RSS

Hila na mbinu za Shetani na jinsi ya kuzishinda. Vita vya Kiroho kweli kweli.

Hila na mbinu za Shetani na jinsi ya kuzishinda. Vita vya Kiroho kweli kweli.  

Mungu amesema, “Mimi ndimi BWANA Mungu wako aliyekutoa Misri, kutoka nchi ya utumwa. Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga katika umbo la kitu cho chote kilicho juu mbinguni au duniani chini au ndani ya maji.” (Kutoka 20:2-4).

Hila ya Shetani ndiyo kupotosha tabia ya Mungu mawazoni mwetu; mbinu za Shetani ndiyo kuharibu sura ya kweli ya Mungu mioyoni mwetu ili tusiamini Mungu, ili tusiamini wema, neema na rehema zake, ili tusiamini Yesu anaweza kutuokoa kabisa! Shetani anajaribu kutushawishi kwamba Mungu ni dhidi yetu (na hata kwamba watu wengine ni dhidi yetu!), kwamba Mungu ametuacha au hata Mungu anatuadhibu kwa ajili ya jambo fulani. Kusudi la Shetani ni tusitambue jinsi Mungu alivyo kweli kweli!

Mwanzoni Shetani alikuja bustani adanganye Eva, kumvuta afanye dhambi. Shetani anakuja na anaongea na maneno kama haya mioyoni mwetu, “Inaonekana tamu sana, siyo ndiyo? Unapenda hiyo, siyo ndiyo? Unahitaji hiyo, siyo ndiyo? Jambo hili litakuletea furaha, raha na anasa! Inavuta sana, siyo nidyo? Huwezi kupinga! Chukue tu! Fanya tu! HUTAPATA HASARA!” Mawazo haya yote ni udanganyifu tu! Shetani anataka ufanye dhambi tu na kukutenga na Mungu! Mawazo haya siyo mawazo yako tu. Shetani mwenyewe anajaribu kuyaingiza mawazo hayo moyoni mwako ili uamini uongo wake na usiamini Mungu!

Lakini hila za Shetani zinakwenda kwa ndani zaidi. Shetani anajaribu kupanda mbegu ya uovu – ya kutokuamini – ndani ya mioyo yetu. Alimwambia Eva,

“Hakika HAMTAKUFA, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu.” (Mwanzo 3:4,5).

Unaona? Shetani anataka kutushawishi kwamba Mungu ni mwongo (‘hamtakufa’) na Mungu hataki tuwe kama Yeye! Lakini hayo yote yalikuwa kinyume cha ukweli! Mungu alikuwa amesema, “Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu.” (Mwanzo 1:26). Hila na mbinu za Shetani ni kukushawishi kuwa Mungu ni dhidi yako, anakunyima baraka Zake, amekuacha peke yako na hata Mungu anakuadhibu. Hilo ndilo lengo lake. Kwa hiyo neno la Mungu linasema, “Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu MOYO MBOVU WA KUTOKUAMINI, kwa kujitenga na Mungu aliye hai.” (Waebr.3:12).

Mara Adamu na Eva walipofanya dhambi, walianguka gizani kabisa (‘siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika’ – Mwanzo 2:17) na mara moja Shetani aliendelea kazi yake kwa KUPOTOSHA TABIA YA MUNGU mioyoni mwao! Adamu na Eva walijificha mara moja! Kwa nini? Kwa sababu walifikiri Mungu atakapokuja atawahukumu, kuwaponda na kuwaharibu! Walifikiri kwamba sasa Mungu hawapendi na Yeye ndiye kinyume chao na dhidi yao. (Je, umewahi kujisikia vivyo hivyo?) Walitetemeka kwa hofu! Mawazo haya siyo toba mioyoni mwao! Mawazo hayo yanatokana na Shetani! Mawazo haya ni matokeo ya kupokea maongo (sumu) ya Shetani anayepotosha sura ya Mungu ili tufikiri Mungu ndiye dhidi yetu! Mbinu za Shetani ni tutekwe nyara na mawazo na hisia za kukatiliwa – anataka tubaki peke yetu tusiende kwake Bwana!

Kwanza Ibilisi anakuja kutuvuta tufanye dhambi. Mara alipofaulu kufanya hivyo, anaanza kutushitaki kwa kali, kutulaumu na kuponda dhamira yetu ili tujisikie hatufai kabisa na tumekataliwa kabisa! Je, umewahi kupatwa na mawazo ya namna hiyo? Kwa uongo wake Shetani anataka tujisikie tumetengwa na Mungu bila tumaini na hatuwezi kwenda Kwake aliye Mwokozi wetu kwa sababu Yeye ni dhidi yetu.

Adamu na Eva waliweza kufikiri na kusema, “Kumbe, tulikosa kabisa, tulifanya dhambi mbele ya Mungu. Kwa kweli Mungu alifanya yote vizuri na alitubariki kupita kiasi na yule nyoka alitudanganya! Haya, na twende kwake Mungu na tukiri dhambi zetu mbele Yake. Na tuiname mbele Yake na tutobe! Mungu ni Mwema na Mwenye huruma, inawezekana atatusamehe!”

Haya ni toba! Haya ni imani! Waliweza kufanya hivyo – lakini sumu (uongo) ya Shetani ambayo inapotosha tabia (sura) ya Mungu machoni pa watu iliingia sana mioyoni mwa Adamu na Eva na iliwaongoza kutokumwamini Mungu na kuamini Mungu ni kinyume chao! Hiyo nidyo hila na kazi ya Shetani. Hilo ndilo lengo lake – ufikiri Mungu hakupendi na hata anakuchukia; kufikiri Mungu ni dhidi yako, ujazwe na hisia na fikra za kukatiliwa! Ibilisi anataka kuharibu imani yetu kwake Yesu na kutuweka gizani ambopo hatuamini Mungu. Tukiendelea kuamini Mungu ni kinyume chetu, ndipo hatutaweza kupokea msaada kutoka Mungu (ila Yeye ni juu yote na anaweza kufanya apendalo) kwa sababu tupo hali ya kutokuamini! Tukumbuke maandiko yasemalo,

“pasipo imani haiwezekani kumpendeza (Mungu).” (Waebr.11:6).

Kwa sababu hiyo, Waisraeli walizunguka jangwani miaka arobaini! Angalie ni wapi kutokuamini kwa Waisraeli kuliwapeleka! Sikilize maneno yao!

“Ni kwa sababu Bwana AMETUCHUKIA, ndipo akatutoa katika nchi ya Misri, apate kututia katika mikono ya Waamori, ili KUTUANGAMIZA.” (Kumbu.1:27).

Kumbe! Mungu alikuwa amefanya miujiza huku Misri na jangwani kwa ajili ya watu Wake ili kuwaokoa kwa sababu aliwapenda sana. Alikuwepo miongoni mwa watu Wake, akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, na usiku, ndani ya moto mfano wa nguzo! HATA HIVYO, kutokuamini kwao kuliwapeleka kuamini Mungu aliwachukia na akatengenza mazingira yao ili kuwaangamiza! Kwa kweli hiyo ni ‘moyo mbovu wa kutokuamini’. Tusifuate mfano wao! Hasa kwa sababu sasa ‘Mungu ameonyesha pendo lake Yeye Mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu’!

Hiyo ni mbinu za Shetani, kama nilivyosema, kupotosha tabia ya Mungu mawazoni mwetu na mioyoni mwetu tusiamini Mungu na atufanye mioyo yetu iwe ugumu! Kwa hiyo maandiko yanasema, “Kwa hiyo, kama anenavyo Roho Mtakatifu, Leo, kama mtaisikia sauti yake, MSIFANYE MIGUMU MIOYO YENU, Kama wakati wa kukasirisha, SIKU YA KUJARIBIWA KATIKA JANGWA.” (Waebr.3:7,8).

Lakini, na tutambue mafundisho ya neno la Mungu – sisi hatuwezi kumlaumu Shetani! Mungu hakumlaumu Shetani kwa ajili ya kutkuamini na dhambi za watu Wake jangwani! Maandiko yanasema juu ya watu Wake jangwani, “wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao,” (1 Wakor.10:5). Na kama tulivyosoma, Mungu aliwalaumu watu Wake kwa ajili ya ‘moyo mbovu wa kutokuamini’ wao.

“Tena ni akina nani aliochukizwa nao miaka arobaini? Si wale waliokosa? Tena ni AKINA NANI aliowaapia ya kwamba hawataingia katika raha yake, ila wale walioasi? Basi twaona ya kuwa hawakuweza kuingia kwa sababu ya KUTOKUAMINI KWAO.” (Waebr.3:17:19).

