Mtu ajulikanaye mbinguni.
“Sala zako na sadaka zako kwa wahitaji zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.” (Mat.10:2-4)
Maneno ya ajabu! Ungependa kuwa na ushuhuda kama huo mbele ya Mungu? Malaika alisema maneno haya kwake Kornelio ambaye alikuwa jemadari wa kile kilichojulikana kama kikosi cha Kiitalia. Kornelio hakuwa mhubiri wala mtume wala mchungaji wala nabii wala mwinjilisti! Alikuwa mtu wa kawaida tu. Alikuwa na kazi na familia. Kama jemadari hakika alikuwa na majukumu na shughuli nyingi! Lakini alimwomba Mungu daima! Alichukua muda kuwa peke yake kuomba mbele ya Mungu. Mambo ya kila siku hayakumzuia kwenda mbele ya Mungu kuomba!
Kornelio hakujulikana ulimwenguni lakini alijulikana mbinguni! Ni bora kabisa kujulikana mbinguni kuliko duniani! Je, tunapendelea tujulikane mbele ya watu, duniani, au tujulikane mbinguni, mbele ya Mungu? Usijibu kwa haraka swali hili! Usijibu ovyoovyo! Bali, tunavyoishi ni jibu!
Je, ninajitenga mwenyewe na wengine kwa ajili ya hamu yangu niwe na Mungu tu? Je, kwa kusudi na kwa mkazo tunachukua muda kuwa peke yetu pamoja na Mungu? Je, na tunafanya hivyo siyo kana kwamba ni jambo la kulazimishwa, lakini kwa sababu tumampenda Bwana na astahili tuutafute uso Wake na tujitoe maisha yetu! Je, kwa makusudi na kwa mkazo tunachukua muda kumwomba Mungu kupitia Yesu Kristo kwa ajili ya watu wake na kazi yake? Na je, tunasema sala kana kwamba ingekuwa orodha ya mahitji tu? Au tunao uhusiano na Mungu wa kina, na maombi na maneno yetu mbele ya Mungu yanatokana na uhusiano huo huo? Je, tunachukua muda kujitenga na mambo yote ya ulimwengu huo ili kumwabudu Mungu, kumpenda tu, kumsifu tu, bila kutafuta kitu kingine cho chote kwa ajili yetu? Je, unachoshwa kuwa na Bwana hata nusu saa? Kama tunakwenda mbele ya Bwana kuomba kwa ajili ya mahitaji tu, basi tutakuwa hatuelewi vizuri tabia ya wokovu wetu katika Kristo Yesu. Watu wengi sana hupenda kuimba kanisani na kuongoza sifa na ibada. Siyo nidyo, jamani? Sasa je, unamsifu Bwana na kumsujudu peke yako mahali pa siri ya maisha yako pia? Kama hapana, kwa nini? ‘Mahali pa siri’ ni kwa mfano chumba chako, au porini, au bustani. Haidhuru. Muhimu ni mahali ambapo upo peke yako mbele ya Mwokozi wako tu – mbele ya macho ya Mungu na siyo ya watu!
Kwa msingi thamani ya maisha yangu hayatokani na jinsi nilivyo au jinsi naishavyo mbele ya watu! Bali yanatokana na jinsi nilivyo na jinsi naishavyo mbele ya Mungu, mahali pa siri ya maisha yangu ambapo Mungu tu ananiona! “Sala zako… zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.” Kama ukipenda kuwa mtu wa Mungu kweli kweli, lazima uwe na ‘mahali pa siri’ katika maisha yako ya kila siku – pale ambapo Mungu tu anakuona, pale ambapo unamtumikia Mungu tu, peke yako, ambapo hakuna mtu ye yote mwingine akuonaye au ajuaye unalofanya kwa siri! (Mtt.6:4-7; 16-18).
Kwa upande moja, tufanyalo kwa siri ni muhumiu kuliko tufanyalo mbele ya watu! Tunafanyeje kwa siri katika maisha yetu? Je, tunamngojea Mungu, tunautafuta Uso Wake, tumsifu, tumpende, tumsujudu na kumwomba kwa ajili ya watu wake na kazi yake? Je, tunatafuta ile sifa itokayo kwa Mungu na siyo kwa watu? Je, tunajitoa maisha yetu kwake mahali pa siri ili tuwe bila hasira, uchungu, wivu, chuki, malalamiko na manung’nuniko na badaka yake tuwe harufu nzuri ya manukato ya Kristo mbele ya Mungu? (2 Wakor.2:15).
“Kila mmoja wao alikuwa na kinubi, nao walikuwa wameshika mabakuli ya dhahabu yaliyojaa uvumba, ambayo ni maombi ya watakatifu.” (Ufunuo 5:8). Biblia inatufundisha kwamba maombi yetu ni kama uvumba mbele Kiti cha Enzi! Huo ndio ukweli wa maana sana! Hebu tufikiri ukweli huo ili uchochee mioyo yetu tuombe! Kumbuka, malaika alisema, “Sala zako na sadaka zako kwa wahitaji zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.”
Unafanya nini kwa siri? Unaangalia nini kwa siri? Unafanya mambo yale ambayo yakusababishe ukue katika Kristo, katika utakatifu, katika imani na katika maisha ya maombi – au mambo yale yanayoharibu maisha yako ya kiroho na hata ya mwili? Maisha yetu ya siri, yaani faraghani, lazima yawe matakatifu.
Wahubiri na wachungaji wengine hupaza sauti sana wanapohubiri wakifikiri hiyo inawakilisha nguvu ya Bwana! Hapana. Wengi kwa sababu ya upungufu wa nguvu ya kiroho katika huduma yao wanapiga kelele wanapohubiri! Nguvu ya huduma yetu inatokana na mahali pa siri (mbele ya Mungu) katika maisha yetu! Ni kweli, huduma inategemea na mwito pia, lakini hata hivyo ni lazima kujitenga kwa ajili ya mwito huo kama Petro alivyosema, “sisi tutatumia muda wetu mrefu kuomba na kulihudumia lile neno.’’ (Mat.6:4).
Na hata mtume Paulo hakupiga mbio kufanya kazi ya Mungu kwa maono yake yenyewe! Alitumikia Bwana kwanza na kuwatumikia watu wa Mungu kanisani kabla ya kwenda kufanya kazi ya mtume! Matendo 13:1,2 inatufundisha jambo la maana sana:
“Katika kanisa huko Antiokia ya Shamu walikuwako manabii na walimu, yaani: Barnaba …na Sauli. Walipokuwa wakimwabudu Bwana na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, “Nitengeeni Sauli na Barnaba kwa kazi ile maalumu niliyowaitia.”
Unaona, Paulo hakujitukuza wala hakutazamia watu wamtambue au kumpokea kama mtume muhimu! Alikataa kufanya mapenzi yake yenyewe, na alikataa kufanya kazi ya Mungu kutokana na hamu yake, akili yake au uwezo wake wenyewe. Alibaki kwa unyenyekevu katika kanisa moja kuwahudumia watu wa Mungu, lakini msingi wa maisha yake ulikuwa kuchukua muda kumwabadu Bwana na kufunga mbele Yake mpaka Mungu Mwenyewe alimwita kufanya kazi ya mtume! Hamna watu wa Mungu wengi kama Paulo! Wengine wamalizapo Shule ye Biblia wanafikiri wametayarishwa kufanya huduma ya mchungaji. Hilo ni wazo lisilo na maana! Shule ya Biblia ya kweli ni MAISHA. Ni lazima kujifunza njia za Bwana katika maisha ya kila siku! Wachungaji na wahuburi kadhaa (au hata wengi) hawana kitu cha kiroho kuwaambia washirika kwa sababu wanakosa kuchukua muda kuwa peke yao mbele ya Bwana – “sisi tutatumia muda wetu mrefu kuomba na kulihudumia lile neno.” Kanisa ambalo linao mchungaji wa namna hiyo, hubarikiwa! Watu kama hawa wanawalisha watu wa Mungu na maneno ambayo wanayoyapata kutoka kwake Bwana wakati wanaposali mbele Yake na kuutafuta uso Wake! Wanajitoa kabisa kwake Bwana na wanamngojea. Wengine wanahubiri mawazo ya kibinadamu tu au mambo mapya yanayotoka Ulaya au Amerika! Wanachukua muda kujenga huduma yao badala ya kumtafuta kwenye mahali pa siri.
Kwa sababu mtume Paulo aliishi maisha yake mbele ya Bwana na siyo mbele ya watu, kumbe, alijulikana mbinguni na hata katika ulimwenguni wa kiroho. Tunasoma, “Basi baadhi ya Wayahudi wenye kutangatanga huku na huko wakitoa pepo wachafu wakajaribu kutumia jina la Yesu juu ya wale wenye pepo, walikuwa wakisema, ‘Kwa jina la Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo, na kuamuru utoke.’ Palikuwa na wana saba wa mtu mmoja Myahudi jina lake Skewa, aliyekuwa kiongozi wa makuhani, ambao walikuwa wanafanya hivyo. Lakini pepo mchafu akawajibu, ‘Yesu namjua na Paulo pia namjua, lakini ninyi ni nani? Kisha yule mtu aliyekuwa na pepo mchafu akawarukia, akawashambulia vikali, akawashinda nguvu wote …”. (Mat.19:13-16). Tunaona watu wanatumia jina la Bwana bila kumjua Yesu. Paulo alijulikana na Mungu, alijulikana na pepo, na alijulikana na watu! Kama tunafanya kazi ya Mungu ni lazima tujitenge na mambo ya kila siku na kuchukue muda kuwa mbele ya Bwana tujitoeeni kwake katika maombi na kumwabudu, na siyo kujaribu kutimiza ‘maono’ au ‘ndoto’ zetu wenyewe!
“Kornelio Yeye alikuwa mcha Mungu pamoja na wote wa nyumbani mwake, aliwapa watu sadaka nyingi na kumwomba Mungu daima. Siku moja alasiri, yapata saa tisa, aliona maono wazi wazi malaika wa Mungu akimjia na kumwambia, “Kornelio!” Kornelio akamkazia macho kwa hofu akasema, “Kuna nini, Bwana?”
“Sala zako na sadaka zako kwa wahitaji zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.” (Mat.10:2-4)
© David Stamen 2015 somabiblia.com
KUDOWNLOAD SOMO HILI, BONYEZA LINK IFUATAYO: Sala Zako
One response to “Mtu ajulikanaye mbinguni.”