RSS

Manabii wa Uongo: ‘Mafanikio’

“Natabiri siku hii ya leo kwamba mizigo yako yote ihusuyo mambo ya kifedha itainuliwa leo! Hutaujua ufukara tena na wale waliokuwa wakisimama kinyume nawe watakujia na kukuheshimu wewe kabla ya mwisho wa mwaka huu. Mafanikio yatakuwa ni yako kuanzia sasa na kuendelea!”

Kuna jumbe za aina hii nyingi nyingi mno katika makundi ya kikristo kwenye facebook. Ikiwa wewe umevutiwa na ujumbe huo hapo juu, ikiwa unauamini ujumbe huo hapo juu, ndipo basi umejiruhusu mwenyewe kudanganyika. Inaonekana kwamba huishi kwa neno la Mungu; unalikataa neno la Mungu kadiri unavyo zifuatilia “njia za mkato” ili kutimiliza matakwa yako binafsi kwa ajili ya baraka na pesa. Maneno kama hayo hapo juu hayailishi imani katika Mungu – yanalisha matakwa yetu wenyewe tu. Na mbaya zaidi ni kwamba watu wanalitumia vibaya jina la Bwana kwa kuzifanya ahadi zilizo tupu (zisizo na kitu) kuamsha matumaini, kuwadanganya watu. Lakini jambo linalovunja moyo ni kuona watu wengi sana, maelfu ya ‘wakristo’ kwa hakika wanaamini ujinga huu na uongo huu. Wanaandika au kukubali kwa kusema “Amen” au “Napokea”. Post moja kwenye facebook ilionyesha picha ya gari mpya, na post nyingine ikaonyesha boksi limejaa mapesa, na hivyo watu wanaamrishwa kudai vitu hivyo iwapo wanavitaka kwa kuandika tu neno “Amen”, na mamia ya watu (wakristo?) wanaandika “Ameni” wakifikiria kuwa Bwana atakwenda kuwapa vitu hivyo viwe vyao kwa sababu tu eti wamevidai! Kupenda vitu vya fedha na baraka za kiinje zimewafanya watu waliache neno la Mungu. Badala ya kuwalisha watu kwa neno la Mungu, hawa manabii wa uongo wao wanachochea watu kupenda vitu, wanachochea tamaa kwa baraka za kiinje, wanachochea uchoyo moyoni mwa watu, na wanalisha watu uchoyo huu kwa kuwapatia ahadi za uongo na zenye mtindo usio wa kibibilia. Ni wazi, tunaweza kuomba kwa ajili ya ndugu zangu ili Mungu awabariki sana katika Kristo na sawasawa na mahitaji yao, na kwa kweli Mungu anaweza ‘kufanya mambo ya ajabu kuliko yote tuyaombayo na tuyawazayo kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu…” (Waefeso 3:20). Na sisi tunaweza kutia moyo sisi kwa sisi kwa kushirikisha neno la Mungu katika ushirika wetu katika Kristo Yesu na katika maombi yetu. Lakini wale wanaotabiri kwa namna hiyo wanaongoza watu wasimtegemee Mungu, wasimngojee Bwana, wasilitafakari neno lake, na badala yake wanawasababisha wakimbiliekimbilie vitu vile wavitakavyo ili wazipate haraka haraka! Na hivyo ndivyo Bilbia inavyotuambia. Paulo anasema,

“Utakuja wakati ambapo watu HAWATASIKILIZA mafundisho ya kweli, ila WATAFUATA TAMAA ZAO wenyewe na kujikusanyia walimu tele WATAKAOWAAMBIA MAMBO YALE TU AMBAYO MASIKIO YAO YAKO TAYARI KUSIKIA.” (2 Tim 4:3). 

Na sasa tunaishi nyakati kama hizo. Je unaona hapo jinsi mtume Paulo anachokisema. Baadhi ya waamini na KWA SABABU YA MATAMANIO YAO WENYEWE, watawatafuta na kuwafuaata “waalimu”  ambao watawaambia MAMBO AMBAYO WANAYAPENDELEA KUYASIKIA. Hivi ndivyo vilevile hawa “manabii”, “wahubiri”, “wainjilisti”, ”mitume” wanavyofanya, wakiwalisha matamanio ya ‘baraka’ na ya kimwili waumini wasiotaka kuishi kwa neno la Mungu.

Nitasimulia kwa nini watu hawa ni manabii wa uwongo baada ya muda mchache tu. Ninaandika haya kwa sababu yawezekana utakuwa unafuata aina hii ya mambo kwa vile unawaona wengine wanafanya hivyo. Au pengine yawezekana unayo maswali kuhusu jambo hili lakini huna uhakika kwa sababu unaona baadhi ya wahubiri mashuuri wanafundisha mambo haya. Au labda wewe ni kijana na wewe mwenyewe unajiuliza juu ya mambo haya. Kwa ajili waamini kama hawa napenda kuwapeni misingi ya kiBilbia kwa ajili ya imani zenu na kuwaonyeni kinyume na kuufuata udanganyifu huu. Ni maombi yangu kuona kuwa baadhi mtageukia mbali na uwongo huo na kutopofushwa na watu hao kwa sababu matokeo ya mafundisho ya aina hii ni kwamba,

“Nao watajiepusha wasisikie  yaliyo kweli,na kuzigeukia hadithi za uwongo.” (2 Tim 4:4).

Sasa, kwa nini watu hawa wanakosea wanaoahidi kwako kwa kukutabiria kuwa mambo yataenda kukubadilikia katika maisha yako? Ni kwa sababu tu kuwa hakuna kitu chochote cha aina hiyo katika Bilbia yote. Hawana mamlaka wala uwezo wowote wa kibilbia au kutoka kwa Mungu ovyohovyo tu huwaambia watu wasiowajua kwamba sasa wanakwenda kupata mafanikio katika maeneo mengi ya maisha yao, eti kwa sabaabu tu unabii au wanaahidi, au kwa sabaabu wanaandika au kuitikia “Amina”! Vilevile kama watu katika 2Kor.11 wanaweza kujisifu kwamba wameitwa na wamepewa uwezo na Bwana. Lakini huwezi kuitwa kufanya mambo ambayo hayafundishwi katika Biblia. Watu wangapi watayasoma mambango / posts zao kwenye facebook? Je, ni mamia ya watu!  Maelfu? Je, wanataka kutuambia kuwa kila mmoja anayeamini maneno yao atakwenda kupata mafanikio mwaka huu, na kwamba watakwenda kuwekwa huru kutokana na ufukara milele! Huo ni udanganyifu, wanaahidi aina nyingi ya mambo mafanikio ya biashara, vibali vya kusafiria, kazi, kupandishwa vyeo, nyumba mpya, afya, kuwa maarufu na watu wengine, na mambo mengi nyingine. Kwa vyovyote watu hupenda vitu hivi, ndio maana hunaswa na ahadi hizi za uongo. Lakini kwa ujumla hawataji ‘kushinda dhambi, upendo, utakatifu, uvumilivu, upole, unyenyekevu nkd. Wanapendalea sana kutabiri ‘baraka za kiinje’ na siyo mambo yahusuyo uzima wa milele na maisha ya kiroho! Hiyo ni undanganyifu kubwa sana.

Kwa kiasi tunaweza kulinganisha manabii wa uongo hawa na manabii wa uongo walioishi wakati wa Yeremia. Manabii wale walitabiri ‘baraka, baraka’ na ‘amani, amani’ ovyo ovyo tu ili wawapendeze watu tu! Mungu alisema juu ya manabii hawa, “Manabii wanatabiri uongo kwa jina langu. Sikuwatuma wala sikuwaweka wala sikusema nao. Wanawatabiria maono ya uongo, maaguzi, maono ya sanamu zisizofaa kitu na madanganyo ya mawazo yao wenyewe.” (Yeremia 14:14). Walidanganya watu wasisikilize neno la Mungu! Wote wawili – manabii na watu waliopenda jumbe zao – hawakujali neno la Mungu na mwishoni walikataa neno la Mungu. Watu walikuwa hamu na shauku kwa ‘baraka’ na maneno mazuri tu, vivyo hivyo inavytokea siku hizi!

Hivyo jambo lingine ninalotaka kusema, huwezi kuahidi mambo haya kwa watu ambao huwajui! Kumpima nabii wa kweli ni pale unapoona mambo anayotabiri hutokea. Hakuna shaka yoyote kuwa ahadi hizi za ziada zinazotolewa haziwezi kuwa na ukweli katika maisha ya watu wengi wanaoamini posts/mabango hayo ya kwenye mitandao ya facebook. Ikiwa itatokea mwamini binafsi akabarikiwa hii ni kwa sababu ya wema na neema ya Mungu katika maisha yao binafsi na wala si kwa sababu ya ahadi hizo za uongo. Kimsingi  ahadi hizo hazina na uwezo kugusa maisha yako wala kubadilisha maisha yako! Ahadi hizo batili hazina matokeo zaidi ya kuwafanyaa watu wajisikie vizuri katika hisia yao kwa muda mfupi tu. Kama watu watakuwa wamebarikiwa basi ni kwa sababu nyinginezo – na tutakwenda kuziangalia sababu hizo nyinginezo muda mfupi!

Nilimpa changamoto mtu mmoja ambaye alikuwa anatoa unabii kwa mambo ya aina hii.

Yeye alinieleza kuwa amepewa mamlaka kufunga kitu chochote kile katika dunia kwa jina la Bwana na hiyo ndiyo huduma ambayo Bwana amempatia. Nikamwambia kuwa huwa mimi natembelea vijijini huko Tanzania na ninakutana na watu wengi sana ambao ni masikini wa kikweli, nilimwambia kuwa watu hao maisha kwao ni magumu na kwamba hilo halikuwa kosa lao hata kwamba wamekuwa masikini. Hivyo nilimwalika kuongozana nami ili tuwatembelee watu hawa pamoja na “akawatabirie mafanikio na maendeleo ikiwa yeye anayo hii huduma ya kufunga na” kufungua”. Kwa vyovyote vile nilijua kuwa asingekubali kwa sababu najua – na pia ndani ya moyo wake lazima alijua – kuwa maneno yake na unabii wake hautakuwa na uwezo ndani ya maisha ya watu hawa masikini. Akanijibu kuwa yeye asingependa kutumia huduma yake ili kujisifu na kujiinua yeye mwenyewe, hivyo hakuandamana nami kuja vijijini. Jambo hili lilinichanganya. Inakuwaje basi kufanya unabii kwa maelfu ya watu usiowajua kwenye  makundi  mbalimbali  ya kikristo  ndani ya facebook isiwe ni kujiinua /kujisifia mwenyewe, bali kuwatembelea watu halisia wachache ambao ni masikini iwe ni kujiinua mwenuewe! Hii kwangu haileti maana yoyote, lakini kwa vyovyote haikushangaza. Ni rahisi kweka ahadi hizi na unabii katika facebook kwa sababu hakuna ambaye atapitia kukagua aone kamamaisha ya watu sasa yamebadilika kwa namna ileile alivyo ahidiwa! Watu wenye kazi zao katika miji kwa kawaida huwa wana fursa bora pia kustawisha maisha yao, kwa hiyo mabadiliko katika baadhi ya maisha huja kutokana na fulsa  zaidi kuliko ahadi hizi za uongo na unabii huo.

Mtu yule aliniambia pia kuwa kama mtu anaishi katika ufukara, basi sababu ya ufukara au umaskini huo imo katika “ulimwengun wa Kiroho”. Sasa sikubaliani na jambo hili, lakini kama hivyo ndivyo ilivyo basi nachanganywa tena. Kwa sababu mtu huyu ameniambia kuwa kama mwanafunzi wa Bwana tunayo mamlaka ya kufunga na kufungua jmbo lolote hapa duniani, sasa kwanini haji ili akazitumie mamlaka hizo kufunga na kufungua sababu za kiroho za ufukara huo? Lakini kwa upande mwingine majibu yake yanathibitisha kile nilichokielezea hapo juu. Yaani, mtu anapaswa kujua mambo yaliyo nyuma ya mtu unaye mhudumia kabla hujaanza kumuahidia mambo maalum au kumwombea!I Anakuwaje yeye au hata watu wengine wanaweza kuahidi watu kwenye mitandao ya internet wakati hawajui chochote kuhusu watu hao? Hii ni machanganyiko na udanganyifu! Mtume Paul anawaambia wafilipi kuwa yeye aliyeianza kazi njema ndani yao ataimaliza katika siku ya Kristo (Wafil. 1:6). Analijuaje jambo hili? Anasema kuwa ni haki kwake kuwa anajisikia namna hiyo kwa ajili yao kwasababu “anao watu hao katika moyo wake”! Ni jambo la uzuri wa jinsi gani hili! Mtume Paulo anawapenda waumini hawa na anawaombea pia anaweza kuwasiliana nao na kuwatia moyo na kuwapa neno la Mungu, kwa sababu watu hao wamo moyoni mwake. Mtume Yohana anaomba kwa ajili ya Gayo (3Yohana1:2), ”Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako kama vile roho yako ifanikiwavyo.” Hapa tena Yohana ansema mambo haya kwa mtu fulani anaye mfahamu, na tafadhali gundua kuwa hapa anaomba hivyo na wala hatoi unabii. Kwa vyovyote tunaweza kuwaombea watu, lakini watu hawa kwenye facebook, wao huenda mbali zaidi ya hili la kuomba. Husema kwa mfano, “Natabiri….”, “Nasimama kwa mamlaka ya Bwana nami natangaza..”, “Bwana asema…”. Kwanini watu hawa wanafanya hivyo? Wanafanya hivyo kwa sababu wanataka kutengeneza matarajio ndani ya wasomaji  waone kuwa jambo hilo linakwenda kutokea! Unabii ni jambo linalo kuja kuwa kweli! Hizo ni mbinu za kuwadanganya watu. Hata kama watu hawa wanataka kuwatia moyo watu wengine, bado wanawadanganya kwa sababu mbinu hii ya kutabiri / kuwatolea unabii wa mafanikio watu katika maeneo yote ya maisha yao pasipo kuwapatia kumbukumbu / nukuu ya neno lolote la Mungu, pasipo kumbukumbu yoyote ya hali ya kiroho ya watu wanaoongea nao, pasipo ufahamu wa maelfu ya watu watakaosoma mabango/maandishi hayo yao – hiyo sio kibiblia.

Zaidi ya hayo, wao huahidi watu wasiowajua mambo yasiyowezekana na kwa ujumla wake sio ya kibiilia. Kama vile kusema, “Furaha ya Bwana Haitakauka.” Ni Kweli? Hii inategemea mwenendo wako wa kiroho mbele za Bwana na wala si kwa mtu anayesingizia kutoa unabii kwenye facebook! “Ninaamuru (‘decree’ kwa Kiingereza) wewe upate hekima ya ki-Ungu.” Unaamuru? Huwezi kufanya hivyo. Mungu tayari amekwisha tuwezesha kupata hekima yake, ikiwa tutamwomba kwa imani anasema atatupatia kwa ukarimu! (Yak 1:5,6). Eti wao wanasema, “Maisha yako ya kimaombi hautasumbuliwa tena.” Huwezi kutabiri au ‘decree’ mambo kama haya kwao wengine! Hii inategemea mwenendo wako wa kiroho na kuishi kwako kiroho mbele za Mungu. Wanasema “Pokea upako wa ziada wa roho wa utii.” Utii ni jambo ambalo Mungu analitarajia litoke kwetu kwa sababu ya neema yake juu yetu na  kwa sababu ya Roho mwake aliyetupatia tayari. Sio roho ambaye humwagwa ovyo ovyo kadiri ya maneno yako! Wanaendelea kusema kuwa, “Maadui wote wanaopambambana nawe wataangamizwa.” Lakini neno la Mungu linatufundisha kuwapenda maadui zetu, na sio kutafuta kuangamizwa  kwao. Wengine wanatabiri kama ifuatayo, “Kutoka siku ya leo matatizo yote yako ya kimwili na kiroho yatahamishwa kwa adui zako!” “Natabiri kila achapaye ‘Amina’, Mungu atawekea kicheko cha furaha ndani yake kwa jina la…”.  Manabii hao wa uwongo husema mambo ambayo ni kinyume kabisa na Bibilia, huvuta mambo hewani tu, jambo lolote linalowajia katika ufahamu wao ambalo wanaamini litawajaribu watu kunaswa katika mtandao wao wa uongo.

Sababu ya pili kwa nini mambo hayo yaandikwe kwenye facebook, au hata sehemu nyingine yoyote, ni makosa kwa sababu ya kile ambacho tayari nimekwisha kisema hapo juu, kwa kutaja tu hayawakilishi neno la Mungu kwa watu. Wanawapatia watu kile ambacho wanakipenda kwa kawaida kuwapa na kuwataka watu “wadai” (‘Claim it”). Hakuna hata sehemu moja katika Biblia inapofanya mambo kama haya kwa namna hiyo. Baraka za Mungu kwa Wakristo huja kutokana na kile ambacho Mungu alikifanya kwa ajili yetu kupitia Bwana wetu Yesu Kristo, na kutokana na kuamini, kumpenda na kumtii Bwana wetu Yesu Kristo. Hakuna mahala popote katika Biblia ambapo nabii hufanya ahadi za ghafla ili kwamba yeyote anaye zidai zitasababisha mafanikio katika biashara zao, ya kwamba muda mfupi watapata muujiza wao utakaowashangaza, eti hawatajua ufukara tena n.k.d. Wanafanya hayo bila hata kuonyesha kumbukumbu ya muktadha wa maisha ya watu hao. Hutauona ujinga huu mahali popote katika Biblia.

Mtu mmoja aliwahi kuniambia kwamba huduma za jinsi hii ziko pale ili kuwatia moyo watu ambao huenda watakuwa wanajisikia kushushwa moyo. Hii ndiyo inayonifikisha mimi katika eneo la kujua kwa nini mtindo huu wa kutia moyo watu ni udangaanyifu na inakubaliana na yale yaliyosemwa katika 2 Tim. 4, ambayo nilikuwa nimenukuu hapo juu. Maandishi hayo katika facebook kwa ujumla wake hayatumii neno la Mungu katika kuwatia moyo watu, kama vile nilivyoonyesha  katika mifano hapo juu wao hutengeneza maelezo ya kiujumla kuhusu mafanikio ambayo watu watapata katika maeneo yote ya maisha yao. Kwa mfano, “Natabiri kuwa kuanzia sasa na kuendelea mafanikio yataanza kukuandama na wala hayatakuacha katika jina la…” Unabii huu hauna mstari wowote wa kibiblia au kweli yoyote ya kibibilia! Inaahidi mambo makubwa pasipo taratibu! “Mafanikio kwa ajili ya maisha yako yako pale kwa ajili yako – kuamini tu na kuanza kudai.” Huo ni udangaanyifu.

Ikiwa tunahitaji kuwatia moyo waumini basi ni kitu gani kilicho bora kuliko neno la Mungu? Mungu anasema, “Sitakuacha wewe wala kukusahau.” “Ikiwa Mungu atakuwa upande wetu ni nani atakuwa kinyume chetu?” “Hufanya njia mahala pasipo na njia.” “Usitegemee akili zako mwenyewe, bali katika kila jambo mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, katika kila njia zako umkiri yeye naye atayanyoosha mapito yako.” “Tafuteni kwanza ufalme wa Mungu na haki yake, na hayo yote mtazidishiwa.” “Na ahimidiwe Mungu, na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, na Mungu wa faraja zote, anayetufariji katika mateso yetu yote…” Je, kuna kutiwa moyo gani kuzuri zaidi ya neno la Mungu lenyewe (Yoh6:63). Lakini manabii hao wa uongo wanazuia kutumia maneno yanayotia uzima ya Mungu. Kwanini wanafanya hivyo? Jibu la swali ni jepesi. Kwa sababu neno la Mungu huielekeza mioyo yetu kwake Mungu (sio kwenye vitu au hata kwa baraka za ‘kinje’).

Kuweka matumaini yetu kwake yeye, kusubiri kwa upole matoleo yake kwa ajili ya maisha yetu! Neno la Mungu pia huzijaribu imani zetu na upendo wetu. “Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako, aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa ili akutweze, kukujaribu, kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake au sivyo. Akakutweza akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua, apate kukujulisha kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Bwana (Kumb.8:2,3). Neno la Mungu huelekeza mioyo yetu kumpenda na kumtegemea Mungu zaidi kuliko mambo ya kinje. Neno la Mungu haliulishi uchoyo wetu, au matamanio ya vitu.

“Lakini utauwa na kuridhika ni faida kubwa….Lakini kama tuna chakula na mavazi, tutaridhika navyo. Lakini wale watu wanaotamani kuwa na mali kwa  huanguka kwenye majaribu na wamenaswa na tamaa nyingi za kipumbavu,  zenye kudhuru, zinazowazamisha watu katika uharibifu na maangamizi. Kwa maana kupenda fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha amani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi. Lakini wewe, mtu wa Mungu, yakimbie mambo haya yote. Fuata haki, utauwa, imani, upendo, saburi na upole.” (1 Tim. 6:6-11)

Biblia haitufundishi sisi kwamba “Tafuteni mafanikio na muamini mafanikio kwa moyo wenu wote na mtayapata!” Inatufundisha kwa urahisi tu na kwa uweza kutafuta kwanza ufalme wa Mungu! Hapa tunaweza kuona kuwa neno la Mungu halichochei matamanio yetu kwa ajili ya mambo ya kidunia! Wala haituahidi sisi mambo tunayo yataka tuyapate, ila inatuhakikishia kuwa Mungu yu pamoja nasi, na kwamba atatupatia mahitaji yetu yote, siyo yote tunayo yataka! Sababu inayowafanya watu hawa wayapende mafundisho hayo ya unabii wa uwongo na wakivutwa nayo, ni kwa sababu wanajitoa kwa njia nyepesi na ya mkato kwa mambo ambayo wangependa kuyapata binafsi wakati huu. Hatuambiwi wala kutiwa moyo kuyatafakari neno la Mungu, na kumwamini yeye, badala yake tunaletewa utimilifu wa harakaharaka wa yale tunayotaka “kuyapokea” au “kuyadai”, au kuandika “Ameni”.

Jambo lingine ambalo nalo nataka kulionyesha ni kuwa tusishangazwe na mambo haya. Tayari nimenukuu Timotheo sura bya pili hapo juu, lakini Paulo anaweka wazi kuwa wale wanaoyatafuta “mambo ya kiinje” na ambao wanavutiwa na watu wanaojifanya wenyewe kuonekana kama ni watu muhimu kwa sababu ya huduma zao, watu wa aina hii hujiandalia wenyewe katika udanganya. Wako tayari “kuipokea injili nyingine”, “Yesu” mwingine na “roho” mwingine.  Sio kwamba walipagawa na mapepo, bali ni kwa sababu watu hao walikuwa na nia isiyo sahihi. Na kwa sababu ya nia hiyo isiyo sahihi shetani angeweza kuwadanganya.

Ninyi hutazama mambo kwa nje tu…Lakini naogopa kwamba, kama vile yule nyoka kwa hila zake za uongo alimdanganya Hawa, fikira zenu zaweza kupotoshwa, mkauacha uaminifu wenu wa kweli kwa Kristo….. Kwa sababu kama mtu akija na kuwahubiria Yesu mwingine ambaye si yule tuliyemhubiri, au kama mkipokea roho mwingine ambaye si yule mliyempokea, au injili tofauti na ile mliyoikubali, ninyi mnaitii kwa urahisi….Kweli ni kwamba mnachukuliana na mtu akiwatia utumwani au akiwatumia kwa ajili ya kupata faida au akiwanyang’anya au akijitukuza mwenyewe au akiwadanganya.” (2 Wakor.10:7; 11:3,4,20).

Paulo alikuwa wazi kabisa kuwahusu wahubiri waliokuwa wakiwapotosha watu! Unaweza kujisomea kuhusu watu hao mwenyewe katika 2 Kor 11. Ikiwa tutawasikiliza watu wanaojiinua wenyewe kwa huduma yao kwa kudai wao ni aina fulani ya manabii, basi tutakuwa tunatembea katika hatari ya kupokea ‘Yesu mwingine’, na ‘injili nyingine – ‘injili ya mafanikio’ – na ‘roho nyingine’, hapa sipambani kuhusu maneno, wala sijaribu kukubadili wewe uelekee kwenye aina nyingine ya mafundishao, bali nataka tuelekeze mioyo yetu na nia zetu kwenye neno la Mungu na kuishi kwa neno la Mungu.

Ni matumaini ya kuwa waweza kuona ahadi hizi zote za uwongo inapingana na neno loa Mungu. Kasoro kubwa, na udanganyifu uliopo ni kuwa wanatupora/nyang’anya ule utoshelevu wetu wa kiMungu, kuliko kutufanya sisi tutosheke na Mungu. Wao huchochea matamanio ya mafanikio, utajiri, ”baraka” na kwa ajili ya mambo ya kidunia.

Ushuhuda wa mtume Paulo ulikuwa ni huu, “kwa Yeye ulimwengu umesulibiwa kwangu, nami nimesulibiwa kwa ulimwengu,” (Wagal.6:14); na kwamba, “Kwa maana kwangu mimi, kuishi ni Kristo na kufa ni faida,”  na kwamba, “Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, sasa nayahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara tupu nikiyangalinisha na faida kubwa ipitayo kiasi ya kumjua Kristo Yesu Bwana wangu, ambaye kwa ajili Yake nimepata hasara ya mambo yote, nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nimpate Kristo,” na tena kwamba, “Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yo yote. Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. Naweza kuyafanya mambo yote katika Yeye anitiaye nguvu.” (Wafilipi 1:21; 3:7,8; 4:11-13). Bwana apewe sifa kwa neema yake! Je utoshelevu wako unatokana na yale mahusiano yako na Baba na Mwana? Au unajisikia kiu kwa mambo yale ambayo yametabiriwa kwenye Facebook? Je, unampenda Yeye kiasi kwamba kumtegemea yeye kukuongoza, kukubariki na kukupatia mahitaji unayoyahitaji kwa muda sahihi? Je, huo ndiyo ushuhuda wako, ndugu yangu, dada yangu? Je, tunampenda Yesu zaidi sana kuliko vitu vyote vingine duniani – zaidi ya ‘mafanikio’ na matekelezo ya ndoto zetu na malengo yetu? Ushuhuda wa Paulo huwakilisha maisha ya mkristo. Tunapaswa kuishi vivyo hivyo. Au tunajaribu tupate yale tunayatakayo binafsi kupitia ya Injili ya Yesu Kristo ili kujipendeza na kujifurahisha? Paulo anatufundisha kwamba tumesulibiwa na Yesu Kristo “ili kwamba wote wanaoishi wasiishi tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili Yake Yeye aliyekufa na kufufuka tena kwa ajili yao.” (2 Wakor.5:15)? Je, Yesu ni thamani kwako sana kiasi kwamba huna shauku kwa mambo yale ambayo watu wengine wanayo? Je, unaishi maisha ya kikristo? Je, Yesu anatosha?

Basi hapo hutakuwa unavutwa au kupotoshwa na hizi ahadi zisizo na kitu. Katika Kristo utajua kuwa Mungu Baba amekubariki wewe kwa baraka zote za rohoni katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo Yesu!

Dhambi ya Wapiga Ramli siku hizi.

Watu (Je, Wakristo?) hutoa mambo wanayoyaita ni jumbe za kiunabii kwa ajili ya wiki inayokuja, mwezi au hata mwaka –  sawa sawa na wapigaramli wa kidunia wafanyavyo. Huu sio tu ni udanganyifu bali ni dhambi baya sana. Ngoja nikueleze kuwa hakuna mtu mwenye ujumbe wa kinabii toka kwa Mungu kwa ajili yako kwenye facebook au hata maeneo mengine yoyote kwenye interneti yahusuyo mambo yanayokwenda kukutokea katika maisha yako wiki hili au mwezi huu na hata mwaka huu.

Mungu amewazuia watu wake maalum kupiga ramli, kufanya ulozi au uaguzi, kama watu wapagani wafanyavyo (Kumb18;14, Isaya 2:6; Mika 5:6; Matendo 16:16). Huko ulaya kwa mfano, watu husoma magazeti kuzisoma nyota zao. Wapo wapiga ramli ambao husema wanasoma nyota kisha huwaambia watu nini kinakwenda kuwatokea katika maisha yao katika wiki hiyo, mwezi au mwaka. Kinachoshangaza watu wanaosema wao ni wakristo huiga mambo ya watu wa dunia ambao wao hutumia mambo hayo yaliyozuiwa na Mungu kuyafanya!

Watu hao wanaweza kutenda au kuamini mambo hayo lakini matendo hayo ya dhambi yanaonyesha jinsi gani tumekuwa mbali na ukweli wa Biblia!.Hatujawahi kuona jambo lolote kama hili katika Biblia eti kwamba “mwezi huu unakwenda kuona biashara yako ikifanikiwa.” Tena aina hii ya unabii wa udanganyifu unawekwe kwenye internet kwa ajili ya kila mmoja kusoma – kana kwamba jambo hilo linakwenda kuwa ni kweli kwa kila mmoja mwenye biashara zake! Watu wanaofanya mambo kama haya au wale wanaofuata habari kama hizi, hao ni wale wanaozifuata ‘roho nyingine’, au ‘Yesu mwingine’. Kwamba mtu yeyote ajaribu kuhalisisha aina hii ya dhambi, inaonyesha jinsi walivyopofushwa  kwa roho ile wanayoifuata.

Tumeitwa kumpenda Mungu na kumtegemea katika kila kitu kwa moyo wetu wote. Bibilia inasema “Basi msisumbukie ya kesho, kwa kuwa kesho yajisumbukia yenyewe; yatosha kwa siku maovu yake.(Mat.6:34).

Kwa nini basi unataka kutafuta mambo yajayo. Unamtenda dhambi Mungu na unaitendea dhambi nafsi yako mwenyewe. Ndiyo kwa vyovyote upo unabii katika Biblia lakini ni maalum kwa mtu au kikundi fulani cha watu katika muktadha/hitimisho maalum. Haiwi ni matangazo ya ujumla kwa ajili ya yeyote yule kusoma na kuyatumia katika maisha yao isivyopasa/ovyohovyo tu.

© David Stamen 2014                          somabiblia.com

Kupakua somo hili bonyeza link: MANABII WA UONGO wa Mafanikio

RUDI KWA HOMEPAGE

 

 

One response to “Manabii wa Uongo: ‘Mafanikio’

  1. Pingback: somabiblia

Leave a Reply