Unaona, watu wa Mungu walichukua jukumu mbele ya Mungu juu ya dhambi zao – hawakuweza kumlaumu Shetani! Shetani yupo. Lakini Mungu ametupa neno Lake na anatazamia TUISHI KWA NENO LAKE na TUZIPINGE HILA ZA SHETANI! Alitazamia Adamu na Eva wafanye hivyo bustanini; alitazamia Waisraeli wafanye hivyo jangwani; na Bwana hutazamia tufanye hivyo maishani mwetu.

Ni wazi Mungu alimruhusu nyoka aingie bustanini awajaribu Adamu na Eva. KWA KUSUDI Mungu aliwaacha watu Wake jangwani waone njaa! Kwa nini? Tusikilize Mungu Mwenyewe alilosema juu ya hayo,

“Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili AKUTWEZE, KUKUJARIBU kuyajua YALIYO MOYONI MWAKO, kwamba UTASHIKA AMRI ZAKE, AU SIVYO. Akakutweza, AKAKUACHA UONE NJAA, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; APATE KUKUJULISHA YA KUWA MWANADAMU HAISHI KWA MKATE TU, BALI HUISHI KWA KILA LITOKALO KATIKA KINYWA CHA BWANA.” (Kumbu.8:3,4).

Unaona? Ni kusudi la Mungu tujaribiwe ili TUKUE katika imani, haki na utakatifu. Mambo mengi yanatokea, siyo kutuadhibu au kutuangamiza, ila kutupeleka TUKUE katika imani na katika Kristo Yesu. Ndio maana maandiko yanasema, “Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno.” (Yakobo 1:2-4). Na tena, “mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini.” (Warumi 5:3,4).

Je, baada ya kubatizwa kwake, Yesu aliongozwa na ROHO MTAKATIFU nyikani KWA SABABU GANI? Biblia inatusema kwa wazi!  “Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ILI AJARIBIWE NA IBILISI.” (Mathayo.4:1). Na Luka anasema, “Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu…akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani, akijaribiwa na Ibilisi. Na siku hizo alikuwa hali kitu; hata zilipotimia, aliona njaa.” (Luka 4:1,2). Kwa siku arobaini Yesu hakula kitu (siku mmoja kwa kila mwaka Waisraeli walizunguka jangwani, yaani, 40).

Na tutambue ukweli huu, Yesu aliongozwa na Roho Mtakatifu ili ajaribiwena Ibilisi. Pia, na tutambue ukweli ufuatao: Yesu alikuwa hali AMEJAA ROHO alipoongozwa nyikani ili ajaribiwa na Ibilisi, lakini baada ya kujaribiwa na Shetani, Biblia inasema kwamba, “Yesu akarudi KWA NGUVU ZA ROHO, akenda Galilaya…”  (Luka 1:1-14). Aliingia nyikani AMEJAA Roho, alitoka kwa NGUVU za Roho! Unaona? Unatambua kitu?

KUSUDI la majaribu ni TUKUE katika imani, haki, utakatifu  – tuchague yaliyo mema na tukatae yaliyo mabaya; tuchague Yesu na tujikane wenyewe; tumpendeze Mungu badala ya kutupendeza wenyewe, tuishi kwa neno la Mungu na kuupinga uongo wa Shetani, siku hadi siku katika mambo yote. Kwa njia hiyo tunakua katika Kristo Yesu na tunaanza kuishi kwa nguvu za Roho!  Wengi hawaishi kwa nguvu za Roho, kwa msingi siyo kwa sababu ya Ibilisi, ambaye ‘kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze,’ bali kwa sababu hawaishi kwa neno la Mungu, hawazipingi hila za Shetani zisiingie mioyo yao! Wengi wetu wanapenda kumshambulia Shetani na kupaza sauti katika maombi yetu, lakini kwa wengi wetu ni wakati tuache kumlaumu Shetani kana kwamba yeye ni sababu ya kosa letu, au yeye ni kisingizio cha dhambi zetu! Ni wakati tutambue tabia ya kweli ya vita vyo kiroho yetu na kupinga na kusimama dhidi ya hila za Shetani! Naomba usinielewe vibaya – hapo ninaongelea mawazo yanayotaka kuingia akili na mioyo yetu. Ninaongelea majaribu yale ya kila siku yanayokupata na ‘yaliyo kawaida ya wanadamu.’ Tunasoma juu ya majaribu hayo katika 1 Wakorintho 10. Na mwanzo wa sura hiyo unashughulika na nini? Inashughulika na kutokuamini na kutokutii kwa Waisraeli jangwani!

Yesu alimshinda Shetani kwa njia gani? Je, alipaza sauti kumfukuza Shetani? Je, alimkemea kwa hasira ili kumfunga na kumtupa shimoni? Hapana! Bwana Yesu alisema tu, “Imeandkiwa…” na tena ‘Imeandikwa…” na tena, “Imeandikwa…” Yaani, Yesu aliishi kwa neno la Mungu! Yesu alinukuu mstari ule tuliousoma hapo juu akimwambia Shetani, “Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.”

Ni muhimu sana kuelewa yale yaliyoyaandikwa kwa wazi wakati Yesu alipokuwepo nyikani. Shetani alipokuja kumjaribu Yesu, lakini Bwana Yesu hakumshambulia Shetani kwa maneno! Yesu hakupaza sauti yake au kupiga kelele ili kumfukuza Shetani atoke nyikani! Ni wazi Bwana Yesu hakujaribu ‘kuifunga’ nguvu za Shetani. Hapana! Aliishi, alisimama kwa neno la Mungu tu! Shetani anakuja kuchochea kutokuamini juu ya upendo wa Mungu na uwezo wa Mungu mioyoni mwetu kwa maneno kama haya: ‘Je, Mungu wako yupo wapi? Je, anakupenda kwa kweli? Kwa nini Mungu alikuacha katika mahitaji yako? Angalia mazingira yako na niambie uwezo wa Mungu upo wapi? Kama wewe ni Mwana wa Mungu, fanya hivi au hivi!’

Ibilisi alikuja kwake Yesu na alitaka kuchochea mawazo kama hayo; Ibilisi alikuja kwao Waisraeli jangwani kuchochea mawazo hayo; nyoka alikuja kwao Adamu na Eva kuchochea mawazo hayo; na ibilisi anataka kuja kwetu na mawazo hayo ili kuchochea kutokuamini ili tusiamini upendo na uwezo wa Mungu. Hivyo ni vita vya kiroho kweli kweli ya kila siku! Tufanye nini katika vita vya kiroho? Na tufanye vile vile Yesu alivyofanya! Tusimame kwa neno la Mungu!

Watu wengi wanafikiri ‘vita vya kiroho’ ni jambo la kupaza sauti katika maombi yao na kumkemea Shetani na ‘kuifunga’ nguvu yake. Hatuna hata mstari mmoja kwenye Biblia unaotuonyesha maombi kama haya. Wengi wanakosa katika kusoma Waefeso 6:12 kwani wanafikiri ni lazima KUOMBA dhidi ya ‘falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.’ Lakini Paulo hafundishi hivyo kama tutaona hapo chini.

Kosa la Adamu na Eva siyo kwamba hawakuomba dhidi ya ‘majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho’! Kosa la Waisraeli siyo hawakuomba dhidi ya ‘majeshi ya pepo wabaya’. Walikosa na walifanya dhambi kwa sababu WALIRUHUSU MAWAZO MAOVU KUINGIA MIOYONI MWAO; waliruhusu uongo wa Shetani kuharibu ukweli na sura ya Mungu ndani ya akili na mioyo yao – na walianguka katika kutokuamini na kutokumtii Mungu. Hawakupinga mawazo maovu ya Shetani yasiinge mioyoni mwao – hawakuishi kwa neno la Mungu. Ni rahisi kupaza sauti dhidi ya Shetani katika maombi yetu. Ni kitu kingine kuishi siku hadi siku kwa neno la Mungu tunapojaribiwa na majaribu ‘yaliyo kawaida ya wanadamu’!

Yesu alimpinga Ibilisi, alimshinda Shetani, KWA KUSHIKA NA KUISHI KWA NENO LA MUNGU! – hakuathiriwa na mawazo ya adui. Hiyo ni njia yetu, yaani, tusimame dhidi ya hila za Shetani kwa kusimama kwa neno la Mungu (Waefeso 6:11), tuzitunze akili na mioyo zetu ili tusiadhiriwe na mawazo ya Ibilisi. Hiyo ndiyo ni ‘vita vya kiroho’ kweli kweli. Tusipozipinga hila hizo za Shetani kwa namna hiyo, bila shaka itaharibu maisha yetu ya kiroho. Ni kwa sababu ya hiyo watu wengi hawaishi kwa nguvu ya Roho Mtakatifu – wanahangaika, hawana amani na hawana furaha – fikra zao zimeadhiriwa na uongo wa Shetani!  

