au ‘nguvu ya Mungu’ kutakuongoza katika udanganyifu ule ule.

Bila shaka, Mungu anafanya miujiza! Amen! Je, tunapenda kuwa na nguvu ya Mungu katika maisha yetu na makanisani mwetu? Ndiyo! Lakini tusitafute short cut (njia ya mkato) kwa ajili ya hayo! Tusijaribu ‘kuumba’ nguvu ya Mungu kwa njia ya kimwili, kwa kujisifu kwa jinsi ya mwili!

“Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi MKIKAA katika NENO langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli,  tena mtaifahamu KWELI, nayo hiyo kweli itawaweka HURU.” (Yoh.8:31,32).

 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

 
%d bloggers like this: