RSS

KWA KWELI MIMI NAPATA SHIDA SANA. MUNGU TU ANIREHEMU KAMA NAKOSEA.

kirimbai

Mch. Carlos R. W. Kirimbai

Kuna vitu vinaendelea katikati ya Ukristo ambavyo mimi kwa kweli vinanisumbua mpaka vinanitoa machozi.                                                       “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.” (Yoh. 15:13 SUV). 

Upendo siku zote utamsukuma mtu kujitoa kwa kujidhabihu kwa ajili ya yule umpendaye.
Yesu alijitoa kwa kujidhabihu kwa ajili yetu kwa sababu alitupenda. Kama mimi pia ninampenda nitajitoa kwa kujidhabihu kwa ajili Yake, Kanisa Lake na Ufalme Wake.
Yesu aliongea na Petro:

“Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, ‘Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa?’ Akamwambia, ‘Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda.’ Akamwambia, ‘Lisha wana-kondoo wangu.’ Akamwambia tena mara ya pili, ‘Simoni wa Yohana, wanipenda?’ Akamwambia, ‘Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda.’ Akamwambia, ‘Chunga kondoo zangu.’ Akamwambia mara ya tatu, ‘Simoni wa Yohana, wanipenda?’ Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, ‘Wanipenda?’ Akamwambia, ‘Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda.’ Yesu akamwambia, ‘Lisha kondoo zangu’.” (YN. 21:15-17 SUV).

Yesu alitaka kujua kama Petro kweli anampenda. Na akadai kutoka kwa Peteo alishe wanakondoo Zake, achunge kondoo Zake na alishe kondoo Zake. Huwezi kudai kuwa unampenda na usiwe tayari kujitoa kwa ajili Yake. Hili haliwezekani kabisa. Ebu tuangalie hili andiko tena,

“Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo. Wote walionitangulia ni wevi na wanyang’anyi; lakini kondoo hawakuwasikia.” (Yoh. 10:7-8 SUV).

Yesu alijitoa kwa ajili yetu akakubali kufanyika mlango wa sisi kuingia kwenye mambo mema ya Ufalme. Hivi tupo tayari kufanyika mlango wa baraka wa wengine au huwa tunawaona wengine kuwa ni fursa ya sisi kubarikiwa au kupata chochote. Yesu anasema waliyokuja kabla Yake ni wevi na wanyang’anyi maana hao walikuwa wanatumia watu wa Mungu kwa faida zao binafsi na sio kuwepo kwao kumekuwa faida kwa watu wa Mungu. Unapowaona watu wa Mungu je unaona fursa ya wewe kuwa baraka kwao au ndo unaona fursa ya wewe kubarikiwa kupitia wao?

Nahisi kuogopa mno na kutetemeka na tena nahisi machozi na kilio moyoni kuwa wengi wetu katika Kanisa la Yesu huduma imekuwa fursa ya ajira na sio fursa ya kumwonyesha Yesu kuwa tunampenda kwa kuwatumikia watu Wake. Ni rahisi sana kujipima ili kujua nini hasa kinasukuma kujitoa kwako kwa ajili Yake.

Upo kwenye huduma na utumishi hasa kwa ajili gani?

“Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya. Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake.” (Yoh.10:11-13 SUV).

Kama kutumika kwako ni kwa nia na kusudi jema utajitoa kwa ajili ya wale unaowatumikia. Utajidhabihu kwa ajili yao. Kujitoa kwako hakutaamuliwa na nini unakipata toka kwao bali unachopata kutoka kwao kitakuwa matokeo ya kujitoa kwako kwa ajili yao. Ukijitoa kwa ajili yao wataona na kuna siku tu watarejesha hilo kwako tena kwa kiwango ambacho kitakutisha sana.

Maandiko yanasema mtenda kazi astahili posho lake lakini utakosea sana kama utafanya posho kuwa ndo sharti la kutenda kwako kazi maana ukishafanya hivyo tayari wewe ni wa mshahara.
Ukiwa mtu wa mshahara tayari unakuwa umejiwekea mpaka kiwango ambacho utabarikiwa Naye kwa sababu ya utumishi wako Kwake. Ukishakuwa mtu wa mshahara hujali tena hali ya kondoo. Hujali kondoo wanaumia kiasi gani alimradi wewe unapata huo mshahara.