Baada ya kuzipinga hila za Ibilisi nyikani kwa neno la Mungu, maandiko yanasema,

“Kisha Ibilisi AKAMWACHA.” (Mathayo 4:11). Na maandiko yanasemaje juu yetu? Yanasema,

“Basi mtiini Mungu. MPINGENI Shetani, naye ATAWAKIMBIA.” (Yakobo 4:7).

Tunakutana na ukweli huo tena na tena katika neno la Mungu:

“Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi MPINGENI huyo, mkiwa THABITI KATIKA IMANI.” (1 Petro 5:8,9). Tunazishinda hila za Shetani kwa imani yetu katika neno la Mungu.

Kwa msingi, vita hivyo vinahusu yanayotokea mioyoni na akilini mwetu, katika fikra zetu! Kwa hiyo Paulo anatufundisha,

“Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili – maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata KUANGUSHA NGOME – tukiangusha MAWAZO na kila kitu kilichoinuka, KIJIINUACHO JUU YA MAARIFA / UKWELI YA MUNGU; na TUKITEKA NYARA KILA FIKIRA IPATE KUMTII Kristo.” (2 Wakor.10:3-5).

Unaona? Ni vile vile kama nilivyosema kwenye mwanzo wa somo hili. Tangu mwanzo Shetani (Ibilisi, nyoka) anataka kujenga ngome za mawazo ya uongo katika akili zetu. Na tunajua kwamba ‘ngome’ ni kitu chenye nguvu sana! Shetani anajaribu kujenga ngome ya mawazo ya kutokuamini na kiburi pamoja na hisia za kutamani YANAYOJIINUA juu ya ukweli ya Mungu na tabia Yake na yanayotaka kutawala juu ya fikra zetu ili tusiamini Mungu, ili tusimjue Mungu, ILI TUSITAMBUE JINSI MUNGU ALIVYO KWELI KWELI! Hiyo ni lengo la Shetani. Tena ni Shetani anayeshambulia AKILI NA MIOYO zetu na MAWAZO ya kumpinga Mungu. Ndio maana tunatakiwa kuchukua silaha za vita vyetu zinazo uwezo KATIKA MUNGU kuangusha mawazo hayo yote, yaani, kuangusha ngome ile, na ‘kukiteka nyara kila fikra ipate kumtii Kristo!’ Ni vita vinavyotokea katika mioyo na akili zetu. Je, ni nini itakayotawala katika mioyo yetu, katika fikra zetu – hila ya Shetani au neno la Mungu?

Ni Waefeso sura ya 6 inayotutoa maelezo na mafundisho zaidi juu ya vita hivyo.

“Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu Zake. VAENI SILAHA ZOTE za Mungu ili kwamba mweze KUZIPINGA HILA za Shetani.” (Waefeso 6:10,11).

Paulo anatuhimiza hapo kwa ukweli ule ule aliotaja kwenye 2 Wakorintho sura ya kumi. Katika vita hivyo tunatakiwa kutumia silaha zote za Mungu kuzipinga hila za Shetani na kuangusha MAWAZO yajiinuayo juu ya ukweli wa Mungu na yanayotuzuia tusimjue Mungu jinsi alivyo! Kwa sababu mashambulio yanatokana na Shetani, lazima silaha zetu ni za Mungu, za kiroho, si za mwili. Paulo anaendelea kueleza ukweli huo,

“Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.” (Waefeso 6:12).

Kwa hiyo, ndugu zangu, tufanyaje? TUOMBE dhidi ya ‘falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho’ sawasawa na mafundisho ya watu wengi? HAPANA! Hata kidogo! Paulo hasemi hivyo, hafundishi hivyo! Paulo anafafanua kwamba vita vyetu ni vya kiroho si vya kimwili na KWA HIYO ni lazima TUVAE silaha zote za MUNGU! Sikilize Paulo asemalo kwenye mstari ufuatao,

“KWA SABABU HIYO twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.” (Waefeso 6:13).

Je, silaha zetu ni ‘maombi dhidi ya ‘majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho’? Hapana. Hasemi hivyo, hafundishi hivyo. Silaha zetu ni nini basi? Paulo anafafanua kwa wazi,

“Basi simameni, hali mmejifunga KWELI viunoni,

na kuvaa DIRII YA HAKI kifuani,

na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa INJILI YA AMANI;

ZAIDI YA YOTE MKIITWAA NGAO YA IMANI, AMBAYO KWA HIYO MTAWEZA KUIZIMA MISHALE YOTE YENYE MOTO YA YULE MWOVU.

Tena ipokeeni CHAPEO YA WOKOVU, na upanga wa Roho AMBAO NI NENO LA MUNGU.” (Waefeso 6:13).

Mafundisho ya Paulo juu ya ‘vita vya kiroho’ inahusu mwendo wetu wa kiroho na nidhamu yetu mbele ya Mungu, yaani, jinsi ya kusimama katika haki, utakatifu na imani katika maisha yetu ya kila siku tunapokutana na mashambulio yanayotokana na Shetani! Hataji maombi juu ya ‘majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.’ Silaha hizo za Mungu zinatukinga na mashambulio ya Shetani; zinatunza akili zetu (chapeo ya wokovu) na mioyo yetu (dirii ya haki). Naomba tusome yafuatayo kwa makini sana kwani yanahusu somo hili kwa ndani sana: Paulo anaposema ‘zaidi ya yote’ anatushauri nini? Anatuhimiza tuitwae NGAO YA IMANI! Ukweli huu unahusu somo hili moja kwa moja; unahusu vita vya kiroho yetu moja kwa moja! Ngao ya imani ni silaha yetu ya muhimu na yenye nguvu! Kama Yohana anavyosema,

“Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu.” (1 Yoh.5:4).

Lakini tunajua imani (chanzo chake ni kusikia; na kusikia) huja kwa neno la Mungu. Kwa hiyo Paulo anatuambia tuutwae upanga wa Roho ambao ni NENO LA MUNGU!

Sasa tupo hapo mwanzo tena! Mungu alitazamia Adamu na Eva waishi kwa neno Lake ambalo alikuwa amewaambia – alitazamia kwa kuamini neno Lake wazipinge hila za Shetani bustani na kusimama dhidi ya uongo wake. Mungu alitazamia watu wake Waisraeli washike na kuishi kwa neno Lake (‘upanga wa Roho’) jangwani na kuizima mishale yote ya yule mwovu kwa imani (‘ngao ya imani’) na kutokuruhusu uongo wa Shetani kuiathiri mioyo yao! Bwana Yesu alitumia neno la Mungu tu kumpinga Shetani nyikani.

Vita vya kiroho kwa msingi vinahusu kuyapinga au kuyaangusha mawazo ambayo Shetani anataka kuchochea moyoni mwetu yajiinuayo juu ya tabia ya Mungu na yanayotupeleka kutokumwamini Mungu na wokovu Wake! Mawazo yale yanakuja kama mishale kukata tamaa kabisa na kutupeleka kujihurumia, kunung’unika, kukasirika na wengine na kuchockea kiburi moyoni mwetu kwa upande moja, na kwa upande mwingine kukufanya ujisikie Mungu ni kinyume chako, amekuacha na anakuadhibu. Kwa msingi mawazo hayo yanaathiri mioyo yetu ili tusitambue Mungu wala matendo Yake katika maisha yetu, na tusimjue Mungu jinsi alivyo. Kwa hiyo ni muhimu sana tuvae silaha zote za Mungu! Na silaha hizo zinazingatia, ‘ngao ya imani’ na ‘upanga wa Roho’. Pia zinazingatia ‘chapeo ya wokovu’. Chapeo kinalinda nini? Kinalinda kichwa chako! Na kichwa ni mahali ambapo mawazo yetu tunatokea!

Baada ya kuvaa silaha zetu zote, je, Paulo sasa anatuelekezea kuomba dhidi ya ‘majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho’? Hapana! Tunaposimama katika imani tukivaa silaha zote anatuelekezea tuombe kwa namna ya ifuatayo,

“kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika KUWAOMBEA WATAKATIFU WOTE; pia na KWA AJILI YANGU mimi, nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili NIIHUBIRI kwa ujasiri ile siri ya INJILI.” (Waefeso 6:18,19).

Hakuna mahali mmoja katika Biblia ambapo tunasoma kwamba hata muumini mmoja katika maombi yake anaomba dhidi ya Shetani, falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, na juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Hata Danieli hakuomba juu ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho – yeye aliomba kwa ajili ya kazi ya Mungu na watu wa Mungu tu! Na kwenye mistari hiyo tunaona vile vile, yaani, Paulo anatuelekeza tusimame imara katika Bwana ili tuweze kuomba kwa ajili ya WATAKATIFU wote – yaani, kwa waumini wote katika Kristo – na kwa ajili ya kazi ya Mungu na Injili!

Kwa nini nilinukulu Kutoka 20:2-4 hapo juu? Kwa sababu Mungu amejidhihirisha kadiri ya ifuatayo:

“BWANA, BWANA, Mungu MWENYE HURUMA na NEEMA, ASIYE MWEPESI WA HASIRA, MWINGI wa UPENDO na UAMINIFU…” (Kutoka 34:6).

Hiyo ndiyo tabia au ‘sura’ ya Mungu, lakini Shetani anataka kuchora ‘sanamu’ mawazoni au ‘kichwani’ mwako; anajaribu kubadilisha ‘sura’ ya Mungu, kumfanya Mungu aonekane kama mtu mkali machoni pako, kama Mungu ndiye mbali nawe na dhidi yako! Hiyo ni mbinu za Ibilisi kila siku!

Lakini hiyo siyo jambo la kumlaumu Shetani, kumtumia kama kisingizio cha dhambi zako au kutokuamini kwako! Mungu ametupa silaha ili tuzipinge hila hizi za Shetani!

Kama nilivyosema, kwanza Ibilisi anakuja kutuvuta na kutushawishi tufanye dhambi. Lakini mara tunapokosa, anabadilisha mbinu yake na anaanza kwa nguvu kutulaumu, “Onaona, hufai! Hufai kabisa! Umekosa tena! Hupendi Mungu kwa kweli. Mungu hakupendi! Ulikosa mara nyingi. Huwezi kushinda dhambi hiyo! Huna uwezo kushinda! Wewe ni mwenye udhaifu! Utashindwa tu! Wewe si kitu! Wengine wanashinda na wanabarikiwa lakini siyo wewe kwa sababu Mungu siyo kwa upande wako!” Kwa maneno na mawazo haya Shetani anataka kukata tamaa kabisa ili tusiamini Mungu, ili tusiende kwake Yesu mara moja tupate neema na msamaha na kuwekwa huru mbali na dhambi!

Mawazo yanayotoka kwake Shetani yanatusukumu MBALI na uwepo ya Bwana, tujisikie peke yetu kabisa. Huduma ya Roho Mtakatifu ni tofauti sana na kazi ya Ibilisi! Kama tukikosa au tukishindwa, Roho ya Mungu anaongea kwa sauti ya pole sana kwa dhamira yetu! Biblia inasema Roho ya Mungu ni kama HUA. Siyo kama mtu mkubwa mkali ambaye anakuja kutupiga na fimbo! Bwana apewe sifa kwa neema Yake! Roho hatupondi, hatusukumu au kutufukuza mbali na Mungu! Roho ya Mungu anatujulisha kosa letu lakini pamoja na hiyo anatuonyesha Yesu ndiye Mwokozi na Msaada wetu, yaani, kwa huduma Yake, Roho ya Mungu anatuvuta tuje kwa Bwana, na tuje mara moja! Na Roho ya Mungu anaongea nasi kwa neno la Mungu! “Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza mimi.” (Yoh.16:13,14).

Unaona, huduma na mawazo ya Shetani yanakusukuma na kufukuza mbali na Bwana, na kinyume chake, huduma na sauti ya Roho ya Mungu inakuvuta kwa Bwana upate msamaha, rehema na neema ya Mungu mara moja na kutuweka huru mbali na dhambi! Bwana asifiwe kwa neema kama hiyo kuu! Na hiyo siyo kwamba tufanye dhambi tena ila tupate faraja na neema ili tumwamini Mungu tushinde kwa neema ya Bwana na kwa nguvu za Roho Yake! Usikate tamaa! Kila mara nenda kwa Bwana; mwamini Yeye kwa moyo wako wote; soma neno lake; chukua muda uwe pamoja na Baba na Mwana; mpende Bwana kwa moyo wako wote na ujitoe kwake kabisa kila siku.

“Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.” (Warumi 8:31-37).

© David Stamen 2017      somabiblia.com

KUDOWNLOAD SOMO HILI, BONYEZA LINK IFUATAYO TU:   HILA NA MBINU ZA SHETANI NA JINSI YA KUZISHINDA. VITA VYA KIROHO KWELI KWELI.

 

Comments are closed.

 
%d bloggers like this: