SOMO JUU YA MAOMBI (Sehemu 1)
Wako wakristo ambao tunashindwa kuwa na maisha ya maombi kwa sababu zifuatazo.
(1) Kukosa muda wa kuomba kwa sababu ya majukumu ya muhimu ya hapa na pale.
(2) Mazingira ya mtu anapoishi.
(3) Mwingine hajui faida za maombi wala umuhimu wake.
(4) Mwingine anasema huwa anaishiwa maneno kwa haraka anapokuwa kwenye maombi.
(5) Mwingine hapendi maombi tu!
(6) Shetani.
(7) Mwili.
Katika maombi kuna vikwazo vingi, kwa sababu maombi yana nguvu!
(A) MAOMBI YANAONGEZA UHUSIANO WA MTU NA MUNGU!
Maombi ni mawasiliano baina ya mwanadamu na Mungu au ni njia ambayo tunaweza kuwasiliana na Mungu. Tunafanya mawasiliano na Mungu kwa njia ya maombi, na kama tunavyojua kwamba! Mawasiliano yanaongeza uhusiano wa mtu na mtu, hata wewe ni shahidi katika hili! Unaweza ukawa na ndugu wengi sana au marafiki wengi sana n.k. Lakini yule ambaye atawasiliana na wewe mara kwa mara huyo ndiye anayeukuza ukaribu kupita wengine. Na pia uhusiano wa mtu unaanzishwa kwa mawasiliano na vilevile unaweza ukafa au kupungua kwa kukosa mawasiliano ya mara kwa mara na kuelekezwa kule kwenye mawasiliano ya mara kwa mara! Mawasiliano yamewafanya watu wengi kuwa karibu, kupitia mitandao yetu. Mtu alipoanza mawasilano na wewe kwa njia ya kukutumia ujumbe wa maandishi au wa picha ulipojibu! Mawasilano yakakua mwisho wake ukaribu ukaongezeka kati yako na huyo….
Tunapokuwa tunaomba mara kwa mara uhusiano wetu na Mungu unakuwa kwa kasi sana kuzidi yule asiyeomba, au yule anayeomba mara moja moja au yule anayeomba kwa viwango vya juu zaidi! Na kama tujuavyo, kadiri uhusiano wa mtu na mtu unavyokuwa na kuongekezeka ndivyo wanavyoweza kushirikishana mambo mengi saaaana!
Ndivyo inavyokuwa kwa Mungu kwetu! Kwa sababu mahusiano yetu yanakuwa na kuongezeka! Mungu hataacha kutushirikisha mambo mengi yanayoendelea ili kuyaombea au kuzuia yasitokee au kuwashauri watu n.k. Mungu atatuonyesha hata hatari iliyopo mbele yetu, kwamba! Kuna ajali mbaya itatokea na kusababisha hiki na hiki na jinsi ya kuikwepa n.k. Yakiambatana na maelekezo yake jinsi ya kufanya ambayo yatakuwa na lengo la kujenga na si kubomoa! Utakuwa na furaha na amani wakati woote hata kwenye dhiki za namna gani! Sijui nitumie lugha gani nieleweke jamani: Ili uelewe hili na kulishika kwamba! MAOMBI YANAONGEZA UHUSIANO WA MTU NA MUNGU!
Tuanze maisha ya maombi kuanzia sasa ili uhusiano wetu na Mungu ukue, anzisha mahusiano yako na Mungu kwa kuwasiliana naye mara kwa mara kwa njia ya maombi. Hata kama zamani tulikuwa na bidii ya kuwasiliana na Mungu kwa njia ya maombi halafu tukayakata mawasilano hayo! Bado tunaweza kuyaanzisha upya na kuyakuza! Pia usiache kuwasiliana na Mungu mara kwa mara kwa njia ya maombi kwa sababu kwa kutofanya hivyo utauvunja au utaupunguza uhusianao wako na Mungu!
Marco Bashiri