Mbaya zaidi kinachokuweka uwahudumie ni huo mshahara sio upendo wako kwa ajili yao. Huwaombei bali unawakamua. Mbwa mwitu akija anatafuta kondoo unakimbia na kumwacha awararue kondoo. Magumu yakitokea unawakimbia hawa kondoo maana unaona kama vile hawastahili huduma yako kwa kuwa hawana uwezo wa kukulipa.

Sijui wewe ulifanya nini au ulimlipa Yesu nini kustahili kuokolewa Naye. Upo hivyo ulivyo kwa sababu kuna mtu alijitoa kwa ajili yako. Na kuna mtu anadai kusogea mahali kwa wewe kujitoa kwa ajili yake. Sijui huu moyo wa kujitoa umekwemda wapi kwenye Mwili wa Kristo. Kinacho niogopesha mimi ni kwamba kuna siku moja tutasimama mbele ya kiti chake cha hukumu. Kinachoniogopesha zaidi ni kwamba huku duniani tunaweza kuona kuwa tunamtumikia lakini siku ile akasema hakuwahi kutujua.

“Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.” (Mathayo. 7:21-23 SUV).

Inatisha sana iwe huku duniani ulitoa unabii kwa Jina Lake, ulitoa pepo na kufanya miujiza mingi lakini siku ile akakuambia waziwazi bila kupepesa macho hakuwahi kukujua. Sasa kama hakukujua ulitoaje unabii? Kama hakukujua ulitoaje pepo? Kama hakukujua ulifanyaje miujiza mingi kwa Jina Lake? Swali kuu la kujiuliza nini hasa ulikuwa msukumo wa moyo wako kuyafanya yote hayo?

Pili, je unafikiri Mungu anakutumia kwa kuwa upo sawa? Mbona hata punda wa Baalamu alitumika kuongea na nabii? Je, punda kuongea sio muujiza? Hivi unajua ilibidi Mungu atumie punda kwa sababu ilibidi tu aongee na Baalamu? Umewahi kujiuliza kuwa kuna uwezekano kuwa unaweza kutumika kutoa unabii, kutoa pepo na kufanya miujiza kwa sababu ya uhitaji uliyopo na hakuna mwingine wa kutumika ila wewe?

Inatisha sana “KUTUMIKA NA MUNGU” alafu siku ile akukane kuwa hakuwahi kukujua. Inatisha kuliko ninavyoweza kusema. Kama tusipojirekebisha, wengi wetu siku hiyo tutalia na kusaga meno.

Kumbuka Yesu alijitoa kwa ajili yako pasipo wewe kumlipa kitu alafu ndipo akapata malipo ya kukupata wewe. Usimwekee sharti Yeye akulipe ili ujitoe kwa ajili Yake maana atakuwa amekununua mara mbili. Atakuwa kakununua kwa Damu Yake alafu bado unadai akulipe! Humwamini kuwa atakulipa kwa hiyo unamwambia kabla sijafanya kitu nilipe kwanza. Hii haijakaa sawa na itatugharimu.

Ngoja niliachie hapo.

Usije ukasema hukuambiwa.

MCHUNGAJI NA MWALIMU

2016  CARLOS RICKY WILSON KIRIMBAI    Senior Pastor Manna Tabernacle Bible Church, Dar Es Salaam

 

One response to “KWA KWELI MIMI NAPATA SHIDA SANA. MUNGU TU ANIREHEMU KAMA NAKOSEA.

 1. Elton mpanda

  March 18, 2022 at 3:27 pm

  Mungu akubariki mchungaji hakika umenena yaliyo ya moyoni …
  Bora kuwa kiherehere kwa Yesu ili upate thawabu iliyobora ..
  Ooohh napenda kutumika katika Yesu

   

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

 
%d bloggers like this: