RSS

MAJI YA UPAKO? FEDHA YAKO NA IPOTELEE MBALI PAMOJA NAWE…

Simoni alikuwa mchawi, lakini mara baada ya kusikia habari njema ikihubiriwa na Filipo, alibatizwa. Lakini alipoona ya kuwa watu wanapokea karama ya Roho Mtakatifu kwa kuombewa na mtume Petro, naye alitamani kupata uwezo huo, ndipo akatoa PESA kumpa Petro akisema, “Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu.” (Matendo 8:19).

Simoni alikuwa bado hajatubu kwa kweli, ule uchawi wake wa zamani. Alikuwa bado anataka kuwa na nguvu za kutenda miujiza ili kuwavutia watu, na kujipatia pesa!

Jibu la Petro ni onyo kwetu sote,

“Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali.” (Matendo 8:20).

Maneno haya aliambiwa nani? Aliambiwa mtu yule ambaye aliyekuwa anatenda mambo ya kichawi, na ambaye sasa alikuwa anajaribu kuingiza tamaduni na fikra za kichawi kanisani!

Niliambiwa na ndugu mmoja kanisani kwetu aliyetokea Zambia, kwamba nchini kwao waganga wa kienyeji huacha uchawi vijijini na kwenda kuwa wachungaji wa makanisa katika miji na majiji, nao husema eti unaweza kupata pesa nyingi ukiwa mchungaji mjini kuliko kuwa mganga wa kienyeji kijijini kwa kuwa kule mjini unatumia nguvu zile zile za kichawi kana kwamba ni nguvu za Mungu kufanya miujiza na kuponya au kuokoa!

Matendo ya mitume sura ya 8 inatufundisha kuwa tamaa ya kutumia miujiza ili kupata pesa inatokana na tamaduni za kichawi.

Inatufundisha pia kuwa kama tunadhani tunaweza KUNUNUA kitu cha kutuponya, kutuokoa au kutupatia usalama, basi tumeingia  katika ushirikina na utamaduni wa kichawi. Kubwa zaidi ni kwamba inatuonya kuwa tupo katika hatari ya kutokuwa na sehemu katika ufalme wa Mungu, tunapotenda hayo!

Iwapo muhubiri yeyote yule akijaribu KUKUUZIA wewe chumvi, maji ya upako, au kitambaa, akidai kuwa vitu hivyo ndivyo vitakuletea baraka na uponyaji au mafanikio, basi mtu huyo atakuwa anajiweka yeye mwenyewe kwenye eneo lenye hatari sana. Ikiwa na wewe utalipa pesa zako ili KUNUNUA uongo wa vituko kama hivyo, ndipo na wewe utakuwa umejiweka mwenyewe katika eneo la hatari pia. Biblia inatupatia maonyo yenye kutuokoa na yenye usalama kutokana na mwenendo mbaya huo na mtazamo wa kiuchawi kama huo pale Petro anapomwambia Simoni,

“Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali.”

Je, wewe unapenda kuwa kwenye kundi lilelile kama Simoni aliyekuwa amefanya uchawi? Hebu basi fikiri na ujiulize wewe mwenyewe, NI SEHEMU GANI katika Agano Jipya au hata ndani ya Biblia nzima ambapo alitokea mtu kumlipa mtumishi wa Mungu pesa ili apokee uponyaji au baraka? Jawabu la swali hili ni wazi kwamba hakuna popote pale! Hakuna kitu kama hiki kinachofundishwa na Biblia. Na kwa sababu hiyo basi yakupasa moja kwa moja kukataa fundisho hili na vitendo vyake wanavyofanya!

“Na katika kutamani watajipatia faida (yaani, pesa) kwenu kwa maneno yaliyotungwa; ambao hukumu yao tangu zamani haikawii, wala uvunjifu wao hausinzii.” (2 Petro 2:3).

Mistari hii inamhusu nani siku hizi?

Inamhusu ye yote (aitwe mtume, nabii, askofu au mchungaji) ANAYEMLAZIMISHA au KUMSHAWISHI mshirika (au mtu ye yote) AMTOE/AMLIPE PESA KABLA YA KUMWOMBEA, yaani, ampe pesa kwa ajili ya maombi yake, au amlipe pesa kununua maji ya upako nk, au kwa ajili ya huduma yake ye yote aliyodai ameipokea kutoka kwa Mungu.

Haya yote ni dhambi kubwa sana! Hiyo ni biashara. Wanajaribu kutumia ‘karama’ ya Mungu au huduma yao kujipatia pesa. Kila afanyaye hivyo yupo chini ya hukumu ya mstari huu wa hapo juu! Haupo hata mfano mmoja katika Biblia ambapo mtumishi wa Mungu ye yote anasema, “Nipe pesa kwanza kabla sijakuombea,” au “Nunue vitu hivyo ambavyo yatakupatia baraka, usalama na mafanikio.”

Tayari wengi wamehamia kwenye kutukuza maji ya upako, mafuta ya upako, sabuni za upako, chumvi ya upako, vitambaa na nguo za upako na kila aina ya vitu vya upako mpaka kanisa linaonekana kama kituo cha waganga wa kienyeji maana mambo ambayo tunaelekezwa kanisani sasa hayana tofauti kabisa na mambo ambayo watu wanaambiwa wakienda kwa waganga wa kienyeji.

Usishiriki matendo ya wale watakao pesa yako kwa ajili ya maombi yao, au ya wale watakao kukuuzia maji ya upako nk! Haijalishi ikiwa ni wengi! Haijalishi ikiwa anaitwa mtume au nabii. Ukumbuke mstari ule uliosema, “Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, KWA KUWA UMEDHANIA YA KUWA KARAMA YA MUNGU YAPATIKANA KWA PESA… moyo wako si mnyofu mbele za Mungu.” (Matendo 8:21,29).

Juu ya karama au huduma tuliyoipewa na Mungu, Yesu alisema, “Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; MMEPATA BURE, TOENI BURE.” (Mathayo 10:8).

Ushuhuda wa Paulo ulikuwa ufuatao: “SIKUTAMANI FEDHA WALA DHAHABU, WALA MAVAZI YA MTU….Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, NI HERI KUTOA KULIKO KUPOKEA.” (Matendo 20:33,35).

[ Lakini naomba usinielewe vibaya. Tafadhali uelewe muktadha wa somo hili kwa makini! Sijaandika juu ya msaada kwa ajili ya kazi ya watumishi wa dhati wa kanisa. Kama mtumishi wa Mungu ameitwa kulitumikia kanisa la Bwana, basi ni jambo la upendo na haki kuwa washirika wamsaidie sawasawa na mahitaji yake na familia yake, sawasawa na neno la Mungu: 1 Wakor.9:7-15; 1 Tim.5:17,18; Luka 10:7. Lakini mhubiri ye yote anayetaka pesa yako kwa ajili ya maombi yake, au anayejaribu kukuuzia “vitu vya upako”, huyo siyo mtumishi wa kanisa la Bwana Yesu. ]

 

David Stamen                      http://www.somabiblia.com

 

Comments are closed.

 
%d bloggers like this: