RSS

Somo juu ya Maombi – Marco Bashiri

SOMO: MAISHA YA MAOMBI KWA MKRISTO (Part 1)

Wako wakristo ambao tunashindwa kuwa na maisha ya maombi kwa sababu zifuatazo.

(1) Kukosa muda wa kuomba kwa sababu ya majukumu ya muhimu ya hapa na pale.
(2) Mazingira ya mtu anapoishi.
(3) Mwingine hajui faida za maombi wala umuhimu wake.
(4) Mwingine anasema huwa anaishiwa maneno kwa haraka anapokuwa kwenye maombi.
(5) Mwingine hapendi maombi tu!
(6) Shetani.
(7) Mwili.

Katika maombi kuna vikwazo vingi, kwa sababu maombi yana nguvu!

(A) MAOMBI YANAONGEZA UHUSIANO WA MTU NA MUNGU!

Maombi ni mawasiliano baina ya mwanadamu na Mungu au ni njia ambayo tunaweza kuwasiliana na Mungu. Tunafanya mawasiliano na Mungu kwa njia ya maombi, na kama tunavyojua kwamba! Mawasiliano yanaongeza uhusiano wa mtu na mtu, hata wewe ni shahidi katika hili! Unaweza ukawa na ndugu wengi sana au marafiki wengi sana n.k. Lakini yule ambaye atawasiliana na wewe mara kwa mara huyo ndiye anayeukuza ukaribu kupita wengine. Na pia uhusiano wa mtu unaanzishwa kwa mawasiliano na vilevile unaweza ukafa au kupungua kwa kukosa mawasiliano ya mara kwa mara na kuelekezwa kule kwenye mawasiliano ya mara kwa mara! Mawasiliano yamewafanya watu wengi kuwa karibu, kupitia mitandao yetu. Mtu alipoanza mawasilano na wewe kwa njia ya kukutumia ujumbe wa maandishi au wa picha ulipojibu! Mawasilano yakakua mwisho wake ukaribu ukaongezeka kati yako na huyo….

Tunapokuwa tunaomba mara kwa mara uhusiano wetu na Mungu unakuwa kwa kasi sana kuzidi yule asiyeomba, au yule anayeomba mara moja moja au yule anayeomba kwa viwango vya juu zaidi! Na kama tujuavyo, kadiri uhusiano wa mtu na mtu unavyokuwa na kuongekezeka ndivyo wanavyoweza kushirikishana mambo mengi saaaana!

Ndivyo inavyokuwa kwa Mungu kwetu! Kwa sababu mahusiano yetu yanakuwa na kuongezeka! Mungu hataacha kutushirikisha mambo mengi yanayoendelea ili kuyaombea au kuzuia yasitokee au kuwashauri watu n.k. Mungu atatuonyesha hata hatari iliyopo mbele yetu, kwamba! Kuna ajali mbaya itatokea na kusababisha hiki na hiki na jinsi ya kuikwepa n.k. Yakiambatana na maelekezo yake jinsi ya kufanya ambayo yatakuwa na lengo la kujenga na si kubomoa! Utakuwa na furaha na amani wakati woote hata kwenye dhiki za namna gani! Sijui nitumie lugha gani nieleweke jamani: Ili uelewe hili na kulishika kwamba! MAOMBI YANAONGEZA UHUSIANO WA MTU NA MUNGU!

Tuanze maisha ya maombi kuanzia sasa ili uhusiano wetu na Mungu ukue, anzisha mahusiano yako na Mungu kwa kuwasiliana naye mara kwa mara kwa njia ya maombi. Hata kama zamani tulikuwa na bidii ya kuwasiliana na Mungu kwa njia ya maombi halafu tukayakata mawasilano hayo! Bado tunaweza kuyaanzisha upya na kuyakuza! Pia usiache kuwasiliana na Mungu mara kwa mara kwa njia ya maombi kwa sababu kwa kutofanya hivyo utauvunja au utaupunguza uhusianao wako na Mungu!

SOMO: MAISHA YA MAOMBI KWA MKRISTO (Part 2)

Kwa nini tunazuiwa kuomba? Pamoja na sababu nyingine zinaonekana kama ni za msingi! ANGALIA HII!

(B) MAOMBI YANAWEZA KUBADILI MAAMUZI YA MUNGU ALIYOYAPANGA KWA TAIFA AU KWA MTU N.K.

Hii tunaipata kwa Nabii Isaya! Tusome maandiko haya kwa makini saaana! ISAYA 38:1 “Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, ‘BWANA asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa,wala hutapona’.”
Ni ujumbe kutoka kwa nabii! Mungu mwenyewe hapo anasema kwamba “UTAKUFA”, hebu jaribu kufikiri! Ingekuwa wewe Mungu anakwambia hivyo ungefanyaje? Lakini mfalme huyu alijua hata kama Mungu amesema, bado ninaweza kubadili maamuzi yake kwa sasa kwa njia ya maombi! Alichokifanya mfalme ni hiki! ISAYA 38:2 “Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba BWANA..Hezekia akalia sana sana.” Hezekia alijua na aliamini kwamba maombi yanaweza kubadili maamuzi ya Mungu kabisa! Baada ya maombi hayo Angalia kilichotokea. ISAYA 38:4, “Ikawa, neno la BWANA likamjia Isaya, kusema, Enenda ukamwambie Hezekia, ‘Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama nitaziongeza siku zako…”. Hapo kuna vitu viwili Mungu aliviangalia wakati Hezekia anaomba,
(1) Kuomba kwa imani. “Ikawa, neno la BWANA likamjia Isaya, kusema, ‘Enenda ukamwambie Hezekia, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako.” (ISAYA 38:4).

(2) Machozi yaliyoambata na kuomba, japokuwa wako watu huwa wanasema walokole wanalialia, tunalia ili Mungu ayapokee maombi yetu, sisi hatulii kama hao waliliao mapenzi usiku na mchana!

Maombi hapa yaligeuza maamuzi ya Mungu, nafikiri sasa unaweza kuelewa kwa nini tunazuiwa kuomba. Ndugu kama unaomba; hata kama ni nani alitamka kitu gani kwako, au katika ukoo wako kwa kulaani laana zozote zile, unakuta familia nyingine hakuna maendeleo yoyote yale pamoja na bidii zote za kufanya kazi na kusoma! Hakuna kuoa wala kuolewa n.k. Maombi yana uwezo wa kubadilisha laana na kuwa baraka na kufumua fumua kila vitu vibaya vinavyohusika kutukandamiza na kutudidimiza katika maeneo fulani fulani. Hata kama bosi alisema nitakusimamisha kazi, maombi yanaweza kubadili maamuzi ya bosi! Kama maombi yaliweza kugeuza maamuzi ya Mungu sembuse bosi ? Sembuse Rais wa nchi?
Twende kwenye mfano wa pili uone maombi ambavyo yanakitu cha kipekee.

Hapa sasa tunaona Ibrahimu ambavyo alikuwa anawashawishi malaika waliotumwa na Mungu kwa ajili ya kuiangamiza Sodoma na Gomora. Mwanzo18:32. “Je! Utaharibu mwenye haki pamoja na mwovu? Huenda wakawapo wenye haki hamsini katika mji, utaharibu wala hutaacha mji.Hasha usifanye hivyo,…BWANA akasema, Nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini mjini, nitapaacha kwa ajili yao.”
Ibrahimu aliendelea kusema na wale malaika mpaka akafikia hesabu ya watu 10! Na ibrahimu akaishia hapo, kama Ibrahimu angeendelea kusihi bila shaka maangamizo yasingetokea. (Mwa 18:30-32). Zaidi sana walichokifanya malaika ni kumuondoa Lutu na mkewe na wanawe ambao inaonyesha hawakufika 10 kama wangekuwa 10 wasingetolewa ili mji uangamizwe kwa sababu Ibra alifanya maombi na yakajibiwa kwamba kwa idadi ya watu 10 tu na kama hao 10 wangekuwepo Sodoma na Gomora isingeangamizwa, wangeachwa na Mungu angetumia njia nyingine! Maana Alisema kama wamgekuwa 10 asingeuangamiza mji.                                                                                                                

Maombi ni ni kumshawishi Mungu kufanya yale ambayo wewe unataka ambayo yatakuwa ndani ya mpango wake. Kama maombi yanaweza kubadilisha maamuzi ya Mungu; sembuse kubadilisha maaumuzi ya mtu? Ndio maana sijatoka kuzungumzia mifano ya maamuzi ya wanadamu yalivyobadilishwa baada ya maombi, nimezungumzia upande wa Mungu ili uone maombi ambavyo yana nguvu! Kuna kitu gani umetamkiwa? Kuna kitu gani unakitaka? Muombe MUNGU kwa imani!

INAWEZEKANA! BARIKIWA ZAIDI NA ZAIDI NA ZAIDI!

SOMO: MAISHA YA MAOMBI KWA MKRISTO (Part 3)

(C) KUWAACHA WATU NA KWENDA KUOMBA!

Hili ni tendo la ajabu sana ambalo Yesu alilifanya! Lilikuwa ni fundisho kwetu! Hebu jaribu kufikiri; Kwa jinsi Yesu ambavyo ana kila kitu, LAKINI PAMOJA NA YESU NA KUWA NA KILA KITU, lakini alijua pasipo maombi yote aliyokuwa nayo HAIWEZEKANI! Yesu mwenyewe alikuwa anajua hapa bila maombi hamna kitu! Alifikia mahali anawaacha makutano halafu anakwenda kuomba. Luka 5:12-16. Hebu tusome mstari wa 16.

“Lakini yeye alikuwa akijiepua,akaenda mahali pasipokuwa na watu,akaomba.”

Hapo Yesu anawakimbia makutano na kuelekea zake kwenye maombi, japokuwa ni ngumu sana kwa baadhi ya watu kuwaacha watu na kwenda kwa kuomba katika mazingira kama haya ya Yesu, kwao ni utukufu. Ikiwa Yesu alifanya hivyo, sisi tunapaswa kufanya hivyo na kuzidi kulingana na maisha yetu na dunia ya leo, lakini leo mtu anasema hana muda wa kuomba, eti kazi zinambana, na kwa sababu nyingine zinazofanana na hizo, lakini bado mtu huyohuyo ambaye anasema hana muda wa kuomba huyo huyo unaweza kumuona katika makundi ya watu au marafiki akiongea muda mrefu, lakini hao hao wanaosema hawana muda wa kuomba ni watu hodari sana kwa kuchat, hana muda wa kuomba lakini ana muda wa kuchat na watu kwa njia ya whatsapp, muda wote anafanya kazi huku yuko whats app! Hana muda wa kuomba lakini ana muda wa kuongea na watu kwenye simu masaa na masaa, hana mua wa kuomba lakini anaangalia movie masaa na masaa; hana muda wa kuomba lakini ana muda wa kuangalia mpira …ninaweza kusema huyu hana muda wa kuongea na Mungu lakini ana muda wa kuongea na watu! Kwa sababu maombi ndiyo kuongea na Mungu.

Kuongea na watu si vibaya; si vibaya kuchat na watu kwa njia mbalimbali za mitandao, lakini ni mbaya kama tuna muda wa kufanya hivyo lakini hatuna muda wa kuomba! Ni mbaya sana! Sana ! Inatakiwa ifikie mahali tunaongea na watu lakini ukifika muda fulani tunajiepua na kwenda mahali kusikokuwa na watu au mahali ambapo tutaweza kuomba bila buguza! Hapa Yesu hakwenda kanisani! Maombi tunaomba popote pale kama mazingira hayaturuhusu kwenda kanisani, tukipata nafasi tu kidogo tu; tunaomba hata kimoyomoyo! Kuomba sio lazima iwe kanisani.

Bila maombi tutajikuta tunaishi maisha ya unafiki! Maisha ya uhitaji wa kupitiliza na kujikuta kwenye madeni wakati wote, ukiondoa maombi hata unahubiri kila siku lazima iko siku utaanguka tu! LAZIMA! Tuache mambo ya kukaa kaa na watu na kuongeaongea muda mwingi tunaumalizia kwa watu. Tena wakati mwingine mambo mengine hayana hata maana, tunaopoteza kuongea na watu ambao hata tukienda kulala hata hawajui yanayotusibu katika usingizi wetu. Hawana sifa ya kuongea na sisi kabla ya kuongea na Mungu wetu! Kama Yesu aliomba mwenye huduma kubwa kuliko huduma yako wewe ambaye unalewa na sifa za watu lakini kuomba hutaki! Sisi tutapona? Shetani alikuwa hana kitu kwa Yesu lakini bado Yesu alikuwa anaomba. Tusidanganywe na sifa zinazotoka vinywani mwa watu.
Tuweke ratiba kwamba! Kuanzia muda fulani ni muda wa maombi. Hapo hata simu ipigwe hakuna kupokea, tunakwenda mahali pasipokuwa na watu kifikra! Yesu alikwenda sehemu halisi! Lakini kama mazingira yetu hayaturuhusu kufanya hivyo, tunapaswa kwenda mbali na watu kifikra! Wakati wa kuomba ikiwezekana zima simu yako au weka silent kama simu yako ndio kila kitu! Nikiwa na maana kuna bible n.k.

Yesu naye tungesema hana muda, kwa sababu pale alikuwa kazini! Lakini alijua umuhimu wa maombi! Kama wewe huna muda usile chakula basi! Kinachokufanya ule nini wakati huna muda?

NB:MAOMBI NI KWA FAIDA YETU WENYEWE!

SOMO: MAISHA YA MAOMBIKWA MKRISTO (Part 4)

(D) MAOMBI YANATUPA NGUVU YA KUTOINGIA MAJARIBUNI!

Yesu aliwawaambia wanafunzi wake maneno haya kwa uzito sana baada ya kuona wanafunzi hawana maisha ya maombi! Walikuwa wanafikiri jukumu la kuomba ni la Yesu tu! Kama sisi tunavyofikiri sasa, kwamba jukumu la kuomba ni la watu fulani tu, na si la kwetu! Kila mahali ambapo Yesu alikuwa anaomba wanafunzi wake ambao leo tunawatambua kama mitume! Walikuwa hawana maisha ya maombi. Angalia hapa Luka 9:28-32,

“Baada ya maneno hayo yapata saa nane, akawatwaa Petro na Yohana na Yakobo, akapanda mlimani ili kuomba (Hilo ndio lilikuwa lengo lakini angalia matokeo yake).Ikawa katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka….”. (Hapa Yesu anaomba peke yake wale aliopanda nao walishamwacha walikuwa na usingizi). Petro na wale waliokuwa pamoja naye walikuwa wamelemewa na usingizi:lakini walipokwisha amka…”

Inaonyesha wazi walikuwa wamelala wakati Yesu anaomba! Walikuwa wanaona shida kuomba kama sisi tunavyoona shida! Lakini tatizo lilikuwa linajirudia tena na tena kwa wanafunzi mpaka ikabidi Yesu awaambie madhara ya kutokuwa na maisha ya maombi! Hapa lilikuwa tukio jingine sio lile la mlimani! Mathayo 26:40-41,

“Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, je! Hamkuweza kukesha nami hata saa moja?.Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni.”

Sio toeni sadaka ili msiingie majaribuni, sio hubirini sana ili msiingie majaribuni, hapa yanatajwa maombi pekee. Kinyume chake hatutaweza kukabiliana na majaribu, tutashindwa bila shaka. Maombi ndio yananifanya mimi na wewe kutoingia majaribuni, majaribu yamejaa kila kona katika dunia ya leo, lakini tutawezaje kuyashinda kama hatuna maisha ya maombi? HATUTAWEZA KAMWE! KAMWE! Yesu akishasema amesema! Mtu yeyote ambaye hana maisha ya maombi ana maisha ya kuingia majaribuni! Mtu ambaye kuomba anaona shida; mtu huyo haina haja ya kupeleleza maisha yake. Jibu lake linajulikana ni mtu wa kuingia majaribuni na matokeo yake anajikuta anaishi maisha ya unafiki! Anaonekana anahubiri na kufundisha, anaoneka anapost vitu vya kutia moyo, anaonekana anaombea watu, lakini maisha yake ni ya kujilaumu wakati wote hana uwezo wa kushinda majaribu. Ndugu yangu hata kama sisi tunajiita mtume nabii hata kama! Hata kama tunajulikana vipi kiuimbaji na kukubalika katika nyimbo za injili, sifa na kuabudu, kama hatuna maisha ya maombi majaribu yakija lazima tutaingia majaribuni! Hatutaweza kushinda hata siku moja! Leo tunaweza tukajipiga piga vifua kama Petro,na kusema, “Mimi nimuache Yesu”. Ukisalimiwa “Mambo”, unajibu “Mambo kwa Yesu”. Misimamo hiyo kama huna maisha ya maombi lazima siku moja utaingia majaribuni tu! Misimamo bila maombi! Hakuna matokeo ya ushindi.

Namkumbuka binti mmoja ambaye alikuwa ameokoka! Binti huyu tulikuwa tunaishi naye jirani! Binti alikuwa na misimamo ya hatari sana! Ilikuwa tukimsalimia “Mambo?”. Aanajibu “Mambo kwa Yesu.” Alikuwa hajibu kwa mizaha! Alikuwa hataki mchezo mchezo ukizingatia pia kwao pesa zipo na wakati huo yupo kidato cha tatu! Mimi wakati huo nilikuwa mbali na Ufalme wa Mungu! Misimamo ya binti huyu haikudumu kwa sababu hakuwa na maisha ya maombi! Akaangukia kwa muuza mitumba na uwokovu akauacha! Akakataa shule wakati huo tayari ameshaanguka tayari; wakati hilo halijaisha vizuri mimba ikaingia akamwacha Yesu! Misimamo bila maisha ya maombi ninakuambia waziwazi wewe binti ambaye unajulikana shuleni kwako unaposoma, chuoni kwako au kazini kwako, bila maisha ya maombi unaweza kujikuta unaanguka mahali usipoptarajia.

Yesu alimwambia Petro waziwazi katika Mathayo 26:34-35, “…Yesu akamwambia, ‘Amin, nakuambia wewe, usiku huu kabla ya kuwika jogoo, utanikana mara tatu. Petro akamwambia, ‘Ijaponipasa kufa nawe, sitakukana kamwe.’”

Petro anajigamba wakati hana maisha ya maombi; muda wa maombi yeye anasinzia, na ndivyo ilivyokuwa, alimkana Yesu kwa kiapo na alisema Mathayo 26:69-74, “Ndipo alipoanza kulaani na kuapa na kusema, simjui mtu huyu.” Unaona, anasema “Mtu huyu.”  Wakati Petro alikuwa ananyenyekea kwa BWANA! Alikuwa anamuita Yesu BWANA! Lakini hapa anasema “Mtu huyu “. Ndivyo ilivyowatokea wengine ambao walipuuza maombi, leo ukiwaona utashangaa! Unajiuliza huyu si alikuwa moto wa kuhubiri, kuomba, kutoa, kuimba n.k.! Peleleza maisha yake kabla, utakuja gundua alikuwa hana maisha ya maombi! Na ndivyo itakavyotokea kwetu kama hatutakuwa na maisha ya maombi, ninakuambia wazi kabisa utashindwa tu!

Ndugu yangu OMBA! OMBA! OMBA! Ndani ya maombi ndio kuna nguvu ya kutuwezesha kushinda ushawishi huu uliotanda kila kona katika dunia, kila siku inafunguliwa mitandao mipya ya kuturahisishia kufanya mambo mema na hapohapo ya kuturahishia kuingia majaribuni! Tutawezaje kushinda vishawishi kama hatuna maisha ya maombi? Tutajikuta tunaishi maisha ya unafiki na mwisho ya siku tutamwita Yesu “mtu ” badala ya “BWANA” kama ilivyotokea kwa Petro! Tusipoomba kuingia majaribuni sio jambo la kutafuta! Mtu yeyote ambaye hana maisha ya maombi, mtu huyo hawezi kujizuia katika majaribu, kama sivyo yesu tunamfanya yesu kuwa ni muongo, na kamwe yesu hawezi kuwa muongo!

NB: Maombi ni kwa faida yetu wenyewe, tukiacha kuomba kwa sababu zozote kumkana yesu kuko karibu! omba! omba! omba!

SOMO: MAISHA YA MAOMBI KWA MKRISTO (Part 5)

MAMBO YA KUZINGATIA TUNAPOKUWA TUNAMUOMBA MUNGU TUNAPOKUWA KATIKA MAOMBI.

(1) HATUPASWI KUWA NA MASHAKA YOYOTE!

Maandiko yanasema katika Yakobo 1:5-7,

“…Ila naombe kwa imani, pasipo shaka yoyote; maana mwenye mashaka ni kama wimbi la bahari la bahari lililochukuliwa na upepo,na kuleperushwa huku na huku. Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana.”

Hayo ndiyo maandiko! Hata kama tunaomba masaa 100 mfululizo, hata kama tunaomba kwa viwango vya vinavyoonekana vya juu sanaa kibinadamu, lazima maombi yetu yawe ndani ya kanuni, lazima tuombe pasipokuwa na mashaka tena mashaka yoyote! Hayo ndio maandiko hakuna njia ya mkato; kama tunamuomba Mungu lakini tuna mashaka moyoni au vinywani hilo ni tatizo linalopelekea kutopokea majibu yetu ya maombi! Kwa nini nasema mtu anaweza akawa na mashaka moyoni. Mtu mwingine anaweza akaonekana ana imani katika mazungumzo yake, hasa pale anapokutana na watu , lakini ndani ya moyo wake kumejaa mashaka, na mashaka hayo Mungu huyaona pale mtu anapokuwa peke yake katika fikra au pale mambo yanapokwenda kinyume na alivyotarajia kutokana na maombi yake! Akizungumza na watu ni kama amejaa imani! Lakini moyoni kumejaa mashaka makubwa! Mashaka ni ile hali ya wasiwasi ya kutokuamini. “Hivi kweli Mungu inawezekana kweli? Itakuwa kweli? Mungu ananisikia kweli?” n.k.

Hayo yote ni mashaka na kwa mashaka hayo kamwe hatutaweza kupokea majibu yetu ya maombi! KAMWE! Tukiruhusu mashaka hata kama ni kidogo tunaambiwa waziwazi, “Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kutoka kwa BWANA.” Yaani, hata ile kudhani, kutegemea, kufikiri, isiwepo. Mashaka ni adui mkubwa sana anayeshindana na majibu ya maombi yetu yasitufikie.
Wakati mwingine mashaka yanakuwepo baada ya kuomba kitu muda mrefu na kutoona majibu ya maombi! Wakati mwingine inatokana na kuona mambo yanakuwa mabaya zaidi kuliko mwanzo! Au uzito wa jambo pia linaweza kuchangia kukaribisha mashaka na hata shetani pia anahusika lakini anapitia maeneo hayo hayo!

Ili tuone majibu ya maombi yetu yakiwa dhahiri, hatupaswi kuruhusu mashaka yoyote hata kidogo! Tukishaomba tu! Mawazo yetu yanapaswa kufikiri sawasawa na majibu ya maombi yetu, kusema kwetu kuendana na majibu yetu ya maombi kwa imani, inaweza kuwa sio rahisi kuishi hivyo haiwezi kuwa rahisi hata kidogo! Na hakuna mbadala wake lazima mashaka yasiwepo ili tupokee majibu yetu ya maombi! Tunamuomba Mungu kwa sababu sisi hatuwezi, tumeshindwa ndio maana tunaomba! Kama mtu unawashwa mgongoni utamwomba Mungu “niwezeshe kujikuna?” La! Tutajikuna kwa sababu jambo hilo liko ndani ya uwezo wetu!

Tunapomuomba Mungu maana yake sisi hatuwezi, tumeshindwa! Rahisi kufikiri nguvu za Mungu hazipo; rahisi kufikiri ukimwomba Mungu basi majibu yanachukua muda mrefu! Hatupaswi kuyaruhusu mawazo hayo kufanya kazi ndani yetu kamwe! SIsi tunachotakiwa kuamini Mungu yupo na anajibu maombi na hakuna gumu la kumshinda! Mashaka yanapokuwa yanakuja kwa njia zozote zile, iwe kupitia watu kwa maneno yao; n.k. Hatupaswi kuyaruhusu kwa sababu, tukiruhusu mashaka maandiko yanasema tusitarajie kupokea kitu kutoka kwa BWANA!

Kuna wakati Yesu alikuwa anatembea juu ya bahari! Na Petro akaomba atembee au apewe uwezo na Yesu wa kutembea juu ya bahari! Yesu akayajibu maombi yake na akamwambia Petro atembee…Lakini Petro aliporuhusu mashaka baada ya kuuona upepo, akazama mbele ya Yesu! Yesu akamuokoa kwa kumshika mkono sio kwa kumuombea bali alimshika mkono na akamwambia! (Mathayo 14:26-31.31):

“Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, ‘Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka?’”

Unaona hapa! Petro anazama mbele ya Yesu kwa sababu aliruhusu mashaka, na sisi sio kama tukimuomba Mungu kitu fulani basi kinakuwa mtelemko! Inaweza ikatokea upepo mkali kwenye biashara zetu kwa viwango vya kuporomosha kabisa mitaji yetu! N.K. Hatutakiwi kuwa na mashaka katika hali yoyote! Tusimamie matokeo tusiangalie mazingira tuliyonayo kwa sasa, tukiwa na mashaka tutazama tu hata kama Yesu yupo ndani mwetu!

Wakati wote tunapomuomba Mungu, tuombe bila mashaka yoyote yale! Mungu yupo na nguvu zake zipo vilevile! Hata mimi nikikufanyia maombi na ukaanza kuona matokeo, yaani, unatembea juu ya bahari kama Petro! Lolote likitokea kama upepo likiwa na lengo la kubadilisha hilo, hupaswi kuwa na mashaka unapaswa kuendelea kuamini! La sivyo utazama kama Petro na kuupoteza muujiza wako! Kama Petro alizama mbele ya Yesu kwa sababu ya kuruhusu mashaka! Sembuse mwanadamu anayeitwa….. .
Yakobo 1:5-6,

“…Ila naombe kwa imani, pasipo shaka yoyote; maana mwenye mashaka ni kama wimbi la bahari la bahari lililochukuliwa na upepo, na kuleperushwa huku na huku. Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana.”

Tumwombe Mungu atuongezee imani atupilie mbali mashaka yaliyomo ndani mwetu na atupe kuyashinda kila yanapoinuka. Hata kama maombi yetu yatachukua muda mrefu bila kuona majibu yake, bado hatupaswi kuruhusu mashaka, tena mashaka yoyote yale.

SOMO: MAISHA YA MAOMBI KWA MKRISTO (Part 6)

MAMBO YA KUZINGATIA TUNAPOKUWA TUNAMUOMBA MUNGU, TUNAPOKUWA KATIKA MAOMBI.

(2) KUOMBA VIBAYA ILI TUVITUMIE KWA TAMAA ZETU!

Tunaweza tukawa kweli tunaomba, tunaomba ili tupate kazi fulani, tunaomba Mungu atutumie tukiombea watu wapone na Mungu akutane na haja zao! Mwingine anaomba apate nyumba nzuri, mwingine gari, honda, n.k. Yote haya ni mema, lakini kama mtu anaomba moyoni kumejaa nia nyingine (kama uchoyo au kiburi), moyoni anasema au anawaza kwamba, “Nikipata gari ninalolitaka, watu watanikoma.” “Nikipata pesa hee! Watanitambua”, n.k.

Mwingine ni kipofu tangu kuzaliwa anamuomba Mungu lakini moyoni anawaza au anasema, “Sijawahi kuona mwanamke tangu kuzaliwa kwangu, nikiona sijui itakuwaje watanikoma, maana naishia kusikia tu na kuhisi” Unaona! Mtu anaomba lakini moyoni mwake anawaza nikikipata nitakutumia hivi au vile, matumzi yenyewe ni nje ya mpango wa Mungu. Ndugu yangu hapo tutaomba na kuombewa lakini kamwe hatuwezi kupokea majibu ya maombi! Tunataka mtoto lakini hatujaoa/hatujaolewa wala hatutaki kusikia habari za kuoa au kuolewa!

Mwingine anataka Mungu amtumie lakini moyoni mwake kumejaa mashindano ya dhahiri, anawaza kumzidi yule, mwingine anataka sifa tu! Mwingine anawaza utajiri kwamba nitakuwa napata sadaka nyingi za watu n.k. Maandiko yanasema katika Yakobo 4:3,

“Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.”

Unaona maandiko hayo? Kama tunamuomba Mungu tukiwa na hali hiyo! KAMWE hatuwezi kupokea majibu ya maombi. Ni kupoteza muda tu! Na mwisho wa siku tunaona kama Mungu hayupo; Mungu yupo na anajibu maombi! Tatizo lipo kwetu tu! Tunaomba ili tukipata tuvitumie vibaya! Kama tunataka kumuona Mungu lazima tuzingatie tunaomba ili tuvitumiaje? Nje ya mpango wa Mungu! Tuko watu wengi tunaomba na kufikia wakati tunafunga! Lakini tunaomba ili tuvitumiaje hivyo tunavyovitaka kwa njia ipi?

“Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.” Yakobo 4:3.

Kuomba tunaomba kweli! Lakini hatupati kwa sababu tunaomba vibaya ili tuvitumie kwa tamaa zetu! Tangu wakati huu tuhakikishe nia zetu zinakuwa safi mbele za Mungu ili tuyaone majibu yetu ya maombi na nguvu ya maombi! Maombi yana kanuni zake na ikiwa mtu anataka kumuomba Mungu na kumuona Mungu dhahiri akijidhihirisha kwake binafsi hatuna budi kuzingatia yote tunayopaswa kuyazingatia.
Lolote tunaloliomba lazima tangu moyoni huko ambako Mungu anaanza nako kwa kumuangalia mtu anataka hili ili iwe nini? Mwingine anatumia pesa kunyanyasa watu, Mungu huwa hamuinui mtu ambaye ana visasi, yaani Mungu akinipa hivi fulani atanikoma! Kila anachofanya Mungu ni kwa utukufu wake tu sio kwa utukufu wa mtu yeyote.

SOMO: MAISHA YA MAOMBI KWA MKRISTO (Part 7)

MAMBO YA KUZINGATIA TUNAPOKUWA TUNAMUOMBA MUNGU, TUNAPOKUWA KATIKA MAOMBI.

(3)HATUPASWI KUKATA TAMAA NA KUACHIA MAOMBI NJIANI BAADA YA KUONA TUNAOMBA MUDA MREFU BILA KUYAONA MAJIBU YETU YA MAOMBI KWA DHAHIRI!

Hakuna sehemu ngumu inayotushinda watu wengi kama hii! Watu wengi tunataka tukishaomba tu; basi tupokee majibu yetu ya maombi muda huo huo! Mungu hafanyi kazi hivyo ndugu yangu! Mungu ni wa utaratibu sana! Tunapomuomba Mungu tunatakiwa kuamini kwamba imekuwa. (Matha 7:7).

Hilo ndilo la kuliamini na kulishikilia wakati wote, haijalishi majibu yetu ya maombi tutayaona lini, sisi tuamini kwamba Mungu ametenda huku tunaendele kumwomba Mungu mpaka liwe dhahiri lile tunaloliomba. Mungu aliumba mbingu na nchi kwa muda wa siku 6, (Mwa 1:1). Unafikiri kwa uwezo wa Mungu! Kwa nini hakutumia siku moja tu kufanya kila kitu? Je! Hakuwa na uwezo huo? Uwezo upo mkubwa tena sana – Mungu ni wa utaratibu sana, ana nguvu ana uwezo lakini ni wa utaratibu mno! Mnoooo! Mbona basi wewe na mimi tunakata tamaa mapema hivyo na kuacha kuendelea kuomba! Tunaona Mungu hatusikii ni kama anawasikia wengine! Ni kama ana watu wake maalumu na sio sisi? Hatupaswi kuwaza hivyo hata kidogo, na tusiyape nafasi mawazo hayo! Tunapaswa kuendelea kung’ang’ania mbele za BWANA mpaka tuone majibu yetu ya maombi yawe dhahiri. Maandiko yanasema katika Luka 18:1,

“Akaawambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa”.

Hayo ni maandiko! Mungu anatambua kwamba! Mtu anaweza akaomba jambo na likachukua muda mrefu na mpaka mtu anafikia mahali kukata tamaa na kuacha kuomba, ndio maana inatajwa hapo “wala wasikate tamaa”.

Uwezekano wa kuchelewa kuyaona majibu yetu ya maombi unawekwa wazi na BWANA mwenyewe, lakini hatupaswi kukata tamaa! Marufuku kukata tamaa, usikate tamaa! Endelea kuomba, usiachie njiani hata kidogo! Usiwaze “Ooh! Labda kuna makosa nimeyafanya, labda nimefanya dhambi.” Kwani ukifanya dhambi hujui? Maandiko yanasema! 1 Petro 5:6, “Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake”. Kumbe kuna wakati wa Mungu! Wakati wa Mungu ni mzuri ndugu kuliko wakati wetu sisi! Mungu ndio anajua wakati mzuri wa kukupa jibu lako la maombi! Usione unakawia, wakati wako ndio unakawia, lakini wakati wa Mungu ni bora saaana! Mungu anajua wakati gani ukipata kazi utakuwa mzuri kuliko wakati fulani; Mungu ndio anajua wakati gani ukipata mtoto utakuwa mzuri zaidi! Wewe unataka mtoto sasa lakini Mungu akiangalia anona sasa sio salama! Unataka Mungu akutumie kwenye hili au lile n.k. Sisi tuendelee kumlilia BWANA! Kupokea ni lazima! Kukata tamaa ni marufuku! Hatupaswi kukata tamaa kamwe! Tuyashinde mawazo ya kutukatisha tamaa! Mungu yupo na anajibu maombi.

SOMO: MAISHA YA MAOMBI KWA MAOMBI KWA MKRISTO (Part 8)

MAMBO YA KUZINGATIA TUNAPOKUWA TUNAMUOMBA MUNGU,TUNAPOKUWA KATIKA MAOMBI.

(4)TUNAPASWA KUWA NA IMANI KWAMBA MUNGU YUPO NA ANATUSIKIA NA ANAJIBU MAOMBI!

Ndugu yangu, hata kama tutaomba na kujigalagaza na kulia kwa uchungu mpaka kutoka makamasi! Lakini kama hatuna imani ni buuure, bure!

Imani ni nini? Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana na mambo yasiyoonekana, Waebrania 11:11. Hiyo ndio imani! Tunaomba tunatarajia kupokea, sasa imani ni kuwa na uhakika kwamba! Hiki ninachikiomba kinakwenda kuwa sawasawa na nilivyoomba! Imani huwa haingalii mtu wala huwa haijilinganishi na mtu yeyote! Imani inaangalia uwezo wa Mungu tu na neno lake basi! Imani haingalii mazingira n.k. Imani inaweza kukufanya wewe kuwa wa kwanza kukipata hicho unachokiomba! Maandiko yanasema,

“Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.” (Waebrania 11:6).

Tunatakiwa kuwa hivyo tunapokuwa tunamuomba Mungu, tusiombe ili mradi tu, tusiombe ili kutimiza wajibu tu, tusiombe kwa desturi na mazoea! Kwa kufanya hivyo tutadangayika kwamba hakuna nguvu yeyote katika maombi, kumbe ni uongo wa ibilisi tu. Tunapaswa kumuamini Mungu tunapokuwa tunaomba! Na imani pasipo matendo imekufa! Baada ya maombi lazima uonyeshe matendo na sio unalala tu na kupigapiga soga na watu! Lazima ufanye matendo kama ni kazi tafuta kazi n.k.

Kutokuwa na imani ni dhambi vilevile! Ndugu yangu inawezekana umekuwa una muomba Mungu kwa muda mrefu lakini huna imani! Yesu alikutana na vipofu,angalia hapa! “Yesu alipokuwa akipita kutoka huko,vipofu wawili wakimfuata wakipaza sauti. Yesu akawaambia, ‘Mnaamini kwamba naweza kufanya hili?’ Wakamwambia, ‘Naam BWANA.’ Ndipo alipowagusa macho yao yakafumbuka.” Mathayo 9:27-30.

Unaona hapo? Baada ya kusema wanaamini ndipo Yesu alipowajibu majibu yao kwa kuwafumbua macho yao! Na hakuwafumbua macho kabla ya kujibu kwamba anaweza! Kabla ya kuionyesha imani yao! Na sisi Mungu anatuuliza kila tunapomuomba! Je! Tunaamini kwamba anaweza kufanya hilo au hayo tunayomuomba? Kila tunapoomba swali linakuja katika ulimwengu wa roho kwako binafsi, “Je! Unaamnini naweza kufanya hili?”

Imani ni lazima tunapokuwa katika maombi!

SOMO: MAISHA YA MAOMBI KWA MKRISTO (Part 9)

MAMBO YA KUZINGATIA TUNAPOKUWA TUNAMUOMBA MUNGU, TUNAPOKUWA KATIKA MAOMBI.
SEHEMU YA 9 NA MWISHO KWA SOMO HILI!

(5) DHAMBI

Maandiko yanasema katika kitabu cha Isaya,

“Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si nzito,hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafirikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone hata hataki kusikia.” (Isaya 59:1-2).

Kama tunafanya dhambi, Mungu kamwe! Hawezi kutusikiliza. Kamwe! Lazima maisha yetu yampendeze yeye tunayemuomba ili atupe kile tunachomuomba! Tunapaswa kuhakikisha dhambi kwetu ni mwiko kabisa kuzifanya wala kuziwaza! Tukiwa hivyo tunauhakika wa wazi wa kupokea majibu yetu ya maombi! Na hivi ndivyo ninavyohitimisha somo la MAISHA YA MAOMBII! Maandiko yanasema katika Isaya 53:1,

“Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na mkono wa BWANA amefunuliwa nani?”

(KUPAKUA SOMO HILI KAMA PDF, BONYEZA LINK:  MAOMBI Marco Bashiri )

                                          —————————————————————

Nawashukuru wote ambao wamepokea mafundisho haya! Ninatoa kibali kwa yeyote mwenye swali lolote kuhusiana na tuliyojifunza, au hajaelewa mahali waweza uliza swali sasa na nitalijibu bila shaka! Kwa kutumia number hizi: + 255 769 081 169

Tutaongea zaidi kuhusu maombi! Kama wewe ni miongoni mwa waombaji waliozinduka kupitia masomo haya! Unikumbuke kwenye maombi yako yaliyojaa nguvu na uhakika.

MUNGU AKUBARIKI SANA!

marksiwaa@gmail.com

RUDI KWA HOMEPAGE

 

 

 

 

 

25 responses to “Somo juu ya Maombi – Marco Bashiri

  1. Pingback: somabiblia
  2. fredrick swai

    July 25, 2016 at 6:42 pm

    ubarikiwe kwa huduma yako njema

     
    • Anonymous

      January 12, 2017 at 7:07 am

      Ameen! Karibu sana.

       
  3. Anonymous

    July 29, 2016 at 1:53 pm

    ubarikiwe

     
  4. Sophia Mihayp

    November 12, 2016 at 3:30 pm

    Umenitoa mahali na kunipeleka sehemu nyingine. MUNGU azidi kukutumia. Ubarikiwe.

     
    • Anonymous

      January 12, 2017 at 7:09 am

      Ameen! Nafurahi kusikia maana ndio kusudi la roho!

       
  5. Juhudi

    November 30, 2016 at 5:51 pm

    Asate Kwamafundisho Mazuri Mungu Akubariki

     
  6. Anonymous

    December 21, 2016 at 11:35 am

    Barikiwa sana mtu wa mungu

     
    • Anonymous

      January 12, 2017 at 7:09 am

      Barikiwa sana mtu wa Mungu

       
  7. maria

    December 26, 2016 at 8:08 pm

    Mtumishi wa Mungu nimebarikiwa sana na andiko lako.. Mungu na akubariki nawe cz, umekuwa mjumbe mwema

     
    • Anonymous

      January 12, 2017 at 7:10 am

      Ameen! Nafurahi kusikia kuwa umepokea kitu

       
  8. IBRAHIM MEDAN

    January 14, 2017 at 7:02 pm

    Amen, ubarikiwe sana mtumishi,, umenizindua leo.

     
  9. Anonymous

    January 15, 2017 at 8:33 am

    barikiwa mtumish8

     
  10. bernard wazaeli

    February 2, 2017 at 7:03 pm

    Sina maono,nimesoma kwa makini somo hilo lote kwa umakini sana na namshukuru sana Mungu kunipa mafundisho haya katika eneo la mashaka,mimi nimeokoka na namtegemea MUNGU kwenye maisha yangu nina jambo la kushauriana kupitia sms ambalo pia linahitaji maombi ya pamoja BWANA YESU ASIFIWE

     
  11. Jaffaryekombe

    February 20, 2017 at 3:47 am

    Maisha bila Maombi kwa wanadamu nikitubure

     
  12. Samson

    February 11, 2018 at 3:07 am

    I’am really blessed thank you,

     
  13. Anonymous

    February 20, 2018 at 12:30 pm

    Be blessed servant

     
  14. Anonymous

    May 23, 2018 at 6:50 am

    asante kwa mafundisho mazuri

     
  15. George Kilomo

    October 12, 2018 at 10:02 am

    Ninamshukuru Mungu kwa ajili yako mtumishi nimejifunza na kupata mambo mengi sana ya msingi kuhusu maisha ya maombi kwa mkristo. Natamani sana kuwadundisha wakristo wengine habari hizi..Naomba nipokee zaidi mafundisho ya kikristo toka kwako. Barikiwa sana mtumishi

     
  16. Essy Makata

    August 10, 2019 at 4:56 am

    Very encouraging indeed,i am going to teach this in my church this sunday

     
  17. FABIANO Simon

    January 19, 2020 at 8:39 am

    Dah!!!!! Haya ndy mafundisho ya nguvu …..nimemuona Bwana ….

    Barikiwa sana mtumishi
    I need your contact

     
  18. Oscar

    April 1, 2020 at 1:45 pm

    Ubarikiwe sana kwa somo zuri, hakika nimejifunza, Roho mtakatifu aliye ndani yetu aendelee kutufundisha yatupasayo kwa habari ya maombi.Ubarikiwe

     
  19. Oswald

    October 7, 2021 at 6:18 am

    Asante sana unanijulisha mungu akubariki tena na tena na tena

     
  20. Happiness Julius

    July 20, 2022 at 2:17 pm

    Bwana akubariki sanaa mpendwa n vingi nmejifunza

    Bwanaa azidi kukutumiaa

     
  21. Joseph p malando

    August 31, 2022 at 3:07 pm

    ubarkiwe sana mtu wa mungu tupo pamoja

     

Leave a reply to George Kilomo Cancel reply